Kumtembelea mgonjwa

Kutoka wikishia

Kumtembelea Mgonjwa (Kiarabu: عيادة المريض) ni katika adabu za Kiislamu ambazo zimetajwa katika hadithi kuwa ni miongoni mwa amali na matendo bora kabisa.  Katika vyanzo vya hadithi vya Kishia, kuna makumi ya hadithi zilizonukuliwa kuhusianaa na maudhui hii. Kumtembelea mgonjwa na kwenda kumjulia hali zilikuwa ni katika sira na mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s), na katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kishia inaelezwa kwamba, ni katika haki zilizobainishwa ambazo ni lazima kuzizingatia na kuzitekeleza kwa Waislamu. Kujibiwa dua, kujumuishwa katika rehema za Mwenyezi Mungu na kunufaika na istighfari (kuombewa maghufira) ya malaika ni miongoni mwa thawabu na ujira uliotajwa anaopatiwa mtu anayemtembea mgonjwa na kumjulia hali.

Baadhi ya ada na adabu za kumtembelea mgonjwa kwa mujibu wa hadithi ni: Kumliwaza mgonjwa, kumpelekea zawadi, kutokaa sana na kukidhi mahitaji ya mgonjwa huyo. Kitabu cha "Adaab Iyadat (adabu za kumtembelea mgonjwa) kilichoandikwa na Muuhammad Baqer Taati na Adaab Iyadat az Mariz (Adabu za kumtembelea mgonjwa) kiLichoandikwa na Muhammad Jawad Nouri na wengineo ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa vikijihusisha tu na maudhui ya kumtembelea mgonjwa.

Nafasi ya Kumtembelea Mgonjwa Katika Utamaduni wa Kiislamu

Kuumtembelea mgonjwa au kwenda kumuona mgonjwa na kumjulia hali [1] ni katika adabu za Kiislamu [2] na hilo limetajwa kuwa miongoni mwa amali na matendo bora kabisa ya kidini. [3] Katika vyanzo vya hadithi vya Waislamu wa Kishia, kuna makumi ya hadithi zilizonukuliwa kuhusiana na maudhui hii [4] na kubainishwa athari za kidunia [5] na Kiakhera [6] zinazopatikana kwa kumtembelea mgonjwa.

Kumtembelea mgonjwa na kwenda kumjulia hali zilikuwa ni katika sira na mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) [7] na Maimamu (a.s) [8], na imenukuliwa katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) [9] na Ahlul-Bayt (a.s) [10] ya kwamba, kumtembelea mgonjwa ni katika haki ambazo ni lazima kwa Waislamu kuzitekeleza baina yao.

Kadhalika imekokotezwa na kusisitizwa katika hadithi juu ya kumtembelea yule ambaye hakumtembelea wakati wa maradhi yake [11] na kuwatangazia wengine ugonjwa wa mgonjwa ili wengine wapate thawabu kwa kwenda kumtembelea na kumjulia hali . [12]

Ujira wa Kidini wa Kumtembelea Mgonjwa

Sayyid Abul Qasim Kashani alipo mtembelea Muhammad Taqi Khonsari katika hospitali ya Fiyruz-Abadi

Katika hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) kumetajwa na kuelezwa athari za kidunia na kiakhera zinazopatikana kwa mtu kumtembelea mgonjwa na kumjulia hali yake. Baadhi yazo ni: Kutakabaliwa dua, kupata rehma za Mwenyezi Mungu, pepo na kunufaika na istighfari ya Malaika.

Katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq kilichoandikwa na Tabarsi, kumenukuliwa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo kwa mujibu wake ni kwamba: Kila ambaye atamtembelea (mgonjwa) mja muuumini katika waja wa Mwenyezi Mungu (s.w.t), basi Allah huwepo kwa mja huyo na kama ataomba haja basi haja yake itajibiwa. [13] Kadhalika Imamu Ali bin Mussa Ridha (a.s) amenukuliwa akisema: Kila Muumini ambaye atamzuru na kumtembelea mgonjwa wakati wa kuugua kwake, Malaika 70,000 hufuatana naye, rehma za Mwenyezi huwa pamoja naye na Malaika humuombea Maghufira mpaka usiku na kama itakuwa ni usiku, basi ujira huo huo atapatiwa mpaka asubuhi.  [14]

Kwa mujibu wa hadithi iliyokuliwa na Sheikh Saduq (aliaga dunia: 381H) kutoka kwa Imamu Ali bin Abi Talib (a.s) ni kuwa, kama mtu atatoka nyumbani akiwa na nia ya kwenda kumtembelea mgonjwa na kisha akafariki dunia akiwa njiani, basi Mwenyezi Mungu huwajibisha pepo kwake. [15]

Adabu za Kumtembelea Mgonjwa

Katika hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Ahlul-Bayt (as) kumetajwa adabu za kumtembelea mgonjwa ambazo baadhi yazo ni:

  • Kumliwaza mgonjwa.  [16]
  • Kumpelekea zawadi.  [17]
  • Kuumlisha mgonjwa kile akipendacho.  [18]
  • Kufupisha uwepo na kutokaa sana kwa mgonjwa; [19] isipokuwa kama mgonjwa mwenyewe atataka ukae sana. [20]
  • Kumuombea dua mgonjwa sambamba na kuonyesha huba.  [21]
  • Kukidhi haja ya mgonjwa. [22]
  • Kumuonyesha mgonjwa huba na mapenzi.  [23]

Monografia

Baadhi ya vitabu vilivyochapishwa na ambavyo vina maudhui ya kumtembelea mgonjwa ni:

  • Adab Iyadat, (adabu za kumtembelea mgonjwa) mwandishi Muhammad Baqer Taati: Katika kitabu hiki, kumekusanywa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) na Maimamu watoharifu (a.s) zinazozungumzia kumtembelea mgonjwa. [24] Kitabu hiki kilichapishwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Barakat Kosar 1386 Hijria Shamsia. [25]
  • Adab Iyadat az Mariz, mwandishi, Muhammad Jawad Nouri na wengineo:  Katika kitabu hiki, mbali na  kubainishwa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) kuhusiana na kumtembelea mgonjwa, kumebainishwa pia hali ya Iran kuhusiana na suala la kuwamtembelea wagonjwa na vilevile nafasi na mchango wa jamii na utamaduni wa watu katika jamii kuhusiana na wagonjwa. [26] Kitabu hiki kilichapishwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Abid Andish mwaka 1395. [27]