Tawassul

Kutoka wikishia

Tawassul (Kiarabu: التَّوسل) ni utaratibu wa kumuomba Mwenye Ezi Mungu kwa njia ya kumweka mbele mtu au kitu fulani kwa ajili ya kumkaribia Yeye (Mungu) na kutimizwa kwa mahitaji au muradi maalum. Tawassul ni sehemu ya imani shirikisho ianayowashirikisha Waislamu wote duniani, na uhalali wake umethibitishwa kwa kupitia ushahidi mbalimbali zikiwemo; Aya za Qur'ani, (kama vile Aya ya Wasila), Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w), nyenendo za Waislamu katika zama mbali mbali, Hadithi za Maimamu watukufu (a.s), na hoja za kiakili. Tendo la kutawasali (Tawassul) lina umuhimu na nafasi maalum miongoni mwa Mashia, wao sio tu huomba msaada kwa kumtanguliza bwana Mtume na Maimamu watukufu (a.s), bali pia kwa kuwatanguliza watu wa familia ya Maimamu (a.s) kama vile; wake zao, mama zao, na pia wana wa Maimamu hao. Mashia wakati wa kutembelea makaburi ya Maimamu na wana wa Maimamu wao (a.s), husoma matini maalumu zijulikanazo kwa jina la matini za ziyara, ambapo kwa kupitia matini hizo, wao huomba msaada kwa njia mbalimbali wakiwa makaburi humo.

Inasemekana kuwa imani ya kutawasali, ilikuwa ni ya kawaida na mashuhuri miongoni mwa madhehebu yote ya Waislamu hadi karne ya nane Hijria; ilipoingia karne hii, kulizuka vuguvugu kubwa kutoka upande wa Kisalafi dhidi ya aina mbali mbali za kutawasali, ambapo aina mbali za kutawasali zilihisabiwa kuwa ni haramu na wanazuoni hao wa Kisalafia, hususan Ibn Taymiyya. Miongoni mwa waliyo yahisabu kuwa ni haramu ni: kutawsali kwa kupitia dhati ya bwana Mtume (s.a.w.w), kupitia watu wema, kutawasali kwa kuzitanguliza hadhi na nafasi walizo nazo watu wema mbele ya Mwenye Ezi Mungu, pamoja na kuomba dua kupitia watu wema baada ya kifo chao. Baada ya karne chache, na kuenea kwa madhehebu ya Kiwahabi, tawassul ilikabiliwa na upinzani mkumbwa mno kutoka kwa Mawahabi.

Sababu kuu itegemewayo ma wanazuoni wa Kisalafi na Mawahabi ambayo huitumia kama ni ushahidi, ni ni madai yao sayemayo kwamba; hakuna ripoti zozote zinazothibitisha utekelezwaji wa aina hizi za kutawasali miongoni mwa masahaba wa bwana Mtume (s.a.w.w). Mtazamo huu wa Masalafi na Mawahabi kuhusiaa na amali ya kutawasali, umepingwa na wanazuoni kadhaa kutoka upande wa Shia pamoja na Sunni. Wao katika kukabiliana na pinzani za upande wa Kisalafia, wamejaribu kutoa baadhi ya Hadithi na ripoti za kihistoria zinazo thibitisha ya kwamba; masahaba wa bwana Mtume walikuwa na kawaida ya kutekeleza aina kama hizi za amali ya kutawasali.

Nafasi ya Tawassul Mbele ya Waislamu

Makubaliano ya Waislamu Kuhusiana na Uhalali wa Asili ya Tawassul (Kutawasali)

Tawassul ni miongoni mwa imani shirikisho na za pamoja kati ya Waislamu. [1] Ibnu Taymiyyah alikubali uhalali wa asili ya Tawassul, na kusema kwamba ni amali yenye makubaliano ya Waislamu wote dunianai. [2] Taqi al-Din al-Subki, mwanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i kutoka Misri aliyefariki mwaka 756 Hijria, katika kitabu chake Shifau al-Saqam, ameeleza akisema kwamba; mabishano na migogoro kuhusiana na amali za Tawassul, ni sawa udadisi na pingamizi dhidi ya mambo msingi ya dini ya Kiislamu. [3] Jafar Subhani, mwanatheolojia wa Shia, pia naye amihisabu amali ya kutawasali katika maisha ya mwanadamu, kuwa ni jambo linalofungamana na hisia za kimaumbile kwa kila mwanadamu. [4]

Upinzani wa Mawahabi Kuhusu Uhalali wa Baadhi ya Aina za Tawassul (Kutawasali)

Imeelezwa ya kwamba; Amali ya kutawasali ni amali maarufu miongoni mwa makundi mbali mbali ya Kiislamu, hususan miongoni mwa Mashia Imamiyya na kwa kiasi fulani miongoni mwa Waislamu wenye imani za Kisufi. Ila kuanzia karne ya nane Hijria, baadhi ya wanazuoni wa Kisalafi, hasa Ibn Taymiyyah, walipinga na kutia shaka na pingamizi kuhusiana na uhalali wa aina fulani za Tawassul. Hili lilisababisha mizozo kati ya Shia, Masunni na Masalafi juu ya kuwepo kwa uhalali wa kutawasali katika sheria za Kiislamu, na vitabu vikaandikwa dhidi ya maoni ya Masalafia hao. [5] Miongoni mwa vitabu hivyo ni Shifa al-Siqam kilichoandikwa na Taqi al-Din al-Subki kinacho pinga maoni mbali mbali ya wanazuoni wa Kisalafi, hasa maoni yao dhidi Tawassul. [6]

Leo (karne ya kumi na tano Hijria) Mawahabi, wakifuata itikadi za Masalafi (wanazuoni wao wa kale), wamekuwa wakijenga shaka na pingamizi kadhaa dhidi ya uhalali wa aina fulani za Tawassul. Jambo ambalo limefufua upya mjadala juu ya Tawassul na kupewa umuhimu mkubwa mbele ya wanazuoni wa Shia na Sunni. Juhudi za wanazuoni wa Kisunni pamoja na Shia, zimepelekea kuandikwa kwa vitabu kadhaa vinavyo kuchunguza na kosoa maoni ya Kiwahabi. [7]

Jinsi ya Mashia Wanavyo Ithamini Tawassul

Tawassul ina nafasi kubwa na maalum miongoni mwa Mashia, wao sio tu hutawasali kwa bwana Mtume s.a.w.w na Maimamu Maasum (a.s), bali pia kwa watu wa familia ya Maimamu wao (a.s), kama vile; kwa wake na mama zao, na pia wana wa Maimamu hao (a.s). [8] Wakati wa kutembelea makaburi ya Maimamu au wana wao (a.s), Mashia husoma matini maalumu ziitwazo matini za ziara, zinazo jumuisha amali ya kutawasali kupitia Maimamu au wana wao (a.s) waliozikwa makaburini humo. [9]

Kutawasali kwenye maana ya kuomba msaada, kunaweza kufanyika kwa namna mbili: kwa njia ya mtu mmoja binafsi au njia ya kikundi. Dua ya Tawassul ni miongoni mwa dua maarufu kati ya Waislamu wa Shia; hasa nchini Iran, dua hii husomwa kwa pamoja kila wiki, na mara nyingi husomwa usiku wa Jumatano. Wasomaji wa dua hii ima hukusanyika majumbani mwao, misikitini, makaburini, au katika majengo yajulikanayo kwa jina la Husseiniyya. Katika dua hii, watu hutawasali na kuomba msaada kutoka kwa Ma'asumina kumi na nne (a.s). [10] Wakati mwingine pia, hufanyika dhifa maalumu kwa ajili ya kutawasali na kuomba msaada huko ili kutimiziwa baadhi ya mahitaji yaombwayo na watu hao. Kwa mfano, nchini Iran, baadhi ya watu hufanya dhifa kwa jina la Imamu Zainul Abidin (a.s), ili kuomba ponyo kwa ajili ya mgonjwa au kutimizwa kwa mahitaji yao mengine. [11] Pia, ni jambo la kawaida miongoni mwa Mashia wa Iran, kuandaa chakula kwa jina la Bibi Rukia (Ruqayyah) kwa ajili ya kuomba usahili katika mambo mbli mbali kama vile; ndoa, kupata kizazi na mahitaji ya kifedha.

Bila shaka miongoni mwa madhehebu ya Kisunni pia kuna matokeo yaliyorikodiwa kuhusiana na amali ya tawassul. Kwa mfano, imeripotiwa ya kwamba; Sam'ani, mwanahistoria, mwanahadithi na faqihi wa madhehebu ya Shafi'i wa karne ya sita Hijria, alikuwa akienda kuzuru kaburi la Imamu Kadhim (a.s) na kumtaka msaada. [12] Abu Ali Khallal, mmoja wa wanazuoni wa Ahlu al-Sunna wa karne ya tatu Hijria, amesema kwamba; kila yeye alipokuwa na tatizo, alikuwa akienda kuzuru kaburi la Musa bin Ja'afar na kumtaka msaada, na tatizo lake lilikuwa likitatuliwa. [13] Pia, imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Idris Shafi'i, mmoja wa mafaqihi wanne wa Ahlu-Sunna, ya kwamba; yeye aliliarifisha na kulielezea kaburi la Musa bin Ja'far kuwa ni "dawa yenye sifa ya uponyaji." [14]

Welewa wa Dhana ya Tawassul na Uhalali Wake

Tawassul inamaanisha ile amali ya mtu kumtanguliza mtu au kitu fulani chenye nafasi maalum mbele ya Mungu, katika maombi yake, kama kiungo na njia ya kukubaliwa dua zake. [15] Kimsingi na kilugha, neno tawassul linahusiana na neno wasila (njia). [16] "Wasila" ni kitu chochote kile kinachotumiwa ili kujikaribisha kwnye kitu chengine. [17]

Baadhi ya watafiti hulichukulia neno Tawassul kuwa na maana sawa na neno istighatha (kuomba wokovu). Hata hivyo, wengine wametofautisha kati ya maneno mawili haya. [18] Wakifafanua juu ya tofauti zake, wamesema kwamba; Istighatha inahusiana na hali ya dharura na shida, wakati tawassul haijachukuliwa tu kwa ajili ya hali ya dhiki au dharura maalumu, bali pia inajumuisha kila hali, ikiwemo hali ya utulivu na faraja. [19]

Hoja Juu ya Uhalali wa Tawassul

Sababu za halali wa kutumia Tawassul kwa mujibu wa vyanzo vya sheria, imeelezewa kama ifuatavyo:

  • Qur’ani: Katika Qur’ani, Mwenye Ezi Mungu amewaamrisha waumini kutafuta njia kwa ajili ya kumkaribia Mola wao. [20] Aidha, katika Aya ya 64 ya Surat An-Nisa, wakosaji waliotenda dhambi, wanashauriwa kwenda kwa bwana Mtume (s.a.w.w) na kumuomba awaombee dua kwa ajili yao, ili Mwenyezi Mungu awakubali na awasamehe makossa yao. [21] Aya nyingine inayoashiria uhalali wa kutumia kutawasali, ni ile Aya ya 97 ya Surat Yusuf, [22] ambapo watoto wa Nabii Ya'aqub walimwomba baba yao kuwaombea msamaha kwa Mola wake. [23]
  • Riwaya: Kuna Riwaya nyingi kutoka vyanzo vya Kishia na Kisunni zinazo onesha uhalali na ruhusa ya kutumia tawassul katika sheria ya Kiislamu. [24] Riwaya hizi zinaashiria uhalali wa kutumia njia (tawassul) kwa ajili ya kuomba dua na kuomtaka Mwenye Ezi Mungu msamaha. [25]
  • Silka na nyenendo za Waislamu: Historia ya Waislamu wa mwanzo pamoja na Masahaba wa bwana Mtume (s.a.w.w) inaonesha kuwa; kutumia njia ya kutawasali kwa Mtume (s.a.w.w) ilikuwa jambo la kawaida na linalokubalika na lenye hadhi katika jamii za Waislamu waliopita. [26] Kwa mfano, katika kitabu Sahih Bukhari kuna sura iitwayo "Abwabu Al-Istisqaa". Sura ambayo imenukuu Hadithi mbalimbali kuhusiana na Masahaba waliokuwa wakimtanguliza na kumtumia bwana Mtume (s.a.w.w), katika dua zao za kuomba mvua. [27] Hii yaonesha kwamba, kutawasali ni jambo linalokubalika kisheria na linalofaa kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.
  • Dalili za kiakili: Kutawasali au kumtanguliza mtu mtukufu Mwenye Ezi Mungu, husababisha waja kumkaribia Mwenye Ezi Mungu, jambao ambalo ndio lengo kuu la ibada za waja katika kumwabudu Mwenye Ezi Mungu; kwani bila kumkaribia Mwenye Ezi Mungu, katu mwanadamu hataweza kuifikia furaha wala mafanikio, si duniani wala si Akhera. Kwa upande mwingine, kujikaribisha huku hakupatikani bila ya mtu kuwa na njia maalumu ya kujikaribisha na Mola wake. Kwa hivyo, furaha na wokovu wa duniani na Akhera, vimeegemea kwenye amali hii ya tawassul. [28]

Upinzani wa Mawahabi Dhidi ya Uhalali wa Kutawasali kwa Mtume (s.a.w.w) na Waja Wema

Miongoni mwa mifano ya kutafuta shufa'a kwa kumtanguliz bwana Mtume (s.a.w.w) au waja wema ni kama vile kauli isemayo: «اللهمَّ انّی أتوسلُ إلیک بنبیکَ محمد (ص) اَن تقضی حاجتی ; Ewe Mwenye Ezi Mungu, mimi najitafutia njia ya kukufikia wewe kwa kumpitia Mtume wako Muhammad (s.a.w.w) ili uitimize haja yangu». [29]

Kulingana na fatwa ya Daru al-Ifta Misri (Kitengo cha Utoaji Fatwa cha Misri), kuhusiana na tawassul:

«Ni kwamba; Ni halali na ni sunna (inapendekezwa) kwa mja fulani kutawasali kupitia manabii, mawalii, na waja wema wa Mwenyezi Mungu na kutafuta baraka na msaada kutoka kwao, pia kuna dalili kadhaa kutoka katika; Qur'ani, Sunna, na matendo ya Masahaba zinathibitisha uhalali na kupendekezwa kwa amali hiyo ya tawassul. Vile vile, kama ilivyokuwa ni halali kwa kupitia kwa nafsi za watu hao, pia ni halali kutawasali kupitia vyeo pamoja na hadhi zao, na wala upinzani wa makundi machache hauwezi kuwa na nafasi ya kulipiku suala hili». [30][1]

Kulingana na maelezo ya Isa bin Abdullah Hamyari, mtafiti wa madhehebu ya Maliki kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ni kwamba; kuanzia karne ya saba Hijria, njia hii ya kutawasali ilianza ilipingwa na baadhi ya wanazuoni wa Kisalafi, na wakati huo huo, wanazuoni wa Kiislamu walisimama kidete na kutoa jawabu dhidi ya upinzani huo wa aina hii ya kutawasali, jambo ambalo lilipelekea kumalizika kwa mzozo huo. Hata hivyo, baadaye, Mawahabi waliibua tena mzozo huu na kuitangaza aina hii ya kutawasali kuwa ni amali batili. [31] Kwa mfano, Muhammad Nasib Rifai (aliyefariki mnamo mwaka wa 1412 Hijria), mmoja wa Mawahabi kutoka Syria, alitangaza kuwa kujikaribisha kwa Mungu kupitia manabii na mawalii wake, ni batili na kukichukulia kitendo hichi kama ni ukafiri na uzushi (bida). [32] Baadae Rifai alidai kuwa hakuna ushahidi wowote ule kutoka kwenye Qur'ani na Sunna za bwan Mtume (s.a.w.w) unaothibitisha uhalali wa aina hii ya kutawasali. [33]

Ukosoaji wa Mtazamo wa Mawahabi Kutoka kwa Wanazuoni wa Kiislamu

Taqiuddin Subki, mwanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i wa karne ya nane Hijria, amesema kwamba; kuna Hadithi nyingi mno ambazo ni sahihi na mutawatir (zilizo pokewa kupitia njia tofauti) zilizotolewa katika kuthibitisha uhalali wa tawassul na kuomba msaada kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na watu wema. [34] Ali bin Abdullah Samhudi (aliyefariki mnamo mwaka 911 Hijria), mwanazuoni wa Kishafi'i kutoka Misri, katika kitabu chake «Wafa' al-Wafa'» alidai kuwa; kuna makubaliano ya wanazuoni (ijmaa) kuhusiana na uhalali wa kutawasali kupitia kwa Mtume (s.a.w.w) pamoja na watu wema. [35] Wanazuoni hawa wamelenga baadhi ya Hadithi zilizopo katika maandiko ya Hadithi za Kisunni ili kuthibitisha madai yao hayo. [36] Kwa mfano, Hadithi iliyopo katika Sahihi Bukhari inasimulia kwamba; Omar bin Khattab aliomba mvua kwa kutawasali kwa Abbas bin Abdul Muttalib (ami ya Mtume). [37]

Pia kuna Hadithi nyingi kutoka kwa Maimamu wa Kishia zinazo onesha uhalali wa kutawasali kwa Mtume (s.a.w.w) pamoja na mawalii wa Mwenye Ezi Mungu. Katika baadhi ya Hadithi hizi, Ahlul-Bayt (a.s) wenyewe wametajwa na kuelezwa kama ni njia za kujikaribisha kwa Mwenye Ezi Mungu. [38] Kwa mfano, Dua ya Tawassul ni moja ya dua ambazo ndani yake watu huomba msaada kutoka kwa Mungu kupitia Ma'asumina kumi na nne (a.s) ili kupata mahitaji yao. [39]

Tuhuma za Uziushi (Bid'a) wa Tawassul Kutoka kwa Ibnu Taymiyyah na Mawahabi

Makala kuu: Kutawasali kupitia wafu

Kwa mujibu wa maoni ya Ibnu Taymiyyah, ni kwamba; Kutawasali kwa Manabii na mawalii wa Mwenye Ezi Mungu baada ya kufa kwao, ni kitendo kisicho halali na ni uzushi (bid'a) katika dini. Yeye yuwasema kwamba; hakuna Sahaba wala faqihi wa zamani aliyewahi kufanya kitendo hichi, na wala hakuna ushahidi unao onesha uhalali ua ruhusa ya tendo hilo. [40] Vilevile, Muhammad bin Abdul-Wahhab, ambaye ni mwanzilishi wa madhehebu ya Mawahaabi, [41] pamoja na wanazuoni wengine wa Kiwahabiwanao shikamana naye, wanalichukulia tendo hili la kutawasali na kuomba msaada kwa kuwaweka kati Manabii na mawalii wa Mwenye Ezi Mungu baada ya kufa kwao, kuwa ni shirki na ni bid'a katika dini. [42]

Uhalali wa Kutawasali kwa Wafu Kulingana na Mtazamo wa Wanazuoni wa Kiislamu

Mtazamo wa Kiwahabi haukuwa ni mtazamo ulioachwa bila jawabu, bali ulikosolewa na kupikuliwa kwa turufu nzito kutoka kwa wanazuoni wa Kishia pamoja na Kisunni. Muhammad bin Ali Shaukani (aliyefariki mnamo mwaka 1250 Hijria), faqihi wa madhehebu ya Zaidiyya, alisimama na kuthibitisha uhalali wa tawassul kupitia kwa Mtume (s.a.w.w), na kuonesha kuwa tendo hili lilifanyika maishani mwa bwana Mtume (s.a.w.w) na hata baada ya kifo chake. Shaukani alithibitisha madai yake kupitia hoja ya makubaliano ya Masahaba, akisema kuwa hakuna Sahaba hata mmoja aliyekataa uhalali wa tawassul kama hii. [43] Ahmad bin Muhammad Qastallani (aliyefariki mwaka wa 923 Hijria), mwanahistoria na mwanahadith wa madhehebu ya Kishafi'i kutoka nchini Misri, amesema kuwa; kuna habari na maandiko yasiyo hisabika kuhusiana na tendo la watu kutawasali kwa bwana Mtume (s.a.w.w) baada ya kifo chake. [44] Kwa mujibu wa maelezo ya Samhudi ni kwamba; hakuna tofauti kati ya kutawasali kwa Mtume (s.a.w.w) wakati wa uhai wake na baada ya kifo chake. [45] Yeye amenukuu Hadithi kutoka katika vyanzo vya Kisunni zinazo onesha kuwa, Sahaba walifanya walitawasali kwa Mtume (s.a.w.w) baada ya kifo chake wakimuomba Mola wa maombi mbalimbali kwa kumtanguliza bwana Mtume (s.a.w.w). [46]

Pia, Jafar Subhani naye amesema kuwa; Kutawasali ilikuwa ni moja ya silka na nyenendo za Waislamu. Na kwamba, kama walivyokuwa wakitawasali kwa Mtume (s.a.w.w) wakati wa uhai wake, pia waliendelea kufanya hivyo baada ya kifo chake. [47] Muhammad bin Zahid Kauthari (aliyefariki mwaka wa 1371 Hijria), mwanazuoni wa madhehebu ya Hanafi kutoka Uturuki, amesema kuwa; Wale wanaokataa tendo la kutawasali kwa manabii na watu wema baada ya kifo chao, kiuhalisia huwa ni sawa wao kukataa uwepo wa roho baada ya kifo cha mwanadamu, na kukataa ufufuo na maisha ya Akhera. [48] Yeye amelihisabu suala la kuzifunga na kuhusisha Hadithi za uhalali wa kutawasali kwa ajili ya wakati wa uhai wa walengwa peke yake, ni kupotosha na kuziweka Hadithi hizo nje ya tafsiri dhahiri bila kutegemea mashiko maalumu katika tafsiri zao hizo za nje ya pazia. [49]

Taqiuddin Subki akiunga mkono suala la kutawasli alisema kwamba:

«Tawassul na istighatha kwa bwana Mtume (s.a.w.w) ni kitendo halali na ni miongoni mwa mambo yapendezayo, ambapo kila mmoja miongoni mwa wacha-Mungu aelewa uhalali na wema wa jambo hilo. Aliendelea kusema kwamba; Kitendo hichi ni miongoni mwa matendo ya manabii na mitume, na ni sunna (silka) ya wanazoni wema waliotangulia (Salafu al-Saleh), pamoja na watu wa kawaida ndani ya jamii za Kiislamu. Katika zama zote na dini zote hakuna aliyekataa kitendo hichi hadi alipo zuka Ibnu Taymiyyah n maneno yake, akawashawishi watu dhaifu na kushuku juu ya jambo hili na kuanzisha bid'a ambayo haijawahi kuwepo katika zama zozote zile zilizopita. [Maelezo 1] Katika nukuu hii, Subki anasisitiza kwamba tawassul na istighatha (kuomba wokovu) yalikuwa ni miongoni mwa mambo yanayokubalika na yanayotambulika kama matendo mema kwa Waislamu wote, na kwamba upinzani dhidi ya vitendo hivi ulianzwa tu na Ibnu Taymiyyah». [50][2]

Maamuzi ya Ibnu Taimiyyah ya Kulihisabu Tendo la Kutawasali Miongoni mwa Ushirikina Kutawasali kwa Hadhi na Heshima ya Mtume (s.a.w.w), huweza kufanyika kwa ibara isemayo: «اللهمَّ إنّی أتوسل إلیک بجاه محمدٍ (ص) و حُرمته أن تقضی حاجتی ; Ewe Mungu, ninakurubisha kwako (ninakuomba) kupitia hadhi na heshima ya bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w), kama ni njia yaw ewe kunipa matilaba yangu». [51] Muhammad Nasib Rifai, mmoja wa wafuasi wa madhehebu ya Kiwahabi, anaamini kuwa; hakuna ushahidi hata mmoja wa kisheria unaothibitisha uhalali wa kujikaribisha kwa Mungu kupitia hadhi na heshima ya bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na mawalii wa Mwenye Ezi Mungu. Yeye anaendelea kwa kusema kwamba; hakuna hata Sahaba mmoja wa Mtume aliyefanya tawassul kama hiyo. [52]Abdulaziz bin Baz (aliyefariki mwaka wa 1420 Hijria), mufti wa madhehebu ya Kiwahabi kutoka Saudi Arabia, naye pia ameihisabu aina hii ya tawassul kama bid'a (uzushi) na shirki katika dini, na akatoa fatwa ya uharamu wa kutenda jambo hili. [53]

Ukosoaji wa Mtazamo wa Mawahabi na Wanazuoni wa Kiislamu

Mtazamo wa Wahaabi dhidi ya kutawasali kupitia hadhi na heshima ya bwana Mtume (s.a.w.w) umekosolewa na wanazuoni mbali mbali wa Kishia pamoja na Kisunni. Kwa mujibu wa maelezo ya Samhudi, kutawasali kupitia hadhi ya bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na kuomba kupitia baraka za kuwepo wake mbele ya Mungu, ni moja ya sunna (nyenendo) za manabii na wanazuoni wema waliotangulia (Salafu al-Saleh). Na hili si jambo geni, bali lilikuwa ikifanyika katika zama mbali mbali, iwe kabla ya uumbwaji, wakati wa uhai wake, na hata baada ya kifo chake (s.a.w.w). [54] Shihabuddin Alusi (aliyefariki mnamo mwaka 1270 Hijria), ambaye ni mfasiri wa madhehebu ya Kishafi'i, pia naye amehalalisha tendo la kutawasali kupitia hadhi na heshima ya bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na watu wema, ambao ni waja wenye nafasi maalum mbele ya Mungu. [55]

Ja'far Subhani, mwanazuoni wa Kishia, akitoa maelezo kuhusiana na amali ya kutawasali anasema: Tendo la kutawasali kupitia haki na hadhi ya manabii na waja wema, haina maana ya kwamba wao wana haki na chaguo huru sambamba na Mwenye Ezi Mungu, ambapo ingeweza kuhesabiwa kuwa ni shirk (ushirikina); bali haki zote ziko mkononi mwa Mungu peke yake, na kutoka na hadhi na heshima maalum walizonazo waja wake hao, Mwenye Ezi Mungu amewafadhili kwa fadhila na ukarimu wake, na kuwapa baadhi hadhi na nafasi fulani, kisha akawatunukia staha maalumu miongoni mwa waja wake. [56]

Daru al-Ifta ya Misri (Kitengo cha Utoaji Fatwa cha Misri), katika kujibu suala la tawassul kupitia hadhi na nafasi ya bwana Mtume (s.a.w.w), kwa kutegemea Aya ya 35 ya Surat Al-Maida na Aya ya 57 ya Surat Al-Isra, pamoja na hadithi kadhaa, imetoa fatwa isemayo kwamba; Hakuna tofauti kati ya tawassul kwa hadhi ya bwana Mtume (s.a.w.w) na kutawasali kupitia nafsi yake yeye mwenyewe binafsi. Pia kitengo kimesema kuwa; Ni halali kutawasali kupitia hadhi na nafasi ya bwana Mtume (s.a.w.w), pamoja na manabii wengine, na uhalali wake umethibitishwa kupitia Qur'an na Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w). [57]

Makubaliano ya Waislamu Juu ya Uhalali wa Kutawasali Kupitia Qur'an na Majina ya Mungu

Tawassul kupitia Majina na Sifa za Mwenye Ezi Mungu

Moja ya mifano ua Tawassul kupitia majina na sifa za Mungu hufanyika kwa kusema: «اللّهُمَّ إِنِّی أَسْأَلُک بِاسْمِک یا اللّهُ، یا رَحْمنُ، یا رَحِیمُ...خَلِّصْنا مِنَ النَّارِ یا رَبِّ ; Ewe Alla, hakika mimi nakusihi (nakuomba) kwa jina lako, Ewe Alla, Ewe Mwingi wa Rehema, Ewe Mwingi wa Huruma...tuepushe na moto wa Jahannam, Ewe Mola». [58] Inasemekana kuwa hakuna tofauti kati ya Waislamu kuhusiana na uhalali wa aina hii ya tawassul. [59] Aya ya 80 ya Surat Al-A'raf inasema kwamba; Mwenye Ezi Mungu amewaamuru waja wake kumwomba kwa kutumia majina yake mame (Asmaul-Husna). [60] Pia kuna Hadithi nyingi kutoka kwa bwana Mtume pamoja na Maimamu Maasumu (a.s), [61] zinathibitisha uhalali wa aina hii tawassul. [62] Dua ya Joshan Kabir ina sehemu (vipengele) mia moja, na ndani yake kuna zaidi ya majina elfu moja ya Mwenye Ezi Mungu na sifa zake yanayo tumika. Dua hii ni miongoni mwa dua na kumwomba Mwenye Ezi Mungu kwa kutumia majina na sifa zake mbalimbali. [64] Pia mependekezwa kusoma dua hii wakati wa usiku wa Laylatul Qadr. [64]

Kutawasali kwa Qur'ani

Miongoni mwa aina za kutawasali, ni kutawasali kwa kupitia Qur'ani, nacho ni miongoni mwa vitendo vitendwavyo ndani ya jamii za Kiislamu. Namna ya kutawasli kwa kupitia Qur’ani ni kumuomba Mwenye Ezi Mungu kwa kusema: «اللّٰهُمَّ إِنِّی أَسْأَلُکَ بِکِتابِکَ الْمُنْزَلِ وَمَا فِیهِ وَفِیهِ اسْمُکَ الْأَکْبَرُ وَأَسْماؤُکَ الْحُسْنیٰ...أَنْ تَجْعَلَنِی مِنْ عُتَقائِکَ مِنَ النّارِ ; Ewe Alla, hakika mimi nakusihi (nakuomba) kwa haki ya kitabu chako kilichoteremshwa (Qur'ani) na kile kilicho ndani yake, na (ambacho) ndani yake kuna jina lako kuu pamoja na majina yako mazuri (mema)...ili uniweke miongoni mwa wale waliookolewa na moto wa Jahannam». [65] Katika Hadithi mbalimbali zilizo katika vyanzo vya Kiislamu vya Kisunni na Kishia, [66] imeoneshwa wazi ya kwamba; ni halali mja kutawasali kupitia Qur'an kwa lengo la kumkaribia Mungu au kuomba kitu fulani kutoka kwake. [67] Aidha, kuna Hadithi kadhaa zitokazo kwa Maimamu watakatifu (a.s) zinazo shauri kutawasali kupitia Qur'ani, hususan wakati wa ibada za usiku wa Laylatul Qadr, ambapo ndani yake kuna ibada maalumu ya kuweka «Qur'an juu ya kichwa». [68]

Amali ya tawassul (kutawasali) kupitia matendo mema, ni moja ya aina nyingine za tawassul ambazo zimejadiliwa katika tafiti mbali mbali. [69] Katika moja ya Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Imam Ali (a.s), imeelezwa ya kwamba; matendo mema ya mja, ni miongoni mwa njia bora za kumkaribia Mungu, na miongoni matendo hayo yaliyo tajwa ndani yake ni; kumwamini Mungu na Mtume (s.a.w), jihad katika njia ya Mungu, kusimamisha sala, kutoa zaka, kufunga, kuhiji, kuunga udugu na kutoa sadaka. [70] Komba dua kutoka kwa mtu fulani na kumtaka yeye akuombee dua kutoka na baraka za uwepo wake, kuna matumaini zaidi ya kukubaliwa kwa dua hiyo, hii nayo ni aina nyingine ya tawassul ambayo hujadiliwa na wanazuoni wa Kiislamu juu ya uhalali wake, ambapo huthibitisha uhalali wake kwa kuzingatia Aya za Qur'ani na Hadithi mbali mbali. [71]

Bibliografia (Vitabu vya Kujitegemea kuhusu Masuala ya Tawassul)

Kuna kazi nyingi zilizo andikwa na wanazuoni wa Kiislamu juu ya suala la tawassul. Baadhi ya kazi hizo ni kama zifuatazo:

  • Al-Tawassul Mafhuumuhu wa Aqsaamuhu wa Hukmuhu fii Shari’ati Al-Gharraa. Mwandishi wa kitabu hichi ni Ja'afar Subhani. Mwandishi wa kitabu hichi ametaja dalili kutoka katika Qur'ani na Hadithi mbali mbali, zinazothibitisha uhalali wa aina mbalimbali za tawassul. Pia amejadili na kukosoa mitazamo kadhaa ya wapinzani wa tawassul kitabuni humo. [72]
  • Al-Taammulu fii Haqiiqati Al-Tawassuli. Mwandishi wa kitabu hichi ni Isa bin Abdullah Hamiri. Kitabu hichi kina sehemu mbili kuu, ambapo mwandishi wake anachambua na kukosoa dalili za wapinzani wa tawassul na kuelezea uhalali wake kwa kuzingatia miongozo ya Qur'ani na Hadithi kutoka vyanzo vya Kisunni, pamoja na mitazamo ya wanazuoni mbali mbali. [73] Kitabu hichi kimetafsiriwa na Sayyid Murtadha Husseni Fadhil kwa lugha ya Kifarsi na kuchapishwa na taasisis ya Nashr Mash'ar kwa jina la «Derangiy Dar Haqiiqaate Tawassul». [74]
  • Mahaqu Al-Taqawwuli Fii Mas-alati Al-Tawassili. Mwandishi wa kitabu hichi ni Muhammad Zahid al-Kawthar (aliyefariki manmo mwaka 1371 Hijiria). Al-Kawthari, mwanazuoni wa madhehebu ya Kihanafi na mkosoaji wa Ibnu Taymiyyah na mawazo ya Kisalafi. Mwandishi huyu amejadili na kujibu hoja za wapinzani wake katika kitabu chake hichi chenye kurasa 22. Miongoni mwa yaliojadiliwa kitabuni humo ni; uhalali wa tawassul na istighatha (kuomba wokovu) kwa kutegemea Qur'an, Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w), na nyenendo za Masahaba. [75]

Maelezo

  1. Ibnu Taymiyyah katika kitabu chake «Qawa'id Jalila fi al-Tawassul wa al-Wasila» aligawanya tawassul katika aina tatu:
    1. Tawassul kwa maana ya kujikaribisha kwa Mwenye Ezi Mungu kwa kupitia utiifu wake Yeye na Mtume wake (s.a.w.w): Aina hii ya tawassul aliiitambua kama ni msingi wa dini, na anaamini kwamba hakuna Mwislamu yeyote aliyewahi kuikataa au kupingana nayo.
    2. Tawassul kupitia dua ya bwana Mtume (s.a.w.w) wakati wa uhai wake au uombezi wake wa Siku ya Kiyama: Anaamini kwamba aina hii ya tawassul ilifanywa na miongoni mwa Masahaba.
    3. Tawassul kwa dhati ya bwana Mtume (s.a.w.w) na kumwomba kitu fulani kutoka kwake: Ibnu Taymiyyah aliiona aina hii ya tawassul kuwa si tawassul halali, na anaamini kwamba hakuna Sahaba hata mmoja aliyewahi kufanya hivyo. (Ibn Taymiyyah, «Qawa'id Jalila fi al-Tawassul wa al-Wasila», 1422 Hijria, uk. 87-88.)

Rejea

  1. Hukumu Tawasul Bil-Anbiyai Wal-Awliyaa Waswalihiin Watalab al-madad Winhum, Tovuti Daru al-Iftai al-Misri.
  2. Subki, Shifau Siqam uk. 293

Vyanzo