Yanayobatilisha Saumu

Kutoka wikishia

Mambo yanayotengua Saumu (Kiarabu: مُبطِلات الصوم أو المُفطِرات): Ni kula na kunywa, jimai (kufanya tendo la ndoa) kupiga punyeto (kujitoa manii), kujitapisha, kuzamisha kichwa chote kwenye maji, kufika vumbi zito kwenye koo, kupiga bomba na vimiminika, kubakia na janaba au hedhi au nifasi mpaka adhana ya asubuhi, kumzulia Mwenyezi Mungu uongo au Mtume Muhammad (s.a.w.w) au Maimamu (a.s).

Mafakihi wanasema kuwa, kufanya kwa makusudi moja kati ya vitengua Saumu ni haramu na hilo linapelekea kafara kuwa wajibu.

Utambulisho

Vitengua Saumu ni mambo ambayo yanabatilisha Saumu. Katika vitabu vya Fiqhi vibatilisha Saumu vinatambulika pia kwa jina la “Muftirat” yaani vinavyofuturisha na kumuondoa mtu katika hali ya Saumu. [1]

Mafakihi wanasema kuwa, kufanya kwa makusudi moja kati ya vitengua Saumu ni haramu [2] na hilo linapelekea kafara kuwa wajibu, [3] lakini kama mtu atafanya moja kati ya hayo hali ya kuwa amesahabu kwamba, yupo katika hali ya funga au amelazimishwa, katika hali hii Saumu yake haitabatilika. [4]

Vitengua Saumu ni:

  1. Kula na kunywa.
  2. Kufanya tendo la ndoa (jimai).
  3. Kupiga punyeto (kujichua uume).
  4. Kumzulia Mwenyezi Mungu uongo au Mtume Muhammad (s.a.w.w) au Maimamu (a.s).
  5. Kufika vumbi zito kwenye koo.
  6. Kuzamisha kichwa chote kwenye maji. (hii ni raia ya mafakihi wengi). [5]
  7. Kubakia na janaba au hedhi au nifasi mpaka adhana ya asubuhi. Mtu ambaye ana janaba, au mwanamke ametoharika kunako hedhi na damu ya nifasi (uzazi) anapaswa kufanya ghusli (kuoga) kabla ya adhana ya Alfajiri, na kama hataoga mpaka adhana ya asubuhi, Saumu ya siku hiyo itabatilika.
  8. Kupiga bomba na vimiminika.
  9. Kujitapisha. [6]
  10. Kunuia kukatisha Saumu au kunuia kufanya moja kati ya yanayobatilisha Saumu. [7]

Siyo haramu kusafiri hali ya kuwa mtu amefunga saumu, [8], lakini kama msafiri hatafika kabla ya adhana ya adhuhuri katika mji wake au sehemu ambayo amekusudia kukaa siku kumi, Saumu yake itabatilika. [9]

Kula na kunywa

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi, kula na kunywa kunabatilisha Saumu pale mtu anapofanya hivyo kwa makusudi, lakini kama amesahau kwamba, amefunga kisha akala au akanywa kitu, Saumu yake itakuwa sahihi. [10] Baadhi ya Marajii Taqlidi kama Imamu Khomeini, Makarim Shirazi, Bahjat na Shubairi Zanjani ni kwamba, kupiga sindano au kutundikiwa dripu ya kutia nguvu ambayo inatumiwa badala ya chakula, kwa mujibu wa tahadhari ya wajibu haijuzu kufanya hivyo kwa aliyefunga; hata hivyo, mafaqihi wengine kama Khui, Sistani, Tabrizi, Safi Golpaygani wanasema kuwa, kupiga sindano au kutiwa dripu, iwe ni ya kutia nguvu au isiyokuwa hiyo hakuna tatizo. [11]

Kiu kikali

Kwa mujibu wa fat’wa ya akthari ya mafaqihi wa Kishia ni kwamba, kama mwenye kufunga Saumu ana kiu kikali ambacho hawezi kukivumilia, anaweza kunywa maji kidogo kwa ajili ya kuondoa kiu. [12] Kuhusiana na taklifu ya aliyefunga baada ya kunywa maji na kuondoa shida hiyo, kuna fatuwa mbili: Baadhi ya wanazuoni wanasema, licha ya kuwa inajuzu kunywa maji lakini kufanya hivyo kunabatilisha Saumu lakini pamoja na hayo, aliyefunga baada ya kufanya hivyo, anapaswa kujizuia na vinavyobatilisha Saumu mpaka adhana ya Magharibi na kisha aje kuilipa siku hiyo. [13] Mkabala na wanazuoni hao, kuna kundi la pili ambalo linasema, licha ya aliyefunga kunywa maji kwa ajili ya kuondoa kiu, lakini Saumu yake haibatiliki na kwa msingi huo hana haja ya kuja kuilipa siku hiyo. [14]

Mambo ya kingono

Mambo ya kingono ambayo yanabatilisha Saumu ni:

Jimai

Jimai au kufanya tendo la ndoa hata kama kufanya hivyo hakutapelekea kutokwa na manii, kunabatilisha Saumu. Kufanya jimai iwe ni kwa mbele au kwa nyuma, kunabatilisha Saumu na hakuna tofauti katika hilo kama ambavyo pia hakuna tofauti ya hukumu baina ya mwanamke na mwanaume.

Kupiga punyeto

Mafaqihi wanasema, kupiga punyeto (kujitoa manii kwa makusudi) nako kunabatilisha Saumu; [16] hata hivyo kwa mujibu wa fat’wa yao ni kwamba, kama mtu hatakuwa na nia ya kujitoa manii , lakini kitendo chake hicho kikapelekea kutokwa na manii, Saumu yake itakuwa sahihi. [17]

Kutomasana na kuchezeana na mke, kama kutapelekea kutokwa na manii bila ya kukusudia, hilo halitabatilisha Saumu; lakini kama mtu atatomasana na mkewe kwa nia ya kutoa manii au afanye hivyo kwa namna ambayo kikawaida hupelekea kutokwa na manii, kama hilo litapelekea kutokwa na manii, Saumu yake itabatilika. [18]

Kujiotea

Kujiotea ni kutokwa na manii usingizini na hili halibatilishi Saumu; lakini kama mtu atajiotea kabla ya adhana ya alfajiri, anapaswa kuoga janaba kabla ya adhana ya alfajiri. [19] Kujiotea katika kipindi chote cha mchana wa Saumu, hakuharibu Saumu. Kwa maana kwamba, atakayelala mchana kisha akajiotea na kutokwa na manii Saumu yake ni sahihi. [20]

Vumbi zito na na moshi

Kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi waliowengi ni kwamba, kufika fumbi zito katika koo kunabatilisha Saumu. [21] Ni kwa msingi huo, ndio maana kuvuta sigara na shisha na mfano wa hivyo ni miongoni mwa mambo ambayo yametambuliwa kuwa yanabatilisha Saumu. [22] Hata hivyo baadhi ya mafakihi hawajaorodhesha katika mambo yanayobatilisha Saumu, kufika vumbi zito katika koo. [23] Pamoja na hayo wanaamini kwamba, kwa mujibu wa tahadhari ya mustahabu, vumbo linabatilisha Saumu na haijuzu kutumia waziwazi tumbaku katika mwezi wa Ramadhani. [24]

Kusema uwongo

Kusema uwongo na dhambi zingine kama kusikiliza ghinaa, kuangalia haramu na husuda pamoja na kuwa ni haramu na dhambi zake katika mwezi wa Ramadhani ni zaidi, [25] lakini hayo hayabatilishi Saumu. [26] Kwa mujibu wa mafaqihi ni kwamba, uongo pekee ambao unabatilisha Saumu ni wa kumzulia Mwenyezi Mungu, Mtume na Maimamu (a.s). [27] Baadhi ya mafakihi wanasema kuwa, kumzulia uwongo Bibi Fatima Zahra (a.s) na Mitume wengine pamoja na warithi wao ni katika mambo yanayobatilisha Saumu. [28] Hata hivyo, Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa yeye mntazamo wake ni kuwa, kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume na Maimamu hakupelekei kubatilika Saumu. Anaamini kwamba, kitendo hiki ni katika madhambi makubwa na kadhalika madhambi mengine katika mwezi wa Ramadhani uharamu wake huwa mkali zaidi. [29]

Kuzamisha kichwa chote ndani ya maji

Baadhi ya mafakihi wanaamini kwamba, kufanya irtimasi ambayo ina maana ya kuzamisha kichwa chote ndani ya maji ni katika mambo yanayobatilisha Saumu. [30] Kwa mujibu wa fat’wa hii, haisihi kufanya josho la irtimasi katika hali ya Saumu mwezi wa Ramadhani na kufanya hivyo kunabatilisha Saumu. [31] Kwa mujibu wa fatwa ya kundi hili la mafakihi ni kwamba, kama sehemu fulani ya kichwa itakuwa nje Saumu itakuwa sahihi. [32]

Kundi jingine la mafakihi linasema kuwa, ni haramu kufanya josho la irtimasi hali ya kuwa mtu amefunga Saumu; hata hivyo hawalitambui hilo kama linabatilisha Saumu. [33]

Vyanzo

  • Āmulī, Muḥammad Taqī. Miṣbāḥ al-hudā fī sharḥ al-ʿUrwa al-wuthqā. Tehran: Nashr-i Muʾallif, 1380 AH.
  • Ḥakīm, Muḥsin al-. Mustamsak al-ʿUrwa al-wuthqā. Qom: Muʾassisat Dār al-Tafsīr, 1374 Sh.
  • Ḥillī, Yaḥyā b. Saʿīd al-. Al-Jāmiʿ li-l-sharāyiʿ’. Edited by Jaʿfar Subḥānī. Qom: Muʾassisat Sayyid al-Shuhadā, 1405 AH.
  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Muntahā l-maṭlab fī taḥqīq al-madhhab. Mashhad: Majmaʿ al-buḥūth al-Islāmīyya, 1412 AH.
  • Ibn Idrīs al-Ḥillī, Muḥammad b. Manṣūr. Al-Sarāʾir al-ḥāwī li-taḥrīr al-fatāwā. Second edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1410 AH.
  • Shubiyrī Zanjānī, Sayyid Mūsā. Risālat tawḍīḥ al-masāʾil. Qom: Salsabīl, 1430 AH.
  • Shahīd al-Awwal, Muḥammad b. al-Makkī al-. Al-Durūs al-sharʿīyya fī fiqh al-imāmīyya. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Yazdī, Muḥammad Kāẓim al-. Al-ʿUrwa al-wuthqā maʿa l-taʿlīqāt. Qom: Muʾassisat al-Nashr al-Islāmī, 1419 AH.