Amina bint Wahb
Amina bint Wahb (Kiarabu: آمنة بنت وهب) (alifariki miaka 46 kabla ya Hijiria mwafaka na mwaka 576 Miladia). Yeye ni mama wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na mke wa Abdullah ibn Abd al-Mutalib. Mwaka wa 7 baada ya mwaka wa tembo, Bibi Amina alimchukua mwanawe yaani Muhammad kwa ajili ya kumpelekea kuzuru kaburi la baba yake (Abdullah) na vilevile kwa ajili ya kwenda kuonana na wajomba wa Abdullah katika mji wa Madina ambao walikuwa wanatokana na kabila la Bani Najjar. Wakati wa kurejea kutoka katika safari hiyo, alifariki njiani katika kijiji kinachojulikana kwa jina la «Abu'a» jirani na mji wa Madina na kuzikwa hapo.
Wasomi na wanazuoni wa madhehebu ya Kishia wameafikiana juu ya imani ya Amina na babu zake Mtume (s.a.w.w) na wanatumia nyaraka za historia kuwathibitishia imani yake wale wanaokana kwamba, hakuwa na imani sahihi ambapo kwa mujibu wao, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akilizuru kaburi la mama yake huko Abwa. Kitabu cha «Ummu al-Nabbi (a.s)» kilichoandikwa kwa lugha ya Kiarabu na Bint al-Shati kinaelezea historia na maisha ya Mtukufu Amina. Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha ya Kifarsi kwa anuani ya Amineh Madar Payambar yaani «Amina mama wa Mtume».
Maisha yake
Amina bint Wahb anatoka miongoni mwa wanawake wa kabila la Qureish: Baba yake ni Wahb ambaye alikuwa mkubwa wa kabila la Bani Zuhra. Mama yake ni Barrah bint Abd al-Uzza ambaye naye alikuwa Mkureishi [1]. Hakuna taarifa za kutosha kuhusiana na maisha ya Amina bint Wahb kabla ya kuolewa na Abdalluh. Hata hivyo imeelezwa kuwa alizaliwa katika mji wa Makka. [2] Alifunga ndoa na kuolewa na Abdullah ibn Abd al-Mutalib mwaka 54 au 53 kabla ya Hijria. [3] Hafla ya harusi ya wawili hawa iliendelea kwa muda wa usiku tatu na katika kipindi hiki kwa mujibu wa ada za wakati huo, Abdullah alikaa nyumbani kwa bibi harusi.[4]
Kuaga Dunia Mume
Siku chache baada ya Abdullah kufunga ndoa na Amina, alikwenda safari ya kibiashara. Wakati anarejea katika safari hiyo aliugua na kuaga dunia huko Yathrib. [5] Abdullah alimuoa Amina bint Wahb mwaka mmoja tu baada ya tukio la kuchinja. [6] Abd al-Mutalib alikuwa ameweka nadhiri kwamba, kama Mwenyezi Mungu atamruzuku watoto kumi wa kiume basi mtoto wa kumi atamtoa mhanga. Hata hivyo hatimaye badala ya kumchinja Abdullah alichinja ngamia 100. [7] Baadhi ya nyaraka za kihistoria zinasema kuwa, Abdullah aliaga dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa Mtume (s.a.w.w). [8]
Kuzaliwa Muhammad (s.a.w.w)
Baada ya Amina kujifungua Muhammad alimkabidhi kwa Halima Saadia. [9] Kwa mujibu wa nadharia mashuhuri ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alizaliwa 17 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal mwaka wa tembo. Hata hivyo lililo mashuhuri baina ya wanazuoni wa Kisuni ni kwamba, Mtume alizaliwa 12 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal mwaka huo huo wa tembo. [10]
Ibn Hisham (aliyefariki 213 au 218 Hijria) ameandika katika kitabu chake cha Sirat al-Nabawiyah: Kwa kuwa Muhammad alikuwa yatima hakuna mtu aliyekuwa tayari kukubali kumpokea na kusimamia malezi yake. Ni kutokana na sababu hiyo hiyo ndio maana awali Halima Saadia alikataa kumpokea Muhammad kwa ajili ya kumlea. Hata hivyo alipoona kwamba, amekosa mtoto mwingine wa kumlea alikubali kumchukua Muhammad. [11] Baada ya kumlea kwa miaka miwili, Halima Saadia alimpeleka Muhammad kwa mama yake yaani Amina bint Wahb. Hata hivyo kutokana na kuona kuwa, Muhammad ni chimbuko la Baraka na kheri nyingi, alimuomba Amina amruhusu abakie na Muhammad kwa muda tena. [12] Kwa msingi huo alikuja kumrejesha Muhammad kwa mama yake baada ya kupita miaka 5 na siku mbili tangu kuzaliwa Muhammad ikiwa ni mwaka wa sita baada ya mwaka wa tembo. [13]
Kufariki Dunia
Mwaka wa 7 baada ya mwaka wa tembo, Amina alimchukua mwanawe yaani Muhammad kwa ajili ya kumpelekea kuzuru kaburi la baba yake Abdullah na vilevile kwa ajili ya kwenda kuonana na wajomba wa Abdullah katika mji wa Madina ambao walikuwa wanatokana na kabila la Bani Najjar. Wakati wa kurejea kutoka katika safari hiyo, aliaga dunia njiani katika kijiji kinachojulikana kwa jina la Al-Abwa jirani na mji wa Madina [14] na kuzikwa hapo. [15] Kwa mujibu wa nukuu nyingine ni kuwa, aliaga dunia katika mji wa Makka na kuzikwa katika makaburi ya Mu'alla au Jannat al-Mu'alla.[16] Yaaqubi mwandishi wa historia wa karne ya 3 Hijiria anasema kuwa, Amina aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 30. [17]
Muhammad bin Omar Waqidi (aliaga dunia 207 au 209 Hijiria) Wakati Qureshi walipoazimia kwenda Madina kwa ajili ya kutaka kulipiza kisasi cha damu ya waliouawa katika vita vya Badr, walipofika Abu'a na kuona kaburi la Amina bint Wahb kundi miongoni mwao lilifikia uamuzi wa kufukua kaburi hilo. Hata hivyo baada ya mashauriano na Abu Sufiyan na watu wenye nadharia na mitazamo miongoni mwa Qureshi, waliachana na uamuzi wao huo. [18] Imenukuliwa pia kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akizuru kaburi la mama yake huko Abu'a. [19] miongoni mwa nukuu hizo ni kwamba, katika tukio la Hudaibiya, Mtume alikwenda katika kaburi la mama yake na akiwa hapo akamlilia sana. [20]
Vyovyote itakavyokuwa, kuna kaburi katika mji wa Makka katika makaburi ya Hajun au Mu'alla ambalo linanasibishwa na Amina bint Wahb. [21] inasemekana kuwa, kaburi lake huko Abu'a na kaburi linalonasibishwa naye huko Makka kuanzia katika zama za utawala wa Othmania yalikuwa yamejengewa kisha baadaye yakabomolewa. [22]
Imani
Muhammad Ibrahim Ayati mwandishi wa historia wa zama hizi anaamini kuwa, wasomi na wanazuoni wote wa Kishia wana mtazamo mmoja kuhusiana na imani sahihi ya Bibi Amina bint Wahb, Abu Twalib, Abdullah ibn Abd al-Muttalib na babu za Mtume wa Allah mpaka kwa Nabii Adam (a.s). [23] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi na riwaya iliyokuja katika kitabu cha al-Kafi ni kuwa: Moto wa Jahanamu umeharamishwa kwa babu za Mtume, baba na mama yake na mtu aliyekuwa msimamizi na muangalizi wake (Abu Twalib). [24]
Baadhi ya wasomi na Maulamaa wa Kisuni wanaamini kuwa, wazazi na babu zake Mtume (s.a.w.w) walikuwa washirikina: Jalal a-Din Suyuti, mfasiri wa Qur'ani wa Kisuni wa karne ya 9 Hijiria, akitumia hadithi mbili kama nyaraka kuhusiana na sababu ya kushuka Aya za 113 na 114 katika Surat Tawba ametoa hukumu ya kuwa mshirikina (kumshirikisha Mwenyezi Mungu) mama wa Mtume wa Allah. [25]
Allama Amini, mwanazuoni wa Kishia, ananuukuu kutoka kwa Imamu Ali (a.s) sababu ya kushuka Aya zilizotajwa na kusema kuwa, zinahusiana na masahaba ambao walikuwa wakiwaombea maghufira baba na mama zao, na kwa uoni wake Aya hii haina uhusiano wowote na kuomba maghufira kwa ajili ya Abu Twalib au Amina. [26] Kadhalika kwa mujibu wa Allama Amini ni kuwa, baadhi ya wafasiri akiwemo Tabari [27] wamefasiri kuomba maghufira katika Aya hizi kwa maana ya kuswali. [28] Allama Amini amezungumzia pia uwezekano wa kuwa bandia hadithi hii au kutokuwa ya kuaminika. [29]
Sheikh Abbas Qommi akitegenmea Aya ya 84 ya Surat Tawba ambapo Mtume anakataza kusimama katika makaburi na kuwaswalia washirikina anaona ni jambo lisilowezekana kwa wazazi wa Mtume kuwa washirikina, kwani Mtume alikuwa akilizuru na kulitembelea kaburi la baba na mama yake. [30]
Rejea
Vyanzo