Maombolezo

Kutoka wikishia

Makala hii inahusiana na maombolezo. Ili kujua kuhusiana na maombolezo ya Imamu Hussein (a.s) angalia maombolezo ya Muharram.

Maombolezo ni ada ambayo hufanyika wakati wa kifo cha mtu. Maombolezo yana historia kongwe na tangu nyakati za kale, na hufanyika kwa ajili ya kumbukumbu ya jamaa au shakhsia wa kidini.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, historia ya maombolezo katika Uislamu inarudi nyuma hadi zama za Mtume (s.a.w.w). Tangu wakati huo hadi sasa kumekuwa kukifanyika maombolezo kwa njia tofauti katika nchi za Kiislamu; miongoni mwao, kwa sura ya kurehemu, shughuli ya kurehemu ya siku tatu na arubaini ya marehemu.

Mafakihi wa Kishia wanaona kuwa, inajuzu kuomboleza na kulia na kusoma nauha na mashairi kwa ajili ya maiti; lakini kwa mujibu wa fat’wa ya mafaqihi wa Kisuni, watu wanaweza kulia tu kimyakimya na bila ya kutoa sauti wanapoomboleza kifo cha wapendwa wao. Baadhi yao wanasema kuwa, haijuzu kulia kwa sauti na kupiga kelele kwa ajili ya maiti.

Maombolezo mengi ya Shia ni ya kidini; yaani hufanyika kwa minajili ya kuwakumbuka viongozi wa kidini, akiwemo Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) na hasa Imam Hussein (a.s). Baadhi ya wanachuoni wa Kisuni wanaona aina hii ya maombolezo kuwa ni bidaa (uzushi) na haramu. Lakini tangu zamani hadi sasa, baadhi ya Masuni hushiriki katika maombolezo yanayofanywa na Mashia.

Maombolezo, kuwakumbuka waliofariki dunia

Maombolezo ni shughuli inayofanywa kwa ajili ya kuomboleza kifo cha mtu fulani. [1] Maombolezo hufanywa kutokana na kufiwa na wapendwa wao au wazee wa kidini. [2]

Historia ya maombolezo

Shughuli za maombolezo zilikuweko tangu kale katika tamaduni mbalimbali. Inaelezwa kuwa, nchini Iran kabla ya Uzartoshti lilikuwa ni jambo lilionea. Na kuna mifano ya wazi ya hilo katika Shahnameh. [3] Katika kitabu cha Bibilia kumesimuliwa habari za maombolezo ya Bani Israil kwa ajili ya ndugu na jamaa zao walioaga dunia. [4]

Katika Uislamu kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, historia ya maombolezo inarejea nyuma katika zama za Mtume (s.a.w.w). Kwa mfano Ibn Kathir, mwandishi wa historia wa karne ya 8 Hijiria ameandika, baada ya vita vya Uhud, wanawake wa Madina walifanya maombolezo kwa ajili ya watu waliouawa. Baada ya Mtume kuona hilo akasema, Hamza hana wa kumlilia na kumuomboleza. Baada ya hapo, wanawake hao wakafanya maombolezo pia kwa ajili ya Hamza ibn Abdul-Muttalib. [5]


Maombolezo katika tamaduni mbalimbali

Hafla za maombolezo ya marehemu zinafanyika kwa namna tofauti katika tamaduni mbalimbali: Nchini Iran, hafla kama kikao cha kurehemu, khitma ya siku ya tatu na ya Arubaini. [6] Katika baadhi ya nchi, kama vile Tajikistan, hafla za maombolezo hufanyika siku ya 20 na Siku ya 40 tangu marehemu aaga dunia kama ambavyo hufanyika pia hauli (baada ya mwaka) yake. [7] Waislamu wa India hufanya hafla na shughuli ya maombolezo katika siku ya tatu kwenye kaburi la marehemu. [8] Katika nchi zingine kama vile Misri, Azerbajani na Iraq, pia wana desturi na ada maalumu za kuomboleza. [9]

Hukumu ya kisheria ya maombolezo kwa ajili ya marehemu

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi wa Kishia, inajuzu kulia na kuomboleza kwa ajili ya maiti. [10] Sahib al-Jawahir (aliyefariki 1266 Hijiria) ameandika: Kuna hadithi nyingi zinazothibitisha kwamba, kulia na kuomboleza kwa ajili ya wafu kunajuzu; miongoni mwazo ni riwaya zinazosimulia juu ya kilio cha Mtume (s.a.w.w) katika maombolezo ya ami yake Hamza na mwanawe Ibrahim, na pia riwaya za maombolezo ya Bibi Fatima (a.s) wakati wa kifo cha Mtume (s.a.w.w). [11] Haijuzu kulalamika na kutokuwa na subira katika misiba kwa wasio Maasumu kwa kujipiga vichwa na nyuso, kupiga kelele, na mambo mengine kama hayo, lakini inajuzu kufanya hivyo kuhusiana na maombolezo ya msiba wa Abu Abdullah (Imam Hussein) na Ahlu-Bayt wengine (as) na kwa mujibu wa baadhi ya mafakihi kufanya hivyo kunahesabiwa kuwa ni ibada. [12]

Mtazamo wa Ahlu-Sunna

Kwa mujibu wa Abdul Rahman Jaziri, fakihi wa Kimisri ni kwamba, kwa mujibu wa Fiqhi ya Sunni, hairuhusiwi kusoma maombolezo kwa ajili ya wafu; lakini hakuna tatizo kuwalilia kimya kimya na bila ya kutoa sauti. Kuhusu kulia kwa sauti kubwa, kuna tofauti za kimitazamo baina ya madhehebu za kifikihi za Kisuni: Maliki na Hanafi wanaona kuwa ni haramu; lakini inaruhusiwa kwa mujibu wa madhehebu ya Shafi'i na Hambali. [13]

Maombolezo ya kidini

Kadhalika angalia: Maombolezo ya Muharram

Baadhi ya maombolezo yana upande wa kidini. Mashia wanatilia maanani sana aina hii ya maombolezo na wanafanya hafla za maombolezo kwa ajili ya viongozi na shakhsia wakubwa wa kidini, wakiwemo Mtume (s.a.w.w), Bibi Fatma Zahra (a.s) na Maimamu (a.s), hususan katika mwezi wa Muharram kwa ajili ya Imamu Hussein (a.s). [14]

Maombolezo ya kidini ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia hufanyika kwa sura tofauti tofauti kama vile kusoma simulizi za msiba [15], kulia, kusoma kaswida za maombolezo, kujipiga kifua, [16] na kujipiga kwa minyororo. [17 [18]

Wanachuoni wa Kishia wameandika vitabu na risala nyingi katika kutetea maombolezo na kueleza uhalali wake, ambapo kitabu cha Iqnau al-Laim Ala Iqamati al-Maatim kilichoandikwa na Sayyid Muhsin Amin ni mfano mmoja tu. [19]

Wanazuoni wa Kisuni, hususan wa Kihambali, wanaona wanaamini kuwa, kufanya maombolezo ni bidaa, uzushi na ni haramu; [20] hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti za kihistoria, nchini Iran, baadhi ya Masuni hususan wa Kishafi'i, na hata wanazuoni wa Kisuni, wakiwemo baadhi ya Maulamaa wa Kihanafi na Kishafi'i, walishiriki katika hafla za maombolezo ya Mashia. [21]

Vyanzo

  • Anuri, Hasan & Tim, Farhangge Buzurg-e Sukhan, Teheran: Entesharat-e Elmi, 1390 HS/2011.
  • Bahrami, Askar, Tarhīm, Majles, Markaz-e Dayerah al-Ma'aref Buzurg-e Eslami, 1387 HS/2008.
  • Baqi, Imaduddin. Azadari. Site cgie.org.ir. Diakses tanggal 26 Juni 2022.
  • Farhanggi, Susan wa Afsane-e Munfared, Dar Danesh-e Jahan-e Eslam, Teheran: Bunyad-e Dayerah al-ma'aref Eslami, 1382 HS/2003.
  • Ibn Kathir, Ismail bn Umar, Al-Bidāyah wa an-Nihāyah, Dar Ihya' at-Turath al-'Arabi, 1408 H.
  • Jaziri, Abdurrahman bin Muhammad Iwadh, Al-Fiqh 'alā al-Madzāhib al-Arba'ah, Beirut: Dar al-Kutub al-'Ilmiyyah, 1424 H.
  • Mazaheri, Muhsen Husam, Azadari Dar Farhangg-e Sug-e Shi'i, Teheran: 1395 HS/2016.
  • Najafi, Muhamad Hassan, Jawāhir al-Kalām fī Sharh Sharā'i' al-Islām, Beirut: Dar Ihya' at-Turath al-'Arabi, 1404 H.
  • Tabataba'i Yazdi, Muhammad Kazem, Al-'Urwah al-Wutsqā. Qom: Muassese-e Entesyarat-e Eslami, 1419 H.