Sala ya Ijumaa
Sala ya Ijumaa (Kiarabu: صلاة الجمعة) ni ibada sala maalum ya rakaa mbili inayoswaliwa wakati wa adhuhuri siku ya Ijumaa, badala ya sala ya kawaida ya Adhuhuri, na huendeshwa kwa jamaa (kuswaliwa kwa pamoja). Ili sala hii iweze kufanyika, lazima kuwe na idadi ya waumini wasiopungua watano, ambapo mmoja wao atachaguliwa kama ni Imamu wa Sala hiyo. Kabla ya kuanza sala hii, Imamu wa Ijumaa huwajibika kutoa hotuba mbili, ambazo zinabeba maudhui muhimu ya kuwasihi waumini kuwa na uchamungu na kujitahidi kuishi kwa misingi ya haki na maadili. Sala hii ni tukio muhimu la kijamii na kidini, likiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa waumini na kuwaweka karibu na mafundisho ya Mwenye Ezi Mungu.
Hukumu ya kifiqhi kuhusiana na usimamshaji wa Sala ya Ijumaa imetajwa katika Surat Al-Jumu’a. Hadithi mbalimbali zimeitaja Sala ya Ijumaa kuwa ni Hija ya masikini na hupelekea msamaha wa dhambi. Aidha, baadhi ya Hadithi zinasema kuwa kuiacha Sala ya Ijumaa ni chanzo cha unafiki na umasikini. Wakati wa uwepo wa Maimamu Maasumu, Sala ya Ijumaa huwa ni wajibu kwa kila Muislamu, lakini katika kipindi cha ghaiba (kutokuwepo kwa Imamu), kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa fiqhi, Sala hii inakuwa ni wajibu wa chaguo la hiari (wajibu takhyiri). yaani mtu ana hiari ya kusali Adhuhuri au kwenda kusali Sala ya Ijumaa.
Nchini Iran, Sala ya Ijumaa ilianza kuwa maarufu wakati wa utawala wa Shah Ismail Safawi, na tangu hapo imeendelea kuswaliwa katika miji tofauti nchini humo. Tangu kipindi cha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu, Sala ya Ijumaa imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya kidini na sasa inaswaliwa katika miji yote nchini humo, ikijenga mshikamano wa kiimani miongoni mwa Waislamu na kuimarisha uhusiano wa kijamii na kisiasa.
Tangu zama za awali, Sala hii inahisabiwa kuwa ni ibada muhimu sana ya kijamii katika Uislamu, na inajulikana kama alama ya mshikamano wa Waislamu. Pamoja na umuhimu wake wa kidini, kutoka na maudhui za kijamii na kisiasa zinazojadiliwa kwenye hotuba za Sala ya Ijumaa, Sala hii hujulikana pia kwa jina la Ibada ya Kisiasa. Kwa hivyo, imekuwani ibada yenye athari kubwa kiroho na kisiasa, ikiimarisha umoja wa waumini na kuchochea mijadala muhimu kuhusu masuala yanayowahusu Waislamu na jamii kwa ujumla katika maeneo na zama mbali mbali.
Umuhimu na Nafasi ya Sala ya Ijumaa
Sala ya Ijumaa ni moja ya muhimu katika dini ya Kiislamu,[1] inayofanyika kila Ijumaa mchana, ambayo husaliwa kwa mfumo wa Sala ya jamaa. Mkusanyiko wa Sala ni mmoja wa mikusanyiko ya kidini inayofanyika katika ibada mbali mbali. Waislamu hufanya ibada zao mbali mbali kwa njia ya Jamaa (mkusanyiko). Miongoni mwa ibada zifanyazo kwa mfumo wa pamoja ni pamoja na; sala za kila siku, mikusanyiko ya Sala ya Eid al-Adha na Eid al-Fitr, pamoja na ibada ya Hija. Kwa hivyo, Sala ya Ijumaa inachukuliwa kuwa ni moja ya matukio makuu manne yenye mikusanyiko ya Waislamu. [2]
Sala ya Ijumaa inachukuliwa kama ashirio la kuwepo kwa ridhaa za wananchi juu ya uwepo wa uongozi wa Kiislamu nchini mwao, [3] na mara nyingi huitwa «Sala ya Ibada ya Kisiasa». [4] Sala hii ni chombo muhimu cha kuelimisha na kuongoza jamii, [5] na ina mchango mkubwa katika kuimarisha welewa na kusambaza poropaganda mbali mbali za kidini. [6] Aidha, Sala ya Ijumaa ina uwezo wa kuwa ni jukwaa la mawasiliano ya umma inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga siasa za jamii. Sala ya Ijumaa ilikuwa na umuhimu mkubwa mno katika nyakati za utawala wa Banu Umayya na Banu Abbas. Katika zama hizo za hisia za ibada ya Sala ya Ijumaa zilipungua polepole, na mwishowe Sala hii ikatumika kuwa ni nembo na kauli mbiu ya utawala wa zama hizo. [7]
Umuhimu wa Sala ya Ijumaa katika Qur'an na Hadithi
Katika Qur'an, Surat Al-Jumu’a ndiyo Sura itoayo mwanga kamili kuhusiana na umuhimu wa Sala ya Ijumaa, ikisisitiza kwa uwazi umuhimu wa waumini kuacha shughuli za kawaida na kushiriki katika ibada hii. Sura hii inasisitiza kuwa; kipindi cha Sala ya Ijumaa ni kipandi muhimu kinachotakiwa waumini kujali na kujitayarisha kwa ajili ya Sala hii. Aidha kuna kiasi cha Hadithi 200 takriban, zinazohusiana na Sala ya Ijumaa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Maimamu (a.s). [8] Hadithi hizi zinathibitisha kuwa kushiriki katika Sala ya Ijumaa kunachangia waja kupata msamaha wa dhambi zao zilizo tangulia, [9] kupunguza mashaka ya Siku ya Kiyama, [10] na kupata thawabu kubwa kwa kila hatua inayochukuliwa kuelekea kwenye ibada hii. [11] Pia, Hadithi zinaeleza kuwa Mwenye Ezi Mungu atawakinga na kuwaharamishia adhabu ya Moto wale waumini wanaoshiriki katika Sala ya Ijumaa. [12] Kukosa kushiriki katika Sala ya Ijumaa kunachukuliwa kuwa na athari mbaya katika maisha ya muumini, ikiwa ni pamoja na kuwa na mafadhaiko na kukumbwa na ukosefu wa baraka. [13] Imeripotiwa Katika historia kwamba; Ali bin Abi Talib (a.s) aliwachia huru baadhi ya wafungwa kutokana na kushiriki kwao katika Sala ya Ijumaa. [14] Hii inaonesha umuhimu mkubwa wa Sala ya Ijumaa katika jamii ya Kiislamu, ikithibitisha jinsi ilivyozingatiwa kama hatua muhimu katika maisha ya kiroho na kijamii. Faidh Kashani, faqihi na mwanahadithi wa karne ya kumi na moja, ameielezea Sala ya Ijumaa kuwa ni mojawapo ya ibada zenye fadhila zaidi katika Uislamu. [15] Aidha, baadhi ya Hadithi zinaeleza kwamba; Sala ya Ijumaa ni sawa na Hija kwa wanyonge, ikiashiria umuhimu wake mkubwa kama ibada ya kiroho na kijamii kwa wale ambao hawawezi kufika Makka kwa ajili idaba ya Hija. [16]
Kuendeshwa kwa Sala ya Ijumaa katika Maeneo Tofauti ya Kiislamu
Ibada ya Sala ya Ijumaa imekuwa ikitekelezwa tangu nyakati za Mtume Muhammad (s.a.w.w) mjini Madina na imeendelea kufanyika kupitia nyakati za Makhalifa katika miji ya Makhalifa pamoja na maeneo mengine mbali mbali. [17] Sababu kama ukupanukaji wa miji, kuwepo kwa madhehebu na mitindo tofauti, pamoja na mambo ya kisiasa na kiusalama, yamepelekea kuanzishwa kwa Sala za Ijumaa kadhaa katika maeneo na miji mbali mbali. [18] Kulingana na ripoti ya Ibn Battuta; mnamo karne ya saba, Sala ya Ijumaa ilisaliwa katika misikiti kumi na moja huko Baghdad. [19] Katika kipindi cha mamlaka na uongozi wa Mamluki, ongezeko la idadi ya watu lilipelekea Sala ya Ijumaa kusaliwa katika misikiti ya mitaani pamoja madrasa za dini. [20] Inasemekana kuwa; Sala ya Ijumaa yenye idadi kubwa zaidi kati ya Waislamu ni ile inayofanyika mjini Makkah kabla ya mahujaji kuondoka kuelekea kanda ya Arafat, ambapo mahujaji kutoka kila pembe ya dunia hushiriki katika Sala hiyo. [21]
Uwajibu wa Sala ya Ijumaa
Waislamu wanakubaliana kwa kauli moja kwamba; Sala ya Ijumaa ni wajibu. Wafaqihi wa Shia pamoja na Ahlu-Sunna hutumia Aya ya 9 ya Surat Al-Jumu’a, Hadithi mbalimbali [22] pamoja na ijmaa (makubaliano ya jumla), kuthibitisha wajibu wa Sala ya Ijumaa, na kuonyesha kwamba wale wanaokataa kushiriki katika sala hii wanastahili adhabu. [23] Hata hivyo, wajibu wa Sala ya Ijumaa haujumuishi wanawake ndani yake, wasafiri, wagonjwa, walemavu, watumwa, na wale walio mbali zaidi ya farsakh mbili (kila farsakh ni sawa na kilomita 5 na nusu) kutoka mahali pasaliwapo Sala ya Ijumaa. [24]
Vyanzo vya fiq’hi vya madhehebu vya madhehebu mbali mbali ya Kiislamu, vinaijadili Sala ya Ijumaa kwa kina kabisa katika mlango maalum uitwao “Kitabu Al-Sala”. [25] Kuandika vitabu tasnifu za kifiq’hi kuhusiana na Sala ya Ijumaa, ni moja ya kazi muhimu za utafiti wa kidini tangu nyakati za mapema, za kuanzishwa kwa vyuo vya kidini. Hii ni kutokana na umuhimu wa mkubwa wa Sala ya Ijumaa katika jamii ya Kiislamu. [26] Katika kipindi cha utawala wa Safawiyya, baada ya kuenea kwa Sala ya Ijumaa nchini Iran, uandishi wa tasnifu maalumu kuhusana na ibada hii ulizidi kukolea rangi katika vyuo mbali mbali. [27] Wanafaq’hi wengi maarufu walitunga tasnifu na vitabu chungu nzima, juu ya Sala ya Ijumaa kupitia lugha tofauti, ikiwemo Kiarabu na Kifarsi. Baadhi ya tasnifu na vitabu hivyo; ima vilikuwa ni majibu dhidi ya tasnifu nyingine zilizo andikwa na wanazuoni wengine, au ni hoja tetezi juu ya umuhimu uwajibu wa Sala ya Ijuma. [28]
Marufuku ya Kuuza na Kununua Wakati wa Sala ya Ijumaa
Kulingana na Aya ya 9 ya Surat Al-Jumu’a, ni marufuku kufanya biashara (kuuza na kununua) wakati wa Sala ya Ijumaa. Aya hii inasisitiza kwamba wakati wa Sala ya Ijumaa, waumini wanapaswa kuacha shughuli hizi ili kuipa kipaumbele ibada ya Sala ya Ijumaa. Kwa mujibu wa Aya ya 10 katika Sura hiyo hiyo, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa, hakuna vikwazo vilivyo wekwa kuhusiana na manunuzi, mauzo, au shughuli nyingine yoyote kama vile kutembelea wagonjwa au kukutana na ndugu mbali mbali wa kiimani. Hii inaashiria kwamba shughuli hizi zinapaswa kuahirishwa hadi baada ya kumalizika kwa ibada ya Sala ya Ijumaa, ili kuzingatia umuhimu wa ibada hiyo katika maisha ya kiroho na kijamii. [29]
Kwa mtazamo wa Ayatullahi Jawadi Amuli, mfasiri maarufu wa Qur'an, ni kwamba; sentensi isemayo: وَذَرُوا الْبَیْعَ (Na acheni mauzo) iliyoko kwenye Aya ya 9 ya Surat Al-Ijum’a, haihusiani tu shughuli za kibiashara kama kununua na kuuza. Kwa mujibu wa tafsiri, Aya hii ina maana pana zaidi kuliko hiyo, nayo imaanisha kuacha shughuli zote zinazo weza kumzuia mtu kushiriki katika Sala ya Ijumaa. Kwa hivyo, yeyote anayejihusisha na shughuli yoyote inayomkosesha nafasi ya kwenda kushiriki Sala hii, atakuwa anatenda dhambi, ingawa amali za manunuzi na mauzaji yake kulingana na hukumu za kisheria, itakuwa ni halali na sahihi. Aidha, Ayatullah Amuli anafafanua kuwa; ikiwa mtu atanunua au kuuza akiwa njiani kuelekea Sala ya Ijumaa, hakuna tatizo kwa kuwa haingiliani na nia yake ya kuhudhuria Sala hiyo. [30]
Hukumu ya Sala ya Ijumaa katika Kipindi cha Ghaiba (Kutokuwepo Imamu Maasumu)
- Makala Asili: Sala ya Ijumaa Katika Kipindi cha Ghaiba
Kusimamisha Sala ya Ijumaa katika kipindi cha ghaiba (kutowepo Imamu Maasum) ni suala lenye mijadala mingi miongoni mwa mafaqihi wa upande wa madhehebu ya Shia. Baadhi ya mafakihi wameona kuwa Sala hii ni haramu, hii inatokana na iamni ya kwamba; Sala hii inahitaji uwepo wa Imamu Maasum au mteule wake ili iweze kuthibiti. Kwa upande mwingine, mafakihi wengine wamesema kuwa Sala ya Ijumaa ni wajibu wa lazima (wajibu ta'yini) na inapaswa kusimamishwa kila inapowezekana, mradi tu kuwe na ruhusa kutoka kwa hakimu mwadilifu. Hata hivyo, kundi jingine la mafakihi linaihisabu Sala ya Ijumaa kuwa ni wajibu wa hiari (wajibu takhyiri), ambapo waumini wanaweza kuchagua kati ya Sala ya Ijumaa na Sala ya Adhuhuri. [31]
- Baadhi ya mafakihi wa awali wa madhehebu ya Shia, kama vile Sallar Dailami [32] na Ibn Idris Hilli, [33] pamoja na baadhi ya mafakihi wengine waliokuja baadae, kama Fadhil Hindi, wanaiona Sala ya Ijumaa kuwa ni amali inayo tegemea uwepo wa Imamu Maasum au mtu aliyeteuliwa na Imamu Maasum kuongoza Sala ya Ijumaa. [34] Kwa mtazamo huu, itakuwa ni haramu kusimamisha Sala ya Ijumaa katika kipindi cha ghaiba, kwa kuwa hakutakuwa na uwepo wa moja kwa moja wa Imamu Maasum au mteule wake katika kuongoza ibada hiyo.
- Fat'wa ya Wajibu usio na hiari wala mwenza (Wujubu Ta'yini) Kuhusu Sala ya Ijumaa Katika Kipindi cha Ghaiba, ni mtazamo mwingine kuhusiana na Sala ya Ijumaa katika kipindi cha ghaiba. [35] Kwa mujibu wa fatwa hii; Sala ya Ijumaa ni wajibu wa lazima (wujubu ta'yini) usio na mwenza. Mtazamo huu unasisitiza kwamba; Sala ya Ijumaa inapaswa kusimamishwa kila pale wakana na zama zinaporuhusu kufanya hivyo, bila kuhitaji uteuzi maalum kutoka kwa Imamu Maasum. [36] Hata hivyo, kunahitajika kuwepo kwa ruhusa kutoka kwa hakimu au Imamu mwadilifu. [37] [38] Mafaqihi kama Shahidu Thani na mjukuu wake, [39] ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Al-Madarik, [40] ni miongoni mwa wanazuoni waliokuwa wakishikilia msimamo huu. Msimamo huu ulienea sana katika kipindi cha utawala wa Safawiy, hii ni kutokana na hali ya kijamii na kisiasa iliyokuwepo wakati huo, ambapo ilionekana kuwa ni muhimu kuimarisha umoja wa jamii kupitia Sala ya Ijumaa hata bila uwepo wa Imamu Maasum. [41]
- Mtazamo wa Wajibu wa Hiari au wajibu mwenza (Wujubu Takhiyiri), katika Kipindi cha Ghaiba. Mafakihi wengi wa zama za kati na wa zama za hivi sasa, ikiwa ni pamoja na Muhakkik Hilli, [42] Allama Hilli, [43] Ibn Fahd Hilli, [44] Shahidu Awwal [45] na Muhakkik Karaki, [46] wanakubaliana na mtazamo wa wajibu wa hiari au mwenza (wujubu takhiyiri) kuhisiana na hukumu za Sala ya Ijumaa. Kulingana na mtazamo huu, katika nyakati za adhuhuri za siku ya Ijumaa, mtu anaweza kuchagua kati ya kusali Sala ya Ijumaa au Sala ya adhuhuri. [47] Mtazamo huu wa wajibu wa hiari umeenea na kupokelewa miongoni mwa mafakihi wa baadae. Fikra za mtazmo huu zilianzia karne ya kumi na tatu na kuendelea hadi sasa, na umeonekana kuwa ndiyo mtazamo rahisi kwa waumini wanaoishi katika kipindi cha ghaiba, ambapo hali ya kusimamisha Sala ya Ijumaa bila uwepo wa Imamu Maasum inaonekana kuwa na mapungufu fulani. [48]
Jinsi ya Kusimamisha Sala ya Ijumaa
Kusimamisha Sala ya Ijumaa kunajumuisha hatua muhimu zinazohitajika kwa utekelezaji sahihi wa ibada hii. Hatua za mwanzo ni kuwasilisha khutba mbili (hotuba), ambazo hutolewa na kiongozi (imamu) wa Sala hiyo. Baada ya khutba hizi, hufuatia Sala ya Ijumaa kwa kuswali rakaa mbili za jamaa (kwa pamoja), kwa nia ya Sala ya Ijumaa. Katika Sala ya Ijumaa, rakaa hizi mbili huambatana na qunut ambayo ni sunna ndani yake. Qunut ya kwanza hufanyika kabla ya kurukuu rakaa ya kwanza, na qunut ya pili hufanyika baada ya ruku katika rakaa ya pili.
Masharti ya Kusimamisha Sala ya Ijumaa
Kwa mujibu wa mafakihi wengi wa Shia, [49] ili Sala ya Ijumaa isimame kisheria, ni lazima kuwepo na angalau watu watano, [50] ingawa baadhi yao wanawajibisha kuwepo idadi ya watu saba. Kwa upande mwingine, madhehebu ya Hanafi yanahitaji uwepo wa watu watatu ukiachana na Imam wa Sala hiyo, wakati madhehebu ya Shafi'i na Hanbali yanahitaji angalau kuwepo watu arobaini. Madhehebu ya Maliki, kwa upande wake, inahitaji angalau watu kumi na mbili waishiwo ndani ya mji huo huo, yaani wasiwe baadhi yao ni wageni kutoka mji mwengine. [51] Aidha, kwa mujibu wa mafakihi wa madhebu ya Shia, ni lazima kuwe na angalau umbali wa farsakh (kilomita 5 hadi 5 na nusu) moja kati ya vituo (miskiti) ya Sala za Ijumaa mbali mbali. Ikiwa masharti haya hayatazingatiwa, Sala ya Ijumaa ya itakayotangulia kusaliwa miongoni mwa misikiti hiyo, ndiyo itakayokubalika na kusihi kisheria, na sala zote zitakazo saliwa baada yake zitakuwa ni batili, kwa sababu ya umbali wa katika ya misikiti mmoja hadi mwengine, ni muhimu kwa ajili ya kupata uhalali wa ibada hii. [52]
Mahali pa Kusimamisha Sala ya Ijumaa
Sala ya Ijumaa mara nyingi hufanyika katika msikiti mkuu wa mji, ambao unaweza kujulikana kwa majina tofauti, kama vile; Msikiti Mkuu au Msikiti wa Ijumaa. [53] Majina haya hutegemea na hadhi ya msikiti na umuhimu wake katika kuandaa mikusanyiko mbali mbali, ikiwemo Sala ya Ijumaa. [54] Katika baadhi ya miji na baadhi ya nchi, huwa kuna maeneo maalum yanayojulikana kama Musalla, ambapo Sala ya Ijumaa husaliwa ndani yake. Mifano ya maeneo hayo ni msikiti wenye jina la Musalla Bozorge Tehran ulioko mjini Tehran, Musalla Quds ulioko Qom, na Musalla Shahid Mazari ulioko mjini Kabul Afghanistan. Maeneo haya ni maalum kwa ajili ya mikusanyiko mikubwa ya ibada, na mara nyingi huwa eneo la kutosha kwa ajili ya kuhamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa waumini.
Hotuba za Sala ya Ijumaa
Hotuba za Sala ya Ijumaa ni sehemu muhimu ya ibada hii, ambapo huwa zinachukua nafasi ya rakaa mbili za mwanzo za Sala ya Adhuhuri. [55] Kwa mujibu wa mafaqihi na wanazuoni wengi wa Kiislamu, hotuba hizi lazima zianze kutolewe baada ya kuingia muda wa Sala ya Adhuhuri kisheria. [56] Kulingana na madhehebu mbalimbali, hotuba hizi zinapaswa kuwa na vipengele vya msingi ndani yake, kama vile kumshukuru Mwenye Ezi Mungu, kumtakia rehema na amani Mtume Muhammad (s.a.w.w), kutoa nasaha, kuhimiza uchaji-Mungu, pamoja na kusoma Sura fupi za Qur'ani ndani yake. [57] Waislamu wanaoswali wanapaswa kuacha shughuli zote zitakazopelekea kutosikiliza khutba hizo, ikiwemo kuzungumza pamoja na kuswali. [58] Kama alivyosema Shahid Murtaza Mutahhari, Qur'ani inazitaja hotuba hizi kama ni «dhikri ya Allah» (utajo wa Mungu), kwa sababu zinaelekeza fikra na roho ya ukumbusho wa Mwenye Ezi Mungu uliomo ndani yake. [59]
Katika moja ya Hadithi kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), kila moja kati ya hotuba mbili hizi, huwa na malengo yake maalumu. Hotuba ya kwanza hulenga kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu, na hotuba ya pili inahusiana na mambo muhimu ya kijamii na kiroho, ikiwemo; mawaidha, dua, amri na maagizo mbali mbali, na tahadhari zinazolenga maslahi ya jamii ya Kiislamu. Ambayo yote hayo huw ni kwa ajili ya kuikielekeza jamii ya waumini katika kufuata mwenendo mwema. [60]
Namna ya Sala ya Ijumaa na Qunuti Zake
Baada ya hotuba mbili za mwanzo, rakaa mbili za Sala ya Ijumaa huswaliwa. Ni mustahabu (inapendekezwa) kusoma Surat Al-Jumu'a kwenye rakaa ya kwanza na Surat Al-Munafiqun kwenye rakaa ya pili, au Surat Al-A’la kwenye rakaa ya kwanza na Surat Al-Ghashiya kwenye rakaa ya pili baada ya kumaliza kusoma Surat Al-Fatiha kwenye kila rakaa ya Sala hii. Pia, inashauriwa (ni mustahabu) kusoma Sura hizi kwa sauti kubwa (jahar). [61] Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kishia, kusoma qunut katika rakaa ya kwanza kabla ya kurukuu, na katika rakaa ya pili baada ya kurukuu, ni miongoni mwa mustahabu za Sala hii. Hii inatoa nafasi kwa waumini kumwomba Mola wao na kutafuta ukuruba wa kuwa karibu Naye kupitia dua na maombi haya maalum yaliomo katika Sala hii muhimu. [62]
Imamu wa Sala ya Ijumaa
- Makala asili: Imamu wa Sala ya Ijumaa
Imamu wa Sala ya Ijumaa anapaswa kuwa na sifa maalum zinazozidi zile zinazohitajika kwa ajili ya Imamu wa sala za kawaida. [63] Sifa hizi ni pamoja na uwezo wa kuzungumza kwa ufasaha, ujasiri, na awe na welewa tosha wa masuala yanayo wakabili Waislamu, ili kuwasilisha kwa uwazi masuala hayo mbele ya Waislamu wanao hudhuria ibada hii muhimu. Aidha, Inapendekezwa Imamu wa Sala ya Ijumaa awe ni miongoni mwa watu wenye elimu kubwa, heshima, na imani thabiti kuliko wengine. [64] Mwanazuoni wa Kishia wa karne ya saba, Muhaqqiq al-Hilli, aliongeza sifa nyengine za ziada juu ya sifa hizo zilizotajwa hapo mwanzo, ikiwemo; ukamilifu wa akili, imani (mfwasi wa madhehebu ya Shia Ithna Ashariyya), pamoja na uadilifu. Yeye ameyahisabu hayo kuwa ni masharti muhimu kwa ajili ya Imamu wa Sala ya Ijumaa. [65] Vilevile, imesisitizwa katika mafunzo ya Kiislamu kwamba mwanamke hawezi kuwa Imamu wa Sala ya Ijumaa, hii ni kwa sababu hudhurio la wanawake si miongoni mwa nguzo za sala hii, na kwamba Sala hii inawalenga wanaume peke yao. [66]
Ingawa Shi'a na baadhi ya wanazuoni wa Sunni hawajaweka masharti ya lazima ya kuomba ruhusa kutoka kwa mtawala au kiongozi wa wakati huo ili kuhalalisha Sala ya Ijumaa, na mfano mzuri wa historia tendo la Imamu Ali (a.s), la kuongoza Sala ya Ijumaa katika kipindi cha kuzingirwa kwa Khalifa Othman. Ila kinacho onekana katika zama mbali ni kwamba Sala ya Ijumaa siku zote ilikuwa ikionekana kuwa ni mambo yalioko katika mamlaka ya serikali. [68]
Maimamu Maarufu wa Sala ya Ijumaa
Baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, Sala ya Ijumaa ilipewa umuhimu mkubwa, na wanazuoni mashuhuri waliteuliwa kuongoza ibada hii muhimu nchini humo. Miongoni mwao, Sayyid Mahmoud Taaleqaniy [69] na Sayyid Ali Khamenei ndio maimamu maarufu walioteuliwa na Imamu Khomeini kuongoza Sala ya Ijumaa mjini Tehran. [70] Viongozi hawa walikuwa na nafasi muhimu katika kusimamia siasa na masuala muhimu ya kidini wakati wa kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo. Katika mji wa Qom, Ali Mishkini Ardabili [71] na Abdullah Jawadi Amuli [72] walikuwa ni miongoni mwa wanazuoni wenye ushawishi mkubwa mjini humo. Wanazuoni hawa ndio waliokuwa na jukumu la kuongoza Sala ya Ijumaa, wakitoa nasaha na miongozo kwa Waislamu wa Kishia katika jamii ya watu wa mji huo. Nchini Iraq, baada ya kuanguka kwa utawala wa Ba’ath (wa Saddam Hussein), viongozi mashuhuri kama vile Abdul-Mahdi Karbalai na Sayyid Ahmad Safi ndiwo walipewa jukumu la kuongoza Sala ya Ijumaa katika mkoa wa Karbala, wlishikila nafasi hizo wakiwa ni wawakilishi wa Ayatullahi Sayyid Ali Sistani, marjaa (mwanafiq’hi) mkubwa wa Kishia nchini Iraq. [73] Viongozi hawa walishika jukumu muhimu katika kuongoza na kudhibiti mivutano ya kisiasa na kidini nchini humo baada ya mabadiliko makubwa ya utawala wa Saddam Hussein.
Viongozi waliokumbwa na ukatili wa kigaidi na kuuawa kupitia mashambulio ya kigaidi katika kipindi cha miaka ya 1360 Shamsia nchini Iran, walijulikana kwa jina la Mashahidi wa Mihraab. [74] Nchini Iraq, Sayyid Muhammad Baqir al-Hakim, aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Kishia, aliuawa mwaka mnamo mwaka 1382 Shamsia baada ya kumaliza kuongoza Sala ya Ijumaa katika Haram ya Imam Ali. Shambulizi ambalo lililosababisha vifo vya watu wengi ndani yake. [75] Kabla yake, Sayyid Muhammad Sadr -aliyekuwa akiongoza Sala ya Ijumaa [76] katika mji wa Kufa chini ya utawala wa Saddam Hussein- pia naye aliuawa mnamo mwaka 1377 Shamsia kufuatia tukio la kigaidi. [77]
Historia ya sala ya Ijumaa
Ushiriki wa Maimamu katika Sala ya Ijumaa
Kupitia mtazamo wa madhehebu ya Shia, maimamu wa Sala ya Ijumaa walioteuliwa kupitia watawala dhalimu, wanaotambulika kama ni Hukkam al-Jawr (watawala wa kidhalimu), hawana haki wala uhalali wa kisheria wa kuongoza ibada hiyo. Kwa mtazamo huu, haijuzu wala si sahihi kwa wafuasi wa madhehebu ya Shia kusali nyuma ya viongozi kama hawa. Hata hivyo, kutokana na dhana ya taqiyya —yaani, kuficha imani ili kuepukana madhara au mateso— kuna Hadithi kadhaa zinazo simulia ushiriki wa Maimamu wa Kishia pamoja na wafuasi wao katika Sala za Ijumaa zilizo ongozwa na watawala wa aina kama hiyo. [87] Hii ilikuwa ni njia ya kulinda usalama wao katika mazingira ya kisiasa yenye ghasia na dhuluma mbali mbali kutokana na watawala hao. Aidha kwa upande wa pili, wapinzani wa tawala dhalimu, mara nyingi walikataa kushiriki katika Sala ya Ijumaa kama ni ishara ya upinzani na kutoridhika kwao na utawala wa kidhalimu. [88] Kukosa kuhudhuria Sala ya Ijumaa mara kwa mara katika hali kama hizi, lilikuwa ni ishara ya kutengwa kwa watu binafsi na jamii, na mara nyingi lilionekana kama kitendo cha kijamii cha kutokuwa na ushirikiano na utawala husika. [89]
Utekelezaji wa Sala za Ijumaa kwa Upande wa Mashia
Katika kipindi cha “Ghaybatu al-Kubra” (Tukio Kubwa la Kutokuwepo kwa Imamu Mahdi), mafaqihi wa umande wa madhdhebu ya Shia waliokuwa ndani ya jamii bila ya kuwa na mamlaka ndani yake, walikuwa na tahadhari kubwa kuhusiana na kutekeleza Sala ya Ijumaa. Mara nyingi walionekana kususia na kutoshiriki katika Sala za Ijumaa zilizokuwa zikiongozwa na watawala wa dhalimu. Hata hivyo, kuna matukio machache katika historia, ambapo Sala ya Ijumaa imeripotiwa kufanyika kupitia wanazuoni wa madhehebu ya Kishia, hasa katika nyakati za utawala wa Aalu Buwaihi (Buwaihids) na Hamdanian (Hamdanids). [90]
Moja ya taarifa za awali kuhusu utekelezaji wa Sala ya Ijumaa katika jamii za Shia ni ile iliyoripotiwa kufanyika katika Msikiti wa Baratha au Buratha (msikiti wa Shia huko Baghdad), iliyofanyika mnamo mwaka wa 329 Hijiria, chini ya uongozi wa Ahmad ibn Fadhli Hashimi. [91] Hata katika kipindi cha machafuko ya mnamo mwaka wa 349 Hijiria, ambapo Sala ya Ijumaa ilisimamishwa mjini Baghdad, bado Msikiti wa Baratha uliendelea kusali Sala ya Ijumaa. [92] Hata hivyo, mnamo mwaka 420 Hijiria, baada ya kuteuliwa kwa imamu wa Kisunni kupitia khalifa wa zama hizo, Sala ya Ijumaa ilisimamishwa kwa kipindi cha muda fulani. [93] Mnamo mwaka 359 Hijiria kuna dalili za kufanyika kwa ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ibn-Tuuluun, na mnamo mwaka 361 Hijiria kuna dalili za kusaliwa Sala hiyo katika Msikiti wa Azhar. [94] Pia kuna dalili ziashiriazo kuwa ibadi ilianza kutekelezwa ndani ya miji hiyo tokea zama za amani zaidi kuliko hapo. [95] Msukumo mkubwa wa kufufua Sala ya Ijumaa miongoni mwa Shia, ulianza baada ya kuanzishwa kwa utawala wa Shia wa Safawiy nchini Iran. Utawala wa Safawiy ulileta mabadiliko muhimu ya kisheria na kijamii, na hivyo kusababisha kuimarika kwa utekelezaji wa Sala ya Ijumaa na kurudisha hadhi yake kama ibada muhimu katika jamii za Shia. [96]
Sala ya Ijumaa Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
- Makala Asili: Sala ya Ijumaa Tehran na Sala ya Ijumaa Isfahan
Kulingana na maelezo ya Abduljalil Qazwini, mwandishi maarufu wa Kishia wa karne ya sita Hijiria, Sala ya Ijumaa imekuwa ikitekelezwa katika miji yote mikubwa yenye idadi kubwa ya Wakazi wa Kishia nchini Iran. Alibainisha katika maandishi yake akisema kwamba; miongoni mwa miji muhimu isimamishayo Sala ya Ijumaa kwa utaratibu rasmi ni paomja na; Qom, Aveh, Kashan, Varamin, pamoja na maeneo ya Mazandaran. [97]
Enzi za Utawala wa Safawiyya (Safavids) na Kuenea kwa Sala ya Ijumaa
Sala ya Ijumaa ilianza kupata umaarufu na kuenea katika jamii za Kishia nchini Iran wakati wa utawala wa Shah Ismail wa Kwanza wa Safawiyya (Safavids) (905-930 Hijiria). Miongoni mwa sababu zilizochangia kuimarika kwa ibada hii ni ukosoaji uliokuwa ukitolewa na Dola ya Othmaniyya (Ottoman Empire) dhidi ya Mashia kwa kutoendeleza Sala ya Ijumaa, pamoja na juhudi za wanazuoni wa Kishia nchini Iran katika kuamsha na kuhamasisha jamii kuhusiana na umuhimu wa Sala hii, hususan Muhaqqiq Karaki. [98] Ili kujenga uhalali wa Sala ya Ijumaa ndani ya jamii za Kishia, wanazuoni wa wakati huo walipaswa kwenda hatua kwa hatua katika kueneza na kutekeleza Sala hii. [99] Hii ni kwa sababu ya kwamba; utamaduni wa kusimamisha Sala ya Ijumaa haukuwa umejengeka na kuzoeleka vyema miongoni mwa Waislamu wa Kishia, jambo ambalo lilipelekea kuwepo kwa upinzani kutoka kwa baadhi ya wanazuoni. [100] Mijadala kuhusu hukumu ya Sala ya Ijumaa katika kipindi cha ghaiba ya Imam Maasum, na kwamba je, ni wajibu au haramu kusimamisha ibada hii, ilifikia kilele chake wakati wa utawala wa Shah Suleiman wa Kwanza wa Safawiyya (Safavids), (ima kuanzia mwaka 1077 au 1078 hadi 1105 Hijiria). Hali hii hatimae ilisababisha Shah Suleiman kuitisha kikao cha mafaqihi, alichoshiriki yeye mwenyewe pamoja na Waziri wake Mkuu, ili kupata maelewano na kutoa uamuzi wa pamoja kuhusiana na sala hii. [101]
Wakati wa utawala wa Shah Tahmasb wa Kwanza (930-984 Hijiria), kwa ushauri wa Muhaqqiq Karaki, alichukua uamuzi wa kuteua maimamu wa Ijumaa kwa kila mji, hatua iliyosaidia kuimarisha utamaduni wa Sala ya Ijumaa. [102] Aidha, wakati wa Shah Abbas wa Kwanza (996-1038 Hijiria), nafasi ya Imamu wa Ijumaa ilianzishwa rasmi na kupewa hadhi maalumu katika zama hizo. [103] Kwa kawaida Sheikh al-Islam (cheo cha mwisho cha wanazuoni wa zama hizo) wa kila mji, ndiye alikuwa na jukumu ya kusimamisha Sala hiyo. Hata hivyo, baadhi ya wakati wanazuoni wakubwa kama vile Faidh Kashani (aliyefariki mwaka 1091 Hijiria) waliombwa kuchukua nafasi ya Imamu wa Ijumaa na mfalme wa zama hizo. [104]
Sala ya Ijumaa ya kwanza katika enzi za Safawiyya (Safavids) iliongozwa na Muhaqqiq Karaki katika Msikiti wa Jami’u ‘Atiiq wa Isfahan. [105] Maimamu wengine maarufu wa Ijumaa katika kipindi hichi ni pamoja na Sheikh Baha’i (aliyefariki 1030 au 1031 Hijiria), Mir Damad (aliyefariki 1041 Hijiria), Muhammad Taqi Majlisi (aliyefariki 1070 Hijiria), na Muhammad Baqir Majlisi (aliyefariki 1110 au 1111 Hijiria), Muhammad Baaqir Sabzewari (aliyefariki mnamo mwaka 1090 Hijiria), na Lutfullahi Isfahani (aliyefariki mnamo mwaka 1032 Hijiria). [106] Katika kipindi hichi, ilishamiri mno kazi ya kuandika vitabu vya khutba za Sala ya Ijumaa. Moja ya vitabu maarufu zaidi vya khutba hizo ni «Basatin al-Khutabaa» kilichoandikwa na Mirza Abdullah Afandi (aliyefariki mnamo mwaka 1130 Hijiria), ambacho kilisaidia kueneza maarifa kuhusiana na khutba na utekelezaji wa Sala ya Ijumaa. [107]
Enzi za Qajar na Uteuzi wa Maimamu wa Sala ya Ijumaa
Katika kipindi cha utawala wa Qajar (1210-1344 Hijiria), wadhifa wa Imamu wa Sala ya Ijumaa uliendelea kuwa na hadhi ya kiserikali, sawa na ilivyokuwa katika enzi za utawala wa Safawiyya (Safavids). [108] Majina ya maimamu wa Ijumaa wa miji mikuu ya wakati wa utawala ya Safawiyya (Safavids) (1148-1210 Hijiria) na Qajar yaliotajwa katika vyanzo mbali mbali, yanaonesha umuhimu na hadhi ya nafasi ya uimamu wa Ijumaa wa nyakati hizo. Vyanzo hivyo vinaonesha kwamba; nafsi ya uimamu wa Sala ya Ijumaa wakati mwengine ilikuwa ikishililiwa kwa njia ya urithi wa kifamilia, na katika miji mingi, familia fulani ndizo zilizokuwa zikichukua jukumu la kuongoza Sala ya Ijumaa kizazi baada ya kizazi. [109] Miongoni mwa familia zilizoongoza ibada hii kizazi baada ya kizazi, ni familia ya Khaatun Abadi mjini Tehran, familia ya Majlisi huko Isfahan, na familia ya Muhammad Muqim Yazdi katika mji wa Yazd. Mfumo huu wa urithi wa wadhifa wa Imamu wa Ijumaa uliimarisha nafasi ya familia hizi katika jamii na kuwapa ushawishi mkubwa wa kidini na kisiasa. [110]
Sala ya Ijumaa na Utawala wa Pahlawi (Pahlavi dynasty)
Nafasi ya maimamu wa Sala ya Ijumaa katika zama za utawala wa Pahlavi (1304-1357 Hijria Shamsia), -hasa katika miji mikubwa kama Tehran- ilikuwa imeunganishwa na serikali. Uhusiano rasmi baina ya maimamu na serikali ulipelekea kupungua kwa umaarufu wao miongoni mwa wananchi, hali iliyosababisha kungukwa kwa hamu za wananchi katika kuhiriki Sala za Ijumaa katika miji kadhaa ya Iran. [111] Licha ya hali hii, baadhi ya wanazuoni wa Kishia waliendelea kusimamisha Sala ya Ijumaa kwa kufuata fatwa zao, hali ambayo ilipelekea waumini kuvutiwa zaidi na Sala zisalishwazo na wanazuoni hao. [112] Miongoni mwa wanazuoni waliosalisha Sala za Ijumaa pila kujali hisia za serikali ni; Sayyid Muhammad Taqi Khansari, Muhammad Ali Araki na Sayyid Ahmad Shubayri Zanjani, ambao waliendesha Sala zao za Ijumaa katika Msikiti wa Imamu Hassan al-Askari (a.s) uliopo mjini Qom. [113] Mmoja wa wanazuoni muhimu walioendesha Sala za Ijumaa kulingana na vigezo sahihi vya kidini ni; Sayyid Muhammad Taqi Ghadhanfari aliyekuwa Imamu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Khwansar kuanzia mwaka 1310 Hijiria hadi kufariki kwake (mnamo mwaka 1350 Hijiria). Wanazuoni wengine walioongoza Sala za Ijumaa katika maeneo mbalimbali ya Iran ni pamoja na; Hussein Ali Muntadhiri aliyekuwa akisalisha mjini Najafabad, Haj Agha Rahim Arbab [114] na Sayyid Jalaluddin Taahiri waliokuwa wakisalisha mjini Isfahan, mwengine ni Sayyid Muhammad Hussein Tehrani aliyesimamia Sala ya Ijumaa mjini Tehran. [115] Wanazuoni hawa waliweka msingi wa mwamko mpya wa Sala ya Ijumaa, ambao ulizidi kuongezeka kadiri wananchi walivyoanza kupendelea kushiriki Sala hizi. Hii ni kutokana na misimamo huru ya wanazuoni hao dhidi ya uhusiano wa karibu na utawala wa Pahlawi.
Sala ya Ijumaa Katika Zama za Utawala wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, Sala ya Ijumaa ilipata nguvu mpya na kuanza kushamiri tena nchini Iran. Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wasaidizi wa Baraza la Sera za Maimamu wa Sala ya Ijumaa, ni kwamba; kufikia Agosti 2024, karibu Sala ya 900 za Ijumaa zilikuwa zikifanyika kila wiki katika miji mbali mbali ya Iran. [116] Sala ya kwanza ya Ijumaa katika kipindi hichi ilifanyika mnamo tarehe 27 Julai 1979, ikiongozwa na Sayyid Mahmoud Taaleqani, aliye teuliwa moja kwa moja na Imamu Khomeini akiwa ndiye Imamu wa kwanza wa Sala ya Ijumaa jijini Tehran, baada ya mapinduzi hayo. Sala hiyo ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran.
Imamu wa pili wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran, alikuwa ni Ayatullahi Hussein-Ali Muntadhiri, ambaye muda mfupi baada ya kuteuliwa kwake alihamia Qom na kujiuzulu nafasi yake ya Imamu wa Ijumaa mjini Tehran. Baada ya hapo, Ayatullahi Sayyid Ali Khamenei ndiye aliye teuliwa kuwa Imamu wa Sala ya Ijumaa ya mji huo wa Tehran. [117]
Kutokana na kuongezeka kwa maombi kutoka kwa wananchi wa miji mingine ya Iran, wakitaka kuteuliwa kwa Maimamu wa Sala ya Ijumaa mijini mwao, Sala ya Ijumaa ilionekana kuenea kote nchini. Imamu Khomeini, akifuata ushauri wa Ayatollahi Khamenei, ambaye wakati huo alikuwa ni Rais wa Iran, aliunda kituo maalumu mjini Qom, kwa ajili ya kushughulikia masuala yote ya Sala za Ijumaa. Manmo Mwaka 1992, Ayatullahi Khamenei, katika wadhifa wake kama ni Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu, alianzisha Baraza la Sera za Maimamu wa Sala ya Ijumaa, lenye wajumbe tisa wa jopo la maulamaa wa Kiislamu, kwa ajili ya kusimamia shughuli za Sala za Ijumaa. [118]
Ensaiklopidia ya Sala ya Ijumaa
- Makala Asili: Ensaiklopidia ya Sala ya Ijumaa
Ensaiklopidia ya Sala ya Ijumaa ni mfululizo wa maelezo ya kina yanayohusiana na masuala mbali mbali ya Sala ya Ijumaa. Ensaklopidia hii imeandikwa kwa na lengo la kutoa welewa wa kitaalamu na wa kina kwa Waislamu kuhusiana na Sala hii muhimu. Mradi huu umeanzishwa chini ya usimamizi wa Baraza la Sera za Maimamu wa Sala ya Ijumaa, nao unajikita katika kujadili vipengele mbalimbali kama vile maana ya Sala ya Ijumaa, hukumu zake za kifiq’hi, matukio muhimu, pamoja na majina ya watu waliochangia kuendeleza na kusimamia Sala ya Ijumaa katika historia ya Kiislamu. [118] Aidha, kuna kitabu kiitwacho “Ensaiklopidia ya Maimamu wa Sala ya Ijumaa”, kilichoandikwa na wanazuoni maarufu, nao ni; Sayyid Muhammad Kazim Mudarrisi na Mirza Muhammad Kadhimaini. Ensaiklopidia hii inatoa taarifa za kina kuhusu maimamu walioteuliwa kuongoza Sala za Ijumaa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, na mchango wao katika kudumisha ibada hii. Mradi huu unachukuliwa kuwa ni hazina na rasilimali muhimu kwa wanafunzi, wanazuoni, na watafiti wa masuala ya Kiislamu, kwani ni mradi utoao mwanga tosha wa kielimu juu ya historia na maendeleo ya Sala ya Ijumaa nchini Iran.
Maktaba ya Picha
-
Sala ya Ijumaa huko Bahrein -
Sala ya Ijumaa huko Bangladesh