Akili
Akili ( العقل) ni mojawapo ya uwezo wa utambuzi wa mwanadamu na mojawapo ya vyanzo vinne vya kupata hukumu za sheria katika fiqhi ya Shia. Akili ina umuhimu maalumu katika mafundisho ya Kiislamu na imekuwa ikizingatiwa kuwa ni uthibitisho na huja kwa wanadamu kama Manabii. Katika baadhi ya riwaya, akili inazingatiwa kuwa, kiumbe wa kwanza kuumbwa na Mwenyezi Mungu.
Wataalamu wa elimu ya ufahamu (epistemolojia) wanasema kuwa, akili ni nguvu ya kuelewa na kudiriki dhana jumla na wanaipa kazi mbili za kushuhudia (kudiriki na kufahamu mambo ya wazi) na ya kihoja (ugunduzi wa maarifa ya kinadharia). Akili imegawanywa katika aina mbili: Akili ya kinadharia na kivitendo; akili ya kinadharia inaelewa na kudiriki ukweli na akili ya kivitendo ina kazi ya nasaha, mapendekezo na maarisho au maagizo.
Pamoja na Qur'ani, Sunna na Ijmaa, akili ni mojawapo ya vyanzo vinne vya kupata hukumu za Sheria kwa mujibu wa madhehehu ya Shia. Wanachuoni wa Shia pia wanathibitisha baadhi ya kanuni za kifiqhi na za usul kupitia akili.
Chanzo cha Maarifa
Wataalamu wa elimu ya ufahamu (epistemolojia) wanaichukulia akili kama ilivyo hisi kuwa ni chanzo cha maarifa na wanaamini kwamba, wanadamu huelewa dhana jumla kupitia kwayo; tofauti na hisi ambayo mambo madogo hueleweka kwayo. [1] Katika epistemolojia, aina mbili za utendaji hubainishwa kwa ajili ya akili: Utendaji wa kushuhudia (kudiriki na kufahamu mambo ya wazi) ambapo kupitia kwayo mtu huweza kudiriki maalumati na mambo ya awali; na ya kihoja (ugunduzi wa maarifa ya kinadharia), ambapo hili humsaidia kupata habari mpya. Kupitia utendaji wa awali wa akili, mwanadamu huweza kufahamu mambo ya wazi na yasiyo na shaka na utendaji wa pili humfanya afikie elimu na maarifa ya kinadharia. [2]
Akili ya Kinadharia na Akili ya Kivitendo
Akili imegawanywa katika makundi mawili. Kwa maana kwamba, kuna akili za aina mbili: Akili ya kinadharia na akili ya kivitendo. Utendaji wa akili ya kinadharia ni kuelewa ukweli na utendaji wa akili ya kivitendo ni kuamuru. Wengine wanaamini kwamba, wanadamu hawana aina mbili tofauti za akili; badala yake mwanadamu ana nguvu ambayo ni chombo chake cha udiriki utambuzi wake. Kulingana na maoni haya, tofauti kati ya akili ya kinadharia na akili ya kivitendo inahusiana na mambo ambayo yanatambuliwa na kudirikiwa. [3] Kwa mujibu wa Muhammad Baqir Sadr, kazi ya akili ya kinadharia ni kufahamu na kudiriki mambo kiujumla yaani yale ambayo yanastahili kujulikana na haina uhusiano wowote na hali ya kivitendo na matumizi; kama vile: aina ya kanuni za kimantiki, hisabati, falsafa na kitheolojia ambazo ni za kategoria za kujua na kuamini. [4]
Nafasi ya Akili katika Uislamu
Kwa mujibu wa Murtaza Mutahari, hakuna dini iliyothamini akili kama Uislamu. Dini ya Uislamu imeipa umuhimu na itibari kubwa akili. [5] Imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba, mazuri yote yanatambuliwa na kudirikiwa kupitia akili na mtu ambaye hana akili, hana dini. [6] Imam Kadhim (a.s) pia ameihesabu akili kuwa ni hoja ya ndani ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kama walivyo Mitume na Maimamu ambao ni hoja ya dhahiri ya Mwenyezi Mungu. [7] Katika hadithi kadhaa zilizonukuliwa kutoka kwa Masuni na Mashia, kumeashiriwa nafasi na daraja ya akili na kwamba, ni kiumbe wa kwanza wa Mwenyezi Mungu. Katika hadithi ndefu ambayo Mtume (s.a.w.w) anamhutubu Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s) amesema katika sehemu moja kwamba: Ewe Ali hakika akili ni kiumbe wa kwanza wa Mwenyezi Mungu, na baada ya kuiumba aliiamwambia: Njoo, ikaja, akasema rudi, ikarudi, akasema, naapa kwa utukufu wangu na adhama yangu, sikuumba kiumbe mpendwa zaidi kwangu kuliko wewe, na hakika amri na makatazo, adhabu na ujira wangu ni juu yako. [8] Kwa maana kwamba, maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu na vilevile adhabu na thawabu yote haya ni kwa mujibu wa akili. Ghazali pia amesema katika kitabu chake cha Ihyaa al-Ulum akinukuu madhumuni kutoka kwa Mtume ya kwamba, akili ni kiumbe wa kwanza wa Mwenyezi Mungu. «أوّل ما خلق اللّه العقل; Kitu cha kwanza alichooumba Mwenyezi Mungu ni akili.» [9] Katika madheherbu ya Shia, mbali na misingi ya kiitikadi ambayo huthibitishwa kwa akili, [10] baadhi ya kanuni za kifikihi na za ki-Usul na hukumu za fikihi pia zinathibitishwa kupitia akili. [11] Jawadi Amuli, mwanafalsafa mkubwa wa Kishia ametumia mstari wa mwisho wa hotuba ya Sheikh Kulayni iliyojaa baraka katika utangulizi wa kitabu cha Usul al-Kafi ambaye ameandika: “Hivyo akili ni nguzo inayozunguka mzingo wa dunia, na kwayo inatumika kuwa hoja, na kwayo ndipo malipo na adhabu hutekelezwa” na kubaisha kwamba, kitovu cha utamaduni wa Kiislamu, hekima na elimu na maarifa katika Uislamu ni akili. Aidha anasema, hotuba hii imetolewa ufafanuzi na Mirdamad katika kitabu chake cha al-Rawashih al-Samawiyah na siri ya ufafanuzi wa Mullah Sadr wa kitabu cha Kafi ni hotuba hii ya Kulayni. [12]
Nafasi ya Akili katika Fikihi ya Shia
- Makala kuu: Hoja ya kiakili
Muhammad Ridha Mudhaffar mmoja wa mafakihi wa karne ya 14 Hijria anasema kuwa, akili pamoja na Qur’an, sunna na Ijmaa, vinahesabiwa kuwa vyanzo vinne vya kunyambua Hukumu za kisheria. [13] Mafakihi wa Kishia, wanatumia sana akili katika Ijtihadi. Baadhi ya maeneo yanayotumiwa akili ni katika elimu ya Usul. Baadhi ya matumizi ya akili ya mchakato wa kunyambua hukumu za fikihi ni:
- Chanzo cha hukumu ya kisheria katika Qur'ani na Sunna: Kuna wakati akili hutumiwa kwa sura ya kujitegemea kwa ajili ya baadhi ya hukumu za kisheria; kama vile hukumu ambazo zinapatikana kupitia njia ya kitu kizuri na kibaya kwa mujibu wa akili. Kuna wakati pia akili huwekwa kando ya hukumu fulani ya kisheria na hivyo kuthibitisha hukumu nyingine ya kisheria; kama vile pale inapolazimu kuweko hukumu ya kisheria na hukumu ya kiakili na hivyo kufikia hukumu mpya ya kisheria.
- Kuthibitisha itibari ya maandiko ya kidini: Moja ya masharti ya itibari ya hadithi na kufanyia kazi maudhui yake ni kwamba, hilo lisiwe na upinzani na hukumu isiyo na shaka ya akili. Yaani hadithi isipingane na akili. Kwa mfano, kwa kuzingatia kwamba, Umaasumu wa Mtume (s.a.w.w) umethibitishwa kiakili, hadithi ambazo zinapinga Umaasumu, hazina itibari na mashiko.
- Kusaidia kunyambua hukumu za sheria kutoka katika Qur'ani na hadithi: Baadhi ya kanuni za Kifikihi ambazo kupitia kwazo hunyambuliwa sheria kutoka katika Kitabu na Sunna, hugunduliwa na kufikiwa kwa msaada wa akili. [14].