Nenda kwa yaliyomo

Sala ya usiku

Kutoka wikishia

Makala hii ni kuhusiana na Sala ya usiku. Kama unataka kujua kuhusiana kumka usiku na kuswali na kuomba dua angalia makala ya Tahajjud.

Sala ya usiku (Kiarabu: صلاة الليل) ni Sala ya mustahabu ambayo wakati wake wa kuisali ni baada ya nusu ya usiku wa kisheria mpaka wakati wa adhana ya alfajiri. Sala ya usiku ilikuwa wajibu kwa Mtume (s.a.w.w) na kwa wengine ni mustahabu na Sala hii imetiliwa mkazo mno kuisali. Kuna hadithi nyingi zinazoonyesha kuweko fadhila za kusali Sala ya usiku na athari zake. Miongoni mwazo ni kwamba, Sala hii imetajwa kuwa Sala bora zaidi miongoni mwa Sala za mustahabu na ni katika ishara za Shia wa kweli.

Sala ya usiku ina rakaa 11 ambayo husaliwa katika muundo wa Sala tano za rakaa mbili mbili na Sala moja yenye rakaa moja. Rakaa tatu za mwisho za Sala hii zina fadhila kubwa zaidi ikilinganishwa na rakaa zingine za Sala hii. Rakaa hizi tatu zinajumuisha rakaa mbili za Sala ya shufaa na rakaa moja ya Sala ya witiri.

Sisitizo la kusaliwa Sala ya usiku

Sala ya usiku ni miongoni mwa Sala za mustahabu ambayo katika hadithi imekokotezwa na kutiliwa mkazo mno juu ya kuisali. Miongoni mwayo ni wasia wa Bwana Mtume (s.a.w.w) kwa Imamu Ali bin Abi Talib (a.s) ambaye alimuusia mara tatu kuhusiana na Sala ya usiku. [1] Kadhalika Mtukufu huyo amenukuliwa akiwahutubu Wislamu ya kwamba: Hongereni kwenu kwa Sala ya usiku, hata kama itakuwa ni rakaa moja; kwani Sala ya usiku inamzuia mtu kufanya dhambi, inazima hasira za Mwenyezi Mungu na ni kinga ya moto siku ya Kiyama." [2] Katika vitabu vya hadithii kuna mlango makhsusi wa hadithi zinazohusiana na Sala ya usiku. [3]

Sheikh Saduq (aliaga dunia 381 Hijiria) msomi na mtaalamu wa elimu ya hadithi wa Kishia anasema, Sala ya usiku ilikuwa wajibu kwa Mtume (s.a.w.w) na ni mustahabu kwa wengine. [4] Sheikh Mufid kwa upande wake ameitambua Sala ya usiku kuwa ni katika sunna zilizotiliwa mkazo. [5]

Ayatullah Qadhi alimhutuhu Allama Tabatabai kwa kumwambia: "Mwanangu, kama unataka dunia sali Sala ya usiku. Kama unataka akhera sali pia Sala ya usiku". [6]

Namna ya kusali Sala ya usiku

Sala ya usiku ina rakaa 11: Rakaa nane zinasaliwa kwa sura ya Sala nne (rakaa mbili mbili) kwa nia ya nafila (sunna) ya usiku. Rakaa mbili nyingine zinasaliwa kwa nia ya Sala ya Shaf'i (Shufaa) na Sala moja ya rakaa moja inasaliwa kwa nia ya Sala ya witiri. [7]

Ni mustahabu katika rakaa ya kwanza ya Sala ya Shaf'i (shufaa) kusoma Surat al-Fatiha na Surat al-Nas na katika rakaa ya pili Surat al-Fatiha na Surat al-Falaq. Kadhalika katika Sala ya witiri baada ya Surat al-Fatih ni mustahabu kusoma Surat Tawhid mara tatu, na kusoma mara moja Surat al-Falaq na al-Nas. [8] Ni mustahabu katika kunuuti ya Sala ya witiri kuwaombea dua au maghafira waumini 40. [9] Vile vile kusema mara 70: «اَسْتَغْفِرُاللهَ رَبّی وَ اَتُوبُ اِلَیه» ; Naomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi, na ninatubu kwake. Kutamka mara 7: «هذا مَقامُ الْعائِذِ بِک مِنَ النّارِ» ; Hapa ni mahala pa kimbiliko kutoka motoni. Na kusema mara 300: «اَلعَفو» ; Msamaha. Kisha baada ya hapo asome dua hii: [10] «رَبِّ اغْفِرْلی وَارْحَمْنی وَ تُبْ عَلی اِنَّک اَنْتَ التَّوّابُ الْغَفُورُ الرَّحیمُ» ; Mola wangu Mlezi, nisamehe na unirehemu na ukubali toba yangu, kwani Wewe ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kusamehe, Mwingi wa rehma. Sheikh Tusi ameusia katika kitabu cha Misbah al-Mutahajjid juu ya kusoma dua ya Hazeen baada ya Sala ya usiku. [11]

Athari na fadhila za Sala ya usiku

Katika hadithi mbalimbali kumetajwa athari na fadhila nyingi zinazopatikana kwa kusali Sala ya usiku; miongoni mwazo ni hadithi iliyokuja katika kitabu cha Bihar al-Anwar ambapo Mtume (s.a.w.w) amenukuliwa akisema: Sala ya usiku ni sababu ya ridha na furaha ya Mwenyezi Mungu, urafiki na malaika, kuwa na maarifa, nyumba kupata nuru, utulivu wa mwili, chuki dhidi ya shetani, kujibiwa dua, kutakabaliwa amali, kaburi kuwa na nuru na kujizatiti kwa silaha mbele ya adui. [12] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ni kwamba: Sala ya usiku inamfanya mtu kuwa na sura nzuri, mwenye tabia njema, anayenukia vizuri, inaongeza riziki, inasaidia kulipa deni, inaondoa ghamu na huzuni na inafanya macho ya mtu kuwa na nuru. [13] Imam Swadiq (a.s) amenukuuliwa katika hadithi nyingine akisema kuwa: Utajiri na watoto ni pambo la maisha ya dunia na rakaa nane za Sala mwisho wa usiku na rakaa moja ya Sala ya witiri ni mapambo ya akhera. [14]

Baadhi ya fadhila zingine za Sala ya usiku zilizokuja katika hadithi ni:

  • Sala bora kabisa ya mustahabu. [15]
  • Chimbuko la fakhari ya muumini. [16]
  • Chimbuko la fahari ya Mwenyezi Mungu kwa Malaika. [17]
  • Ishara za kuwa Shia wa kweli. [18]

Kwa mujibu wa hadithi zilizonukuliwa na Sheikh Saduq kwenye kitabu cha Ilal al-Sharai’ kutoka kwa Maimamu ni kwamba: Dhambi ni sababu ya kunyimwa tawfiki ya kusali Sala ya usiku. [19]

Hukumu

Baadhi hukumu za Sala ya usiku kwa mujibu wa vitabu vya fiq’h ni kwamba:

  • Sehemu bora kabisa ya Sala ya usiku ni Sala ya Shaf’i (shufaa) na Sala ya witiri, na Sala ya witiri ni bora zaidi kuliko Sala ya Shaf’i. Katika Sala ya usiku inawezekana kutosheka na kusali Sala za Shaf’i na witiri au Sala ya witiri. [20]
  • Wakati wa Sala ya usiku ni kuanzia nusu ya usiku wa kisheria mpaka wakati wa kuchomoza kwa alfajiri na kusali Sala hii wakati wa kukaribia alfajiri ni bora zaidi kuliko nyakati zingine. [21] Sayyid Ali Sistani, mmoja wa Marajii Taqlidi anasema kuwa, wakati wa Sala ya usiku ni kuanzia mwanzoni mwa usiku. [22]
  • Endapo mtu atasali Sala ya usiku kwa kukaa, ni bora akahesabu kila rakaa mbili za kukaa kwamba, ni rakaa moja ya kusimama. [23]
  • Msafiri na mtu ambaye kwake yeye ni vigumu kusali Sala ya usiku baada ya nusu ya usiku, anaweza kusali mwanzoni mwa usiku. [24]
  • Kama mtu hakusali Sala ya usiku, anaweza kuilipa kadhaa. [25]
  • Kulipa kadha Sala ya usiku ni bora zaidi kuliko kuisali Sala hii kabla ya nusu ya usiku.

Monografia

Kumeandikwa kwa lugha mbalimbali vitabu tofauti kuhusiana na athari za Sala ya usiku. Katika makala ya utambuzi wa kitabu kuhusu Sala ya usiku, kumetambulishwa vitabu 70 ambapo waandishi wa Kishia wameandika vitabu hivyo kwa lugha ya Kiarabu na Kifarsi. [27] Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Adab Salat al-Layl (adabu za Sala ya usiku), kilichoandikwa na Muhammad Baqir Fesharaki (aliaga dunia: 1315 Hijiria)
  • Salat al-Layl; Fadhluha wawaqtuha waadaduha wakaifiyatuha wal-Khususiyat al-Rajiah Ilayha minal kitab Wasunnah: Mwandishi Ghulam reza Erfaniyan (aliaga dunia: 1382 Hijiria Shamsia).
  • Adab Salat al-Layl Wafadhliha, mwandishi, Sayyid Muhammad Baqir Shafati (aliaga dunia: 1260 Hijria). [28]

Vyanzo

  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • ʿIrfāniān, Mīrzā Ghulām Riḍā. Ṣalāt al-layl, faḍluhā wa waqtuhā wa ʿadaduhā wa kayfīyatuhā wa al-khuṣūṣiyāt al-rājiʿa ilayhā min al-kitāb wa al-sunna. Najaf al-Ashraf: Maṭbaʿat al-Adab, 1401 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Muttaqī Hindī, 'Ala al-Dīn. Kanz al-ʿummāl fī al-sunan wa al-'af'āl. [n.p]. [n.d].
  • Qummī, Abbās. Mafātīḥ al-jinān. with Persian translation. 1st edition. Tehran: Nashr-i Mashʿar, 1387 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. 2nd edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Sijistānī, Sulaymān b. al-Ashʿath al-. Sunan-i Abī Dāwūd. [n.p]. [n.d].