Riwaya ya Ndoa ya Ali na Fatima (a.s)

Kutoka wikishia

Ndoa ya Ali (a.s) na Fatima (a.s) (Kiarabu: زواج الإمام علي من فاطمة الزهراء عليهما السلام) ni tukio kuhusiana na ndoa ya Imamu Ali (a.s) na bibi Fatimah (a.s), ambaye ni binti wa bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). Kulingana na vyanzo vya Hadithi ni kwamba; Kabla ya Imam Ali (a.s) kupeleka posa kwa ajili ya binti huyu, tayari watu wengine walikuwa wameshatangulia kutaka kufunga ndoa na Fatima (a.s), lakini bwana Mtume (s.a.w.w) aliwajibu kuwa suala la ndoa ya Fatima (a.s) liko mikononi mwa Mwenye Ezi Mungu.

Hotuba ya ndoa ya Imamu Ali na Fatima (a.s), ilisomwa na bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). Kulingana na imani maarufu miongoni mwa Waislamu ni kwamba; mahari ya bibi Fatima (a.s) ilikuwa ni dirhamu 500 (sawa na gramu 1500 za fedha safi), mahari ambayo huitwa mahari ya Sunna. Kulingana na maelezo ya Riwaya, Imamu Ali (a.s) aliuza ngao yake kisha Mtume Muhammad (s.a.w.w) akatumia pesa hizo kwa ajili ya kumnunulia bibi Fatima (a.s) vifaa na mahitaji ya kuanzia maisha ya kifamilia. Aidha, usiku wa ndoa ya Imamu Ali (a.s) na bibi Fatima (a.s), watu wa Madina walishiriki katika karamu ilioandaliwa kwa ajili ya sherehe za ndoa hiyo.

Ripoti za kihistoria pamoja na Hadithi zinaonyesha kuwa; ndoa ya Ali na Fatimah (a.s) ilitokea mnamo mwaka wa pili au wa tatu baada ya Hijra, ila kuna khitilafu za juu siku na mwezi halisi lilipotendeka jambo hilo. Kulingana na maelezo yalioko katika kitabu Manaqibu Aali Abi Talib (kiliyoandikwa katika karne ya 6 Hijiria) ni kwamba; mkataba wa ndoa wa ya Fatimah ulifungwa tarehe 1 ya Dhu al-Hijjah, na ndoa yao halisi ikanyika tarehe 6 ya Dhu al-Hijjah katika mwaka wa pili baada ya Hijra. Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tarehe 1 ya Dhu al-Hijjah inatambuliwa kama ni siku ya maadhimisho ya ndoa ya Imamu Ali na Fatima (a.s).

Posa ya Bibi Fatima (a.s)

Kulingana na vyanzo na vielelezo vya maandiko mbali mbali; kabla ya Imam Ali (a.s) kupeleka posa kwa bwana Mtumte (s.a.w.w), tayari kulikuwa na masahaba kadhaa waliomtangulia kabla yake, ambao baadhi yao walikuwa ni Abu Bakar na Omar ibnu Khattab. Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kurudisha jawabu kuhusiana na posa zao, aliwajibu kwa kauli isemayo: “Ndoa ya Fatima iko mikononi mwa Mwenye Ezi Mungu”. [1] Kulingana na Hadithi kutoka kwa Imamu Ali (a.s), ilioko katika kitabu cha Sheikh Tusi kiitwacho Aamali ni kwamba; Imamu Ali alimposa bibi Fatima kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w.), Mtume naye akaacha jawabu na uamuzi wa posa hiyo kwenye mikono ya Fatima. Kusalia kimwa ndio ikawa jawabu ya bibi Fatima (a.s), bwana Mtume (s.a.w.w) akakichukulia kimya chake hicho kuwa ishara na dalili ya ridhaa yake. [2] Baada ya hilo, Jibrilu (Gabriel) alimshukia bwana Mtume (s.a.w.w) na kumtaka amwoze binti yake (Fatima) Ali (a.s), kwani Mwenye Ezi Mungu alipenda kumwona bibi Fatima awe mikononi kwa Ali (a.s) na Ali (a.s) awe mikononi kwa bibi Fatima (a.s). [3] Baada ya ndoa ya Imamu Ali na bibi Fatima (a.s), baadhi ya Wahajirina (wahamiaji waliotoka Makka na Kuhamia Madina) ambao hapo awali walimposa bibi Fatima, walilalamikia bwana Mtume (s.a.w.w.), naye aliwajibu kwa kusema: “Ndoa ya Ali na Fatimah ilipita kwa amri ya Mwenye Ezi Mungu. [4]

Khutba Katika Mkataba Wao wa Ndoa

Kulingana na maoni ya Ibnu Shahri Ashub (aliyefariki mwaka 588 Hijiria) katika kitabu chake Manaqibu Aali Abi Talib, ni kwmaba; wakati wa ndoa ya bibi Fatima na Ali (a.s) ulipojiri, bwana Mtume (s.a.w.w) alipanda mimbari na kutoa hotuba akisema: Mwenye Ezi Mungu ameniamrisha Fatimah nimwozeshe Ali, nami nikafanya kama nilivyo amrishwa." [a.s] Katika maisha yake ya ndoa Imamu Ali na bibi Fatima (a.s), hakuwahi kuoa mke mwingine kando na Fatima (a.s). [5]

Kulingana na Hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Al-Aamali cha Sheikh Tusi, ni kwamba; ilikuwa ni haramu kwa Imam Ali (a.s) kuoa mke mwengine wakati wa uhai wa Bibi Fatima (a.s). [6]

Kufunga Ndoa Hadi Harusi

Baadhi ya vitabu vimeripoti kwamba baada ya ndoa, Ali (a.s) alihisi haya kumwomba Mtume kumruhusu amchukue mkewe na kuishi naye nyumbani kwake. Pia haikuwa ni jambo rahisi kwa Mtume kuanzisha mazungumzo juu suala hilo kabla ya ombi la Ali (a.s). Hii ilisababisha kupita muda, kati ya kufunga kwao hadi kuishi maisha ya kifamili, hata imekadiriwa kuwa; pengo la muda huo liliendelea kwa kiasi cha miezi kadhaa. [7] Hatimaye, Aqil aliuliza sababu ya suala hilo kutoka kwa kaka yake (Ali (a.s)) na baada ya kujua haya alizokuwa nazo Ali (a.s), aliandamana naye ili waweze kuzungumzia suala hilo na bwana Mtume. Pale Ummu Aiman aliposikia habari za suala hilo, alipendekeza wasiende kwa bwana Mtume (s.a.w.w), bali wazungumze na Ume-Salama. Ummmu Salama baada ya kujua kinacho enelea, alishikamana pamoja na wake wengine wa bwana Mtume (s.a.w.w), na kuelekea kwa bwana Mtume (s.a.w.w) na kuzungumza naye. Baada ya Mtume (s.a.w.w) kujua sababu ya Ali (a.s) ya kuto omba ruhusa ya kumchukua mkewe, alimwita kwake na kumwahidi harusi na kumtaka aandae nyumba kwa ajili Fatima (a.s). [8]

Baadhi ya wanazuoni wametaja Hadithi nyingine kuhusiana na jinsi ya Ali (a.s) alivyomwomba Mtume (s.a.w.w) kumchukua Fatima (a.s) na kwenda kuishi naye nyumbani kwake. [9]

Tarehe ya Ndoa

Kuna tofauti za maoni kuhusu tarehe ya ndoa ya Ali (a.s) na Fatima, kauli tofauti kuhusiana na tukio hilo ni kama ifuatavyo:

  • Ndoa ilifungwa siku ya kwanza ya Dhul-Hijjah, na sherehe za harusi zilifanyika tarehe sita ya Dhul-Hijjah, mwaka wa pili baada ya Hijra. [10] Kitabu cha Al-Misbah cha Kuf’ami (kilichoandikwa karne ya tisa baada ya Hijra), pia kinaelezea tarehe moja ya Dhul-Hijjah kama ni siku ya ndoa ya Ali (a.s) na Fatima. [11] Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku hii ya terehe moja imepewa jina la "Siku ya Ndoa".
  • Ndoa ilifungwa mwezi Mwishoni mwa mwezi Safar, mwaka wa pili baada ya Hijra. [12]
  • Ndoa ilifanyika mwezi wa Rajabu na sherehe za harusi zikafanyika baada ya Ali (a.s) kurudi kutoka katika vita vya Badr. [13]
  • Ndoa ilifungwa mwezi Ramadhani na sherehe za harusi zilifanyika mwezi wa Dhul-Hijjah, mwaka wa pili baada ya Hijra. [14]
  • Ndoa ilifanyika tarehe 21 Muharram, mwaka wa tatu baada ya Hijra. [15]
  • Ndoa ilifungwa mwishoni mwa mwezi wa Safar, na sherehe za harusi zikafanyika mwezi wa Dhul-Hijjah, mwaka wa pili baada ya Hijra. [16]
  • Ndoa pamoja na sherehe za harusi ilifanyika katika mwezi wa Rabi al-Awwal, mwaka wa pili baada ya Hijra. [17]

Kulingana na Muhammed Hadi Yusufi Ghurawi (aliyezaliwa mwaka wa 1327 Shamsia), ambaye mtafiti wa mambo ya historia, kipindi kati ya ndoa ya Ali na Fatima (a.s), hadi kufanyika kwa sherehe za harusi, takriban kilikuwa ni kipindi cha miezi kumi. Yeye anadhani ya kwamba; haraka za Mtume katika kufunga mkataba wa ndoa, ni kwa ajili ya kufikisha ujumbe kwa wale waliomposa bibi Fatima, ili wapate majibu wazi kabisa kutoka kwake. Pia, kuchelewa kwa sherehe ya harusi, ni kwa ajili ya kumpa bibi Fatima (a.s), muhula wa kukua kimwili na aweze kufikia umri wa wanawake wengine. [18]

Umri wa Bibi Fatima Wakati wa Kufunga Ndoa

Kuna tofauti za maoni kuhusiana na umri wa bibi Fatima (a.s) wakati wa ndoa yake. Kulingana na maoni ya Sayyid Muhsin Amin, mfasiri wa Kishia (aliye fariki mnamo mwaka 1371 Hijiria),ni kwamba; tofauti hizi zinahusiana na tofauti katika tarehe ya kuzaliwa pamoja na tarehe ya ndoa yake. Kulingana na maoni maarufu, ni kwamba; bibi Fatima alizaliwa mwaka wa tano baada ya Utume. Ambapo tofauti ya maoni kuhusiana na ndoa yake ni kwamba; ima yeye aliolewa mwaka wa kwanza, wa pili, au wa tatu kulingana na kalenda ya Hijria. Umri wake wakati wa ndoa umetajwa kuwa miaka tisa, kumi, au kumi na moja. [19] Hata hivyo, katika vyanzo vingine, umri wa bibi Fatima wakati wa ndoa yake, ni miaka kumi na nane [20] au miaka kumi na tano na miezi mitano. [21]

Pia, katika kitabu cha Al-Istii'aab ambacho ni miongoni mwa vyanzo vinavyo husiana na Masahaba wa karne ya tano Hijria, imeelezwa kwamba; umri wa Imamu Ali (a.s) wakati wa ndoa yake na bibib Fatima (a.s) ulikuwa ni miaka ishirini na moja. [22]

Mahari na Nyenzo za Kuanzia Maisha

Makala Asili: Nyenzo za Fatima (a.s) za Kuanzia Maisha

Kulingana na yaliokuja katika Hadithi ni kwamba; mahari ya bibi Fatima (a.s) ilikuwa ima ni wakia kumi na mbili na nusu, [23] ua dihamu 500, dirhamu 480 au dirhamu 400. [24] Kulingana na maelezo ya Ibnu Shahraashub (aliye ishi kati yam waka 488 na 588 Hijiria), ambaye ni mfasiri wa Shia, ni kwamba; habari sahihi zaidi juu ya mahari hayo, ni dirhamu mia tano. [25] Anaelezea akisema kwamba; tofauti hiyo inatokana na Hadithi fulani ambazo kwa mujibu wake, mahari mahari ya Fatima ilikuwa kitambaa cha kitani kilichotengenezwa nchini Yemen, au ngozi ambayo haijatolewa manyoya, au mmea wenye harufu nzuri. Pia kulingana na Hadithi nyingine, ilikuwa ni silaha na ngozi ya kondoo au ngamia ambayo haijatolewa manyoya. [26] Kwa kuwa Dinari 500 ilikuwa ndiyo mahari ya wake pamoja binti za Mtume (s.a.w.w), hivyo basi kiwango hichi cha mahari kinajulikana kama ni mahari ya Sunaa. [27] Dinari 500 kiuhalisia ni takriban gramu 1500 za fedha safi. [28]

Kulingana na maelezo ya Sheikh Tusi katika kitabu chake Al-Aamali, ni kwamba Imam Ali (a.s) kwa amri ya Mtume (s.a.w.w), aliuza vasi lake la kivita, [29] na Mtume (s.a.w.w) alimpa sehemu ya pesa hizo Bilal Habashi ili kununua manukato kwa ajili ya bibi Fatima. [30] Kisha sehemu iliyobaki ilipewa Abu Bakar ili atayarishe vifaa vya kuanzia maisha ya kifamilia, akiwa pamoja na Ammar bin Yasir na masahaba wengine kadhaa, walifanya kazi hizyo chini ya uangalizi wa Abu Bakar, na wakanunua vitu vyote muhimu vilivyo hitajika. [31] Moja ya vitu vilivyo tayarishwa kwa ajili ya bibi Fatima (a.s) ilikuwa gauni, gauni ambalo bibi Fatima (a.s) alilitoa na kumpa mwanamke mwenye shida usiku wa harusi yake, huku yeye mwenyewe akitosheka na nguo iliokwisha tumika. [32]

Karamu na Makazi Yao

Kulingana na Hadithi iliyosimuliwa na Sheikh Tusi katika kitabu chake cha Al-Aamali, bwana Mtume (s.a.w.w) na Ali (a.s) walipika karamu kubwa iliolisha idadi kubwa mno ya watu miongoni mwa masahaba. Bwana Mtume (s.a.w.w) alitoa nyama na mikate, Ali naye akatayarisha tende na mafuta. Baada ya kumaliza karamu hiyo, bwana Mtume (s.a.w.w) alimkauweka mkono wa bibi Fatima (a.s) kwenye mkono wa Imamu Ali (a.s) na akawaombea dua na akusema: Ewe Ali! Fatima ni mke mzuri mno, na kwa upande wa Fatima kamwambia akisema: Ewe Fatima! Ali ni mume mzuri mno. Kisha wawili hao akawaruhusu waende nyumbani kwao, kisha bwana Mtume (s.a.w.w) akawafuata na kuwaombea dua ya baraka kwa watoto wao. [33]

Kulingana na vyanzo vya kihistoria; siku chache baada ya Ali na Bibi Fatima (a.s) kumaliza harusi, nyumba yao ikahamia karibu na nyumba ya bwana Mtume (s.a.w.w), hii ni kwa sababu bwana Mtume (s.a.w.w) hakuwa akistahamili umbali uliopo baina yake na binti yake (bibi Fatima) (a.s). Kwanza, bwana Mtume alitaka kuwaweka katika nyumba yake, lakini Haritha bin Nu'man, mmoja wa masahaba wake, alitoa nyumba yake ambayo ilikuwa jirani na nyumba ya Mtume (s.a.w.w) ili iwe nyumba ya Ali na Fatima (a.s). [34]

Angalia pia: Nyumba ya Bibi Fatima (a.s)

Vyanzo

  • Ibn Saad, Muhammad, Tabaqat al-Kabri, iliyotafitiwa na Muhammad Abd al-Qadir Atta, Beirut, Dar al-Kitab al-Alamiya, 1410 AH/1990 AD.
  • Ibn Shahrashob, Muhammad Bin Ali, Menaqib Al Abi Talib, Qom, Allamah Publications, 1379 AH.
  • Ibn Tawoos, Ali Ibn Musa, Iqbal al-Amal, Tehran, Dar al-Kitab al-Islamiya, 1409 AH.
  • Ibn Abd al-Barr, Yusuf bin Abd Allah, Al-Istiyab fi Marafah al-Ashab, utafiti wa Ali Muhammad al-Bajawi, Beirut, Dar al-Jeel, 1412 AH/1992 AD.
  • Erbali, Ali Ibn Isa, Kashf al-Ghamma fi Marafah Al-Ima, imesahihishwa na Seyyed Hashem Rasouli Mahalati, Tabriz, Bani Hashemi, 1381 AH.
  • Amin, Seyyed Mohsen, Ayan al-Shia, iliyotafitiwa na Seyyed Hasan Amin, Beirut, Dar al-Taf kwa Vyombo vya Habari, 1403 AH.
  • Hosni, Hashem Ma'rouf, Maisha ya Maimamu wa Kumi na Mbili, Najaf, Al-Maktab Al-Haydariyya, 1382 AH.
  • Shoshtari, Nurullah bin Sharifuddin, Ihqaq al-Haq na Izhaq al-Batil, Qom, Ayatollah Mar-ashi Najafi Maktaba ya Umma, 1409 AH.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan, al-Mali, iliyosahihishwa na Est. Al-Baath, Qom, Dar al-Thaqafa, 1414 AH.
  • Sadouq, Muhammad bin Ali, Al-Muqnaa, Qom, taasisi ya Imam Mahdi (A.S.), 1415 AH.
  • Tabarsi, Fazl bin Hasan, I’Ilamu al-Waraa bii Alam al-Huda, Qom, Al-Al-Bayt, 1417 AH.
  • Tabari, Muhammad bin Jarir, Taarikh Al-Umam na Al-Muluk, iliyofanyiwa utafiti na Muhammad Abulfazl Ibrahim, Beirut, Dar al-Turath, chapa ya pili, 1387/1967 AD.
  • Kafaami, Ibrahim bin Ali, al-Masbah, Qom, Dar al-Rezi, chapa ya pili, 1405 AH.
  • Majlisi, Mohammad Baqir, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ahya al-Trath al-Arabi, chapa ya pili, 1403 AH.
  • Masoudi, Abdul Hadi, "Utafiti kuhusu Mehr al-Sunnah (Muhuri wa Mohammedan)", kutoka kwa mtazamo wa Qur'an na Hadith, Qom, Dar al-Hadith, toleo la 2, 2009.
  • Yaqoubi, Tarikh Eliaqoubi, Beirut, Dar Sadir, Bita.
  • Yousefi Gharavi, Mohammad Hadi, Historia ya Utafiti ya Uislamu: Encyclopedia of History of Islam, iliyotafsiriwa na Hossein Ali Arabi, Qom, Imam Khomeini Institute Publications, 1383.