Nenda kwa yaliyomo

Sunna

Kutoka wikishia

Sunna (Kiarabu: السنة) ni maneno yanayoashiria kauli, kitendo (mwenendo) cha Mtume (s.a.w.w) na taqrir (kusemwa au kufanywa jambo mbele yake na kutokemea au kunyamazia kimya) na kwa mujibu wa itikadi ya Mashia, mbali na Mtume wanasema pia ni kwa Maimamu ni hivyo hivyo. Sunna ni katika Addilat al-Ar’ba’ kwa ajili ya kuthibitisha hukumu za Kisheria. Baada ya Qur'an, Sunna inatambuliwa kuwa chanzo cha pili cha Ijtihad.

Maulamaa wa Kiislamu wanazipa itibari kubwa mno Sunna za Mtume (na Maimamu kwa mujibu wa Mashia) zina nafasi muhimu katika kujua mafundisho ya dini na imekuwa na nafasi muhimu katika ufahamu wa Waislamu kuhusu dini na kupatikana elimu za Kiislamu, kama vile fiq'h, usul, teolojia na tafsiri. Waislamu wamekubaliana kwa ijmaa (kauli moja) kwamba, Sunna za Mtume (s.a.w.w) ni hoja. Hoja zao ni kwamba, Mtume (s.a.w.w) ni Maasumu na hakosei. Matokeo yake ni kwamba, kila kinachotoka kwake kina itibari na ni lazima kukifuata. Kadhalika kwa hoja hii kwamba, baadhi ya Aya za Qur’an zimeamrisha kufuatwa Mtume (s.a.w.w).

Kwa mtazamo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kwamba, Maimamu kama alivyo Mtume nao ni Maasumu (hawakosei) na kwa hivyo Sunna (sira na mienendo) zao ni hoja. Mbali na hoja za kiakili, Mashia wanatumia Aya za Qur’an na hadithi kuthibitisha hilo. Miongoni mwa hoja zao ni Aya ya Utakaso (Ayat Tat’hir) ambayo inaonyesha kuwa, Ahlul-Bayt (a.s) wametoharishwa na kutakaswa na hivyo ni hawakosei wala kutenda dhambi; kadhalika wanatumia hadith Thaqalaeyn (hadithi ya Vizito Viwili) ambayo inatoa agizo na amri ya kuwafuata Ahlul-Bayt.

Utambuzi wa maana na nafasi

Sunna kwa Maulamaa wa Kiislamu inahesabiwa kuwa moja ya vyanzo vya kunyambua na kutoa hukumu za kisheria [1] na makusudio yake kwa madhehebu ya Ahlu-Sunna ni kauli, kitendo cha Mtume (mwenendo) na taqrir (kusemwa au kufanywa jambo mbele yake na kutokemea au kunyamazia kimya) [2] na kwa Waislamu wa Kishia ni kauli, kitendo cha Maasumu (mwenendo) na taqrir (kusema au fanywa jambo mbele yake na kutokemea au kunyamazia kimya). [3] Muhammad Ridha Mudhaffar anasema, chimbuko la istilahi ya “Sunna” ni hadithi ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambazo ndani yake zinawataka wafuasi wake kufuata Sunna zake. [4] Kwa mtazamo wa Usuliyyun ni kwamba, suala la mjadala wa hoja ya Sunna kwa anuani ya moja ya nyanzo vya hukumu za kisheria ni jambo ambalo hujadiliwa katika uwanja wa elimu ya Usulul-Fiq’h. [5]

Istilahi ya “Sunna” katika fasihi ya fiq’h pia ina matumizi ambayo yana tofauti kidogo na maana yake katika usul (kwa anuani ya moja ya vyanzo vya hukumu za kisheria). [6] Kwa mfano wakati mwingine Sunna huelezwa kuwa ni amali na matendo ambayo ni mustahabu mkabala wa amali na matendo ya wajibu. Kwa mfano Sala za Nafila ambazo ni mustahabu huitwa kuwa ni Sunna na Sala za wajibu huitwa kuwa ni faradhi. [7] Kadhalika wakati mwingine hutumika mkabala wa bidaa (uzushi). Bidaa maana yake ni kukitaja kitu fulani kuwa ni katika sheria katika hali ambayo kiuhalisia si katika sheria (au kuweka kiti katika Uislamu ambacho kimsingi hakikuweko hii yangu). [8]

Tofauti ya Sunna na hadithi

Sunna ni kauli, kitendo au taqrir ya Mtume au Maasumu kiujumla. Taqrir maana yake ni kunyamazia kimya Mtume au Maasumu neno lililosemwa au kitendo kilichofanywa mbele yake na kutoonyesha upinzani). Sunna husimuliwa na kuelezewa kupitia hadithi; hivyo wakati mwingine inajuzu kutumia istilahi mbili na Sunan na hadithi katika nafasi ya istilahi nyingine. [9] Kwa maana kwamba, wakati mwingine inajuzu kutumia Sunna sehemu ya hadithi na kinyume chake pia.

Umuhimu na itibari ya Sunna

Baada ya Qur’an, chanzo chenye itibari zaidi kwa ajili ya kunyambua na kutoa hukumu za kisheria kwa mafakihi wa Kiislamu ni Sunna. [10] Katika fikihi ya Kiislamu kuna hukumu nyingi za kisheria ambazo katika Qur’an zimekuja kwa sura jumla na ufafanuzi na undani wake unapatikana katika hadithi. [11] Maulamaa wa Kiislamu wanatambua kuwa, itibari ya Sunna katika Uislamu ni jambo la dharura [12] na kwamba, kukana kuwa kwake hoja ni sawa na kufanya majadala wa kupinga moja ya dharura miongoni mwa dharura za dini na matokeo yake ni kutoka katika Uislamu. [13] Kadhalika Sunna inahesabiwa kuwa ufunguo wa kufahamu Qur’an na inaaminika kuwa, ni jambo la dharura kurejea Sunna kwa ajili ya kufahamu Qur’an. [14]

Mpaka wa Sunna

Madhehebu za Kiislamu zina mitazamo tofauti kuhusiana na kuwa, Sunna inajumuisha mambo na vitu gani: Katika madhehebu ya Shia Imamiya, Maimamu Maasumu (a.s) wameteuliwa na Mtume kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kwamba, baada ya Mtume wao ndio wenye jukumu la kubainisha hukumu na sheria za Mwenyezi Mungu na wenyewe ni chanzo cha kweli cha utungaji wa sheria za Mwenyezi Mungu. [15] Kwa muktadha huo, madhehebu haya mbali na Sunna za Mtume (s.a.w.w) yanafanyia kazi pia Sunna za Maimamu na yanazitamnbua kuwa ni hoja. [16]

Katika madhehebu ya Sunni, Sunna inaishia tu katika kauli, kitendo na taqrir ya Mtume (saww). [17] Hata hivyo, baadhi ya Maulamaa wa madhehebu haya kama Shatibi, wanaamini kuwa, Sunna za masahaba pia ni hoja; [18] kwani kwa mtazamo wao matendo ya masahaba yalikuwa kwa mujibu wa Sunna ambazo zilithibiti kwao lakini hazikutufikia sisi au walifanya hivyo kwa mujibu wa ijtihadi yao. [19]

Madhehebu zingine za Kiislamu

Madhehebu ya fikihi ya Ibadhi an Zaydiyyah yamnetambuliwa kuwa yanakaribiana na Ahlu Sunna katika misingi ambayo yanategemea Sunna za Mtume kwa anuani ya moja ya vyanzo vya kunyambua hukumu za sheria. [20] Maibadhi mbali na Sunna za Mtume, wanayahesabu maneno ya masahaba na sira na mwenendo wao kuwa ni hoja pia. [21] Zaydiyyah pia mbali na Sunna za Ahlu-Bayt (a.s) wanafanyia kazi Sunna za masahaba kwa anuani ya moja ya vyanzo vya hukumu za kisheria. [22]

Aina

Sunna imegawanywa katika sehemu tatu za kitendo, kauli na taqrir (kusemwa au kufanywa jambo mbele yake na kutokemea au kunyamazia kimya): [23]

Sunna ya kivitendo

Ni kitendo na jambo ambalo limefanywa na Mtume au Maasumu kwa nia ya kuonyesha hukumu ya kisheria, kama vile kutia udhu, kusali na kuhiji. Hii huitwa sunna ya kitendo. Kwa maana kwamba, Mtume au Maasumu ameonyesha kivitendo namna ya kufanya jambo fulani. [24] Vitu kama ishara, andiko, kuacha Mtume au Maasumu kufanya jambo fulani nayo yahesabiwa kuwa ni aina ya sunna ya kivitendo. [25]

Kuhusiana na vipi kitendo cha Mtume au maasumu kinaashiria hoja kwa hukumu ya kisheria kuna hali mbili:

  • Kitendo ambacho kilifanywa na Mtume au Maasumu kinapaswa kuambatana na ishara na dalili ambapo kupitia ishara hizo ifahamike kwamba, Mtume au Imamu Maasumu yupo katika nafasi ya kubainisha hukumu miongoni mwa hukumu au ibada miongoni mwa ibada kama Sala, udhu, Hija na mfano wake. Aidha kupitia ishara na dalili (qarain) ifahamike kwamba, kitendo hiki ni cha wajibu au cha mustahabu au yasiyo kuwa hayo. [26]
  • Kitendo ambacho kilifanywa na Mtume au Maasumu hakikuambatana na ishara na dalili ili ifahamike kinatoa ishara na dalili gani. [27] Hapa kuna mitazamo kadhaa: [28] baadhi wanasema, kinaashiria dalili ya wajibu wa kitendo hicho, [29] kuna wanaoamini kwamba, kinaashiria kuwa mustahabu kitendo hicho [30] na kundi jingine linaamini kwamba, hakina dalili yoyote na kinachofahamika hapo ni kwamba, kukifanya kwa ajili yetu ni mubaha na jambo linalojuzu. [31]

Kadhalika Usuliyuun wamesema, kama kitendo kinachotoka kwa Mtume au Maasumu kitaambatana na ishara na kupitia kwazo ikafahamika kwamba, kitendo hiki ni maalumu kwa Mtume au Imamu Maasumu, kama vile wajibu wa tahajjud (Sala ya usiku) kwa Mtume, kitendo hiki hakiwezi kuwa hoja kwa Waislamu wengine; [32] lakini kama kitendo kinachotoka kwa Mtume au Imamu Maasumu haifahamiki kwamba, maalumu kwao tu au kinajumuisha Waislamu wote kuna hitilafu za kimitazamo kuhusiana na kuwa hoja kitendo kama hiki kwa Waislamu wengine. [33] Baadhi wanaamini wamba, kitendo kama hiki ni maalumu kwao wao tu na wengine wanasema, ni hoja pia kwa Waislamu wote na wote wanawaeza kukifanyia kazi. [34]

Sunna ya kauli

Maneno ya Mtume (s.a.w.w) na Maasumina wengine yanafahamika kwa jina la Suna ya kauli. [35] Akthari ya sunna ni katika sunna hii ya kauli au ya maneno yaliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) au Maimamu Maasumu. [36]

Sunna ya taqriri

Makala asili: Taqrir ya Maasumu

Taqrir ya Mtume au Maasumu maana yake ni kusemwa au kufanywa jambo mbele yake asilikemee au akalinyamazia kimya. [37] inaelezwa kuwa, taqrir ya Maasumu kwa masharti fulani huwa ni ishara na dalili ya kujuzu au kusihi neno au kitendo kilichofanywa mbele yake; [38] kwa hoja hii kwamba, Maasumu ana jukumu kumzua mkosaji kufanya jambo baya na kama si mwenye kufahamu basi anapaswa kumuongoza na kumuonyesha njia sahihi. [39]

Hoja zenye itibari na Sunna kuwa hoja

Maulamaa wa Kiislamu wakiwa na lengo la kuthibitisha kwamba, Sunna za Mtume ni hoja, wametegemea Qur’ani, ijmaa na hoja za kiakili. Miongoni mwa Aya za Qur’an zinazotumiwa katika uga na uwanja huu ni Aya ambazo zinawajibisha kumtii Mtume (s.a.w.w). [40] Kuhusiana na ijmaa imeelezwa kuwa, makundi yote ya Kiislamu yameafikiana kwa kauli moja juu ya kuwa hoja kauli, kitendo na taqrir ya Mtume na kuifuta [41] hoja za kiakili pia ni: Katika elimu ya teolojia imethibiti kwamba, Mtume (s.a.w.w) ni Maasumu, hakosei na hatendi dhambi na wala haghafiliki; kwa msingi huo kauli, kitendo na kunyamazia kwake neno lililosemwa na kitendo kilichofanywa mbele yake ni hoja na ni kitu cha kuaminika. [42]

Maulamaa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia mbali na kutoa hoja za kuthibitisha kuwa hoja Sunna za Mtume (s.a.w.w) hutumia hoja tatu za Qur’an, Sunna za Mtume na akili kwa ajili ya kuthibitisha kuwa hoja Sunna za Maimamu Maasumina: [43]

  • Qur’an: Kwa mujibu wa Aya ya Tat’hir (utakaso) na Aya ya Ulul-Amr, Maimamu (a.s) ni Maasumu na hawatendi dhambi na kwa msingi huo Sunna zao ni za kuaminika na ni lazima kuzifuata. [44]
  • Sunna za Mtume: Kwa mujibu wa Hadithi ya Vizito Viwili (Hadith Thaqaleyn) ambayo ni mutawatir (iliyopokewa kwa wingi) iliyopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), ili kuzuia upotovu na kupotea, Waislamu wametakiwa kuifuata Qur’an na Ahlu-Bayt (a.s). [45]
  • Akili: Kigezo cha akili cha kuwa hoja Sunna za Mtume ni Umaasumu wake. Kwa upande mwingine katika elimu ya teolojia imethibiti kwamba, Ahlul-Bayt (a.s) nao kama alivyo Bwana Mtume (s.a.w.w) na wao ni Maasumu. Hivyo basi Sunna zao pia ni hoja. [46]

Vyanzo

  • Farhangnāma-yi uṣūl-i fiqh. Qom: Pazhūhishgāh ʿUlūm wa Farhang-i Islāmī, 1390 Sh.
  • Abū Zuhra, Muḥammad. Uṣūl al-fiqh. Beirut: Dār al-Fikr al-ʿArabī, 1957.
  • Bahāʾī, Muḥammad b. Ḥusayn al-. Mashriq al-shamsayn wa iksīr al-saʿādatayn. Edited by Mahdi Raja'i. Mashhad: Intishārāt-i Āstān-i Quds Raḍawī, 1387 Sh.
  • Baḥr al-ʿUlūm, Muḥammad al-. Al-Ijtihād uṣūlih wa aḥkāmih. Beirut: Dār al-Zahrā, [n.d.].
  • Fāḍil Lankarānī, Muḥammad. Sayrī kāmil dar uṣūl-i fiqh. Qom: Nashr-i fayḍīyya, [n.d.].
  • Jannātī, Muḥammad Ibrāhīm. Manābi'-i ijtihād. Tehran: Kayhān, 1370 Sh.
  • Jurjānī, ʿAlī b. Muḥammad al. Kitāb al-ta'rīfāt. Tehran: Intishārāt-i Nāṣir Khusraw, 1370 Sh.
  • Muḥammadi, ʿAlī. Sharḥ-i uṣūl-i fiqh. Qom: Dār al-Fikr, 1387 Sh.
  • Mūsawī Bujnūrdī, Muḥammad. Maqālāt-i uṣūlī. Tehran: [n.p.], [n.d.].
  • Muzaffar, Muḥammad Riḍā al-. Uṣūl al-fiqh. Qom: Nashr-i Muʾallif, 1387 Sh.
  • Shahābī, Maḥmūd. Adwār-i fiqh. Tehran: Wizārat-i Farhang wa Irshād-i Islāmī, 1366 Sh.
  • Ṭabāṭabāʾī al-Ḥakīm, Muḥammad Taqī al-. Al-Uṣūl al-ʿāmma li-l-fiqh al-muqārin. Tehran: al-Majmaʿ al-ʿālamī li-Ahl al-Bayt, 1432 AH.
  • Wilāyī, ʿĪsa. Farhang-i tashrīhī-yi iṣṭilāḥāt-i uṣūl. Tehran: Nashr-i Nay, 1374 Sh.
  • Zuḥaylī, Wahba al-. Al-Wajīz fī uṣūl al-fiqh. Tehran: Nashr-i Iḥsān, [n.d.].