Bibi Fatima amani iwe juu yake

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Binti ya Mtume (s.a.w.w))

Bibi Fatima (a.s) (Kiarabu: السيدة فاطمة الزهراء عليها السلام) anayejulikana kwa jina la Fatimatu Al-Zahraa, ni binti wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupitia mkewe wa mwanzo, bibi Khadijatu Al-Kubra (a.s). Bibi Fatima (a.s) ni mke wa Imamu Ali (a.s). Yeye ni miongoni mwa watu watano wa kizazi kitukufu cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) (Ahlul-Bait). Watano ambao hutambulika na Mashia wanao amini Maimamu Kumi na mbili, kama ni maasumina (waliotakaswa). Imamu wa pili na watatu (Imamu Hussein) (a.s) wa Mashia, bibi Zainab, pamoja na Ummu Kulthum, wote kwa pamoja ni watoto wa bibi Fatima (a.s). Zahraa, Batuul, Sayyidatu Nisa-u Al-Alamiin, na Ummu Abiiha, ni lakabu zake maarufu. Bibi Fatima (a.s) alikuwa ni mwanamke pekee aliyefuatana na Mtume (s.a.w.w) siku ya Mubahala ‌‌Baina ya Mtume na Wakristo wa Najrani.

Suratu al-Kawthar, Ayatu Al-Tat-hiir (Aya Utakaso), Aya ya Mawaddah, na Ayatu Al-It-a’a’m (Aya ya Kulisha Maskini), ziliteremka zikizungumzia wasifu wa bibi Fatima (a.s) na tabia zake njema. Kuna Hadithi kadhaa, ikiwemo Hadithi ya Bidh-'ah, zimesimulia wazi heshima na fadhila za bibi Fatima (a.s). Imesimuliwa Hadith Mtume (s.a.w.w) ikisema kwamba; Mtume (s.a.w.w) alimtambulisha bibi Fatima (a.s) kuwa ni mwanamke bora ulimwenguni na Akhera. Na alimsifia kwa kusema; Hasira na radhi za bibi Fatima (a.s) zinafunagamana moja kwa moja na ghadhabu na radhi za Mwenyezi Mungu (s.w).

Kuna ripoti chache tu zilizoripotiwa kuhusiana na maisha ya utoto na ujana kwake. Ripoti pekee zilizonukuliwa kuhusiana na zama za utotoni na ujanani kwake, ni ile ripoti inayohusiana na usuhaba wake na Mtume (s.a.w.w) dhidi ya vurugu za washirikina, ripoti ya kuwa pamoja na Mtume (s.a.w.w) katika bustani maarufu ya Shu'uba Abi Talib, na ile ripoti inayozungumzia kushiriki kwake katika safari ya kuhama kwa Mtume (s.a.w.w) na kuelekea Madina yeye pamoja na Imamu Ali (a.s).

Fatima (a.s) aliolewa na Imamu Ali (a.s) mwaka wa pili wa Hijiria. Alifanya shughuli mbali mbali za kijamii akishirikiana na Mtume (s.a.w.w) katika baadhi ya vita. Moja kati ya kumbukumbu za kazi hizo, ni ule ushirikiano wake akiwa pamoja na Waislamu wengine katika tukio la ukombozi wa Makka (Fathu Makka).

Katika tukio la Saqifa, wakati alipo simama kidete kupinga maamuzi ya baraza la Saqifah, Fatima (a.s) alikataa kuutambua Ukhalifa wa Abu Bakar na hakutoa kura ya kiapo cha utiifu kwake. Badala yake, aliuhisabu uamuzi huo wa kumteua Abu Bakar kushika nafasi ya Ukhalifa, kuwa ni mapinduzi yaliyo fosi kwa nguvu nafasi ya Ukhalifa. Katika tukio la kutekwa na kuporwa kwa Fadak akiutetea Ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), bibi Fatima (a.s) alitoa hotuba yake maarufu iliyojulikana kwa jina la Kiarabu Khutbatu Al-Fadakiyyah. Muda mfupi baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), wakati wa mashambulizi ya mawakala wa Abu Bakar kwenye nyumba yake, bibi Fatima (a.s) alijeruhiwa, akaugua, na baada ya muda si mrefu, akafa shahidi akiwa katika mji wa Madina tarehe 3 Mfunguo Tisa (Jumadi Al-Thani), mwaka wa 11 Hijiria. Mwili wa binti wa Mtume (s.a.w.w) ulizikwa usiku na kwa siri kupitia amri na wasia wake yeye mwenyewe. Kaburi la bibi Fatima (a.s) halikujulikana kamwe wapi lilipo hadi leo.

Tasbihatu Al-Zahraa (Tasbihi zisomwazo kila baada ya sala ya faradhi), Mus'hafu Fatima na Khutba ya Fadakiyyah, ni sehemu ya urithi na mafunzo ya kiroho kutoka kwa bibi Fatima (a.s). Mus'hafu Fatima ni kitabu chenye mafunzo na miongozo maalumu iliyotokana na Malaika wa Mwenyezi Mungu. Kitabu hichi baadae kilihaririwa na Imamu Ali (a.s). Kwa mujibu wa Hadithi, kitabu hichi kilikuwa mikononi mwa Maimamu kumi na moja waliopita (a.s), na kwa sasa kiko mikononi mwa Imamu wa kumi na mbili, ambaye ni Imamu Mahdi (a.t.f.s).

Mashia wanamtambua bibi Fatima (a.s) kama ni kigezo chao cha kuigwa. Mashia huomboleza kila mwaka siku ya kumbukumbu ya kifo chake cha kishahidi, maombolezo hayo huchukua siku kadhaa. Siku za maombolezo ya kifo cha bibi Fatima (a.s) hutambulikana kwa jina la Siku za Fatimiyyah. Nchini Iran, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Fatima (a.s), ambayo ni sawa ana mwezi 20 Mfunguo Tisa (Jumadi al-Thani), ni siku ya wanawake nchini humo. Jina Fatima na Zahra ni miongoni mwa majina mengi na maarufu kwa wasichana wanaoishi nchini Iran.

Majina na Nasaba Zake (a.s)

Bibi Fatima ni binti wa Mtume Muhammad bin Abdullah (s.a.w.w), na ni mwana wa Khadijah binti Khuwailid. Bibi Fatima (a.s) ana lakabu karibu 30. Miongoni mwazo ni: Al-Zahraa, Al-Siddiqah, Al-Muhaddathah, Al-Batul, Sayidatu Nisa-u Al-Alamin, Al-Mansurah, Al-Taahirah, Al-Mutahharah, Al-Zakiyyah, Al-Mubaarakah, Al-Radhiyyah na Al-Mardhiyyah. Hizi ni baadhi ya lakabu maarufu za bibi Fatima (a.s). [2]

Kuna Lakabu kadhaa zilizonasibishwa kwa bibi Fatima (a.s), nazo ni kama vile; Ummu Abiiha, Ummu Al-A-immah, Ummu Al-Hassan, Ummu Al-Hussein na Ummu Al-Muhsen. [3]

Angalia pia: Orodha ya Kuniya na Lakabu za Bibi Fatima Zahraa (a.s)


Maisha Yake

Bibi Fatima (a.s) ni mtoto wa mwisho wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Khadijah. [16] Kwa mujibu wa maandiko ya wanahistoria, Bibi Fatima (a.s) alizaliwa Makka katika nyumba ya bibi Khadijah (a.s) kwenye mtaa na chochoro iitwayo Al-Attaarin au Zuqaq Al-Hajar karibu na eneo la ibada ya Safa na Marwa. [17]

Kuzaliwa na Maisha ya Utotoni Mwake

Kwa mujibu wa maoni ya wengi miongozi mwa Mashia ni kwamba, bibi Fatima (a.s) alizaliwa ndani ya mwaka wa tano wa Utume. Mwaka uliojulikana kwa jina la Sanatu Al-Ahaqafiyyah (mwaka wa kuteremshwa kwa Surat Al-Ahqaf) [18] [19] Sheikh Mofid na Kaf-ami wanaamini ya kwamba, tokeo hilo limetokea mwaka wa pili baada ya Utume. [20] Kwa mujibu wa maoni mashuhuri ya wanazuoni wa Kisunni, bibi Fatima (a.s) alizaliwa mwaka wa tano kabla ya Utume. [21]

Vyanzo vya Kishia vimeelezea kuwa, bibi Fatima (a.s) alizaliwa mwezi 20 Jumadi Al-Thani. [22] Kuna ripoti chache za kihistoria lilizozungumzia maisha ya utotoni na ujanani mwake (a.s). [23] Maandiko ya kihistoria yanasema kwamba, baada ya kutanganzwa kwa Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), bibi Fatima (a.s) alishuhudia matukio mbali mbali ya unyanyasaji wa washirikina wa Kikuraish dhidi ya baba yake. Aidha, miaka mitatu ya utotoni mwake (a.s), ilimpita akiwa katika adhabu ya vikwazo vya kiuchumi na kijamii, ambapo yeye pamoja Masahaba wengine, walikaa ndani ya bustani ya Abu Talib (Shu'uba Abu Talib), chini ya mashinikizo ya kiuchumi na kijamii yaliowekwa na washirikina dhidi ya ukoo wa Bani Hashem na wafuasi wa Mtume (s.a.w.w). [24]

Fatima bado akiwa mdogo, alimpoteza mama yake (bibi Khadijah) na kumpoteza ami ya baba yake (Abu Talib), ambaye alikuwa ni mfuasi na mtu muhimu katika Uislamu. [25] Uamuzi wa Maquraishi kumuua Mtume (s.a.w.w), [26] kuhama kwake Mtume (s.a.w.w) kutoka Makka kwenda Madina na kuhajiri (kuhama) kwake bibi Fatima (a.s) yeye na Imamu Ali (a.s) pamoja na baadhi ya wanawake, ndiyo matukio muhimu zaidi ya kihistoria kuhusiana na bibi Fatima (a.s). [27]

Kuposwa na Kuolewa Kwake

Makala Asili: Ndoa ya Ali na Fatima (a.s)

Bibi Fatima (a.s) aliposwa na wachumba wengi; Lakini mwishowe, akaolewa na Imamu Ali (a.s). Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, kufuatia kuhama kwa Mtume (s.a.w.w) kwenda Madina na kutokana na nafasi ya baba yake (s.a.w.w) ya uongozi wa umma wa Kiislamu, na kutokana na nasaba yake, yaani kule yeye kuwa ni binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), kulimfanya bibi Fatima (a.s) awe na nafasi ya juu ndani ya jamii. Na kukapelekea kupewa heshima kubwa mno miongoni mwa Waislamu [28]. Kwa upande mwengine, kule Mtume Muhammad (s.a.w.w) kumpenda Fatima (a.s) [29] ukiongezea na sifa azlizosifika nazo ukilinganisha na wanawake wengine wa zama zake, [30] kulisababisha baadhi ya Waislamu kuwa na shauku ya kumuo binti huyu wa Mtume (s.a.w.w). [31] Wengi miongoni mwa waliosilimu mapema au waliokuwa na uwezo wa kutosha wa kifedha, walionekana kupendekezwa na bibi Fatima (a.s).[32] Abu Bakar, Omar [33] na Abdul Rahman bin Auf [34] walikuwa ni miongoni mwa watu hawo. Wachumba wote walipokea jawabu na kauli ya kukataliwa kwa posa zao kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). [35] Akiwajibu ombi la posa zao, Mtume (s.a.w.w). alisema: “Ndoa ya Fatima ni jambo la mbinguni linalohitaji hukumu ya Mwenyezi Mungu (s.w). [37]

Ali (a.s) alitamani sana kumuoa bibi Fatima (a.s), hasa kwa kutokana na uhusiano wake wa kifamilia na Mtume (s.a.w.w) na kutokana na sifa zake za kimaadili na kidini alizosifika nazo [38]. Lakini kwa mujibu wa maandiko ya wanahistoria, nafsi yake haikumruhusu kirahisi kumposa binti ya Mtume (s.a.w.w) [39], ila Saa’d bin Maa'dh aliifikisha khabari hiyo kwa Mtume (s.a.w.w). Na Mtume (s.a.w.w) akakubaliana na pendekezo hilo la Ali (a.s) [40]. Mtume (s.a.w.w) alilifikisha pendelezo la Ali (a.s) kwa bibi Fatima (a.s) na kumsifia sifa zake nzuri alizopambika nazo za kitabia na kimaadili, sifa ambazo ziliambatana na ridhaa ya bibi Fatima (a.s). [41] Kilichofuatia hapo kilikuwa ni kule Mtume (s.a.w.w) kumuoza Ali (a.s) binti yake Fatima (a.s). [42] Miezi kadhaa baada hijra, Ali (a.s) alikuwa na hali ngumu ya kiuchumi na kimaisha sawa na hali waliokuwa nayo wahajiri wengine katika wakati huo. [43] Kutokana na hali hiyo aliyokuwa nayo, kufuatia ushauri wa Mtume (s.a.w.w), aliuza au kuiweka rehani nguo ambayo ilikuwa ni ngao yake ya kivita, kisha akatoa mahari na kumpa bibi Fatima (a.s).[44] Sherehe ya aqdi ya ndoa kati ya Ali (a.s) na bibi Fatima (a.s), ilifanyika mbele ya Waislamu msikitini. [45] Kuna utata kuhusu tarehe ya sherehe ya ndoa hiyo. Vyanzo vingi vimeashiria kuwa, tokeo hilo lilitokea mnamo mwaka wa pili wa Hijiria. [46] Sherehe ya harusi ilifanyika baada ya Vita vya Badri ndani ya mwezi wa Shawwal au Dhul Hijjah ya mwaka wa pili wa Hijiria.

Maisha Yake ya Ndoa Pamoja na Ali (a.s)

Tazama pia: Nyumba ya Fatima (a.s)

Katika Riwaya za kihistoria na simulizi mbali mbali imeelezwa kwamba, bibi Fatima (a.s) alimpenda sana Ali (a.s) kwa njia tofauti, na hata alipokuwa mbele ya Mtume (s.a.w.w) haficha mapenzi yake juu ya mumewe. [48] Kumheshimu mumuwe pia kulikuwa ni moja kati ya sifa muhimu alizosifika nazo bibi Fatima (a.s). Imeripotiwa kwamba, bibi Fatima (a.s) alikuwa akimtaja Ali (a.s) kwa maneno ya upendo [49] na pale mumuwe alikuwa mbele ya hadhara ya watu, alikuwa akimwita kiheshima kwa kutumia jina la kunia la Aba Al-Hassan. [50] Alijitahidi kujipamba kwa manukato na vipodozi mbali mbali pale alipokuwa nyumbani kwake. [50] Kipindi cha mwanzoni mwa maisha ya Fatima na Ali (a.s) kiliambatana na hali ngumu ya kiuchumi [52] kiasi ya kwamba wakati Fulani, hawakuweza kupata chakula cha kumlisha Hassan (a.s), [53] ila katu bibi Fatima (a.s) hakuonekana kulalamika kutokana na hali hiyo. Wakati mwengine alionekana akisokota nyuzi kupitia manyoya ya kondoo ili kumsaidia mumuwe kupata riziki.[54]

Kwa kuzingatia ushauri wa Mtume (s.a.w.w) [55], bibi Fatima (a.s) alipenda kufanya kazi za ndani ya nyumba yeye mwenyewe, huku akimwachia kazi na mambo ya nje ya nyumba mumewe (Ali) (a.s). [56] Hata pale Mtume (s.a.w.w) alipomtafutia msaidizi aliyejulikana kwa jina la bibi Feddhah, bado bibi Fatima (a.s) aliendelea kufanya nusu ya kazi za nyumbani mwake yeye mwenyewe. [57] Kulingana na baadhi ya ripoti, imeripotiwa ya kwamba; bibi Fatima (a.s) kwa hiari na ridhaa yake mwenye, alimshauri bibi Feddhah kufanya naye kazi kwa zamu. Yaani siku moja ni ya bibi Fatima katika kufanya kazi za nyumba, na siku ya pili ni zamu ya bibi Feddhah.

Watoto Wake

Vyanzo vya pande zote mbili, vya Kishia na Kisunni vinakubali ya kwamba, Hassan [59], Hussein [60], Zainab [61] na Ummu Kulthum [62] ni watoto wanne wa bibi Fatima na Ali (a.s). [63] Pia kutoka katika vyanzo vya Kishia na baadhi ya vyanzo vya Kisunni, imenukuliwa kuwepo kwa mtoto mwingine wa kiume aliye julikana kwa jina Muhsin au Muhsan. Mtoto ambaye anasadikiwa kufa tumboni baada ya bibi Fatima (a.s) kukumbwa na matatizo mbali mbali yaliyo msibu baada ya kifo cha baba yake Mtume Muhammad (s.a.w.w). [64]

Matukio ya Mwisho mwa Maisha Yake (a.s)

Ndani ya miezi michache ya mwishoni mwa maisha ya bibi Fatima (a.s), kama ilivyo nukuliwa na waandishi wa historia. Bibi Fatima (a.s) alikumbwa na matatizo mbali mbali yaliyomjeruhi nafsi yake. Nukuu za kihistoria zaeleza ya kwamba, katu bibi Fatima (a.s) hakuonenaka kutabasamu ndani ya kipindi hicho. [65] Miongoni mwa yale yaliomkuta ndani ya kipindi hicho ni; Kifo cha Mtume (s.a.w.w) na vugu vugu la kisiasa na kinyang'anyiro cha Ukhalifa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). [66] Uporaji wa Ukhalifa kupitia amri kutoka kwa Abu Bakar, ambapo bibi Fatima (a.s) alilazimika kuhutubu hotuba yake muhimu ya Fadak mbele ya Masahaba. [67] Hayo ndiyo yaliokuwa matukio muhimu sana katika kipindi cha mwishoni mwa maisha yake. bibi Fatima (a.s) akiwa sambamba bega kwa bega na Ali (a.s), alikuwa ni mmoja wa wapinzani wakuu wa baraza la Saqifah na Ukhalifa wa Abu Bakar. [68] Jambo ambalo lilipelekea kupata vitisho vya mara kwa mara vilivyukuwa vikiratibiwa na wakuu wa mfumo wa Ukhalifa wa baraza la Saqifah. Moja ya mfano wa vitisho hivyo, ni lile jaribio la kuichoma moto nyumba ya Fatima (a.s). [69] Kule Ali (a.s) kuto kubali kula kiapo cha utiifu cha kuuukubali Ukhalifa wa Abu Bakar, pamoja na wafuasi wa Ali (a.s) ambao ni wapinzani wa Abu Bakar kujificha ndani ya nyumba ya bibi Fatima (a.s), kulisababisha wapinzani wao waliokuwa wakiuunga mkono Ukhalifa wa Abu Bakar kuivamia nyumba yake. Katika shambulio hilo, bibi Fatima (a.s) alijeruhiwa akiwa katika harakati za kuwazuia wapinzani wake wasimchukue Ali (a.s) na wasimlazimishwa kula kiapo cha utiifu wa lazima wa kumkubali Abu Bakar. [70] Kujeruhiwa kwa bibi Fatima (a.s) kulipelekea mimba ya mtoto wake aliye tomboni kuharibika. [71] Baada ya tukio hili, bibi Fatima (a.s) aliugua na baada ya muda usio mrefu akafa kishahidi. [72] Kumeripotiwa Maneno mengi yaliyo nukuliwa kutoka kwa wanawake wa mji wa Madina waliokuwa wakimtembelea (wakimdaukia) akiwa katika hali ya ugonjwa. Ripoti hizi zinashiria kuto ridhika kwake na jamii iliyomzungu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). [73]

Bibi Fatima (a.s) alimuusia Ali (a.s) ya kwamba; wapinzani wake wasishiriki katika kuuswalia mwili wake, na wala asiwaruhusu kuhudhuria harakati za maziko yake. Kisha akamtaka Ali (a.s) amzike usiku. [74] Kwa mujibu wa maoni ya wengi miongoni mwa wanahistoria ni kwamba; [75] Fatima (a.s) Alikufa kishahidi akiwa ndani ya mji wa Madina mnamo Mwezi 3 Jumadi Al-Thani mwaka wa 11 Hijiria. [76] Kuna waliosema kuwa; umri wake ulikuwa ni miaka kumi na nane, [77] lakini katika Riwaya ya Imamu Baqir (a.s), umri wake ulitajwa kuwa ni miaka 23. [78]

Michango na Misimamo Yake Kisiasa

Bibi Fatima (a.s) alijishughulisha na shughuli nyingi za kijamii na kuwa na misimamo mbali mbali ya kisiasa. Kuhama kakwe kwenda Madina, kumtibu Mtume (s.a.w.w) wakati wa Vita vya Uhud, [79] kumpelekea chakula Mtume (s.a.w.w) akiwa katika Vita vya Khandaq [80] na kuandamana naye katika harakati za ukombozi wa kuikomboa Makka (Fathu Makka). [81] Ni miongoni mwa shughuli zake kabla ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). Pia bibi Fatima (a.s) alijishughulisha na shughuli nyingi za kisiasa ndani ya muda mfupi wa maisha yake, baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). Baadhi ya misimamo muhimu ya kisiasa ya bibi Fatima (a.s) ni: kupinga tukio la Saqifah la kuteuliwa kwa Abu Bakar kuwa Khalifa baada ya Mtume (s.a.w.w), kwenda kwenye nyumba za viongozi wa Muhajirina na Ansari na kuwataka wakiri juu ya ustahiki na ubora wa Imamu Ali (a.s) kwa ajili ya Ukhalifa, jitihada za kurudisha umiliki wa bustani ya Fadak, kusoma hotuba ya Fadaki mbele ya kundi la Wahajirina na Ansari, na kumtetea Ali (a.s) katika tukio la uvamizi wa nyumba yake. Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, maneno na tabia nyingi za Fatima (a.s) baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) zilikuwa ni ashirio la mwitikio wa kisiasa unaopinga unyakuzi na uporaji wa Ukhalifa uliofanywa na Abu Bakar na waliouunga mkono Ukhalifa wake. [82]

Kuto Kukubaliana na Uamuzi wa Baraza la Saqifa

Makala Asili: Tukio la Saqifa ya Bani Saa'idah

Baada ya kuundwa kwa baraza la Saqifah na kukusanywa kura na viapo vya utiifu kutoka kwa baadhi ya watu vilivyo muunga mkono Abu Bakar kuwa Khalifa. Bibi Fatima na Ali (a.s) pamoja na Masahaba kadhaa kama vile Talha na Zubeir, walikaa pembeni na kupinga vikali kitendo hicho. [83] Walifanya hivyo kwa sababu ya tukio la Ghadir la Mtume (s.a.w.w) kumtangaza Imamu Ali (a.s) kuwa ndiye naibu atakaye shika nafasi ya Ukhali baada yake. [84] Kwa mujibu wa Riwaya na maandiko ya kihistoria, bibi Fatima pamoja na Ali (a.s) walikwenda kwa Masahaba na kuwaomba msaada. Wakijibu ombi la bibi Fatima (a.s), Masahaba walisema kwamba; kama wangelifanya ombi kama hilo kabla ya kuapa kiapo cha utiif kwa Abu Bakar, basi wangeliweza kuunga mkono Ukhalifa wa Ali (a.s).[85]

Hadithi na Hotuba ya Fadak

Makala Asili: Kisa cha Fadak na hotuba ya Fadak

Baada ya Abu Bakar kuipokonya Fadak kutoka kwa bibi Fatima (a.s) na kuitaifisha kwa ajili ya manufaa ya Ukhalifa wake, bibi Fatima (a.s) alismama kidete na kupinga vikali tendo hilo. Baada ya mazozano na majadiliano ya muda mrefu baina ya Abu Bakar na bibi Fatima (a.s), hatimae Abu Bakar aliridhika na dalili madhubuti zilizotolea na bibi Fatima (a.s) katika kuitetea haki yake. Hatimae Abu Bakar akathibitisha kimaandishi kuwa; Fadak ni mali ya bibi Fatima (a.s). Lakini Umar bin Khattab alichukua maandishi yale kwa dharau kutoka kwa bibi Fatima (a.s) na kuyararua. [88] Baadhi ya vyanzo vimeripoti kwamba, Umar alimpiga bibi Fatima (a.s), pia imeelezwa kwamba, bibi Fatima (a.s) alijeruhiwa na kuharibika mimba yake katika tukio hilo. [89] Baada ya juhudi za bibi Fatima (a.s) za kutaka kuikamata tena Fadak kugonga ukuta na kukosa matunda, alienda kwenye Msikiti wa bwana Mtume (s.a.w.w) akasimama mbele ya Masahaba na kusoma hotuba. Hotuba ambayo baadae ilijulikana kama ni Hotuba ya Fadak, ambapo alilani vikali kitendo cha Abu Bakar cha kuitaifisha Bustani ya Fadak na kufosi nafasi ya Ukhalifa. Katika hotuba hiyo, bibi Fatima (a.s) alielezea ya kwamba; hatima ya matendo ya Abu Bakar na wafuasi wake, ni moto wa Jahannam.[90]

Kuunga Mkono Upande wa Waliopingana na Abu Bakar

Makala Asili: Tukio la Kukaa Ndani ya Nyumba ya Bibi Fatima

Baada ya Masahaba kumtangaza Abu Bakar kuwa ni Khalifa na kutoa kiapo chao cha utiifu kwake, huku wakupuuza hotuba ya Mtume (s.a.w.w) juu ya urithi wa Imamu Ali (a.s), bibi Fatima, Ali (a.s), Bani Hashim na idadi kadhaa ya Masahaba walipinga vikali, na hawakukubali kuliunga mkono suala hilo, na waliendelea kukaa kikao cha mgomo ndani ya nyumba ya bibi Fatima (a.s). [91] Abbas bin Abdu Al-Muttalib, Salman Farsi, Abu Dharr Al-Ghafari, Ammar bin Yasir, Miqdad, Ubayyah bin Kaa’b, na kundi la Bani Hashim walikuwa ni miongoni mwa waliogoma. [92]

Kumtetea Ali (a.s) katika Tukio la Kuvamiwa Nyumba Yake

Makala Asili: Tukio la kushambuliwa nyumba ya Bibi Fatma (a.s)

Kufuatia mashambulizi ya wafuasi wa Ukhalifa wa Abu Bakar kwenye nyumba ya Ali (a.s), bibi Fatima (a.s) alisimama mbele ya wavamizi hao na kuzuia azimio lao la kumlazimisha Ali (a.s) kula kiapo cha utiifu kwa Abu Bakar. Kwa mujibu wa nukuu na maelezo ya Ibn Abdi Rabbi, mmoja wa wanachuoni wa Kisunni wa karne ya 3 na 4, ni kwamba; Baada ya Abu Bakar kupewa habari kuhusu kukaa ndani kwa wapinzani wake katika nyumba ya Fatima (s.a.w.w.), kunakoashiria mgomo dhidi yake, aliamuru kufanyike mashambulizi ya kutawanywa kikao hicho. Na iwapo wataamua kujibu mashambulizi hayo, aliwataka wafuasi wake kupigana vita na wapinzani hao. Umar alikwenda nyumbani kwa bibi Fatima (a.s) akiandamana na idadi ya watu kadhaa, alipofika aliwakataka wapinzani hao watoke nje ya nyumba hiyo, huku akitishia kuichoma moto nyumba ya bibi Fatima (a.s), iwapo wataipuuza amri yake. [94] Omar na washambuliaji wengine waliingia ndani ya nyumba hiyo kwa nguvu. Wakati huo huo, bibi Fatima (a.s) aliwatishia wavamizi hao kwa kuwambia kwamba; ikiwa hawatatoka nje ya nyumba yake, basi atanyanyua mikono na kumlalamikia Mungu juu ya suala hilo. Hapo ndipo wavamizi hao walipoamua kutoka nje, huku wakimuacha Ali (a.s) na watu wa kizazi cha Bani Hashim peke yao. Wengi wote wakakokotwa na kupelekwa msikitini kwa nguvu, ili watoe kauli ya kiapo cha kumtii Abu Bakar”. [96]

Washambuliaji na wavamizi hao, baada ya kuchukua kwa nguvu kiapo cha utiifu kutoka kwa wapinzani hao, walirudi tena nyumabi kwa bibi Fatima (a.s), ili -kwa hali yoyote ile- wapate kiapo cha utiifu kutoka kwa Imamu Ali (a.s) na Bani Hashim. Waliamua kuishambulia tena nyumba ya bibi Fatima (a.s) na kuuchoma moto mlango wake. Bibi Fatima (a.s) ambaye alikuwa nyuma ya mlango wake, alijeruhiwa na kupelekea mimba yake changa ya (Muhsin) (a.s) kuharibika kutokana na athari za moto na shinikizo la Omar. Baadhi ya Riwaya zimeashiria ya kwamba; Qunfudh (Omar) alimweka bibi Fatima (a.s) baina ya mlango na ukuta wa nyumba, kisha akamsukumia mlango [98] na kumbamiza nao. Jambo ambalo lillpelea kuvunja ubavu wake. [99] Baada ya tukio hili, bib Fatima (a.s) alibaki kuuguzwa kitandani na mwishowe kufariki. [100]

Hasira za Bibi Fatima (a.s) Dhidi ya Abu Bakar na Omar

Kulikuwa na makabiliano makali yaliosimamiwa na Abu Bakar na Umar dhidi ya bibi Fatima (a.s) na Ali (a.s), juu ya suala la Fadak na matukio yanayohusiana na kulazimishwa kutoa kiapo cha utii juu ya Khalifa aliye chukua Ukalifa kimabavu. Hasira za bibi Fatima (a.s) dhidi ya Abu Bakar na Umar hazikusita hadi mwisho wa maisha yake. [101] Kwa mujibu wa ripoti kadhaa, baada ya Omar na wavamizi wengine kuishambulia nyumba ya bibi Fatima (a.s), Abu Bakar na Omar waliamua kwenda nyumbani kwa bibi Fatima (a.s) kwa ajili ya kumuomba msamaha. Lakini bibi Fatima (a.s) hakuwaruhusu kuingia nyumabai kwake. Hatimaye waliingia nyumbani humo baada kumbemeleza Ali (a.s), naye akawaombea ruhusa kutoka kwa bibi Fatima (a.s). Walipoingia ndani, bibi Fatima (a.s) aligeuza uso wake na kuelekea ukutani na hata salamu zao pia hakuzijibu. Baada ya kuwakumbusha ile Hadithi ya Bidh-'ah isemayo kwamba; furaha na hasira za Mtume (s.a.w.w) zimeegemea kwenye furaha na hasira za bibi Fatima (a.s), hapo bibi Fatima (a.s) aliwatangazia Abu Bakar na Omar kwamba wamemsababishia hasira. [102] Kuna baadhi ya ripoti zilizosema ya kuwa; bibi Fatima alikula kiapo kuwa atawaapiza kila baada ya sala zake. [103]

Kifo na Mazishi Yake (a.s)

Makala Asili: Kufariki kishahidi kwa bibi Fatima (s.a)

Bibi Fatima (a.s) alifariki mwaka wa 11 Hijiria baada ya ugonjwa uliosababishwa na majeraha ya kimwili aliyoyapata katika matukio yaliyo tokea baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w). [104] Kuna khitilafu kubwa juu ya tarehe halisi ya kifo chake (a.s). Khitilafu za wanahistoria juu ya uhalisia wa tarehe ya kifo chake (a.s), ni zenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa, tofauti ambazo zinaanzia kwenye kauli iliyosema kwamba, bibi Fatima (a.s) alifariki baada ya siku 40 hadi kufikia kauli iliyosema kuwa alifariki baada ya kupita miezi minane baada ya kifo Mtume (s.a.w.w). Ila kauli maarufu miongoni mwa Mashia ni ile isemayo kwamba; bibi Fatima (a.s) alifarika mwaka wa tatu wa Jumadi Al-Thani [106]. [107] Yaani, siku tisini na tano baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w). [108] Hati iliyo tegemewa katika ushahidi wa maneno haya, ni Riwaya kutoka kwa Imam Swadiq (a.s). [109] Ila kama tulivyo ashiria hapo mwanzo ya kwamba kuna khitilafu juu ya suala hili. Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengine ni kwamba, aliishi siku sabini na tano baada ya kifo cha Mtume Muhammad (s.a.w.w). [110] Yaani kifo cahake kilikuwa ni sawa na mwezi 13 Jumadi al-Awwal. Wengine wanasema alifariki mwezi nane Rabi al-Thani [111], na wengine wakasema alifariki mwezi kumi na tatu Rabi al-Thani. [112] Pia kuna waliosema ya kwamba, alifariki mwezi tatu Ramadhani. [113] Hivyo ndivyo wanazuoni walivyo khitalifiana katika kuainisha siku ya kifo chake (a.s). Hizo basi ndizo siku zinazodhaniwa kufa kishahidi kwa bibi Fatima (a.s).

Katika Riwaya mashuhuri, Imamu Kadhim (a.s) alibainisha wazi kuwa Bibi Fatima (a.s) alikufa kifo cha kishahidi. [114] Pia katika Riwaya ya Imamu Sadiq, imebainishwa wazi ya kwamba; kifo chake kilisababishwa na pigo la ala ya upanga wa Qunfudh (Omar). Ala aliyo mpiga nayo na kumsababishia kuharibika kwa mimba ya mwanawe aliye kuwa tumboni, ambaye alijulikana kwa jina la Muhsin. Pigo ambalo lilimsababishia bibi Fatima (a.s) maradhi na hatimae kufariki. [115]

Kulingana na maoni ya baadhi ya watafiti ni kwamba, wasia wa Fatima (a.s) wa kutaka kuzikwa mwili wake kwa siri na kificho, ilikuwa ni kitendo chake cha mwisho cha kisiasa cha kupinga na na kuonesha msimamo wake dhidi ya Ukhalifa.[116]

Mahali Alipozikwa

Makala Asili: Mahali alipozikwa Bibi Fatima (a.s)

Kabla ya kifo chake cha kishahidi, bibi Fatima (a.s) alikuwa ameusia ya kwamba, hataki watu waliomdhulumu na kumpandisha hasira wausalie mwili wake na kuhudhuria mazishi yake. Kwa hiyo, alitaka mazishi yake yafanyike kwa siri, na mahali pa kaburi lake pia pawe ni sehemu ya siri pasipojulikana. [117] Kwa mujibu wa kauli za wanahistoria, Ali (a.s) alimkosha mkewe kwa msaada wa bibi Asma binti Umais [118] kisha akamsalia. [119] Mbali na Imamu Ali (a.s), watu wengine kadhaa pia walishiriki katika sala hiyo, ila kuna khitilafu kuhusu idadi na majina ya watu hao. Vyanzo vya kihistoria vimewatambua watu hao kama ni: Imamu Hassan, Imamu Hussein, Abbas bin Abdul Muttalib, Miqdad, Salman, Abu Dharr, Ammar, Aqiil, Zubeir, Abdullah bin Masoud na Fazli bin Abbas. Historia imewataja wao kuwa ndio watu walioshiriki katika sala hiyo ya maiti.[120]

Baada ya kuzikwa tu, Imamu Ali (a.s) alitawanya athari za kaburi hilo, ili kaburi hilo lisijulikane. [121] Pamoja na ukweli ya kwamba, mahala na nukta halisi ya kaburi hilo halijulikani, ila kuna Riwaya mbalimbali kuhusu eneo lilipo kaburi hilo, ila nukta halisi ya kaburi hilo haijulikani. [122]

  • Baadhi ya wanahistoria wamesema, bibi Fatima (a.s) amezikwa katika eneo la Raudhatu Al-Nabi.[123]
  • Pia nyumba ya bibi Fatima na Imamu Ali (a.s) ni miongoni mwa mahali pengine palipodhaniwa kuwa ndio mahala alipozikwa bibi Fatima (a.s). Mahali ambapo pamegeuka kuwa ni sehemu ya msikiti, baada ya Masjidu Al-Nabi kupanuliwa katika kipindi cha utawala wa Banu Umayyah. [124]
  • Kuna baadhi ya vyanzo vilivyo ashiria kidole moja kwa moja mava ya Baqii' kuwa ndio mahali alipozikwa bibi Fatima (a.s). [125]
  • Nyumba ya Aqeel bin Abi Talib ni sehemu nyingine iliodhaniwa. Na kuna vyanzo vya kihistoria vinavyo ichukulia nyumba hiyo kuwa ni ndio mahali alipozikwa bibi Fatima (a.s). [126] Nyumba ya Aqeel ilikuwa ni nyumba kubwa, iliopo karibu na makaburi ya Baqi’i [127] na baada ya kuzikwa baadhi ya miili ya baadhi ya watu watukufu, akiwemo bibi Fatima binti Asad, Abbas bin Abdul Muttalib na idadi kadhaa ya maimamu wa Kishia (a.s) lilibadilika eneo hilo kutoka eneo la makazi na kugeuka kuwa ni mahali pa ziara ya watu kuja kuzuru makaburi ya watukufu hao. [128]

Fadhila na Wasifu wa Bibi Fatima (a.s)

Makala Asili: Fadhila za bibi Fatima (a.s)

Kuna sifa na fadhila nyingi mno zilizoripotiwa na kunukuliwa kutoka katika vyanzo vya Riwaya na Hadithi, vikiwemo vyanzo ya kihistoria vya Kishia pamoja na Kisunni. Baadhi ya sifa na maadili mema yalio nukuliwa kuhusiana na Fadhila na sifa za bibi Fatima (a.s), ni zile sifa zilizorikodiwa kutoka katika Aya za Qur'ani. Zikiwemo sifa zilizorikodiwa kutoka katika Aya ya utakaso na Aya ya Mubahala. Katika Aya hizo, Allah amewasifu watu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w) wote kwa pamoja. Bibi Fatima (a.s) naye moja kwa moja hufungamana na sifa hizo, kwa sababu naye ni mmoja wa watu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w). Pia kuna idadi kadhaa ya fadhila zilizotajwa katika Hadith, kama vile Hadithi ya Bidh-'ah na ile Hadithi iliompa sifa ya kuwa ni mwenye kusemezwa na Malaika (Al-Muhaddathah).

Utukufu na Isma Yake

Makala Asili: Isma ya Bibi Fatima

Kwa mujibu wa kauli ya Allamah Majlisi ni kwamba, Mashia hawakukhitalifiana juu ya uhakika wa umaasumu wa bibi Fatima (a.s). [129] Aya ya Tat-hir, [130] Hadithi ya Bidh-'ah na Hadithi nyengine zinazoungumzia umaasumu wa Ahlul-Bayt (a.s) ni miongoni mwa Hadithi zinazo thibitisha umaasumu wa bibi Fatima (a.s). [131] Kwa mujibu wa Aya ya utakaso (Ayatu Al-Tat-hiir), ni kwamba; Mwenyezi Mungu alitaka kuwatakasa Ahlul-Bait (a.s) kutokana na dhambi na aina zote za uchafu. Kwa mujibu wa Hadith nyingi za pande zote mbili za Kishia na Kisunni, bibi Fatima (a.s) ni mmoja wa watukufu wa kizazi cha Mtume (Ahlul-Bait) (a.s) waliotoharishwa kutokana na machau pamoja na maovu yote. [132] Kule yeye kuwa maasumu, kunapelekea awe na baadhi ya mambo na sifa ziendazo sawa na sifa za Mitume na Maimamu (a.s), kama vile kauli yake, tabia zake, mtazamo wake katika kuifasiri dini na Qur'ani, takriri yake (kulinyamazia jambo litendwalo mbele yake), nyenendo na mtindo wake wa kivitendo, pamoja na misimamo yake, kuwa ni vigezo vya kupambanua haki na batili. Maisha yake ya kisiasa na kijamii ni kigezo kamili cha kupambanua haki na batili. [133]

Vyanzo vya masimulizi Riwaya na historia vya Kisunni pia vimeripoti kwamba, Mtume (s.a.w.w) kupitia Aya ya Tat-hiir amewatambua watu wa familia yake ambao ni, bibi Fatima (a.s), Ali (a.s), Hassan (a.s) na Hussein (a.s), kuwa ni watu waliotoharishwa na Mwenye Ezi Mungu kutokana na dhambi. [134]

Ibada za Bibi Fatima (a.s)

Makala Asili: Sala za Bibi Fatima (a.s)

Bibi Fatima (a.s) kama alivyo Mtume (s.a.w.w), alikuwa akipenda sana ibada na alitumia sehemu muhimu ya nyakati zake katika sala na maombi. [135] Ndani ya baadhi ya vyanzo, kuna ripoti inyo elelezea kuwepo kwa usaidizi wa Kiungu kwa bibi Fatima (a.s); Kwa mfano, kuna siku Salman Farsi alishangazwa kumuona bibi Fatima (a.s) akisoma Qur'ani karibu na jiwe la kusagia huku jiwe la kusagia likiwa linajigeuza lenyewe. Salman alikwenda na kulijadili jambo hilo mbele ya Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w). Akamjibu kwa kusema: “...Mwenyezi Mungu amemtuma Jibril amgeuzie kinu (kiwe) chake.” [136] Kusimama kisimamo kirefu akisali sala za usiku, kukesha katika ibada, kuwaombea dua wengine wakiwemo majirani, [137] kufunga, na kuzuru makaburi ya mashahidi ni miongoni mwa sifa na tabia za kila siku za bibi Fatima (a.s). Matendo hayo aliyoshikamana nayo bibi Fatima (a.s), yalikuwa ni miongoni mwa matendo yaliosisitizwa mno, kutoka katika vinywa vya Masahaba, Matabiina pamoja na Ahlul-Bait (a.s). [138] Kule bibi Fatima (a.s) kushikamana na kuto tengana na matendo hayo, kumepelekea vitabu vya sala na dua, kuzinasibisha moja kwa moja baadhi ya sala na dua kwa bibi Fatima (a.s). [139]

Nafasi ya Bibi Fatima (a.s) Mbele ya Mungu na Mtume (s.a.w.w)

Wanazuoni wa Kishia [140] na Kisunni [141], kwa kuzingatia Aya ya 23 mashuhuri ya Surat Shura, inayojulikana kama ni Aya ya Mawaddah, wamesema kuwa; kumpenda bibi Fatima (a.s), ni jambo la faradhi na ni amri ya Mungu kwa Waislamu. Katika Aya ya Mawaddah, wafasiri wa Qur'an wameeleza kibaga unaga ya kwamba; ujira ambao Waislamu wanatakiwa kumlipa Mtume (s.a.w.w) ni kuwafanyia mapenzi watu wa nyumba yake (Ahlul-Bayt (a.s)). Kulingana na Riwaya na fafanuzi za wafasiri wa Qur'an, kizazi cha Mtume (s.a.w.w) ni bibi Fatima (a.s), Ali (a.s), pamoja na Hassanein, yaani Hassan na Hussein (a.s). 143] Mbali na Aya ya Mawaddah, kuna Riwaya tofaoti kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ambazo muktadha wake unaashiria kuwa, Mungu hukasirika endapo bibi Fatima (a.s) atakasirika na hufurahishwa na furaha yake (a.s). [144]

Sayyid Muhammad Hassan Mirjahani, amenukuu Hadithi katika kitabu chake kiitwacho Junnatu Al-‘Asimah, isemayo kwamba, kuumbwa kwa bibi Fatima (a.s) ndio sababu ya kuumbwa kwa mbingu. Hadithi hii, iitwayo Hadithi ya Laulaka, imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), na msingi wa muktadha wake ni kwamba, uumbwaji wa mbingu ulitegemea kwenye kuumbwa kwa bwana Mtume (s.a.w.w), na kuumbaji kwa Mtume kumetegemea katika kuumbwa kwa Ali (a.s), na kuumbwa kwa Mtume pamoja na Ali (a.s), kumetegemea kwenye kuumbwa bibi kwa bibi Fatima (a.s). [145] Baadhi na wanazuoni kuzingatia udhaifu wa mapokezi ya Riwaya hii, ila mamesema kuwa upo uwezekano wa kupata mashiko ya kufasiri maudhui yake. [146]

Mtume (s.a.w.w) alikuwa akimpenda sana bibi Fatima (a.s). Alionekana kumpenda na kumheshimu zaidi kuliko wengine. Katika Hadith ijulikanayo kwa jina la Hadithi ya Bidh-'ah, Mtume (s.a.w.w) anamtambulisha bibi Fatima (a.s), kama ni kipande cha mwili wake, na alisema kwamba, kumuudhi bibi Fatima (a.s), ni sawa na kuniudhi mimi. Riwaya hii imepokewa na tabaka la wanazuoni wa kwanza, akiwemo Sheikh Mufidu kwa upande wa wanazuoni wa Kishia, na Ahmad Ibn Hanbal kwa upande wa wanazuoni wa Kisunni. Ieleweke ya kwamba, Riwaya hii imepokewa kupitia njia tofauti. [147] Katika Hadithi nyingi zilizosimuliwa na wanazuoni wa upande wa Shia na Sunni, imeelezwa ya kwamba, bibi Fatima (a.s) ni mbora wa wanawake wa Peponi, mbora wa wanawake wa duniani na Akhera, na ni mbora wa wanawake wote wa uma huu. [148]

Mbora wa Wanawake

Katika Hadith nyingi zilizosimuliwa na Shia na Sunni, imeelezwa kwamba Fatima ni mbora wa wanawake wa peponi, mbora wa wanawake wa nyilimwengu mbili, na mbora wa wanawake wa Ummah.[158]

Mwanamke Pekee Aliyechaguliwa Kuhudhuria Mubahala

Miongoni mwa wanawake wa Kiislamu, bibi Fatima (a.s), ndiye mwanamke pekee aliyechaguliwa kuhudhuria tukio la Mubahala ‌‌Baina ya Mtume na Wakristo wa Najrani. Tukio hili limetajwa katika Aya ya Mubahala. Kwa mujibu wa vyanzo vya tafsiri na na simulizi za Riwaya pamoja na nukuu za kihistoria, Aya ya Mubahlah imewateremkia wata wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w), yaani imeshuka kwa ajili ya kuwasifu Ahlul-Bait wa Mtume (s.a.w.w). [149] Waliohudhuria katika tukio la Mubahalah wakiwa pamoja na Mtume (s.a.w.w) kutoka upande wa Waislamu walikuwa ni: Bibi Fatima (a.s), Imamu Ali (a.s), Imamu Hassan na Imamu Husein (a.s).

Uendelevu wa Kizazi cha Mtume (s.a.w.w) ni Kupitia kwa Bibi Fatima (a.s)

Uendelevu wa nasaba ya kizazi cha Mtume (s.a.w.w) ni kupitia kwa bibi Fatima (a.s). Moja kati ya fadhila za bibi Fatima (a.s) zilizoashiriwa kupitia vitabu tofauti, ni kule kuteuliwa kwa Maimamu wa Kishia kutoka katika kizazi chake (a.s). [151] Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wamezingatia kuwa, moja ya maana na tafsiri ya neno Kauthar, ni kule kuendelea kwa nasaba ya Mtume (s.a.w.w) kupitia kizazi cha bibi Fatima (a.s). Na ile tafsiri inayo lifasiri neno Kauthar kuwa ni kheri nyingi, maana ya kheri hizo, ni huko kuendelea kwa kizazi cha Mtume (s.a.w.w) kupitia kwake (a.s). [152]

Ukarimu Wake (a.s)

Ukarimu wa bibi Fatima (a.s) umeripotiwa kama ni moja ya sifa zake za kitabia na kimaadili. Katika maisha yake akiwa pamoja na Ali (a.s), wakati ambao alikuwa katika hali nzuri ya kiuchumi, bibi Fatima (a.s) alionekana kuishi katika hali ya maisha inayolingana na maisha ya watu wa kawaida. Aliishi na watu huku akiwa ni mkarimu kwa wengine. [153] Pia alikuwa ni sahili wa kutoa sadaka mara kwa mara. Miongoni mwa yaliorikodiwa katika ukarimu wake ni: kumzawadia muhitaji nguo ya yake ya harusi ndani ya usiku wa harusi yake (a.s),[154] kumzawadia maskini mkufu wake, [155] na kwalisha maskini, mayatima na mateka. [156] Kwa mujibu wa vitabu vya tafsiri, bibi Fatima, Imamu Ali pamoja na Hassan na Hussein (a.s) walitoa chakula chao kwa muda wa siku tatu mfululizo na kuwapa maskini, huku wao wenyewe wakibaki na njaa. Na hiyo ikawa ndio sababu ya kuteremka Aya ya 5 hadi 9 ya Surat Al-Insan, inayojulikana kama ni Aya Al- It-'aam (Aya ya kulisha). [157]

Kusemezwa Kwake na Malaika (a.s)

Miongoni mwa sifa zake bibi Fatima (a.s) zilizomfanya aitwe muhaddathah, ni kule kuzungumzishwa na Malaika. [158] Mazungumzo ya Malaika na bibi Fatima (a.s) wakati wa Mtume na baada ya kifo chake, yalikuwa na lengo la kumliwaza bibi Fatima (a.s). Malaika walimjuza bibi Fatima (a.s) habari za mustakabali wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w). [159] Khabari za matukio ya baadae aliompashwa habari bibi Fatima (a.s) na malaika wa Mwenyezi Mungu, yaliandikwa na kurikodiwa na Imamu Ali (a.s) na kupewa jina la Mus-haf Fatima. [160]

Urithi wa Kiroho

Maneno ya bibi Fatima (a.s), maisha yake ya kiibada, kisiasa na kijamii, yametambuliwa kama ni mabaki muhimu ya urithi kutoka kwake, urithi ambao umepewa thamani kubwa na Waislamu. Waandishi wa mambo ya kihistoria wameurikodi na kuutambua kama ni moja kati ya mabaki ya athari za kihistoria za Waislamu ulimwenguni. Mushaf Fatima (Msahafu wa Fatima), Khutba ya Fadakiyyah, nyiradi na sala za bibi Fatima (a.s), ni sehemu ya urithi wa kiroho uliorithiwa kutoka kwa bibi Fatima (a.s).

  • Masimulizi ya Riwaya zake ni sehemu moja muhimu ya urithi wa bibi Fatima (a.s). Riwaya zilizorikodiwa kutoka kwa bibi Fatima (a.s) zimekusanya ndani yake aina tofaut za maudhui. zipo zilizo husiana na masuala ya kiitikadi, kifiqhi, kimaadili na kijamii. Baadhi ya Hadithi zake zimetajwa katika vitabu vya Hadith vya Kishia na Kisunni. Pia kuna idadi kadhaa ya hadithi zilizokusanywa katika vitabu vinavyojitegemea na vyenye majina maalumu, kama vile «Musnad Fatima» na «Akhbaru Fatima». Baadhi ya vitabu hivyo vimepotea na kutoweka na kukabaki simulizi tu zilizosimuliwa na wasimuliaji pamoja na waandishi wa vitabu. Baadhi ya simulizi za vitabu hivyo, zimesimuliwa ndani ya vitabu vya elimu ya nasaba za wapokezi wa Hadithi (Elmu Al-Rijaal). [165]
  • Msahafu wa bibi Fatima (a.s), una maudhui ambazo bibi Fatima (a.s) alizisikia moja kwa moja kutoka kwa Malaika wa Mwenyezi Mungu. Maudhui ambazo ziliandikwa na kurikodiwa na Imamu Ali (a.s). [166] Kwa mujibu wa mtazamo wa wanazuoni wa Kishia, Msahafu wa bibi Fatima (a.s), ulibaki katika mikono ya Maimamu wa Kishia, na kila Imamu aliukabidhi Msahafu huo kwa Imamu mwingine aliye fuatia baada yake. [167] Kwa mujibu wa mtazamo huo, hakuna yeyote isipokuwa aliyeweza kuushika Msahafu huo Maimamu (a.s). Inaaminiwa ya kwamba, kwa hivi sasa Msahafu huo uko mikononi mwa Imamu Zaman, yaani Imamu Mahdi (a.s).[168]
  • Hotuba ya Fadakiyyah ni moja wapo ya hotuba maarufu za bibi Fatima (a.s) iliyo husiana na tukio la Saqifa, unyakuzi wa Ukhalifa na upokonyaji wa Fadak. Maandiko kadhaa yaliyo andikwa kuhusiana na Hotuba ya Fadakiyyah, mengi yake yanatambuliwa kuwa ni ufafanuzi na tafsiri ya hotuba hiyo ya bibi Fatima (a.s). Pia wengine huzitambua tafsiri hizo kuwa ni tafsiri za Hotuba ya Lumma (jina lingine la Hotuba ya Fadakiyyah). [169]
  • Tasbihat Fatima, ni uradi wa bibi Fatima (a.s) aliofunzwa na Mtume (s.a.w.w). [170] na Fatima akafurahishwa sana na zawadi ya funzo la uradi huo aliofundishwa na baba yake (s.a.w.w). [172] Kuna ripoti kadhaa zilizonukuliwa kutoka katika vitabu vya wanazuoni wa Kisunni kuhusiana na habari ya Mtume (s.a.w.w) kumfunza binti yake (bibi Fatima) (a.s) uradi huo. Imeripotiwa wa kwamba, baada ya Ali (a.s) kuusikia uradi huu, alishikamana nao na katu hakuachana nao. [172]
  • Swala za bibi Fatima Zahraa (a.s), ni maombi ambayo ya bibi Fatima (a.s) aliojifunza ima kutoka kwa Jibril au kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Sala hizo zimetajwa katika baadhi ya maandiko ya simulizi za Riwaya na vitabu vya dua.[173]
  • Mashairi yanayohusishwa na bibi Fatima (a.s) yameripotiwa katika vyanzo vya kihistoria na simulizi za Riwaya. Kihistoria, mashairi haya yanahusiana na vipindi viwili: kipindi cha kabla ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) na kipindi cha baada ya kifo chake (s.a.w.w). Kuna baadhi ya vitabu vilivyoandika maandiko kadhaa kuhusiana na mashairi hayo. [174]

Bibi Fatima (a.s) katika Tamaduni na Fasihi ya Kishia

Mashia wanamtambua bibi Fatima (a.s) kama ni mfano wao wa kuigwa. Nyenendo na mfumo wa maisha ya bibi Fatima (a.s) unaendelea kufuatwa na kuendelezwa kama ni moja kati ya tamaduni za Kishia. Miongoni mwa mifano yake ni:

  • Mahari ya Sunna: Kwa mujibu wa Hadithi, kiwango cha mahari alichokianisha Imamu Jawad (a.s) kwa ajili ya mkewe, kilikuwa ni sawa na kiwango cha mahari ya bibi Fatima (a.s), yaani, ni dirhamu mia tano. [175] Kiasi hichi cha mahari kinaitwa Mahru Al- Sunnah (Mahari ya Kisunnah). Nayo ni mahari yaendayo sawa na mahari ya wake na mabinti wa Mtume (s.a.w.w). [176]
  • Ayyamu Fatimiyyah (Siku za Fatima): Ifikapo ya mnasaba wa tarehe ya kifo cha kishahidi cha bibi Fatima, Mashia hufanya sherehe za maombolezo ya kuadhimisha siku ya kifo chake (a.s). Nchini Iran siku rasmi ya kuadhimisha kifo cha kishahidi cha bibi Fatima (a.s), ni Mwezi Tatu Jumadi Al-Thani. [177] Wanazuoni hushiriki momboleza hayo yanayo, ambayo fanyika kwa mfumo wa matembezi ya miguu [178].
  • Siku ya Wanawake: Nchini Iran, ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa bibi Fatima (a.s), ambayo ni sawa na mwezi 20 Jumadi Al-Thani. Hii ndiyo siku iliyochaguliwa kuwa ni Siku ya Wanawake nchini humo. [179] Wairani husherehekea na kuadhimisha siku hiyo kwa kuwapa zawadi mama zao pamoja na wake zao. [180]
  • Siku ya Ndoa (siku ya harusi): Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya mwezi mosi ya Dhul-Hijjah, ni siku ya kuadhimisha ndoa ya Imamu Ali na Fatima (a.s). Siku hiyo hutambuliwa nchini Iran kama ni Siku ya Harusi, hivyo ndoa nyingi nchini Iran hufanyika katika siku kama hiyo.
  • Ujenzi wa shabihisho lenye kumithiliana na mtaa au kiambo cha Bani Hashim: Katika siku zijulikanazo kama ni Siku za Fatimiyyah, Wairani hujenga kiambo chenye nyumba za mtindo wa kizamani zilizomathiliana au kufanana na kiambo cha Bani Hashim. Watu wengi hutembelea kiambo hicho na kupata hisia za kiroho zinazosababishwa na dhana itokanayo na mtindo wa zamani wa picha ya kiambo hicho. [181]
  • Kufanyika matamasha ya michezo ya kuigiza: Katika miaka ya hivi karibuni, kumedhihiri kwa kasi kubwa matamasha ya michezo ya kuigiza. Matamasha ambayo hufanyika barabarani na kumpa kila mmoja nafsi ya kufaidika nayo bila ya pingamizi. «Bibi Mwenye Umbile la Maji na Kioo» [182] na «Bibi Aliye keti Pekee» [183] ni miongoni mwa majina ya michezo hiyo maalum ichezwayo ndani ya matamasha hayo. Matamasha ambayo hufanyika katika siku za maombolezo ya kifo cha kishahidi cha bibi Fatima (a.s).
  • Upewaji wasichana Majina: Kulingana na takwimu zilizotangazwa mnamo Mwezi 15, 1392 Shamsia nchini Iran, majina ya Fatima na Zahra ni miongoni mwa majina kumi bora yanayo chukua nafasi ya mwanzo nchini humo. [184]
  • Nasaba zifungamanazo na kizazi cha bibi Fatima (a.s): Miongoni mwa madhehebu ya Shia, waumini wa dhehebu la Zaidiyyah wanaamini ya kwamba, Nafasi ya Uimamu na uongozi ni haki maalumu, na hakuna anayestahiki kukamata nafasi hiyo, ila yule tu anayetokana na nasaba ya bibi Fatima (a.s). Kwa hiyo, Wafuasi wa dhehebu la Zaidiyyah hawamfuati kiongozi yeyote yule atakaye toka katika kizazi kisichokuwa cha bibi Fatima (a.s). Na kiongozi wa haki kwao ni yule atokaye na kizazi hicho kitukufu. [185] Ukiachana na Zaidiyyah, kundi la Fatimiyyah vilevile lilikuwa na itikadi kama hiyo. Hata uongozi wao uliotawala mji wa Misri katika zama zilizopita, waliuta jina la Uongozi wa Fatimiyyah. [185]

Fasihi na Mashairi Kuhusiana na Bibi Fatima (a.s)

Baadhi ya washairi na waandishi wa Kiajemi wameandika wametunga tungo kadha za kifasihi kuhusiana na bibi Fatima (a.s). Pia waandishi hao wametunga mashairi tofauti yanayohusiana naye (a.s). Baadhi wanaamini kwamba, shairi kongwe zaidi lililomsifu bibi Fatima (a.s) lilitungwa mnamo karne ya 5 Hijiria. [187] Tungo za mashairi kuhusiana na bibi Fatima (a.s), yamechukuwa nafsi kubwa katika zam za hivi sasa. Katika zama zetu za leo, kumejitokeza makongamano kadhaa yanayo fungamana moja kwa moja na uhamasishaji wa tungo zaa mashairi kwa jina la bibi Fatima (a.s). Makongamano hayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na mabingwa wa mashairi waandishi kutoka pande tofauti. [188] Ongezeko na mfumuko wa mashairi yanayoandikwa juu ya bibi Fatima (a.s), kumesababisha baadhi ya watafiti wa fani ya fasihi kuuhesabu na kuutambua mtindo huu mpya wa kiushairi, wenye mfumo maalumu wa tungo za kiroho zenye nia ya kuisifu na kipambanua hadhi na daraja ya bibi Fatima (a.s), kuwa ni mtindo mpya wa kishairi ndani ya tamaduni na fani za mashairi. Ambapo hadhi na maisha ya bibi Fatima hujadiliwa ndani yake. [189]

Miongoni mwa kazi za fasihi zinazoweza kuashiriwa ndani ya zama zetu hizi, ni kitabu kiitwacho Kesht Pahlu Gerefteh (Meli Iliyo Egeshwa) na Fatima Fatemeh Ast (Fatima ni Fatima). Miongoni mwa mashairi mashuhuri yaliyoandikwa kuhusu hadhi na nafasi ya bibi Fatima (a.s), ni shairi maarufu la marehemu Ayatullahi Sheikh Muhammad Hussein Gharawi Esfahani, ambaye umaarufu wake ni Kompany. Yeye ni mwandishi aliye andika shairi maarufu lililoanza na kipengele kisemacho: Dokhtare fikre bikre mane... Yaani: Ewe binti wa fikra bikra za tafakuri yangu.

Rejea

Vyanzo