Imamu Swadiq (a.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Imam Swadiq (a.s))
Imam Ja'far Swadiq (a.s)
Imamu wa Sita wa Mashia
Mava ya Baqi'i
KuniaAbu Abdillah
Siku ya Kuzaliwa17 Rabiul-Awwal 83 Hijria
Mahali AlipozaliwaMadina
Kipindi cha UimamuMiaka 34 (114 - 148)
Kifo25 Shawwal 148 Hijria
AlipozikwaMadina - Mava ya Baqi'i
AlipoishiMadina
LakabuSadiq, Sabir, Tahir, Fadhil
BabaImamu Muhammad al-Baqir
MamaUmmu Farwa binti Qassim
WakeHamida, Fatma binti wa Hussein bin Ali
WatotoIsmail, Abdallah, Umm Farwa, Mussa (a.s), Is'hak, Muhammad, Abbas, Ali, Asma na Fatma
UmriMiaka 65
Maimamu wa Kishia
Imamu Ali • Imamu Hassan MujtabaImamu Hussein • Imamu Sajjad • Imamu Baqir • Imamu SwadiqImamu Kadhim • Imamu Ridha • Imamu JawadImamu Hadi • Imamu Mahdi


Imam Ja'far Swadiq (a.s) (Kiarabu: الإمام جعفر الصادق عليه السلام) (83-148 H) ni Ja'far ibn Muhammad, Imam wa sita katika mlolongo wa Maimamu kumi na mbili wa Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna'asharia. Alichukua jukumu la Uimamu baada ya baba yake Imam Muhammad Baqir( a.s). Alikuwa Imamu na kiongozi wa Waislamu kwa muda wa miaka 34 (kuanzia 114-148) ambapo uongozi wake ulisadifiana na Ukhalifa wa watawala watano wa mwisho wa ukoo wa Bani Umayyah yaani kuanzia Hisham bin Abdul-Malik na kuendelea na makhalifa wawili wa mwanzo wa utawala wa Bani Abbas ambao ni Abul-Abbas Abdallah bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Abul-Abbas al-Saffah na Mansour Dawaniqi.

Kutokana na udhaifu wa utawala wa Bani Umayyah, Imam Swadiq (a.s) alifanikiwa kuendesha harakati zaidi za kielimu ikilinganishwa na Maimamu wengine wa Kishia. Nyaraka mbalimbali za historia zinaonyesha kuwa, Imam Swadiq (a.s) alifanikiwa kulea na kutoa wanafunzi na wapokezi wa hadithi 4,000. Idadi kubwa ya wapokezi wa hadithi wa Ahlul-Bayt (a.s) wanatokana na Imam Swadiq (a.s), na kutokana na sababu hiyo ndio maana madhehebu ya Shia Imamiyyah yameondokea kufahamika pia kwa jina la Madhehebu ya Ja'fariyah. Imamu Swadiq (a.s) ana nafasi muhimu na anaheshimika mno, pia miongoni mwa viongozi na Maimamu wa fikihi wa madhehebu ya Ahlu-Suna, Abu Hanifa na Malik ibn Anas wamenukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s). Abu Hanifa amemtaja Imam Swadiq(a.s) kama mtu msomi zaidi miongoni mwa Waislamu.

Licha ya kuweko mapungufu na udhaifu wa utawala wa Bani Umayyah na hata kuweko matakwa na Mashia, lakini Imam Swaqiq(a.s) hakuanzisha harakati dhidi ya utawala huo. Alikataa maombi na matakwa ya Abu Muslim Khorasani na Abu Salama ya kuchukua cheo cha Ukhalifa. Imam Swadiq(a.s) hakushiriki hata katika harakati ya ami yake Zayd ibn Ali na alikuwa akiwataka pia Mashia kujiepusha na harakati hiyo; lakini licha ya hayo yote hakuwa na uhusiano mzuri na watawala wa zama zake. Kutokana na mashinikizo ya kisiasa na tawala za Bani Umayyah na Bani Abbas alikuwa akitumia mbinu ya taqiya na alikuwa akiwausia pia wafuasi wake kushikamana na taqiya.

Imam Swadiq (a.s) akiwa na lengo la kuwa na mawasiliano na maingiliano zaidi na Mashia, kujibu masuala yao ya kisheria kuhusu hukumu mbalimbali, kupokea fedha zao za malipo ya kisheria (Wujuhat Shar’ia) kama Zaka, Khumsi na kadhalika na kushughulikia matatizo ya Waislamu aliunda mtandao wa uwakala. Harakati na shughuli za mtandao huu ulichukua mkondo mpana zaidi katika zama za Imam aliyekuja baadaye na ulifikia kilele katika zama za Ghaiba Ndogo (Ghaibat Sughra). Katika zama zake harakati za Maghulati (kundi la watu waliokuwa na misimamo ya kufurutu mpaka katika madhehebu ya Shia) zilichukua wigo mpana zaidi. Imam Swadiq(a.s) alisimama na kukabiliana vikali na fikra ya uchupaji mipaka na ya kuwatukuza Maimamu kupita kiasi na akawatambulisha Maghulati kuwa ni makafiri na washirikina.

Imekuja katika baadhi ya vyanzo ya kwamba, Imam Swadiq (a.s) alisafiri na kuelekea Iraq baada ya kuitwa na utawala na kufanikiwa kwenda katika miji ya Karbala, Najaf na Kufa. Katika safari hiyo aliwaonyesha masahaba zake kaburi la Imam Ali (a.s) katika mji wa Najaf ambalo kabla ya hapo halikuwa likifahamika kwa uwazi. Baadhi ya Maulamaa wa Kishia wanaamini kwamba, Imam Swadiq (a.s) aliuawa shahidi kwa sumu kwa njama na maagizo ya mtawala Mansur Dawaniqi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya hadithi vya Kishia, alikuwa amemtambulisha Imam Kadhim (a.s) kwa masahaba zake wa karibu kuwa ndiye Imam anayefuata baada yake; hata hivyo akiwa na lengo la kumhifadhi na maadui na kulinda maisha na uhai wake, aliwataja watu na kuwatambulisha watu watano katika wasia wake akiwemo Mansur Dawaniqi mtawala wa Bani Abbas kwamba, ndio mawasii wake. Baada ya kuuawa shahidi Imam Swadiq (a.s), kuliibuka makundi tofauti katika Ushia ambapo baadhi yake ni Ismailia, Fatahiyya na Nawusiyya.

Kuna vitabu 800 vilivyoandikwa kuhusiana na Imam Swadiq (a.s) ambapo vitabu vya Akhbar al-Swadiq Maa Abi Hanifa na Akhbar al-Swadiq Maa al-Mansur vilivyoandikwa na Muhammad ibn Wahban Ardebili (karne ya 4) ndio vikongwe zaidi miongoni mwavyo. Baadhi ya vitabu vingine vilivyoandikwa kuhusiana na Imam Swadiq(a.s) ni: Imam Swadiq (a.s) wal-Madhahib al-Ar’ba, kilichoandikwa na Asad Haidar, Ensaiklopedia ya Imam Swadiq, kilichoandikwa na Muhammad Kadhim Qazwin, Zendegani Imam Swadiq, mwandishi Sayyid Ja'far Shahidi na Ensaiklopedia ya Imam Swadiq mwandishi Baqir Sharif al-Qureshi.

Jina, Nasaba na Kuniya

Makala Asili: Orodha ya kuniya na lakabu za Imam Swadiq (a.s)

Ja'far ibn Muhammad ibn Ali ibn Hussein ibn Ali ibn Abi Twalib (a.s), ni Imamu wa Sita katika mlolongo wa Maimamu kumi na mbili wa Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna’asharia [1]. Madhehebu ya Ismailiya inamtambua Imamu Swadiq (a.s) kama Imamu wao wa 5. [2] Baba yake ni Imam Muhammad Baqir (a.s) na mama yake ni Ummu Farwa binti wa Qassim ambaye ni mtoto wa Muhammad bin Abu Bakr. [3] Kwa mujibu wa nukuu ya kitabu cha Kashf al-Ghummah cha mmoja wa Maulamaa wa Kisuni ni kuwa, kwa kuwa nasaba ya mama wa Imam Swadiq (a.s) kwa upande wa baba na kwa upande wa mama pia ilikuwa inaishia kwa Abu Bakr, Imam Swadiq (a.s) akasema: Nimezaliwa mara mbili kutoka kwa Abu Bakr. Hata hivyo baadhi ya wanazuoni akiwemo Allama Shushtari na Muhammad Baqir Majlisi wanaamini kwamba, hadithi hii ni bandia. [4]

Jina mashuhuri la Imam Swadiq (a.s) ni Abu Abdillah (kwa kuzingatia mtoto wake wa pili yaani Abdallah Aftah). Ana kuniya zingine pia kama Abu Ismail (kwa kuzingatia mtoto wake mkubwa, Ismail) na Abu Mussa kwa sababu ya kuwa na mtoto aliyejulikana kwa jina la Mussa ambaye ndiye Imamu Mussa al-Kadhim (a.s).[5] Lakabu yake mashuhuri zaidi ni Swadiq. [6] Kwa mujibu wa hadithi na riwaya mbalimbali, Mtume(s.a.w.w) ndiye aliyempa lakabu hii ili kuweko na tofauti kati yake na Ja'far Kadhab; [7] hata hivyo baadhi wanasema kuwa, Imam Swadiq aliondokea kufahamika kwa lakabu ya Swadiq kutokana na kujiweka mbali na kutoshiriki katika harakati na mapinduzi yaliyoibuka katika zama zake; hii ni kutokana na kuwa katika zama hizo mtu aliyekuwa akikusanya watu na kuwachochea ili waanzishe harakati na mapinduzi dhidi ya utawala alikuwa akiitwa kwa jina la kadhab (muongo). [8] Lakabu hii ilikuwa ikitumika kwa Imam Swadiq (a.s) katika zama za Maimamu (a.s). [9] Baadhi ya Maulamaa wa Kisuni kama Malik ibn Anas, Ahmad bin Hanbal na Jahidh walikuwa wakimuita Imamu Swadiq (a.s) kwa lakabu hii. [10]

Historia ya Maisha yake

Imam Swadiq (a.s) alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal mwaka 83 Hijria katika mji wa Madina na alikufa shahidi katika mji huo huo mwaka 148 Hijria akiwa na umri wa miaka 65. [11] Baadhi wameandika kuwa, alizaliwa mwaka 80 Hijria. Kadhalika ibn Qutaybah Dinawari amesajili kuwa, Imam Swadiq aliaga dunia 146 Hijria [13] ambapo hilo limetambulika kuwa ni kosa katika kusajili. [14] Kuna hitilafu za kimitazamo kuhusiana siku na mwezi aliokufa shahidi Imamu Swadiq (a.s). Mtazamo na rai ambayo ni mashuhuri baina ya Maulamaa wa zamani wa Kishia ni kwamba, Imam Swadiq (as) alikufa shahidi Mfunguo Mosi Shawwal. Hata hivyo katika vyanzo vya wanazuoni waliotangulia siku ya kufa kwake shahidi haijatajwa. [15] Pamoja na hayo yote, vyanzo na vitabu vya baadaye vimeitaja tarehe ya kufa shahidi Imamu Swadiq (a.s) kuwa ni 25 Mfunguo Mosi Shawwal. [16]. Mkabala na mtazamo na rai mashuhuri, kuna Maulamaa kama Tabrasi katika kitabu chake cha I’lam al-Wara [17] na Muhammad Baqir Majlisi katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar wakinukuu kutoka katika kitabu cha Misbah Kaf’ami wameripoti kwamba, siku aliyokufa shahidi Imam Swadiq (a.s) ni tarehe 15 Rajab; hata hivyo wahakiki wa kitabu cha Bihar al-Anwar hawajalipata jambo hili katika kitabu cha Misbah. [8]

Wake na Watoto

Sheikh Mufid ametaja watoto 10 na wake kadhaa wa Imam Swadiq (a.s); [19] katika baadhi ya vyanzo imeashiriwa binti mwingine wa Imam Swadiq kwa jina la Hakima au Halima ambapo hili kwa mujibu wa vyanzo hivyo limenukuliwa kutoka kwa Imam Mussa al-Kadhim(as).

  • Mke: Hamida, Nasaba: Binti ya Sa’id au Salih
  • Watoto: Imam Kadhim (a.s) Is’haq na Muhammad
  • Ufafanuzi: Imam Kadhim (a.s) ni Imamu wa Saba wa Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna'asharia. [21]
  • Mke: Fatma
  • Nasaba: Binti ya Hussein bin Ali bin Hussein (a.s)
  • Watoto: Ismail, Abdallah Aftah na Umm Farwa
  • Ufafanuzi: Abdallah baada ya kuaga dunia baba yake alidai Uimamu na wafuasi wake walijulikana kwa jina la Fatahiyya. [22] Ismail aliaga dunia katika zama za uhai wa Imam Swadiq (a.s) lakini baadhi hawakukubali na kuamini kifo chake na hivyo wakaanzisha kundi la Ismailiya. [23]
  • Wake wengine….
  • Watoto: Abbas, Ali, Asmaa na Fatma

Kwa mujibu Sheikh Mufid ni kuwa, kila mmoja kati ya watoto hawa alitokana na kijakazi (ummu Walad). [24]

Zama za Uimamu

Maisha ya Imam Swadiq (a.s) yalisadifiana na ukhalifa na uongozi wa makhalifa kumi wa mwisho wa Bani Umayya akiwemo Omar ibn Abdul-Aziz na Hisham ibn Abdul-Malik na makhalifa wawili wa Bani Abbas ambao ni Abul-Abbas Abdallah bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Abul-Abbas al-Saffah na Mansour Dawaniqi. [25] Aliambatana na baba yake yaani Imam Muhammad Baqir(a.s) katika safari ya kuelekea Shamu iliyofanyika kwa amri ya Hisham bin Abdul-Malik. [26] Kipindi cha Uimamu wake kilisadifiana na makhalifa watano wa mwisho wa Bani Umayyah yaani kuanzia Hisham ibn Abdul-Malik na kuendelea na Saffah na Mansur makhalifa wa Bani Abbas. ]27] Katika kipindi hiki utawala wa Bani Umayyah ulidhoofika na hatimaye ukaondolewa madarakani na baada ya hapo Bani Abbas wakashika hatamu za uongozi. Udhaifu na tawala kutokuwa na usimamizi, ni mambo ambayo kwa hakika yalimuandalia Imam Swadiq (a.s) fursa mwafaka kwa ajili ya kuendesha harakati za kielimu. [28] Hata hivyo uhuru huu ulikuweko tu katika muongo wa tatu wa karne ya pili Hijria na kabla ya hapo, kwani baada ya harakati za mapinduzi ya Muhammad Nafs al-Zakiyah na kaka yake Ibrahim kulikuweko na mashinikizo mengi ya kisiasa dhidi ya Imam Swadiq (a.s) na wafuasi wake. [29]

Ushahidi wa Uimamu

Kwa mtazamo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kwamba, Imamu anapaswa kuteuliwa na Mwenyezi Mungu na njia za kumjua ni kupitia ushahidi na hoja za wazi kama hadithi kutoka kwa Bwana Mtume(s.a.w.w) au kauli ya Imam wa kabla yake inayoeleza bayana kwamba, baada yake Imam atakuwa ni fulani. [30] Sheikh Kulayni ameleta katika kitabu chake cha al-Kafi hadithi kwa ajili ya kuthibitisha Uimamu wa Imam Ja'far Sswadiq (a.s). [31]

Mtandao wa Uwakala

Makala ya Asili: Mtandao wa Uwakala

Kutokana na sababu mbalimbali kama vile kutawanyika Mashia katika maeneo tofauti tofauti, mawasiliano na Mashia kuwa magumu, kukithiri mashinikizo ya kisiasa na kutoweza Mashia kuwasiliana moja kwa moja na Imamu Swadiq (a.s), Imam Swadiq aliteua na kuainisha kundi la wawakilishi katika maeneo mbalimbali katika ulimwengu wa Kiislamu na kundi hilo likawa linajulikana kwa jina la mtandao wa uwakala. [32] Mtandao huo ulikuwa na jukumu kama la kupokea fedha za malipo ya kisheria (Wujuhat Shar’ia) kama Zaka, Khumsi, nadhiri pamoja na zawadi za Mashia na kukabidhi kwa Imam Swadiq (a.s). Jukumu jingine la mtandao wa uwakala lilikuwa ni kushughulikia matatizo ya Mashia, kuleta mawasiliano baina ya Maimamu na Mashia na kujibu maswali ya Kisheria. [33] Mtandao huu wa uwakala ulichukua wigo mpana zaidi katika kipindi cha Maimamu waliokuja baadaye na katika zama za Ghaibat Sughra (Ghaiba Ndogo) na shughuli zake zilifikia kilele kupitia Manaibu Wanne wa Imam Mahdi (a.t.f.s) na shughuli zake zilifikia tamati sambamba na kuanza duru ya Ghaibat al-Kubra (Ghaiba Kubwa) ya Imam Mahdi na kuaga dunia naibu wake wanne yaani Ali ibn Muhammad al-Samuri. [34]

Kukabiliana na Maghulati

Makala ya Asili: Maghulati

Katika zama za Imam Baqir (a.s) na Imamu Swadiq (a.s) harakati za maghulati (watu ambao walichupa mipaka kuhusiana na shakhsia ya Maimamu Maasumina) ziliongezeka. [35] Kundi hilo lilikuwa likiamini cheo cha uungu kwa Maimamu au walikuwa wakiwatambua kuwa ni Mitume. Imam Swadiq(a.s) alisimama kuipinga vikali fikra hii na alikuwa akiwakataza watu kukaa pamoja na maghulati. [36] na aliwatambua watu wenye fikra hizo kuwa ni mafasiki, makafiri na washirikina. [37] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq(a.s) kuhusiana na maghulati ambapo aliwausia Mashia na wafuasi wake inasema: “Msikae pamoja nao, msile nao, msinywe nao na msipeane nao mikono.” [38] Imam Swadiq(a.s) aliwatahadharisha Mashia kuwa makini na vijana wao pale aliposema: “Chungeni maghulati wasije kuwaharibu vijana wenu. Wao ni maadui wabaya kabisa wa Mwenyezi Mungu; wanamdogosha Mwenyezi Mungu na wanaamini uungu kwa waja wa Mwenyeziu Mungu.” [39]

Harakati za Kielimu

Katika zama za Imamu Swadiq (a.s) kutokana na udhaifu wa utawala wa Bani Umayyah, kulijitokeza uhuru zaidi kwa ajili ya kudhihirisha na kuionyesha itikadi na kulifanyika midahalo mingi ya kielimu katika maudhui mbalimbali. [40] Anga hii ya uhuru wa kielimu na kidini ilishuhudiwa kwa uchache mno kwa Imam miongoni mwa Maimamu kumi na mbili. Hali hii iliandaa uwanja na mazingira kwa wanafunzi wa Imam kushiriki kwa uhuru kamili katika vikao na mijadala ya kielimu. [41] Anga ya wazi ya kielimu ilipelekea kunukuliwa hadithi nyingi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) katika nyuga mbalimbali za kifikihi, teolojia na kadhalika. [42] Ibn Hajar Haytami anasema: Watu walikuwa wakinukuu kutoka kwake elimu nyingi na umashuhuri wake ulifika kila mahali. [43] Naye Abu Bahr Jahidh ameandika: Elimu na fikihi yake (Imamu Swadiq) ilikuwa imeujaza ulimwengu. [44] Hassan ibn Ali Wash'haa naye amesema, aliwaona watu 900 katika msikiti wa Kufa ambao walikuwa wakinukuu hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s). [45] Allama Tehrani anaamini kwamba, baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w) na matukio machungu yaliyotokea baada ya hapo kuhusiana na kupotoshwa ukweli wa Uislamu na kukengeushwa kutoka katika maktaba ya Ahlul-Bayt (a.s) na jamii ya Waislamu, ilikuwa ikihitajia mitikisiko miwili, mshtuko na harakati. Mshtuko wa kivitendo kwa minajili ya kuuamsha umma harakati ambayo ilifanywa na Imamu Hussein (a.s) na mshtuko mwingine ulikuwa ni wa kielimu kwa ajili ya kuhuisha maarifa ya Qur'ani na dini, ambapo kazi hii ya pili ilifanywa na Imamu Swadiq (a.s). [46]

Madhehebu ya Ja'fariya

Makala ya Asili: Madhehebu ya Ja'fariya

Kati ya Maimamu wa Waislamu] wa madhehebu ya Shia, iwe ni katika Usul a-Din (Misingi ya Dini) au katika Furu’ al-Din (Matawi ya Dini), riwaya na hadithi nyingi zimenukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s). [47] Aidha Imamu Swadiq (a.s) alikuwa na wapokezi wengi zaidi wa hadithi. Irbili ametaja idadi ya wapokezi wa hadithi wa Imamu Swadiq (a.s) kuwa ni 4,000. [48] Aban bin Taghlib anasema kuwa, kila mara Mashia walipokuwa wakihitalifiana kuhusiana na maneno ya Bwana Mtume (s.a.w.w) walikuwa wakishikamana na Imam Ali (a.s) na walipokuwa wakitofautiana kimitazamo kuhusiana na maneno ya Ali (a.s) walikuwa wakirejea maneno ya Imamu Swadiq (a.s). [49] Kutokana na kunukuliwa hadithi nyingi za maudhui ya kifikihi na kitheolojia kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) madhehebu ya Shia Imamiyyah yameondokea kufahamika pia kwa jina la Madhehebu ya Ja'fariya. [50] Hii leo Imam Swadiq [a.s] ameondokea kuwa mashuhuri kwa anuani ya kiongozi wa madhehebu ya Ja'fariya (madhehebu ya Shia). [51] Katika mwaka 1378 Hijria Sheikh Mahmud Shaltut Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar cha nchini Misri, baada ya kuandikiana barua na Ayatullah Borujerdi aliyatambua rasmi madhehebu ya Ja'fariya na akasema kuwa, kisheria inajuzu kufanya amali kwa mujibu wa madhehebu hayo. [52][53][54

Midahalo na Majadiliano ya Kielimu

Katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia, kunaonekana midahalo na mijadala mbalimbali ya Imam Ja'far Swadiq (a.s) na wasomi wa elimu ya theolojia (wanatheolojia) wa madhehebu zingine na vilevile mjadala wake na baadhi ya waliokuwa wakikana uwepo wa Mwenyezi Mungu. [55] Katika baadhi ya midahalo hiyo, baadhi ya wanafunzi wa Imamu Swadiq (a.s) walifanya mijadala na watu wengine katika uga waliokuwa na utaalamu nao lakini kwa kuweko pia Imamu Swadiq (a.s). Katika vikao hivyo, Imam Swadiq(a.s) alikuwa msimamizi na mtazamaji na wakati mwingine mwenyewe alikuwa akiingia katika mjadala na maudhui iliyokuwa ikijadiliwa. [56] Kwa mfano, katika mjadala na mazungumzo na alimu na msomi kutoka Shamu ambaye mwenyewe aliomba mjadala na wanafunzi wa Imamu Swadiq (a.s), Hisham bin Salim alitakiwa na Imam Swadiq ajadiliane na msomi huyo katika maudhui ya itikadi (theolojia). [57] Kadhalika kila mtu ambaye alitaka mjadala naye, kwanza alimtaka ajadiliane na wanafunzi wake katika uga na maudhui yoyote anayotaka na kama atawashinda basi wakati huo anaweza kujadiliana naye. Yule Bwana alishindwa na Humran ibn A'yan katika maudhui ya Qur'ani, akashindwa na Aban ibn Taghlib katika uga wa fasihi ya kiarabu, akashindwa na Zurarah ibn A'yun katika fikihi na akafanya mdahalo na Mu’min al-Taq na Hisham ibn Salim katika theolojia na kushindwa. [58].

Ahmad ibn Ali Tabarsi ameorodhesha orodha ya midahalo ya Imamu Swadiq (a.s) katika kitabu chake cha al-Ihtijaj na baadhi yake ni:

  • Mdahalo na mmoja wa wakanaji wa uwepo wa Mwenyezi Mungu. [59]
  • Mdahalo na Abu Shakir Deisani, kuhusu uwepo wa Mwenyezi Mungu. [60]
  • Mdahalo na ibn Abil Aujaa kuhusiana na uwepo wa Mwenyezi Mungu. [61]
  • Mdahalo na ibn Abil Aujaa kuhusiana na kutokea ulimwengu. [62]
  • Mdahalo mrefu na mmoja wa wakanushaji wa uwepo wa Mungu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kidini. [63]
  • Mdahalo na Abu Hanifa kuhusiana na mbinu ya kunyambua hukumu za kifikihi hususan qiyas (kulinganisha jambo ambalo halikutajwa katika hukumu na jingine lililotajwa kutokana na kuwa na sababu moja). [64]
  • Mdahalo na baadhi ya Maulamaa wa Mu'tazilah kuhusiana na mbinu ya kuchagua mtawala na baadhi ya hukumu za kifikihi. [65]

Sira ya Kisiasa

Maisha ya Imam Swadiq(a.s) yalisadifiana na uongozi wa makhalifa 10 wa Bani Umayyah akiwemo Omar ibn Abdul-Aziz na Hisham ibn Abdul-Malik na vilevile makhalifa wawili wa Bani Abbas ambao ni Abul-Abbas Abdallah bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Saffah na Mansur Dawaniqi. [66] Aliambatana na baba yake, yaani Imam Muhammad Baqir(a.s) katika safari ya kuelekea Shamu iliyofanyika kwa amri ya Hisham bin Abdul-Malik. [67] Kipindi cha Uimamu wake kilisadifiana na utawala wa makhalifa watano wa mwisho wa Bani Umayyah, yaani kuanzia Hisham ibn Abdul-Malik na kuendelea na Saffah na Mansur makhalifa wa Bani Abbas. [68]

Kujitenga na Mapinduzi ya Silaha

Licha ya kuwa kipindi cha Uimamu cha Imamu Swadiq (a.s) kilisadifiana na udhaifu na kusambaratika utawala wa Bani Umayyah, lakini yeye alijiweka mbali na mapigano ya kijeshi na kisiasa na hata alikataa ombi la kuchukua Ukhalifa. Muhammad ib Abdul-Karim Shahrastani ameandika katika kitabu chake cha al-Milal wa al-Nihal: Baada ya kifo cha Ibrahim al-Imam, Abu Muslim Khorasani alimuandikia barua Imamu Swadiq (a.s) akimtaka achukue jukumu la ukhalifa na kumtaja katika barua hiyo kwamba, yeye ndiye mtu anayestahiki zaidi cheo hicho. Imam aliandika katika jibu lake: “Wewe si katika wafuasi wangu na wala zama sio zama zangu.”[69] Aidha alijibu barua ya Abu Salama iliyokuwa na takwa kama hilo kwa kuichoma moto. [70] Imam Swadiq kadhalika alijiweka mbali na harakati na mapinduzi dhidi ya utawala ikiwemo harakati ya ami yake Zayd ibn Ali. [71] Kwa mujibu wa hadithi, kutokuweko wafuasi na masahaba wakweli ndio sababu iliyomfanya Imamu Swadiq (a.s) kujiepusha na suala la kuanzisha harakati na mapinduzi. [72] Imekuja katika baadhi ya hadithi ya kwamba, Imam Swadiq alitaja idadi ya masahaba 17 na wakati mwingine wafuasi watano tu kwamba, wanatosha kwa ajili ya kuanzisha harakati, na mkabala wa msisitizo wa baadhi ya masahaba zake waliokuwa wakimtaka aanzishe harakati alikuwa akiwamaambia, sisi tunafahamu zaidi ni wakati gani na tuna jukumu gani. [73]

Hitilafu na Abdallah ibn Hassan al-Muthanna

Katika miaka ya mwishoni mwa utawala wa Bani Umayyah, kundi miongoni mwa Bani Hashim akiwemo Abdallah ibn al-Muthanna na watoto wake, Saffah na Mansur, walikusanyika katika eneo la al-Abwa ili wampatie baia na kiapo cha utiifu mmoja miongoni mwao kwa ajili ya kuanzisha harakati ya upinzani dhidi ya utawala. Katika kikao hicho Abdallah alimtambulisha mwanawe Muhammad kuwa ni Mahdi na akawataka wale waliohudhuria wampe bai na kiapo cha utiifu. Wakati Imamu Swadiq (a.s) alipopata taarifa ya tukio hilo alisema: “Mwanao sio Mahdi na hivi sasa sio wakati wa kudhihiri Mahdi.” Abdallah alikasirika kutokana na maneno hayo ya Imam Swadiq na akamtuhumu kwa kufanya husuda. Imamu Swadiq (a.s) aliapa kwamba, hazungumzi hayo kutokana na husuda na akasema, watoto wake watauawa na uongozi utawafikia Saffah na Mansur. [74]. Rasul Ja’fariyan anasema: Chimbuko la hitilafu baina ya watoto wa Imam Hassan (a.s) na watoto wa Imamu Hussein (a.s) ni hili tukio. [7

Uhusiano na Watawala

Licha ya Imamu Swadiq (a.s) kujiweka mbali na harakati na mapinduzi ya silaha dhidi ya tawala, lakini hakuwa na uhusiano mzuri na watawala wa zama zake. Wakati alipoenda Hija akiwa pamoja na baba yake Imam Muhammad Baqir (a.s) aliwatambulisha katika marasimu hiyo ya ibada ya Hija kwamba, Ahlul-Bayt (a.s) ni waja wateule wa Mwenyezi Mungu na kuashiria uadui wa Khalifa Hisham ibn Abdul-Malik dhidi ya Ahlul-Bayt (a.s). [76] Katika jibu lake kwa Mansur Dawaniqi aliyemtaka aende kumuona kama wanavyofanya watu wengine Imamu Swadiq (a.s) aliandika: Sisi hatuna kitu ambacho kutokana nacho tukuogope, na wewe huna kitu katika mambo ya akhera ambacho sisi tuwe na matumaini na wewe, na wala wewe hauko katika neema hata sisi tukupongeze na wala hauamini kwamba, uko katika msiba hata sisi tukupe mkono wa pole kwa hilo. Sasa kwa nini tuje kwako?! [77]

Kuchomwa Moto Nyumba ya Swadiq (a.s)

Kwa mujibu wa hadithi iliyokuja katika kitabu cha Kafi, wakati Hassan ibn Zayd, alipokuwa liwali na mtawala wa Makka na Madina, alichoma moto nyumba ya Imamu Swadiq (a.s) kwa amri ya mtawala Mansur Dawaniqi. Kwa mujibu wa hadithi hii katika tukio hili la moto, mlango na korido ya nyumba ya Imam Swadiq vilikuwa vikiungua huku Imam akipita katikati ya moto na kisha akatoka nje na kusema: Mimi ni mtoto wa A’raq al-Thara (lakabu ya Nabii Ismail yenye maana ya mtu ambaye watoto na kizazi chake kitaenea ardhini kama mishipa na mizizi). Mimi ni mtoto wa Ibrahim Khalilullah. [78] Hata hivyo Tabari ameandika kuwa, Mansur katika mwaka 150 Hijiria yaani miaka miwili baada ya kufa shahidi Imamu Swadiq (a.s) alimfanya Hassan ibn Zayd kuwa mtawala wa Madina. [79]

Kutumia Taqiya

Ghairi ya muongo wa tatu wa karne ya pili Hijiria ambao ulisadifiana na kusambaratika utawala wa Bani Umayyah, daima Makhalifa wa Bani Umayyah na Bani Abbas walikuwa wakizifuatilia nyayo na harakati za Imamu Swadiq (a.s) na wafuasi wake. Mashinikizo ya kisiasa yalifikia kilele mwishoni mwa maisha ya Imam Swadiq(a.s). [80] Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, makachero na vibaraka wa Mansur walikuwa wakifanya uchunguzi na kuwatambua watu ambao walikuwa na uhusiano na Mashia wa Imamu Swadiq (a.s) na kisha walikuwa wakiwaua. Kutokana na hilo, Imamu Swadiq na wafuasi wake walikuwa wakitumia mbinu na mkakati wa taqiya (kuficha itikadi). [81] Imamu Swadiq (a.s) alimwambia na kumnasihi Sufyan al-Thawri aliyekuja kuonana naye kwamba, aondoke hapo kutokana na kuwa wote wawili walikuwa chini ya uangalizi wa utawala. [82] Katika hadithi nyingine, Imam Swadiq alimtaka Aban bin Taghlib ajibu maswali ya kifikihi ya watu kwa kunukuu mitazamo ya Maulamaa wa Kisuni ili kusitokee tatizo. [83] Kadhalika imenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Swadiq(a.s) ambazo zinatilia mkazo juu ya suala la kufanya taqiya. Katika baadhi ya hadithi hizo, taqiya imewekwa katika nafasi moja na Swala. [84] Kwa mtazamo wa Ayatullah Ali Khamenei mchambuzi wa sira ya Maasumina ni kuwa, vigezo, dondoo na mifano muhimu ya maisha ya Imamu Swadiq (a.s) ni:

  1. Kubainisha na kufikisha ujumbe wa kadhia ya Uimamu, lengo lake lilikuwa ni kuwapinga moja kwa moja na kwa uwazi kabisa watawala wa zama zake na kujitambulisha yeye kuwa ndiye mstahiki halisi wa haki ya kweli Wilaya na Uimamu kwa watu.
  2. Kufikisha ujumbe (kufanya tablighi) na kubainisha sheria na hukumu za dini kwa mbinu na mtindo wa fikihi ya Kishia na vilevile tafsiri ya Qur'ani kwa muundo na mtazamo wa Kishia kwa namna ya kipekee zaidi, ya wazi zaidi na sahihi zaidi ya kile ambacho kinawezekna kuonekana katika maisha ya Maimamu wengine; kwa namna ambayo fikihi ya Kishia ikaondokea kuwa na jina la Fikihi ya Ja'fari na mpaka ikafikia kwamba, watu wote ambao walipuuza harakati zake za kisiasa wakafikia natija ya maneno haya kwamba, Imam Swadiq alikuwa na chuo kikubwa zaidi (au moja ya vyuo vikubwa zaidi) vya kielimu na kifikihi katika zama zake.
  3. Kuweko vikundi vya siri vya kiadiolojia-kisiasa kwa ada na mtazamno wa Kishia. Kuunda na kuongoza kwa siri mtandao mpana wa kitablighi na ufikishaji ujumbe kwa minajili ya kueneza mwanga wa Uimamu wa Ahlu-Bayt (a.s) na kubainisha kwa usahihi kadhia ya Uimamu; mtandao ambao ulikuwa umeenea katika maeneo mbalimbali ya mataifa ya Waislamu hususan kando kando Iraq, Khorasan, harakati kubwa na zenye matunda kuhusiana na Uimamu zilikuwa chini ya usimamizi na uongozi wake. [85].

Sifa Maalumu za Kimaadili, Karama na Fadhila

Imekuja katika vitabu na vyanzo vya hadithi katika uga wa sifa maalumu za kimaadili za Imamu Swadiq (a.s) ya kwamba, mtukufu huyu alikuwa na zuhdi (mtu mwenye kuipa mgongo dunia), mwenye kutoa na kusaidia watu, alikuwa na elimu isiyo na mithili katika zama zake, mwenye kufanya ibada kwa wingi na alikuwa akisoma sana Qur'ani. Muhammad ibn Talha anataja wasifu wa Imamu Swadiq (a.s) kwamba, alikuwa shakhsia mkubwa zaidi wa Ahlul-Bayt (a.s), mwenye elimu nyingi, ameshikamana sana na ibada, kuipa mgongo dunia na kusoma Qur'ani. [86]

Malik ibn Anas, mmoja wa Maimamu wa kifikihi wa Ahlu-Sunna amesema: Katika kipindi ambacho nilikuwa nikienda kwa Imamu Swadiq (a.s), daima nilikuwa nikimkuta katika moja kati ya hali tatu: Nilikuwa namkuta ima anaswali, amefunga au anamdhukuru na kuumtaja Mwenyezi Mungu. [87]

Kitabu cha Bihar al-Anwar cha Allama Muhammad Baqir Majlisi kimeandika: Imamu Swadiq (a.s) alimpatia masikini aliyemuomba dirihamu 400, baada ya kuona hajashukuru akatoa pete yake iliyokuwa na thamani ya dirihamu 10,000 na kumpatia. [88] Kuna hadithi pia zinazoonyesha kuwa, Imamu Swadiq (a.s) alikuwa akitoa na kuwasaidia watu kwa siri na kwa kificho. Kitabu cha al-Kafi kilichoandikwa Muhammad bin Yaqub ibn Is'haq Kulayni (Thiqat al-Islam) kinaeleza kuwa, Imamu Swadiq (a.s) alikuwa akitoka wakati wa usiku akiwa amebeba mikate, nyama na pesa na kugonga milango ya watu masikini na wenye kuhitaji, hali ya kuwa ameficha uso wake asijulikane na kugawa vitu hivyo baina yao katika mji. [89] Abu Ja'far Khath'ami ananukuu ya kwamba, Imamu Swadiq (a.s) alimpatia mfuko wenye fedha na kumtaka ampatie mtu mmoja katika Bani Hashim na asimwambie kuwa umetoka kwa nani. Khath'ami anasema: Wakati mtu yule alipochukua mfuko ule uliokuwa na fedha, akamuombea dua mtu aliyeutuma na akaonyesha malalamiko kwa Imam Swadiq(a.s) ya kwamba, licha ya kuwa na utajiri lakini hampatii chochote. [90] Abu Abdallah Balkhi yeye pia ananukuu kwanmba: Siku moja Imamu Swadiq (a.s) alizungumza na kuhutubu mtende uliokuwa umechakaa kwa kuuambia: Ewe mtende unayemtii Mola wako, tulishe kutokana na yale aliyoweka ndani yako Mwenyezi Mungu, katika hali hiyo mara zikaanza kutunyeshea tende za rangi kwa rangi kutoka katika mtende ule. [92]

Safari ya Kuelekea Iraq

Katika zama za utawala wa Saffah na vilevile katika kipindi cha utawala wa Mansur Dawaniqi, Imamu Swadiq (a.s) alifanya safari huko Iraq kutokana na kuitwa na tawala hizo. Katika safari hizo, Imam alikwenda katika miji ya Karbala, Najaf, Kufa na Hira. [92] Muhammad bin Maaruf Hilali ananukuu kwamba, katika safari ya Imam huko Hira, watu walimpokea kwa wingi sana; kiasi kwamba, kutokana na msongamano mkubwa wa watu mpaka kwa siku kadhaa hakufanikiwa kukutana na Imam. [93] Mihrabu ya Imamu Swadiq (a.s) katika msikiti wa Kufa ipo katika upande wa mashariki wa msikiti jirani na kaburi la Muslim ibn Aqil na mihrabu yake katika msikiti wa Sahla ni miongoni mwa kumbukumbu zilizoachwa na Imam huyu huko Iraq. [94] Imamu Swadiq (a.s) alilizuru na kulitembelea kaburi la Imamu Hussein (a.s) katika mji wa Karbala. [95] Katika pwani ya mto Husseiniya katika mji wa Karbala kuna jengo ambalo ndani yake kuna mihrabu ambayo inanasibishwa na Imamu Swadiq (a.s). [96]

Kuonyesha Kaburi la Imam Ali (a.s)

Imekuja katika baadhi ya hadithi kuhusiana na ziara za Imam Swadiq (a.s) katika kaburi la Imam Ali (a.s). [97] Imamu Swadiq aliwaonyesha masahaba zake kaburi la Imam Ali (a.s) ambalo kabla ya hapo halikuwa likitambuulika wazi. Sheikh Kulayni anasema: Kuna siku Imam Swadiq alimchukua Yazid ibn Amru ibn Talha katika eneo moja huko Hira na Najaf na akamuonyesha kaburi la babu yake yaani Imam Ali (a.s). [98] Sheikh Tusi pia amenukuu kwamba, Imamu Swadiq (a.s) alikwenda katika kaburi la Imam Ali (a.s) akaswali kisha akamuonyesha Yunis ibn Dhabyan lilipo kaburi la Imam Ali (a.s). [99]

Wanafunzi na Wapokezi wa Hadithi

Makala asili: Orodha ya Masahaba wa Imam Swadiq (a.s)

Sheikh Tusi ameandika katika kitabu chake cha Rijal takribani majina 3200 ya watu waliopokea hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) [100] Sheikh Mufidu ametaja katika kitabu chake cha Irshad idadi ya wapokezi wa hadithi wa Imamu Swadiq (a.s) kuwa ni 4,000. [101] Inaelezwa kuwa, ibn Uqdah alikuwa na kitabu kuhusiana na wapokezi wa hadithi wa Imamu Swadiq (a.s) ambapo ndani yake ameorodhhesha majina ya wapokezi 4000. [102] Idadi kubwa ya waandishi wa Usul Ar'ba Mia (ni majimui ya vitabu 400 vya hadithi ambavyo vilikusanywa na wapokezi wa awali wa hadithi wa Kishia) walikuwa ni wanafunzi wa Imamu Swadiq (a.s). [103] Kadhalika ikilinganishwa na Maimamu wengine, Imam Swadiq alikuwa na wanafunzi wengi miongoni mwa As'hab Ij'maa (kundi maalumu la wapokezi wa hadithi ambalo kwa mujibu wa wataalamu wa elimu ya hadithi wana daraja ya juu ya kuaminika) ambalo linaaminiwa mno na Maimamu miongoni mwa wapokezi wa hadithi. [104] Baadhi ya wanafunzi mashuhuri wa Imamu Swadiq (a.s) ambao ni miongoni mwa As'hab Ij'maa ni:

  1. Zurara ibn A'yun.
  2. Muhammad ibn Muslim.
  3. Burayd ibn Mu'awiya.
  4. Jamil ibn Darraj.
  5. Abdallah ibn Muskan.
  6. Abdallah ibn Bukayr.
  7. Hammad ibn Othman.
  8. Hammad ibn Issa.
  9. Aban ibn Othman.
  10. Abu Basir Asadi.
  11. Hisham ibn Salim.
  12. Hisham ibn Hakam. [105]

Kuna hadithi iliyopokewa kutoka kwa Muhammad ibn Omar ibn Abdul-Aziz Kashi kuhusiana na mdahalo wa wanafunzi wa Imamu Swadiq (a.s) ambayo inaonyeshha kuwa, baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wamebobea katika uga na taaluma fulani. [106] Kwa mujibu wa hadithi hii Humran ibn A'yan alikuwa amebobea katika Ulum al-Qur'an (elimu ya Qur'ani), Aban ibn Taghlib alikuwa na umahiri katika fasihi ya lugha ya Kiarabu, Zurarah ibn A'yun alikuwa na ubobezi katika Fiq'h, Mu'min al-Taq na Hisham ibn Salim walikuwa wametabahabari na kubobea katika elimu ya theolojia. [107] Baadhi ya wanafunzi wengine wa Imamu Swadiq (a.s) waliokuwa wamebobea katika elimu ya theolojia ni Humran ibn A'yan, Qays al-Masir na Hisham ibn al-Hakam. [108]

Ahlu-sunna

Baadhi ya Maulamaa na Maimamu wa fiq'hi wa Kisuni walikuwa ni wanafunzi wa Imamu Swadiq (a.s). Sheikh Tusi amemtaja Abu Hanifa katika kitabu chake cha Rijal kwamba, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Swadiq(a.s). [109] Ibn Abi al-Hadid Mu'tazili naye pia amemtaja kuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imamu Swadiq. [110]. Sheikh Swaduq amenukuu kutoka kwa Malik ibn Anas ya kwamba, kipindi fulani alikuwa akienda kwa Imam Swadiq na kusikiliza hadithi kutoka kwake. [111] Malik ibn Anas amenukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) katika kitabu chake cha Muwatta. [112] Ibn Hajar Haytami ameandika, wanazuoni wa Kisuni kama Abu Hanifa, Yahya bin Said, Ibn Jurayh, Malik ibn Anas, Sufyan ibn Uyayna, Sufyan al-Thawri, Shu'bah ibn al-Hajjaj na Ayub Sakhtiyani walinukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s). [113] Katika kitabu cha Aimah al-Ar'ba imeelezwa kuwa, uwepo wa Malik ibn Anas mjini Madina na kustafidi kwake na darsa na masomo yaliyokuwa yakitolewa na watu kama Imamu Swadiq (a.s) ilikuwa moja ya sababu za yeye kuwa na upeo wa kielimu. [114]

Mtazamo wa Ahlu-Sunna Kuhusu Imamu Swadiq (a.s)

Imamu Swadiq (a.s) alikuwa na nafasi na daraja ya juu kwa shakhsia na wasomi wakubwa wa Ahlu-Sunna. Abu Hanifa ni mmoja wa wanazuoni na viongozi wa madhehebu ya Kisuni ambaye yeye alimtaja na kumtambua Imamu Swadiq (a.s) kwamba, ndiye fakihi zaidi na msomi zaidi miongoni mwa Waislamu. [115] Ibn Shahrashub ananukuu ya kwamba, Malik ibn Anas amesema: “Kwa upande wa fadhila, elimu, kufanya ibada na uchaji Mungu hakuna jicho lililoona na hakuna sikio lilisikia mtu mwingine zaidi ya Ja'far ibn Muhammad.” [116] Kwa mujibu wa mtazamo wa Shahrastani katika kitabu chake cha al-Milal wa al-Nihal ni kwamba, Imamu Swadiq (a.s) ana elimu nyingi na kubwa katika katika mambo ya dini, ana elimu na maarifa kamili katika hekima na zuhdi (kuipa mgongo dunia) ya daraja ya juu duniani na uchaji Mungu na kujiweka mbali na kikamilifu kabisa na hawaa na matamanio ya nafsi ambapo kipindi fulani aliishi mjini Madina ambapo aliwanufaisha Mashia na wafuasi wake na kuwafundisha wafuasi wake maalumu siri za elimu na yaliyojificha katika maarifa. Imam Swadiq ni mtu ambaye alikuwa amezama na kubobea katika bahari ya maarifa na elimu na ambaye alikuwa amefikia daraja ya juu kabisa ya ukweli na uhakika na katu hakuwa na woga wa kuporomoka na kushuka katika daraja za dunia. [117] Ibn Abil al-Hadid anasema, wanazuoni na Maulamaa wa Kisuni wakiwemo viongozi wao wa Kifikihi kama Abu Hanifa, Ahmad ibn Hanbal na Imam Shafi walikuwa wanafunzi wa Imam Swadiq(a.s) moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kwa muktadha huo, fikihi ya Ahlu-Sunna ina mizizi ya fikihi ya Kishia. [118] Lakini pamoja na hayo yote katika fikihi ya Ahlu-Sunna licha ya uwepo wa uzingatiaji mkubwa wa mafakihi walioishi katika zama za Imamu Swadiq kama Awzai na Sufyan al-Thawri, mitazamno yake haijazingatiwa. [119] Ni kutokana na hili ndio maana baadhi ya Maulamaa wa Kishia kama Sayyid Murtadha aliwakosoa Maulamaa wa Ahlu Sunna.

Kufa Shahidi

Sheikh Swaduq amesema wazi na bayana kabisa kwamba, Imamu Swadiq (a.s) aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala Mansur Dawaniqi kutokana na athari ya sumu aliyokuwa amepewa. [120] Ibn Shahrashub pia ana mtazamo huo huo na amelibainisha hilo katika kitabu chake cha Manaqi Aal Abi Talib kama ambavyo Muhammad ibn Jarir Tabari wa tatu ana mtazamo kama huo pia ambao ameueleza katika kitabu chake cha Dalail al-Aimah. [121] Mkabala na hao, Sheikh Mufid anaamini kwamba, hakuna hoja madhubuti kuhusiana na jinsi Imamu Swadiq (a.s) alivyokufa shahidi. [122] Kaburi lake linapatikana mjini Madina katika makaburi ya Baqii, kando ya kaburi la baba yake Imamu Baqir (a.s) na kaburi la Imamu Sajjad (a.s) na Imamu Hassan (a.s). [123]

Wosia wa Imamu Swadiq (a.s)

Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali Imamu Swadiq (a.s) alimtambulisha Imam Kadhim (a.s) mara chungu nzima mbele ya masahaba zake kwamba, ndiye Imamu na kiongozi baada yake; [124] hata hivyo kutokana na kufuatiliwa mno na utawala wa Bani Abbas na akiwa na lengo la kulinda roho na uhai wa Imamu Kadhim (a.s) aliwatambulisha watu watano katika wosia wake akiwemo Mansur Dawaniqi mwenyewe kwamba, ndio warithi na wasii wake baada ya yeye kuaga dunia. [125] Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana baadhi ya masahaba wake mahiri kama Mu’min al-Taq na Hisham ibn Salim waliingiwa na shaka kuhusiana na mrithi wa Imam Swadiq(a.s). Awali walimuendea Abdallah Aftah na kumuuliza maswali, hata hivyo majibu ya Abdallah hayakuwatosheleza. Kisha wakakutana na Mussa ibn Ja'far (a.s) na wakatosheka na majibu yake na wakaukubali Uimamu wake.[126]

Mgawanyiko katika Ushia

Baada ya kufa shahidi Imamu Swadiq (a.s) kuliibuka makundi mbalimbali katika Ushia na kila kundi mingoni mwa makundi hayo lilimtambua mmoja wa watoto wake kuwa ni Imam. Hata hivyo Mashia waliowengi walimtambua na kumkubali Imamu Musa Kadhim (a.s) kuwa ni Imam wa Saba. [127] Kundi fulani miongoni mwa Mashia, lilikataa kukubali kifo cha Ismail mtoto mkubwa wa Imamu Swadiq (a.s) na kumtambua kama ndiye Imam na kiongozi baada ya Imamu Swadiq (a.s). Kundi miongoni mwa makundi hayo ambalo lilikuwa limekata tamaa na suala la kwamba, Ismail angali hai, lilikuwa likimtambua Muhammad mtoto wa Ismail kuwa ndiye Imam. Kundi hili likaondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Ismailiya. Wengine walikuwa wakimtambua Abdallah Aftah kuwa mtoto wa pili wa Imam Swadiq kuwa ndiye Imam ambapo likaondokea kuwa mashuhuri wa jina la Fatahiyah; lakini baada ya kifo chake ambacho kilitokea takriban siku 70 baada ya kufa shahidi Imam Swadiq(a.s), wakaamini Uimamu wa Mussa bin J’afar. Kuna kundi jingine pia ambalo lilikuwa likimfuata mtu aliyejulikana kwa jina la Nawus na hivyo kuondokea kundi jingine lililojulikana kwa jina la Nawusiyyah. Wengine pia walikuwa wakiamini Uimamu wa Muhammad al-Dibaj mtoto mwingine wa Imam Swadiq(a.s). [128]

Vitabu vya Imam Swadiq (a.s)

Katika baadhi ya vitabu vya hadithi vya Shia kuna barua ndefu za Imamu Swadiq (a.s) ambapo kuna shaka juu ya kuzungumzia baadhi yake. Hata hivyo baadhi yake zimekuja katika vitabu kama al-Kafi na zina zinazingatiwa kwa hali ya juu. [129] Baadhi ya barua hizo ni:

  • Risala ya Imamu Swadiq (a.s) kwa masahaba. Barua hii inajumuisha nasaha na maagizo kwa Mashia katika nyuga mbalimbali na barua hii imekuja katika kitabu cha al-Kafi. [130]
  • Risalt al-Ahwaziyah: Barua hii iliandikwa kwa ajili ya Najjashi, liwali na gavana wa Ahwaz.
  • Tawhid al-Mufadhal au Kitabu Fakkir: Risalaa hii ni mkusanyiko wa maneno ya Imam Swadiq kuhusiana na kumtambua Mwenyezi Mungu ambayo alimuandikia Mufadhal ibn Omar.
  • Matini mashuhuri kwa jina la Tafsiri ya Imamu Swadiq (a.s).

Kuna vitabu vingi vilivyoandikwa kuhusiana na Imamu Swadiq (a.s). Kuna vitabu takribani 800 vilivyochapishwa vinavyohusiana na Imam Swadiq.[131] Vitabu vikongwe na vya kale zaidi ni Akhbar al-Swadiq Maa Abi Hanifa, Akhbar al-Swadiq Maa al-Mansur vilivyoandikwa na Muhammad ibn Wahban Dubail, Dabil (vya karne ya 4 H) na Akhbar Ja'far ibn Muhammad kilichoandikwa na Abdul-Aziz Jaludi (karne ya 4 H). [132].

Baadhi ya vitabu kuhusiana na Imamu Swadiq (a.s) ni:

  • Al-Imam Swadiq(a.s) Wal-Madhahib al-Ar’baa mwandishi Asad Haidar. Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi na Kiswahili. [133]
  • Kitabnameh Imam Swadiq(a.s), mwandishi: Reza Ostadi.
  • Al-Imam Swadiq(a.s), mwandishi: Muhammad Hussein Muzaffar.
  • Mausuat al-Imam Ja'far al-Swadiq, mwandishi: Hisham al-Qutait.
  • Al-Imam Ja'far al-Swadiq, mwandishi: Baqir Sharif Qureshi.

Rejea

Vyanzo