Tawhidi

Kutoka wikishia

Tawhidi (Kiarabu: التوحيد) ndio msingi wa mwanzo kabisa katika misingi mikuu ya imani ya Kiislamu, tawhidi ina maana ya kumuamini ya kwamba; hakuna Mungu zaidi ya Mwenyezi Mungu mmoja tu naye ni Allah asiye kuwa na mwenza katika uungu wake wala katika kuumba kwake. Ibara ya kwanza kabisa ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliyoanza nayo katika hatua yake ya kuwalingania waja wa Mwenyezi Mungu, ilikuwa ni kuwataka wamuamini Mungu mmoja na kuepukana na ushirikina wa kuabudu au kuamini Mungu zaidi ya mmoja. Tawhidi ni moja kati ya mambo msingi yalio sisitizwa ndani ya Qur'an Tukufu pamoja na Hadithi za Maasumina, pia Surat al-Tawhidi imebeba ndani yake madhumuni muhimu ya tawhidi.

Imani ya Mungu mmoja katika utamaduni wa Kiislamu, inazingatiwa kuwa ni imani dhidi ya ushirikina. Wanatheolojia wa Kiislamu wameichambua tawhidi katika ngazi tofauti:

 1. Tawhidi ya dhati ya Mwenyezi Mungu; ambayo ina maana ya kuamini umoja wa dhati ya Mwenyezi Mungu.
 2. Tawhidi ya sifa; ambayo ina maana ya kuamini kuwa hakuna uwili baina ya dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake.
 3. Tawhidi ya matendo; ambayo ina maana kwamba Mwenyezi Mungu hahitaji msaada na wasaidizi katika utendaji wake.
 4. Tahidi 'ibadi (tawhidi ya ibada); ambayo ina maana kwamba hakuna Mungu isipokuwa Allah tu ndiye anaye stahiki kuabudiwa. Kuna hatua nne katika imini ya tawhidi, hatua ya kwanza ni tawhidi ya dhati na hatua ya juu kabisa ni tawhidi ya matendo.

Kuna ithibati, bayana na hoja mbalimbali za kuthibitisha tawhidi kupitia; Aya za Qur'an Tukufu, Hadithi za Maasumina, pia kupitia kazi mbalimbali za wanafalsafa na wanatheolojia wa Kiislamu. Bayana ya tamanu'u (برهان التمانع) inayo thibitisha upweke wa Mwenyezi Mungu kupitia hoja ya "mafahali wawili kuto kaa zizi moja", bayana ya kutumwa kwa mitume na bayana ya ta'ayyun ambayo inathibitisha dhihiriko la Mwenyezi Mungu. Hizo ni miongoni mwa ithibati za kuthibitisha upweke (tawhidi) wa Mwenyezi Mungu.

Kundi kubwa la wafuasi wa madhehebu ya Kisunni, akiwemo Ibn Taimiyyah, Muhammad Ibn Abd al-Wahhab, na Abd al-Aziz Ibnu Bazi, wamezingatia imani ya kuomba shufaa, na kuomba haja kupitia jaha ya bwana Mtume (s.a.w.w) na mawalii baada ya kufa kwao, kuwa ni dalili za ushirikina na ukafiri dhidi ya tawhidi ya ibada. Mashia kwa kutegemea Aya za Qur'an Tukufu, wanakanusha madai hayo na kuyahisabu kuwa yasio ya kweli. Kwa hoja ya kwamba, tofauti na Wapagani na waliotuhumiwa kwa ushirina kutokana na kuomba shufaa kupitia kwa bwana Mtume (s.a.w.w) na mawalii wa Mwenyezi Mungu, ni kwamba; wenye kuomba shufaa kupitia kwa bwana Mtume (s.a.w.w) na mawalii wa Mwenyezi Mungu, huwa hawafanyi hivyo kwa kuamini kuwa bwana Mtume (s.a.w.w) na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni sehemu ya uungu, bali maombi yao hayo yanatokana na kuthamini hadhi ya Mitume na mawalii mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo hufanya hivyo wakiamini kuwa ni moja ya njia za kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwao.

Wanachuoni wa madhehebu ya Shia wamejadili mada ya tawhidi katika kazi nyingi zilizozungumzia suala hilo. Kuna vitabu kadhaa ambavyo vimejikita katika mada hiyo tu, huku vitabu vyingine vikiwa vimijadili mada hiyo ya tawhidi mjumuiko wa mada mbalimbali za misingi ya dini ya Kiislamu. Kitabu Al-Tauhid cha Sheikh Sadouq, Gohar Murad kilichoandikwa na Abdul Razzaq Lahiji, Al-Rasail al-Tauhid cha Allamah Tabatabai na Tawhidi cha Morteza Motahari ni miongoni mwa vita maalumu vilivyojikita katika kujadili mada ya tawhidi.


Semantiki (Mizizi ya kilugha)

خوشنویسی کلمه توحید لا اله الا الله.jpg

Neno tawhidi lina maana ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na ndiyo fundisho kuu la itikadi katika dini ya Uislamu [1] Kwa mujibu wa imani ya Waislamu, Mwenyezi Mungu ndiye muumba pekee wa ulimwengu na wala hana mshirika. [2] Maana ya Tawhidi kwa jinsi ilivyo elezewa ndani ya Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu wa Kishia, akiwemo Imam Ali na Imamu Sadiq (a.s) ni kwamba, Tawhidi ina maana ya kushahadia na kuamini ya kwamba; “Hapana Mola isipokuwa Allah, Naye ni mpweke asiye na mshirika”. [3]

Pia neno tawhidi wakati mwengine hutumika likiashiria mada na maudhui za kitheolojia zinazohusiana na masuala ya upweke wa Mungu, sifa na matendo yake. Katika kujibu maswali kuhusu maana ya tawhidi, Imam Swadiq pamoja na Imam Ridha (a.s) wameashiria baadhi ya mada za kitheolojia, ikiwa ni pamoja na kumtakasa Mwezyezi Mungu kutokana na sifa za kibinadamu. [4]

Kuna nadharia tatu tofauti juu ya suala la upweke wa Mwenyezi Mungu; nadharia za kitheolojia, kiirfani (kisufi) na kifalsafa. Tawhidi ya kitheolojia imeegemea na kujikita kwenye kuamini upweke wa Mungu kimoyo, tawhidi ya kifalsafa imeegemea kwenye imani upweke wa Mwenyezi Mungu kupitia ithibati za kiakili na tawhidi ya kiirfani (kisufi) inategemea uangavu wa nuru ya Mwenyezi Mungu kupitia elimu inayotokana na Mungu mwenyewe. [5] Imani ya Mungu Mmoja katika falsafa inajadili kuhusu dhana na welewa juu ya ufahamu wa upweke Mungu Mwajibika kuwepo (وحدت واجب الوجود), katika kiwango cha dhana juu ya suala hilo. Ila katika nadharia za kiirfani, haihusu wala kujadili dhana ya tawhidi kama, bali inajadili uhalisia wa Mungu kama Mungu kati dhihiriko au madhihiriko yake, yaani Mungu ambaye ni mmoja tu na viumbe wengine wote wapo kupitia uwepo wake yeye. [6] Hata hivyo, jitihada za wanafalsafa ni kuthibitisha upweke wa Mungu Mwajibika kuwepo (وحدت واجب الوجود), Ama jitihada za wanairfani, ni kumdiriki Mwenyezi Mungu kupitia nuru ya elimu ya mwenyezi Mungu mwenyewe. Fani ya hikmatu al-muta'alia inayonasibishwa na Mulla Sadra Shirazi inachukuliwa kuwa muunganiko wa Qur'an, irafani, na falsafa katika uwanja wa kuthibitisha upweke wa Mwenyezi Mungu.

Nafasi ya Tawhidi katika Uislamu

Tawhidi ndio fundisho muhimu zaidi katika mafunzo ya Kiislamu, na ndio jambo linalo upambanua Uislamu na dini nyingine. [8] Kwa mujibu wa Qur'an, ujumbe wa Mitume wote ulikuwa ni juu ya wito wa Tawhidi [9] Ingawa neno tawhidi -kama lilivyo- halionekani ndani ya Qur'an Tukufu, ila Aya zake nyingi zinahusu kuthibitisha tawhidi na kukanusha ushirikina. [10] Mulla Sadra katika kitabu chake cha tafsiri ya Qur'an, ameelezea ya kwamba; lengo hasa la kuu la Quran Tukufu ni kuthibitisha tawhidi ya Mwenyezi Mungu. [11]

Kushahadia au kuamini upweke wa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na shirki ndio ibara ya kwanza ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwatangazia watu wa Makka mwanzoni mwa wito wake wa juu ya Uislamu. [12] Wawakilishi wa Mtume, akiwemo Ma'adh bin Jabal, ambao walikwenda sehemu tofauti kwa ajili ya kueneza Uislamu, daima waliwalingani watu kumpwekesha Mwenyezi Mungu. [13] Baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu, wakizingatia nafasi maalum na muhimu ya itikadi ya tawhidi katika Uislamu, waliwapa Waislamu jina la "Ahlu al-Tawhiid". [14] Pia wanazuoni huichukulia tawhidi kama ishara ya kuwa Mwislamu. [15] Imam Ali (a.s), ameotambua itikadi ya tawhidi na upweke wa Mungu kuwa ndio msingi wa kumtambua Mwenyezi Mungu. [16]

Tawhidi na upweke wa Mwenyezi Mungu, imesisitizwa mara nyingi katika Quran Tukufu kupitia ibara tofauti; Kwa mfano, katika Surat Tauhid, Mwenyezi Mungu Mungu ameitwa kwa jina la “Ahad” lenye maana ya upweke usio kubali kugawika kidhahiri wala kiakili. [17] Pia kuna aina kadhaa za tawhidi zilizoelezwa ndani ya Qur'an kama vile; Kukanusha miungu mingine, upweke wa Mungu Mmoja, Mungu mmoja kwa viumbe wote, Mungu wa walimwengu wote, kuwaponda wanao amini kuwepo kwa miungu zaidi ya mmoja, msisitizo wa kukanusha imani ya miungu mingi, Kukataa madai ya wale wanaoamini Utatu, pamoja na kukataa kuwepo kwa kitu chochote au kiumbe chochote kinacho fanana na Mungu. Yote hayo ni miongoni mwa dhana zinazohusiana na tawhidi zilizotajwa ndani ya Qur'an Tukufu. [18] Miongoni mwa Aya za Qur'an Tukufu zinazoashiria moja kwa moja imani ya uwepo wa Mungu mmoja ni:

 • Qul Huwa Allahu Ahad (قُل هُوَ اللهُ أحَد): Sema Yeye ndiye Mungu pekee.
 • La ilaha illa Allah (لا إلٰه إلّا الله): Hapana mungu ila Allah peke yake [20]
 • La ilaha illa huu (لا إلٰه إلّا هو): Hapana mungu ila Yeye tu [21]
 • İlaahukum Ilahun Waahid (إلٰهُکُم إلٰهٌ واحِد): Hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja pekee. [22]
 • Maa Min ilahin illa Allah (ما مِن إلٰهٍ إلّا الله): Hapana mungu ila Allah. [23]

Daraja na viwango vya Tawhidi

لا اله الا الله 2.jpg

Wanatheolojia, wanafikra na wanafalsafa wengi wa Kiislamu, wakitegemea Qur'an Tukufu na Hadith za Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu na Maimamu wa Kishia, wameorodhesha viwango na daraja tofauti za tawhidi. Ya kwanza ikiwa ni tawhidi ya dhati, kisha tawhidi ya sifa za Mwenyezi Mungu na matendo, na daraja la juu kabisa ni tawhidi katika ibada. [24]

Katika Quran Tukufu na utamaduni wa Kiislamu, tawhidi inazingatiwa kuwa ni imani dhidi ya ushirikina, na mapambano dhidi ya ushirikina ni mojawapo ya mada kuu katika Qur'an Tukufu. [25] Kama vile Waislamu wanavyoamini kuhusiana na ngazi na daraja za tawhidi, wao pia wanaorodhesha ngazi na daraja kadhaa katika ushirikina. [26] Kwa kuzingatia hilo, miongoni mwa daraja za ushirikina ni; kuamini wingi katika Dhati ya Mwenyezi Mungu, huitwa ushirikina katika Dhati ya Mwenyezi Mungu, [27] kuamini kwamba ulimwengu una zaidi ya mtendaji mmoja, huitwa ushirikina katika vitendo [28] pia, kuamini uwili baina ya sifa za Mwenyezi Mungu na dhati yake, huitwa ushirikina wa sifa za Mwenyezi Mungu [29] na kumwabudu mungu asiyekuwa Mungu mmoja, kunaitwa ushirikina katika ibada. [30]

Tawhidi ya dhati ya Mwenyezi Mungu

Makala Asili: Tawhidi ya dhati

Tawhidi ya Dhati ni daraja la kwanza miongoni mwa daraja za tawhidi [31] na moja ya maana zake ni kuamini umoja na kuamini kuwa Mungu hana aina yoyote ile ya kitu au kiumbe kinacho fanana Naye. Aya ya nne ya Surat Tawhidi isemayo: "Walam Yakun Lahu Kufuwa Ahad" (وَلَمْ یکُنْ لَه کُفُواً أحَدٌ) imekuja kusisitiza maana hiyo ya tawhidi. [32] Maana nyingine ya tawhidi ya dhati, ni kuamini ya kwamba; Dhati ya Mwenyezi Mungu haiakisi wingi wala uwili, na wala haina mfano unaolingana nayo. [33] Pia maana hiyo ya tawhidi imesisitizwa ndani Aya ya kwanza ya Suratu Tawhidi, pale Allah aliposema katika Sura hiyo: "Qul Ho Allah Ahad" (قُل هُو الله أحَدٌ). [34].

Tawhidi ya sifa za Mwenyezi Mungu

Makala Asili: Tawhidi ya sifa za Mwenyezi Mungu

Tawhidi ya Sifa: Humaanisha itikadi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwenye ngazi ya Dhati na Sifa. Yaani ni kuamaini kuwa; hakuna uwili wala wingi baina dhati ya Dhati na Sifa za Mwenyezi Mungu. Tawhidi ya Sifa maana yake ni kuelewa na kutambua kuwa Dhati ni kiini cha Sifa, na Sifa ni kiini cha Dhati. [35] Kwa mfano: pale tunapo amini kuwa, Mungu ni mjuzi wa yote, hii haimaanishi ya kwamba; ujuzi wa Mungu ni nyongeza juu ya Dhati Yake, bali ni kwamba, Dhati Yake ni sawa na ujuzi Wake, na wala hakuna kilicho ongezeka kwenye Dhati Yake. Mungu ni tofauti na mwanadamu, ambaye ujuzi na nguvu zake huwa ziko nje ya asili yake ambapo huongezeka hatua kwa hatua. [36] Sifa za Mungu, pamoja na kutotenganishwa na Dhati ya Yake, pia huwa hakuna uwili baina ya Sifa mmoja na nyingine. Yaani ujuzi wa Mungu ni sawa na uwezo Wake, na uwezo Wake ni kitu kimoja na elimu Yake, na elimu yake ni sawa na Dhati Yake. [37] Kwa mujibu wa nadharia ya Misbahu Yazdi; Tawhidi ya sifa katika istilahi ya wanafalsafa na wanatheolojia, humaanisha sifa maalumu kama vile; Sifa ya elimu, uhai na uwezo tunazozihusisha na Mwenyezi Mungu. Bila shaka Sifa za Mungu si kitu kingine zaidi ya Dhati Yake. Ukweli ni kwamba; tofauti iliopo baina ya Sifa na Dhati Yake, ni tofauti ya ufahamu na maana ya dhana tu, iliopo baina ya Sifa moja na nyengine. [38] Qur'an Tukufu inamtakasa Mwenyezi Mungu kila aina ya Sifa zinazonasibishwa kwake. Imamu Swadiq (a.s) katika moja ya mafunzo yake yaliyo nukuliwa na Abu Basiir ni kwamba Imamu (a.s) amesisitiza wazi ya kuwa: "Elimu, Kusikia, Kuona na Uwezo wa Mwenyezi Mungu ni sawa na Dhati Yake, na kabla ya Yeye Kuona na kusikia chochote kile, Yeye alikuwa ni Mwenye kuona na kusikia. [40]

Tawhidi ya matendo ya Mungu

Makala Asili: Tawhidi ya matendo ya Mungu

Tawhidi ya matendo: Ni kuamini ya kwamba; kama vile Mungu alivyokuwa ni Mpweke katika Dhati Yake, basi pia Yeye ni Mpweke na hana mshirika katika matendo Yake yote, ikiwa ni pamoja na uumbaji, ulezi, umiliki pamoja na uwendeshaji na udhibiti wa nyenendo na matukio ya kimaumbile. [41] Sharti la kuwa muumini wa Tawhidi ya matendo, ni kuamini ya kwamba; chimbuko la ulimwengu mzima linatokana na kitendo cha Mwenyezi Mungu, pia asili ya vitendo vyote vya waja na viumbe wote vinatokana na Mungu na matakwa yake. [42] Kama ilivyo kwamba; viumbe ulimwengunmi havijitegemei kudhihiri au katika uwepo wa dhati zao, pia viumbe hivyo havina uwezo wa kujitegemea katika lolote lile. Kwa hiyo matendo au taathira zitokazo kwa viumbe huidhinishwa na Mola wao, na bila ya kupata idhini ya Mwenyezi Mungu, viumbe hivyo haviweza kutenda tendo lolote lile. Kwa mujibu wa ibara za Qur'an, Mwenyezi Mungu ndiye nguzo na mhimili wa kila kilichomo ulimwenguni humu. [43]

Qur’an Tukufu imemtaja Mwenye zi Mungu; kuwa Yeye ndiye Muumba wa kila kitu na ndiye Mweza pekee. [44] Imamu Swadiq (a.s) amemsifu Mwenyezi Mungu; kuwa ndiye Muumba pekee anayeumba bila ya kutegemea mali ghafi, na ndiye Muumba mwenye uwezo wa kuvitoa vitu kutoka katika ulimwegu wa uwepo na kuvirejesha katika hali ya kutoweka kabisa kabisa. [45]

Tawhidi ya ibada

Makala Asili: Tawhidi ya ibada

Tawhidi ya ibada: Ina maana ya kuamini kwamba; hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah tu peke yake, na kwamba ibada ni haki maalumu ya Mwenyezi Mungu peke yake. [47]

Tawhidi ya ibada imeelezwa wanzi ndani ya baadhi ya Aya za Qur'an Tukufu; Kwa mfano, katika Surat Nahli, Mwenyezi Mungu amesema:(وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ); Ufafanuzi wake ni kwamba; "Mwenyezi Mungu hakutuma mtume yeyote yule katika jamii za wanadamu, isipokuwa kwa lengo la kuwalingania watu kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja na kuepukana na Shetani". [48] Katika Aya nyingine miongoni mwa Aya za Quran, Mtume amekataza kuwaabudu wale wanaolingania kuabudu asiye kuwa Allah, na kuamrisha kumwabudu Muumba wa walimwengu peke yake. [49]

Qur’an ikielezea suala hilo inasema: (قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ لَمَّا جَاءَنِيَ الْبَيِّنَاتُ مِنْ رَبِّي وَأُمِرْتُ أَنْ أُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ) ; “Sema (uwaambie), kwa hakika mimi nimekatazwa kuabudu mnao waomba (mnao waabudu) kinyume na Mwenyezi Mungu, kwa vile tayari zimeshanifikia bayana kutoka Mola Mlezi wangu, na nimeemrishwa kujisalimisha kwa Mola Mlezi wa walimwengu.” Aya ya 66 ya Surat Ghafir.

Mtume Muhammad (s.a.w.w), katika maneno yake aliyowaambia washirikina, aliwauliza pale mnapotengeneza masanamu kutokana na yale aliyoyaumba Mwenyezi Mungu kisha kuyaabudu na kuyasujudia, au mnaposwali na kuweka nyuso zenu chini katika kuyaabudu masanamu hayo, hivi kuna mlichombakishia Muumba wa walimwengu? [50] Kwa mujibu wa bayana za Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni kwamba; moja ya haki za mwenye kusujudiwa ni kwamba mwabudiwa asiwe sawa kidaraja na wanye kumuabudu. [51]

Uthibitisho wa Imani ya Mungu Mmoja

Makala Asili: Uthibitisho wa Imani ya Mungu mmoja

Kuna ushahidi na bayana tosha juu ithibati kuhusiana na tawhidi kutoka katika vyanzo mbalimbali. Mwenyezi Katika Quran Tukufu, Hadithi za Maasumina, wanafalsafa wa Kiislamu na wanatheolojia, wametoa hoja na ithibati kadhaa juu ya suala hilo la upweke wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya hoja hizo ni kama ifuatavyo:

 • Hoja ya tamaanu’u (برهان تمانع); hoja hii imesimama kwenye msingi maarufu usemao: “Mafahali wawili hawakai zizi moja”. Hoja hii inatokana na Aya ya Qur'an isemayo: ((لَوْ کانَ فیهِما آلِهَةٌ إِلاَّ اللهُ لَفَسَدَتا)) ; Tafsiri yake ni kwamba; "Lau kama kwenye mbingu na ardhi kungelikuwa na miungu kadhaa zaidi ya Mungu Mmoja, basi pangelitokea maharibiko ndani yake." [52] Aya hii inathibitisha tawhidi kwa kukataa uwepo wa miungu zaidi ya Mungu Mmoja (ushirikina). [53] Katika maelezo ya hoja hii, imeelezwa ya kwamba; iwapo patakuwepo miungu wawili, kisha mmoja akadhamiria kufanya jambo fulani, huku wa pili akawa na dhamira kinyume na dhamira ya mungu wa kwanza, hapo panaweza kupatikana hali tatu tofauti;
 1. Ima hakutaweza kutendeka hata dhamira moja kati ya dhamira mbili hizo. Katika taswira hii, miungu wawili hao watakuwa ni miungu wasio na uwezo, sifa ambayo ni kinyume na sifa za kiungu.
 2. Hali ya pili ni kwamba; dhamira zote mbili zitafanikiwa kutendeka. Katika taswira hii, kutazaliwa mambo mawili yasio oana, au kwa lugha nyengine, kutazaliwa jambo na kinyume cha jambo hilo, kitu ambacho kiakili au kimantiki haikwezi kutokea. Haiwezekani kukapatikana usiku na mchana kwa wakati mmoja.
 3. Hali ya tatu ni kwamba; moja kati ya dhamira mbili hizo itekelezeke na ya pili ishindwe, katika hali hiyo, itahisabiwa ya kwamba; mungu aliyeweza kutimiza dhamira yake, yeye ndiye mungu halisi na mweza, na mungu wa pili atakuwa ni mungu bandia. [54]
 • Ithibati ya tawhidi kupitia bayana na hoja ya uwili au wingu katika hakika ya Mwenyezi Mungu. Hii ni mojawapo ya hoja za kifalsafa katika falsafa ya Kiislamu. Bayana ya hoja hii imejikita kwenye kuthibitisha imani ya upweke wa Mungu mmoja kwa kukataa hali ya mchanganyiko wa uwili au wingi katika hakika na uwepo wa Mungu. Kwa kuzingatia hili, imani ya kuamini mchanganyiko fulani katika uwepo na uhakika wa Mungu, itapelekea kuamini wajibu wa kuwepo zaidi ya mungu mmoja ambao ni wajibu kuwepo (yaani wana lazimika kuwepo kwa kuwa wao ni miungu). Katika hali hiyo, ni lazima kuwepo mungu (sababu) mwengine ambaye ni muunganishi wa uwili au wingi uliosababisha uwepo wa aina hiyo ya mungu mwenye mchanganyiko. Kwa hiyo ita kuwa ni muhali kupatikana kwa mungu mwenye mchanganyiko, bali mungu halisi ni yule mungu mwenye sifa umoja usio gawika kidhahiri wala kiakili. Ni wazi ya kwamba; mchanganyiko hauendani ya hali ya uungu, na hapa tutakuwa tumepata natija ya kwamba; mungu wa haki ni yule mungu asiyekuwa na uwili wala wingi katika hakika yake. [55]

Mbali na bayana na ithibati zilizotajwa hapo juu, pia kuna naina kadhaa za ithibati kuhusiana na upweke wa Mwenyezi Mungu, miongoni mwazo ni kama vile; ithibati kupitia hoja na bayana ya dhihiriko la uwepo wa Mungu, ithibati kupitia hoja na bayana ya uthibitisho wa umuhali wa kuwepo mungu zaidi ya mmoja, uthibitisho wa upweke wa Mungu kupitia bayana na hoja ya kutumwa kwa mitume na uthibitisho wa upweke wa Mungu kupitia hoja na bayana ya uwepo wa viumbe na matukio mbalimbali ulimwenguni. Hizo ni miongoni mwa bayana na ithibati zilizotajwa katika falsafa na teolojia ya Kiislamu kuhusiana na upweke wa Mungu. [56] Imamu Ali (a.s) katika barua kwa Imamu Hassan (a.s), akielezea moja miongoni mwa dalili za upweke wa Mwenyezi Mungu, alisema kwamba; kama Mwenyezi Mungu angekuwa na mshirika, bai mitume wa mshirika huyo wangewajia waja wake. [57] Wanatheolojia wa Kiislamu wameitambua hoja na bayana hii, kwa jina la hoja na bayana ya kutumwa kwa mitume. [58]

Kuwatuhumu Mashia na shirki

Mawahabi wanaichukulia imani ya Shia juu ya suala la shufaa, la kuomba kupitia jaha ya Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu, pia baraka za Shia katika makaburi ya mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu kuwa ni shirki. Mashia wamejibu tuhuma hizo kwa kusema; Wanaofanya vitendo hivyo, huwa hawakusudii kuwaabudu manabii wala hawana itikadi yu uungu juu ya manabii na mawalii wa Mungu, bali nia yao ni Kujikurubisha Kwa Mwenyezi Mungu wao kupitia jaha ya mawalii na mitume hao, kwa kuwa wao wanaamini ya kwamba; mitume na mawalii, huwa na nafasi na hadhi maalumu mbele ya Mola wao. [60]

Kwa mujibu wa imani ya Ibnu Taimiyyah, yeyote anayeomba msaada kupitia jaha ya Imamu Ali (a.s) na yeyote yule mwenye kutilia shaka ukafiri wa mtu huyo, naye pia ni kafiri. [61] Kwa imani ya Ibnu Taimiyyah; yeyote anayekwenda kwenye kaburi la Mtume au mmoja wa watu wema na kuumba haja fulani katika kaburi hilo, atakuwa ni mshirikina na ni lazima alazimishwe kutubia, na asipotubu ni lazima auawe. [62] Abdu al-Aziz bin Bazi, mufti wa Kiwahabi, katika vitabu vyake amesema ya kwamba; kuombea na kutaka msaada kwenye makaburi, kuomba shufaa na ushindi dhidi ya maadui ni moja ya alama za ushirikina namba moja. [63]

Kwa kutegemea Aya za Qur'an Tukufu, Mashia wamesema ya kwamba; maombi tu yasio halali ni yale maombi yanayo elekezwa moja kwa moja kwa mwombwaji na kutaraji kutoka kwake yeye binafsi, bila ya kuyaelekeza maombi hayo kwa mola mwenyewe. Kuomba kwa mfumo huo huwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika sifa ya kuruzuku na mipango yake. [64] Wanachuoni wa kishia wametumia jitihada kadhaa katika kujibu hoja za Muhammad bin Abdul Wahhab na Abdul Azizi bin Bazi zilizotegemea Aya za Qur'an Tukufu ambzo zimekataza kumwomba Mungu kupitia masanamu na kukana suala hilo. Mashia wamefafanua tofauti za kimsingi zilizopo kati ya kuomba shufaa kupitia jaha ya Mtume (s.a.w.w) na maombi ya wanaoabudu masanamu, Mashia wanaamini kwamba; Waislamu ni tofauti na wanaoabudu masanamu waliotajwa ndani ya Quran Tukufu, wao kamwe hawamchukulii Mtume kuwa Mungu, Bwana au mtawala wa ulimwengu. [65]