Nenda kwa yaliyomo

Suratu al-Kawthar

Kutoka wikishia

Surat al-Kawthar ni sura ya 108 na ni miongoni mwa sura za Qur’ani zilizoshuka Makka. Sura hii iko katika Juzuu ya 30. Hii ndio sura ndogo zaidi ya Qur’ani ikiwa na Aya tatu tu. Imeitwa Kawthar (kheri nyingi) kutokana na kuzungumzia kwake neema na kheri nyingi kwa ajili ya Mtume (saww) katika Aya ya kwanza na Mtume ametakiwa asali na kuchinja mkabala wa neema na kheri hizi nyingi alizopatiwa na Mwenyezi Mungu.

Hodhi ya Kawthar, mto wa peponi, kheri nyingi, Uislamu, Utume, Qur’ani, masahaba wengi, uombezi na wingi wa dhuria ni miongoni mwa misdaqi na mifano ya kheri nyingi ambayo imeelezwa. Akthari ya Maulamaa wa Kishia wanaamini kuwa, Bibi Fatma Zahra (as) na watoto wake ni moja ya misdaqi na mifano ya wazi ya kheri nyingi; kwani sura hii ilishuka kutoa majibu kwa watu ambao walikuwa wakimsema Mtume (saww) kwamba, amekatikiwa na kizazi na hana dhuria. Kuhusiana na fadhila za kusoma Sura hii inaelezwa kuwa, someni sura hii katika Swala zenu za kila siku, kwani siku ya Kiyama mtakunywa katika hodhi ya Kawthar na mtakuwa ni watu watakaokaa pamoja na Mtume (saww) katika mti wa Tuba (moja ya miti iliyoko peponi).

Utambulisho

Kutaja

Sura hii imeitwa Kawthar kutokana nna kuwa katika Aya yake ya kwanza inazungumzia moja ya neema na kheri nyingi zinazojulikana kwa jina la Kawthar ambazo Mwenyezi Mungu (swt) amempatia Bwana Mtume (saww).

Mpangilio na Mahali Iliposhuka

Sura ya Kawthar ni miongoni mwa sura za Qur’ani tukufu zilizoshuka Makka na katika mpangilio ni sura ya 15 ambayo ilishuka kwa Bwana Mtume (saww). Katika mpangilio wa sasa wa msahafu sura hii ni ya 108 na ipo katika Juzuu ya 30 katika Qur’ani.

Idadi ya Aya na Maneno Yake

Surat al-Kawthar ina Aya tatu, maneno 10 na herufi 43. Hii ndio sura ndogo na fupi zaidi katika Qur’ani.

Muhtawa (kinachozungumziwa)

Surat al-Kawthar kama zilivyo sura nyingine kama al-Dhuhaa na al-Sharh (al-Inshrah) katika Aya zake zote zinamhutubu Bwana Mtume (saww) , inaashiria neema inayojulikana kwa jina la Kawthar ambayo Mwenyezi Mungu amempatia Mtume wake. Wafasiri wa Qur’ani Tukufu wamefasiri Kawthar kwa maana ya kheri nyingi , kheri ambazo mkabala wake Bwana Mtume ametakiwa asali na achinje.

Makusudio ya Kawthar

Wafasiri wa Qur’ani Tukufu wametofautiana kuhusiana na makusudio hasa ya Kawthar katika sura hii. Hodhi ya Kawthar, mto wa peponi, kheri nyingi, Uislamu, Utume, Qur’ani, masahaba wengi, uombezi na wingi wa dhuria ya Mtume ni miongoni mwa misdaqi na mifano ya kheri nyingi ambayo imeelezwa na wasomi.

Katika tafsiri ya Nemooneh ya Ayatullah Makarem Shirazi imeelezwa kuwa, moja ya mifano ya Kawthar (kheri nyingi) ni Bibi Fatma Zahra (as); kwani sura hii ilishuka kutoa majibu kwa watu ambao walikuwa wakimsema Mtume (saww) kwamba, amekatikiwa na kizazi na hana dhuria, hii ni katika hali ambayo, kizazi cha Mtume kiliendelea kupitia kwa binti yake yaani Fatma (as) na kizazi hicho hicho kikawa na Uimamu. Abdallah Jawad Amoli (1312 Hijria Shamsia), mfasiri wa Qur’ani Tukufu anasema: Muendelezo wa sura hii unathibitisha kwamba, Kawthar na kuweko kheri nyingi kunahusiana na kadhia ya Bibi Fatma Zahra( as) ambapo Allah alimpatia mwanamke huyu mtukufu ambapo kupitia kwake wamezaliwa Maimamu 11 ambao ni fakhari ya dunia ambapo mashariki na magharibi ya ulimwengu majina matukufu ya Maimamu 11 (as) na watoto wao yanaiongoza dunia.

Sababu ya Kushuka Kwake

Surat al-Kawthar ilishuka kujibu maneno ya Aas bin Wail kuhusiana na Mtume (saww). Kutokana na mtoto wa Mtume yaani Abdallah kuaga dunia na Mtume akawa hana mtoto wa kiume, Aas bin Wail akamuita Mtume kwa jina la Abtar (mtu asiye na kizazi au aliyekatikiwa na kizazi) na alilifanya hilo mbele ya mkusanyiko wa shakhsia wakubwa wa Kikureshi. Kwa kuteremsha sura hii, Mwenyezi Mungu akawa amemliwaza Bwana Mtume (saww) ya kwamba, amempatia neema na kheri nyingi. Kisha akambashiria kwamba, maadui zake ndio watakaokatikiwa na kizazi.

Neno Nahar (نحر)

Wafasiri wa Qur’ani Tukufu wana mitazamo tofauti kuhusiana na neno Nahar (kuchinja). Wafasiri kama Fadhl bin Hassan Tabarsi (aliyeaga dunia 548 Hijria) na Allama Tabatabai (aliyeaga dunia 1360 Hijria Shamsia) wakitegemea hadithi zizolipokewa na Waislamu wa Madhehebu ya Shia na Suni wamefasiri kwamba, lina maana ya kunyanyua mikono na kuileta mkabala na uso wakati wa kupiga takbira.

Lakini Ayatullah Makarem Shirazi (aliyezaliwa 1305 Hijria Shamsia) anaamini kuwa, kulifasiri neno hilo kwa maana ya kuchinja ni bora zaidi, kwani makusudio ni kupinga amali za waabudu masanamu ambao walikuwa wakifanya ibada na kumchinjia asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kusoma Surat al-Kawthar Katika Swala za Mustahabu

Imeusiwa kusoma Surat al-Kawthar katika baadhi ya Swala za mustahabu; kama vile:

  • Swala ya usiku wa tarehe 11 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani: Swala hii ina rakaa mbili; katika kila rakaa, baada ya Surat al-Fatiha inasomwa Surat al-Kawthar mara 20.
  • Swala ya usiku wa tarehe 18 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani: Swala hii ina rakaa nne ambapo katika kila rakaa baada ya Surat al-Fatiha inasomwa Surat al-Kawthar mara 25.

Fadhila na Sifa Maalumu ya Sura Hii

Abu Baswir amenukuu kutoka kwa Imam Ja’afar Swadiq (as) ya kwamba: Mtu anayesoma Surat al-Kawthar katika Swala zake za kila siku, Siku ya Kiyama atakunywa katika hodhi ya Kawthar na atakuwa katika watu watakaokaa pamoja na Mtume (saww) katika mti wa Tuba (moja ya miti iliyoko peponi). Imekuja katika Maj’maa al-Bayan ambayo ni nukuu kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ya kwamba amesema: Mtu anayesoma Surat al-Kawthar, Mwenyezi Mungu atamshibisha na mito ya peponi na kumpa malipo kwa idadi ya wanyama wanaochinjwa na waja wa Allah katika Sikukuu ya Eidul Adh’ha na vilevile idadi ya wanyama wanaochinjwa na Ahlul Kitab na Mushirikina.

Vyanzo

  • Khamegar, Muhammad Sakhtar Surehaye Qur'an Karim, Muandaaji: Taasisi ya Utamaduni wa Qur'an na Itra ya Nur-al-Thaqalein, Qum, Taasisi ya Uchapishaji ya Nashra, Chapa ya Kwanza, 1392 Hijria Shamsia.
  • Khorramshahi, Qiwam al-Din, "Surat al-Kawthar, katika Daneshnameh va Qur'an Pezhuhi, Tehran: Dustan Nahid, 1377 Hijria Shamsia.
  • Swaduq, Muhammad bin Ali, Thawabul al-A'amal Waiqab al-A'amal, Qum, Dar al-Sharif Radhii, 1406 Hijria.
  • Tabatabai, Muhammad Hussein, al-Mizan Fi Tafsir al-Qur'ani, Beirut, Taasisi ya al-A'lami Lil-Matbuat, 1390 Hijriaa.
  • Tabatabai, Muhammad Hussein, al-Mizan Fi Tafsir al-Qur'ani, Utangulizi, Muhammad Javad Balaghi, Tehran, Nasser Khosrow, 1372 Hijria Shamsia.
  • Qur'an Karim, mtarjumi: Muhammad Mahdi Fooladvand, Tehran, Darul-Qur'an al-Karim, 1418 Hijria/1376 Hijria Shamsia.
  • Qumi, Sheikh Abbas, Mafatihul-Jinan, Tehran, Us'veh, 1384 Hijria Shamsia.
  • Makarem Shirazi, Nasser, Tafsir Nemooneh, Tehran, Darul-Kutub al-Islamiya
  • Vahidi, Ali bin Ahmad, Asbab Nuzul al-Qur'an, Beirut, Darul Kutuub al-Ilmiyah, 1411 Hijria.