Nenda kwa yaliyomo

Mwandamo wa Mwezi

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Kuangalia Mwezi Mwandamo)
Makala hii inahusu maana ya Istihlal (kuangalia mwezi mwandamo). Kama unataka kufahamu kuhusua kuangalia mwezi mwandamo na hukumu zinazohusiana na hilo, angalia makala ya kuona mwezi mwandamo.
Miongoni mwa vifaa vya kutazamia Mwandamo wa Mwezi

Istihlal (Kiarabu: الاستهلال) ni kuangalia na kutafuta mwezi mwandamo katika usiku wa kwanza wa mwezi wa Hijiria. Ni mustahabu kuangalia mwezi mwandamo na katika baadhi ya wakati ni wajibu Kifai (wakifanya wajibu huo baadhi ya watu, kwa wengine wajibu huo unawaondokea). Baadhi ya ibada za mtu binafsi na za kijamii za Waislamu kama vile kuanza na kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kutekeleza baadhi ya amali katika ibada ya Hija na kuanisha miezi mitakatifu kunafungamana au kutegemea mwanzo na kuanza kwa miezi ya Hijiria. Katika baadhi ya nchi kumeundwa kamati za kuangalia mwezi mwandamo.

Akthari ya wanazuoni wa fikihi mtazamo wao ni kwamba, kuona mwezi mwandamo kwa jicho (bila ya kutumia chombo kama darubini) ndio kigezo cha kuthibiti mwanzo wa mwezi wa Hijiria. Hata hivyo mtazamo wa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa, kuona mwezi kwa kutumia chombo pia ni jambo lenye itibari katika kuthibitisha mwezi mwandamo.

Utambuzi wa Maana (Conceptology) na Nafasi Yake

Kuangalia mbinguni kwa ajili ya kutafuta na kutazama mwezi mwandamo katika usiku wa kwanza wa mwezi wa Hijiria kutambulika na kufahamika kuwa ni Istihlal. [1] Istihlal katika lugha ina maaana ya kunyanyua sauti. [2] Sheikh Mufid anasema, mwezi mwandamo umeitwa kwa jina hili kwa sababu watu wanapouona hupiga takbira na ili kuuonyesa na kuuashiria walikuwa wakipaza sauti zao. [3]

Baadhi ya amali na matendo katika ibada ya Hija na ibada zingine za Waislamu zinafanyika kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu (Hijiria) na moja ya njia za kuainisha na kuthibitisha kuanza kwa mwezi Hijiria ni kuonekana hilali. [4]

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, ni mustahabu kuangalia mwezi mwandamo ingawa katika baadhi ya wakati huwa wajibu, lakini ni wajibu Kifai (wakifanya wajibu huo baadhi ya watu, kwa wengine wajibu huo unawaondokea); [5] kwa mujibu hadithi mbalimbali, kuwa wajibu kufunga Swaumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kumalizika kwake na hivyo kuadhimisha sikukuu ya Eidul-Fitr kunategemea kuonekana mwezi mwandamo. [6] Kadhalika katika fiqh, kuainisha wakati wa kutekeleza amali za ibada ya Hija, kusimama katika jangwa la Arafa, kubakia Mash'ar al-Haram (Muzdalifa) na Mina yote hayo yanafungamana na kuthibiti kuandamana mwezi wa Dhul-Hija (Mfunguo Tatu). [7] Kwa msingi huo, baadhi ya wanazuoni wa fiqh wa Kishia na Ahlu-Sunna wanaamini juu ya kuwa wajib kifai suala la kuangalia mwezi mwandamo wa miezi ya Ramadhani, Shawwal na Dhul-Hija. [8]

Kuangalia Mwezi Mwandamo kwa Jicho na Kutumia Chombo

Wanazuoni wa fiqh wana mitazamo tofauti kuhusiana na namna ya kuangalia mwezi mwandamo. [9] Baadhi ya wanazuoni wa fiqh wa Kishia wanaamini kuwa, kuangalia mwezi kunapaswa kufanyika kwa kutumia jicho la kawaida na kwamba, kuangalia mwezi mwandamo kwa kutumia chombo kama darubini haifai na hilo halina itibari. [10] Ayatullah Ali Khamenei, mmoja wa Marajii wa Kishia na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yeye rai na mtazamo wake ni kwamba, mbali na kutumia jicho kuangalia mwezi mwandamo kwa kutumia chombo pia ni jambo lenye itibari katika kuthibitisha mwezi mwandamo. Ndio maana nchini Iran hutumiwa kamera za darubini kuangalilia mwezi mwandamo. [11] Kwa muktadha inawezekana kwa kutumia darubini mwezi mwandamo ukaonekana, lakini usionekane kwa kutumia jicho la kawaida. Na hivyo kutokana na kuweko misingi tofauti ya kuthibitisha mwezi mwandamo ni jambo la kawaida kuweko hitilafu baina ya wanazuoni na marajii juu ya kutangaza kutimia mwisho wa mwezi wa Hijiria na kuanza mwezi mwingine likiwemo tangazo la kumalizika mwezi wa Ramadhani na kuandama mwezi wa Shawwal ambao huambatana na maadhimisho ya sikukuu ya Eidul-Fitr. [12] Vivyo hivyo mafakihi wa madhehebu ya Ahu-Sunna katika baadhi ya nchi kama Saudi Arabia na mataifa ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi wanaamini kuwa, kuona kwa jicho na bila ya kutumia darubini ni kigezo cha kuthibitisha mwezi mwanadamo. [13]

Kamati ya Kuangalia Mwezi Mwandamo

Nchini Iran kumeundwa Kamati ya Kuangalia Mwezi Mwandamo ikiwa ni kutekeleza agizo la Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kamati hiyo hutuma vikundi mbalimbali katika maeneo tofauti ya nchi kwa ajili ya kuangalia mwezi mwandamo [14] na kutoa ripoti yake kila mwezi. [15] Aidha hii leo mbali na Iran, kuna nchi nyingi zimeunda kamati maalumu za kuangalia mwezi mwandamo.