Nguzo za Sala

Kutoka wikishia
Kwa ajili ya matumizi mengine angalia nguzo

Nguzo za Sala (Kiarabu: أركان الصلاة) ni idadi kadhaa ya mambo ya wajibu ya Sala ambayo kupunguzwa au kuongezwa hata kwa kusahau kunapelekea Sala ibatilike.

Mafakihi mashuhuri wa Kishia wametambua nia, kisimamo (Qiyam), Takbira ya Kuhirimia (Takbirat al-Ihram), rukuu na sijida mbili kuwa ni nguzo za Salama.

Maana ya Rukn (Nguzo)

Rukn maana yake ni nguzo na msingi wa kila kitu na katika ibada za kisheria ni kipengee ambacho kukipunguza au kukiongeza kwa makusudi au kwa kusahau kunapelekea kubatilika ibada.[1] Baadhi ya vipengele vya Sala, Hija na Umra ni nguzo.[2]

Nguzo za Sala

Kwa mujibu wa kauli na nadharia mashuhuri ni kwamba nguzo za Sala ni: Nia, Qiyam (kusimama) Takbira ya Kuhirimia, kurukuu na sijida mbili.[3] Makusudio ya nia ni ile hali ya kusali kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na kujikurubisha Kwake ambapo wakati mwingine hilo huelezwa kuwa ni kuwa na kusudio. Katika nia sio lazima kuleta taswira ya kitu katika akili na fikra au kutamka kwa ulimi.[4] Makusudio ya Qiyam ni kusimama wakati wa kutoa takbira ya kuhirimia na vilevile kisimamo kilichoungana na rukuu. Kwa maana kwamba, rukuu iwe imetokana na hali ya kusimama.[5]

Baadhi ya wanazuoni msimamo wao ni kuwa, kuelekea kibla katika hali ya hiari nayo ni katika nguzo za Sala;[6] kama ambavyo baadhi ya mafakihi wa zamani wamenukuliwa pia wakikitaja kipengee cha kisomo (qiraa) kuwa ni miongoni mwa nguzo za Sala. [7]

Kuondoa au Kupunguza Nguzo

Mafakihi mashuhuri wanasema kuwa, kuongeza au kupunguza nguzo ya Sala kunabatilisha Sala bila kujali nyongeza na punguzo hilo limefanywa kwa makusudi au kwa kusahau.[8] Hata hivyo, baadhi ya mafakihi (wanazuoni wa fiq’h) wanasema kwamba, kuleta nyongeza kwa kusahau katika kipingee ambacho ni nguzo katika Sala hakubatilishi Sala. [9]Swahib Ur’wah Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi mwandishi wa kitabu cha al-Ur’wat al-Wuthqa yeye anaamini kuwa, kuleta nyongeza katika nia kwa maana ya kuongeza nia na kusudio la kusali ni jambo lisilotasawarika na kwa maana ya kuleta taswira ya Sala katika fikra ni jambo ambalo anasema, halidhuru nia na halibatilishi Sala.[10]

Kuacha kwa Kusahau

Wakati wowote mwenye kusali atakapoacha nguzo miongoni mwa nguzo za Sala, madhali hajaingia katika nguzo nyingine anaweza kukileta kipengee alichokisahau ambacho ni nguzo.[11]

Rejea

  1. Muhaqiq Hilli, Sharaih al-islami, 1409 H, juz. 1, uk. 62; Najafii, Muhammad Hussein, Jawahiru al-kalam, juz. 9, uk. 239
  2. Khomeini, Tahriru al-wasila, Nashir: Muasase tandhim wa nashr athar Imam Khomeini(r.a), juz. 1, uk. 153
  3. Allamah Hilli, Mukhtalaf shia, 1412 H, juz. 2, uk. 139-140
  4. Tabatabai Yazdi, Al-uruwat al-uthqa, 1419 H, juz. 2, uk. 434
  5. Tabatabai Yazdi, Al-uruwat al-uthqa, 1419 H, juz. 2, uk. 473
  6. Ibnu Hamze Tusi, Al-wasila, 1408 H, uk. 93
  7. Sheikh Tusi, Al-mabsuut, Maktabat al-mardhiyah, juz. 1, uk. 105
  8. Shahidu Thani, Rawadhat al-bahiyyah, Intisharat ilmiye islamiye, juz. 1, uk. 644
  9. Najafii, Jawahir al-kalam, Dar ihyau turath al-arabi, juz. 9 uk. 239-241
  10. Tabatabai Yazdi, Al-uruwat al-uthqa, 1419 H, UK. 433
  11. Najafii, Jawahir al-kalam, Dar ihyau turath al-arabi, juz. 12 uk. 238-239

Vyanzo

  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Mukhtalaf al-Shīʿa fī aḥkām al-sharīʿa. Edited by Markaz al-Abḥāth wa l-Dirāsāt al-Islāmīyya. Qom: Daftar-i Tablīghāt-i Islāmī, 1412 AH.
  • Ibn Ḥamza al-Ṭūsī, Muḥammad b. ʿAlī. Al-Wasīla ilā nayl al-faḍīla. Edited by Muḥammad al-Ḥasūn. Qom: Maktabat Ayatollah al-Marʿashī al-Najafī, 1408 AH.
  • Najafī, Sayyid Muḥammad Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharāyiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1362 AH.
  • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn ʿAlī b. ʾAḥmad al- ʿĀmilī al-. Al-Rawḍa al-bahīyya fī sharḥ al-Lumʿa al-Dimashqīyya. Tehran: Intishārāt al-ʿIlmīyya al-Islāmīyya, n.d.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al- Al-Mabsūṭ fī fiqh al-Imāmīyya. Edited by Muḥammad Bāqir Bihbūdī. Tehran: Maktabat al-Murteḍawīyya, n.d.
  • Yazdī, Sayyid Muḥammad Kāẓim al-. Al-ʿUrwa al-wuthqā. Qom: Ismāʿīlīyān, 1419 AH.