Taqwa

Kutoka wikishia

Taqwa au uchamungu (Kiarabu: التقوى): Ni hali maalumu au nguvu zilizoko katika roho ya mtu fulani, zinazompa yeye kinga ya kiroho na kimaadili; kwa njia ambayo ikiwa atajikuta katika mazingira ya dhambi, hali hiyo na zile nguvu za kiroho alizokuwa nazo humhifadhi na kumkinga na dhambi hizo. Katika Qur'ani, hadithi za Mtume (s.a.w.w) pamoja Riwaya za Maimamu Watakatifu ambao ni Maasumina (a.s) na pia kwenye maneno ya wanazuoni wa dini kuna masisisitizo makubwa juu ya umuhimu wa taqwa (uchamungu) na athari zake katika maisha ya kidunia na Akhera. Kusamehewa dhambi, kukubaliwa kwa vitendo na amali za mja mbele ya Mwenye Ezi Mungu, kufikia wokovu, kuwa na uwezo wa kutofautisha kati ya haki na batili, wasaa katika rizq na kupata riziki ya halali na kuokoka kutokana na shida mbali mbali, ni baadhi ya athari za taqwa.

Mbali na Hadithi nyingi zilizoangazia mada hii, hotuba ya 193 ya Nahjul Balagha, maarufu kama hotuba ya Hammam, imejitolea katika kueleza sifa za wenye taqwa (wachamungu). Kuna daraja kadhaa zilizo elezewa kuhusiana na uchamungu. Kuna daraja tatu muhimu zilizotajwa katika Hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), daraja hizo ni:

  • Taqwa ya jumla: ambayo ni kuacha mambo ya haramu kwa sababu ya kuogopa adhabu ya moto wa Jahannam.
  • Taqwa ya pekee (makhususi): nayo, sio tu mtu kuacha mambo ya haramu tu, bali pia mambo ambayo yawezekana kuwa haramu. Yaani iwapo atakuwa na shaka juu ya uharamu wa tendo fulani, basi pia mtu mwenye taqwa maalumu huamua kutotenda tendo hilo.
  • Taqwa ya pekee na yenye kiwango pekee: Hii ni daraja ambayo mtu sio tu huachana na matendo ya dhambi na yale anayo yashakaia kuwa si halali tu, bali pia yeye huachana na baadhi ya halali.

Pia wanazuoni wa dini kwa kuzingatia Hadithi zilizoko katika vyanzo vya kidini, wamebainisha aina maalumu ya taqwa kwa kila kiungo cha mwili ambacho kiko katika hatari ya kukabiliwa na dhambi, kama vile; taqwa ya masikio, macho, ulimi pamoja na moyo.

Ufafanuzi wa dhana ya taqwa

Taqwa ni hali anayokuwa nayo mtu fulani, ambayo humpa kinga ya kiroho na maadili ambayo humfanya yeye pale anapokuwa katika mazingira ya dhambi aweze kujizuia na kuto kuingia makosani kwa tenda dhambi hizo. [1] Neno taqwa limetokana na neno la Kiarabu, ambalo asili yake ni waqaa linalomaanisha kuhifadhi na kulinda, na kwa maana ya lugha ya kisheria, lina maana ya kujizuia na kuihifadhi nafsi. [2]

Maana za Taqwa katika Qur'an

Baadhi ya watafiti, wakizingatia aya za Qur'an, wametaja maana nne za taqwa, nazo ni kama ifuatavyo: [3]

  1. Kwa maana ya kitu (kizuizi) ambacho mtu hukiweka kati yake na kitu ambacho anakiogopa ili kujilinda kutokana na madhara ya kile anachokiogopa. [4] Mwenye Ezi Mungu katika Qur’ani amesema: ((وَ جَعَلَ لَکُمْ سَرَابِیلَ تَقِیکُمُ الْحَرَّ ; Na akujaalieni nguo ambazo zinakukingeni kutokana na joto)). [5] Katika Aya hii, neno limetumika kwa maana ya kizuizi na kinga inayomkinga mja kutokana na madhara fulani (joto). [6] Kulingana na maelezo ya Toshihiko Izutsu‏‎; Maana hii ilikuwa inatumika miongoni mwa Waarabu kabla ya kabla ya Uislamu. [7]
  2. Kwa maana ya kuogopa ghadhabu au adhabu ya Mwenye Ezi Mungu katika Akhera. [8]

Mwenye Ezi Mungu anasema: ((وَ اتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ شَدِیدُ الْعِقَابِ ; Na muogopeni Allah, bila shaka Alla ni Mkali wa kuadhibu)). [9] Neno taqwa katika Aya hii Iimetumika maana kuwa na khofu. [10]

  1. Kwa maana ya kutii na kuacha dhambi. [11] Allah katika Qur’ani anasema: ((یا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا اتَّقُوا اللهَ وَلْتَنْظُرْ نَفْسٌ ما قَدَّمَتْ لِغَدٍ ; Enyi mlioamini mwogopeni Allah, na kila mmoja aangali nini kajiwekea kwa ajili ya kesho Akhera)). [12] Neno katika Aya hii Iimetumika kwa maana ya kutii na kuacha dhambi. [13]
  2. Maana nyingine ya taqwa ni aina ya hali ya kimoyo na tabia ya nafsi (iliyo ota mizizi kwenye nafsi) ambayo huwa ndio chanzo cha mtu kuwa na nuru ya ufahamu wa kutambua uhalisia wa utiifu (uchamungu) na uhalisia wa dhambi. Ili mwanadamu kufikia daraja aina hii ya ufahamu, yampasa kushikamana na kufuata amri za Mwenye Ezi Mungu na kuachana na makatazo yake. [14]

Inasemekana kwamba maana hizi nne ni maana zenye mafungamano baina yake, na zote kwa pamoja zinapokutana huunda mfumo na maana kamili ya taqwa (uchamungu). Kwa maana kwamba khofu ya kuogopa adhabu ya Mwenye Ezi Mungu (maana ya pili ya taqwa), husababisha kuzingatia na kushikamana na amri za Mwenye Ezi Mungu na kuachana na makatazo yake, ambapo kufanya huwa kuna maanisha mtu kuwa na taqwa maana ya tatu. Na maana hiyo humaanisha kule mtu kuweka kizuizi kati yake na ghadhabu za Mwenyezi Mungu, kizuizi ambacho huwa ni kinga ya kuepukana na adhabu ya Mola wake (maana ya taqwa kwa maana ya kwanza). Pia kutii amri na kuachana makatazo ya Mwenye Ezi Mungu, polepole huepelekea taqwa kuwa ndio tabia katika moyo wa muumini (maana ya nne ya taqwa). [15]

Uwiano kati ya Taqwa na Wara’a (kujiepusha na dhambi)

Makala asili: Wara’a (kujiepusha na dhambi)

Katika baadhi ya Hadithi, neno taqwa limekuja sambaba na neno wara’a. [16] Muhammad Mahdi Naraki [17] ameyafasiri maneno mawili haya kama ni visawe, pia ametaja maana mbili za neno wara’a ambazo pia hutumika kwa maana ya taqwa: Moja ni kwamba; wara humaanisha kujilinda na mali haramu ambayo, kwa mujibu wa maoni ya Naraki ni kwamba; katika baadhi ya Hadithi pia neno taqwa limekuja kwa maana hii. Maana ya pili; ni kujilinda kutokana na kufanya aina zote za dhambi, kutokana na khofu ya ghadhabu ya Mwenye Ezi Mungu na pia kwa ajili ya kutafuta radhi Yake. [18]

Wengine, kama vile Abdulqadir Mullahuweish al Ghazi, mwanachuoni wa madhehebu ya Hanafi kutoka Syria, ambaye ni mwanazuoni wa karne ya 14 Hijiria, amefasiri neno wara’a kwa maana tofauti na taqwa akisema kwamba; wara’a ni wasifu wenye daraja kubwa zaidi kuliko taqwa. [19] Kwa maoni yake; taqwa ni kujiepusha na haramu na kufanya wajibu wa Mwenye Ezi Mungu, na wara ni daraja ya juu zaidi ambayo humaanisha kujiepusha na mabo yenye shaka na pia kujiepusha na mambo halali ambayo yanaweza kusababisha au kuwa ni hatua fulani itakayo pelekea kutenda dhambi. [20]

Nafasi na hadhi ya taqwa

Neno taqwa ni mojawapo ya maneno ya kawaida na yanayotumiwa sana katika dini. Mara nyingi neno hili katika Quran limekuja kwa mfumo wa kinomino na kitenzi. [21] Kwa mujibu wa maoni ya mwanafalsafa wa Kiislamu Shahid Murtadha Mutahhari, ni kwamba; idadi ya neno taqwa ima inakaribiana au inaendana sawa na ya neno imani, matendo mema, sala, na zaka katika Qur’ani. [22] Kwa mujibu wa maoni ya baadhi ya wanazuoni, neno taqwa limetumika mara 17 katika Quran, na kuna kiasi maneno 200 yaliotajwa katika Qur’ani, ambayo ima yanatokana na mzizi wa neno hilo au ni visawe vya neno hilo. [23] Neno taqwa pia limetumika kwa wingi katika Hadithi za Imamu Ali (a.s) pamoja na Hadithi za Maimamu wengine wa Ahlul Bayt (a.s). [24] Kolaini ametenga mlango maalumu katika kitabu chake kiitwacho Al-Kafi, malango ambao ameupa jina la Mlango wa Uchamungu na Taqwa (بَابُ الطَّاعَةِ وَ التَّقْوَی), mlango umekusanya ndani Hadithi tu zinazohusiana na taqwa. [25]

Pia Katika kitabu Nahju al-Balagha; Neno taqwa linaonekana kuwa ni mojawapo ya maneno yamepewa kipaumbele mno, ni miongoni mwanguzo msingi katika ibara zilizomo kitabuni humo. [26] Kwa mujibu wa wa maoni ya baadhi ya wanazuoni, neno taqwa na viambishi vyake limetumika mara 100 katika Nahj al-Balagha na ni mojawapo ya maneno muhimu na msingi katika maneno ya Imam Ali (a.s). [27] Katika kazi na fasihi zilizoeandikwa katika uwanja wa maadili ya Kiislamu, neno taqwa na athari zake, ni moja wapo ya mada muhimu zilizo jadiliwa na waandishi wa kazi hizo. [28] Pia, taqwa ni moja ya daraja zenye hadhi maalumu katika maneno ya Masufi na wanafani wa irfani (usufi wa Kishia), ambapo table mbele ya wanazuoni hawa, ni mojawapo ya nafasi maalumu inayofasirika kupitia dhana mbili; dhana ya wara’a na qalbu (moyo). [29]

Katika maneno ya wanazuoni wa kifiqhi, kunapatika uchambuzi wa nafasi ya taqwa katika baadhi ya hukumu za kisheria (kifiqhi). [30] Miongoni mwa mambo mengine, kwa mujibu wa fatwa za wanazuoni, ni wajibu kwa imam wa sala ya Ijumaa kisisitiza taqwa katika hotuba yake ya sala ya Ijumaa. [31] Kwa mujibu wa fatwa za baadhi ya wanazuoni, ikiwa wanaijitihadi wawili watakuwa sawa kwa suala la kitaaluma, ni wajibu kwa mfuasi kumfuata yule mujitahidi ambaye ni mcha Mungu (mwenye taqwa) zaidi kati yao. [32]

Baadhi ya chambuzi kutoka katika Qur’ani, Hadithi na wanazuoni kuhusiana na Taqwa

Kulingana na Aya ya 13 Suratu al-Hujurat ni kwamba; Taqwa ndio kipimo na kigezo cha thamani ya mtu miongoni mwa mwanadamu. [33] Kulingana na aya ya 197 Surat al-Baqara, ni kwamba; Taqwa ndio zawadi bora zaidi ya kiroho kwa ajili ya Akhera. [34] Katika Aya ya 26 Surat al-A'raf, baada ya Mwenye Ezi Mungu kutaja nguo za kustiri mwili, ameusifu uchamungu (taqwa) kuwa ndio nguo bora na muhimu zaidi kwa mwanadamu. [35]

Katika khutba ya 112 ya Nahj al-Balagha, Imam Ali (a.s) amenukuliwa akisema kuwa; Mwenye Ezi Mungu uchamungu imewalinda wapenzi wake kupitia uchamungu, ambapo kupitia uchamungu huo amewaweka wao katika ulinzi wake, na kuwaepusha na kuvuka mipaka ya utakatifu wa wake na ukawazuia wasitende maharamisho yake, na kupitia uchamungu huo huo ameweifanya hofu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu imee nyoyoni mwao. [36] Katika khutba ya 16, Imamu Ali (a.s) ameufananisha uchamungu (taqwa) kipando, katika khutba hii amenukuliwa akisema; Taqwa ni kama vipando (wanyama) ambao ni makini wenye kutiririka kwa mtirirko maridhawa, ambao hatamu zao zimo mikononi mwa wale walioko migongoni mwa wanyama hao, wanyama ambao huwadhamini wapandaji wake kuwafikisha kwenye kituo cha mwisho wa safari zao, ambacho ni Pepo ya Mwenyezi Mungu. [37] Katika khutba ya 189; Imamu ameusifu uchamungu (taqwa) kwa kusema kuwa; manufaa ya uchamungu (taqwa) katika ulimwengu wa hapa duniani kwa Mwanadamu ni kama uzio na ngao, na kesho Akhera taqwa ndio njia ya kuelekea Peponi. [38] Katika khutba ya 228, aliusifu uchamungu akisema kuwa; taqwa ni ufunguo wa haki na ni hazina ya Siku ya Kiyama, taqwa ni ufunguo wa uhuru kutokana na utumwa na ni wokovu kutokana na kila balaa [39] Imamu Sajjad (a.s) aliuchukulia uchamungu kuwa ndio sababu ya mtu kupata hadhi. [40] Pia katika baadhi ya dua za Sahifa Sajjadiyya, Imamu Sajjad (a.s) ameonekana kulilia Mwenye Ezi Mungu akimuomba kumpa daraja ya uchamungu (taqwa). [41]

Katika moja ya Hadithi kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), taqwa imesifiwa kwa kupewa uzito mkubwa mno. Katika Hadithi hiyo imeelezewa kuwa; taqwa sifa ambayo ndani imekusanya aina zote za matendo mema ndani yake. [42] Imepokelewa kutoka kwa Imamu Baqir (a.s) kwamba; mja anayependwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni yule mwenye taqwa zaidi miongoni mwa waja wake. [43] Pia katika Hadithi nyingine kutoka kwake, Mashia halisi wameelezewa kuwa ni wale wanaozingatia taqwa na uchamungu. [44] Kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), tendo dogo lililoambatana na taqwa ni bora zaidi kuliko tendo kubwa lilotendwa bila ya taqwa. [45] Raghibu Isfahani (alifariki mwaka 396 Hijiria), mwanafalsafa na mwanaisimu (mtaalamu wa lugha), katika kitabu chake "Al-Dhari'ah ila Makarim al-Shari'ah, amesema kwamba; " taqwa na utakaso wa nafsi ndio sharti kuu la mtu kupata ukhalifa wa kiungu kwa wanadamu. [46] Ibn Fadhl al-Hilli katika kitabu chake "'Iddat al-Da'i" akielezea umuhimu wa taqwa amesema kwamba; kama kungekuwa na tabia bora zaidi, yenye manufaa zaidi, na yenye hadhi ya juu zaidi kuliko taqwa katika ulimwengu kwa ajili ya mwanadamu, bila shaka Mwenye Ezi Mungu angeliwajulisha waja wake kupitia njia ya wahyi. [47] Muhammad Mahdi Naraqi katika kitabu chake "Jamiu' al-Sa’adaat" amielezea taqwa kwa kusema kuwa; taqwa ni mwokozi mkubwa wa mwanadamu na ni mojawapo ya njia muhimu za kufikia faraja na kupata daraja za juu. [48] Imam Khomeini pia katika kitabu chake "Sharhu Chehel Hadith" ameeleza akisema kuwa; kufikia daraja na kupata hadhi za kimaadili za juu za ukamilifu wa kibinadamu bila taqwa ni jambo lisilowezekana. [49]

Daraja za taqwa

Baadhi ya Wafasiri, wakizingatia baadhi ya Aya kama vile Aya isemayo: “اِنَّ اَکرَمَکُم عِندَ اللّهِ اَتقـکُم” "Bila shaka mbora wenu kwa Mwenye Ezi Mungu ni yule mcha Mungu zaidi miongoni wenu", [50] wamesema kwamba; taqwa kiuhalisi ni sifa yenye daraja tofauti. [51] Katika Hadithi iliyo nukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), kuna daraja tatu zimeorodheshwa katika Hadithi hiyo kuhusiana na taqwa, ambazo ni kama ifuatavyo:

  1. Taqwa ya kiujumla: ambayo husimama kama ni kinga inayo mfanya mtu kuacha mambo ya haramu kwa sababu ya kuogopa adhabu ya Jahannam.
  2. Taqwa ya makhususi: taqwa ambayo si kwamba mtu, humlinda asitende mambo ya haramu, bali humzuia kutenda hata mambo ambayo ni yenye shaka (kitu ambacho kinashakiwa kuwa na uwezekano wa kuwa ni haramu).
  3. Taqwa ya makhususi yenye umakhususi wa kipekee: taqa ambayo mwenye nayo, pamoja na kuachana na mambo yanayo shakiwa kuwa ni haramu, pia yeye hujihadhari na mambo Halali ambayo yanawezekana kumtelezesha mtu na kumwingiza makosani. [52]

Baidhawi, mfasiri wa Qur'ani na faqihi wa Kishafi'i wa karne ya saba na nane Hijiria, akitoa maelezo kuhusiana na taqwa, ameigawa taqwa katika daraja tatu za taqwa:

  1. Ya kwanza ni kujiepusha na shirki.
  2. Ya pili ni kujiepusha na dhambi.
  3. Ya tatu ambayo ndiyo daraja ya juu kabisa, ni kusalimu amri mbele ya Mwenye Ezi Mungu na kujiepusha na chochote kile kinachoweza kumzuia mtu kutenda haki. [53]

Al-Allāmah al-Majlisi pia katika kitabu chake "Bāhār al-Anwār" amefafanua daraja tatu tofauti za taqwa, ambazo:

  1. Ya kwanza ni kuilinda nafsi kutokana na adhabu ya milele kwa njia ya kufuata imani na itikadi sahihi.
  2. Ya pili ni kujiepusha na aina zote za dhambi.
  3. Ya tatu ni kujidhibiti dhidi ya chochote kile kinachoweza kuushughulisha moyo wa mwanadamu na kuwa ni pazia au kizuizi baina yake na Mola wake. [54]

Uchambuzi wa viwango vinne vya uchamungu wa Imam Khomeini Imam Khomeini, katika kitabu chake Adaab al-Salat, ametaja viwango vinne vya uchamungu (taqwa) ambavyo ni:

  1. Uchammungu wa nje, ambao ni kuizuia nafsi na dhambi za nje. Huu ni uchamungu wa pata sote, yaani ni uchamungu wa kijumla jamala, ambao unahusiana vitendo na tabia za nje za mtu. Kwa mfano, kuacha kula nyama ya nguruwe, kunywa pombe, na kuzini.
  2. Uchammungu wa ndani, ambao ni kujiepusha na kupita kiasi na kuvuka mipaka ya wastani katika maadili na silika ya kiroho. Huu ni uchamungu wa watu maalum, ambao unahusu tabia na hisia za ndani za mtu. Kwa mfano, kujiepusha na hasira zinazovuka viwango vya kisheria, kuwa na furaha zinazopindukia mipaka na kuwa tamaa za kupita budi.
  3. Uchammungu wa akili, ambao ni uchamungu na taqwa ya kuhifadhi na kuitakasa akili kutokana na kujishughulisha na sayansi au elimu zisizo za Kimungu. Huu ndio uchamungu wenye kuipamba akili kwa sifa maalumu (elimu maalumu), katika uchamungu huu, mtu hujiepusha na elimu zisizofaa, kama elimu ya kutengeneza madawa ya kulevya, elimu ya kutengeneza virusi kwa ajili ya kuwadhuru wnadamu na elimu ya kutengeneza sumu ya kutokomeza viumbe.
  4. Uchammungu wa moyo, ambao ni kuuzuia moyo kuto kuwa na utajo zaidi ya Mwenye Ezi Mungu na kutojishighulisa na mafungamano yasiokuwa ya Kiungu. Huu ndio uchamungu wa daraja ya kwanza kabisa, ambao unahusu moyo na roho ya mtu. Kwa mfano, kupenda akipendacho Allah na kuchukia akichikiacho. [55]

Taqwa ya mwili na ya moyo

Kwa kuzingatia Hadithi zilizonukuliwa kuhusu maadili, wanazuoni wa fani ya maadili, wameweza kutenga aina maalumu ya taqwa kwa kila kiungo cha mwili kinacho weza kukabiliwa na dhambi, kulingana na hadhi na nafasi ya kiungo hicho. Baadhi ya takwa hizo kulingana na nafasi za viungo ni kama ifuatavyo:

  • Taqwa ya ulimi: ni kujizuia na kushikamana na mambo maalumu, kama vile; kusema ukweli, [56] kutamka kumdhukuru Mungu, [57] kuzungumza kwa upole na adabu, [58] kutamka maneno mema, kudhibiti ulimi kutokana na matusi na kuacha maneno yasiyo na manufaa ambayo hayana faida. [59]
  • Taqwa ya macho: kutoa kodolea macho kila kitu ambacho Mungu amekiharamisha. [60]
  • Taqwa ya masikio: hii ni taqwa ambayo yabidi mja kujidhibiti na yanayo hisiana na sauti, kama vile; kudhibiti masikio yake kutokana na kusikia mambo yalio haramishwa na Mungu, [61] na vile vile kusikiliza mambo ya elimu zenye manufaa, [62] hekima yenye manufaa ya kidini na nasaha na maonyo yenye manufaa na uokovu. [63]
  • Taqwa ya moyo: Katika aya ya 32 ya Surat al-Hajj na Aya ya 3 ya Surat al-Hujurat, na vile vile katika Hadithi kutoka kwa Maimamu waadilifu (Maasumina), moyo wa mwanadamu umezingatiwa kuwa ndio makazi ya taqwa. [64] Kwa sababu hiyo, baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba; taqwa ni jambo la kiroho na la batini, ambalo linahusiana na roho na nafsi ya binadamu. [65] Wakati huo huo, wengine wanaamini kwamba; taqwa ya moyo ni ile taqwa inayopelekea moyo wa mtu kuwa safi kutokana na shaka, shirki, ukafiri na unafiki. [66] Baadhi wameihisabu takwa ya moyo kuwa ndio taqwa yenye kiwango cha juu zaidi kuliko aina nyengine za taqwa. [67]

Athari za takwa

Wanazuoni wa Kiislamu, kwa kuzingatia Aya za Qur'an na Hadithi za Maimamu waadilifu (Maasumina), wameorodhesha idadi kadhaa za athari za takwa. Baadhi ya athari hizi ni kama ifuatavyo:

  • Kutambua haki na batili, yaani hupelekea mtu kuweza kutofautisha baina ya haki na batili. [68]
  • Kukubaliwa kwa matendo mbele yam ja mblele Mwenyezi Mungu. [69]
  • Kufaidika na mafunzo ya Mwenyezi Mungu. [70]
  • Kuokoka kutoka na shida mbali mbali. [71]
  • Kufaidika na mwongozo wa Qur'an. [72]
  • Kusamehewa dhambi. [73]
  • Kuufikia wokovu (kufuzu). [74]
  • Kufikia cheo na kupata daraja ya juu mbele ya Allah. [75]
  • Kurekebishika (kunyooka) kwa moyo. [76]
  • Kizuizi kinacho mzuia mja kutumbukia katika yenye shaka. [77]
  • Kusafishwa kutokana na uchafu wa dhambi. [78]
  • Kupata rizki ya halali. [79]
  • Kupata maisha ya milele Peponi. [80]

Khutba al-Mutaqqina

Makala asili: Khutba al-Mutaqqina

Khutba al-Mutaqqina (خطبه متقین), ni mojawapo ya khutba maarufu ilioko katika kitabu Nahju al-Balagha ambayo imengazia sifa za wacha Mungu. [81] Imam Ali (a.s) aliyatoa khutba hii kupita ombi alililo aombwa na mmoja wa wafuasi wake aliyeitwa Hammam, aliorodhesha katika khutba yake hii zaidi ya sifa mia moja za kiroho, kiakili, kimaadili, na vitendo vwa watu wenye taqwa. [82] Sifa kama vile kuwa na kauli njema, kuwa mtu wa kati na kati katia nyenendo na silka, kusikiliza elimu zenye manufaa, kuwa na uvumilivu katika nyakati ngumu, kudhibiti ulimi, kumtaja Mungu katika hali zote, na kusimama usiku ni miongoni mwa sifa zinazohusishwa na watu wenye taqwa katika khutba hii maarufu. [83]

Bibliografia (seti ya vitabu kuhisana na maudhi ya taqwa)

  • Kitabu Risaleye Taqwa: Kitabu hichi ni kazi ya Murtadha Mutahhari. Kazi hii ni mkusanyo wa hotuba za mihadhara miwili kuhusiana na mada ya asili ya taqwa, umuhimu wake, na athari (matokeo) yake kutoka katika Qur'an na Hadithi. Mihadhara hii ilitolewa katika miaka ya 1339 hadi 1341 Shamsia, pamoja na hutuba nyingine kadhaa, ambazo zilikusanywa na kuandikwa katika kitabu kilichoitwa “Dah Goftar” yaani Kauli Kumi. [84]
  • Kitabu Taqwa Sakuye Parwaz, yaani Kituo cha Kurukia: Hichi ni kitabu kilichoandikwa na Jalili Jaliliy. Kazi hii Inajumuisha utangulizi na sura tano ndani yake. Mwandishi katika utangulizi ameelezea ufafanuzi na maana ya taqwa pamoja na namna lilivyotumika neno hili ndani ya Qur'an. Sura ya kwanza ya kitabu hichi inahusu chimbuko la taqwa, na sura ya pili, tatu, na nne zinahusiana na taqwa ya kibinafsi, taqwa ya kijamii, na taqwa ya kisiasa. Sura ya tano ya kitabu hichi inajumuisha ndani yake mada kuhusiana na athari (matokeo) za taqwa katika ulimwengu na Akhera. Toleo la kwanza la kazi hii lilichapishwa mnamo mwaka 1400 Shamsia na Chuo Kikuu cha Maarifa ya Kiislamu, ambacho kwa lugha ya akiajemi kinajulikana kwa jina la Intisharat Daaneshgaahe Maarife Islaamiy. [85]