Shetani

Kutoka wikishia

Shetani (Kiarabu: شيطان) ni jina la kila kiumbe mwovu na muasi. Shetani (au Iblisi) kama nomino maalum, ni jina la kiumbe ambaye hakumsujudia Adamu jambo ambalo lilimsababishia kufukuzwa kutoka katika Pepo ya Mungu. Kuna khitilafu kati ya wasomi juu ya asili ya Shetani, lakini wafasiri wengi wa Qur'an wanamchukulia kuwa ni kiumbe anaye tokana na majini.

Neno Shetani likiwa katika hali ya witiri na wingi wake, limetumika mara 88 katika Qur'an, ambapo mara nyingi kati yazo linammaanisha Ibilisi mkuu (Shetani aliye kataa kumsujudia Adamu). Kwa mujibu wa Aya za Qur'an, Shet'ani alikataa kutii amri ya Mwenyezi Mungu ya kumsujudia Adamu, na akafukuzwa kutoka katika nafasi na mahali alipokuwapo. Baada ya yeye kufanya kosa hili alimwomba Mwenye Ezi Mungu ampe muhula mpaka Siku ya Kiyama. Na Mwenye Ezi Mungu akampa muhula mpaka siku maalumu. Katika Aya kadhaa za Qur'an, Mwenye Ezi Mungu amemjulisha na kumtahadharisha mwanadamu juu ya hatari kubwa ya Shetani, na kumtaka ajihadhari na wasiwasi wa Shetani ili asije mhadaa na kumtoa nje ya ibada na utumwa (uja) wa Mola wake.

Katika Hadithi, kuna mada mbalimbali zilizo jadiliwa kuhusiana na Shetani, ikiwa ni pamoja na visa vya Shetani na baadhi ya Manabii na Maimamu, njia za kumuepuka shetani, wasifu na sifa maalumu za Shetani. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, Shetani anaweza tu kuwajaribu na kuwashawishi watu kutenda dhambi, na wala yeye hana nguvu juu ya mwanadamu zaidi ya kumshajiisha kutenda dhambi, na kwamba hana mamlaka yoyote yale ya kumlazimisha mwanadamu kutenda dhambi. La mwisho ni kwamba; hatima ya Shetani na wafuasi wake ni kuishia motoni.

Nafasi na umuhimu wake

Katika utamaduni wa Kiislamu, Shetani ni nomino ya kawaida na ya kiujumla inayo ashiria kiumbe yeyote yule mpotoshaji na mwasi dhidi ya Mwenye Ezi Mungu, ambaye anaweza kuwa ni miongoni mwa wanadamu au majini. Qur'an imemwarifisha Shetani kuwa ni adui wa daima kwa mwanadamu mwenye kujitahidi mno katika kwapotosha wanadamu. [1] Neno shetani linapatikana mara 88 mara katika Quran; kati yake mara 70 kwa namna ya umoja (yaani Shetani), na mara 18 mara kwa namna ya wingi, yaani mashetani. [2] Allamah Majlisi katika kitabu chake kiitwacho Bihar al-Anwar, anasimulia Riwaya 177 kutoka kwa Maasumina zinazohusiana na Shetani (Ibilisi).

Ayatollah Jawadi Amuli mwanafalsafa wa Kiislamu amesema: “Sisi na adui aitwaye Shetani; ambaye hana suluhu na mtu, na hatuachii mpaka atufanye watumwa wake. Katika vita, wakati mwingine mtu hushinda, na wakati mwingine anashindwa, na pia huenda wakati mwingine akakamatwa kama mateka. Wanazuoni wa fani ya maadili wamesema kuwa; hata katika vita ndani -vilivyopo baina ya mtu na nafsi yake-, wakati mwingine mtu anakufa shahidi katika mapambano bina yake na nafsi yake. Yaani mtu huyu hadi mwisho wa maisha yake, hubakia na mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s), na katu hang’oi nanga na kuondoka kwenye mkondo wa mapenzi yao. Kwa mujibu wa masimulizi ya Hadithi, kama mtu atakufa kitandani mwake hali akiwa na upendo wa Ahll-Bayt (a.s), atakuwa amekufa shahidi, kwa sababu amekufa katika uwanja wa Jihadu al-Akbar (jihadi kuu) na hakujisalimisha ndani ya uwanja huo. Wakati mwingine mtu huchukuliwa mateka katika uwanja wa Jihadu al-Akbar na huondoka na mateka uwanjani humo, na Shetani husalimu amri mikononi mwake. Ila wakati mwingine Mungu aepushe mbali, yeye hugeuka mateka wa Shetani na kuondoka na pingu za Shetani mikononi mwake.

Kwa mujibu wa tafsiri ya al-Mizan ya Ayatullahi Tabatabai ni kwamba; Uwepo wa Ibilisi, ambaye humhimiza mwanadamu kutenda mabaya na kufanya dhambi, ni mojawapo ya nguzo za uwepo wetu ambazo zinaonyesha hiari ya mwanadamu na safari yake katika njia ya ukamilifu. [3] Uwanja wa Ibilisi unachukuliwa kama ni uwanja wa akisiko la uhuru wa chaguo la mwanadamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, Ibilisi anaweza tu kumshawishi mwanadamu na kumhadaa ili atende dhambi. Kwa hivyo, Shetani hana mamlaka wala nguvu zozote zile juu ya mwanadamu zaidi ya kumhimiza kutenda dhambi. [4]

Uhusiano wa shetani na ibilisi

Neno “Shetani” pia lilihusishwa na Iblisi katika matumizi yake ndani msamiati wa vyanzo vya Kiislamu, Shetani ambaye alikataa kumsujudia Adamu katika tukio la kuumbwa kwake, na badala yake akadhamiria kuwapotosha wanadamu. [5] Zaidi ya hayo, neno “Shetani” pia limeonekana kutumika katika Aya nyingine za Qur'an, ikiwemo Aya ya 36 ya Suratu al-Baqara likimaanisha Iblisi. Pia katika aya ya 121 ya Suratu al-An’aam, nomino hii imetumika kwa ajili ya kuashiria askari na wafuasi wa Iblisi. [6] Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tabataba'a kuhusu matumizi ya nomino ya “Shetani” katika maneno ya Qur'an na wafasiri wake, ni dhahiri kwamba; mara nyingi kabisa nomino ya “Shetani” imetumika kwa maana sawa na nomino ya Ibilisi, au kwa uchache tunaweza kusema; nomino hiyo imetuka ikimuashiria Ibilisi kama ni mfano hai wa Mashetani. [7] Wengine pia wamesema kwamba neno “Shetani” hutumiwa zaidi kama kisawe cha Ibilisi, [8] na kwa kutokana na ueneaji uliosambaa zaidi katika maana hii, nomino hii imegeuka kuwa ni kama nomino kuu na maalimu kwa Ibilisi. [9]

Mashetani wa kijini na kibinadamu

Kulingana na maandiko ya Kiislamu kama vile Quran na Hadithi; Ni muhimu kuelewa kuwa shetani hana asili maalum, bali ni kiumbe mwenye uwezo wa kudanganya na kuwapotosha watu. Shetani anaweza kuwa miongoni mwa majini, kama vile Iblisi na uzao wake, au hata kutoka kwa wanadamu wenyewe. Mfasiri maarufu Allahah Tabatabai ameeleza katika tafsiri yake ya juu kipengele kisemacho ((مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ )) "miongoni mwa majini na watu", kuwa sentensi hii inalenga (الخنَّاسِ) "waharibifu" ambao ni washirika wa mashetani. Hii inaonyesha kuwa baadhi ya watu, ambao ni binadamu, wanaweza kuwa washirika wa mashetani na kuwa sehemu ya kundi lao. Hii pia inathibitishwa na Aya ya 12 ya Surat al-An'aam inayo zungumzia juu ya uwepo wa ((شَياطِينَ الْإِنْسِ وَالْجِنِّ)) "mashetani wa kibinadamu na majini". [10]

Wasifu wa Shetani

Katika aya nyingi za Qur'an, Shetani anaonyeshwa kama adui wa wazi na wa kutisha wa ubinadamu, [11] ambaye humpotosha na kumnyang'anya mtu hadhi yake wazi wazi (مُضِلٌ مُبین), [12] na kumwacha katika mazingira magumu na ya kidhalili wakati wa uhitaji. [13] Anawashawishi watu kwa ahadi za uwongo, huwafanya tamaa zao, [14] na kuwavuta kuelekea makaazi ya laana ya milele (makaazi ya Jahannam). [15] Aidha, katika Qur'an, Shetani na wafuasi wake wametajwa kama ni; makafiri (wasio na shukurani), [16] waasi, [17] wenye kiburi, [18] wapotovu, [19] warafiki waovu, [20] fitina na wadanganyifu. [21] Hatima ya mashetani pamoja na wafwasi wao ni kuteseka katika moto wa Jahannam na kughadhabikiwa na Mola wao. [22]

Njia za Shetani katika kuhadaa wanadamu

Miongoni mwa njia na mbinu za Shetani za kupotosha wanadamu zilizotajwa ndani ya Qur'an Tukufu, ni pamoja na; kujenga uadui, [23] kuzuia kumkumbuka Mwenye Ezi Mungu, hasa katika sala, [24] na kutishia umaskini na dhiki nyingine za kidunia. [25] Kupamba dhambi na kuvutia mawazo yanayo pelekea vitendo vya batili, [26] kusisitiza mapenzi ya kushikamana na mambo ya kidunia na kujiunga na ushawishi wa mapenzi ya wanawake, watoto, na mali, [27] kuamsha tamaa-ongo ya kudhani kuwa na maisha marefu, [28] kueneza ufisadi na kukuza ukahaba na maasi, [29] ni njia zingine za Shetani za kupotosha wanadamu kama ilivyotajwa na Qur'an Tukufu.

Katika Aya za Qur'an Tukufu, ushawishi wa Shetani unaelezewa kuwa ni mdogo na dhaifu. [30] Katu mashetani hawawezi kufahamu mambo ya ghaibu na yaliyofichika, na wala hawawezi kupata habari za mbinguni.[31] Ikiwa mtu yuko kwenye njia ya utumwa wa Mungu, basi kamwe mashetani hawatakuwa na mamlaka juu yake; na udhibiti wao pekee uko juu ya wale wanaofuata mashetani. [32] Allamah Tabatabai pamoja na Makarim Shirazi, wanaamini kwamba; Shetani anaweza kujibadilisha katika maumbile tofauti, isipokuwa umbo la Manabii na warithi wao (Maimamu). [33]

Njia za kukabiliana na shetani

Kulingana na Hadithi zilizo nukuliwa na Allamah Majlisi katika kitabu chake kiitwacho Bihar al-Anwar kutoka kwa Maimamu watakatifu ni kwamba; kumtaja Mungu na kusema kwa kusema الرحمن الرحیم بسم الله (kwa jina la Mwenye Ezi Mungu…), mwanzoni mwa kila tendo vile: kula, [34] kusafiri na kutoka nje ya nyumba, [35] kutawadha, [36] kusala, [37] na kuingiliana na mke [38] ni njia ya kuepukana na Shetani.

Sababu juu kuumbwa kwa Shetani na kupewa nguvu

Wafasiri wa Kiislamu wametoa majibu kadhaa kuhusu kwa nini shetani aliumbwa na kwa nini ana nguvu ya kuwapotosha waja. [39]

Kulingana na maelezo ya Qur’an, ikiwa tunamaanisha shetani kama Ibilisi, baada ya kufukuzwa kutoka kwenye ufalme wa Mwenye Ezi Mungu kwa sababu ya kukataa amri ya kumsujudiu Adamu, Shetani alimwomba Mwenye Ezi Mungu ampe muda wa kuishi hadi siku ya Kiyama, lakini Mwenye Ezi Mungu alimpa muda hadi siku maalumu, ambayo iko kabla ya Siku ya Kiyama. [40] Kwa hivyo Mwenye Ezi Mungu kiasili, hakumuumba shetani akiwa kiumbe mbaya, kwani yeye alimwabudu Mwenye Ezi Mungu kwa miaka elfu sita, alikuwa pamoja na malaika na pamoja wamwabudio Mungu. Lakini kwa sababu ya jeuri yake mbele ya Mungu, alifuata njia ya uasi na akatoka katika rehema ya Mungu. [41] Kwa maoni ya Ayatullah Tabatabai katika tafsiri yake iitwayo al-Mizan, uwepo wa Ibilisi sio uovu halisi, lakini uovu uliochanganyika na wema. [42]

Ibilisi ni nyenzo na mizani ya kuwapima wanadamu

Kwa mujibu wa mazingatio yaliyomo ndani ya Qur’an; Uwepo wa Shetani una malengo na dhamira ya kuwatahini wanadamu. [43] Mwenye Ezi Mungu, hadaa za Shetani na ndoana zake ameziweka ziwe ni mitihani kwa wenye kutu na maradhi ya nyoyo. [44]

Masuala yanayo fungamana

Vyanzo

  • ʿAskarī, Insīyya. Maʿnāshināsī-yi nuwīn az wāja-yi shayṭān. Qabasāt No 64. Winter 1389 Sh.
  • Bayḍāwī, ʿAbd Allāh b. ʿUmar. Anwār al-tanzīl wa asrār al-taʾwīl. 1st edition. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. al-ʿUmar al-. Mafātīḥ al-ghayb or al-Tafsīr al-Kabīr. 11th edition. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1411 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1375 Sh.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣāliḥ. Beirut: Dār al-Kitāb al-Lubnānī, 1980.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʾ al-bayān ʿan taʾwīl āyāt al-Qurʾān. Edited by Jamīl al-ʿAṭṭār Ṣidqī. Beirut: Dār al-Fikr, 1415 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān f