Ndoa

Kutoka wikishia

Ndoa (Kiarabu: النكاح أو الزواج)) ni maafikiano rasmi ya mafungamano baina ya mwanaume na mwanamke ili waweze kuishi pamoja kama mke na mume, na hilo linapatikana na kutimia kwa nikaha (kufunga ndoa). Qur'an Tukufu inaitaja ndoa na suala la wanaume kuwa kando ya wake zao kuwa ni chimbuko la utulivu na linawataka Waislamu wawaozeshe wanaume na wanawake wasio na wenza wa ndoa. Kwa mujibu wa hadithi, ndoa ni neema kubwa kabisa baada ya neema ya Uislamu na kuoa ni kuhifadhi nusu ya dini na ni Sunna ya Bwana Mtume (s.a.w.w).

Kushikamana na dini, tabia njema na familia nzuri na ya heshima ni miongoni mwa sifa na vigezo vilivyokokotezwa na kutiliwa mkazo katika hadithi kwa ajili ya kuchagua mwenza wa ndoa. Kwa mtazamo wa mafakihi, ndoa yenyewe kama ndoa ni mustahabu na sunna iliyotiliwa mkazo, lakini kama kwa kutooa au kutoolewa mtu atatumbukia katika maasi na dhambi, basi kwake yeye ndoa ni wajibu

Katika madhehebu ya Shia Imamiyah, ndoa inagawanyika katika sehemu mbili: Ndoa ya daima na ndoa ya muda (muta’); katika tamko la nikaha (la kufunga ndoa) ya muda, ni sharti kuainisha muda na kiwango cha mahari na baada ya kumalizika muda, mke na mume hutengana pasi na ya kupeana talaka. Kwa maana kwamba, kumalizika muda ndiko kunakowatenganisha.

Katika vitabu va fiq'h vya Tawdhih al-Masail (ufafanuzi wa hukumu na sheria za Kiislamu) kumezungumziwa hukumu za kifiq'h nyingi kuhusiana na ndoa ambapo muhimu zaidi miongoni mwazo ni kusoma tamko la nikaha ambalo ni mwanamke kumwambia mwanaume baada ya maafikiano na maridhiano juu ya mahari na muda: "Zawwajtuka nafsi bimahri qadruhu kadha ilal-ajalil-maalum" (Nimekuoza nafsi yangu kwa mahari kadha kwa muda maalumu), na muda unabainishwa wazi. Na jibu la mwanaume bila ya kuchelewa linakuwa: "Qabiltu" (Nimekubali), na ndoa haitimii tu kwa mwanamke na mwanaume kuwa wameridhiana, la hasha. Kwa binti ambaye ni bikira, ridhaa na idhini ya baba yake au babu mzaa baba kwa ajili ya ndoa ya muda ni jambo la lazima. Ndoa hufikia tamati kwa kulaaniana, talaka, kifo, kubadilisha jinsia, kuritadi na kuweko moja ya mambo yanayopelekea kubatilishwa ndoa au kuvunjwa. Baada ya kuachana, mke anapaswa kukaa eda.

Fasili (maana) na aina za ndoa

Ndoa ni kuleta mfungamano wa mke na mume kupitia nikaha na kufunga ndoa kwa tamko la nikaha. Katika madhehebu ya Shia Imamiyyah ndoa inagawanyika katika sehermu mbili; ndoa ya daima na ndoa ya muda. Katika tamko la ndoa ya muda (ambalo ni mwanamke kusema kwamba, anaiozesha nafasi yake) suala la kuainisha muda linazingatiwa, na baada ya kumalizika muda, mke na mume hutengana pasina ya kupeana talaka. Kwa maana kwamba, kumalizika muda ndiko kunakowatenganisha. [1]

Ndoa ya muda

Makala Kuu: Ndoa ya Muta’

Ndoa ya Muda (muta’) ilikuwa halali katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w); lakini Khalifa wa pili akaja kuiharamisha katika kipindi cha utawala wake. [2] Miongoni mwa madhehebu za Kiislamu, Shia Imamiyyah peke yao ndio wanaoitambua ndoa ya Muta’ (muda) kuwa ni halali. [3] Tofauti ya kimsingi na muhimu baina ya ndoa ya daima na ya muda ni kuwa na muda na wakati maalumu; kwa namna ambayo kuainisha muda wakati wa kufunga na kutoa tamko la nikaha katika ndoa hii ni jambo la lazima na la dharura. [4]

Tofauti baina ya ndoa ya daima na ya muda

Ndoa za daima na ndoa za muda zina hukumu nyingi ambazo zinashirikiana; miongoni mwazo ni kusomwa au kutolewa tamko la nikaha ambalo ni jambo la lazima kwa ndoa zote mbili. Ndoa hizi mbili zina tofauti kadhaa ambazo ni:

 • Katika ndoa ya daima, kinyume na ndoa ya muda, mwanamume lazima atoe matumizi kwa mke (amhudumie).
 • Katika ndoa ya daima, mwanamke hawezi kutoka ndani ya nyumba bila ya idhini ya mume; lakini katika ndoa ya muda, idhini ya mume katika hilo siyo lazima.
 • Katika ndoa ya daima, tofauti na ndoa ya muda, mume na mke wanarithiana. [5]
 • Kama katika tamko la nikaha kwenye ndoa ya muda kama mahari haitatajwa, ndoa inabatilika; lakini katika ndoa ya daima, ndoa huwa sahihi na kama mume na mke watakutana kimwili, mwanamke hupatiwa mahari ya mithili. (kiwango cha mahari kwa mujibu wa ada na mazoea na kwa kuzingatia hali ya mwanamke kiumri, uzuri, elimu, nafasi ya kijamii na kadhalika). [6]

Nafasi ya ndoa

Dini tukufu ya Kiislamu inazingatia na kutoa umuhimu mkubwa kwa suala la ndoa na imeitambulisha kuwa ni moja ya Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w). [7] Kadhalika Qur’an Tukufu imeitambua ndoa kuwa sababu na chimbuko la kupatikana utulivu [8] na imewausia Waislamu kuwaoezesha wanawake na wanaume wasio na wake au waume (wenza wa ndao). [9]

Katika hadithi kumetajwa sifa nyingi maalumu na upendeleo usio na kifani kwa suala la ndoa. Miongoni mwazo ni kwamba, ndoa imetajwa kuwa moja ya neema kubwa zaidi baada ya neema ya Uislamu, [10] ni sababu ya kheri duniani na akhera, [11] kuwa katika ndoa ni kuhifadhi nusu au theluthi ya dini [12] na ni sababu ya kuongezewa riziki. [13] Kadhalika wafu wabaya kabisa wa Waislamu wanatambulishwa kuwa ni watu ambao wameaga dunia hali ya kuwa hawakuwa katika ndoa. [14]

Hukumu

Katika Tawdhif al-Masail (vitabu vya ufafanuzi wa sheria za Kiislamu), Marajii Taqlidi wamebainisha hukumu mbalimbali za kifiq’h kuhusiana na ndoa ambapo baadhi yazo ambazo ni muhimu zaidi ni:

 • Kwa mtazamo wa mafaqihi ndoa yenyewe kama ndoa ni mustahabu na sunna iliyotiliwa mkazo, lakini kama kwa kutooa/kutoolewa mtu atatumbukia katika maasi na dhambi, basi kwake yeye ndoa ni wajibu. 15]
 • Katika ndoa ya daima na ya muda, ni lazima kusoma tamko la nikaha (tamko la kufunga ndoa) na haitoshi tu kwa mwanamke na mwanaume kuridhia suala hilo. [16]
 • Mwanaume na mwanamke wanaweza kusoma wenyewe tamko la nikaha (wanaweza kujifungisha ndoa wao wenyewe) au wakamfanya mtu kuwa wakili wao ambaye atasoma tamko hilo la kufunga ndoa kwa niaba yao yaani kwa kuwawakilisha. [17]
 • Kama mwanamke na mwanaume wana uwezo wa kusoma tamko la ndoa la lugha ya Kiarabu wao wenyewe, basi ni lazima walisome kwa Kiarabu. [18]
 • Binti ambaye ni bikira anapaswa kupata idhini ya kuolewa kutoka kwa baba yake au babu mzaa baba. [19]
 • Ni haramu kwa mwanaume kuoana na maharimu kama mama, dada na mama mkwe. [20]
 • Haijuzu kwa mwanamke wa Kiislamu kufunga ndoa ya daima au ya muda na mwanaume asiyekuwa Muislamu. [21]
 • Inajuzu kwa mwanaume wa Kiislamu kufunga ndoa ya muda na mwanamke asiyekuwa Mwislamu kama atakuwa ni Ahlul-Kitab. [22]

Vigezo vya kuchagua mke kwa mujibu wa hadithi

Katika baadhi ya hadithi kumebainishwa vigezo kwa ajili ya ndoa ambavyo vinapaswa kuzingatiwa wakati wa kuchagua mke. Kwa mujibu wa hadithi ni kwamba, Mtume (s.a.w.w) alimnasihi mtu mmoja kwamba, aoane na watu wenye dini. [23] Katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq, Imamu Swadiq (a.s) amenukuliwa akisema: Oaneni na familia stahiki; kwani sifa maalumu za familia zinahamia kwa watoto. [24] Imamu Ridha (a.s) pia amenukuliwa akisema: Jiepushe kufunga ndoa na mtu mwenye tabia mbaya. [25]

Sababu ya kufikia tamati ndoa

Sababu za kufikia tamati ndoa kwa mujibu wa mafaqihi ni: Kubadilisha jinsia, [26] kifo, talaka na vitu ambavyo vinapelekea ndoa kubatilishwa na kuvunjwa. [27] Baada ya ndoa kuvunjika au kufikia tamati, mwanamke anapaswa kukaa eda (muda maalumu ambao mke hana haki ya kuolewa). [28]

Vizuizi vya ndoa

Katika fiq’h ya kiislamu (sheria) kutokana na kuweko vizuizi, ni haramu kuwaoa baadhi ya wanawake:

 • Vizuizi vya muda: Mazingira na masharti ambayo ndani yake ni haramu kuoana mwanamke na mwanaume kwa muda fulani na kwa kuondoka mazingira hayo, uharamu nao huondoka. [29]

Kama vile:

 1. Kutimia idadi: Kwa maana kwamba, mwanaume hawezi kuoa zaidi ya wake wanne huru kwa ndoa ya daima (kuwa na zaidi ya wake wanne kwa daima kwa wakati mmoja). [30] Aidha kwa kuwa na wake wawili makanizi (binti au mwanamke asiyekuwa Mwislamu aliyekuwa akikamatwa mateka katika vita vya Waislamu na makafiri) hawezi kuoa kanizi wa tatu (kwa maana kwamba, hawezi kuwa na makanizi zaidi ya wawili kwa wakati mmoja). [31]
 2. Kuwaoa kwa pamoja dada wawili: Ni haramu kuwaoa dada wawili kwa wakati mmoja. Lakini kama mume atafiwa na mkewe au wakaachana basi anaweza kumuoa dada wa mke wake wa zamani. [32]
 3. Kukufuru na kuritadi: Haijuzu kwa mwanamke Mwislamu kuolewa na kafiri harbii (anayeupiga vita Uislamu) au kafikafiri Ahl Kitaba ambavyo haijuzu kuolewa na murtadi. [33] Kadhalika haijuzu kwa mwanaume Mwislamu kumuoa kafiri asiyekuwa Ahl Kitab au murtadi. [34]

Sheria ya kusajili ndoa

Katika nchi nyingi ndoa husajiliwa kisheria. [44] Nchini Iran pia kwa mujibu wa kifungu cha 645 cha sheria ya adhabu za Kiislamu, inahesabiwa kuwa ni kosa na uhalifu kwa mke na mume kutosajili ndoa. [45] Baadhi ya malengo ya kusajili kisheria ndoa ni: Kupata uhakika wa usahihi wa nikaha, kuzuia mizozo na kurahisisha kuthibitisha haki za wanandoa. [46]

Vyanzo

 • Asadī, Leylā Sādāt. Naqd wa barrasī qawānīn-i thabt-i izdiwāj. Muṭāliʿāt Rāhburdī Zanān. Tehran: Shurā-yi Farhangī Ijtimaʿī-yi Zanān wa khāniwāda, Summer 1387, No 40.
 • Akbarī, Maḥmūd. Aḥkām-i khāniwāda. Qom: Fityān, 1393 Sh.
 • Ḥusaynī, Sayyid Mujtabā. Aḥkām-i izdiwāj. (According to the view of 10 Marjaʿ). 7th edition. Qom: Daftar-i Nashr-i Maʿārif, 1389 Sh.
 • Khomeini, Sayyid Rūḥ Allāh. Taḥrīr al-wasīla. Tehran: Muʾassisa-yi Tanẓīm wa Nashr-i Āthār-i Imām Khomeini, 1384 Sh.
 • Khomeini, Sayyid Ruḥ Allāh. Tawḍīh al-masāʾil. Edited by Sayyid Muḥammad Ḥusayn Banī Ḥāshimī. 8th edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1424 AH.
 • Subḥānī, Jaʿfar. Izdiwāj-i muwaqqat dar kitāb wa sunnat. Fiqh-i Ahl al-Bayt (a), No 48. 1385 Sh.
 • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn b. ʿAlī. Masālik al-ifhām ilā tanqīh sharāyiʿ al-Islām. 1st edition. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1413 AH.
 • Ṣanʿānī, ʿAbd al-Razzāq b. Humām. Al-Muṣannaf. [n.p]. Majlis-i ʿIlmī, 1390 AH.
 • Ṭabrisī, Ḥasan b. al-Faḍl al-. Makārim al-akhlāq. 4th edition. Qom: al-Sharīf al-Raḍī, 1412 AH.
 • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Mabsūṭ fī fiqh al-imāmīyya. Edited by Muḥammad Taqī Kashfī. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya li Iḥyāʾ al-Āthār al-Jaʿfarīyya, 1387 AH.