Daku

Kutoka wikishia
Makala hii inazungumzia maudhui ya kula daku. Kama unataka kufahamu kuhusiana na kuamka kwa ajili ya kula daku, basi angalia makala ya kukesha.

Daku (Kiarabu: السحور )ni chakula maalumu ambacho huliwa na Waislamu wakati wa mwezi Ramadhani. Chakula hiki huliwa na watu wenye nia ya kufunga Swaumu kesho yake. Daku huliwa kabla ya adhana ya Alfajiri. Kwa maana kwamba, kukishaadhiniwa kisheria mtu mwenye nia ya kufunga haruhusiwi tena kula daku. Kuna hadithi nyingi zilizopokewa ambazo zinatilia mkazo kuhusu umuhimu wa kula daku. Kwa mujibu wa mtazamo wa wanazuoni wa fiqh, kula daku ni mustahabu. Hata hivyo kula daku huwa wajibu endapo kuacha kula daku kutamfanya mwenye kufunga adhoofu mno wakati wa mchana na hilo kumpelekea afungue Swaumu yake kutokana na kushindwa kuendelea kufunga. Katika mataifa na jamii mbalimbali kuna ada tofauti za kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku hasa maeneo ya vijijini. Katika maeneo ya Afrika Mashariki vikundi mbalimbali hutumia dufu, vigoma na kuimba kaswida kwa ajili ya kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku. Ada na utamaduni huu wa kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku, ni mkongwe sio Afrika Mashariki tu bali hata katika mataifa mengine ya dunia.

Umuhimu Wake

Daku ni mlo ambao huliwa kabla ya adhana ya alfajiri na wanaofunga Swaumu.[1] Kwa mujibu wa hadithi, kula daku kumetajwa kuwa na umuhimu zaidi kuliko mlo wa futari.[2]Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume(s.a.w.w) ni kuwa, kula daku kuna baraka ambayo umma wake hauwezi kuiacha.[3] Kadhalika katika hadithi nyingine iliyopokewa kutoka kwa Mtume inasema: Salamu na rehma za Mwenyezi Mungu na Malaika zinawafikie wanaofanya toba na waumini ambao wanakula daku.[4] Katika hadithi za Maasumina 14 suala la kula daku hata kama ni kwa kiwango cha kunywa fumba moja ya maji limekokotezwa na kushajiishwa mno [5], ili kupunguza magumu ya funga ya Swaumu.[6] Katika hadithi zingine kuna baadhi ya vyakula kama tende vimetajwa kuwa vyakula bora kabisa kwa ajili ya daku, [7]. Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir(a.s), Mtume(s.a.w.w) alikuwa akila tende na zabibu kavu kama mlo wake wa daku.[8] Aidha hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’far Swadiq(a.s) inasema: Kila mfungaji anaposoma Surat al-Qadr wakati wa kula daku na kufuturu baina ya nyakati hizi mbili atakuwa mithili ya shahidi aliyeuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu.[9]

Hukumu

Hukumu zifuatazo ni miongoni mwa masuala ambayo mafakihi (wanazuoni wa fikihi) wamebainisha kuhusiana na suala la kula daku:

  • Ni mustahabu kula daku [10] na hadithi mbalimbali zimetilia mkazo zaidi juu ya kula daku katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.[11]
  • Ikiwa mtu atafahamu kwamba, asipokula daku atalazimika kufungua Swaumu yake, basi kula daku kwake ni wajibu.[12]
  • Mtu hawezi kuacha kufunga Swaumu kwa sababu hakula daku, lakini kama kutokula kwake daku kunamsababishia udhaifu mkubwa wa mwili kiasi kwamba, hawezi kuvumilia, katika hali hii anaweza kufungua na kisha akailipa kadhwa siku hiyo wakati mwingine.[13]
  • Ikiwa mtu ataamka na kula daku bila ya kufanya utafiti kama wakati wa adhana umewadia au la, kisha baadaye ikafahamika kuwa alikula daku baada ya adhana ya alfajiri, analazimika kulipa kadhwa siku hiyo.[14]
  • Ikiwa mtu yupo katika hali ya kula daku, kisha wakati wa adhana ya asubuhi ukawadia, anapaswa kutema chakula kilichoko kinywani mwake na kama atameza kwa makusudi na kwa ufahamu kamili, basi Swaumu yake itabatilika. Katika hali hii atalipa kadhwa siku hiyo pamoja na kutoa kafara.[15]

Ada na Mazoea

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, mwanzoni mwa Uislamu Ibn Maktum alikuwa akiwaamsha Waislamu wakati wa daku kwa kuadhini, na watu baada ya kula daku wanaposikia sauti ya Bilal Habashi akiadhini walikuwa wakifahamu kwamba, wakati wa swala ya alfajiri umewadia, hivyo walikuwa wakiacha kula.[16] Tangazo la kuwadia wakati wa swala na kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku ni mambo ambayo yalikuwa yakifanyika kwa mbinu mbalimbali kama vile waadhini kuzunguka katika mitaa,[17] kuwasha taa za chemli na kuzitundika sehemu, [18], kugonga milango ya nyumba Sabrtarii,((pazuhesh mardum-shenasii, ayniha va sunatihaye farhangii tarkimanha dar Iran mahe mubarak ramadhani)), kurasa ya 59 na kadhalika.[19] Katika jamii mbalimbali kuna ada tofauti za kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku hasa maeneo ya vijijini. Katika maeneo ya Afrika Mashariki vikundi mbalimbali hutumia dufu na kuimba kaswida kwa ajili ya kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku. Ada na utamaduni huu wa kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku, ni mkongwe sio Afrika Mashariki tu, bali hata katika mataifa mengine ya dunia. Baadhi ya maeneo hutumia upigaji ngoma na kadhalika kwa ajili ya kuwaamsha watu kwa ajili ya kula daku.

Rejea

  1. Dahkhodah, Lughat-namee Dahkhodah, Mada"suhurii"
  2. Sheikh Saduq, Man la yahdhuruhu al-faqih, 1413 Qamarii, juzuu ya 2, kurasa ya 136
  3. Kuleini, Al-kafii, 1407 Qamarii juzuu ya 4, kurasa ya 95
  4. Sheikh Saduq, Man la yahdhuruhu al-faqih, 1413 Qamarii, juzuu ya 2, kurasa ya 136
  5. Sheikh Saduq, Man la yahdhuruhu al-faqih, 1413 Qamarii, juzuu ya 2, kurasa ya 135-136; Sheikh Tousi, Tahdhibul-ahkam, 1407 Qamarii, juzuu ya 4, kurasa ya 198
  6. Sheikh Tousi, Tahdhibul-ahkam, 1407 Qamarii, juzuu ya 4, kurasa ya 199
  7. Sheikh Saduq, Man la yahdhuruhu al-faqih, 1413 Qamarii, juzuu ya 2, kurasa ya 136
  8. Sheikh Tousi, Tahdhibul-ahkam, 1407 Qamarii, juzuu ya 4, kurasa ya 198
  9. Sayyied Ibnu Tausi, Iqbalul-amal, 1409 Qamarii, juzuu ya 1,kurasa ya 83
  10. Allam Hilli, Tadhkiratul-fuqaha, 1414 Qamarii, juzuu ya 6, kurasa ya 231
  11. Tazama: Kuleini, Al-kafii, 1407 Qamarii, juzuu ya 4, kurasa ya 94
  12. Makareem Shirazi,((Hukumu khordan suhuri))
  13. Makareem Shirazi,((Hukumu ruzee nagiriftan fardii ke suhuri nakhordee
  14. Yazdi, Al-urwatul-mahshaa, 1419 Qamarii, juzuu ya 3, kurasa ya 604-606
  15. Musawi Khomeini, Taudhihul-masail(mahshaa), 1424 Qamarii, juzuu ya 1, kurasa ya 892
  16. Sheikh Saduq, Man la yahdhuruh al-faqih, 1413 Qamarii, juzuu ya 1, kurasa ya 297
  17. Khawajeiyan, ((Neghahi be ayinihaye mahe ramadhan)), kurasa ya 91
  18. Yar-Ahmadi, ((Ayinha, manasik wa marasim mahe ramadhani dar Iran)), kurasa ya 7
  19. Malikizadee,((shalik tup mahe ramadhan be riwayat isnad arashu milli Iran)), kurasa ya 189

Vyanzo