Nenda kwa yaliyomo

Kufa shahidi

Kutoka wikishia

Kufa shahidi (Kiarabu: الشهادة) kunaashiria mtu kufa katika njia ya Mwenyezi Mungu ambapo katika hadithi mbalimbali kumetajwa kuwa ni kifo bora na chenye thamani zaidi. Katika Aya za Qur’an na Hadithi mbalimbali kumetajwa athari mbalimbali za kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu kama vile kuwa hai, kuwa na haki ya kutoa uombezi (shifaa) na kusamehewa madhambi.

Kwa mujibu wa mafaqihi, shahidi hana ghusli wala sanda, na kugusa mwili wake hakufanyi kuwa wajibu kuoga ghusli ya kugusa maiti. Hata hivyo hukumu hizi ni makhsusi kwa mashahidi waliokufa kwenye medani ya vita (uwanja wa vita) na hazijumuishi watu wengine waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu au waliouawa shahidi nje ya uwanja wa vita.

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Maimamu wote wa Shia wanakufa kifo cha shahada (kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu). Hata hivyo Sheikh Mufid, mmoja wa wanachuoni mashuhuri wa Shia, ametilia shaka kuuawa shahidi baadhi yao.

Katika fasihi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wale wote wanaouawa katika njia ya kuhifadhi mapinduzi ya mwaka 1979 na kuihami nchi ya Iran wanaitwa mashahidi. Katika nchi hii, Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Wenye Kujitolea ilianzishwa ili kushughulikia masuala ya familia za mashahidi na wenye kujitolea. Pia, Machi 12 inaitwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Shahidi.

Utambuzi wa maana

Kuuawa shahidi (shahada) maana yake ni kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu, na mwenye kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu anaitwa shahidi. [1] Katika fiqhi, shahidi ni maalumu na mahususi kwa Muislamu aliyeuawa katika uwanja wa vita na makafiri au kwa sababu ya vita nao. [2]

Imeelezwa katika tafsiri ya Nemooneh kwamba shahada ina maana aam (jumla) na khaas (mahsusi). Maana yake makhsusi ni ndio ile maana ya kifiqhi, na maana yake kwa ujumla ni kwamba mtu anauawa au kufa akiwa katika njia ya kutekeleza wajibu wa Kimungu. Kwa hiyo, katika hadithi, anayekufa akiwa anatafuta elimu, mtu anayekufa kitandani mwake akiwa na elimu na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu, Mtume na Ahlul-Bayt zake (a.s), mtu anayeuawa kwa ajili ya kulinda mali yake dhidi ya wavamizi n.k... wanahesabika kuwa ni mashahidi. [3]

Kuitwa Jina la Shahidi

Shahada (kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu) katika lugha ina maana kama uwepo na kushuhudia. [4] Kwa kuzingatia jambo hili kumetajwa mitazamo kadhaa kuhusu kuitwa jina hili la shahidi au kupewa mtu jina hili la shahidi: Miongoni mwayo ni:

  • Malaika wanamuona.
  • Mwenyezi Mungu na malaika wanatoa ushahidi kwamba, yeye ni mtu wa peponi.
  • Yeye hajafa na yuko mbele ya Mwenyezi Mungu.
  • Yeye anaona vitu ambavyo watu wengine hawavioni. [5]
  • Siku ya Kiyama atakuwa ni mwenye kushuhudia amali za wengine. [6]

Daraja

Kuna hadithi nyingi zinazoeleza daraja, fadhila na nafasi muhimu ya kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwayo ni kwamba, kuuawa shahidi ni daraja ya juu [7] na kifo bora kabisa [8] na baadhi ya vifo vingine vimefananishwa nayo katika ujira na malipo. [9] Pia, katika dua zilizopokewa kutoka kwa Maasumina kumi na wanne, kumeombwa kuuawa kishahidi, [10] kuuawa shahidi chini ya bendera ya Mtume (s.a.w.w) [11] na kuuawa na watu wabaya zaidi [12].

Katika Qur'an, neno shahadat limetajwa kwa ibara ya: ((قَتْل فی سبیل‌ الله ; kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu)) na maana ya shahidi katika Qur'an ni mtu ambaye ni shahidi (mwenye kushuhudia) wa amali za mwanadamu. [13] Katika vitabu vya sheria, kifo cha shahada na kufa shahidi vinajadiliwa katika mlango wa hukumu za tohara. [14]

Athari za Kuuawa Shahidi

Kadhalika Angalia: Shahidi na Haki za Watu

Katika Aya na hadithi kumebainishwa athari za kuuawa shahidi. Miongoni mwazo ni:

  • Kuwa hai: Kwa mujibu wa Aya za Qur’an watu ambao wanauawa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hawajafa bali ni wahai [15] na wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi. [16]
  • Kuwa na haki ya uombezi: Shahidi akiwa kando ya Mitume na wanazuoni ni miongoni mwa watu watakaokuwa wakifanya uomboze Siku ya Kiyama. [17]
  • Kusamehewa madhambi na rehma za Mwenyezi Mungu. [18] Katika riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Imam Baqir (a.s), linapotoka tone la kwanza la damu ya shahidi, husamehewa madhambi yake yote isipokuwa Haqq al-Nas (haki za watu) [19], ikiwa hakufanya uzembe katika suala la haki za watu na na alikuwa na nia ya kulipa; Mungu hufidia haki hiyo na humridhisha mwenye haki. [20]
  • Kuingia peponi: [21] Shahidi ni miongoni mwa watu wa kwanza watakaoingia peponi. [22]

Hukumu za Shahidi Vitani

Wanazuoni wa fikihi wametaja na kubainisha hukumu za shahidi aliyeuawa katika medani ya vita:

  • Kuosha maiti: Kwa mujibu mtazamo wa mafakihi wa Kishia, shahidi ambaye ameuawa katika medani ya vita hafanyiwi ghusl; [23] lakini mtu ambaye amejeruhiwa katika medani ya vita na kisha akaja kufa shahidi baadaye nje ya medani ya vita, anapaswa kuoshwa.
  • Sanda: Kwa mujibu wa mtazamo wa wanazuoni wa Kishia ni kuwa, shahidi ambaye ameuawa katika medani ya vita havishwi sanda (hakafiniwi) [25] bali anazikwa na nguo alizokuwa nazo; [26] isipokuwa kama atakuwa hana nguo, katika hali hii anavishwa sanda. [27]
  • Kugusa maiti ya shahidi: Kugusa maiti ya shahidi hakupelekei mtu kuoga josho la kugusa maiti. [28]
  • Hunuti (kupaka kafuri): Hunuti ni kumpaka kafuri maiti katika maeneo saba yanayogusa chini wakati wa kusujudu. Kwa shahidi jambo hili sio wajibu; kwa sababu hunut hufanywa baada ya maiti kuvishwa sanda na shahidi hana sanda. [29]

Hukumu zilizotajwa zinajumuisha watu ambao wameshiriki katika vita ambavyo vimefanyika kwa idhini ya Maasumu au naibu wake mahususi. [30] Kadhalika kwa mujibu wa fatwa ya akthari ya mafakihi, hukumu hizi zinajumuisha watu ambao katika zama za ghaiba walishiriki katika vita kwa idhini ya naibu wa Imamu (fakihi) au bila ya idhini yake vita ambavyo vilikuwa kwa ajili ya kutetea na kulinda nchi mkabala wa hujuma na mashambulio ya maadui wa Uislamu. [31] Mkabala na msimamo huo, shahidi Thani anasema, licha ya kuwa watu hawa (na vilevile watu ambao wameuawa katika njia ya kutetea mali na familia yao) ni washirika wa fadhila za shahidi aliyeuawa katika vita. [32]

Kuuawa Shahidi Maimamu wa Shia

Kwa mujibu wa itikadi na imani ya Maulamaa wa Kishia, Maimamu wote wa Kishia wameaga dunia kwa kuuawa shahidi. [33] Hoja yao ni uwepo wa baadhi ya hadithi kuhusiana na hilo. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) inayosema: (وَ اللهِ مَا مِنَّا إِلَّا مَقْتُولٌ شَهِید ; Wallahi! hakuna miongoni mwetu isipokuwa ameuawa shahidi). Kwa mujibu wa hadithi hii, Maimamu wote wa Kishia wanaondoka duniani hali ya kuwa wameuawa shahidi, [34] na mkabala wa mtazamo huo, Sheikh Mufid katika kitabu cha: Tas’hih I’tiqadaat al-Imamiyah ameafikiana na mtazamo wa kwamba, Imamu Ali, Hassan, Hussein, Mussa al-Kadhim na Ridha (a.s) kwamba, waliuawa shahidi lakini ametilia shaka kuhusiana na kuuawa shahidi Maimamu wengine waliobakia. [35]

Shahidi Katika Fasihi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Mazishi ya mashahidi kadhaa walio uwawa katika vita vya Iran na Iraq huko Isfahan (Machi 12, 2015)

Katika fasihi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wale wote wanaouawa katika njia ya kuhifadhi mapinduzi ya mwaka 1979 na kuihami nchi ya Iran wanaitwa mashahidi kama ambavyo pia wanaouawa katika njia ya kulinda nguzo za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mamlaka ya kujitawala Iran na kukabiliana na vitisho vya maadui pia wanahesabiwa kuwa ni mashahidi. [37] Kwa mujibu wa kanuni za Tasisi ya Boniyad Shahidi tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 hadi mwanzoni mwa 2021 takribani watu 220,000 wameuawa shahidi. [38] Nchini Iran, Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Wenye Kujitolea ilianzishwa ili kushughulikia masuala ya familia za mashahidi na wenye kujitolea. [39] Pia, Machi 12 inaitwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Shahidi. [40]

Istilahi

Mazishi ya mashahidi kadhaa ambao walikuwa walinzi wa Haram kutoka Jeshi la Fatimiyyun huko Qom (Mei 1, 2016) [41]

Baadhi ya istilahi ambazo zinatumika katika fasihi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na mashahidi ni:

  • Shahidi wa Mihrabu: Inaashiria Maimamu wa Sala ya Ijumaa ambao waliuawa wakati wa Sala ya Ijumaa na wapinzani wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. [42]
  • Mashahidi wa Kujihami Kutakatifu: Ni Wairani waliouawa katika vita vya Iran na Iraq [43] ambao wanafahamika pia kwa jina la mashahidi wa vita vya kutwishwa/kulazimishwa. [44] Mahali walipozikwa mashahidi hawa panajulikana kwa jina la Golzar Shohada. [45]
  • Mashahidi wasiofahamika utambulisho wao: Hawa ni Wairani waliouawa shahidi katika vita vya Iran na Iraq na utambulisho wao haufahamiki. [46] Nchini Iran makaburi ya mashahidi hawa kikawaida hujengewa [47] na wakati wa minasaba ya kidini hufanyika hafla kando ya makaburi yao. [48]
  • Shahidi mlinzi wa Haram: Hiki ni kikosi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilichotumwa kwenda kupambana na kundi la kigaidi la Daesh kwa ajili ya kuiunga mkono na kuisaidia serikali ya Syria na kuuawa katika nchi hiyo. Wapiganaji wa kikosi hicho ni kutoka mataifa ya Iran, Iraq, Lebanon na Afghanistan. [49]
  • Mashahidi wa mapinduzi: Ni watu ambao waliuawa katika njia ya mapambano na utawala wa Kipahlavi kuanzia 1964-1979. Takwimu za mashahidi hawa zinatajwa kuwa ni 2,800-10,000. [50]
  • Mashahidi wa usalama: Hawa ni watu ambao wameuawa katika njia ya kuleta na kuchunga usalama wa jamii [51], kupambana na wauzaji wa madawa ya kulevya [52] na waendesha fujo na machafuko ambao ni kama Arman Aliverdi na Ruhollah Ajamiyan. [53]
  • Mashahidi wa serkta ya afya: Ni watu ambao wameuawa katika njia ya tiba na kutoa huduma katika sekta ya afya ya wananchi wa Iran. Anuani hii ilienea katika kipindi cha kuenea maradhi ya Corona (Covid-19) mwaka 2019. [54]

Kadhalika nchini Iran waliopoteza maisha katika baadhi ya matukio wametambuliwa kuwa ni mashahidi. Kama mahujaji walioaga dunia katika maafa ya Mina nchini Saudi Arabia katika msimu wa Hija mwaka 2015, wazimamoto walioaga dunia wakati wa kuzima moto ulioteketeza jengo mashuhuri la kibiashara la Plasco mjini Tehran mwaka 2017, [55] na walioaga dunia katika tukio la ndege ya Boeing 737 ya Ukraine mwaka 2020. [56]

Bibliografia

Kuumeandikwa vitabu mbalimbali kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kuhusiana na shahidi na kuuawa shahidi. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Shuhadayi 'Asr payambar (Mashahidi wa zama za Mtume (as), mwandishi: Abu l-Fadhl Banayi Kashi. Kitabu hiki cha lugha ya Kifarsi kinaelezea mashahidi wa kabla ya hijra, mashahhidi wa vita vya Badr, Uhud, Khaybar, Hunayn na kadhalika.
  • Shuhada al-Fadhilah, mwandishi Alllama amini.
  • Shuhadayi Sadr-i Islam wa-shuhadayi waqi'a-yi Karbala, mwandishi Ali Akbar Qurashi. [57]

Rejea

Vyanzo

  • Anṣārī, Murtaḍā. Kitāb al-ṭahāra. Qom: Kungira-yi Jahānī-yi Shaykh Anṣārī, 1415 AH.
  • Gharawī Tabrīzī, Alī . Al-Tanqīḥ fī sharh-i ʿurwat al-wuthqā; taqrīrāt-i dars-i Aytullāh al-Khoeī. Qom: 1418 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Nihāyat al-aḥkām fī maʿrifat al-aḥkām. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1419 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Taḥrīr al-aḥkām al-sharʿiyya ʿalā madhhab al-imāmiyya. Edited by Ibrāhīm Bahādurī. Qom: Muʾassisat Imām al-Ṣādiq, 1420 AH.
  • Ḥimyarī, ʿAbd Allāh b. Jaʿfar al-. Qurb al-isnād. Tehran: Niynawā, [n.d].
  • Ibn Ḥayyūn al-Tamīmīyy, al-Nuʿmān b. Muḥammad. Daʿāʾim al-Islām wa dhikr al-ḥalāl wa l-ḥarām fī al-qaḍāyā wa al-aḥkām. 2nd edition. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1385 AH.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Edited by Ḥāshim Rasūlī. Qom: Nashr-i ʿAllāma, 1379 Sh.
  • Kāshif al-ghiṭāʾ, ʿAlī b. Muḥammad Riḍā. Al-Nūr al-sāṭiʿ fī al-fiqh al-nāfiʿ. Najaf: Maṭbaʿt al-Ādāb, 1381 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār al-jāmiʿa li-durar akhbār al-aʾimmat al-aṭhār. Third edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1374 Sh.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Taṣḥīḥ al-'iʿtiqād. Edited by Ḥusayn Dargāhī. Qom: al-Muʾtamar al-ʿĀlamīyya li-alfīya al-Shaykh al-Mufīd, 1414 AH.
  • Qurashī Bunābī, ʿAlī Akbar. Qāmūs-i Qurʾān. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1412 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Khiṣāl. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmiyya, 1362 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn b. ʿAlī. Masālik al-ifhām ilā tanqīh sharāyiʿ al-Islām. 1st edition. Qom: Muʾassisat al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1413 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Iʿlām al-warā bi-aʿlām al-hudā. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth, 1417 AH.
  • Ṭurayḥī, Fakhr al-Dīn b. Muḥammad al-. Majmaʿ al-baḥrayn. Edited by Sayyid Aḥmad Ḥusaynī. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya, 1416 AH.