Aya ya Saumu

Kutoka wikishia
Faili:Baqara 183.jpg
Aya ya Saumu

Aya ya Saumu (Kiarabu: آية الصوم) (Surat al-Baqarah:183) inaashiria wajibu wa Saumu kwa waumini. Wafasiri wa Qur’an wanaamini kwamba, wajibu wa Saumu sio mahususi na maalumu kwa waumini tu, bali wajibu huu unawajumuisha watu wote ambao wameukubali Uislamu hata kama hawatakuwa na imani thabiti na imara. Katika Aya kumeashiriwa pia kuwajibishwa funga ya Saumu kabla ya kuja sheria za Kiislamu kama ambavyo taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu kumetambulishwa kuwa ni miongoni mwa faida za Saumu.

Andiko la Aya na Tarjumi Yake

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ


Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuwa na takua (uchajimungu).



(Quran: 2: 183)


Wajibu wa Saumu kwa waumini

Aya ya 183 ya Surat al-Baqarah inazungumzia wajibu wa Saumu ikiwa moja ya maagizo na maamrisho ya sheria za Kiislamu. Kwa mujibu wa Abu Hayyan Andalusi (aliyefariki 745 Hijiria) katika tafsiri ya Bahr al-Muhit ni kwamba, Aya za kabla za Surat al-Baqarah zimefaradhisha nguzo tatu za Uislamu (imani, Sala na Zaka) na katika Aya hii kumebainisha nguzo ya nne yaani Saumu.[1] Allama Tabatabai anaamini kwamba, Aya hii na Aya mbili zinazofuata zimekuja na sheria ya Saumu na kuifaradhisha funga hii katika mwezi wa Ramadhani.[2]

Wajibu wa Saumu sio Mahususi kwa Waumini tu

Wafasiri wa Qur’an Tukufu hawaoni kama wajibu wa Saumu katika Aya hii ni makhsusi kwa waumini tu; bali unawajumuisha pia watu wote ambao wameikubali dini ya Uislamu, hata kama hawatakuwa na imani imara na madhubuti.[3] Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) inaeleza kuwa, hukumu hii inajumuisha watu wote waliopotea, wanafiki na kila mtu ambaye amekubali Uislamu.[4] Allama Tabatabai anasema kuwa, kutumika ibara ya “Enyi mlioamini” katika Aya hii ni kuwafanya watu wazingatie sifa ya imani yao ili wakubali hukumu na sheria ambazo zinatoka kwa Mola wao.[5]

Ayatullah Makarim Shirazi anasema kuwa, kwa kuzingatia kuwa funga ya saumu ina mashaka na ugumu, katika Aya hii kumetumika ibara ambazo zinaandaa roho ya mwanadamu kwa ajili ya kuipokea na kuikubali na ni kwa msingi huo ndio maana Imamu Sadiq (a.s) anasema: Ladha ya kuhutubiwa kwa neno “Enyi mlioamini” iko kwa namna ambayo inaondoa ugumu wa ibada hii.[6]

Kufaradhishwa Saumu Katika Sheria za Kabla ya Uislamu

Wajibu wa Saumu kwa wafuasi wa sheria za kabla ya Uislamu pia umebainishwa na kuwekwa wazi. Kwa maana ya kwamba, Saumu ilikuwa wajibu na faradhi pia kwa umma zilizotangulia kabla ya kuja dini ya Uislamu. Hii kwamba, makusudio ya wafuasi wa sheria za kabla ya Uislamu ni akina nani na Saumu ilikuwa kwa namna gani kwao, kuna kauli mbalimbali. Sheikh Tusi anaashiria kauli tatu: Baadhi wamesema, Saumu iliwajibishwa kwao kama ilivyo Saumu ya Waislamu. Baadhi ya wengine wanaamini kuwa, makusudio ya umma wa kabla ni manasara ambao waliwajibishiwa pia Saumu ya Ramadhani. Kuna wengine pia wamezungumzia suala la tofauti ya muda wa Saumu baina ya Waislamu na umma za kabla.[7]

Allama Muhammad Hussein Tabatabai haoni kama Aya hii iko katika kubainisha namna ya Saumu katika sheria za kabla ya Uislamu na kwa watu ambao Saumu imefanywa kuwa wajibu kwao; bali mtazamo wake ni kwamba, Aya hii inaashiria wajibu wa Saumu kwa ajili ya wafuasi wa sheria za kabla ya Uislamu na kuziandaa fikra na akili za Waislamu kwa ajili ya kuikubali sheria ya Saumu na kutoiona kuwa ni ngumu.[8] Anaendelea kusema: Wajibu wa Saumu haupatikana katika Torati na Injili zilizopo licha ya kuwa katika vitabu hivi Saumu imesifiwa, na baadhi ya Mayahudi na Wakristo wanafunga Saumu kwa nama ambayo ni tofauti na Saumu ya Waislamu. Mwisho, Allama Tabatabi anaashiria kisa cha Saumu ya Nabii Zakaria (a.s) na Saumu ya Bibi Maryam mama yake Nabii Issa (a.s) katika Qur’an Tukufu ambayo inatofautiana na Saumu ya Waislamu.[9]

Falsafa ya Saumu

Allama Tabatabai anaamini kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur’an Tukufu athari za kutii na kuasi zinamrejea mwanadamu mwenyewe na kuhusiana na Saumu pia kubebainishwa athari za Saumu kwamba, zinarejea wapi. Hilo linabainishwa katika sehemu ya mwisho ya Aya ya Saumu ambayo ni: “ili mpate kuwa na taqwa (uchajimungu).” Anaamini kwamba, Saumu ni nyenzo muhimu na athirifu kwa ajili ya kulea taqwa na uchajimungu.[10]

Rejea

  1. Abu Hayyan Andalusi, al-Bahr al-Muhīth, juz. 2, uk. 177.
  2. Tabataba'i, al-Mīzān, juz. 2, uk. 5.
  3. Shiekh Tusi, at-Tibyān, juz. 2, uk. 115; Tabrasi, Majma' al-Bayān, juz. 2, uk. 490; Bahrani, al-Burhān, juz. 1, uk. 385.
  4. Ayyashi, Tafsīr al-'Ayyāshī, juz. 1, uk. 78.
  5. Tabataba'i, al-Mīzān, juz. 2, uk. 6.
  6. Makarim Shirazi, Tafsir-e Nemune, juz. 1, uk. 624.
  7. Sheikh Tusi, at-Tibyān, juz. 2, uk. 115.
  8. Tabataba'i, al-Mīzān, juz. 2, uk. 5.
  9. Tabataba'i, al-Mīzān, juz. 2, uk. 7.
  10. Makarim Shirazi, Tafsir-e Nemune, juz. 1, uk. 623-624.

Vyanzo

  • Abu Hayyan Andalusi, Muhammad bin Yusuf, Al-Bahr al-Muhīth Fī at-Tafsīr, Beirut, Dar al-Fikr, 1420 H.
  • Ayyashi, Muhammad bin Mas'ud, Tafsīr Ayyāshī, Tehran, Percetakan al-'Ilmiyyah, 1380 HS/2001.
  • Bahrani, Sayyid Hashim, Al-Burhān Fī Tafsīr al-Qur'ān, Tehran, Bunyad-e Be'sat, 1416 H.
  • Makarim Shirazi, Nashir, Tafsir-e Nemune, Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, 1374 HS/1995.
  • Shiekh Thusi, Muhammad bin Hassan, At-Tibyān Fī Tafsīr al-Qur'ān, Beirut, Dar Ihya' at-Turats al-'Arabi.
  • Tabataba'i, Sayyid Muhammad Hussein, Al-Mīzān Fī Tafsīr al-Qur'ān, Qom, Jame'e-e Mudarrisin-e Hauze-e Ilmiyyee-e Qom, 1417 H.
  • Tabrasi, Fadhl bin Hassan, Majma' al-Bayān FīTafsīr al-Qur'ān, Tehran, Entesyarat-e Nashir Khusru, 1372 HS/1993.