Nenda kwa yaliyomo

Itikafu

Kutoka wikishia
Itikafu
Itikafu katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran
Itikafu katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran
Maelezo ya Picha1Waislamu Wakiwa Kwenye Itikafu
Wakati wa KufanyikaHaina Muda Maalumu
Mahali pa KufanyikaMsikitini
Asili KihistoriaKuanzia Kipindi cha Mtume (s.a.w.w)


Itikafu (Kiarabu: الاعتكاف) ni kukaa na kubakia msikitini kwa muda maalumu (kwa uchache siku tatu) sambamba na kufunga Saumu. Ibada ya itikafu haina wakati maalumu, lakini katika hadithi mbalimbali imeelezwa kuwa, kipindi bora kabisa cha kukaa itikafu ni kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kuna hukumu na adabu mbalimbali kuhusiana na itikafu, namna ya kubakia msikitini na kutotoka na kadhalika.

Nchini Iran ibada ya itikafu hufanyika katika masiku meupe (tarehe 13, 14 na 15) katika mwezi wa Rajab katika misikiti mikubwa katika miji mingi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, itikafu ni kama ilivyo Hija na Umra ambapo inapelekea kusamehewa madhambi na kuokolewa na moto wa jahanamu.

Umuhimu na Fadhila Zake

Itikafu ni ibada ambayo ni mustahabu ambapo katika hadithi za Maasumina imetambuliwa kuwa iko sawa na Hija na Umra. [1] Ibada ya itikafu hufanyika katika nchi za Kiislamu ikitambuliwa kuwa ni Sunna ya Bwana Mtume (s.a.w.w).

Utambuzi wa Maana

Katika Fiqhi, kubakia msikiti kwa muda wa siku tatu au zaidi kwa nia ya kujikuribisha kwa Mwenyezi Mungu na kufanya amali na kuchunga masharti maalumu kunafahamika kama itikafu na mtu ambaye anafanya ibada hii anajulikana kama Mu'takif (mfanya itikafu). [2] Itikafu imetokana na neno a-k-f (akafa) na katika lugha ina maana ya kukipokea au kukizingatia kitu na kukithamini. [3] Kadhalika katika Qur'an Aakif [4] ina maana ya mkaaji, mkazi na Ma'kuf [5] imetumika kwa maana ya marufuku na kushikiliwa (kizuini).

Itikafu katika Mtazamo wa Maurafaa

Itikafu katika istilahi ya kiirfani, maana yake ni kufanya moyo kuachana na mambo ya dunia na kuisalimisha nafsi kwa Mwenyezi Mungu. [6] Allama Majlisi anasema kuwa, hakika ya itikafu ni mja kujikabidhi na kuwa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu, kufungamana na kujichunga. [7] Kadhalika anasema, ukamilifu wake ni kuufanya wakfu moyo, akili na viungo vya mwili kwa ajili ya kufanya mambo na matendo mema sambamba na kujiepusha na mghafala na wakati huo huo kujifunga kwa ajili ya kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kupatikana irada yake na kujiweka mbali na mambo yasiyo ya Mwenyezi Mungu na ambayo Allah hayaridhii. [8]

Adabu na Hukumu Zake

Wakati

Hakujaanishwa na kutengwa wakati maalumu kwa ajili ya kufanya itikafu, lakini kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akifanya itikafu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. [9] Kwa msingi huo wakati bora kabisa kwa ajili ya itikafu ukatambulika kuwa ni mwezi wa Ramadhani hususan kumi la mwisho la mwezi huo mtukufu. [10] Nchini Iran imezoeleka ibada ya itikafu kufanyika katika masiku meupe (tarehe 13, 14 na 15) ya mwezi wa Rajab [11] na katika baadhi ya nchi nyingine pia ibada ya itikafu hufanyika katika siku hizi. [12]

Muda

Kwa mujibu wa mafakihi wa Kishia muda wa itikafu kwa uchache unapaswa kuwa siku tatu na baada ya kumalizika siku ya pili, itikafu katika siku ya tatu huwa wajibu. [13] Wakati wa kuanza itikafu ni mwanzoni mwa kuchomoza alfajiri ya siku ya kwanza mpaka magharibi (kuzama jua) ya siku ya tatu. [14] Hata hivyo kwa mtazamao wa Malik bin Anas [15] na Shafi [16] miongoni mwa viongozi wa madhehebu nne za Ahlu-Sunna ni kwamba, anayefanya itikafu anapaswa kuweko mahali pa kufanyia itikafu kabla ya jua kuzama. [17]

Sehemu

Katika baadhi ya hadithi imeelezwa kuwa, itikafu ni maalumu kufanyika katika Masjid al-Haram, Masjd al-Nabi, Msikiti wa Kufah na Msikiti wa Basra. Hata hivyo kuna hadithi ambazo zinajuzisha kufanya itikafu katika msikiti mkuu au msikiti ambao imamu muadilifu anaswalisha Sala ya Ijumaa au Sala ya Jamaa. [18] Kwa msingi huo akthari ya wanazuoni wa fikihi waliotangulia wanaamini kwamba, itikafu ni maalumu kufanyika katika misikiti hiyo minne iliyotajwa, [19] hata hivyo Shahid Thani amesema: Hii kwamba, tuifanye itikafu ni maalumu tu kufanyika katika misikiti hiyo minne ni kauli dhaifu. [20] Aktahri ya mafakihi wa karne ya nne pia wanaamini kuwa, ni sahihi na inajuzu kukaa itikafu katika misikitu mikuu ya miji mbalimbali [21] na baadhi yao wanaona kuwa, kufanya itikafu katika misikiti isiyokuwa minne iliyotajwa (mbali na misikiti mikuu na isiyokuwa mikuu) inajuzu kwa nia ya matarajio (rajaa) ya kupata thawabu. [22]

Sharti la Saumu

Kwa mujibu wa Fiq'hi ya Kishia, Saumu ni katika nguzo za itikafu; [23] kwa msingi huo mtu ambaye hawezi kufunga kama vile msafiri, mgonjwa na mwanamke aliyeko katika siku zake (mwenye hedhi) haijuzu kwake kukaa itikafu. [24] Katika itikafu inajuzu kufunga Saumu kwa nia ya kadha au nadhiri. [25] Muhammad ibn Idris Shafi na Ahmad ibn Hambal miongoni mwa viongozi wa madhehebu manne za Kisuni wao hawaoni kama ni wajibu kwa mwenye kukaa itikafu afunge Saumu. [26] Lakini katika fikihi ya Maliki na kauli mashuhuri katika fikihi ya Hanafi, itikafu haikamili wala kutimia bila ya kufunga Saumu. [27]

Kutoka Msikitini

Katika kipindi cha kukaa itikafu inajuzu kutoka msikitini kwa ajili ya mambo ya dharura; kama vile kwenda kutafuta chakula, kukidhi haja, au mambo yenye maslahi kama vile kwenda kusali Sala ya Ijumaa, kushiriki mazishi, kwenda kutoa ushahidi na kwenda kumtembelea mgonjwa. Hata hiyo katika masuala haya pia, mwenye kukaa itikafu anapaswa kutosheka kwa kadiri ya dharura tu na hapaswi kukaa sehemu na ajitahidi kwa kadiri awezavyo asipite katika kivuli. [28] Sayyid Kadhim Tabatabai anasema katika kitabu cha al-Ur'wat al-Wuthqa kwamba, inajuzu kutoka sehemu ya itikafu kwa ajili ya jambo la dharura lililozoeleka na la kisheria na ambalo lina maslahi (bila kujali maslahi hayo yanamhusu mtu mwenyewe mwenye kukaa itikafu au mtu mwingine). [29] Kadhalika kwa mujibu wa ripoti zilizokuja katika kitabu cha Bihar al-Anwar ikinukuliwa kutoka katika kitabu cha Uddat al-Dai ni kwamba, Imamu Hassan Mujtaba (a.s) akiwa na lengo la kulipa deni la mmoja wa wafuasi wake, alikatisha tawafu na akaandamana naye ili akamtekelezee shida yake. [30]

Mambo ya Haramu katika Itikafu

Mafakihi wanasema kuwa, ni haramu kutumia na kunusa manukato, kugombana, kujadiliana mambo ya kidunia, kununua na kuuza (isipokuwa kwa ajili ya dharura) kupiga punyeto, kukutana kimwili (hata kwa kiwango cha kubusu) na mambo ambayo yanabatilisha itikafu. [31] Kadhalika kila kitu ambacho kinabatilisha Saumu, basi kinabatilisha itikafu pia. [32]

Falsafa na Athari Zake

Kwa mujibu wa hadithi ni kwamba, kukaa itikafu huwa sababu ya kusamehewa madhambi [33] na kuwa mbali na moto wa jahanamu. [34] Kadhalika itikafu huandaa uwanja na mazingira ya kufikiri, fursa ya kuomba dua na kunong'ona na Mwenyez Mungu kama ambavyo hilo huandaa mazingira ya kufanya toba na hayo ni mambo ambayo yametajwa kama falsafa ya kukaa itikafu. [35]

Historia ya Itikafu

Waislamu walijifunza itikafu kutoka katika Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w). [36] Kwa mujibu wa hadithi, kabla ya Uislamu itikafu ilikuweko pia. [37]

Kile ambacho kimenukuliwa kutoka kwa Mtume kuhusiana na itikafu kinahusianan na kipindi cha baada ya Hijra, yaani mjini Madina na katika mwezi wa Ramadhani ambapo Mtukufu huyo alikuwa akiwekewa hema katika Masjid al-Nabi. [38] Hii leo msikiti wa Mtume (Masjid al-Nabbi) upande wa mashariki wa nguzo ya toba kuna nguzo inajulikana kwa jina la Sarir (kitanda) ambapo inaelezwa kuwa, katika masiku ya itikafu, Mtume alikuwa akiweka tandiko lake kando yake na kufanya itikafu. [39]

Katika Ramadhani ya mwaka wa pili Hijiria, Mtume (s.a.w.w) hakuweza kukaa itikafu kutokana na kutokea vita vya Badr; hata hivyo mwaka uliofuata alikaa itikafu kwa muda wa siku 20 za mwezi wa Ramadhani; siku kumi kwa ajili ya mwaka huo na siku kumi nyingine alilipa kadha ya mwaka wa kabla ya yake. [40] Katika vyanzo vya hadithi kumenukuliwa pia taarifa mbalimbali kuhusiana na kukaa itikafu Maimamu wa Kishia wakiwemo Imamu Hassan Mujtaba (a.s) [41] na Imamu Ja'afar Swadiq (a.s). [42]

Vitabu Vilivyoandika Kuhusu Itikafu

Kumeandikwa vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kifarsi na Kiarabu kuhusiana nna maudhui ya itikafu na baadhi yavyo ni:

Katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuenea ada na sunna ya kukaa itikafu, kumeandikwa na kuchapishwa makumi ya vitabu kuhusiana na maudhui hii. [50]

Rejea

Vyanzo