Mkopo:Dhamana za Uimamu
Dhamana za Uimamu (وَدَائِع الإِمَامَة) ni vitu na athari za kale za Manabii, Imam Ali (a.s), na Bibi Fatima (a.s) ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa na kubaki mikononi mwa Maimamu wa Kishia, na vilikuwa vikitambuliwa kama miongoni mwa vigezo na alama kuu za kumjua Imamu wa haki. Upanga na pete ya Mtume (s.a.w.w), Fimbo ya Musa, Pete ya Suleiman, na vitabu vya Mus'haf wa Fatima (a.s), pamoja na vitabu vya Al-Jafr na Al-Jamiah ni miongoni mwa vitu hivyo.
Maimamu wa Kishia walikuwa wakitumia uwepo wa dhamana hizi za Uimamu zilizo mikononi mwao kama dalili thabiti wakati walipokuwa wakikabiliana na wale waliokuwa wakidai Uimamu kwa njia ya uongo, au pale walipotaka kuondoa shaka na mikanganyiko ya Mashia katika kumtambua Imamu wa kweli.
Dhana na Nafasi Yake
Makusudio ya dhamana (Wada'i) ni vitu maalum, kama vile upanga, kitabu, na pete, ambavyo hukabidhiwa kama amana kutoka kwa Imamu mmoja kwenda kwa Imamu anayefuata, na navyo ni alama ya Uimamu wake. Dhamana za Uimamu, zikienda sambamba na wasia wa Imamu aliyetangulia, zilikuwa miongoni mwa vigezo muhimu vya kumtambua Imamu anayofuata;[1] hususan kwa kuwa uthibitisho wa Uimamu kupitia wasia ulikuwa jambo lisilowezekana katika mazingira ya Taqiyyah (kuficha imani kwa usalama).[2] Kwa ajili hiyo, dhamana za Uimamu zilitiliwa mkazo mkubwa ili kusiwepo na shaka wala utata wowote katika kumtambua Imamu husika.[3]
Mifano na Vielelezo
Katika riwaya zilizopokelewa kwenye vyanzo vya Kishia, kuna mambo kadhaa ambayo yamehesabiwa kuwa ni miongoni mwa dhamana za Uimamu. Maimamu walikuwa wakiashiria kuwepo kwa vitu hivyo mikononi mwao kwa kutumia maneno kama “Indana” (kiko kwetu) au “Indi” (kiko kwangu):
| Dhamana za Uimamu | Maelezo |
|---|---|
| Upanga wa Mtume (s.a.w.w)[4] | Katika riwaya kutoka kwa Imam al-Sadiq (a.s), baada ya kuufanisha upanga wa Mtume na sanduku la Bani Israil, inasema: “Upanga wa Mtume (s.a.w.w) ukiwa kwa yeyote miongoni mwetu, basi amepewa Uimamu.”[5] Kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, upanga huu ni ule ule wa Zulfiqar.[6] |
| Al-Jafr[7] | Ni kitabu ambacho ndani yake yametajwa matukio yote yajayo hadi Siku ya Kiyama.[8] |
| Al-Jamiah | Ni kitabu kilichoandikwa kwa imla ya Mtume (s.a.w.w) na kwa mwandiko wa Imam Ali (a.s), na ndani yake kuna hukumu zote za Halali na Haramu.[9] |
| Kitabu cha Ali (a.s)[10] | Baadhi ya wanazuoni wamekiona kitabu cha Al-Jamiah na Kitabu cha Ali kuwa ni kitabu kimoja chenye majina mawili tofauti;[11] lakini Aqa Bozorg Tehrani amekitaja kitabu hiki kwa anuani ya *Amali ya Mtume wa Mwenyezi Mungu* na kukiona kuwa ni tofauti na Al-Jafr na Al-Jamiah.[12] |
| Mus'haf wa Fatima (a.s) | Kitabu ambacho Malaika wa mbinguni alikuwa akimwambia Bibi Fatima (a.s) kisha Imam Ali (a.s) akawa anakitengeneza kwa kukiandika.[13] |
| Sahifa ya Faradhi | Inahusu masuala ya Mirathi kwa mwandiko wa Imam Ali (a.s).[14] |
| Pete ya Mtume (s.a.w.w)[15] | |
| Dirii ya Mtume (s.a.w.w)[16] | Katika riwaya mbalimbali imeelezwa kuwa, miongoni mwa alama za Imamu ni kwamba dirii (nguo ya chuma ya vita) ya Mtume (s.a.w.w) inakuwa inamwenea vizuri mwilini mwake.[17] |
| Al-Jafr Jekundu | Ni mfuko wa ngozi ambao ndani yake kuna silaha za Mtume (s.a.w.w).[18] |
| Al-Jafr Jeupe | Ni mfuko wa ngozi uliomo vitabu vya Torati, Injili, Zaburi, na vitabu vingine vya mbinguni.[19] |
| Diwani ya Mashia | Ambayo ina majina ya Mashia wote. Katika baadhi ya riwaya, kitabu hiki kimetajwa kwa jina la “Namus”.[20] |
| Urithi wa Manabii wengine | Kama vile Mbao za Torati, tasi (bakuli kubwa), Sanduku la Agano (Tabut), Fimbo ya Musa, na Pete ya Suleiman.[21] |
Hoja za Maimamu Kupitia Dhamana za Uimamu
Maimamu wa Kishia walikuwa wakitumia uwepo wa dhamana hizi za Uimamu zilizo mikononi mwao kama dalili na hoja madhubuti mbele ya watu waliokuwa wakidai Uimamu kwa uongo au pale walipokuwa wakikabiliana na shaka na mikanganyiko ya Mashia. Kwa mfano, Imam Ali (a.s) katika Baraza la Watu Sita alisema: “Nakuapieni kwa Mwenyezi Mungu! Je, kuna yeyote kati yenu asiyekuwa mimi ambaye silaha, bendera, na pete ya Mtume wa Mwenyezi Mungu viko mikononi mwake?”[22]
Imam al-Sadiq (a.s)—ambaye kwa upande mmoja alikuwa akikabiliana na harakati ya ma-Hasani waliokuwa wakieneza propaganda za umahdi wa Muhammad bin Abdallah al-Mahdh,[23] na kwa upande mwingine alikuwa akizikabili harakati mbili za Kaysaniyyah na Zaidiyyah—alikuwa akitumia uwepo wa silaha za Mtume mikononi mwake kama nyenzo ya kuwasimamishia hoja dhidi yao.[24] Imepokelewa kuwa Imam al-Sadiq (a.s) aliambiwa: “Kuna kundi la watu linalodhani kuwa upanga wa Mtume wa Mwenyezi Mungu uko mikononi mwa Abdallah bin Hassan.” Yeye akajibu:
“Naapa kwa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, Abdallah bin Hassan hajawahi hata kuuona upanga huo. Upanga na bendera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ziko kwangu mimi. Silaha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kama lile sanduku (Tabut) lililokuwa kwa Bani Israil. Popote pale sanduku lilipokuwa linapatikana, basi utume ulikuwa hapo hapo. Silaha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu pia ikiwa kwa yeyote yule, basi yeye ndiye Imamu.”[25]
Uhamishaji wa Dhamana kutoka Imamu mmoja kwenda Imamu anayefuata
Kwa mujibu wa riwaya za Kishia, dhamana za Uimamu zilikuwa zikikabidhiwa kutoka kwa Imamu mmoja kwenda kwa Imamu mwingine; iwe ni kwa njia ya moja kwa moja au kupitia mtu wa kati. Imepokelewa kutoka kwa Ja'far al-Sadiq (a.s) akisema: "Vitabu vilikuwa mikononi mwa Ali (a.s). Wakati alipoelekea Iraq, aliviweka vitabu hivyo kama amana kwa Ummu Salama. Baada yake, vitabu hivyo vilikuwa kwa Hassan (a.s), na baada yake vilikuwa kwa Hussein (a.s), na baada yake vilikuwa kwa Ali bin Hussein (a.s), na baada yake vilikuwa kwa baba yangu."[26]
Pia imepokelewa kuwa, wakati Imam Husayn (a.s) alipoondoka kuelekea Iraq, aliacha vitabu na wasia kama amana kwa Ummu Salama, mke wa Mtume (s.a.w.w). Wakati Ali bin Husayn (a.s) aliporejea, Ummu Salama alimkabidhi vitu hivyo.[27]
Kadhalika, imepokelewa kutoka kwa Muhammad al-Baqir (a.s) akisema: "Wakati wakati wa kufa kwa Ali bin Husayn (a.s) ulipowadia, alileta sanduku na kuniambia: 'Ee Muhammad, chukua sanduku hili'. Ndani ya sanduku hilo mlikuwa na upanga wa Mtume wa Mwenyezi Mungu pamoja na vitabu vyake."[28]
Mahali zilipo Dhamana katika kipindi cha Ghaiba
Kwa mujibu wa ripoti ya Allamah Majlisi, dhamana za Uimamu katika kipindi cha Ghaybah Ndogo zilikuwa mikononi mwa wawakilishi maalum wa Imam wa Zaman (a.f). Katika ripoti yake imeelezwa kuwa, wakati mwakilishi wa pili, Muhammad bin Uthman, alipofariki dunia, mtumishi wake alimkabidhi mwakilishi wa tatu, Husayn bin Ruh al-Nawbakhti, kisanduku kidogo ambacho ndani yake mlikuwa na dhamana za Uimamu.[29]
Kwa mujibu wa maelezo ya Aqa Bozorg Tehrani, ikitegemewa riwaya za Kishia, hivi sasa dhamana zote za Uimamu ziko mikononi mwa Imamu wa Kumi na Wawili (a.f).[30]
Rejea
- ↑ Sheikh Tusi, Al-Iqtisad, Uk. 375.
- ↑ Tabataba'i, «Justari dar Asib-shenasiye Chalesh-haye Aghaze Imamate Imam Kadhim», Uk. 104.
- ↑ Tabataba'i, «Justari dar Asib-shenasiye Chalesh-haye Aghaze Imamate Imam Kadhim», Uk. 79.
- ↑ Al-Kulaini, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 305.
- ↑ Al-Kulaini, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 238.
- ↑ Ibn Shahr Ashub, Al-Manaqib, Jz. 4, Uk. 135 na 253.
- ↑ Al-Kulaini, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 239; Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 152.
- ↑ Sheikh Saduq, Kamal al-Din, Jz. 2, Uk. 353.
- ↑ Sheikh Mufid, Al-Irshad, Jz. 2, Uk. 186.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 147.
- ↑ Askari, Ma'alim al-Madrasatayn, Jz. 2, Uk. 335-338.
- ↑ Aqa Bozorg Tehrani, Al-Dhari'ah, Jz. 2, Uk. 306-307.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 152-153.
- ↑ Aqa Bozorg Tehrani, Al-Dhari'ah, Jz. 2, Uk. 162.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 156.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 156.
- ↑ Ibn Shahr Ashub, Al-Manaqib, Jz. 1, Uk. 253; Sheikh Mufid, Al-Irshad, Jz. 2, Uk. 217.
- ↑ Sheikh Mufid, Al-Irshad, Jz. 2, Uk. 186.
- ↑ Sheikh Mufid, Al-Irshad, Jz. 2, Uk. 186.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 173.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 175.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 182.
- ↑ Najafiyan Razavi, «Barresi-ye Chegungi-ye Monasabate Hasaniyan wa Imamane Shia, Motale'ate Tarikhe Islam».
- ↑ Sheikh Mufid, Al-Irshad, Jz. 2, Uk. 187-188.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 175.
- ↑ Saffar, Basa'ir al-Darajat, Uk. 162.
- ↑ Kulaini, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 304; Ibn Shahr Ashub, Al-Manaqib, Jz. 4, Uk. 172.
- ↑ Kulaini, Al-Kafi, Jz. 1, Uk. 305.
- ↑ Majlisi, Bihar al-Anwar, Jz. 85, Uk. 211.
- ↑ Aqa Bozorg Tehrani, Al-Dhari'ah, Jz. 21, Uk. 126.
Vyanzo
- Askari, Sayyid Murtadha, Ma'alim al-Madrasatain, Beirut, Mu'assasat Nuuman, 1410 H / 1990 M.
- Agha Bozorge Tehrani, Muhammad Muhsin, Al-Dhari'ah ila Tasanifu al-Shia, Qom, Isma'ilian, 1408 H / 1988 M.
- Ibn Shahr Ashub, Muhammad bin Ali, Al-Manaqib, Qom, Nashre Allamah, 1379 H / 1959 M.
- Kulaini, Muhammad bin Yaqub, Al-Kafi, Tehran, Islamiyyah, chapa ya 2, 1362 Sh / 1983 M.
- Majlisi, Muhammad Baqir, Bihar al-Anwar al-Jamiah li-Durar Akhbar al-A'immat al-Athar, Beirut, Mu'assasat al-Wafa, 1403 H / 1983 M.
- Mufid, Sheikh, Muhammad bin Muhammad, Al-Irshad fi Ma'rifat Hujaj Allah ala al-Ibad, Qom, Kongresi ya Sheikh Mufid, 1413 H / 1993 M.
- Najafiyan Razavi, Layla, “Barresiye Chegunegiye Monasabate Hasaniyan wa Emamane Shia ta Sal-e 145 Hejri Qamari” (Uchunguzi wa Jinsi ya Uhusiano Kati ya Watu wa Kizazi cha Imamu Hasani na Maimamu wa Kishia Mpaka Mwaka 145 Hijiria), Motale'ate Tarikhe Islam Utafiti wa Historia ya Uislamu, nambari 5, 1392 Sh / 2013 M.
- Saffar, Muhammad bin Hasan, Basa'ir al-Darajat fi Fada'il Aal Muhammad, Qom, Maktaba ya Ayatullah Mar'ashi Najafi, chapa ya 2, 1404 H / 1984 M.
- Saduq, Sheikh, Muhammad bin Ali, Kamal al-Din wa Tamam al-Ni'mah, uhakiki: Ali Akbar Ghaffari, Tehran, Islamiyyah, chapa ya 2, 1395 H / 1975 M.
- Tabataba'i, Muhammad Kazim, “Justari dar Asib-shenasiye Chalesh-haye Aghaze Imamate Imam Kadhim” (Utafiti Kuhusu Changamoto za Mwanzo wa Uimamu wa Imam Kadhim), Majalleh Imamat-pazhohi (Jarida la Utafiti wa Uimamu), nambari 8, wakati wa baridi, 1391 Sh / 2012 M.
- Tusi, Sheikh, Muhammad bin Hassan, Al-Iqtisad fima Yajibu ala al-Ibad, uhakiki: Sayyid Kadhim Musawi, Qom, Dalile Ma, chapa ya 1, 1430 H / 2009 M.