Nenda kwa yaliyomo

Hadithi ya Thaqalaini

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Hadithi ya vizito viwili)
Hadithi ya Thaqalaini

Hadithi ya Thaqalaini au Thiqlaini (Kiarabu: حَدیث الثقلين أو الثِقْلَیْن): ni Hadithi mashuhuri na mutawatiru (iliyopokewa kupitia matabaka tofauti ya wapokezi wa Hadithi) kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Hadithi hii ni Hadithi izungumziayo nafasi ya Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) katika uongofu na ulazima wa kushikamana na viwili hivyo. Kwa mujibu wa Hadith ya Thaqalaini, Qur'an na Ahlul-Bayt ni vitu viwili vyenye thamani kubwa mno. Daima Qur'an haitatengana na Ahlul-Bay na Ahlu al-Baiti hawatatengana na Qur'an hadi siku ya Kiama ambapo viwili hivyo vitakapo kutana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwenye bwawa la Kauthar (hodhi).

Hadithi ya Thaqlaini ni Hadithi inayo tegemewa na wanatheolojia wa Kishia ili kuthibitisha mamlaka na uimamu wa Maimamu wa Shia (a.s). Kwa kuzingatia Hadithi hii, wanazuoni wa Kishia wameeleza ya kwamba; kila kipengele kuhusiana na sifa za ukamilifu ilizosifika Qur'an Tukufu, pia sifa hizo zinachukuwa nafasi kwa Ahlul-Bayt (a.s), yaani sifa za Qur'an zinakwenda sambamba na sifa za Ahlul-Bayt (a.s). Baadhi ya dhana na welewa wa kitheolojia kuhusiana na Hadithi hii ni kwamba: Hadithi hii imebeba ndani yake ushahidi na ithibati ya Uimamu wa Maimamu wa Kishia na kuendelea kwa mamlaka ya uongozi huo hadi Siku ya Kiyama. Dhana nyingine kupia Hadithi hii, ni umaasumu wa Ahlul-Bayt, ulazima wa kuwafwata na kushikamana nao, mamlaka ya kielimu, uongozi na mamalaka juu ya Waislamu, na la mwisho ni kutokuwepo tofauti kati ya Ahlul-Bayt na Qur'an.

Kwa maoni ya baadhi ya wanazuoni wa Kisunni, Hadithi hii inasisitiza mapenzi ya Ahlul-Bayt, ihsani na heshima juu yao . Pia kwa mtazmo wa Hidithi hii inasisitiza kuwaheshimu, kuwatukuza na kutekeleza haki zao za faradhi na za sunna wanazopaswa kutekelezewa na Waislamu. Pia baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wamekubali kwamba malengo ya Hadithi juu ni kuthibitisha na kutoa bayana juu ya ulazima wa kushikamana na Ahlul-Bayt; Lakini wanaamini kwamba; Hadithi hii haitoi mwelekeo wa moja kwa moja juu ya mamalaka ya uongizi, uimamu au ukhalifa wao.

Kwa mujibu wa wanachuoni wa Shia na Sunni; Hadithi ya Thaqalaini haikusimuliwa mara moja tu kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) bali katika matukio kadhaa, Mtume Muhammad aliwasimulia Masahaba zake Hadithi hii. Kule Hadithi ya Thaqalaini kukaririwa na mara kadhaa na bwana Mtume (s.a.w.w) kulizingatia umuhimu na na hadhi yake kwenye jamii. Hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo kadhaa vya Hadithi vya Shia pamoja na Sunni. wote wawili, Mashia na Masunni wanakubaliana juu ya madhumuni na usahihi wa Hadithi hii.

Hadithi hii imepokewa na zaidi ya Masahaba ishirini wa Mtume (s.a.w.w) na imerikodiwa katika vyanzo mbalimbali. Sayyid Hashim Bahrani katika kitabu chake "Ghaya al-Maram", ameorodhesha hadithi 82 zenye madhumuni ya Hidithi ya Thaqalaini kutoka vyanzo mbalimbali vya Kishia, kama vile Kafi, Kamal al-Din, 'Uyunu Al-akhbar al-Ridha, Basairu al-Darajati. Pia ameorodhesha Hadithi 39 zenye madhumuni sawa na Hadithi ya Al-thaqalaini kutoka vyanzo vya Kisunni, kama vile; Sahihu Muslim, Sunanu Al-tirmidhi, Sunan Al-Nasai, Sunan Al-daarmi na Musnadu Ahmad bin Hambal.

Kuhusu mfano hai na halisi wa neno Al-itra pamoja na maana ya Ahlul-Bayt lililopo kwenye ibara ya Hadithi ya Thaqalaini, kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wa Kishia ni maimamu kumi na mbili wa Kishia. Katika baadhi ya Hadithi, maana au tafrisi hiyo inaonekana wazi kabisa na wala haina mjadala mbele ya wanazuoni wa Kishia. lakini kwa upande wa wanazuoni wa Kisunni, wao wamekhitalifiana juu ya mfano hai na halisi wa walio kusudiwa katika Hadithi ya Thaqalaini; Kundi moja miongoni mwao liwamewazingatia watu wa Kisaa -waliofunikwa Shuka na bwana Mtume (s.a.w.w)- kuwa ndiwo Ahlul-Bayt na 'Itrah za bwana Mtume (s.a.w.w), na wengine miongoni mwao wamewaorodhesha watu maalumu kuwa ndiwo Ahlul-Bayt wa Mtume (s.a.w.w), nao ni; Aali za Ali bin Abi Talib (kizazi cha Ali), Aali za 'Aqil, Aali za Jaafar, na Aali za Abbas, ambao sadaka ni haramu kwao.

Kuna vitabu kadha vilivyo chapishwa kuhusiana na Hadithi ya Thaqalaini, miongoni mwavyo ni; (موسوعةُ حدیثِ الثَّقلین), yaani ensaiklopidia ya Hadithi ya Thaqalaini chenye juzu nne.

Umuhimu Wake

Hadithi Thaqalaini ni Hadithi maarufu ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) [1] Pia ni Hadithi mutawatiru (iliyopokewa kupitia matabaka tofauti ya wapokezi). [2] Pia Hadithi hii ni Hadithi ambayo Waislamu wote wanakubaliana nayo. [3] Hadithi hii ni muhimu mno, moja ya dalili ya umuhimu wake, ni kule kukaririwa mara kadhaa na bwana Mtume (s.a.w.w). [4] Wanatheolojia wa Kishia wanatumia Hadithi ya Thaqalaini kama ni hoja na bayana katika kuthibitisha mamlaka ya uongozi wa familia ya Mtume (s.a.w.w) katika jamii. [5] Hadithi hii ndiyo Hadithi muhimu inayoonekana kujadiliwa na madhehebu mbalimbali ya Kiislamu. Hadithi ya Thaqalaini ndiyo duru katika mijadala ya kitheolojia, na mijadala kuhusu mrithi wa ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w). Hadithi hii imezingatiwa kuwa ndio Hadithi imara zaidi inayoweza kutoa jawabu muwafaka kuhusiana na dhana ya uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w). [6]

Katika kitabu 'Abaqatu al-Anwar, imeelezwa ya kwamba; Kutokana na Hadithi hii kunukuliwa kutoka katika vyonzo kadhaa, thamani yake na uzito wa ibara uliomo katika maandishi yake, imekuwa ni maalumu inayopewa uzito mbele ya wanazuoni na wenye kunukuu Hadithi. Kundi miongoni mwa wanazuoni hao wamitafiti Hadithi ya Thaqalaini na kuandika risala (makala) au vitabu makhususi juu ya Hadithi hii [7] Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti; Kutoka karne ya kwanza Hijiria, Hadithi hii ilianza kusambaa na kunukuliwa na wahakiki wa wanahadithi wa pande zote mbili za Kishia na Kisunni. Baada ya hapo, Hadithi ya Thaqalaini ikaonekana kusambaa kadhaa vya; kihistoria, vya 'ilmu al-rijali (fani ya uhakiki juu ya wapokezi wa Hadithi), vya kitheolojia, vya kimaadili na vya kifiqhi pamoja na usuli. [8]

Kwa mujibu wa mwandishi wa makala ya Hadithu Al-thaqalain iliopo katika "دانشنامه جهان اسلام" Encyclopedia of the Islamic World, kwa muda mrefu wanazuoni wa Kishia wamekuwa wakiinukuu Hadithi hii katika vyanzo vyanzo vyao vya Hadithi. Hata hivyo, katika vitabu vya zamani vya theolojia, Hadithi hii haikuonekana kunukuliwa kwa wingi, na ilikuwa ni nadra Hadithi hii kutajwa katika mijadala na mada zinazohusiana na uimamu au ukhalifa. Pamoja na hayo, kundi la wanazuoni wa Kishia wameonekana kuinukuu katika baadhi ya mada za kitheolojia; Kwa mfano, Sheikh Saduqu ameonekana kuitumia Hadithi Thaqalaini, katika kuthibitisha ya kwamba; Ni muhali ardhi kubaki tupu bila ya kuwa na Mteule wa Mungu. Sheikh Tusi kwa upande wake naye ameitumia Hadithi hiyo, katika kujadili ulazima wa kuwepo Imamu kutoka upande wa Ahlul-Bayt katika zama zote. Allamah Hilli naye ameitumia Hadithi Thaqalaini, katika kitabu chake Nahj al-Haq katika jitihada za kuthibitisha ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), na Faidhu Kashani pia ametumia hadithi hii alipokuwa akijadili hadhi na nafasi ya Qur'an. [9]

Imesemekana ya kwamba; Miri Haamid Hussein Hindi (aliyefariki mwaka 1306 Hijiria) ni mwenye nafasi ya kawanza katika kueneza na kuitangaza Hadithi ya Saqlaini, kwa kule yeye kutenga sura na milango makhususi iliyo jadili kwa urefu na mapana juu ya mlolongo wa upokezaji pamoja na kujadili dhana na madhumuni ya Hadithi hiyo. Baada ya kazi yake hiyo maridadi, Hadithi ya Thaqalaini ilipata hadhi mbele ya watafiti mbali mbali, kiasi ya kwamba katika zama za hivi sasa, Hadithi hii imekuwa ndiyo Hadithi muhimu zaidi inayotumika katika kuthibitisha umuhimu na ulazima wa kushikamana na kuwafwata Ahlul-Bayt (a.s). [10]

Hadithi ya Thaqalaini ni Hadithi inayotumika na kunukuliwa na wanatheolojia wa Kishia katika kujadili tafiti tofauti kama vile; Utafiti juu ya ulazima wa kushikamana welewa dhahiri wa dhana za Qur'an, tafiti juu uwiano baina ya Qur'an na hadithi za Ahlul-Bayt na tafiti zinazojadili Qur'an na kuitambua kuwa ni mizani ya kupimia Hadithi zinazo nasibishwa kwa Ahlul-Bayt (a.s). [11]

Kwa kuzingatia msisitizo uliosisitizwa na Hadithi ya Thaqalaini juu ya nafasi na mamlaka ya kielimu ya Ahlul-Bayt (a.s), Hadithi hii inazingatiwa kuwa ndiyo ufunguo wa kufungua njia mpya katika mijadala baina ya madhehebu ya Kiislamu. Hata majadiliano na mazungumzo ya Sayyid Abdul Hussein Sharafu Al-ddin na Sheikh Salim Bushra, yalikuwa yakizunguka katika duru ya Hadithi hiyo. [12]

Matini ya Hadithi

Hadithi ya Thaqalain imesimuliwa kupitia vyanzo mbalimbali vya Shia [13] na Sunni, [14] pia kupitia maneno tofauti kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). [15] Hadithi hii ipo katika orodha ya Hadithi za kitabu maarufu kijulikanacho kwa jila la Kafi, ambacho ni mojawapo ya vitabu vinne vikuu vya Kishia. Ibara ya Hadithi hii katika kitabu hicho ni kama ifuatavyo:


((...إِنِّی تَارِکٌ فِیکمْ أَمْرَینِ إِنْ أَخَذْتُمْ بِهِمَا لَنْ تَضِلُّوا: کِتَابَ اللَّهِ عَزَّ وَ جَلَّ وَ أَهْلَ بَیتِی عِتْرَتِی. أَیُّهَا النَّاسُ اسْمَعُوا وَ قَدْ بَلَّغْتُ إِنَّکُمْ سَتَرِدُونَ عَلَیَّ الْحَوْضَ فَأَسْأَلُکُمْ عَمَّا فَعَلْتُمْ فِی الثَّقَلَیْنِ وَ الثَّقَلَانِ کِتَابُ اللَّهِ جَلَّ ذِکْرُهُ وَ أَهْلُ بَیتِی فَلَا تَسْبِقُوهُمْ فَتَهْلِکُوا وَ لَاتُعَلِّمُوهُمْ فَإِنَّهُمْ أَعْلَمُ مِنْکُم))
Kwa hakika mimi ninakuachieni mambo mawili miongoni mwenu, ambayo mkishikamana nayo kamwe hamtapotea, nayo ni; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na 'Itra zangu (kizazi changu), ambao ni Ahlul-Bayt zangu (Aali zangu). Enyi watu, sikilizeni, bila shaka nimeshafikisha ujumbe! kwa hakika mtanijia -Siku ya Kiama- nikiwa kwenye Hodhi la Kauthar, nami nitakuulizeni namna mliviamili vitu viwili hivi vizito vyenye thamani; ambavyo ni kitabu cha Mungu Aliyetukuka Utajo wake, na familia yangu (Ahlu al-Baiti zangu). Msiwatangulie mkaangamia, wala msiwafundishe chochote, kwani wao ne wenye elimu zaidi kuliko nyinyi.[16]


Matini ya Hadithi hii kulingana na kitabu Basairu al-Darajati, mojawapo ya vyanzo vya Hadithi vya madhehebu ya Shia, kutoka kwa Imam Baqir (a.s), ni kama ifuatavyo:


((أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّی تَارِکٌ فِيكُمُ الثَّقَلَيْنِ أَمَا إِنْ تَمَسَّكْتُمْ بِهِمَا لَنْ تَضِلُّوا: كِتَابَ اللَّهِ وَ عِتْرَتِی أَهْلَ بَيْتِی فَإِنَّهُمَا لَنْ يَفْتَرِقَا حَتَّى يَرِدَا عَلَیَّ الْحَوْض))
Enyi watu, hakika mimi ninakuwachieni miongoni mwenu vitu viwili vizito (vya thamani), endapo mtashimana navyo hamtapotea kamwe, navyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'an) na 'Itrat zangu ambao ni Ahlu al-Baiti zangu. Kamwe viwili hivyo hawatafarikiana mpaka vinifikie nikiwa kando ya bwawa (Hodhi la Kauthar).[17]


Hadithi ya Thaqalaini imepokewa katika Sahih Muslim kutoka kwa Zaid bin Arqam kama ifuatavyo:


((... وَأَنَا تَارِکٌ فِيكُمْ ثَقَلَيْنِ: أَوَّلُهُمَا كِتَابُ اللهِ فِيهِ الْهُدَى وَالنُّورُ فَخُذُوا بِكِتَابِ اللهِ، وَاسْتَمْسِكُوا بِهِ فَحَثَّ عَلَى كِتَابِ اللهِ وَرَغَّبَ فِيهِ، ثُمَّ قَالَ: «وَأَهْلُ بَيْتِی أُذَكِّرُكُمُ اللهَ فِی أَهْلِ بَيْتِی، أُذَكِّرُكُمُ اللهَ فِی أَهْلِ بَيْتِی، أُذَكِّرُكُمُ اللهَ فِی أَهْلِ بَيْتِی)) [18]
...Nami Ninaacha vitu viwili vya thamani miongoni mwenu; cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye mwongozo na nuru, Basi shikamaneni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Baada ya Mtume (s.a.w.w) kusema hayo, akasisitiza na kuhimiza juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu kisha akasema: Na cha pili ni Ahlu al-Baiti zangu, ninakukumbusheni kwa jina la Mwenyezi Mungu juu ya haki za Ahlul-Bayt zangu. Mtume (s.a.w.w) aliikariri ibara yake hii isemayo; (ninakukumbusheni kwa jina la Mwenyezi Mungu juu ya haki za Ahlu al-Baiti zangu) mara tatu mfululizo. [19]


Katika nukuu za baadhi ya vyanzo vyengine, ima limetumika neno Khalifataini (خَلیفَتَین) (viongozi wawili) [20] au Amraini (اَمرَین) (mambo mawili) [21] badala ya neno Thaqalaini (ثقلین). Pia Katika baadhi ya vyanzo vya Hadithi, linatumika neno Sunnati (سنّتی‌) badala ya neno Itrati (عِترتی‌). Nassir Makarim Shirazi, mwanazuoni mwenye uwezo na mamlaka ya kutoa fat'wa, na mwandishi wa tafsiri ya Qur'an ijulikanayo kwa jina la Tafsiri Nemune, anaamini kwamba nukuu za Hadithi ya Thaqalaini, ambazo ndani yake limetumika neno Sunnati (سنّتی‌) badala ya neno Itrati (عِترتی‌) si riwaya zinazoweka kutegemewa. Yeye anaamini ya kwamba; hata kama Hadithi hizo zitachukuliwa na kuhisabiwa kuwa ni sahihi, pia bado hakuna ukinzani kati ya nukuu mbili hizo, kwa sababu wakati mmoja Mtume alisisitiza kushikamana na Kitabu na Sunnah, na wakati mwengine akasisitiza kushikamana na Kitabu pamoja na 'Itra zake. [23]

Ayatullahi Jawadi Amoli amenukuliwa akisema: Mfano halisi na pekee wa binadamu mkamilifu na maasumu (asiye fanya dhambi), ni 'Itra za Mtume (s.a.w.w), wao ni kigezo sawa na Qur'an, (Yaani wao na Qur'ani ni sawa na mapacha wawili). Kwa mujibu wa Hadithi mutawatiru (yenye mlolongo wa matabaka tofauti katika mapokezi yake) ya Saqlain, katu hawawezi kutengana na Qur'an kwa namna yoyote ile. Qur'an ni dhihiriko la kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa umbile la kimaandishi, na Maasumu (mwanadamu mkamilifu asiye tenda dhambi) ni udhihiriko la kitabu chake katika mfumo na umbile la kiumbe hai. ... Hadithi za Maasumina (a.s) pia zinaeleza uhusiano usioweza kuvunjika kati ya Qur'an na 'Itra, na ni sambamba na Hadithi ya Thaqalaini, na ni uthibitisho wa kutotengana baina yao na hukumu zao... Kimoja kati yo hakitawez kueleweka bila ya kuwepo cha pili. [24]

Hadhi na Usahihi wa Hadithi

Wanachuoni wa Kishia wanaichukulia Hadithi ya Thaqalaini kuwa ni mutawatiru (iliyopokewa kupitia milolongo na matabaka tofauti ya wapokezi wa Hadithi). [25] Kwa mujibu wa Sahibu Al-hadaiq, ambaye ni mwanafaqihi na mwanahadithi wa Kishia wa karne ya 12 Hijiria, ni kwamba; Hadithi hii ni mutawatiru kimaana kati ya Mashia na Sunni.[26] Hadithi mutawatiru kimaana, humaanisha kwamba; Hadithi hiyo imepokewa kupitia ibara au maneno tofauti, ila dhana na roho ibara hizo ni moja tu. Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wanazuoni kama vile Mullah Saleh Mazandarani, ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa Kishia wa karne ya kumi na moja Hijiria, ni kwamba; Mashia na Masunni wanakubaliana juu ya maudhui na madhumuni ya Hadithi hii, pia wanakubaliana kimtazamo juu ya usahihi wake. [27] Jafar Subhani, mwanatheolojia wa Kishia, amesema ya kwamba; Hakuna yeyote isipokuwa wajinga au wabishani tu, ndio wanaotilia shaka usahihi wa Hadith hii. [28]

Mbali na kunukuliwa Hadith hii ndani ya Sahih Muslim [29], ambacho ni kitabu muhimu zaidi cha Hadithi cha Masunni baada ya Sahih Bukhari, pia mwanahadithi wa Kisunni Hakim Nishaburi, katika chake al-Mustadrak, ameisimulia Hadithi ya Thaqalaini kutoka kwa Zaid bin Arqam na kuthibitisha usahihi wake kwa kuzingatia masharti ya Bukhari na Muslim Neishaburi. [30] Ibn Hajar Haitami, mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i pia amekubaliana na usahihi wa Hadithi hii. [31] Abdul Raouf Manaawi katika kitabu chake Faidhu al-Qadir, amenukuu kutoka kwa Haitami ya kwamba; wapokezi wote wa Hadithi ni waaminifu. [32] Ali bin Abdullah Samhudi, miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i katika Jawahiru al-'iqdaini, amesema kwamba; Ahmad bin Hambal katika kitabu chake kiitwacho Musnad, ameinukuu Hadhithi ya Thaqalaini kupitia mlolongo sahihi usio nadosari wa wapokezi wake, na Sulaiman bin Ahmad Tabarani ameinukuu Hiadithi hiyo katika kitabu chake Muu’jamu al-Kabiir, kupitia mlolongo wa wapokezi waaminifu wameisimulia Hadithi hiyo.[33]

Ibnu Jauzi, ambaye ni mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Hanbali wa karne ya 6 Hijiria, ameisimulia Hadithi ya Thaqalaini katika kitabu chake Al-elalu al-Mutanaahiyah, kupiti chanzo maalum na nadra, kisha akaihisabu kuwa ni Hadithi dhaifu kutokana na udhaifu wa baadhi ya wapokezi wake alionukuu kutoka kwao. [34] Wanachuoni kama vile Samhoudi na Ibn Hajar Hitami, wanamchukulia Ibn Jauzi kuwa hakufanya insafu katika kuihukumu Hadithi na kuihisabu kuwa usahihi, kwa sababu Hadithi hii imepokewa ndani ya Sahihi Muslim pamoja na vyanzo vyengine tofauti kupitia mlolongo salama na sahihi katika mapokezi hayo. [35]

Wasimulizi na Vyanzo

Kwa mujibu wa maelezo ya Allamah Sharafuddin [36] na Jafar Subhani [37] amabo ni kutoka jopo la wanazuoni wa Kishia, na Samhoudi [38] na Ibn Hajar Hitami [39] kutoka kwa wanazuoni wa Kisunni, Hadith ya Thaqalaini ilipokewa na zaidi ya masahaba ishirini kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w). Pia kuna baadhi waliosema kuwa imepokea na zaidi ya masahaba hamsini. [40] Miri Hamid Hussein katika kitabu chake 'Abaqatu al-Anwar ameorodhesha zaidi ya masahaba thelathini wa Mtume (s.a.w.w) na zaidi ya wanazuoni mia mbili wakubwa wa Kisunni waliosimulia Hadithi hii katika vitabu vyao. [41] Yeye ameorodhesha majina ya wasimulizi wa Kisunni kuanzia karne ya 2 hadi ya 13. [42] Kulingana maoni ya Qawamu Al-ddin Muhammad Washnawi, ni kwamba; Hadithi ya Thaqalaini imepokewa kupitia njia zaidi ya sitini. [43]

Kupitia vyanzo vya Kishia, hadithi hii imenukuliwa kutoka kwa masahaba kadhaa wa bwana Mtume (s.a.w.w), kama vile; Imamu Ali (a.s), [44] Imamu Hassan (a.s), [45] Jabir bin Abdullah Al-ansari, [46] Hudhaifa bin Yaman, [47] Hudhaifa bin Usaid, [ 48] Zaid bin Arqam, [49] Zaid bin Thabit, [50] Omar bin Khattab [51] na Abu Huraira. [52] Pia Maimamu kadha wainukuu Hadithi hiyo kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), kama vile; Imamu Baqir (a.s), [53] Imamu Swadiq (a.s) [54] na Imam Ridha (a.s). [55]

Vyanzo vya Kisunni navyo pia vimenukuu Hadithi ya Thaqalaini kutoka kwa masahaba kadhaa kama vile; Imamu Ali (a.s), [56] Fatima Zahraa (a.s), [57] Imamu Hassan (a.s), [58] Zayd bin Arqam, [59] Abu Dhar Ghafari, [ 60] Salmani Al-farsi, [61] Abu Said Al-khudri, [62] Ummu Salamah, [63] Jaber bin Abdullah Al-ansari, [64] Zaid bin Thabit, [65] Hudhaifa bin Usaid, [66] Abu Hurairah, [67] Jubair bin Mut-'im, [68] Abu Raafi'i, [69] Dhumairah al-aslami, [70] Ummu Hani binti ya Abu Talib [71] na Amru bin 'Aas. [72] Kwa mujibu wa maelezo ya Allamah Tehrani ni kwamba; Hadithi ya Thaqalaini ilisimuliwa zaidi kupitia njia ya Zaid bin Arqam katika vyanzo vya Hadithi, na hata wanazuoni wa Kisunni nao pia wameinukuu zaidi Hadithi hiikupita njia yake yeye. [73]

Sayyid Hashm Bahrani amenukuu na kuorodhesha Hadithi kadhaa zenye madhumuni na dhana sawa na Hadithi ya Thaqalaini, katika katika kitabu chake Ghayatu Al-marami. Yeye ameweza kukusanya Hadithi 82 zenye mada na madhumuni sawa na Hadithi ya Thaqalaini kutoka vyanzo mbalimbali vya Shia kama vile; Al-kafi, Kamaluddin, Al-aamali Saduq, Al-aamali Mufid, Al-aamali Tusi, Ayunu Al-akhbari Al-ridha na Basairu al-Darajaati. [ 74] Kwa upande wa vyanzo vya Sunni, yeye pia ameweza kukusanya hadith 39 kutoka katika vyanzo hivyo. [75] Miongoni mwa vyanzo vya kuaminika vya Kisunni ambavyo vimeinukuu Hadithi ya Thaqalaini ni; Sahih Muslim, [76] Sunan al-Tirmidhi, [77] Sunan Nasa'i, [78] Sunan Darimi, [79] Musnadu Ahmad bin Hambal, [80] Al-mustadrak al-Sahihain, [81] Al-Sunanu al-Kubra, [82] Al-manaqibu cha Kharazmi, [83] Al-Mu'ujamu al-Kabir, [84] Kitab al-Sunnah, [85] Majma'u Al-zawaid wa Al-manba'u al-Fawaid, [86] Faraidu al-Simtain, [87] Jawahiru al-'Iqdain, [88] Jami'u al-usul fi Hadith Al-rasul (s.a.w.w), [89] Kanzu Al-'ummal, [90] Hilyatu Al-auliyaa wa tabakaatu Al-asfiyaa, [91] Al-muutalafu wa Al-mukhtalafu, [92] Istijlaabu Irtaqai Al-ghorafi, [93] Ihyaa-u Al-mayyiti Bifadhaili Ahlul-Bayt (a.s) [94] na mwisho Jami'u Al-masaaniidi wa Al-sunani. [95]

Wakati na Mahali Palipo simuliwa Hadithi

Kwa mujibu wa maelezo ya wanazuoni wa Kishia kama vile Sheikh Mufid [96] na Qadhi Noorullah Shoshtari, [97] ni kwamba; Hadithi ya Thaqalaini ilisimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) katika matukio kadhaa. [98] Kwa maelezo na maoni ya mwanzuoni wa Kishia Nassir Makarem Shirazi, ni kwamba; Haingii akilini ya kwamba kama Mtume (s.a.w.w) aliwasimulia masahaba zake katika zama na eneo moja, huku akiwa ametumia maneno na ibara tofauti katika kumfikishia kila mmoja wao dhana ya Hadithi hiyo. Bali kinachoonekana ni kwamba; yeye aliwasimulia masahaba zake Hadhithi hiyo mara kadhaa akiwa katika zama na nyakati tofauti. Na hilo ndilo lililopelekea kupatikana kwa Hadithi hiyo katika ibara na maneno tofauti. [99] Kwa mujibu wa nadharia ya Qadhi Noorullah Shoshtari aliyo ielezea katika kitabu chake Ihqaaqu al-Haqi, ni kwamba; Hadithi ya Thaqalaini imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) katika zama na sehemu nne tofauti; Siku ya Arafah huku akiwa juu ya ngamia, katika Msikiti wa Khaif, Katika Bonde la Ghadir alipokuwa akitoa khutba ya Ghadir katika tukio la Hijjatu al-Wida'a na katika khutba akiwa juu ya mimbari kabla ya kifo chake. [100] Sayyied Abdul Hussein Sharafuddin ametaja sehemu tano zilizosimuliwa Hadithi hii, nazo ni: Siku ya Arafah, Ghadir Khum, alipokuwa anarudi kutoka Taif, huko Madina akiwa juu ya mimbari na alipokuwa chumbani kwake bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa mgonjwa. [101]

Ibn Hajr Hitami, mmoja wa wanazuoni wa Kisunni, pia naye amerikodi nyakati na sehemu tofauti zilisimuliwa kwa Hadithi ya Thaqalaini, ambazo ni: Hijjatu al-Wida'a, Madina wakati wa maradhi ya Mtume (s.a.w.w), Ghadir Khum, na katika moja ya hotuba zake baada ya kurejea kutoka Taif. Kulingana maoni yake; hakuna aina yoyote ile ya ukinzani kati ya hati na matini ya Hadithi hiyo iliyonukuliwa katika zama, nyakati na sehemu tofauti. Kwa sababu inawezekana kwamba bwana Mtume (s.a.w.w) aliisema na kuihadithia Hadithi hii katika sehemu mbalimbali kutokana na umuhimu, hadhi na nafasi ya Qur'an pamoja na 'Itra zake [102].

Nyakati, zama na maeneo tofauti yaliyotajwa kuhusiana na mapokezi yalionukuu Hadithi hii moja kwa moja kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w), kutoka katika vyanzo vya Shia na Sunni ni kama ifuatavyo:

  • Ghadir Khum wakati Bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akirudi kutoka Hijjatu al-Wida'a. [103]
  • Siku ya 'Arafa katika Hijjatu al-Wida'a akiwa juu ya ngamia. [104]
  • Katika hotuba ya mwisho aliyowasomea watu siku ya kufa kwake.[105]
  • Katika ardhi ya Mina [106] au katika msikiti wa Khaif, siku ya mwisho ya siku za Tashriqi katika Hijjatu al-Wida'a. [107]
  • Katika hotuba ya siku ya Ijumaa baada ya swala ya Ijumaa. [108]
  • Katika hotuba baada ya swala yake ya mwisho ya jamaa aliyo wasalisha watu. [109]
  • Katika kitanda cha maradhi yake ya mwisho, pale masahaba walipokusanyika * karibu na kitanda cha Mtume (s.a.w.w). [110]
  • Akiwa katika kitanda cha mauti kabla ya kufa kwake. [111]

Mifano Hai, Pekee na Halisi ya Itra na Ahlu al-Baiti (a.s)

Neno Ahlul-Bayt katika nukuu kadhaa za Hadithi ya Thaqalaini, [112] limeonekana kukaa bega kwa bega na neno "'Itrati". [113] lakini katika baadhi ya nukuu za Hadithi hii, ni neno "'Itrati" tu ndilo lililotajwa ndani yake, [114] huku nukuu nyengine juu ya Hadithi hiyo, zikiwa zimelitaja neno "Ahlu al-Baiti" peke yake. [115] Pia katika baadhi ya Riwaya, badala ya kutumika neno "'Itrati", ndani yake wametajwa Aali za Ali bin Abi Talib. [116] Katika baadhi ya rikodi za Hadithi ya Thaqalaini, ibara ya Ahlu al-Baiti (a.s) imesisitizwa na kukaririwa mara kadhaa. [117]

Katika baadhi ya nukuu, neno "'Itrati" limetajwa bila ya kuambatanishwa na neno Ahlu al-Baiti, ila baada ya watu kumuuliza bwana Mtume au Maimamu kinachokusudiwa katika neno "'Itrati" wajibiwa kuwa; makusudio ya neno "'Itrati" ni Ahlul-Bayt za Mtume (s.a.w.w). [118] Katika moja ya orodha za Hadithi ya Thaqalaini ya upande wa madhehebu ya Shia kuhusiana na ufafanuzi wa makusudio yanayokusudiwa katika matumizi ya neno "Ahlul-Bayt", imeelezwa ya kwamba; Neno "Ahlul-Bayt" linalenga Maimamu kumi na mbili wa Kishia. [119] Miongoni mwa Riwaya zizofafanua lengo la matmizi ya neno hilo, ni ile Riwaya kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), ambapo baada ya watu kumuuliza; Ni wepi hao Ahlul-Bayt zako? Mtume (s.a.w.w)) alijibu kwa kusema: "Ni Ali(a.s), wajukuu zangu wawili na watoto tisa kutoka katika kizazi Hussein (a.s) ambao ni Maimamu waaminifu na maasumu. Fahamuni ya kwamba hao ndio Ahlul-Bayt na 'Itra zangu, wao wanatokana na nyama yangu na damu yangu. Imam Ali (a.s) naye pia alisema katika moja ya Hadithi zake, akijibu kuhusiana ni nani mfano pekee wa "'Itra" katika Hadithi ya Thaqalaini, alisema ya kwamba; mfano pekee wa "'Itra" ni mimi, Hassan, Hussein, na Maimamu tisa kutoka kizazi cha Hussein (a.s), ambao hitimisho lao litakuwa ni Imamu Mahdi (a.s). [121]

Wanachuoni wa Kishia kama vile Sheikh Saduqu [122] na Sheikh Mufid, [123] wamesema kwamba; kinachomaanishwa katika Hadithi ya Thaqalaini kupitia neno "'Itra" pamoja na neno "Ahlu al-Bait", ni Maimamu kumi na mbili wa Kishia. [124] Ayatullah Boroujerdi katika utangulizi wa kitabu chake kiitacho Jaami’u Ahadithu Al-shia amesema kwamba; Wanazuoni wote wa Shia wanakubaliana ya kwamba; wakusudiwa katika maana ya maneno mawili haya ('Itra na Ahlu al-Baiti) ni wale wanao miliki jumuisho la elimu zote na siri za kidini, ambao hawatelezi wala hawakosei katika matendo yao, nao ndio Maimamu wa Kishia (a.s). [125]

Marejeo ya Neno Itra Katika Vyanzo vya Sunni

Abdul Raouf Manawi katika kitabu chake kiitwacho Faidhu al-Qadiir, amelirejesha na kuliweka sambamba kimaana neno "Ahlul-Bayt na neno "Itra", na akasema ya kwamba; walengwa waliokusudiwa katika maneno mawili haya ni watu wa Kisaa (wailio funikwa shukwa na bwana Mtume (s.a.w.w)). [126] Naye Ibnu Abi Al-hadid Mu'utazili katika kitabu chake Sharhu Nahju Al-balagha ameandika akisema; 'Mtume (s.a.w.w) alipokuwa anawaarifisha Ahlul-Bayt zake kupitia Hadithi ya Thaqalaini, alilirejesha neno "'Itra" kwa Ahlul-Bayt zake. Na mafunzo yake mengine, aliwatambulisha watu wa Kisaa kuwa ndio Ahlul-Bayt zake. katika Hadithi ya Kisaa, Mtume (s.a.w.w) alisema: اللهم هؤلاءِ اهلُ بَیتی. Maana yake ni kwamba: "Ewe Mola wangu, hawa ndio Ahlul-Bayt zangu". Hakim Hasakani amenukuu kutoka kwa Barraa bin 'Aazib Al-ansari ya kwamba: "Mtume (s.a.w.w) amewaarifisha 'Itra zake kuwa ni; Ali (a.s), Fatima (a.s), Hassan (a.s) pamoja Hussein (a.s). [128] Samhudi naye amesema kwamba; "Miongoni mwa Ahlul-Bayt za bwana Mtume (s.a.w.w), Ali bin Abi Talib ni Imamu na mwanachuoni wao na ndiye anayestahiki zaidi kumfuatwa na kushikamana naye.” [129] Katika baadhi ya vyanzo, Ahlu-sunnah, imepokewa kutoka kwa Zaid bin Arqam ya kwamba: "Ahlu al-Baiti wa Mtume ni wale walioharamishiwa kupokea na sadaka, nao ni Aalu Ali, Aalu 'Aqiil, Aalu Ja'afar na Aalu Abbas. [130] Neno "Aalu" lililotumika hapo, linamaanisha kizazi au watoto.

Neno 'Itra katika kamusi, inamaanisha kizazi na jamaa wa karibu, [131] watoto na vizazi vizazi vyao [132] au jamaa makhususi. [133]

Sababu ya Kuitwa Thaqalaini

Hadithi ya Thaqalaini inajulikana kwa jina hilo kutokana na uwepo wa neno thaqalaini (ثَقَلَیْن) ndani yake [134] Neno hili husomeka kwa matamshi ya aina mbili; Thaqlaini (ثَقَلَیْن) na Thiqlaini (ثِقْلَیْن). Matamshi ya kwanza humaanisha vitu viwili vyenye thamani na ya pili humaanisha vitu viwili vizito. [135] Maoni mbalimbali yametolewa kuhusiana na sababu ya kule Qur'an na Ahlu Albaiti kuitwa "Thaqlaini". Katika utangulizi wa kitabu kiitwacho Jami'u Ahadithi Al-shia, kuna idadi ya nadharia tisa zilizotajwa kusiana na suala hili [136], baadhi yake ni kama ifuatavyo:

  • Abu al-Abbas Tha’lab, mwashairi na mwanalugha mashuhuri wa karne ya tatu, alipoulizwa kuhusiana na sababu ya Qur'an na Ahlul-Bayt jina la Thaqalaini, alisema kwamba; Viwili hivi vimepewa jina hilo kwa kuwa ni vigumu kushikamana na kufuatana navyo. Kwa sababu viwili hivi ni vyenye kuamrisha uchamungu na kutenda mema, na vinakataza maovu, kufuata matamanio ya nafsi na shetani. [138]
  • Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti, lengo la kuitaja Qur'an na 'Itra kwa jina la Thaqalaini, inatokana na uzito na ugumu uliopo katika kuitendea Qur'ani pamoja na Ahlu al-Baiti (a.s), na vigumu kufanya hivyo kutoka na utakatifu wa vitu viwili hivyo. [139]
  • Kwa mujibu wa maoni ya kundi la wanazuoni wa Kisunni ni kwamba; viyu viwili hivyo vimepewa jina hilo ili kuvitukuza na kuonesha thamani na adhama ya Qur'an na Ahlu al-Baiti (a.s), [140] kwa sababu kila chenye thamani huhisabiwa kuwa ni chenye uzito. [141]
  • Kwa mujibu wa kauli za baadhi ya watu kama Samhoudi ni kwamba; Sababu yake inatokana na kule viwili hivyo, kuwa ndio chimbuko la elimu na pia Ahlu al-Baiti kuwa ndio wenye kujua siri na sababu za kanuni za Sharia. Hayo basi ndiyo yaliyo mfanya bwana Mtume (s.a.w.w) kuvipa viwili hivyo jina la Thaqalaini. Pia hiyo ndiyo sababu ya yeye kuhimiza kuwafuata na kujifunza kutoka kwa Ahlu al-Baiti (a.s). [142]

Kizito Kikubwa na Kizito Kidogo

Makala Asili: Kizito kikubwa na Kizito kidogo

Katika baadhi ya nukuu za Hadithi ya Thaqalaini, Qur'an imezingatiwa kuwa ndio kizito kikubwa, na Ahlul-Bayt wakaitwa kizito kidogo. [143]

Kuna maoni mbalimbali yaliowasilishwa kuhusina na sababu sifa mbili hizi (kizito kikubwa na kidogo): Ibn Maitham Bahrani amesema kwamba; "Qur’an imeitwa kizito kikubwa, kutokana na Qur'an kuwa ndiyo asili kuu inayopaswa kufuatwa na kutiiwa. [144] Kwa mujibu wa nadharia ya Mirza Habibullah Khui, Ahlul-Bayt pia wanapaswa kufuatwa kama inavyopaswa Quran. Yeye anaamini ya kwamba; Qur'an imepewa jina la Kizito kikubwa na kutangulizwa mbele, kutokana na kulea Qur'an kuwa ndio muujiza wa Utumu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na ndiyo msingi mkuu wa dini ya Kiislamu. Inawezekana pia kwamba Qur'an ni dalili hoja kamili kwa watu wote, akiwemo Mtume mwenyewe na Maimam (a.s), lakini Ahlul-Bayt ni ni hoja na dalili umma peke yake, ndio maana Qur'an ikaitwa ikahisabiwa kuwa ni kizito kikubwa na Ahlul-Bayt wakapewa jina la Kizito kidogo. [145]

[145] Kulingana na maoni ya Abdullah Jawadi Amuli, ambaye ni mfasiri wa Qur'an; Ahlul-Bayt, katika sura ya uwanja dhahiri wa ulimwengu na katika dira ya kutoa mafunzo na kuielewesha dini, wao wanaonekana na kuhisabiwa kuwa ni Kizito kidogo; Lakini kwa upande wa cheo vya kiroho na kimaana katika ulimwengu batini, wao wana daraja ya juu zaidi kuliko Qur’an [146] Imam Khomeini, katika Kitabu chake Wasiyatnameh Siasi Ilahi, amewahisabu na kuwaweka Ahlul-Bayt (a.s) kwenye nafasi ya Kizoto kikubwa, yaani amewapa jina la “Kizito kikubwa”, ambacho ni kikubwa kuliko kila kitu, isipokuwa kile kizito kisicho na mipaka, ambacho kimepindukia kila kitu (yaani Mwenyezi Mungu. [147]

Tegemeo la Wanachuoni wa Kishia Katika Kuthibitisha Imani ya Shia Kuhusu Uimamu

Kwa ujumla, imeelezwa ya kwamba; kwa kutegemea dhana ya Hadithi ya Thaqalaini, kila kipengele na sifa ya kamilifu iliyo sifiwa nayo Qur'an Tukufu, pia sifa hiyo itachukuwa nafasi yake kwa Ahlul-Bayt (a.s). Baadhi ya sifa hizo ni ile sifa ya kuweka bayana baina ya haki na batili, sifa ya upambanuzi, sifa ya nuru na sifa ya wao kuwa ndio njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka. [148] Wanazuoni wa Kishia wameitegemea Hadithi ya Thaqalaini katika kuthibitisha idadi kadhaa za imani na itikadi za Shia. Baadhi ya imani hizo ni:

Uimamu wa Maimamu wa Shia

Moja kati ya vielelezo ya kuthibitisha nafasi ya Uimamu wa Maimamu wa Shia, Hadithi ya Thaqalaini imeonekana kukamata nafasi muhimu juu ya kuthibitisha suala hilo. [149] Miongoni mwa vielelezo na hoja muhimu zilizotajwa kutoka Hadithi ya Thaqalaini, kuhusiana na haki ya Uimamu wa Imam Ali (a.s) na maimamu wengine ni:

  • Uwazi wa maelezo ya Hadithi hiyo usemao ya kwamba; Qur'an na Ahlul-Bayt ni vitu viwili vilivyo shikamana pamoja bila ya kutengana, dhana ambayo inaashiria ukweli wa kwamba, Ahlul-Bayt wana elimu kamili ya Qur'an na wala wao hawaipingani na Qur'an hii, si kwa kauli wala matendo. Ukweli huu ni uthibitisho juu ya ubora wa Ahlu al-Baiti, na kiuhalisia watu bora ndio wanastahiki zaidi kushika nafasi ya Uimamu.
  • Katika Hadithi ya Thaqalaini, Ahlu al-Baiti wamewekwa sambamba na kufananishwa moja kwa moja na Qur'an. Hii inaonesha ya kwamba; kama ilivyokuwa ni wajibu kushikamana na kuifuata Qur'an, basi pia ni wajibu kuwafuata Ahlu al-Baiti (a.s). Ni lazima ifahamike wazi ya kwamba; si waju kumfuata mtu katika kila hali, isipokuwa Mtume na Maimamu Maasumu (a.s).
  • Katika baadhi ya nukuu za Hadithi ya Thaqalaini, badala ya neno "Thaqalaini خلیفتین", limetumika neno "khalifataina" (makhalifa wawili) limetajwa. Ni wazi kwamba; ukhalifa wa mtu unatokana na Uimamu wake jambo ambalo linampa yeye uhalali wa kutenda kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya manufaa ya Ummah.
  • Imeelezwa katika Hadith ya kwamba; hatopotea katu yule atakayeshikamana na Thaqalaini (Vizito viwili). Bwana Mtume (s.a.w.w) Thaqalaini imeifanya kuwa ndio ngao ya kuulinda umma wake na upotofu, kwa sharti ya wao kushikamana na ngao hiyo. [150]

Kuna baadhi walio sema ya kwamba; lau kwamba Mashia wasingekuwa na uthibitisho ule juu ya kuthibitisha ukhalifa wa Imam Ali (a.s) baada ya Mtume (s.a.w.w) zaidi ya Hadithi ya Thaqaqalaini, hadithi hii ingeliwatosha Mashia katika kusimamisha hoja dhidi ya wapinzani. [151]

Muendelezo wa Uimamu

Kwa mujibu wa maoni ya Muhammad Hassan Mudhaffar; katika baadhi ya vipengele vya Hadithi ya Thaqalaini, vinaonyesha ya kwamba, hadi Siku ya Kiyama lazima kuwe na mtu hai kutoka kwa 'Itra ya bwana Mtume (s.a.w.w). Miongoni mwavyo ni:

  • Ibara isemayo: اِن تَمَسَّکْتُم بِهِما لَن تَضِّلّوا (Iwapo mtashikamana na Vizito viwili, kamwe hutapotea): Kuto potea kamwe kunatokana na ukweli wa kwamba kile mtu anachoshikamana nacho kipo na kitaenedelea kuwepo daima.
  • Kwa mujibu wa kipengele kisemacho: "لَن یَفتَرِقا" (Katu viwili hivi havitatengana), ikiwa kutatokea zama fulani ambazo hakutakuwa na mtu kutoka 'Itra ya bwana Mtume (s.a.w.w), hapo patakuwa tayari pamesha patikana utengano kati ya Qur'an na 'Itra yake. Kwa hiyo, katika kila zama, ni lazima kuwe na mtu kutoka katika 'Itra ya bwana Mtume (s.a.w.w). [152]

Kwa mujibu wa maoni ya mwanazuoni Nassir Makarim Shirazi ni kwamb; ile ibara isemayo: “Viwili hivi daima vitakuwa pamoja hadi vinijie nami nikiwa karibu na bwawa (hodhi) la Kausar” inaonesha wazi kwamba, katika historia yote, ni lazima kuwe na mtu kutoka ukoo wa Ahlul-Bayt (a.s) kama ni kiongozi Maasumu. Kama ilivyo Qur'an, daima ni nuru ya uongofu, wao pia ni nuru ya uongofu wa daima. [153]

Umuhimu wa Kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s)

Wanazuoni wa Kishia wanasema kwamba; katika Hadith ya Thaqalaini, Ahlu al-Baiti (a.s) waliwekwa bega kwa gega na Qur'an na kuchukuliwa kuwa katu hawatatengana na Qur'an hiyo. Hivyo basi, kama ilivyo wajibu kwa Waislamu kuitii Qur-aan, pia itakuwa ni wajibu wao kuwatii Ahlul-Bayt (a.s). Kwa vile Mtume (s.a.w.w) hakutaja masharti yoyote yale katika kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s), itakuwa ni wajibu kuwafuata kikamilifu katika nyenendo zao, tabia na kikauli zao. [154]

Umaasumu wa Ahlul-Bayt (a.s)

Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wa Kishia, Hadith ya Thaqalaini inaashiria Umaasumu wa Ahlul-Bayt (a.s), kwa kuzingatia bayana katika Hadithi hiyo ya kwamba Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) ni vitu viwili vilivyo shikaman pamoja; Kwa sababu kutenda dhambi au kosa lolote kutasababisha kutengana kwa Ahlul-Bayt (a.s) na Qur'an. [155] Pia, bwana Mtume (s.a.w.w) amebainisha katika Hadithi hii kwamba; yeyote mwenye kushikamana na Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) hatapotea. Ikiwa Ahlul-Bayt (a.s) si maasumu, basi kuwafuata bila ya masharti kutaishia kwenye upotofu. [156] Kwa mujibu wa itikadi ya Abul Salaahi Halabiy, ambaye ni faqihi mwanatheolijia wa Kishia wa karne ya nne na ya tano Hijiria, ni wajibu wa kuwatii Ahlul-Bayt (a.s) bila ya masharti, ni kielelezo na uthibitisho wa umaasumu wao. [157] Ushahidi juu Umaasumu wa Ahlul-Bayt (a.s) umefafanuliwa kwa namna ya hoja kutoka katika Hadithi ya Thaqalaini kama ifuatavyo:

Ikiwa mtu daima yuko pamoja na Qur'an, bila shaka mtu huyo atakuwa amehifadhika kutokana na dhambi na kutenda makosa; Kwa sababu Qur'an ni kinga dhidi ya makosa na mitelezo ya nafsi. Kwa mujibu wa Hadithi ya Thaqaqalaini, Ahlul-Bayt (a.s) daima wako pamoja na Qur'an na hawatatenga nayo hadi Siku ya Kiyama. Kwa hiyo Ahlul-Bayt (a.s) ni maasum kama Qur'an ilivyo imara na maasumu. [158] Kwa mujibu wa ripoti ya Sayyid Ali Husseiniy Milaniy; Baadhi ya watafiti wa Kisunni kama vile Ibnu Hajar Hitami pia wameikubali Hadithi ya Thaqalaini kama ni kielelezo juu ya usafi na umaasumu wa Ahlul-Bayt (a.s). [159]

Mamlaka ya Kielimu ya Ahlul-Bayt (a.s)

Wanachuoni wa Kishia wameichukulia Hadithi ya Thaqalaini kuwa ni kielelezo cha mamlaka ya kielimu walionayo Ahlul-Bayt (a.s). [160] Hii ni kwa sababu kaulim biu ya Mtume (s.a.w.w) ya kushikamana na Kitabu chake pamoja na Ahlul-Bayt (a.s) unabainisha ya kwamba; hakuna mwenye mamlaka ya kielimu isipokuwa Ahlul-Bayt (a.s) na Waislamu wanapaswa kuwarejelea wao katika matukio na miongozo ya kidini yao. [161] Kwa hiyo, kauli na maoni ya Ahlul-Bayt (a.s), ni sawa na Qur'an, na ni hoja na dalili tosha kwa Waislamu.162]

Vile vile imesemwa ya kwamba; Hadith hii inaashiria kwamba Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s) kila moja ni dalili halali inazojitegemea. Kwa hivyo, ikiwa amri fulani, itatoka kwa upande wowote kati yao, iwe katika uwanja wowote ule, kama vile itikadi, hukumu za kifiqhi na maadili, itatosha kuwa ni uthibitisho na ushahidi juu ya ulazima wa kushikamana na amri hiyo. [163]

Katika baadhi ya nukuu za Hadith ya Thaqalaini, mwishoni mwake kuna kipengele kisemacho; (لَا تَسْبِقُوهُمْ فَتَهْلِكُوا وَ لَا تُعَلِّمُوهُمْ فَإِنَّهُمْ أَعْلَمُ مِنْكُم‏) Msije mkawatangulie mkaja kuangamia na wala msiwafundishe chochote kwani wao ni werevu kuliko nyinyi. [164] Katika utangulizi wa kitabu Jaami'u Ahadithi al-Shia, kwa kutegemea nukuu hii, kumeweza kuchopolewa nukta saba makhususi kuhusiana na mamlaka pamoja na elimu ya Ahlul-Bayt (a.s) kutoka katika Hadith ya Thaqalaini. Nazo ni kama ifuatavyo:

  1. Wajibu wa kujifunza kutoka kwa 'Itra ya Mtume (s.a.w.w) ili kusalimika kutokana na upotofu.
  2. Hatamu na mamlaka ya elimu kushikwa 'Itra ya Mtume (s.a.w.w) katika masuala ya amri na hukumu za Mwenyezi Mungu, ambapo kilelezo chake ni kule Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kuwajibisha watu kutafuta elimu kupitia 'Itra yake.
  3. Kutoka na mamalaka na hatamu za elimu kwa wasiokuwa ndani kundi la Ahlu al-Baiti, na kutokuwa na uwezo wa kielimu wa kuelewa hukumu zote za kisheria na kuwepo uwezekano wa kupotea endapo haturudisha maswali yao kwa Ahlu al-Baiti (a.s).
  4. Kutokuwa na ukamilifu wa kuielewa Qur'ani kwa wasiokuwa Ahlu al-Baiti, na kwamba 'Itra ya Mtume (s.a.w.w) ndio watu makhususi wenye uwezo wa kuchopoa na kuzivua hukumu za Mungu kupitia wavu wao wa kieleimu, pamoja na kuto kuwepo umahiri wa kuwafunza watu hukumu za Mungu isipokuwa kwa Ahlul-Bayt peke yao (a.s).
  5. Kuwa ni haramu kukataa maneno maamuzi ya 'Itra ya Mtume (s.a.w.w) kwa sababu ya ujuzi na mamalaka ya kielimu walio nayo.
  6. Kuwa na uwezo wa kielimu kuliko wote katika fani zote za kidini na zisizo za kidini. [165]

Sayyid Kamal Haidari, mwanatheolojia wa Kishia, akitegemea kielelezo cha Hadithi ya Thaqalaini, ameielezea na kusifu elimu ya Maimamu kuwa ni elimu isio na mipaka wala kikomo. [166]

Ubora wa Ahlul-Bayt

Makala Asili: Obora wa Ahlul-Bayt (a.s)

Imeemelezwa ya kwamba; Hadithi ya Thaqalaini imeweka wazi ubora wa Ahlul-Bayt (a.s) juu ya wengine; Kwa sababu Mtume (s.a.w.w) hakumweka mtu yeyote yule sambamba na Qur'an Ahlul-Bayt peke yao (a.s). Natija ya tendo hili la bwana Mtume (s.a.w.w), linasisitiza ya kwamba; Kama vile Qura'n Tukufu ilivyo bora na tukufu kuliko Waislamu, Ahlul-Bayt (a.s) pia nao ni bora kuliko wengine. [167]

Utawala na Mamlaka ya Uongozi

Kwa mujibu wa maoni ya Jafar Subhani, mwito wa Mtume (s.a.w.w) wa kuwataka Wislamu kushikamana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt zake (a.s) katika Hadith ya Thaqalaini, unaonesha kwamba; mamlaka na nafasi ya uongozi wa kisiasa, ni wa inastahiki kushikwa na Ahlul-Bayt peke yao (a.s). [169] Kwa mujibu wa riwaya hii, Ahlul-Bayt (a.s), ni makhalifa na warithi wa Mtume, na urithi wao ni urithi mpana na endelevu, unajumuisha mambo yote ya kisiasa pamoja. Ulazima na wajibu wa kuwafuata katika mamlaka ya uongozi wa kisiasa umethibitishwa kupitia hoja ya wajibu wa kufuata. Wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s), ni wajibu ulikusanya mambo yote; kiuchumi, kiibada, kisiasa pamoja na kitamadui. Hivyo basi ni wajibu kwa kila Muislamu kuwafuata wao katika masuala ya kisiasa yanayohusiana na jamii pamoja na mamlaka ya uongozi wa serikali. [171]

Kutokuwepo Tofauti Kati ya Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s)

Miongoni mwa tafsiri nyengine za kitheolojia za Hadith ya Thaqalaini ni kwamba; kulingana na kipengele katika Hadith ya Thaqalaini kisemacho: "لَنْ يَفْتَرِقَا حَتَّى يَرِدَا عَلَیَّ الْحَوْض" "Katu viwili hivyo havitatengana mpaka viwasili kwenye bwawa (Hodhi la Kauthar)", inaonekana ya kwamba; hakuna tofauti kati ya Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s). [172] Kwa mujibu wa mtazamo wa Mohammad Waidhzadeh Khorasaniy ni kwamba: Sababu ya uwiano ambatano baina ya Qur'an na Ahlul-Bayt (a.s), ni kwamba; elimu ya Imamu Inatokana na elimu ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na hatimaye inaishia kwenye wahyi wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo sababu ya kuto wepo tofauti yoyote kati ya viwili hivyo, na daima vipo bega kwa bega hadi siku ya Kiama. [173]

Kielelezo cha Hadith Juu ya Kutotiwa Mkono kwa Qur’an

Imeelezwa ya kwamba; kuwa Hadithi ya Thaqalaini inaashiria kusalimika kwa Qur'an kutokana na upotoshwaji; Kwa sababu Mtume (s.a.w.w) amesema ndani ya Hadithi hiyo kwamba; Qur'an na Ahlul-Bayt vitaendelea kubaki pamoja mpaka Siku ya Kiyama na yeyote atakayeshikamana nazo hatapotea. Kama Qur'an haikuhifadhiwa kutokana na upotoshwaji, kusingekuwa na kushikamana na Qur'an hiyo, kwani kukifuata kitabu kilicho potoshwa hupelekea kuingi katika upotofu tu. [174]

Mtazamo wa Ahlu al-Sunna

Wanazuoni wa Kisunni pia nao wana ufahamu kadhaa katika tafsiri ya dhana ya Hadithi ya Thaqalaini, baadhi yake ni kamai zifuatazo: Kwa mujibu wa maoni ya Ibn Hajari Hitamiy na Shams al-Din Sakhawiy, mwanahadithi na mfasiri kutoka madhehebu ya Shafi'i wa karne ya 9 Hijiria ni kwamba; katika Hadithi ya Thaqalaini kuna masisitizo makubwa juu ya wajibu au sunna katika kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s), kuwafanyia hisani na kuwaheshimu. Hilo linatokana na kwamba Ahlul-Bayt (a.s), ndio watu watukufu zaidi duniani kuliko watu wote, kinasaba na kiubora. [175]

Ali bin Abdullah Samhudi amesema kwamba: "Kutokana na Hadith hii, ni lazima inafahamika kwamba mpaka Siku ya Hukumu, ni lazima kuwepo mtu kutoka 'Itra ya bwana Mtume (s.a.w.w) anayestahiki kufuatwa na kutegemewa. Hilo ndilo litakaloweza kuakisi tafsiri ya sisitizo liliotajwa katika Hadithi hii, na kwamba yeye ndiye melngwa, kama anavvyo onekana wazi wa pili wa Hadithi hiyo , ambaye ni Quran Tukufu. Kwa hiyo, wao (yaani 'Itra) ndiyo sababu kusalimika kwa watu wa ardhini, na kutokuwepo kwao ndani ya ardhi hii, kutapelekea kutoweka kwa waishiwo ardhini humo. [176]

Kwa mujibu wa nadharia ya Abdul Raouf Munaawi, mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i wa karne ya 10 na 11Hijiria, Hadith ya Thaqalaini imeweka bayana ya kwamb; Bwana Mtume (s.a.w.w) aliusia umma wake kuheshimu Qur'an na Ahlu al-Baiti (a.s), kwa kuwatanguliza na kushikamana nao katika masuala yao ya dini. Kulingana na maoni yake, Hadith hii inaashiria kwamba; katika zama zote hadi kufukia Siku ya Kiama, ni lazima kuwe na mtu kutoka kwa Ahlu al-Baiti atakaye kuwa na mamlaka na sifa za kushikamana naye. [177]

Sa'ad al-Din Taftazani, mwanatheolojia wa Ash’ari wa karne ya 8 ya mwandamo anaamini kwamba; Hadithi ya Thaqalaini inahusiana na ubora wa Ahlu al-Baiti juu ya wengine, na kigezo cha ubora wao ni elimu, uchamungu, na nasaba ya ukoo wao. Jambo hili linafahamika kutokana na kule kuwekwa kwao sambamba na Qur'an. Jambo ambalo linatupa welewa juu ya wajibu wa kushikamana nao; Kwani kushikamana na Qur'an si jingine isipokuwa ni kutenda matendo yetu kulingana elimu na mwongozo wa Qur'an na 'Itra. [178]

Fadhlu bin Ruuzbahan, mmoja wa wanazuoni wa Kisunni wa karne ya tisa na kumi ya Hijiria, anaamini kwamba; Hadith za Thaqalaini inaashiria wajibu wa kushikamana na kuwafuata Ahlu al-Baiti (a.s) katika maneo yao pamoja na vitendo vyao, pia Hadithi hiyo inasisitiza kuwaheshimu na kuwapenda na kuwapa taadhima; Ila kwa mtazamo wake yeye Hadithi ya Thaqalaini haijabainisha suala Uimamu na ukhalifa wao. [179]

Orodha ya Vyanzo Vinavyo Husiana na Mada (Bibliografia)

Ukuachana na kunukuu Hadithi ya Thaqalaini, pia Wanazuoni wa Kishia wameandika vitabu kwa makhususi kuhusu mada ya Hadithi ya Thaqalaini. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Hadithu al-Thaqalaini حدیث‌ الثقلین: kiliyoandikwa na Qawamu al-Ddin Muhammad Washenawi Qommiy: Katika kitika kitabu chake hicho, ametafiti ndani yake nukuu tofauti kuhusiana na Hadithi hii na kuchunguza kwa makini tofauti za maneno kati ya riwaya tofauti zilizo nukuu Hadithi hiyo. [180]
  • Hadith al-Thaqalain حدیث‌ الثقلین: cha Najmu al-Ddin Askariy; Kitabu hichi kimeandikwa kwa Kiarabu katika juzu moja na kilikamilika uandishi wake mnamo mwaka 1365 Hijiria.
  • Hadith al-Thaqalain حدیث‌ الثقلین: cha Sayyid Ali Milani: Kitabu hichi kimeandikwa kwa Kiarabu katika kujibu maswali ya changamoto yaliyotolewa na Ali Ahmad Al-Saaluds kuhusu Hadith al-Saqlain. [181]
  • Hadith al-Thaqalain wa Maqaamaatu Ahlu al-Baiti حدیث الثقلین و مقامات اهل البیت: Kitabu hichi, kilikusanywa na kuandikwa kupitiana kikundi cha wanafunzi wa Bahrain wa Madrasatu Ahlu al-Dhikri, kilichoandikwa kupitia mihadhara mbali mbali juu ya Hadith al-Thaqalain ya Ahamad al-Maahuuziy, ambaye ni mwanazuoni wa Kishia wa Bahrain. [182]
  • Hadith al-Thaqalain حدیث الثقلین؛ سنداً و دلالةً: ambcho ni mkusanyiko wa mihadhara ya Sayyied Kamal Haidari, iliyokusanywa na kuhaririwa na Asadu Hossein Ali Shimriy katika sura tatu; tafiti juu ya molongo wa nukuu ya Hadithi, kielelezo cha hadithi, na kujibu changamoto juu ya Hadithi ya Thaqalaini, kitabu hichi kmechapishwa na Taasisi ya al-Huda. [183]
  • Encyclopedia ya Hadithi ya al-Thaqqlin موسوعةُ حدیثِ الثَّقلین: Kitabu hichi kimeandikwa katika juzu nne kilichokusanywa na Markazu Abhahi al-'Aqaaidiyyah, katika juzuu mbili zake za mwanzo, kinachunguza kazi zilizoandikwa au kurikodiwa na watu madhehebu ya Shia Ithnaashariyyah kuanzia karne ya kwanza hadi ya kumi, na katika juzuu ya tatu na ya nne. , kazi za Mashia wa madhehebu ya Zaidiyyah na Mashia Ismailiyyah hadi karne ya kumi Hijiria, kuhusu Hadithi ya Thaqalaini.

Masuala Yanayo Fungamana

Rejea

Vyanzo

  • Albani, Nasir al-Din, Zilal al-Janna
  • Amini, 'Abd l-Husayn, Al-Ghadir. Qom: Markaz al-Ghadir li al-Dirasat al-Islamiyya, 1421
  • 'Aqili, Muhammad b. 'Amr al-, Du'afa' al-kabir. Beirut: Dar al-Kutub al-'Ilmiyya, 1418
  • 'Ayyashi, Muhammad b. Mas'ud al-, Al-Tafsir. Qom: Hashim Rasuli Mahallati, 1380-1381
  • Bahrani, Sayyid Hashim b. Sulayman al-, Ghayat al-maram wa hujja al-khisam
  • Bazzaz, Ahamad b. 'Amr al-, al-Bahr al-zikhar. Maktaba al-'Ulum al-Hikam
  • Darqutni, 'Ali b. 'Umar al-, al-Mu'talaf wa al-mukhtalaf. Beirut: Dar al-Maghrib al-Islami
  • Daylami, Hasan b. Muhammad, Irshad al-qulub. Qom: 1368
  • Hakim al-Niyshaburi, Muhammad b. 'Abd Allah al-, Al-Mustadrak 'ala al-Sahihayn. Beirut: Dar al-Ma'rifa
  • Hanbal, Ahmad, Musnad Ahmad. Cairo
  • Haytami, Ibn Hajar al-, Al-Sawa'iq al-muhriqa fi al-radd 'ala ahl al-bida' wa al-zandiqa. Cairo: 'Abd al-Wahhab 'Abd al-Latif,1385
  • Haythami, 'Ali b. Abibakr al-, Kashf al-astar. Beirut: Mu'assisa al-Risala, 1979
  • Ibn Athir, 'Ali b. Muhammad, Usd al-ghaba. Beirut: Dar al-Kutub al-'Ilmiyya, 1415
  • Juwayni, Ibrahim b. Muhammad al-, Fara’id al-Simatayn. Beirut: Muhammad Baqir Mahmudi, 1398-1400
  • Kulayni, Muhammad b. Ya'qub al-, Al-Kafi. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiyya
  • Majlisi, Muhammad Baqir al-, Bihar al-anwar li durar akhbar al-a'imma al-athar. Beirut: Mu'assisa al-Wafa'
  • Manawi, Zayn al-Din Muhammad al-, Fayd al-ghadir sharh al-jami' al-saghir. Egypt: Al-Maktaba al-Fikriyya al-Kubra, 1356
  • Mufid, Muhammad b. Muhammad al-, Al-Irshad fi ma'rifa hujaj Allah 'ala al-'ibad. Qom: 1413
  • Muttaqi al-Hindi, 'Ala' al-din 'Ali al-. n.d. Kanz al-'Ummal fi Sunan al-'Aqwal wa al-'Af'al. Beirut
  • Nasa'i, Ahamd b. 'Ali al-, Sunan al-kubra. Beirut: Dar al-Kutub al-'Ilmiyya, 1411
  • Niyshaburi, Muslim b. Hajjaj al-, Sahih. Istanbul: 1401
  • Saduq, Muhammad b. 'Ali al-, Al-Amali. Beirut: 1400
  • Saduq, Muhammad b. 'Ali b. Babawayh al-, Kamal al-din wa itmam al-ni'ma. Qom: 'Ali Akbar Ghaffari, 1363
  • Saduq, Muhammad b. 'Ali b. Babawayh al-, 'Uyun akhbar al-Rida. Qom: Mahdi Lajiwardi, 1363
  • Saffar al-Qummi, Muhammad b. Hasan, Basa'ir al-darajat fi fada'il al muhammad. Qom: Muhsin Kuchi Baghi Tabrizi, 1404
  • Samhudi, 'Ali b. 'Abd Allah al-, Jawahir al-'aqdayn fi fadl al-sharafayn. Beirut: Mustafa 'Abd al-Qadir 'Ata, 1415
  • Sharaf al-Din, Sayyid 'Abd al-Husayn, al-Muraji'at. Beirut: Husayn Radi, 1402
  • Tabarani, Sulayman b. Ahmad al-, al-Mu'jam al-awsat. Dar al-Haramayn, 1415
  • Tabarani, Sulayman b. Ahmad al-, al-Mu'jam al-kabir. Beirut: Hamdi 'Abd al-Majid Salafi, 1404
  • Tabrisi, Ahmad b. 'Ali, Al-Ihtijaj. Najaf: 1386
  • Tirmithi, Muhammad b. 'Isa al-, Sunan. Istanbul: 1401
  • Wa'iz zada Khurasani, Muhammad, Hadith al-Thaqalayn. Tehran: 1416
  • Zurqani, Muhammad b. 'Abd al-Baqi, Sharh al-mawahib al-ladunniyya. Beirut: Dar al-Kutub al-'Ilmiyya