Nenda kwa yaliyomo

Laylatul Qadr

Kutoka wikishia

Laylatul-Qadr au usiku wa cheo kitukufu (Kiarabu: ليلة القدر) ni usiku wa kushuka Qur'ani na kukadiriwa amali za watu kwa muda wa mwaka mmoja. Qur'ani Tukufu imezungumzia usiku huu katika Surat al-Qadr na Dukhan. Kwa mujibu wa Aya za Qur'ani na hadithi, usiku huu una thamani mno na bora kuliko miezi elfu moja. Usiku huu ndio wenye fadhila zaidi katika nyusiku za mwaka. Ni usiku wa rehma za Mwenyezi Mungu na kusamehewa madhambi. Katika usiku huu, Malaika huteremka ardhini na kwa mujibu wa baadhi ya hadithi zilizopekewa na Waislamu wa Madhehebu ya Shia, taqdir na makadiro ya mwaka ujao ya waja huoneshwa Imamu.

Haifahamiki hasa usiku huu ni upi, lakini kwa mujibu wa hadithi nyingi usiku huu unapatikana katika mwezi mtukufu wa Ramadhani; lakini kwa mujibu nyingi, kuna uwezekano mkubwa ukawa ni moja kati ya usiku wa tarehe 19, 21 na 23 katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanasisitiza zaidi katika usiku wa tarehe 23 Ramadhani, huku Waislamu wa Madhehebu ya Sunni wakitilia mkazo zaidi katika usiku wa tarehe 27 Ramadhani.

Waislamu wa Madhehebu ya Shia wakifuata sira na mwenendo wa Maasumina (a.s) hukesha katika nyusiku hizi wakisoma Qur'ani, dua na kufanya ibada. Kupigwa upanga Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na kufa kwake shahidi katika nyusiku hizi ni mambo ambayo yameongeza umuhimu wa nyusiku hizi kwa Waislamu wa Madhehebu ya Shia, kwani humuomboleza pia Imam Ali (a.s) katika masiku haya Laylatul-Qadr.

Kupewa Jina

«Qadr» ni neno la Kiarabu lenye maana ya kiwango, makadirio na (kuainisha) hatima. Kuhusiana na kuwa, kwa nini usiku huu umeitwa kwa jina la «Laylatu Qadr», kumetajwa hoja mbalimbali ambapo baadhi yake ni:

  • Kwa mujibu wa mtazamo wa baadhi akiwemo Allama Tabatabai, usiku huu umeitwa kuwa ni Laylatul-Qard kutokana na kuwa, katika usiku huu mambo ya wanadamu hukadiriwa kwa ajili ya mwaka mmoja ujao. Ayatullah Makarem Shirazi anaamini kuwa, mtazamo huu ni maarufu zaidi na bora zaidi na kwamba, unaoana na riwaya na hadithi.
  • Endapo mtu atakesha na kuhuisha usiku huu atapata makadario, hatima na daraja.
  • Sababu ya usiku huu kupewa jina la Qadr ni heshima na utuk ufu wa juu ulionao usiku huu.
  • Kwa sababu ni usiku ambao makadirio yaliyomo ndani ya Qur'ani huteremshwa.
  • Laylatul Qadr inajulikana kwa majina kama «Laylatu Adhamah» na «Laylat al-Sharaf».

Nafasi na Umuhimu

Laylatul Qadr ndio usiku bora zaidi, muhimu zaidi na wenye fadhila zaidi katika utamaduni wa Kiislamu. Kwa mujibu wa hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w), Laylatul Qadr ni katika adia na neema za Mwenyezi Mungu kwa Waislamu na hakuna umma katika umma zilizotangulia ambao ulipatiwa zawadi na ataa hii. Mwenyezi Mungu ameteremsha sura kamili katika Qur'ani Tukufu ya kusifu na kuelezea Laylatul Qadr na sura hiyo inafahamika kwa jina la Surat al-Qadr. Katika sura hii, usiku wa Laylatul Qadr umeelezwa kuwa ni bora kuliko miezi 1000. Aidha aya ya 1-6 za Surat Dukhan zinaeleza kuhusu umuhimu na matukio ya Laylatul Qadr ambapo baadhi ya Aya hizo zinasema: Naapa kwa Kitabu kinachobainisha. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima.

Imenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) kwamba, mwezi bora kabisa ni Ramadhani na moyo wa mwezi wa Ramadhani ni Laylatul Qadr. Aidha imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba, Laylatul Qadr ni Bwana wa nyusiku. Katika hadithi nyingine iliyonuukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) Laylatul Qadr imearifishwa kama Raas al-Sannah (mwanzo wa mwaka) , ambapo yumkini makusudio ni kuanza mwaka wa kimaanawi na kiibada na yawezekana madhumuni ni kufahamika makadirio ya mwaka mzima ya mwanadamu. Kwa mujibu wa vyanzo vya hadithi na fikihi, nyakati za mchana za masiku ya Laylatul-Qadr nazo zina fadhila na thamani kama ilivyo nyusiku zake. Kutokea matukio kama kuupigwa upanga Imam Ali (a.s) katika usiku wa 19 wa Ramadhan na kufa kwake shahidi usiku wa 21 katika mwezi huo mtukufu, ni mambo ambayo yanaongeza umuhimu wa nyusiku hizi kwa Waislamu wa Madhehebu ya Shia. Katika nyusiku hizi, mbali na wao kujihusisha na ibada za mustahabu ambazo ni maalumu na makhsusi kwa nyusiku hizi, hufanya maombolezo pia ya kumbukumbuka ya kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (a.s).

Imekuja katika baadhi ya hadithi kwamba, Fatma Zahra (a.s) ni siri ya Laylatul- Qadr. Kila ambaye atamfahamu Fatma (a.s) kwa ukamilifu, basi ataudiriki usiku wenye cheo kitukufu (Laylatul-Qadr).

Kushuka Qur'an

Aya ya kwanza ya Surat al-Qadr na Aya ya tatu katika Surat Dukhan inabainisha kushushwa Qur'ani katika usiku wenye cheo kitukufu (Laylatu-Qadr). Muhammad Abdu anaamini kwamba, kuanza kushuka hatua kwa hatua Qur'ani kulianza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hata hivyo wafasiri wengi (wa Qur'ani) wanaamini kuwa, katika usiku huuu Qur'ani Tukufu ilishushwa kwa mkupuo mmoja kutoka katika Lauhi Mahfudh (ubao uliohifadhiwa) na kuwekwa katika Beit al-Maamur (nyumba katika mbingu ya nne) au moyo wa Bwana Mtume (s.a.w.w), ambapo uteremshwaji huu wa Qur'ani unafahamika kama uteremshwaji wa mkupuo mmoja au uteremshwaji wa jumla wa Qur’ani.

Kukadiriwa Mambo

Imam Muhammad Baqir (a.s) anasema akitoa ufafanuzi wa Aya ya nne ya Surat Dukhan kwamba: Kila mwaka katika usiku huu (Laylatul Qadr) kila mwanadamu huandikiwa makadirio na hatima ya mambo yake ya mwaka ujao. Ni kwa msingi huo, ndio maana katika baadhi ya hadithi Laylatu Qadr imetajwa na kutambuliwa kama mwanzo wa mwaka. Allama Tabatabai anasema: Makusudio ya Qadr ni makadirio na kitu cha kupimia na kukadiria; na Mwenyezi Mungu katika usiku huu wenye cheo kitukufu huainisha hatima ya mambo kama ya maisha, kifo, riziki, saada na kadhalika. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi ni kuwa, Wilaya na uongozi wa Imam Ali (a.s) na Ahlul-Bayt (a.s) wengine, nao umekadiriwa na kutiwa saini katika usiku huu.

Kusamehewa Dhambi

Vyanzo vya Kiislamu vinaeleza kuwa, Laylatul Qadr ni usiku maalumu wa rehma za Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi na kwamba, katika usiku huu, shetani hufungwa minyororo na kuburuzwa huku milango ya pepo ikifunguliwa kwa ajili ya waumini. Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ya kwamba amesema: Kila ambaye atakesha na kuhuisha usiku wenye cheo kitukufu (Laylatul Qadr), akawa ni muumini na akawa ni mwenye kuamini siku ya malipo, basi atasamehewa dhambi zake zote.

Kuteremka Malaika

Kwa mujibu wa Aya zilizoko katika Surat al-Qadr ni kwamba: Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo , na kwa mujibu wa baadhi ya hadithi ni kuwa, Malaika hao huteremka kwa Imam kwa ajili ya kuwasilisha makadirio ya mwaka ujao na hivyo kukabidhi kile ambacho Mwenyezi Mungu amekikadiria na kukiainisha. Kuhusiana na hili, Imam Muhammad Baqir (a.s) anasema: Katika usiku huu, Malaika hutuzunguka na kwa hilo, sisi hufahamu usiku huu wenye cheo kitukufu. Katika hadithi nyingine, Mashia wameusiwa kwamba, walitumie hili kama hoja ya kuthibitisha udharura wa Uimamu na kwamba, Madhebu ya Shia ni madhehebu ya haki; kwa msingi huo, katika kila zama lazima kuweko na Imamu Maasumu ili akabidhiwe na Malaika yale aliyoyakadiria na kuyaainisha Mwenyezi Mungu kwa kwa ajili ya waja wake kwa mwaka mmoja ujao.

Usiku wa Laylatul Qadr ni Lini?

Picha ya sherehe za Laylatul Qadr katika haram ya Imam Ridha (a.s)

Kuhusiana na kwamba, ni usiku upi ambao ndio Laylatul Qadr kati ya nyusiku za mwaka kuna mitazamo tofauti:

Mtazamo wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia

Wafasiri wa Qur’ani wa Kishia wakitumia hoja ya hali ya dhahiri ya Aya za Surat al-Qadr wanaamini kwamba, Laylatul Qadr siyo maalumu kwa usiku ambao Qur’ani ilishuka katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w), bali kila mwaka usiku huu hutokea na kujikariri. Kuna hadithi nyingi pia ambapo kwa mujibu wa itikadi ya baadhi zimefikia kiwango cha kuwa mutawatir (mapokezi yake yamekuwa mengi), jambo ambalo linaunga mkono hoja hii.

Pamoja na hayo, usiku huu haufahamiki hasa ni upi na katika hadithi na Qur’ani hakuna mahali ambapo imeelezwa bayana na wazi kwamba, Laylatul Qadr ni tarehe au usiku fulani. Lakini pamoja na hayo, kuna hadithi nyingi zinazosisitizwa kuwa, usiku huu unapatikana ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Allama Majlisi anasema kuwa, Laylatul Qadr kwa mujibu wa Maulamaa wa Imamiyyah ni moja kati ya siku tatu za usiku wa tarehe 19, 21 na 23 katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuna hadithi nyingi zinazoeleza hili. Sheikh Swaduq amesema: Walimu wetu wanakubaliana kwamba, Laylatul Qadr ni usiku wa tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mulla Fat’hllah Kashani ameandika katika kitabu chake cha Manhaj al-Swadiqin kwamba, kwa mujibu wa mtazamo wa wanazuoni na Maulamaa wengi wa Imamiyah Laylatul Qadr ni usiku wa tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Inaelezwa kuwa, kuna hadithi mbalimbali zilizonukuliwa ambazo zinaeleza kwamba, usiku wa tarehe 23 Ramadhani ndimo mnamopatikana Laylatul Qadr. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi katika usiku wa tarehe 19 Ramadhani hatima na makadirio huandikwa ambapo usiku wa tarehe 21 Ramadhani hufikiwa natija kamili na usiku wa tarehe 23 Ramadhani hutiwa saini na kuidhinishwa rasmi. Aidha usiku wa tarehe 27 Ramadhani na usiku wa tarehe 15 ya mwezi wa Shaaban, ni tarehe mbili ambazo kuna uwezekano wa kuweko Laylatul Qadr.

Laylatul Juhani ni Moja ya nyusiku ambazo kuna uwezekano ukawa ni Laylatul Qadr na kuna hadithi ambazo zimekokoteza na kutilia mkazo juu ya kukesha kwa ibada na kuhuisha ni usiku wa tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwa mujibu wa hadithi usiku huu umeondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Laylatul Juhna. Abdallah bin Bukeir amenukuu kutoka kwa Zurarah ambaye anasema: Nilimuuliza Imam Baqir au Imamu Swadiq (a.s) kuhusiana na nyusiku za mwezi mtukufu wa Ramadhani ambazo ndani yake ni mustahabu kufanya ghusli na josho naye akasema: Ni usiku wa tarehe 19, 21 na 23 na akasema: Usiku wa tarehe 23 Ramadhani ni Juhani na kisa chake ni kwamba, mtu mmoja aliyejuliakana kwa jina la Juhani (Abdallah bin Anis Ansari) alimwambia Bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba: Nyumba yangu iko mbali na Madina, hivyo nitajie usiku ambao ili nije huku. Mtume (s.a.w.w) akamwambia aje Madina katika usiku wa 23. Aidha kisa cha usiku wa Juhani kimeelezewa hivi katika hadithi kwamba: Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Abdallah bin Unais Ansari ambaye alikuwa ni mkazi wa Juhani alifika kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na kumwambia: Nyumba yangu iko mbali na Madina, na nina ngamia, kondoo na wajakazi, ningependa unijulishe usiku fulani ili katika usiku huo nije Madina na katika Masjdu an-Nabi kwa ajili ya kufanya ibada. Mtume (s.a.w.w) akamwambia amkaribe, kisha akamnong'oneza kitu masikioni, kisha baada ya hapo na kuendelea, Bwana yule akawa kila mwaka anakuja Madina katika usiku wa 23 wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kubakia usiku wote katika Masjdu al-Nabi akifanya ibada kisha asubuhi yake alikuwa akirejea alikotoka. Baada ya kushuhudiwa mazungumzo hayo na mwenendo wa Abdallah bin Unais Ansari katika usiku wa 23 wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, usiku huu ukapewa jina la Laylatul Juhani (usiku wa Juhani) na jina hilo likawa moja ya majina ya Laylatul-Qadr kiasi kwamba, masahaba na wafuasi wa Maimamu wakawa wakiuliza kuhusiana na Usiku wa Juhani. Abu Baswir anasema: Nilimuuliza Imam Swadiq (a.s): Roho yangu iwe fidia kwako! Hivi usiku wa 23 mwezi wa Ramadhani ni usiku wa Juhani? Imam akajibu kwa kusema: Inasemwa hivyo. Imam Swadiq akasema: Usiku wa tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni usiku wa Juhani ambapo kwa mujibu wa hekima ya Mwenyezi Mungu, kila jambo linafanyiwa tadibiri na kutenganishwa na katika usiku huo, balaa na vifo, umri, riziki na mambo ya Mwenyezi Mungu na kila ambacho Mola Muumba anataka kitokee katika mwaka mmoja ujao, huandikishwa; hivyo basi, hongera kwa mja ambaye anakesha na kuuhuisha usiku huu kwa kurukuu na kusujudu (kwa kufanya ibada).

Mtazamo wa Ahlu-Sunna

Masuni wengi wakitumia hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) wanaamini kuwa, Laylatul-Qadr inapatikana katika kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani. Allama Tabatabai anasema kuwa, ni mashuhuri baina ya Ahlu-Sunna kwamba, Laylatul-Qdr ni katika usiku wa tarehe 27 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Aidha baadhi ya Waislamu wa madhehebu ya Suni wanaamini kuwa, Laylatul Qadr ilikuwa ikijikariri kila mwaka katika zama za uhai wa Bwana Mtume tu; lakini baada ya hapo, hakuna tena kitu kinachoitwa Laylatul Qadr. Aidha kwa mujibu wa kauli ya wengine ni kuwa, Laylatul Qadr haipo katika usiku fulani maalumu, bali katika mwaka ni usiku usiofahamika. Kundi hili linaamini kuwa, usiku huu ulikuwa katika mwaka wa kubaathiwa na kupewa Utume Bwana Mtume (s.a.w.w) katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini katika miaka ya baada ya hapo yumkini ukawa katika miezi mingine.

Tofauti ya Majira na Kuainisha Usiku Wenye Cheo Kitukufu

ni usiku mmoja tu kati ya nyusiku za mwaka ndio ambao ni Laylatul Qadr. Lakini kutofautiana majira ya mataifa mbalimbali (kwa mfano Iran na Saudi Arabia) ni jambo ambalo hupelekea wakati wa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani uwe tofauti katika maeneo mbalimbali, na kwa mujibu wa hilo, bila shaka nyusiku za kuamkia tarehe 19, 21 na 23 katika mwezi wa Ramadhani nazo zitakuwa tofauti kwa mujibu wa sehemu moja na sehemu nyingine. Wanazuoni na mafaqihi (wabobezi wa elimu ya fiqih) wanasema kuhusiana na mgongano huu kwamba,, tofauti ya majira ya mataifa, siyo hoja ya kuweko nyusiku nyingi na tofauti za Laylatul Qadr na watu wa maeneo tofauti ya dunia wanapaswa kuainisha Laylatul-Qadr na nyakati nyingine takatifu kama Eidul-Fitr na Eidul Adh'ha kwa mujibu wa majira yao. Kwa mujibu wa Ayatullah Makarem ni kuwa, usiku ni kile kivuli cha nusu ya dunia kwenye nusu nyingine, na kivuli hiki hutembea pamoja na mzunguko wa dunia, na muda kamili huchukua masaa 24. Kwa hiyo, usiku wa Qadr unaweza kuwa ni mzunguko kamili wa mzunguko wa ardhi kujizunguka yenyewe; Inamaanisha kwamba, saa 24 za giza zinazofunika sehemu zote za dunia. Kwa hiyo Laylatul Qadr huanza kutoka eneo moja na kudumu kwa saa 24, na ardhi yote inadiriki Laylatul Qadr.

Sira ya Maasumina

Imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s) kwamba, Mtume (s.a.w.w) lilipokuwa likiwadia kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani alikuwa akikusanya tandiko lake na alikuwa akiondoka na kuelekea msikiti kwa ajili ya itikafu. Licha ya kuwa Msikiti wa Madina haukuwa na paa, lakini hakuwa akiondoka msikitini hapo hata wakati ambao mvua ilikuwa ikinyesha. Aidha imenukuliwa kwamba, katika nyusiku za Laylatul Qadr Mtume (s.a.w.w) alikuwa akibakia macho na alikuwa akiwamwagia maji usoni watu waliokuwa wakisinzia.

Mtindo wa Fatma (a.s) ulikuwa huu kwamba, katika nyusiku za Laylatul Qadr alikuwa akifanya ibada mpaka asubuhi na alikuwa akiwataka watoto na familia yake nao wabakie macho kwa ajili ya kufanya ibada; na alikuwa akilitatua tatizo lao la usingizi kwa kuwapa chakula kidogo na kuwalaza mchana. Maasumina (a.s) hawakuwa wakiacha suala la kuhudhuria msikiti na kukesha wakifanya ibada. Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ni kuwa, alikuwa mgonjwa sana katika moja ya nyusiku za Laylatul Qadr, lakini pamoja na hayo aliwataka watu wake wa karibu wampeleke msikitini ili akafanyie ibada huko.

Rejea

Vyanzo

  • Qur'ani Tukufu
  • Ibn al-Miftah, Abdallah, Sharh al-Azhar, al-Hijaz, Cairo, Bita.
  • Iftikhari, Sayyid Ataullah," Du ava Shabe Qadr az Manzar Mussa Sadr" Dar Majale Ulum Qur'ani va Hadis, Namba 3, 1389 Hijria Shamsia.
  • Al-Qassimi, Muhammad Jamal al-Din, Tafsir al-Qassimi, Beirut, Bita.
  • JuwAizi, Ali bin Jum'a, Tafsir Nur al-Thaqalein, Qum. Ismailiyan, 1415 Hijria.
  • Shakir, Abu al-Qassim " Shabi Bartar az Hizar Mah" dar Majaleh Morabiyan, Toleo namba 360, 1389 Hijria Shamsia.
  • Sheikh Swaduq, Muhammad bin Ali, al-Khiswal, msahihishaji, Ali Akbar Ghiffari, Qum, Jamiat Modaressin, 1379 Hijria Shamsia.
  • Sheikh Swaduq, Muhammad bin Ali, Maani al-Akhbar, Qum, Taasisi ya Entisharat Eslami, yenye mfungamano na Jamiat Modaresin, 1379 Hijria Shamsia.
  • Sheikh Swaduq, Muhammad bin Ali, Man Laa Yahdhuruh al-Faqih, mhakiki na msahihishaji Ali Akbar Ghiffari, Qum, Taasisi ya Entisharat Eslami, Chapa ya Pili, 1413 Hijria.
  • Sheikh Tusi, Muhammad bin Hassan, al-Tahdhib, Tehran, Darul Kutub al-Islamiyah, 1365 Hijria Shamsia.