Nenda kwa yaliyomo

Muhajirina

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na Muhajirina. Ili kujua kuhusiana na maana ya kuhajiri au kuguura (hijra) kuelekea Madina na Uhabeshi angalia makala za Hijra kuelekea Madina na Hijra kuelelea Uhabeshi.

Muhajirina (Kiarabu: المهاجرون) ni Waislamu waliokuwa wakiishi Makka na baada ya kusilimu na kustahimili mashinikizo ya washirikina, walihajiri na kuhahamia Madina kwa amri ya Mtume (s.a.w.w). Muhajrina hao walikuwa na nafasi kubwa katika kuutangaza Uislamu kwa kuhama na kuhajiri kwao huko, na walistahimili matatizo na masaibu mengi katika njia hii; kwa msingi huo, Mtume (s.a.w.w) aliwazingatia sana na Qur’ani imewataja kwa wema.

Kabla ya Uislamu, kulikuweko na uadui na migogoro baina ya watu wa Makka na Madina, ambayo ilitoweka baada ya Bwana Mtume kugura na kuhamia Madina na kuungwa udugu baina ya Muhajirina na Ansari. Lakini baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w) ushindani kati ya Ansari na Muhajirina ulianza tena na ukaendelea mpaka katika zama za Bani Umayyah. Mfano wa hili ulikuwa ni ushindani baina ya Muhajirina na Ansari katika tukio la Saqifa, ambapo Abu Bakr bin Abi Quhafa alifanikiwa kuinia katika Ukhalifa kwa himaya na uungaji mkono wa Muhajirina.

Imam Ali (a.s) Imamu wa kwanza wa Mashia, Bibi Fatima, binti wa Mtume (s.a.w.w) Abu Salama, Ummu Salama, Hamza bin Abdul Muttalib, ami yake Mtume na makhalifa watatu, ni miongoni mwa Muhajirina mashuhuri na watajika.

Utambuzi wa Maana

Makala kuu: Hijra kulelekea Madina

Jina na anuani ya Muhajirina inajumuisha Waislamu wote waliohajiri na kuhama kwa amri ya Mtume (s.a.w.w.)[1] kutoka Makka na kwenda Madina kutokana na mateso na maudhi ya washirikina wa Makka. Aidha, Waislamu wa Madina ambao walipokea Mtume (s.a.w.w) na Waislamu wengine huko Madina [2] wanajulikana kwa jina la Ansari.[3] Kwa msingi huo, Ansari ni Waislamu wa Madina waliompokea Mtume na Muhajirina waliotokea Makka.

Jina na anuani ya Muhajirina inajumuisha Waislamu wote waliohama kutoka Makka kwenda Madina hadi kutekwa na kukombolewa Makka katika mwaka wa nane wa Hijiria. Pamoja na hayo, Waislamu ambao waliwasili na kuingia Madina kabla ya Sulhu ya Hudaybiyah (mwaka wa 6 wa Hijria) wana hadhi na nafasi ya juu zaidi.[4]

Daraja

Kwa mujibu wa Ayatullah Makarim Shirazi, Marjaa Taqlid na mfasiri wa Qur'ani ni kuwa, Mtume (s.a.w.w) aliwajali na kuwazingatia sana Muhajirina; kwa sababu waliweka maisha yao ya kimaada na mali zao kwenye huduma ya mwito na da’wa yake na kwa kuhajiri kwao wakaifikisha sauti ya Uislamu katika masikio ya walimwengu. [5]

Katika Qur'an, neno linalotokana na hijra (kuhama na kuhajiri) limetajwa mara 24 kwa anuani ya Muhajirina: (الذین هاجروا و مَن هاجر),[6] Pia, Qur'an imewataja Muhajirina pamoja na wanajihadi[7] na kuwasifu kwa sifa za subira na kutawakali [8] kwa Mwenyezi Mungu imani[9] na Waumini wa kweli[10] ambao kwa kuhajiri kwao imani yao imethibiti.[11] Qur’ani Tukufu inazungumzia kusamehewa dhambi zao[12] na kuingizwa peponi.[13] Hata hivyo kwa mujibu wa wanazuoni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kwamba, inafahamika dhahiri ya Aya kwamba, makusudio ya Mwenyezi Mungu ni wale Muhajrina[14] ambao walibakia katika ahadi yao na hawakubalika na sio Muhajrina wote. [15]

Kuwa muhujar (mtu aliyehama Makka na kwenda Madina) kulihesabiwa kuwa na heshima na hadhi kubwa katika karne za kwanza za Hijria; Omar bin al-Khattab, alikuwa akiwapa Muhajirina hisa zaidi wakati wa ugawaji wa Bait al-Mal, kutokana na kutangulia kwao katika Uislamu, [16] na aliwachagua wajumbe wa baraza la watu sita kutoka miongoni mwao ili kumchagua khalifa na mrithi wa uongozi baada ya Mtume;[17] ingawa kazi ya kuifuatilia na kusimamia aliikabidhi kwa Ansari/[18]

Muhajirina wa Mwanzo

Kabla ya Mtume (s.a.w.w) kuhamia Madina, aliwaamuru masahaba zake waanze safari ya kuelekee Madina.[19] Ali bin Hussein Mas’oudi anasema, baadhi ya watu wa kwanza kuingia Madina kabla ya Mtume (s.a.w.w) walikuwa: Abdullah bin Abdul Asad, Aamir bin Rabi'ah, Abdullah bin Jahsh, Omar bin Khattab na Ayash bin Abi Rabi'ah bin Yahya.[20] Baladhuri mwanahistoria wa karne ya tatu, anawachukulia Muhajirina wa kwanza kuwa Mus’ab bin Umayr na Ibn Umm Maktum, ambao walifika na kuingia Madina kabla ya Abdullah bin Abdul Asad.[21] Kwa mujibu wa ripoti yake, Mus’ab bin Umayr alitumwa Madina Mtume (s.a.w.w) katika mwaka wa kumi na mbili tangu kubaathiwa na kupewa Utume Mtume kwa ajili ya kwenda kuhubiri dini ya Kiislamu na kwamba, alitumwa huko baada ya Baiya ya Aqaba.[22]

Muamala wa Washirikina wa Makka dhidi ya Muhajirina

Kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, washirikina wa Makka walilikuwa wakiwazuia Waislamu kuhamia Madina kwa njia mbalimbali; waliwaweka baadhi ya watu gerezani na pia wakazuia baadhi ya familia za muhajirina kujumuika nao. Miongoni mwa matukio hayo ni kuwazuia kwa muda Ummu Salama mke wa Abu Salama (Abdullah bin Abdul Asad) na mwanawe kwenda Madina.[23] Na Sohayb Rumi aliruhusiwa kuhajiri na kwenda Madina lakini makabala wake atoe mali yake.[24]

Kadhalika, baadhi ya Waislamu hawakuhama kwa sababu wake zao na watoto wao waliwavunja moyo na walikuwa wakilia na kuwazuia kuhama. (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ ; Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu, basi tahadharini nao).[25] Fadhl bin Hasan Tabarsi, mfasiri wa Qur’ani wa Kishia katika karne ya sita ya Hijiria, alinukuu kutoka kwa Ibn Abbas na Mujahid kwamba Aya hiyo ilishuka kuhusiana na maudhui hiyo.[26]

Himaya na Uungaji Mkono wa Ansari kwa Muhajirina

Baada ya Mtume (s.a.w.w) kuhajiri na kuhamia Madina, alianzisha na kufunga udugu kati ya Muhajirina na Ansari.[27] Kwa mujibu wa maoni ya wengi, watu 45 kutoka miongoni mwa Muhajirina na na watu 45 kutoka upande wa Ansari walikuwepo katika makubaliano na mkataba huu wa udugu. [28]

Mtume alianzisha udugu baina ya Abu Bakr na Khārija bin Zayd, Omar bin al-Khattab na ʿItbān bin Mālik, Uthman bin Affan na Aws bin Thabit al-Khazraji, Abu Ubayda al-Jarrah na Sa'd bin Mu'adh, Abd al-Rahman bin 'Awf na Sa'd b. Rabī', Talha bin Ubaydulla na Kaʿb bin Malik, Zubayr bin Awam na Salamah bin Salam, Salman al-Farsi na Abu Darda’, na Ammar bin Yasir na Hudhayfa bin Najjar au Thabit bin Qays kwa mujibu wa nukuu nyingine.[29] Aidha, Mtume kwa upande wake alifunga mkataba wa udugu na Ali bin Abi twalib (a.s).[30]

Ansari walikuwa wakitoa himaya na msaada wa kimaada kwa Muhajirina walioacha mali zao huko Makka, hadi katika mwaka wa nne Hijria ambapo, Mtume (s.a.w.w) aligawanya ngawira zilizopatikana katika vita na Bani Nadhir miongoni mwa Muhajirina kwa makubaliano ya Ansari na hivyo himaya na msaada wa kimaada wa Muhajirina ukafikia tamati.[31]

Ushindani Baina ya Muhajirina na Ansari

Kwa mujibu wa Jawad Ali, mwandishi wa Al-Musafal Al-Mufassal Fi Tarikh al-Arab Qabla al-Islam kabla ya Mtume kuhama Makka na kwenda Madina, kulikuwa na uadui kati ya watu wa Yathrib (Madina) na watu wa Makka, ambao ulitoweka kwa kuhamia Mtume (s.a.w.w) katika mji wa Madina na kuanzishwa udugu baina ya Muhajir na Ansari. Hata hivyo baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), kulidhihirika uadui na mivutano baina ya Muhajirina na Ansari; kama ilivyotajwa katika mashairi ya Hassan bin Thabit, Nu’man bin Bashir na Tarmah bin Hakim. [32] Muhajirina walikuwa wakijifaharisha kwa kuwa Mtume (s.a.w.w) alikuwa mmoja wao, na Ansari walikuwa wakijifaharisha kwa kuwa wao walimpokea na kumhifadhi, na Mama wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.w) anatoka katika kabila la Bani Najjar kutoka Madina.[33]

Kwa mujibu wa JaWad Ali, kulikuwa na mgogoro kati ya Muhajirina na Ansar wakati wa zama za Muawiya bin Abi Sufyan na zama za Yazid bin Muawiya; ingawa, katika kipindi hiki, neno Muhajirina na Ansari lilitumiwa kwa uchache mno na zaidi kulitumika maneno kama vile Qureshi na Yamani.[34]

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, tukio la Saqifa ilikuwa medani na uwanja wa ushindani na mzozo kati ya Muhajirina na Ansari.[35] Wakati wa kupewa baiya na kiapo cha utii Abu Bakr, Habab bin Mundhir, ambaye alikuwa anatokana na Ansari, alichomoa upanga na kuwaelekezea Muhajirina. Aidha Omar bin al-Khattab alimhutubu Saad bin Ubadah, aliyekuwa mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kiansari na kumuita kuwa ni mnafiki.[36]

Nafasi ya Muhajrina katika Saqifa

Baada ya kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kundi la Ansari lilikusanyika katika ukumbi wa Saqifa Bani Saidah ili kumchagua Sa'd bin Ubadah kuwa khalifa. Lakini wakati Muhajirina akiwemo Abu Bakr bin Abi Qahafa, Omar bin Khattab na Abu Ubaydah Jarrah, walipoungana nao, kulizuka mabishano na migongano.[37] Abu Bakr, ambaye yeye mwenyewe alikuwa mmoja wa Muhajirina alisema kwamba Muhajirina walikuwa bora kuliko Ansari na hivyo walistahili zaidi ukhalifa.[38] Habab bin Mundhir, ambaye alitokana na Ansari, alipendekeza kuchaguliwa kwa Amir kutoka kwa Ansari na Amir kutoka kwa Muhajirina ambapo pendekezo lake lilipingwa na Omar bin Khattab. Kisha Abu Bakr akapendekeza Omar bin Al Khattab na Abu Ubaidah Jarrah, ambao walikuwa miongoni mwa Muhajirina kwa ajili ya ukhalifa. Lakini wawili hao hawakukubali, na kwa kusema mambo mazuri kuhusu Abu Bakr, walimwona kuwa anastahiki ukhalifa na wakatoa baiya kwake.[39] Kisha kabila la Bani Aslam, ambao walikuwa na mfungamano na Muhajarina liliingia Madina na kutoa baiya na kiapo cha utii kwa Abu Bakr.[40]

Muhajirina Mashuhuri

Baadhi ya watu mashuhuri waliohajiri kwa amri ya Mtume (s.a.w.w) na wakaondoka Makka na kwenda Madina ni:

  • Imamu Ali (a.s) ni Imamu wa kwanza wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia na mrithi wa Mtume (s.a.w.w). Yeye katika Laylat al-Mabit (usiku wa kuhajiri Mtumer) alilala katika tandiko la Mtume ili washirikina wadhani kwamba, Mtume bado hajaondoka Makka.[41] Aidha, alipewa jukumu na Mtume (s.a.w.w) la kukabidhi kwa wenyewe amana za watu zilizokuwa mikononi mwa Mtume na kisha baada ya siku tatu aliondoka na kuelekea Madina.[42]
  • Fatima (a.s) binti ya Mtume (s.a.w.w) ambaye alifunga ndoa na Imamu Ali (a.s) katika mwaka wa pili Hijria.[43] aliondoka Makka na kuelekea Madina akiwa pamoja na wanawake wengine kadhaa akiwemo Fatima bint Asad msafara ambao uliongozwa na Imamu Ali (a.s). Tukio hilo lilijiri siku tatu baada ya Mtume kuondoka Makka na kuhamia Madina.[44]
  • Ummu Salama, mke wa Abdallah bin Abdul-Asad ambaye watu wa kabila lake kwa muda fulani walimzuia kuhajiri pamoja na mumewe kuelekea Madina. Baada ya kuuawa shahidi Abu Salama aliolewa na Mtume (s.a.w.w). [45]
  • Abu Bakr bin Abi Quhafa alikuwa pamoja na Mtume (s.a.w.w) wakati wa kuhajiri kuelekea Madina na alijificha pamoja na Mtume katika pango la Thaur. [46] Baada ya kuaga dunia Mtume, Abu Bakr alichaguliwa kuwa Khalifa na kwa mtazamo na itikadi ya Waislamu wa Madhehebu ya Suni, Abu Bakr ndiye Khalifa wa Kwanza wa Waislamu. Hata hivyo Waislamu wa Madhehebu ya Shia hawamtambui Abu Bakr kama Khalifa wa Kwanza wa Weaislamu bali wanaamini kwamba, Mtume (s.a.w.w) kabla ya kuaga dunia alimuainisha na kumtangaza mrithi wake ambaye ni Imamu Ali (a.s).[47]

Omar bin al-Khattab (Khalifa wa Pili),[48] Othman bin Affan (Khalfa wa Tatu), Hamza bin Abdul-Muttalib ami yake Mtume, Othman bin Madh’un, Abu Hudhayfa, Miqdad bin Amru, Abu Dhar al-Ghiffari na Abdallah bin Mas’oud ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao ni Muhajirina. Kadhalika Zaynab binti ya Mtume (s.a.w.w), Ummu Kulthum binti ya Mtume (s.a.w.w), Ruqayyah binti ya Mtume (s.a.w.w), Fatima bint Asad, Ummu Aiman, Zaynab bint Jahsh na Sauda bint Zam’ah bin Qays ni miongoni mwa wanawake wengine ambao ni Muhajirina (waliohama Makka na kwenda Madina).

Masuala Yanayo Fungamana

Rejea

  1. Maqrizi, Imta al-Asma, juz. 9, uk. 75, 1420 H. Baladhuri, Ansab al-Ashraf, juz. 1, uk. 257, 1959 M.
  2. Maqrizi, Imta al-Asma, juz. 9, uk. 169, 1420 H.
  3. Maqrizi, Imta al-Asma, juz. 9, uk. 82, 1420 H.
  4. Makarim shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 8. uk. 261-262, 1374 S.
  5. Makarim shirazi, al-Amthal, juz. 8. uk. 194, 1421 H.
  6. Ja'fari, Tafsir Kauthar, juz. 2, uk. 536, 1376 S.
  7. Tazama: Surat Al-Anfal, Ayat 72-75, Surat Al-Baqarah, Ayat 218.
  8. Surat An-Nahl, Ayat 42.
  9. Makarim shirazi, al-Amthal, juz. 8. uk. 95, 1421 H.
  10. Surat Al-Anfal, Ayat 74.
  11. Tabrasi, Majma' al-Bayan, juz. 4, uk. 499, 1372 S.
  12. Surat Al-Baqarah, Ayat 218; Surat Al-Anfal, Ayat 74.
  13. Surat Ali Imran, Ayat 195.
  14. Tazama: Allamah Tabatabai, al-Mizan, juz. 9. uk. 374, 1417 H, Subhani, Ilahiyat, juz. 4, uk. 445, 1412 H.
  15. Tazama: Sheikh Tusi, al-Tibyan, juz. 9. uk. 329.
  16. Ibnu Sa'ad, al-Tabaqat al-Kubra, juz. 3. uk. 214, 1410 H.
  17. Tazama: Ya'qubi, Tarikh Ya'qubi, juz.2. uk.160,
  18. Ya'qubi, Tarikh Ya'qubi, juz.2. uk. 160.
  19. Tabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 2. uk. 369, 1387 H.
  20. Mas'udi, al-Tanbih wa al-Ishraf, uk. 200.
  21. Baladhuri, Ansab al-Ashraf, juz. 1. uk. 257, 1959 M.
  22. Baladhuri, Ansab al-Ashraf, juz. 1. uk. 257, 1959 M.
  23. Baladhuri, Ansab al-Ashraf, juz. 1, uk. 258-259, 1959 M; Ibnu Hisham, al-Sirah al-Nabawiyah, juz. 1, uk. 469.
  24. Ibnu Athir, Usad al-ghabah, juz. 2, uk. 419, 1409 H.
  25. Surat. Al-Taghabun, Ayat 14.
  26. Tabrasi, Majma' al-Bayan, juz. 10, uk. 451, 1372 S.
  27. Tazama: Amili, al-Sahih Min Sirat al-Nabi al-A'zam, juz. 5, uk. 99, 1426 H.
  28. Tazama: Amili, al-Sahih Min Sirat al-Nabi al-A'zam, juz. 5, uk. 101, 1426 H; Maqrizi, Imta al-Asma, juz. 1, uk. 69, 1420 H.
  29. Diyar Bakri, Tarikh al-Khamis, juz. 1, uk. 353.
  30. Tazama: Amili, al-Sahih Min Sirat al-Nabi al-A'zam, juz. 5, uk. 103, 1426 H.
  31. Maqrizi, Imta al-Asma, juz. 1, uk. 191-192, 1420 H.
  32. Ali, Al-Mufassal Fi Tarikh al-Arab Qabla al-Islam, juz. 2, uk. 134, 1422 H.
  33. Ali, Al-Mufassal Fi Tarikh al-Arab Qabla al-Islam, juz. 2, uk. 136, 1422 H.
  34. Ali, Al-Mufassal Fi Tarikh al-Arab Qabla al-Islam, juz. 2, uk. 134-136, 1422 H.
  35. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 3, uk. 220-221, 1387 H.
  36. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 3, uk. 220-221, 1387 H.
  37. Ibnu Athir, al-Kamil, juz. 2, uk. 325, 1385 H.
  38. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 3, uk. 219-220, 1387 H.
  39. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 3, uk. 220-221, 1387 H.
  40. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 3, uk. 205 1387 H.
  41. Mas'udi, al-Tanbih wa al-Ishraf, uk. 200.
  42. Mas'udi, al-Tanbih wa al-Ishraf, uk. 200.
  43. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 2, uk. 410, 1387 H.
  44. Ibnu Shahr Ashub, Manaqib, juz. 1, uk. 183, 1379.
  45. Ibnu Hisham, al-Sirah al-Nabawiyah, juz. 1, uk. 469.
  46. Thabari, Tarikh al-Umam wa al-Muluk, juz. 2, uk. 273-274, 1387 H.
  47. Tazama: Mudhaffar, al-Saqifah, uk. 60-65, 1415 H.
  48. Mas'udi, al-Tanbih wa al-Ishraf, uk. 200.

Vyanzo

  • Al-Qur’an Al-Karim
  • Ibnu Athir, Ali bin Muhammad. Usd al-ghabah fi Ma'rifah al-Sahabah. Beirut: Dar al-Fikr, 1989 M/1409 H.
  • Ibnu Athir, Ali bin Muhammad. Al-Kamil fi al-Tarikh. Beirut: Dar Sadir, 1965 M/1385 H.
  • Ibnu Sa'd. Muhammad bin Sa'd. Al-Tabaqat al-Kubra. Tahqiq: Muhammad Abdul Qadir Ata. Beirut: Dar al-Kutub al-Ilmiyah, 1990 M/1410 H.
  • Ibnu Shahr Ashub, Muhammad bin Ali. Manaqib Al Abi Talib. Qom: Allamah, 1379 H.
  • Ibnu Hisham, Abdul Malik bin Hisham. Al-Sirah al-Nabawiyah. Tahqiq: Mustafa al-Saqa va Ibrahim al-Abyari va Abdul Hafidh Shibli. Beirut: Dar al-Ma'rifah, Bita.
  • Baladhuri, Ahmad bin Yahya. Ansab al-Ashraf. Tahqiq: Muhammad Hamidullah. Misr: Dar al-Ma'arif. 1959 M.
  • Ja'fari, Yaqub. Tafsir Kauthar. Qom: Muassasah Intesharat Hijrat, 1376 S.
  • Diyar Bakri, Hussein bin Muhammad. Tarikh al-Khamis fi Ahwali Anfusi al-Nafis. Beirut: Dar Sadir, Bita.
  • Subhani, Ja'far. Ilahiyat ala Huda al-Kitab wa al-Sunnah wa al-A'ql. Qom: al-Markaz al-Alami li al-Dirasati al-Islamiyah. 1412 H.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan. Al-Tibyan fi Tafsir Al-Qur'an. Tahqiq: Ahmad Qasir Amili. Muqadame Agha Buzurg Tehrani. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi,Bita.
  • Tabatabai, Sayid Muhammad Hussein. Al-Mizan fi Tafsir Al-Qur'an. Qom: Daftar Intesharat Islami vabaste ba Jami’ah Mudarrisin Hauzah Ilmiyah Qom, 1417 H.
  • Tabarsi, Fadhl bin Hassan. Majma' al-Bayan fi Tafsir Al-Qur'an. Muqadame: Muhammad Jawad Balaghi. Teheran: Nasir Khosro, 1372 S.
  • Tabari, Muhammad bin Jarir. Tarikh al-Umam wa al-Muluk. Tahqiq: Muhammad Abu al-Fadhl Ibrahim. Beirut: Dar al-Turath, 1967 M / 1387 H.
  • Amili, Jafar Murtadha. Al-Sahih Min Sirah al-Nabi al-A'dham. Muassasah Ilmi Farhanggi Dar al-Hadith, 1426 H/1385 S.
  • Ali, Jawad. Al-Mufassal Fi Tarikh al-Arab Qabla al-Islam. Dar al-Saqi. 2001 M/1422 H.
  • Mas'udi, Ali bin Hussein. Al-Tanbih wa al-Ishraf. Tas-hih: Abdullah Ismail al-Sawi. Kairo: Dar al-Sawi. Bita. (Qom: Muassasah Nashr al-Manabi' al-Thaqah al-Islamiyah)
  • Mudhaffar, Muhammad Ridha. Al-Saqifah. Tahqiq: Mahmud Mudhaffar. Qom: Muassasah intesharat Ansariyan, 1415 H.
  • Maqdisi, Matahar bin Tahir. Al-Bad'u wa al-Tarikh. Bur Said. Maktabah al-Thaqafah al-Diniyah, Bita.
  • Maqrizi, Ahmad bin Ali. Imta' al-Asma' bima li al-Nabi min al-Ahwal wa al-Amwal wa al-Hafadah wa al-Mata. Tahqiq: Muhammad Abdul Hamid al-Nasimi. Beirut: Dar al-Kutub al-Ilmiyah. 1999 M/1420 H.
  • Makarim shirazi, Nasir. Al-Amthal fi Tafsir Kitabillah al-Manzil. Qom: Madrasah Imam Ali bin Abi Talib, 1421 H.
  • Makarim shirazi, Nasir. Tafsir Nemuneh. Tehran: Dar al-Kutub al-Ilmiyah, 1374 S.
  • Ya'qubi, Ahmad bin Abi Ya’qub. Tarikh Ya'qubi. Beirut, dar Sadir, Bita.