Zakat al-Fitr

Kutoka wikishia
Makala hii ni kuhusiana na mafuhumu ya Zakat al-Fitr. Ili kufahamu kuhusiana na Zaka ya mali, angalia makala ya Zaka.

Zakat al-Fitr au al-Fitra (Kiarabu: زكاة الفطرة أو الفطر) ni miongoni mwa wajibu za kimali katika Uislamu ambayo hutolewa katika siku ya Eidul-Fitr. Kiwango cha Zakat al-Fitr kwa kila mtu ni kilo tatu za chakula cha kawaida; kama ngano na mchele ambapo inawezekana pia kutoa pesa ambayo ni thamani ya kilo tatu hizo.

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi, Zaka hii ni wajibu kutoa kwa mtu ambaye katika usiku wa Eidul-Fitr hakuwa fakiri, awe ni mwenye akili, aliye baleghe na mwenye utambuzi. Mtu mwenye sifa hizi anapaswa kutoa Zaka yake al-Fitr pamoja na watu wa familia yake anaowatunza na kuwalisha.

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi, maeneo ya matumizi ya Zaka ni yale yale manane; lakini baadhi ya mafakihi wanaamini kwamba, kwa mujibu wa tahadhari ya wajibu, Zakat al-Fitr inapaswa kutolewa tu kwa fakiri ambaye ni Shia.

Maana ya Zakat al-Fitr na Umuhimu Wake

Zakat al-Fitr ni mali ambayo ni wajibu kutolewa kwa mafakiri katika siku ya Eidul-Fitr au itumike katika mambo mengine. [1] Katika hadithi mbalimbali imekokotezwa na kutiliwa mkazo juu ya umuhimu wa Zakat al-Fitr. Kwa mujibu wa hadithi hizo, Zakat al-Fitr inapelekea kukamiilika kwa Saumu. Abu Basir na Zurarah wamenukuu kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba: Kama ambavyo mwenye kuswali akiamua kwa makusudi akiwa katika tashahudi [2] kuacha kumswalia Mtume Swala yake inabatilika, ni vivyo hivyo kama mtu atafunga Saumu na akaacha kwa makusudi kutoa Zakat al-Fitr, Saumu yake haikubaliwi. [3] Na huenda kutotoa Zakat al-Fitr kukasababisha kifo. [4] Zakat al-Fitr inajulikana pia kwa majina ya Fitriya [5] na Fitra. [6]


Masharti ya Kuwa Wajibu Zakat al-Fitr, Kinachotolewa na Kiwango Chake

Kwa mujibu wa fat'wa ya mafakihi, Zakat al-Fitr huwa wajibu kwa mtu ambaye ni baleghe, mwenye akili timamu na mwenye utambuzi kamili na asiwe fakiri au mtumwa. [7] Seyyid Muhammad Kadhim Yazdi, mmoja wa mafakihi wa Kishia na mwandishi wa kitabu cha al-Ur'wat al-Wuthqa amesema: Maulamaa wa Kiislamu wana ijmaa (kauli moja) katika jambo hili. [8]

Mtu aliyetimiza masharti haya anapaswa kujitolea yeye Zakat al-Fitr na kuwatolea wale ambao wanahesabiwa kuwa anawatunza na kuwalisha. Kila mtu ni wajibu kutoa Swaa (takribani kilo 3) za ngano, tende, zabibu kavu, mchele, mahindi na mfano wa hivyo au thamani yake na kumpatia anayestahiki. [9]

Kuhusiana na kwamba, ni kipi kati ya hivyo kinapaswa kutolewa, kuna tofauti za kimtazamo baina ya mafakihi; baadhi wanasema kigezo ni chakula cha kawaida cha mtu na baadhi wanasema anapaswa kutoa chakula ambacho kimezoeleka mahali anapoishi. [10] Kwa mujibu wa kitabu cha Farhang Fiq'h (utamaduni wa fikihi) fat'wa mashuhuri baina ya mafakihi ni kwamba, kigezo ni kutolewa chakula kilichozoeleka baina ya watu mahali anapoishi mtoaji. [11]

Miongoni mwa Marajii Taqlidi, Ayatullah Sistani na Safi Golpeygani wana mtazamo huu; lakini Ayatullah Makarim Shirazi, Noori Hamedani na Ali Khamenei wao wanasema, anaweza kutoa chochote miongoni mwa hivyo. [12]

Wakati wa Kutoa Zakat al-Fitr

Kwa mujibu wa fat'wa ya Marajii Taqlidi, wakati wa kutolewa Zakat al-Fitr ni siku ya Eidul-Fitr mpaka wakati wa adhuhuri; [13] miongoni mwa Ayatullah Shubairi Zanjani yeye anasema kuwa, siku nzima ya Eidul Fitr ni wakati wa kutoa Zakat al-Fitr. Kwa maana kwamba, wakati wowote katika siku hiyo mtu anaweza kutoa Zakat al-Fitr. [14] Hata hivyo kama mtu anaswali Sala ya Eidul Fitr anapaswa kutoa Zaka yake hiyo kabla ya kuswali au kwa mujibu wa fat'wa ya baadhi, awe ameshaitenga kando fitiri yake na mali zake nyingine. [15] Kadhalika kwa mujibu wa Sahib al-Jawahir ni kwamba, kwa mujibu wa nadharia mashuhuri, wakati wa kuwa wajibu Zakat al-Fitr ni magharibi ya siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani. [16] Baadhi ya wengine wamesema, kuwa wajibu kwake ni wakati wa kuchomoza alfajiri ya siku ya Eidul-Fitr. [17] Sahib al-Jawahir anasema, kuna uwezekano makusudio ya watu hawa ni wakati wa kutenganisha na kuweka kando fitiri na sio wakati wa kuwa wajibu kwake. [18] Mafakihi wanasema kwamba, haiwezekani kutoa Zakat al-Fitr kabla ya mwezi wa Ramadhani. Baadhi yao kama Imamu Khomeini na Makarim Shirazi wanasema, kwa mujibu wa tahadhari ya wajibu, haipaswi kutolewa pia katika mwezi wa Ramadhani; lakini baadhi akiwemo Ayatullah Sistani, Khui, Tabrizi na Shubairi Zanjani wanaamini kwamba, inajuzu, lakini ni bora isitolewe katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani. [19]

Zakat Al-Fitr Inatumika Wapi?

Baadhi ya Marajii Taqlidi akiwemo Imamu Khomeini, Behjat na Shubairi Zanjani, wamezingatia kwamba, matumizi ya Zakat al-Fitr ni katika zilezile sehemu nane za Zaka ya mali. [20] Maeneo hayo ya matumizi ni:

  1. Fakiri.
  2. Masikini.
  3. Mkusanyaji Zaka.
  4. Kafiri ambaye kama atapatiwa Zakat al-Fitr atasilimu au atasaidia katika vita vya Waislamu.
  5. Kununua na kuachilia huru mtumwa.
  6. Mdaiwa ambaye hawezi kulipa mkopo wake.
  7. Kazi zenye manufaa ya kidini kwa umma kama kujenga msikiti na daraja.
  8. Kumsaidia msafiri aliyekwama safarini. [21]

Lakini kundi jingine kama Ayatullah Sistani, Safi Golpeygani na Makarim Shirazi wanaamini kwamba, kwa mujibu wa tahadhari ya wajibu, Zakkat al-Fitr inapaswa kutolewa tu kwa fakiri ambaye ni Shia. [22] Hata hivyo, kundi la kwanza pia wameona hilo kuwa ni kwa tahadhari, lakini tahadhari ya mustahabu. [23]

Kumtolea Zakat Al-Fitr Mgeni

Kwa mujibu wa fat'wa ya mafakihi Zakat al-Fitr ya mgeni ambaye amewasili katika nyumba ya mwenyeji wake kabla ya jua kuzama na anahesabiwa kuwa ni katika watu anaowalisha iko mikononi mwa mwenyeji. [24] Hata hivyo kuna tofauti za kimitazamo kuhusiana na kwamba, ni nani anyehesabiwa kuwa ni katika watu anaowalisha: Baadhi kama Ayatullah Ali Sistani na Muhammad Taqi Bahjat Foumani wamemhesabu kuwa anayelishwa hata mgeni ambaye ugeni wake ni wa usiku mmoja na hivyo kutoa Zakat al-Fitr yake ni jukumu na mwenyeji wake; [25] hata hivyo Ayatullah Shubairi Zanjani, Fadhil Lankarani na Makarim Shirazi wanasema: Usiku mmoja tu hauwezi kuhesabiwa kuwa mgeni huyo amekuwa miongoni mwa watu wanaolishwa na mwenyeji, bali ni lazima awe na uamuzi wa kukaa muda fulani kwa mwenyejii wake huyo. [26]

Baadhi ya Hukumu Zingine

Baadhi ya hukumu zingine za Zakat al-Fitr kwa mujibu wa vitabu vya Tawdhih al-Masail (ufafanunzi wa sheria za Kiislamu) ni:

  • Mtu ambaye fitiri yake ni wajibu mtu mwingine kumtolea, halazimiki tena kutoa Zakat al-Fitr.
  • Kama mtu ni wajibu kwake kutoa Zakat al-Fitr ya mtu fulani kisha asitoe, utoaji wa Zakat al-Fitr hauwi wajibu kwa yule ambaye alikuwa atolewe, lakini mhusika hakutoa. Hata hivyo baadhi ya Marajii Taqlidi wamesema, kwa mujibu wa tahadhari ya wajibu anapaswa kutoa mwenyewe baada ya kutotoa yule ambaye alipaswa kumtolea.
  • Ikiiwa mtu Zakat al-Fitr yake ni wajibu kutolewa na mtu mwingine kisha yeye mwenye akatoa, wajibu wa yule ambaye alipaswa kutoa Zakat al-Fitr yake haumuondokei. Pamoja na hayo, baadhi wamesema, kama kutoa Zakat al-Fitr huko kumefanyika kwa idhini ya yule ambaye ilikuwa wajibu kwake kumtolea basi itatosheleza.
  • Mtu ambaye siyo sharifu (anayetokana na kizazi cha Mtume) hawezi kumpatia Zakat al-Fitr mtu ambaye ni Seyyid yaani sharifu.
  • Ikiwa kutoa Zakat al-Fitr ni wajibu kwa mtu lakini hakutoa na wala hakuiweka kando (ili baadaye atoe) kwa tahadhari ya wajibu anapaswa kuitoa baadaye lakini bila ya nia ya adaa au kadha.
  • Ikiwa mtu ataweka kando Zajkat al-Fitr, hawezi tena kuichukua na kisha kuchukua mali nyingine kwa ajili ya Zakat al-Fitr.