Sala ya Tarawehe
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Sala ya Tarawehe (Kiarabu: صلاة التراويح) ni miongoni mwa Sala za mustahabu ambayo huswaliwa katika nyusiku za mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wa madhehebu ya Kisuni wakifuata agizo la Omar bin al-Khattab huziswali Sala hii kwa jamaa. Hata hivyo Waislamu wa madhehebu ya Shia wanasema kuwa, ni bidaa na uzushi kuziswali Swala hizi kwa sura ya jamaa. Vyanzo vya hadithi na historia vya Masunia na Mashia vinasema kuwa, nafila za mwezi wa Ramadhani zilikuwa zikiswaliwa kwa sura ya furada katika zama za Mtume (s.a.w.w) na katika zama za Khalifa wa Kwanza (kwa mujibu wa itikadi ya Masuni) Abu Bakr ibn Abi Quhafa; lakini Oma ibn al-Khattab alitoa amri katika kipindi cha ukhalifa wake Sala ya tarawehe iswaliwe kwa jamaa. Msimamo wa Ahlul-Bayt (a.s) ulikuwa kwamba, kuswali kwa jamaa Sala za Sunna za Ramadhani ni bidaa na uzushi. Baadhi ya mafakihi na shakhsia wakubwa wa Ahlu-Suna nao walikuwa wakiswali Sala hii kwa sura ya furada.
Kila mwaka Sala ya tarawehe huswaliwa kwa sura ya jamaa katika wakati wa usiku wa masiku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani hususan katika Masjid al-Haram (Makka) na Masjid al-Nabbi (Madina). Mafakihi wa Kisuni wametofautiana kuhusiana na Sala hii pamoja na hukumu zake.
Kupewa Jina
Sala ya tarawehe ni katika Sala za mustahabu ambayo husaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika nyusiku za mwezi mtukufu wa Ramadhani. [1] Makusudio ya tarawehe ni kukaa na kupumzika anayesali baada ya kusali rakaa mbili [2] au nne katika mwezi wa Ramadhani. [3] Na ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana rakaa mbili au nne za Sala ya nafila katika mwezi wa Ramadhani zinatambulika pia kiistiara kuwa ni tarawehe; kwa sababu wanaosali hurefusha kisimamo katika Sala hii na baada ya kukamilisha Sala hukaa na kupunguza. [4]
Nafasi na Umuhimu Wake
Mafakihi wa Kishia na Kisuni wametofautiana kuhusiana na kuswali Sala za Sunna za mwezi wa Ramadhani kwa sura ya jamaa au furada. [5] Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaamini kwamba, inafaa na inajuzu kusali Sala ya tarawehe kwa jamaa na kila mwaka wamekuwa wakisali Sala hii katika nyakati za usiku za mwezi mtukufu wa Ramadhani katika misikiti yao. [6] Hata hivyo Maulamaa wa Kishia na baadhi ya Maulamaa mahiri wa Kisuni wanaamini kuwa, ni bidaa na uzushi kusali tarawehe kwa jamaa. [7]
Kila mwaka Sala ya tarawehe husaliwa kwa sura ya jamaa katika wakati wa usiku wa masiku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani hususan katika Masjid al-Haram na Masjid al-Nabbi.
Bidaa au Sunna?
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Omar bin al-Khattab ndiye aliyeamrisha Sala ya tarawehe isaliwe kwa jamaa wakati akiwa khalifa. Tukio hili lilitokea mwaka wa 4 Hijria. [8] Bukhari ananukuu kutoka kwa Abdul-Rahman bin Abdul-Qadir kwamba: Usiku mmoja Omar alikwenda msikitini na akaona watu wanasali kwa sura ya furada, akatoa amri watu wamfuate Ubayy ibn Ka’b na waswali kwa jamaa. Usiku mwingine alikwenda msikitini na alipoona watu wanaswalishwa na mmoja wa maqarii akasema: Hii ni bidaa nzuri. [9]
Omar ibn al-Khattab aliwateua watu kama Muadh bin Harith, [10] Abu Bakr bin Mujahid [11] na Suleiman bin Abi Hathma Adawi kuwa Maimamu wa Sala ya tarawehe. [12]
Kwa mtazamo wa mafakihi wa Ahlu-Sunna ni kwamba, Sala ya tarawehe ni bidaa mustahabu na sunna. [13] Abu Hamid Ghazali ameigawa bidaa katika makundi mawili, bidaa nzuri na bidaa mbaya na ameitambua Sala ya tarawehe kuwa ni katika bidaa nzuri. [14] Ibn Abi Ya’la mmoja wa wanazuoni na mafakihi wa Kihanbali anaamini kuwa, Omar hakuweka sunna hii, bali Bwana Mtume (s.a.w.w) ndiye aliyeifanya Sala ya tarawehe kuwa sunna ambapo anadai Mtume alisema: Mwenyezi Mungu amefaradhisha funga ya Saumu ya mwezi wa Ramadhani na mimi nimefanya Qiyam (kusimama kwa ajili ya kufanya ibada usiku) katika mwezi huu kuwa sunna. [15]
Kwa mujibu wa mafakihi wa madhehebu ya Shia, nafila za mwezi wa Ramadhani zinaswaliwa furada [16] na kusali Sala za sunna kwa jamaa ni bidaa na uzushi [17] na kwamba, katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) Sala hii haikuwa ikisaliwa kwa jamaa. [18] Sheikh Tusi amelitambua suala la kusali Sala za sunna za Ramadhani kwa jamaa kuwa ni bidaa na uzushi kwa mujibu wa ijmaa na makubaliano ya Maulamaa wa Shia Ithnaasharia. [19] Allama Majlisi mmoja wa wanazauoni mahiri wa Kishia anasema kuwa, Maulamaa wa Kishia hawana hitilafu za kimitazamo kuhusiana na kwamba, haijuzu Sala za sunna za Ramadhani kuswaliwa kwa jamaa. [20] Kwa maana kwamba, wote wamekubaliana na wanaamini kwamba, haijuzu Sala hizi za sunna kuswaliwa kwa jamaa.
Sira ya Ahlul-Bayt (a.s)
Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’far Swadiq (a.s) ni kuwa, wakati Imam Ali (a.s) alipochukua jukumu la Ukhalifa alimtaka mwanawe Hassan (a.s) awakataze watu kuswali Sala ya tarawehe kwa jamaa. Watu baada ya kusikia maneno hayo walipaza sauti kupinga hilo huku wakitaja jina la Omar; [21] Imam Ali akiwa na lengo kuzuia kusambaratika jeshi lake, aliachana na uamuzi wake huo. [22]
Masahaba kadhaa wa Maimamu (a.s) kama Zurarah, Muhammad bin Muslim na Fudhayl walimuuliza Imam Baqir na Imam Swadiq (a.s) kuhusiana na hukumu ya kuswali Swala za sunna katika mwezi wa Ramadhani kwa jamaa. Maimamu hao wakitegemea sira ya Bwana Mtume (s.a.w.w) walisema kuwa ni bidaa kuwali Sala hii kwa jamaa. [23] Kadhalika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) kuhusiana na idadi ya rakaa na namna ya kusali nafila ya Ramadhan ambapo Imam akitegemnea maneno ya Mtume (s.a.w.w) amesema: Haiwezekani kuswali Sala ya sunna kwa jamaa, kwani Mtuyme aliswali Suna kwa sura ya furada mpaka mwishoni mwa umri wake. [24] Hii ina maana kwamba, katika zama za Mtume, mbora huyo wa viumbe hakuwahi hata mara moja kusali Sala hii kwa jamaa.
Hukumu za Tarawehe
Baadhi ya hukumu zinazohusiana na Swala ya tarahewe ni:
- Kuswali kwa jamaa: Kuhusiana na kwamba, kusali Sala ya tarawehe kwa jamaa ni wajibu [25] au mustahabu [26] au mtu ana hiari baina ya kusali kwa jamaa au furada mafakihi wa Ahlu-Sunna wana mitazamo tofauti. [27] Hata hivyo inaelezwa kuwa ni mashuhuri baina ya Maulamaa wa Kisuni kwamba, Sala hii inasaliwa kwa jamaa. [28] baadhi ya mafakihi wa Kihanafi wanaamini kwamba, kusali Sala ya tarawehe kwa jamaa ni Sunna Kifai (sunna ambayo ikitekelezwa na mtu mmoja huwaondokea waliobakia). [29] Kadhalika Malik ibn Anas, kiongozi wa madhehebu ya Maliki anasema kuwa, ni bora Sala hii ikasaliwa nyumbani na kwa furada. [30] Ibn Asakir anasema, watu kama Abdul-Rahman ibn Muhammad ibn Idris (Abu Muhammad ibn Hatami Razi) [31] na Muhammad ibn Idris Shafi’i (150-204 Hijiria) miongoni mwa mafakihi wa madhehebu nne za Kisuni, walikuwa wakisali Sala ya tarawehe nyumbani na kwa sura ya furada. [32]
- Idadi ya rakaa: Kuhusiana na idadi ya rakaa za Sala ya tarawehe kuna nadharia na mitazamo tofauti. Sababu ya hitilafu hii ni kutokuweko hadithi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na badala yake imetumika kauli na kitendo cha masahaba kama ndio hoja. [33] Aghalabu ya mafaklihi wa Kisuni wametaja idadi ya rakaa za Sala ya tarawehe kuwa ni 20. [34] Inaelezwa kuwa, watu kama Abu Hanifa, Shafi’i na Ahmad ibn Hanbal wao pia wana mtazamo huu. [35] Lakini Malik ibn Anas ametaja idadi ya rakaa za Sala hii kuwa ni 36. [36] Idadi ya rakaa za Sala ya tarawehe imetaja kuwa ni 11 mpaka 47. [37] Kadhalika inaelezwa kuwa, lililoenea zaidi baina ya Waislamu ni rakaa 11. [38]
- Kwa mujibu wa mtazamo wa Mashia ni kwamba, nafila ya Ramadhani ni rakaa 100 ambapo katika kila usiku wa siku 20 za mwanzo kunasaliwa rakaa 20, katika kila usiku wa siku 10 za mwisho kunasaliwa rakaa 30 na katika usiku kati ya nyusiku za Laylatyul-Qadr zinasaliwa rakaa 100. [39]
- Wakati wa Sala: Kwa mtazamo wa Waislamu wa Ahlu-Sunna, Sala ya tarawehe inasaliwa wakati wa usiku katika siku za mwezi wa Ramadhani na ni baada ya Sala ya Isha mpaka kuchomoza alfajiri. [40]
Imeelezwa kwamba, kwa mtazamo wa wanazuoni wa fikihi wa Hanafi, Maliki na Hanbali, Sala ya tarawehe haina kadha; hata hivyo Shafi’i yeye anasema, baada ya kupita muda huo mtu anaweza kulipa kadha ya Sala ya tarawehe. [41]
Kuadhini na kukimu, [42] kusoma kwa sauti Bismillahi [43] na kumsalia Mtume [44] ni katika hukumu nyingine zinazohusiana na Sala hii. Katika vyanzo vya Ahlu-Sunna kumebainisha hukumu zinazohusian na Sala ya tarawehe [45]. Sarkhasi (aliyeaga dunia 483 Hijiria) ameweka faslu maalumu 12 katika kitabu chake cha al-Mabsut kuhusiana na Sala hii. [46]
Kuhitimisha Qur’ani
Baadhi ya shakhsia na wanazuoni wakubwa wa Ahlu-Sunna wameusia kuhitimishwa Qur’ani katika rakaa za Sala ya tarawehe. Wenye kusali hutumia mgawanyo wa Qur’ani wenye maana na maudhui moja. [47] Baadhi wanaamini kuwa, sababu ya mgawanyo huu ni kuweko uhusiano na Sala ya tarawehe. [48]
Bibliografia
Kumeandikwa na kusambazwa vitabu mbalimbali vyenye maudhui ya Swala ya tarawehe ambapo baadhi ya vitabu hivyo ni: «Salat al-Taraweh Sunat Mash’ruah au bidaa Muhdathah» kimeandikwa na Ja’far Baqiri, [49] na «Salat al-Taraweh Baina al-Sunah Wal-Bidaa» mwandishi Najm al-Din Tabasi [50] ni miongoni mwa athari za waandishi wa Kishia ambazo zimeandikwa kuchunguza na kukosoa Swala ya tarawehe.
Vilevile «Taraweh» kilichoandikwa na Imam Hissam al-Din Omar bin Abdul-Aziz, [51] «al-masabih Fi Swalat Taraweh» kilichoandikwa na Abdul-Rahman Suyuti, [52] «Nur al-Masabih Fi Swalat al-Taraweh» kilichoandikwa na Ali ibn Abdukafi Subki [53] na “Iqamat al-Burhan Al Kamiyat al-Taraweh Fi Ramadhan” ambacho kimeandikwa na Abdul-Rahman ibn Abdul-Karim Zubaydi ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa Kisuni kuhusiana na Swala ya tarawehe. [54]