Pete

Kutoka wikishia
Pete ya fedha yenye vito vya carnelian

Pete (Kiarabu: خاتَم) ni kitu cha duara cha chuma chenye kito, ambacho, kwa mujibu wa hadithi, ni moja ya sunna za Mtume (s.a.w.w). Katika Fiqhi kumebainishwa sheria na hukumu za pete. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na Imam Hassan Askary (a.s), kuvaa pete kwenye mkono wa kulia ni mojawapo ya dalili tano za kuwa muumini. Katika riwaya za Shia, kumependekezwa kuhusu aina ya pete na muundo juu yake na matumizi ya mawe ya thamani. Imepokewa kwamba maandishi kwenye pete za Maimamu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia yalikuwa ni maneno kama vile Al-Mulk Lilah na Hasbiallah. Mashia pia huchonga na kuandika maneno kama vile La Ilaha Illallah Muhammad Nabi Allah na Ali Wali Allah kwenye pete zao.

Pete ilikuwa ikitumika kupigia muhuri barua. Mtume (s.a.w.w) na wanachuoni wa Kishia nao wametumia njia na mbinu hii.

Nafasi na umuhimu

Katika kitabu cha Farahang Fiq’h Eslami (utamaduni wa sheria za Kiislamu), pete imearifishwa na kutambuliwa kama ni kitu cha duara. Ringi ambayo kawaida ni ya chuma na inajumuisha aina za vito na zisizo na vito, na ni maalumu kwa ajili ya kidole. [1] Katika baadhi ya hadithi inaelezwa kuwa, kuvaa pete mkono wa kulia ni katika sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w) [2] na ni katika alama za Mashia [3] na miongoni mwa alama za Muumini. [4]

Inaelezwa kuwa, kuvaa pete kwenye mkono wa kulia ni miongoni mwa alama ambazo Mashia wanatambulika nazo. [5] Maudhui ya pete imekuja katika milango mbalimbali ya fiq’h kama Sala, [6] Hija [7] na Jihad. [8]

Mifano ya Maimamu kuvaa pete mkononi

Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa katika vyanzo vya Shia [9] na Sunni [10], Imam Ali (a.s) alimzawadia mtu masikini pete yake akiwa amerukuu katika Sala. [11] Tukio hili linajulikana kama kuzawadia pete. Kadhalika kwa mujibu wa kile kilichokuja katika kitabu cha Luhuf cha Ibn Tawus (aliaga dunia 664 Hijiria), wakati Imamu Hussein (a.s) alipouawa shahidi alikuwa na pete na Bajdal bin Sulaym al-Kalbi mmoja wa askari wa jeshi la Omar bin Sa’ad akiwa na nia ya kupora pete hiyo alikata kidole cha Imamu Hussein. [12]

Katika riwaya moja, Imamu Kadhim (a.s) aliulizwa kuhusu sababu ya kuvaa pete Imamu Ali (a.s) kwenye mkono wa kulia ambapo alijibu kwa kusema: Kwa sababu Imam Ali (a.s) alikuwa kiongozi wa watu wa mkono wa kuume baada ya Mtume (s.a.w.w). [13]

Kupigia muhuri barua

Kupiga muhuri barua kwa kutumia pete inahesabiwa kuwa sunna na ada za Kiislamu. [14] Inasemekana kwamba mwishoni mwa mwaka wa 6 Hijiria Mtume (s.a.w.w) aliamuru kutengenezwa pete ili kupigia muhuri barua alizowaandikia wafalme wakubwa. [15] Kufanyia kazi sunna na ada ya kupiga muhuri barua kwa kutumia pete, kumenukuliwa pia na wanazuoni wa Kishia. [16] Ni kwa msingi huo, ndio maana inaitwa Khatam yaani muhuri. [17]

Aina na maandishi

Katika hadithi zilizonukuliwa na Waislamu wa madhehebu ya Kishia inaelezwa kuhusiana na aina ya pete na maandiko yake. [18]

  • Aina: Katika baadhi ya hadithi, aina ya pete ya Mtume (s.a.w.w) imetajwa kuwa ni ya fedh). [19] Katika Uislamu imeusiwa na kukokotezwa kuhusu kutumia baadhi ya mawe matukufu kama vile aqiq, [20] firuz, [21] yaqut [22] na zomrod. [23] Kadhalika katika kitabu cha Wasail al-Shiah zimenukuliwa hadithi zinazoonyesha juu ya kuwa duara na cheusi kito cha pete ya Mtume (s.a.w.w). [24]
  • Maandishi: Kuhusiana na mchoro wa maandishi juu ya pete, kuna hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu (a.s). [25] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) inaelezwa kuwa, pete ya Mtume (s.a.w.w) ilikuwa imeandikwa: Muhammad Rasullah, pete ya Imamu Ali (a.s) ilikuwa imeandikwa, al-Mulku Lillal na pete ya Imamu Baqir (a.s) ilikuwa imeandikwa al-Izzatu Lillah. [26] Pete ya Imamu Kadhim ilikuwa imeandikwa, Hasbiallah Hafidhi, [27] na Walmulku Lilalh Wahdahu. [28] Ibara ya: Muhammad Nabiullah na Aliyu Waliullah ni miongoni mwa ibara ambazo zimeusiwa kuandikwa na kuchongwa juu ya pete. [29] Pete zilizoandikwa namna hii zinapatikana miongoni mwa Mashia.

Hukumu

Katika milango mbalimbali ya fiq’h kuna sheria na hukumu zilizobainishwa kuhusiana na pete ambapo baadhi yazo ni:

  • Tohara: Baadhi ya mafakihi wanasema, ni makuruhu wakati wa kustanji (kusafisha sehemu ya haja ndogo na kubwa baada ya kujisaidia) [30] kuwa na pete ambayo imeandikwa jina la Mwenyezi Mungu au Aya miongoni mwa Aya za Qur’ani. [31] Muhammad Hassan Najafi, mwandishi wa kitabu cha Jawahir al-Kalam ameandika, majina ya Maimamu na jina la Bibi Fatima pia yana hukumu hii. [32]
  • Udhu: Wakati wa kutia udhu ni lazima maji yafike katika ngozi chini ya pete. Kwa muktadha huo ni mustahabu wakati wa kutia udhu kuitikisa pete ili maji yafike chini yake na kama maji hayafiki basi mtiaji udhu anapaswa kuvua pete. [33]
  • Sala: Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi, ni mustahabu kuvaa pete ya aqiq wakati wa kuswali. [34] Hata hivyo ni haramu kwa mwanaume kuswali akiwa amevaa pete ya dhahabu na Sala yake inabatilika. [35] Kadhalika ni makuruhu kwa wanaume na wanawake kuvaa pete ya chuma wakati wa Sala na nje ya Sala pia. [36] Baadhi ya mafakihi wanaamini kwamba, kusali na pete ya kupora (kughusubu) kunabatilisha Sala. [37]
  • Hija: Baadhi ya mafakihi katika mjadala wa utangulizi wa Hija, wanasema kuwa, kuvaa pete ya aqiq ya rangi ya njano ni katika mambo ya mustahabu ya safari ya kuelekea Hija. [38] Mtazamo wa Sayyid Abul-Qassim Khui, mmoja wa Marajii Taqlidi ni kuwa, kuvaa pete ya chuma kwa muhrim (aliyevaa vazi la ihramu) kama ni kwa ajili ya mapambo ni haramu, lakini kama sio kwa ajili ya mapambo inajuzu. [39] Kadhalika Imamu Khomeini anasema kwa mujibu wa Ihtiyat ya wajibu, kufanya Hija sambamba na kuvaa pete yenye najisi, kunabatilisha ibada hiyo. [40]
  • Jihadi: Pete inahesabiwa kuwa miongoni mwa salab. [41] Salab ni zile mali za aliyeuawa katika jihadi ambazo muuaji ana haki ya kuzimiliki na hazigawanyi kama ilivyo kwa ghanima. [42]
  • Ndoa: Kwa mujibu wa Muhaqqiq Bahrani, ni makuruhu kufanya tendo la ndoa hali ya kuwa mtu amevaa pete ambayo imeandikwa jina la Mwenyezi Mungu au Aya ya Qur'an. [43]
  • Mirathi: Pete inahesabiwa kuwa miongoni mwa hab'wah yaani mali na vitu maalumu vya baba ambavyo viko nje ya urithi na ambavyo hupatiwa mtoto mkubwa wa kiume kabla ya kuanza kugawanywa mirathi. [44]
  • Pete ya dhahabu: Mafakihi wa Kishia wanasema kuwa, ni haramu kwa wanaume kuvaa pete iliyotengenezwa kutokana na dhahabu. [45]

Pete ya Nabii Sulaiman (a.s)

Makala kuu: Pete ya Nabii Suleiman (a.s)

Katika hadithi kumezungumziwa pete ya Nabii Sulaiman (a.s) ambayo ilikuwa nembo ya nguvu na mamlaka yake. [46] Pete hii ilikuwa mikononi mwa Maimamu mmoja baada ya mwingine [47] na Imamu Mahdi (a.t.f.s) wakati atakapodhihiri itakuwa mkononi mwake. [48]

Vyanzo

  • ʿĀmilī, Sayyid Jawād. Miftāḥ al-karāma fī sharḥ qawāʿid al-ʿallāma. Edited by Muḥammad Bāqir Khāliṣī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1419 AH.
  • Baḥrānī, Yūsuf al-. Al-Ḥadāʾiq al-nāḍira fī aḥkām al-ʿitrat al-ṭāhira. Edited by Muḥammad Taqī Irawānī and Sayyid ʿAbd al-Razzāq al-Muqarram. Qom: Intishārāt-i Islāmī, 1405 AH.
  • Ḥaskānī, ʿUbayd Allāh b. ʿAbd Allāh al-. Shawāhid al-tanzīl li-qawāʿid al-tafḍīl. Edited by Muḥammad Bāqir Maḥmūdī. Tehran: Majmaʿ Iḥyāʾ al-Thiqāfat al-Islāmī, 1411 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Taḥrīr al-aḥkām al-sharʿiyya ʿalā madhhab al-imāmiyya. Edited by Ibrāhīm Bahādurī. Qom: Muʾassisat Imām al-Ṣādiq, 1420 AH.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Hidāyat al-umma ʾilā ahkām al-ʾaʾimma. Mashhad: Majmaʾ al-Buhūth al-Islāmiyya, 1412 AH.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Tafṣīl wasāʾil al-Shīʿa ilā taḥṣīl masā'il al-sharī'a. 1st Edition. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Al-Luhūf ʿalā qatlay al-ṭufūf. Tehran: Nashr-i Jahān, 1348 Sh.
  • Khoeī, Sayyid Abū l-Qāsim al-. Mawsūʿat al-Imām al-Khūʾī. First edition. Qom: Muʾassisa Ihyāʾ Āthar al-Imām al-Khūʾī, 1418 AH.
  • Khomeini, Sayyid Rūḥ Allāh. Taḥrīr al-wasīla. Qom: Dār al-ʿIlm, [n.d].
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Muʾassisat al-Wafāʾ, 1403 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Kitāb al-Mazār. Edited by Muḥammad Bāqir Abṭaḥī. Qom: 1413 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Masār al-Shīʿa fī tawārīkh al-sharīʿa. Edited by Mahdī Najaf. Qom: al-Muʾtamar al-ʿĀlamī li-Alfīyat al-Shaykh al-Mufīd, 1413 AH.
  • Najafī, Muḥammad al-Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāʾiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Ṣaffār, Muḥammad b. Ḥasan. Baṣāʾir al-darajāt fī faḍāʾil-i Āl-i Muḥammad. Edited by Muḥsin Kūchabāghī. Qom: Kitābkhāna-yi Āyat Allāh al-Marʿashī, 1404 AH.
  • Shāhrūdī, Sayyid Maḥmūd. Farhang-i fiqh muṭābiq bā madhhab-i Ahl al-Bayt. Qom: Muʾassisat Dāʾirat al-Maʿārif al-Fiqh al-Islāmī, 1385 Sh.
  • Sayyid Murtaḍā, 'Alī b. Ḥusayn. Al-Intiṣār fī infirādāt al-imāmīyya. 1st edition. Qom: Intishārāt-i Islāmī, 1415 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī Yazdī, Muḥammad Kāẓim al-. Al-ʿUrwat al-wuthqā fīmā taʿummu bih al-balwā. . Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1419 AH.
  • Ṭabrisī, Ḥasan b. al-Faḍl al-. Makārim al-akhlāq. Qom: al-Sharif al-Raḍī, 1412 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Mabsūṭ fī fiqh al-imāmīyya. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya li Iḥyāʾ al-Āthār al-Jaʿfarīyya, 1387 AH.
  • Zāriʿī, Muḥammad. Angushtarī dar Islām. Majalla-yi farhang-i kawthar, 32 (1387 SH).