Hajar

Kutoka wikishia

Hajar ni mke wa Nabii Ibrahim (a.s) na ndiye mama yake Nabii Ismail. Hajar alikuwa kanizi wa mfalme wa Misri ambaye alimtoa zawadi na kumpatia Sarah mke wa Ibrahim (a.s). Kisha Sarah baadaye alimuuza Hajar kwa Ibrahim na baada ya muda akamzaa Ismail.

Baada ya kuzaliwa kwa Ismail, kufuatia kukasirika na kukosa raha Sarah kutokana na Hajar kuzaa ilihali yeye hakuwa na uwezo wa kuzaa, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Ibrahim alimhamisha Hajar na mtoto wake kutoka Sham hadi Makka, ambayo ilikuwa jangwa kavu na lisilokaliwa na watu wakati huo. Kwa mujibu wa nukuu ya Torati, kinyume na vyanzo vya Kiislamu, kuhama kwa Hajar kulikuwa baada ya kuzaliwa kwa Is'haq na bila ya kufuatana na Ibrahim. Kaburi la Hajar liko katika sehemu ya Hijr Ismail.

Familia

Kulingana na nukuu moja, Hajar alikuwa binti ya mfalme wa Misri ambaye alifanywa mtumwa na kuuzwa kwa mfalme mpya wa Misri baada ya kikundi cha watu wa Ain al-Shams kumuasi mfalme wa Misri.[1] Katika simulizi ya kihistoria, Mtume wa Uislamu, Muhammad (s.a.w.w), aliwataka masahaba wake waamiliane na watu wa Misri kwa upole; kwa sababu Hajar alikuwa mmoja miongoni mwao.[2]

Hajar, zawadi ya mfalme wa Misri kwa Sarah

Kwa mujibu wa ripoti ya Ibn Athir, Ibrahim aliagizwa na Mwenyezi Mungu kuhama kutoka Babeli alipokuwa na umri wa takribani miaka 70; [3] kwa muktadha huo akiwa pamoja na mkewe Sarah, mpwa wake Lut na baadhi ya wafuasi wengine, walikwenda Misri. Mfalme wa Misri alimtamani Sarah na kumtaka. Ibrahim naye akifanya Taqiyyah alikuwa amemtambulisha Sarah kuwa ni dadake. Kwa mujibu wa ripoti ya ibn Athir, kila mara mfalme alipokuwa na nia mbaya kwa Sarah, mkono wake ulikuwa ukikauka. Tukio hilo lilijikariri mara tatu. Hatimaye mfalme wa Misri akamtaka Sarah amuombee dua ili mkono wake urejee katika hali ya kawaida. Baada ya Sarah kuomba dua na mkono wa mfalme ukarejea kama ulivyokuwa mwanzo, alimuachia huru na akamapatia Hajar kama zawadi ambaye alikuwa kanizi. [4] Kwa mujibu wa Allama Tabatabai ni kuwa, hii kwamba, Ibrahim alimtambulisha Sara kama dada yake ni jambo ambalo haliendani na cheo cha Utume, na ni mojawapo ya mambo yanayokinzana (migongano) na Torati ya sasa, ambayo yamekuja katika vyanzo vya kihistoria na hadithi za Sunni. [5] Pia, kwa mujibu wa hadithi iliyonukuuliwa na Allama Tabatabai kutoka katika kitabu cha al-Kafi ni kwamba, katika mkasa huu Ibrahim alimtambulisha Sarah kama mke wake, na kila wakati mkono wa mfalme ulipokauka, ilikuwa ni kwa sababu ya maombi ya Ibrahim ambapo mkono wake ulikuwa ukirejea katika hali yake ya awali. [6]

Tukio la kuhajiri kutoka Sham kwenda Makka

Ibrahim hakuwa akiweza kupata mtoto pamoja na Sarah, kwa hiyo Sara akamuuza Hajar ili Ibrahim apate mtoto kutoka kwake yaani aweze kuzaa naye. [7] Baada ya muda Hajar alipata ujauzito na akajifungua Ismail. [8] Hata hivyo hilo lilimhuzunisha Sarah ambaye hakuwa na uwezo wa kuzaa na hakuwa na watoto. [9] Baada ya Ismail kuzaliwa na jambo hilo kutomfurahisha Sarah, Mwenyezi Mungu alimwamuru Ibrahim kuwahamisha Ismail na mama yake kutoka Sham (Syria ya leo) hadi Makka. [10] Ibrahim akawahamishia wawili hao huko Makka, ambayo ilikuwa jangwa lenye ukame na lisilokaliwa na watu wakati huo, na akawaweka mahali ambapo baadaye nyumba ya Mungu ilijengwa upya, karibu na kisima cha Zamzam.[11] Jina la Hajar halijatajwa katika Quran, lakini katika Surat Ibrahim, tukio la kuhama kwake kutoka Sham kwenda Makka limezungumziwa. [12]

Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq, Ibrahim alipowaacha Hajar na Ismail katika ardhi ya Makka na kurejea. Ismail alihisi kiu na Hajar akaenda huku na huko baina ya milima miwili ya Safa na Marwa mara saba kwa ajili ya kutafuta maji, lakini hakupata. Wakati Hajar alipomkaribia Ismail, aliona kwamba alikuwa amelala chini kwa sababu ya kiu na maji yalianza kutoka chini ya miguu yake, na eneo hilo kugeuka kuwa chemchemi na ndio inayojulikana hii leo kwa jina la kisima cha Zamzam. Tukio hili limekuwa sababu ya kuwa wajibu mojawapo ya matendo ya Hija nayo ni kutembea mara saba baina ya Safa na Mar’wa. [14]

Kulingana na vyanzo vya Kiislamu, kuhama kwa Hajar kulikuwa kabla ya kuzaliwa kwa Is’haq na kwa sababu ya kuchukizwa kwa Sarah kutokana na Hajar kuzaa na kupata mtoto. [15] Ingawa kulingana na ripoti ya Torati, Hajar alihama baada ya kuzaliwa kwa Is’haq. [16] Katika Torati, sababu ya agizo la Mungu kwa Ibrahim kuwahamisha Hajar na Ismail kutoka Sham na kuwapeleka Makka inaelezwa kuwa Sarah alimuona Ismail akimsumbua Is’haq, hivyo alimwambia Ibrahim, mtoto wa huyu kijakazi (Hajar) yaani Ismail hawezi kuwa mrithi wako kutokana na kuweko mwanangu Is’haq; hivyo mfukuze Sarah na mtoto wake kutoka katika nyumba. [17] Kadhalika kwa mujibu wa Torati na kinyume na mapokeo ya Kiislamu [18] Ibrahim hakufuatana na Hajar na Ismail katika hijra hii.[19]

Kuaga dunia

Picha ya Hijr Ismail na mahali alipozikwa Hajar.

Kwa mujibu wa nukuu, Hajar alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90. [20] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s), Ismail alimzika Hajar mahali pa Hijr Ismail na akainua kaburi lake na akajenga ukuta juu yake ili watu wasiweze kulikanyaga wakati wakipita. [21]

Kulingana na baadhi ya riwaya, ni kwa ajili ya kuheshimu kaburi lake ambapo Waislamu wakati wa kufanya tawafu (kuzunguka al-Kaaba) huwa hawapiti ndani yake badala yake wanapita pembeni yake ili wasikanyage kaburi la Hajar.[22]


Vyanzo

  • The Qurʾān.
  • The Bible, New Revised Standard Version.
  • Balʿamī, Tārīkhnāma-yi Ṭabarī. Edited by Muḥammad Rawshan. Tehran: Intishārāt-i Alburz, 1373 Sh.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kabīr. Edited by ʿAbd al-Qādir Aḥmad ʿAṭā. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1410 AH-1990.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Ṭayyib Mūsawī Jazāʾrī. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿIlal al-sharāʾiʿ. Qom: Intishārāt-i Dāwarī, 1385 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Mūhammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Fifth edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.