Bibi Ma'sumah (s.a)

Kutoka wikishia
Haram ya Bibi Ma'asumah (a.s) katika mji wa Qom

Bibi Ma'asumah (a.s) (Kiarabu: السيدة فاطمة المعصومة (ع)), ambaye jina lake halisi ni Fatima, ni binti wa Imamu Kadhim (a.s) na dada wa Imamu Ridha (a.s). Yeye anajulikana kuwa ndiye bint bora zaidi wa Imamu Kadhim (a.s), na imesemwa kuwa; hakuna mtu mwenye hadhi ya kumpindukia bibi Ma’asuma kati ya watoto wa Imam Kadhim (a.s), isipokuwa Imamu Ridha (a.s). Hakuna habari nyingi kuhusu maisha ya Bibi Ma'sumah (a.s), katika vyanzo vya kihistoria, hata tarehe ya kuzaliwa na kifo chake pia hazijarekodiwa ndani ya vyanzo vya kihistoria. Habari juu ya ndoa yake pia hazina ukamilifu vyanzoni humo, lakini inajulikana kuwa yeye kamwe hakufunga ndoa maishani mwake.

Bibi Ma'asumah na Karimah Ahlul Bayt (a.s) ni majina maarufu ya bibi Fatimah binti ya Imam Kadhim (a.s). Kulingana na Hadithi kutoka Imam Ridha (a.s), anajulikana kwa jina la Ma'sumah, yaani jina hili ndilo lililonukuliwa ndani ya khabari za Hadithi hiyo.

Mnamo mwaka 201 Hijiria, Bibi Ma'asumah alisafiri kutoka mji wa Madina na kwenda Iran kwa ombi la ndugu yake (Imamu Ridha (a.s)) na alipokuwa njiani alipatwa na ugonjwa. Kwa ombi la watu wa mji wa Qom, alikwenda kwenye mji huo na akakaa nyumbani kwa mtu anayejulikana kama Mussa bin Khazraj Ash'ari, na baada ya siku 17 alifariki dunia. Mwili wake ulizikwa katika makaburi yaliyojulikana kama Babilaan (Haramu ya bibi Ma’asuma ya sasa ilioko mjini Qom). Sayyid Ja'far Mudhaffari (aliye fariki mwaka 1441 Hijiria) anaamini kuwa; Bibi Ma'asumah (a.s) aliuawa kwa sumu akiwa huko Saweh.

Mashia wanamheshimu na kumpa umuhimu mkubwa Bibi Ma'asumah (a.s) na wanathamini sana safari kwa ajili ya ziara yake (kulizuru kaburi lake). Pia kuna Riwaya zinazozungumzia juu ya shufa'a (kumwombea mtu mbele ya Mwenyezi Mungu) yake kwa ajili ya Mashia siku ya Kiama, na Jannah (Pepo) ndio ujira na malipo ya kumtembelea yeye (a.s). Inasemekana kuwa; baada ya binti ya Mtume (s.a.w.w) (Bibi Fatimah (a.s)), yeye (Bibi Ma'asumah) ndiye mwanamke pekee ambaye ziara (sala na salamu) yake imenukuliwa kwa Maimamu (a.s).

Khabari na ripoti chache kuhusiana na bibi Ma’asuma

Kama ilivyosemwa na Zabihullahi Mahallati katika kitabu chake Riyahinu al-Shari'ah, habari chache sana zinapatikana juu ya maisha ya Bibi Ma'sumah (a.s), na wala katika historia hakuna habari zilizosajiliwa kuhusiana na tarehe ya kuzaliwa kwake, kifo chake, umri wake wala tarehe ya kuondoka Madina. Pia hakuna khabari ya kuwa alifariki kabla au baada ya kifo cha Imamu Ridha (a.s). [1]

Nasaba yake

Fatima ni binti Imamu Kadhim (a.s) na dada wa Imamu Ridha (a.s), umaarufu wake anajulikana kwa jila la Ma'sumah. Sheikh Mufid katika kitabu chake Al-Irshad amewataja mabinti wawili wa Imam Kadhim (a.s) waitwao; Fatima Kubra na Fatima Sughra, lakini hakufafanua ni yupi kati yao anayejulikana kama Ma'sumah. [2] Ibn Jauzi, mmoja wa wanazuoni wa Sunni wa karne ya sita Hijiria, ametaja mabinti wanne waitwao Fatima miongoni mwa mabinti wa Imam Kadhim, lakini hakusema ni yupi kati yao ndiye Ma'sumah. [3] Kwa mujibu wa maelezo ya Muhammad bin Jarir, mwandishi wa kitabu Dalail al-Imamah, mama wa bibi Ma'sumah anajulikana kwa jina la Najmakhatun, ambaye pia ni mama wa Imam Ridha (a.s). [4]

Tarehe ya kuzaliwa na kufariki kwake

Kulingana na vyanzo vya zamani vya Shia, hakuna tarehe iliyotajwa kuhusu kuzaliwa wala kufariki kwa bibi Fatimah Ma'asumah. Kulingana kauli ya Ridha Ostadi ni kwamba; kitabu cha kwanza kilicho taja ndani yake tarehe kuhusiana na matukio hayo ni Noor al-Aafaaq kilichoandikwa na Jawad Shah Abduladhimi, [5] kilichapishwa mwaka 1344 Hijiria. [6] Kitabu hichi kinasema kuwa; Fatima Ma'asumah alizaliwa tarehe 1 Dhul-Qa'ida, mwaka 173 Hijiria, na kufariki tarehe 10 Rabi'u al-Thani, mwaka 201 Hijiria, na baada ya hapo ripoti hii ilianza kunukuliwa kwenye vitabu vyengine kwa kutegemea kauli ya mwandishi huyu. [7] Walakini, baadhi ya wanazuoni kama vile Ayatullahi Mar’ashi Najafi, [8] Ayatullahi Shubeiri Zanjani, [9] Ridha Ostadi, [10] na Zabihullahi Mahallati, [11] wamepinga tarehe zilizotajwa katika kitabu hicho na kuziona kuwa ni ripoti zisizo sahihi.

Katika kalenda rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya kwanza ya Dhul-Qa'idah imepewa jina la Siku ya Wasichana, kupitia dhana hiyo juu ya tarehe ya kuzaliwa kwake. [12]

Majina ya lakabu kwa bibi Fatima

Ma'asumah na Karimah Ahlul Bayt (a.s) ni majina na lakabu maarufu zaidi kwa binti huyu wa Imamu Kadhim (a.s) (bibi Fatimah). [13] Inasemekana kuwa jina "Ma'asumah" limechukuliwa kutoka katika Hadithi inayohusishwa na Imamu Ridha (a.s). [14] Katika Hadithi hiyo ambayo inayopatikana katika kitabu cha Zaad al-Ma'aad kilichoandikwa na Muhammad Baqir Majlisi, Imam Ridha (a.s) amemtaja bibi Fatima kwa jina la Ma'sumah ndani yake. [15]

Bibi Fatimah Ma'sumah (a.s) katika zetu za hivi sasa pia anajulikana kwa jina la "Karimah Ahlul Bayt". [16] Inasemekana kuwa jina hili limetokana na ndoto ya kuaminika ya Sayyid Mahmoud Marashi Najafi, baba yake Ayatullah Marashi Najafi, ambapo aliota usingizini mwake ya kwamba; mmoja wa Maimamu (a.s) alimwita Fatimah Ma'sumah kwa jina la Karimah Ahlul Bayt. [17]

Ndoa

Kulingana na maelezo yalioko katika kitabu cha Riyahinu al-Shariah, ni kwamba; haijulikani iwapo bibi Fatima Ma'asumah (a.s) aliolewa au aliwahi kuwa na watoto au la. [18] Walakini, inafahamika sana kwamba kwamba; Fatima Ma'asumah (a.s) hakuwahi kuolewa [19] na kuna sababu mbalimbali zilizotajwa kuhusiana na kuto olewa kwake, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mwenza anayefaa kuoana naye. [20] Aidha, Ya'aqubi, mwanahistoria wa karne ya tatu Hijria, amwandika akisema kuwa; Imamu Kadhim (a.s) aliwasihi mabinti zake wasiolewe. [21] Hata hivyo, kuna shaka juu ya uhalali wa taarifa hiyo, kwani ripoti hiyo haipatikani katika wasia uliowasilishwa na Kulaini katika kitabu chake cha Al-Kafi kutoka kwa Imamu Kadhiim (a.s). [22] [23] Baadhi ya watafiti pia wanaamini ya kwamba; uamuzi wa bibi Fatima Ma'sumah (a.s) na dada zake wa kuto kuolewa, ulitokana na utawala mkali wa Bani Abbas, hasa chini ya uongozi wa serikalai ya Harun na Ma'mun. [24]

Safari yake Irani, kuingia mjini Qom na kufariki kwake

Kulingana na maelezo yalioko katika kitabu kiitwacho Tarikh Qom ni kwamba; mnamo mwaka 201 Hijiria baada ya kuondoka Madina, bibi Fatima Ma'asumah alisafiri kuelekea Iran na hatimae kufika mjini Qom kwa ajili ya kukutana na ndugu yake (Imam Ridha (a.s)). [25] Kulingana na Riwaya ilinukuliwa na Baqir Sharifi Gharashi, mtafiti wa historia ya Shia, katika kitabu chake Jawharatu al-Kalam fi Mad-hi al-Sadat al-A'alama, sababu ya safari ya Fatima Ma'asumah (a.s) ya kwenda Iran, ilikuwa barua kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) aliyo mtumia na kumwomba aende kwake huko Khorasan. [26] Wakati huo, Imamu Ridha (a.s) alikuwa ni mrithi mteule wa Khalifa Mamun aliyekuwa akiishi mjini Khurasan. Akiwa njiani katika safari yake, Fatima Ma'asumah alipatwa na ugonjwa na hatimaye akafariki dunia. [27] Kwa mujibu wa imani ya Sayyid Ja'afar Murtadha Amili, bibi Fatima Ma'sumah (a.s) aliuawa kwa sumu na kfa shahidi akiwa katika kitongoji kiitwacho Saweh. [28]

Kuna ripoti mbili kuhusiana na sababu hasa iliyo mfanya yeye kwenda mji wa Qom: Kulingana na ripoti ya kwanza, ni kwamba; Yeye alipatwa ugonjwa akiwa katika kitongoji cha Saweh, akawaomba wenzake kuelekea Qom. [29] Kulingana na ripoti ya pili, iliyo elezwa na mwandishi wa kitabu cha historia ya mji wa Qom ambayo kwa mtazamo wake anadhani kuwa ndio sahihi zaidi, ni kwamba; Watu Qom wao wenyewe ndio walimwomba aende mji wa Qom. [30]

Bibi Fatima Ma'asumah alikaa Qom katika nyumba ya mtu binafsi aitwaye Mussa bin Khazarj Ash'ari, na baada ya siku 17 akafariki dunia. [31] Mazishi yake yalifanyika katika mava iitwayo Baabilaan (kwa sasa ni Haramu ya bibi Ma’asuma) huko Qom. [32] Watu wa ukoo wa Al-Saad walizozana juu ya mazishi ya Fatima Ma'sumah. Hatimaye, ilikaamuliwa kwamba Qadir, ambaye alikuwa ni mtumishi mzee na mchamungu, achukue jukumu la mazishi hayo. Ghafla, wapanda farasi wawili waliovalia nikabu walitokea kutoka eneo la jangwani, wakakaribia haraka, wakamsalia na kumzika. baada tu ya kumaliza mazishi hayo, wawili hao waliokuwa wamevaa nikabu walipanda farasi wao na kutoweka bila kuzungumza na mtu yeyote. [33] Fadhil Lenkraniani (aliye fariki mwaka 1386 Shamsia), ameandika akisema kuwa; yawezekana kuwa wawili hao walikuwa Maimamu. [34]

Hadhi na nafasi yake mbele ya Mashia

Wanazuoni wa Kishia wanaamini kuwa; bibi Fatima Ma'asumah ana nafasi na hadhi kubwa, pia kuna Riwaya kadhaa zinazohusiana na hadhi yake na umuhimu wa kulitembelea kaburi lake. Alama Majlisi katika kitabu chake Bihar al-Anwar amenukuu Hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ambapo kwa mujibu wa Hadithi hiyo, Mashia wote wanaingia Peponi kupitia shufa'a (uombezi) wa bibi Fatima Ma'asumah (a.s). [35] Katika sehemu moja vipengele vya ibara ya Ziara (maamkizi ya taadhima ya sala na salamu) ya Fatima Ma'asumah, ndani yake kuna kipengele cha kuomba shufa'a yake (uwokovu au uombezi), kutokana na hadhi yake na nafasi yake mbele ya Mwenye Ezi Mungu. [36] [Maelezo 1]

Maandamano ya amani ya kuomboleza siku ya Ashura katika viwanja vya Haram ya Masoumeh.

Muhammad Taqi Shushtari, aliye ishi katika karne ya kumi na nne Hijria, katika kamusi yake Qamus al-Rijal ameandika ya kwamba: Kati ya watoto wengi wa Imam Kadhim (a.s), baada ya Imamu Ridha (a.s), hakuna mwengine anayeweza kulinganishwa na bibi Ma'sumah. [37] Sheikh Abbas Qommi pia amemtambua kuwa ndiye binti bora zaidi kati ya mabinti wa Mussa bin Ja'far (a.s) [38]. Pia amemchukulia Fatima Ma'asumah kuwa ni mwana mmoja jasiri miongoni mwa wana wa Mmamu, na bila shaka yeye ni mtoto wa Imam Kadhim (a.s) na pia hakuna shaka ya kwamba yeye amezikwa katika Haram hii maarufu iliyopo mjini Qom. [39]

Kulingana na Riwaya zilizo nukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), Imam Kadhim (a.s) na Imam Jawad (a.s), ni kwamb; Pepo ndio malipo kwa yule atayemtembelea bibi Fatima binti wa Imamu Kadhim (a.s). [40] Ingawa katika baadhi ya Riwaya, imeelezwa ya kwamba; malipo hayo ya Pepo ni kwa yule atayemtembelea binti huyu hali akiwa welewe kamili juu ya hadhi na nafsi ya bibi Fatima Ma'asumah, yaani ni kwa yule mwenye kukiri uadhimu wake na nafsi yake. [41]

Mwandishi wa kitabu cha maisha ya Karima Ahlul Bayt (a.s), akinukuu kutoka kwa Mahmoud Ansari Qummi (aliyefariki mwaka 1377 Hijiria), naye akinukuu kutoka kwa Sayyid Nasrullah Mastanbat, ambaye ni mwanazuoni wa Kishia (aliyefariki mwaka 1364 Hijiria), alinukuu akisema kwamba; katika kitabu cha kilichoandikwa kwa hati za mkono cha Saleh bin Arandas Halli kiitwacho Kashfu al-Luaali, ambaye ni mwanazuoni wa Shia wa karne ya tisa Hijria, kuna Hadithi ambayo ndani yake, Imamu Kadhim (a.s) anamhutubu bibi Fatimah Ma'sumah kwa lugha isemayo: Fadaha abuha; baba yake awe ni muhanga kwake. Kulingana na Hadithi hii, Imamu Kadhim (a.s) alisema hivyo baada ya Fatima Ma'asumah kujibu maswali ya Waislamu wa Kishia kwa usahihi kabisa wakati wa kutokuwepo kwa Imamu (a.s). Mwandishi wa kitabu cha maisha ya “Karima Ahlul Bayt (a.s)”, kama alivyokiri mwenyewe ya kwamba; Hadithi hii hakuipata katika chanzo chengine chochote, isipokuwa katika kitabu hicho peke yake. [42]

Sala na salamu za kumuadhimu

Allama Majlisi katika vitabu vyake kama vile Zadu al-Ma'ad, Bihar al-Anwar, na Tuhfatu al-Zaa'ir amenukuu Ziara (taadhima ya sala na salamu) kutoka kwa Imam Ridha (a.s) makhususi kwa ajili ya kumuadhimu bibi Fatima Ma'asumah. [43] Hata hivyo, katika "Tuhfatu al-Za'ir" baada ya kutaja Ziara hiyo, ametoa maelezo yasemayo kwamba; kuna uwezekano kuwa, sehemu inayofuatia katika Hadithi ya Imamu Ridha si endelezo la maneno yake, bali ni nyongeza ya maneno ya wanazuoni. [44] Inasemekana kuwa; bibi Fatima (a.s) (binti ya Mtume (s.a.w.w)) na bibi Ma'sumah, ndiwo wanawake pekee ambao wana matini ya Ziara zilizonukuliwa moja kwa moja kutoka Maimamu (a.s). Yaani mlolongo wa wapokezi matini ya Ziara kihistoria unaishia kwa Maimamu (a.s). [45]

Eneo la kaburi takatifu la bibi Ma’asumah

Makala asili: Haram ya Bibi Ma’asumah

Hapo awali Kaburi la Fatima Ma'asumah huko Qom lilijengwa kwa mfumo wa banda, kisha baadaye kupanuliwa kuwa ni qubba. [47] Kaburi hili limeenedelea kukua kwa kiwango ambacho hivi leo, kaburi hili ndilo linaloshika nafasi ya pili kwa ukubwa na uzuri baada ya Haram ya Imam Ridha (a.s). Kaburi la Imamu ridha na bibi Ma’asumah ndiyo makaburi mazuri na maarufu zaidi nchini Iran.[48] Haram ya Fatima Ma'asumah inamiliki majengo kadhaa, mali za waqfu, pamoja na ofisi kadhaa zinayohusiana na uendeshaji wa Haram hiyo. Kwa kiasi kikubwa mali na majengo hayo yapo katika mji wa Qom nchini Iran. [49]

Kongamano la Kumbukumbu na Filamu za Sinema

Kongamano la kumuadhimu Sayyida Ma'asumah

Kongamano kubwa la kumuadhimisha Sayyida Ma'sumah lilifanyika mwaka wa 1384, kwa agizo la Ali Akbar Masoudi Khomeini, ambaye ni msimamizi wa Haram ya bibi Ma’asumah. Kongamano hili liliandaliwa katika Haram ya Sayyida Ma'sumah, ambapo viongozi wa kidini kama vile Naser Makarem Shirazi na Abdullah Jawadi Amoli walitoa hotuba kongamanoni humo. [51]

Ahmad Abidi, mkuu wa kongamano hilo, alitangaza kuchapishwa kwa vitabu 54 na kongamano hilo kuhusia na nafasi na umuhimu waSayyida Ma'sumah, vitabu ambavo vilichapisha kupitia Harm yake, Hawza ya Qom (Chuo Kikuu cha Kiislamu Qom), na Serika ya Mapinduzi ya Kiislamu huko Qom. [52]

Filamu ya sinema ya "Ukhti al-Ridha

Filamu ya sinema ya Ukhti al-Ridha inaelezea safari ya Sayyida Ma'asumah (s.a) kutoka Madina hadi Qom. Filamu hii ilionyeshwa mnamo mwezi 24 Rabi’u al-Awal mwaka 1445 Hijiria (sawa na 18 Mehr 1402 Shamsia) huko Qom. [53]

Bibliografia (seti ya orodha ya vitabu)

Baadhi ya vitabu kuhusia na bibi Fatimah Ma'sumah (a.s) ni kama ifuatavyo:

  1. Hazrat Ma'sumah Fatimah Dovvom cha Muhammad Muhammadi Ishtehaardi
  2. Partue az Ruye Dust cha Ismail Kirmanshahi
  3. Zindegani Hadhrate Ma’asumeh wa Taarekh Qom cha Sayyid Mahdi Sahafi
  4. Goghrafiai Taariikhi Hadhrate Fatimeh Ma’asumeh cha Sayyid Ali Redha Sayyid Kabari
  5. Hazrat Ma'sumeh wa Shahre Qom cha Muhammad Karimi
  6. Hayatu wa Karamatu Fatimah al-Ma'sumah cha Sayyid Muhammad Ali Husseini Baqai Lubnani
  7. Banuye Malakuti cha Ali Karimi Jahromi
  8. Ammeh Saadaat cha Sayyid Abu Al-Qasim Hamidi

Maelezo

  1. ((یا فاطِمَةُ اِشْفَعی لی فِی الْجَنَّهِ فَاِنَّ لَکِ عِنْدَاللهِ شَأْناً مِنَ الشَّأْن))

Vyanzo

  • ʿĀmilī, al-Sayyid Jaʿfar al-Murtaḍā al-. Al-Ḥayāt al-sīyāsīyya li-l-Imām al-Riḍā. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmīyya, 1403 AH.
  • Ibn Qūlawayh, Jaʿfar b. Muḥammad. Kāmil al-zīyārāt. 1st edition. Najaf: Dār al-Murtaḍawīyya, 1356 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Kungira-yi Buzurgdāsht-i Haḍrat-i Fāṭima Maʿṣūma. Majmūʿa Maqālāt. 1st edition. Qom: Intishārāt-i Zā'ir, 1384 Sh.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Edited by a group of researchers. 2nd Edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Tuḥfat al-zāʾir. Edited by Muʾassisa Imām Hādī. 1st edition. Qom: Muʾassisa Imām Hādī, 1386 SH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Zād al-maʿād. Edited by ʿAlā al-Dīn Aʿlamī. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1423 AH.
  • Maḥallātī, Ḍhabīḥ Allāh. Rayāḥīn al-sharī'a. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, [n.d].
  • Mahdīpūr, ʿAlī Akbar. Karīma-yi Ahl Bayt (a). 1st edition. Qom: Nashr-i Ḥādhiq, 1374 SH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Irshād fī maʿrifat ḥujaj Allāh ʿalā l-ʿibād. Beirut: Dār al-Mufīd, 1414 AH.
  • Qarashī, Bāqir Sharīf al-. Ḥayāt al-Imām Mūsā b. Ja'far (a), Dirāsat wa taḥlīl. 2nd edition. Beirut: Dār al-Balāgha, 1413 AH.
  • Qummī, Ḥasan b. Muḥammad. Tārīkh-i qom. Edited by Jalāl al-Dīn Tehrānī. Tehran: Tūs, [n.d].
  • Qummī, Shaykh ʿAbbās. Muntahā l-āmāl fī tawārīkh al-Nabī wa al-Āl. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1422 AH.
  • Shūshtarī, Muḥammad Taqī. Tawārīkh al-Nabī wa al-Āl. Tehra: 1391 AH.
  • Sibṭ b. al-Jawzī, Yūsuf b. Qazāwughlī. Tadhkirat al-khawāṣ. Qom: al-Sharīf al-Raḍī, 1418 AH.
  • Shubayrī Zanjānī, Sayyid Mūsā . Jurʿa-eī az daryā. Qom: Muʾassisa kitāb shināsī Shīʿa, 1394 SH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿUyūn akhbār al-Riḍā. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1404 AH.
  • Sajjādī. "Āstāna-yi Haḍrat-i Maʿṣūma", Dāʾirat al-Maʿārif buzurg-i Islāmī. volume 1. Tehran: Markaz-i Dāʾirat al-Maʿārif buzurg-i Islāmī, 1367 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Dalāʾil al-imāma. Qom: Nashr-i Biʿthat, 1413 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Edited by ʿAbd al-Amīr Muhannā. 1st edition. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1413 AH.
  • Shirāfat, Amīr Ḥusayn. Kungira-yi Buzurgdāsht-i Haḍrat-i Fāṭima Maʿṣūma wa Makānat-i Farhangī-yi Qom. Waqf-i Mīrāth-i Jāwīd, no 52, 1384 SH.
  • Aṣgharīnizhād, Muḥammad. Nazarī bar asāmī wa al-qāb-i Hadrat-i Fāṭima Maʿṣūma. Farhang-i Kawthar. no 35. 1378 SH.
  • Ustādī, Riḍā. Āshnāʾī bā ʿAbd al-ʿAzīm wa maṣādir sharḥ-i ḥāl-i ū. Nūr al-ʿIlm: [n.p. p. 50 and 51.