Futari

Kutoka wikishia
Makala hii ni kuhusiana na ada na sunna ya futari pamoja na vyakula vinavyoliwa wakati wa kufuturu. Ili kujua kuhusiana na adabu na hukumu za kufuturu, angalia makala ya kufuturu.
Karamu ya futari katika haram tukufu ya Imam Ridha (a.s)

Futari (Kiarabu: مائدة الإفطار) ni mlo wa kwanza unaoliwa na mtu aliyefunga Saumu au ni mlo ambao mtu anautumia kufungulia Saumu yake. Kwa mujibu wa hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Ahlul-Bayt (a.s), ujira wa kufuturisha ni sawa na ujira wa kufunga Saumu na hilo limetiliwa mkazo sana. Kufuturisha ni moja ya ada na utamaduni wa Waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wana ada na utamaduni maalumu wa kufuturisha kulingana na tofauti ya mataifa na nchi zao.

Fadhila

Futari ni mlo wa kwanza unaoliwa na mtu aliyefunga Saumu au ni mlo ambao mtu anautumia kufungulia Saumu yake. Kwa mujibu wa riwaya na hadithi mbalimbali kufuturisha kuna fadhila nyingi sana. [1] Miongoni mwa hadithi zinazongumzia fadhila za kufuturisha ni ile iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ambayo inasema: Ujira na malipo ya mtu anayefuturisha ni sawa na ujira wa kufunga Saumu. [2] Kadhalika Mtume (s.a.w.w) katika hadithi ambayo ni mashuhuri kwa jina la Khutba ya Shaabaniyah, ameeleza kuwa, thawabu za malipo ya kumfuturisha muumini aliyefunga ni sawa na thawabu za kumuachilia huru mtumwa na huwa sababu ya kufutiwa madhambi. [3]

Vitanga vya Futari

Kufuturisha ni katika ada na tamaduni za Waislamu ambazo hufanyika katika nchi mbalimbali kwa ada na mila tofauti. Katika nchi za Kiislamu watawala na wananchi tangu kale walikuwa wakiandaa na kutandika vitanga vya chakula kwa ajili ya kufuturisha. [4] Katika zama za utawala wa Fatimiyah (297-567 Hijiria) nchini Misri kulikuweko na sehemu maalumu ambamo ndani yake watu walikuwa wakigaiwa futari wakati wa kufuturu unapowadia. [5]

Katika zama za Aali-Bueih au Buuiyan (322-448) kulikuwa na mialiko ya futari katika mwezi wa Ramadhani huko Baghdad, Iraq ambapo zaidi ya watu 1000 walikuwa wakihudhuria. [6] Ibn Battuta mtalii wa karne ya 7 Hijria katika safari yake huko Damascus Syria anawataja watawala, viongozi, makadhi na shakhsia wakubwa ambao walikuwa wakialika kundi kubwa la watu kwa ajili ya futari, kiasi kwamba, hakuna mtu ambaye katika mwezi wa Ramadhani alikuwa akifuturu peke yake. [7] Kadhalika ada na mazoea ya kufutirisha ilikuwa imeenea katika zama za utawala wa Safawi [8] na Qajar nchini Iran. Kwa mujibu wa Abdallah Mustawfi, katika zama za utawala wa Qajar akthari ya watu matajiri na wenye cheo kikubwa walikuwa wakifuturisha watu. [9]

Futari ya Kawaida

Katika kipindi cha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran pia kumekuwa kukiandaliwa vitanga vya futari za kawaida (isiyo na mambo mengi) katika maeneo matakatifu kama Haram ya Imamu Ridha (a.s) na katika Haram ya Bibi Fatma Maasuma na katika baadhi ya misikiti. [10] Kadhalika katika maeneo ya kidini katika nchi nyingine kama katika Haram za Imamu Ali na Imamu Hussein (a.s) nchini Iraq, [11] katika msikiti mtakatifu wa Makka na msikiti wa Mtume mjini Madina nchini Saudi Arabia [12] pia hutandikwa vitanga vya futari za kawaida. Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa maagizo na kutilia mkazo juu ya kuandaliwa vitanga vya futari za kawaida (zisizo na aina kwa aina ya vyaku na zisizo na isirafu). [13]

Vyakula Vilivyozoeleka

Kwa mujibu wa hadithi ni mustahabu kufuturu kwa tende na maji ya vuguvugu [14] na inaaminika kuwa, kufuturu kwa tende kuna thawabu nyingi. [15]

Vyakula vya kufuturia viko vya aina mbalimbali kulingana na mataifa na mila za watu. Hata hivyo vyakula vilivyozoeleka kwa ajili ya futari ni: Tende, mkate, maziwa, maji ya moto, aina za halwa, jelebi, mandazi, chai, uji na kadhalika. Ikumbukwe kuwa baadhi ya vyakula vya kufuturia huenda vikawa mashuhuri taifa fulani lakini katika baadhi ya mataifa vikawa havifahamiki kabisa. [17]

Kwa upande wa Afrika Mashariki hasa katika jamii ya Waswahili baadhi ya vyakula na milo mashuhuri ya kufuturia ni: Tende, maziwa, maji, chai, uji, juisi ya asili, ndizi zilizoiva na kupikwa, magimbi, maboga, viazi vitamu, maharage na mihogo.

Masuala Yanayo Fungamana

Rejea

Vyanzo