Shia

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Madhehebu ya Shia)
Makala hii ni kuhusu Shia, kama unataka kufahamu kuhusiana na Shia Ithnaashariyah, angalia makala ya Shia Imamiyyah.

Shia (Kiarabu: التشيع) ni moja ya madhehebu mawili makubwa katika dini ya Uislamu. Kwa mujibu wa madhehebu haya, Mtume (s.a.w.w) aliamrishwa na Mwenyezi Mungu amteue Imam Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa mrithi wake mara moja baada tu ya kuaga dunia Mtume. Uimamu ni katika misingi na mizizi ya madhehebu ya Shia na hilo ni katika mambo yanayowatofautisha Mashia na Ahlul-Sunna. Kwa mujibu wa msingi huu, Imam anateuliwa na Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume (s.a.w.w) na hivyo yeye kumtambulisha na kumtangaza Imamu huyo kwa watu.

Mashia wote ukiacha Zaydiyyah, wanaamini kwamba, Imam ni maasumu (hatendi dhambi) na wanaamini kuwa, Imamu wa mwisho ambaye ni Muhammad Mahdi Muahidiwa (a.t.f.s) yuko ghaiba (haonekani katika upeo wa macho ya watu) na kuna siku atadhihiri kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuja kuijaza dunia uadilifu na usawa baada ya kuwa imejaa dhulma na ukandamizaji.

Baadhi ya mambo mengine ya kiitikadi ambayo yanawatofautisha Waislamu wa madhehebu ya Mashia na Waislamu wengine ni: Uzuri na ubaya wa kiakili, upambanuzi wa sifa za Mwenyezi Mungu, jambo baina ya mambo mawili, masahaba wote sio waadilifu, taqiya, tawassuli, na uombezi (shufaa).

Katika madhehebu ya Shia kama ilivyo katika madhehebu ya Kisuni, vyanzo vya kunyambua (kutoa) hukumu za kisheria ni Qur’an, Sunna, akili na ijma'a (itifaki na makubaliano ya Maulamaa). Hata hivyo, Mashia pamoja na Sunna za Mtume wanazichukulia Sunna za Maimamu pia, yaani kitendo na maneno yao kuwa ni hoja. Hii leo madhehebu ya Shia yapo katika makundi matatu: Imamiyyah, Ismailiyyah na Zaydiyyah. Shia Imamiyyah au Shia Ithnaashariya ndilo dhehebu lenye wafuasi wengi zaidi miongoni mwa madhehebu ya Kishia hii leo duniani. Wao wanaamini Uimamu wa Maimamu kumi na mbili, wa kwanza wao ni Ali bin Abi Talib (a.s) na wa mwisho wao ni Muhammad Mahdi Muahidiwa (a.t.f.s).

Shia Ismailiyyah, wanawakubali Maimamu mpaka Imamu wa Sita yaani wanaishia kwa Imam Ja’afar Swadiq (a.s) na baada ya hapo wanaamini kwamba, Imam anayefuata ni Ismail mtoto wa Swadiq na wanaamini kuwa, Muhammad mtoto wa Ismail ni Imam na wanaamini kwamba, yeye ndiye Mahdi Muahidiwa.

Shia Zaydiyyah wao hawaweki mpaka wa idadi ya Maimamu bali wanaamini kwamba, kila mtoto miongoni mwa mtoto wa Fatma (a.s) ambaye ni mjuzi, mwenye kuipa mgongo dunia, shujaa na mkarimu na akaanzisha harakati na mapinduzi basi ni Imam. Tawala za Aal-Idris, Alawiyun wa Tabarstan, Aal-Buweih, Zaydiyyah wa Yemen, Fatimiyyah, Ismailiyyah, Sarbdaran wa Sabzevar, Safawiyyah na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilikuwa tawala za Kishia katika ulimwengu wa Kiislamu. Nchini Iran hadi leo kuna utawala wa Kishia.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha utafiti cha masuala ya kidini na maisha cha Pew (Pew Research Center) cha Marekani ni kwamba, Mashia wanaunda asilimia 10 hadi 13 ya Waislamu wote duniani. Idadi ya Mashia inakadiriwa kuwa baina ya milioni 154 hadi 200. Akthari ya Mashia wanaishi katika nchi za Iran, Pakistan na Iraq.

Utambulisho

Mashia ni jina la kundi la Waislamu ambao ni wafuasi wa Imam Ali (a.s) na watu ambao wanaamini kwamba, Mtume (s.a.w.w) alimtangaza Imam Ali (a.s) kuwa kiongozi na mtu atakayemrithi mara tu baada ya yeye kuaga dunia na kurejea kwa Mola wake. [1] Sheikh Mufid anaamini kuwa, wakati neno Shia linapokuwa na limeambatana na alif na laam (al-Shiah) katika hali hiyo huitwa na kurejea tu kwa wafuasi wa Imam Ali (a.s) ambao wanaamini juu ya Wilaya (uongozi) na Uimamu baada tu ya Mtume (yaani bila kuchelewa). [2] Mkabala na wao Ahlu-Sunna wanasema, Mtume (s.a.w.w) hakumteua na kumuainisha mrithi na kiongozi baada yake na kutokana na ijma'a ya Waislamu katika kumpa baina na kiapo cha utii Abu Bakr, basi yeye ndiye kiongozi na mrithi wa Mtume. [3]

Rasul Ja’afariyan, mtafiti wa historia wa Kishia anasema kuwa, karne kadhaa baada ya kudhihiri Uislamu wafuasi na wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s) na watu waliokuwa wakimtanguliza Imam Ali (a.s) na Othman (khalifa wa tatu), walikuwa wakiitwa kwa jina la Shia. [4] Hawa walikuwa mkabala wa kundi la kwanza yaani Shia wa kiitikadi na kundi hili la pili lilijulikana kwa jina la Shia wa kupenda. [5] Shia kilugha ina maana ya ufuasi, kusaidia na kundi. [6]

Historia ya kutokea kwake

Kuna maoni tofauti kuhusu historia ya kutokea na kuibuka Ushia; miongoni mwayo ni: Kuweko Ushia tangu enzi za uhai wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w), baada ya tukio la Saqifah, baada ya kuuawa Othman, na baada ya tukio la kihistoria katika vita vya Siffin (La hukm illa Lilahi), zimetajwa kuwa ni tarehe za kuibuka na kuzaliwa Ushia. [7]

Baadhi ya wanachuoni wa Kishia wanaamini kwamba tangu wakati wa uhai wa Mtume wa Uislamu, baadhi ya masahaba walikuwa karibu na mhimili wa Hadhrat Ali (a.s) na kwamba Shia walikuwepo wakati huo huo. [8] Ili kuthibitisha hilo wanatumia hadithi [9] na ripoti mbalimbali za kihistoria [10] ambazo kwa mujibu wazo katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) Mashia wa Ali walibashiriwa au kuna watu walikuwa wakiitwa kwa jina la Mashia (wafuasi) wa Ali. [11] Kundi hili baada ya kuaga dunia Bwana Mtume, lililalamikia uamuzi wa Baraza la Saqifa lililomchagua Abu Bakr kuwa Khalifa na likakataa kumpa baia na kiapo cha utii kwa anuani ya Khalifa. [12]

Kwa mujibu wa Nashi Akbar katika kitabu cha Masail al-Imamah, Shia wa kiitikadi (mkabala wa Shia wa kiupendo) walikuweko tangu zama za Ali bin Abi Talib (a.s). [13]

Matumizi rasmi ya neno Shia kwa wafuasi wa Amirul-Mu'minin (a.s) na Mtume mwenyewe ni uthibitisho mwingine kwamba Ushia unarudi nyuma hadi mwanzo wa Uislamu. Kwa maana kwamba, Ushia ulikuweko tangu zama za Mtume. Barua ambayo Amirul Muminina (a.s) aliyoiandika baada ya kurejea kutoka Nahrwan kufuatia baadhi ya maswali kuhusu baadhi ya watawala waliomtangulia, inawaita wafuasi wake kwa jina la Shia na anatumia Aya kutoka kwenye Qur'an kuhusu suala hili. Anasema:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Kutoka kwa mja wa Mwenyezi Mungu, Ali Amirul-Muuminin, kwenda kwa Mashia wake. Kutoka kwa waumini kwenda kwa Waislamu. Hakika Mwenyezi Mungu anasema: وَإِنَّ مِنْ شِیعَتِهِ لَإِبْرَاهِیمَ ; Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake (katika Shia wake), (Surat Safat Aya 83). Na hapana shaka kuwa, kwamba, Ibrahim alikuwa miongoni mwa wafuasi wa Nuhu.

"Shia" ni jina ambalo Mwenyezi Mungu amelifanya kuwa kubwa (amelitukuza) katika kitabu chake, na nyinyi ni Shia wa Muhammad (s.a.w.w), kama ambavyo Muhammad alikuwa ni Shia wa Ibrahim, na jina hili halikuwekwa kwa mtu maalumu, na matumizi yake si uzushi. [14]

Nadharia ya Uimamu

Makala asili: Uimamu

Mtazamo wa Mashia kuhusiana na Uimamu una upande wa ushirikiano na makundi ya Kishia. [15] Uimamu una nafasi muhimu sana na ya kimhimili katika mijadala ya kitheolojia ya Shia. [16] Kwa mujibu wa Mashia, Imamu ndiye marejeo ya juu kabisa yaa tafsiri ya hukumu za kidini baada ya Mtume. [17] Katika hadithi

zilizopokewa na Mashia, nafsi na daraja ya Imam iko kwa namna ambayo kama mtu ataaga dunia bila ya kumtambua na kumfahamu Imam wake, atakuwa amefariki kafiri. [18] Madhumuni haya yamenukuliwa pia katika vyanzo vyenye itibari vya Ahlu-Sunna. Kwa mfano: Imekuja katika sherhe ya al-Maqasid Saad al-Din Taftazani, Musnad Ahmd bin Dawud, Musnad Ahmad bin Hanbal, Sahih Muslim n.k. [19]

Mtuyme (s.a.w.w) amesema: {من مات ولم يعرف إمام زمانه مات ميتة جاهلية ; Yeyoye yule atakayekufa bila kumtambua na kumjua Imam wa zama zake, basi mtu huyo atakuwa amekufa kifo kijahili (yaani atakufa kifo cha ukafiri)}. Taftazani, Sherh al-Maqasid, Juz. 5, uk. 239.

Mashia wanaamini kwamba, Uimamu ni katika misingi ya kiitikadi ya dini na ni cheo cha Kiungu; yaani Mitume hawawezi kukabidhi watu suala la kumchagua Imam. Kwa maana kwamba, Imam anachaguliwa na Mwenyezi Mungu. Na ni wajibu kwao kama Mitume kumuainisha mrithi wao. [20] Kwa msingi huo, wanatheolojia wa Kishia (ukiacha Zaydiyyah) [21], wanasisitiza juu ya ulazima wa kuteuliwa Imam (na Mtume au na Imam wa kabla yake), [22] na wanatambua kuwa, Nass na andiko (neno au kitendo kinachobainisha na kuweka wazi maana iliyokusudiwa) [23] ndio njia pekee ya kumtambua Imam. [24]

Hoja yao ni kwamba, Imam lazima awe maasumu na ni Mwenyezi Mungu tu ndiye Mwenye kutambua umaasumu wa watu; [25] kwani umaasumu ni sifa ya ndani na haiwezekani kufahamu na kudiriki umaasumu wao kupitia hali ya kidhahiri. [26] Kwa msingi huo, kuna udharura wa Mwenyezi Mungu kuianisha Imam, na Imam huyo kutambulishwa kwa watu kupitia kkwa Mtume. [27]

Katika vitabu vya kiitikadi (kitheolojia) vya Kishia kumezungumziwa na kujadiliwa suala la udharura wa uwepo wa Imam katika jamii na kumenukuliwa hoja za kinakili na kiakili. [28] Aya ya Ulul- Amr na hadithi ya Man maata (atakayekufa hali ya kuwa si mwenye kumjua Imam wa zama zake…) ni miongoni mwa hoja za kinakili za Mashia za kuonyesha ulazima wa uwepo wa Imam. [29] Kwa kutumia pia qaidat lutf (kanuni ya ukarimu) nayo ni katika hoja zao za kiakili. Katika kubainisha hoja hii imeandikwa: Kwa upande mmoja, kuwepo kwa Imam kunawafanya watu wamtii Mungu zaidi na kuelekea kwa uchache upande wa madhambi, na kwa upande mwingine, kwa mujibu wa kanuni ya ukarimu, ni wajibu kwa Mwenyezi Mungu kufanya kila jambo ambalo linasababisha kitu kama hiki; kwa muktadha huo, uteuzi wa Imam kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni jambo la wajibu. [30]

Umaasumu wa Imam

Makala kuu: Umaasumu wa Maimamu

Umaasumu wa Maimamu ni miongoni mwa masharti ya Uimamu katika mtazamo wa Mashia Ithaashariyyah na ni katika itikadi zao za kimsingi. [31] Kwa mujibu wa nukuu ya Allama Majlisi ni kuwa, Mashia Imamiyyah wameafikiana kwamba, Maimamu (a.s) wana kinga na umaasumu wa kutofanya madhambi yote makubwa kwa madogo, iwe ni kwa makusudi au kwa kusahau na katu sio wenye kufanya kosa. Inaelezwa kuwa, Shia Ismailiyyah nao wanatambua umaasumu kama sharti la Uimamu. Ili kuthibitisha hilo wanatumia hoja za kinakili na kiakili [32] ambapo Aya za Ulul-Amr, [33], Aya ya Ibtilaa (majaribu) Ibrahim [34] na hadithi ya Thaqalayn [35].

Mashia wote wanaamini umaasumu wa Maimamu isipokuwa kundi la Zaydiyyah lenyewe haliamini umaasumu wa Maimamu. Kwa mujibu wa itikadi yao ni kwamba, Ahlul-Kisaa (Kishamia) yaani Mtume (s.a.w.w), Ali (a.s), Fatma (a.s), Hassan na Hussein (a.s) ndio maasumu (wasiotenda dhambi), [36] ama Maimamu wengine waliobakia ni kama watu wengine wanafanya makosa na hawana kinga ya umaasumu ya kutofanya dhambi. [37]

Kiongozi baada ya Mtume (s.a.w.w)

Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, Mtume (s.a.w.w) alimtambulisha na kumtangaza kwa watu Imam Ali (a.s) kuwa mrithi na kiongozi baada yake na alilitambua suala la Uimamu kwamba, ni haki ya Imam Ali (a.s) na watoto wake. [38] Hata hivyo kundi la Mashia Zaydiyyah lenyewe limeukubali uongozi na Uimamu wa Abu Bakr na Omar; ingawa hawa hawa Zaydiyyah pia wanaamini kwamba, Imam Ali (a.s) ni mbora zaidi ya wawili hao na wanasema kuwa, “Waislamu walifanya kosa kumchagua Omar na Abu Bakr kuwa Maimamu. Hata hivyo kwa kuwa Imam Ali aliridhia hilo, sisi tunaukubali Uimamu wa wawili hao (Abu Bakr na Omar). [39]

Wanatheolojia wa Kishia wakiwa na lengo la kuthibitisha uongozi wa Uongozi wa Imam Ali (a.s) baada tu ya Mtume, wanatumia Aya na hadithi kama hoja ya hilo na miongoni mwazo ni Aya ya Wilaya (Hakika walii wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukui), hadithi ya Ghadir (Yule ambaye mimi kwake ni kiongozi basi na huyu Ali ni kiongozi wake) na hadithi ya manzila, yaani daraja. (Mtume (s.a.w.w) alimhutubu Imam Ali (a.s) akisema: Wewe kwangu daraja yako ni mithili ya Harun kwa Mussa; kwa tofauti hii kwamba, baada yangu hakuna tena Mtume. [40]

Makundi ya Kishia

Makala kuu: Makundi ya Kishia

Makundi mashuhuri na muhimu ya Kishia ni Imamiyyah, Zaydiyyah, Ismailiyyah, Maghulati, Kaisaniyyah na kwa kiwango fulani kundi la Waqifiyyah. [41] Haya yanatambuliwa kama makundi mashuhuri na muhimu zaidi ya Kishia. Baadhi makundi haya yenyewe yana matawi pia; kama Mashia Zaydiyyah ambao matawi yao yametajwa kuwa yanafika mpaka kumi, [42] na Kaisaniyah wamegawanyikka katika makundi manne. [43] Hili ndilo lililopelekea makundi mbalimbali yatajwe kuwa ni katika makundi ya Kishia. [44] Hata hivyo kuna makundi mengi ya Kishia ambayo yamemalizika na kutokomea (hayapo tena), na hii leo ni makundi matatu tu ya Kishia ambayo yako hai na yana wafuasi ambayo ni, Imamiyyah, Zaydiyyah na Ismailiyyah. [45]

Kaisaniyyah walikuwa wafuasi wa Muhammad Hanafiyyah. Baada ya Imam Ali (a.s), Imam Hassan (a.s) na Imam Hussein (a.s), wao walimtambua Muhammad bin Hanafiyyah mtoto mwingine wa Imam Ali (a.s) kuwa ndiye Imam. Walikuwa wakiamini kwamba, Muhammad bin Hanafiyyah hajafa na kwamba, ndiye Mahdi Muahidiwa na yupo katika Mlima Radhwa. [46]

Waqifiyyah ni kundi ambalo liliishia kwa Uimamu wa Imam Kadhim (a.s); kwa maana kwamba, baada ya kufa shahidi Imam Mussa al-Kadhim (a.s), kundi hili halikuamini juu ya kuweko Imam mwingine, bali lilimtambua Imam Kadhim kuwa ndiye Imam wa mwisho. [47]

Maghulati hili nalo ni kundi ambalo lilichupa mipaka kuhusiana na nafasi na daraja ya Maimamu; kwa maana kwamba, lilikuwa likiamini kwamba, Maimamu wana sifa ya uungu. Maghulati hawakuwa wakiwatambua Maimamu kwamba, ni viumbe na walikuwa wakiwashabihisha na kuwafananisha na Mwenyezi Mungu. [48]

Shia Ithnaashariyyah

Makala asili: Imamiyyah

Shia Ithnaashariyyah au Mashia wa Maimamu kumi na mbili ndilo kundi kubwa zaidi miongoni mwa makundi ya Kishia. [49] Kwa mujibu wa madhehebu ya Imamiyyah, baada ya Mtume (s.a.w.w) kuna Maimamu kumi na mbili ambao wa kwanza wao ni Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) na wa mwisho wao ni Imam Mahdi (a.t.f.s), [50] ambaye angali hai, yuko ghaiba (haonekani katika upeo wa macho ya watu) na atakuja kudhihiri siku moja kwa idhini ya Mwenyezi Mungu aje kujaza dunia uadilifu na usawa. [51]

Raja’a (ufufuo) na Badaa (utokezo) ni katika itikadi maalumu za Shia Ithnaashariyyah. [52] Kwa mujibu wa mafundisho ya Raj’a, baada ya kudhihiri Imam Mahdi, baadhi ya wafu watafufuliwa. Wafu hawa wanajumuisha watenda mema miongoni mwa Mashia na maadui wa Ahlul-Bayt (a.s) ambao watapata adhabu ya matendo yao hapa hapa duniani. [53]

Badaa (ufunuo) maana yake ni kwamba, Mwenyezi Mungu kutokana na maslahi anayoyajua, atalibadilisha jambo ambalo alishalidhihirisha kwa Mtume au Imam na kuweka jambo jingine badala yake. [54]

Miongoni mwa wasomi na wanazuoni mahiri na watajika wa theolojia wa Kishia ni: Sheikh Mufid (236 au 238 – 413 Hijria), Sheikh Tusi (385 – 460 Hijria), Khwajah Nasir al-Din al-Tusi (598 – 672 Hijiria) na Allama Hilli (648 – 726 Hijiria). [55] Aidha wanazuoni mahiri wa fiq’h (mafakihi) wa Imamiyyah ni: Sheikh Tusi, Muhaqqiq Hilli, Allama Hilli, Shahid al-Awwal, Shahid Thani, Kashif al-Ghitaa, Mirza Qomi na Sheikh Murtadha Ansari. [56]

Idadi kubwa ya Mashia Ithnaashariyyah wanapatikana nchini Iran ambapo wanaunda asilimia 90 ya jamii ya nchi hiyo. [57]

Zaydiyyah

Makala asili: Zaydiyyah

Madhehebu ya Zaydiyyah inanasibishwa na Zayd mtoto wa Imam Sajjad (a.s). [58] Kwa mujibu wa misingi ya madhehebu haya ni kwamba, Imam Ali (a.s), Hassan (a.s) na Hussein (a.s) ndio walioteuliwa na Mtume (s.a.w.w). [59] Ghairi ya Maimamu hawa watatu, kila ambaye anatokana na kizazi cha bibi Fatma Zahraa (a.s) na akaanzisha harakati na mapinduzi, akawa ni alimu, msomi, mwenye kuipa mgongo dunia, shujaa na mkarimu basi ni Imam. [60].

Kuhusiana na Uimamu wa Abu Bakr na Omar, Shia Zaydiyyah wana misimamo miwili: Baadhi yao wanaamini Uimamu wa wawili hawa na baadhi ya wengi hawakubaliani na Uimamu wao. [61] Mtazamo wa leo wa Mashia Zaydiyyah wa Yemen unakaribiana na mtazamo wa kwanza. [61]

Jarudiyah, Salihiyah na Suleimaniyah yalikuwa makundi matatu makuu ya madhehebu ya Zaydiyyah. [62] Kwa mujibu wa Shahristani, mwandishi wa kitabu cha al-Milal Wanihal, Mazaydiyyah wengi wameathirika na Mu’tazilah katika theolojia na katika fiq’h wameathirika na madhehebu ya Hanafi, moja kati ya madhehebu nne za Kifq’h za Ahlu-Sunna. [63] Kwa mujibu wa kitabu cha Atlas Shiah, Zaydiyyah wanaunda asilimia 35-40 ya wakazi milioni 20 nchini Yemen. [64]

Ismailiyyah

Makala kuu: Ismailiyyah

Ismailiyyah ni kundi miongoni mwa makundi ya Kishia ambalo baada ya Imam Swadiq (a.s) linaamini Uimamu wa mtoto wa wake mkubwa Ismail na baada ya hapo Imam Kadhim (a.s) na hawakubali Maimamu wengine wa Imamiyyah. [65] Ismailiyyah walikuwa wakiamini kwamba, Uimamu una duru na vipindi saba na kila duru huanza kwa Natiq (mtu ambaye hutambulika kama Mtume) ambaye huleta sheria mpya na kila kipindi baada yake Maimamu saba huongoza. [66]

Wajumbe (Mitume) wa duru sita za kwanza za Uimamu ambao ni Mitume wa Ulul-Azm ambao ni: Adam, Nuhu, Ibrahim, Mussa, Issa, na Mtume Muhammad (s.a.w.w). [67] Muhammad Maktum mtoto wa Ismail, ni Imam wa saba katika duru ya sita ya Uimamu ambayo ilianza na Mtume (s.a.w.w). Yeye ndiye Mahdi Muahdiwa ambapo wakati atakapoanzisha harakati na mapinduzi, atakuwa mjumbe (Mtume) wa duru ya saba ya Uimamu. [68] Inaelezwa kuwa, baadhi ya mafundisho haya yalifanyiwa mabadiliko katika kipindi na zama za utawala wa Fatimiyyah. [69]

Sifa muhimu na maalumu ya Ismailiyyah ni muelekeo wa kibatini; kwani wao wanafanyia taawili Aya za Qur’an, hadithi, maarifa na hukumu za Kiislamu na huja na maana ambayo ni kinyume na dhahiri yake. Kwa mujibu wa itikadi yao, Aya za Qur’an na hadithi zina dhahiri na batini. Wanamtambua Imam kuwa ni batini wao, na falsafa ya Uimamu ni mafundisho ya kibatini ya dini na kubainisha maarifa ya kibatini. [70]

Qadhi Nu’man, ametambuliwa kuwa, fakihi mkubwa zaidi wa Ismailiyyah [71] na kitabu chake cha Da'aim al-Islam kinafahamika kuwa, chanzo kikuu cha fiq’h cha madhehebu haya. [71] Abu Hatim Razi, Nassir Khosrow na kundi lililojulikana kwa jina la Ikhwan al-Saffa nao wanahesabiwa kuwa miongoni mwa wanafikra mahiri wa Ismailiyyah. [72] Rasail Ikhwan al-Saffa na a’lam al-Nub’wah kilichoandikwa na Abu Hatim al-Razi ni miongoni mwa vitabu vyao muhimu vya kifalsafa. [73]

Hii leo Ismailiyyah wanagawanyika katika makundi mawili ya Aga Khan na Bohora ambayo ni mabaki ya matawi mawili ya Fatimiyah wa Misri ya Nazariyah na Mustaalawiyah. [74] Kundi la kwanza linatambuliwa kuwa na wafuasi wapatao milioni moja ambao kawaida wanaishi katika mataifa ya India, Pakistan, Afghanistan na Iran. [75] Idadi ya kundi la pili nalo ambalo linakadiriwa kuwa na wafuasi takribani 500,000 zaidi ya asilimia 80 kati yao wanaishi nchini India. [76]

Itikadi ya Umahdi

Makala asili: Umahdi

Itikadi ya Umahdi ni mafundisho ya pamoja baina ya madhehebu zote za Kiislamu; [77] lakini fikra hii ina nafasi maalumu katika madhehebu ya Shia na kumekuja maelezo mengi katika hadithi, vitabu na makala nyingi kuhusiana na maudhui hii. [78]

Makundi ya Kishia licha ya kushirikiana katika suala la asili ya uwepo wa Mahdi yanatofautiana katika mambo ya kina na vielelezo vyake. Shia Ithnaashariyah wanaamini kwamba, Mahdi ni mtoto wa Imam Hassan Askary (a.s), ni Imam wa Kumi na Mbili na ndiye yule Mahdi Muahidiwa (a.t.f.s) na kwa sasa yuko ghaiba (haonekani katika upeo wa macho ya watu). [79] Ismailiyyah wao wanamtambua Muhammad Maktum mtoto wa Ismail ambaye naye ni mtoto wa Imam Swadiq (a.s) kwamba, ndiye Mahdi Muahidiwa (a.t.f.s). [80] Zaydiyyah wao kutokana na kuwa, wanaamini kwamba, kuanzisha harakati na mapinduzi ni sharti la Uimamu, hawana itikadi na intidhar (kusubiri faraja na kudhihiri Imam Mahdi) na ghaiba. [81] Wao wanamchukulia kila Imam kuwa ni Mahdi na mwokozi. [82]

Mitazamo Mingine Muhimu ya Kiteolojia

Mashia sambamba na kushirikiana na Waislamu wengine katika masuala la Misingi ya Dini yaani Tawhidi, Utume na Ufufuo, wana itikadi ambazo zinawatofautisha na Ahlu-Sunna wote au baadhi yao.

Itikadi hizo mbali na masuala mawili ya Uimamu na itikadi ya Umahdi ni: Uzuri na ubaya wa kiakili, upambanuzi wa sifa za Mwenyezi Mungu, jambo baina ya mambo mawili (katika suala la Jabr –kulazimishwa- na watafwidh-kuachiwa uhuru kamili usio na mipaka), masahaba wote sio waadilifu, taqiya, tawassuli, na uombezi (shafaa).

Maulamaa wa Kishia kama lilivyo kundi la Mu'tazila wanaona kuwa, uzuri na ubaya ni jambo la kiakili (ni jambo la akili kuainisha kwamba, hili ni baya au zuri). [83] Uzuri na ubaya kuwa ni jambo la kiakili maana yake ni kuwa, matendo licha ya kuwa hakuna shaka kuhusiana na kwamba, Mwenyezi Mungu amehukumu kuwa jambo fulani ni baya na jambo fulani ni zuri, kwa upande wa kiakili linagawanywa katika makundi mawili ya baya na uzuri. [84] Maneno haya ni kinyume na mtazamo wa Asha'irah ambao wao wanaona kuwa, uzuri na ubaya ni jambo la kisheria; [85] wao wanasema kuwa, ubaya na uzuri ni mambo ambayo hayana uwepo wa kiuhalisia bali ni kitu cha kiitibari na kujaalia tu; hivyo basi kila ambacho Mwenyezi Mungu amekiamrisha ni kizuri na kila ambacho amekikataza ni kibaya. [86]

Fiq'h

Makala asili: Fiq'h

Qur'an na Sunna za Mtume (s.a.w.w) kwa Mashia vinahesabiwa kuwa vyanzo viwili vikuu na vyenye itibari vya Hukumu za Kisheria. [103]; lakini wana mitazamo tofauti kuhusiana na namna ya kutumia vyanzo viwili hivi na vilevile vyanzo vingine vya Fiq'h.

Mashia wengi, yaani Imamiyyah na Zaydiyyah kama ilivyo kwa Ahlu-Sunna, mbali na Qur'an na Sunna za Mtume, wanatambua akili na ijma'a kwamba, navyo ni hoja; [104] lakini Ismailiyyah wao hawana mtazamo kama huu. Kwa msingi huo, katikka madhehebu ya Ismailiyyah, haijuzu kufuata (kufanya taqlidi) kwa Mujtahidi yeyote na hukumu za kisheria zinapaswa kuchukuliwa moja kwa moja kutoka katika Qur'an, Sunna za Mtume na mafundisho ya Maimamu. [105]

Kundi la Zaydiyyah lenyewe linaamini kuhusiana na Sunna kwamba, kauli na kitendo cha Mtume tu ndio hoja na linarejea katika vyanzo vya hadithi vya Ahlu-Suuna kama Sahihi Sita (Sihah Sitta); [106] lakini Shia Imamiyyah na Ismailiyah hadithi ambazo zinmenukuliwa na kutoka kwa Maimamu wao wanazihesabu kuwa ni vyanzo vya Fiq'h. [107]

Kadhalika Shia Zaydiyyah kama walivyo Ahlu-Sunna nao wanatambua kwamba, kutumia Qiyas (kukisia) kwa maana ya kulinganisha jambo ambalo halikutajwa katika hukumu na jingine lililotajwa kutokana na kuwa na sababu moja na istihsan (kuchukulia kuwa ni vizuri) ni hoja; [108] hata hivyo mambo haya mawili hayana itibari yoyote kwa Mashia Imamiyyah na Ismailiyah. [109] Hata hivyo Zaydiyyah katika baaadhi ya hukumu zenye hitilafu baina ya Imamiyyah na Ahlu-Sunna wamechagua fat'wa ya Mashia; miongoni mwayo ni: Kinyume naa Ahlu-Sunna, wao wanaitambua ibara ya Ḥayy-a ʿalā khayr al-ʿamal kwamba, ni sehemu ya adhana na wanaona kuwa ni haramu kusema katika adhana ibara ya " al-Swalata Khairu min naum (Swala ni bora kuliko usingizi). [110]

Kuhusiana na ndoa ya Mutaa (muda) ambayo ni katika mambo wanayohitalifiana Waislamu wa Kisuni na Kishia, madhehebu ya Ismailiyyah na Zayidiyyah wanaafikiana na Masuni katika hili; [111] kwa maana kwamba, kinyume na Shia Imamiyyaah ambao wao wanaitambua ndoa ya Mutaa kuwa ni halali na yenye kujuzu kuifanya, wao wameiharamisha. [112].

Idadi na mgawanyiko wa kijiografia

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2014, Mashia walikuwa wakiunda zaidi ya asilimia 50 katika mataifa ya Iran, Azerbaijan, Bahrain, Iraq na Lebanon.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha utafiti cha masuala ya kidini na maisha cha Pew (Pew Research Center) cha Marekani ni kwamba, Mashia wanaunda asilimia 10 hadi 13 ya Waislamu wote duniani. [114] Hata hivyo, baadhi wanasema kuwa, takwimu hizo haziakisi uhalisia wa mambo na kwamba, idadi halisi ya Mashia duniani ni zaidili ya milioni 300 yaani asilimia 19 ya Waislamu wote ulimwenguni. [115] Takwimu za asasi hiyo zinaonyesha kuwa, asilimia 68-80 ya Mashia duniani wanaishi katika nne za Iran, Pakistan, Iraq na India. Iran ina Mashia milioni 66 hadi 70 ambao ni sawa na asilimia 37-40- ya Mashia wote ulimwenguni. Katika nchi tatu za India, Pakistan na Iraq kuna Mashia zaidi ya milioni 16 wanaoishi katika kila nchi moja kati ya nchi hizo. [116]

Katika nchi za Iran, Azerbaijan, Bahrain na Iraq wakazi wake wengi ni Mashia. [117]. Katika eneo la Masharikli ya Kati, Kaskazini mwa Afrika, Asia-Oceania, Marekani, Canada [118] na China [119] kuna Mashia pia wanaoishi katika maeneo hayo.

Tawala

Tawala za Aal-Idris, Alawiyun wa Tabarstan, Aal-Buweih, Zaydiyyah wa Yemen, Fatimiyyah, Ismailiyyah, Sarbdaran wa Sabzewar, Safawiyyah na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilikuwa tawala za Kishia katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hadi leo nchini Iran kuna utawala wa Kishia. Utawala wa Aal Idris ulikuwa ukitawala huko Morocco na baadhi ya maeneo ya Algeria, [120] na ulihesabiwa kuwa utawala wa kwanza kuundwa na Mashia. [121] Utawala huu uliundwa mwaka 172 Hijiria na Idris mjukuu wa Imam Hassan Mujtaba (a.s) na ulidumu kwa takribani karne mbili. [122] Utawala wa Alawiyan ulikuwa wa Mashia Zaydiyyah. [123] Kadhalika Shia Zaydiyyah kuanzia mwaka 284-382 walikuwa wakitawala huko Yemen. [124] Tawala za Fatimiyyah na Ismailiyyah Alamut zilikuwa na madhehebu ya Ismailiyah. [125] Kuhusiana na Aal-Buweih kuna hitilafu za kimitazamo. Baadhi yao wanawatambua kama wafuasi wa madhehebu ya Zaydiyyah na wengine wanawahesabu kuwa ni Shia Imamiyyah. Aidha kuna wanaoamini kwamba, awali Aal Buwaih ulikuwa mfuasi wa madhehebu ya Zaydiyyah na kisha baadaye ukawa mfuasi wa Imamiyyah. [126]

Sultan Mohammad Khodabande ambaye ni mashuhuri kama Uljaitu (aliyetawala (703-716 Hijiria) kwa kipindi fulani alitangaza madhehebu ya Shia Imamiyah kuwa dhehebu rasmi la serikali yake; lakini kutokana na mashinikizo ya muundo wa serikal, yake, ambayo ilijengeka juu ya msingi wa madhehebu ya Kisunni, alitangaza tena madhehebu ya Kisuni kuwa madhehebu rasmi ya utawala. [127]

Utawala wa Sarbdaran wa Sazbzevar nao unafahamika kuwa utawala wa Kishia. [128] Hata hivyo kwa mujibu wa Rasul Ja'fariyan, mwandishi na mtafiti wa masuala ya kihistoria ni kwamba, madhehebu ya viongozi na watawala wa Sarbdaran hayafahamiki; hata hivyo inaeleweka wazi kwamba, viongozi wao wa kidini walikuwa Masufi wenye mielekeo ya Kishia. [129] Khoja Ali Muayyid mtawala wa mwisho wa Sarbdaran [130] aliyatangaza madhehebu ya Imamiyyah kuwa madhehebu rasmi ya utawala wake. [131]

Katika utawala wa Safavi ambao uliasisiwa 907 Hijiria na Shah Ismail, madhehebu ya Shia Imamiyyah yalitambuliwa rasmi. [132] Utawala huu ulieneza madhehebu ya Shia Imamiya katika taifa la Iran na ukaibadilisha nchi na kuifanya kuwa ya Kishia kikamilifu. [133].

Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia misingi ya madhehebu na Fiq'h ya Shia Ithnaashariyaa imefanywa kuwa msingi na nguzo. [134]