Tharallah

Kutoka wikishia

Tharullah (Kiarabu: ثارُ الله) kwa maana ya damu ya Mwenyezi Mungu ni moja ya lakabu za Imamu Hussein (a.s). Katika Ziyarat Ashura Imamu Hussein anasalimiwa kwa anuani hii. Kumebainishwa tafsiri mbalimbali kuhusiana na Tharullah’ miongoni mwazo ni kuwa, Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kulipiza kisasi cha damu ya Imamu Hussein; kadhalika mtu ambaye amelipiza kisasi cha damu katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Lakabu ya Imamu Hussein (a.s)

Tharullah ni katika lakabu za Imamu Hussein (a.s). Katika baadhi ya matini za hadithi ikiwemo Ziyarat Ashura Imamu Hussein (a.s) anasalimiwa kwa anuani ya Tharullah na Ibn Tharih (mtoto wa Tharullah). [2] Allama Majlisi anasema: Katika baadhi ya nakala za Kitabu cha al-Kafi [3] neno Tharullah limetumika. [4]

Neno Tharullah limetumika pia katika mashairi ya baadhi ya washairi wa kale. Kwa mfano Ibn Rumi mshairi wa Kishia (aliaga dunia 283 Hijiria) katika beti zake za mashairi alizotunga katika maombolezo ya Yahya bin Omar alitumia neno Tharullah. [5] Yahya bin Omar alikuwa anatokana na kizazi cha Imamu Hussein (a.s) na ni katika wajukuu zake, ambaye alianzisha harakati na mapambano dhidi ya al-Muntasir Abbasi Khalifa wa Bani-Abbas. [6]

Maana

Tharullah imechukuliwa kutoka katika neno Tha’ar na miongoni mwa maana zake ni kupigania damu ya aliyeuawa au kulipiza kisasi cha damu ya aliyeuawa. [7] [8] Katika baadhi ya hadithi, baada ya kuashiriwa kwamba, Imamu Hussein ni “Tharullah fil Ardh”, Mwenyezi Mungu ametambulishwa kuwa yeye ndiye mlipizaji kisasi cha damu yake ambapo anawaita na kuwataka watu walipize kisasi cha damu yake. [9] Allama Majlisi anasema, makusudio ya Tharullah ni kuwa, Imamu Hussein mwenyewe ndiye atakayelipiza kisasi cha damu yake na familia yake katika kipindi cha Rajaa. [10]

Maana zingine

Katika kitabu chake cha Shifa al-Sudur akitoa ufafanuzi kuhusiana na Ziyarat Ashura, Abul-Fadhl Tehrani ametaja maana tano ambazo anasema inawezekana zote hizo zikawa na maana ya Tharullah:

  1. Tharullah katika asili ilikuwa ni “Ahl Tharallah”. Kwa msingi huo ni kwa maana ya mtu ambaye anastahiki Mwenyezi Mungu alipize kisasi cha damu yake.
  2. Aliyeuawa ambaye Mwenyezi Mungu analipiza kisasi cha damu yake.
  3. Tharullah katika asili ilikuwa ni “al-Thair Lilah” lakini ikabadilishwa kimakosa katika kusikia au kuandika (Tas’hif). Kwa msingi huo maana yake ni mtu ambaye amepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na akalipiza kisasi cha damu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
  4. Tharullah ni mithili ya Ainullah (jicho la Mwenyezi Mungu) na Yadullah (mkono wa Mwenyezi Mungu) ambapo haijakusudiwa maana yake ya kidhahiri ya damu ya Mwenyezi Mungu bali ni kama ilivyo katika sifat Khabariyah ambapo hutumika maana ya kimajazi yaani isiyo ya kiuhalisia, kama vile Wajhullah, (uso wa Mwenyezi Mungu) Yadullah (mkono wa Mwenyezi Mungu) na kadhalika.
  5. Tharullah kwa maana ya damu iliyolipizwa kisasi na kuongezwa neno Allah inatokana na kuwa, Mwenyezi Mungu ndiye walii halisi wa damu hii. [11]

Athari zinazohusiana

Ali Akbar bin Muhammad Amin Lari, katika karne ya 13 aliandika kitabu kwa jina la Ufafanuzi wa hadithi “Ya Tharallah wabna tharih” ambapo maudhui kuu katika hilo ni kuthibitisha utoharifu wa damu ya Maimamu. Katika kitabu hiki kuna maudhui pia kuhusiana na Umaasumu. [16] Nakala ya hati ya mkono ya kitabu hiki yenye namba 4086 inapatikana katika Maktaba ya Ayatullah Mar’ashi Najafi katika mji wa Qom, Iran. [17]

Vyanzo

  • Abū l-Faraj al-Iṣfahānī, Maqātil al-ṭālibīyyīn. Edited by Sayyid Aḥmad Ṣaqar. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Farāhīdī, Khalīl b. Aḥmad al-. Al-ʿAyn. Edited by Mahdī Makhzūmī & Ibrāhīm Sāmirrāʾī. Qom: Hijrat, 1410 AH.
  • Ibn Qulawayh, Jaʿfar b. Muḥammad. Kāmil al-zīyārāt. Edited by ʿAbd al-Ḥusayn Amīnī. Najaf: Dār al-Murtaḍawīyya, 1356 Sh.
  • Ibn Rūmī, ʿAlī b. ʿAbbās. Dīwān. Edited by ʿAbd al-Amīr ʿAlī Mahnā. Beirut: [n.d], 1411 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Ṭihrānī, Abū l-Faḍl b. Abū l-Qāsim al-. Shifāʾ al-ṣudūr fī sharḥ zīyārat al-ʿĀshūr. Tehran: Murtaḍawī, 1376 Sh.
  • Zubaydī, Muḥammad Murtaḍā al-. Tāj al-ʿarūs min jawāhir al-qāmūs. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Fikr, 1414 AH.