Hukumu za kisheria

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Hukumu za Kisheria)

Hukumu za kisheria (Kiarabu: الأحكام الشرعية) ni kanuni na sheria zinazohusiana na wadhifa na majukumu ya mwanadamu. Hukumu za kisheria zinagawanyika katika sehemu mbili ambazo ni: Hukumu taklifi na wadh'i. Hukumu za taklifi zinabainisha moja kwa moja wadhifa na majukumu ya mwanadamu; kama vile hukumu ya kwamba, anapaswa kuswali au hapaswi kunywa pombe na kadhalika. Ama kwa upande wa hukm wadh'i ni zile ambazo zina uhusiano usio wa moja kwa moja na wadhifa na majukumu ya mwanadamu; kama vile kuswali na nguo yenye najisi kunabatilisha Swala. Hukumu za kisheria zinapatikana kupitia adilat shar'ii (vyanzo vinavyotumika kwa ajili ya kunyambua na kupata hukumu ya jambo fulani) ambavyo ni Qur'ani, hadithi, akili na ij'maa (mwafaka wa wanazuoni). Mtu ambaye ana uwezo (wa kielimu) wa kunyambuua hukumu kutoka katika vyanzo hivi anafahamika kwa jina la Mujtahidi. Hii leo hukumu za kisheria zinapatikana katika vitabu vya sheria za Kiislamu (majimui ya fat'wa kuhusiana na masuala mbalimbali) ambavyo vinabainisha fat'wa, nadharia na mitazamo ya Marajii Taqlidi kuhusiana na hukumu mbalimbali. Kwa mujibu wa fat’wa za Marajii Taqlidi, ni wajibu kwa mukalafuu kujifunza hukumu za kisheria ambazo aghalabu anakumbana nazo katika maisha yake ya kila siku kama Swala, Saumu na kadhalika.

Maana ya kifikihi na mgawanyiko wake

Kanuni za dini ambazo zina uhusiano na wadhifa na jukumu la mwanadamu zinafahamika kwa jina la Hukumu za Kisheria;[1] kama vile wajibu wa Swala, wajibu wa Swaumu, uharamu wa kunywa pombe na masharti yaliyobainisha kuhusiana na kusihi ndoa, kuuza na kununua na kadhalika.[2]

Aina za hukumu za kisheria

Mafakihi (wanazuoni waliobobea katika elimu ya fikihi) wamegawanya hukumu za kisheria katika makundi kadhaa. Miongoni mwayo ni:

  • Hukumu taklifi na wadh'i
  • Hukumu awla na thanawi
  • Hukumu Waq'i na Dhahiri
  • Hukumu Mawlawi na irshadi
  • Hukumu taasisi na imdhai[3]

Hukumu Taklifi na Wadh'i

Makala asili: Hukumu Taklifi na Hukumu Wadh'i

Hukumu Taklifi ni ile ambayo inabainisha moja kwa moja jukumu la mwanadamu kuhusiana na jambo au maudhui fulani; kwa mfano inamtaka mja kutekeleza ibada ya Swala au inamkataza kunywa pombe. [4] Hukumu taklif imegawanyika katika sehemu tano: Wajibu, mustahabu, haramu, makuruhu na mubaha[5]( jambo ambalo inajuzu mtu kutenda au kuacha hakuna thawabu ndani yake wala dhambi). Hukumu hizi zinafahamika kwa pia kwa jina la Hukumu Tano. [6]

Ama hukumu wadh'i haibainishi moja kwa moja amri au maagizo; bali kwa mfano inabainisha masharti ya kusihi amali au jambo fulani;[7] kwa mfano, hukumu hii kwamba, Swala inayoswaliwa kwa nguo yenye najisi ni batili. Hukumu wadh'i zina uhusiano usio wa moja kwa moja na majukumu ya mwanadamu. Kwa mfano hukumu za ndoa ni hukumu wadh'i ambazo zinabainisha tu mazingira na masharti ya kusihi ndoa; lakini baada ya ndoa, kila mmoja yaani mke na mume ana wadhifa na majukumu kwa mwenzake ambayo anapaswa kuyatekeleza ambapo majukumu hayo ni hukumu taklifi. [9]

Hukumu ya Awli na Thanawi

Makala asili: Hukumu ya awli na hukumu ya thanawi

Hukumu awaliya au awla ni zile hukumu ambazo katika mazingira ya kawaida ziko katika mabega na jukumu la mwanadamu; kama vile wajibu wa kuswali Swala ya Alfajri na kuharamishwa kunywa pombe. Hukm thanawi ni hukumu ambayo inafanyika wakati wa dharura au kulazimishwa. Kama vile kuruhusiwa kutofunga Swaumu kwa mtu ambaye Swaumu inahatarisha afya na uzima wake au watu ambao wamelazimishwa kula na kufungua Swaumu. [10]

Hukumu Taasisi na Imdhai

Makala asili: Hukumu Taasisi na Hukumu Imdhai

Hukumu taasisi ni hukumu ambayo kwa mara ya kwanza imeletwa katika Uislamu. [11] na hukumu Imdhai ni hukumu na sheria ambayo ilikuweko kabla ya Uislamu na baada ya Uislamu kuja ukaiidhinisha na kuikubali. [12]

Hoja za hukumu za kisheria

Makala ya asili: Adilat al-Ar'ba'

Hukumu za sheria zinapatikana kupitia msaada wa elimu mbalimbali kama Diraya (kuchunguza sanadi na mapokezi ya hadithi), Rijaal (kuchunguza sifa na hali za wapokeaji wa hadithi na kubainisha misingi na kanuni zake), Usulul Fiqhi na fiqh. [13] Mafaqihi wakiwa na lengo la kunyambua hukumu za masuala mbalimbali yaani hukumu za kisheria hurejea katika vyanzo vinne: Qur'ani, sunna, akili na ijmaa (mwafaka wa wanazuoni) ambavyo vinajulikana kwa jina la al-Adilah al-Ar'ba (Hoja nne) [14]. Makusudio ya sunna ni hadithi, ambayo kauli nn kitendo kilichonukuliwa kutoka kwa Maasumina. [15] Katika fikihi ya Ahlu-Sunna inatumiwa sunna za Mtume tu; lakini katika fikihi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia mbali na sunna za Mtume (s.a.w.w) zinarejewa pia sunna za Maimamu Maasumu. [16] Katika fiqihi ya Shia Ithnaasharia, Qur'an na hadithi za Maimamu Kumi na Mbili ni vyanzo viwili vikuu vya hukumu za kidini. [17]

Jukumu la kunyambua hukumu za kisheria kutoka vyanzo hivi liko mikononi mwa Mujtahidi. Mujtahidi ni mtu ambaye amefikia daraja ya Ijtihadi; yaani ana uwezo (wa kielimu) wa kunyambua hukumu za kisheria katika vyanzo vyake vikuu vinne. [18]

Wajibu wa kufahamu hukumu za kisheria

Kwa mujibu wa fat'wa za mafakihi ni kwamba, ni wajibu kujifunza hukumu za kisheria ambazo aghalabu tunakumbana nazo katika maisha yetu ya kila siku. [19] Kadhalika mtu anapaswa kuwa ima Mujtahidi ambapo yeye mwenye ananyambua hukumuu kutoka katika vyanzo vyake au amfuate Marjaa Taqlidi au kupitia njia ya ihtiyati (tahadhari) awe na yakini na hivyo aweze kutekeleza jukumu lake la kisheria; kwa mfano kama baadhi ya Mamujitahidi wanaamini jambo fulani ni haramu na wengine wamejuzisha, basi yeye asifanye jambo hilo, au amali ambayo baadhi ya Mamujitahidi wamesema ni wajibu na wengine wakasema inajuzu, basi yeye aifanye amali hiyo. [20]

Vitabu maalumu vya hukumu

Hii leo hukumu za kisheria zipo katika kalibu ya vitabu maalumu vinavyofahamika kama Taudhih ala-Masail (Ufafanuzi wa Mas'ala) au risala amaliya ambazo zimeandikwa na Marajii Taqlidi tofauti. [21]. Marjaa Taqlidi ni mtu ambaye wengine wanamkalidi na kumfuata; kwa maana kwamba, watu wanaomfuata wanafanya amali zao mbalimbali za kidini kwa mujibu wa mitazamo na nadharia zake za kifikihi (fat'wa) na fedha zao za malipo ya kisheria (Wujuhat Shar’i) kama Zaka, Khumsi na kadhalika wanampatia yeye au wawakilishi wake. [22]

Rejea

Vyanzo

  • Banī Hāshimī Khomeinī, Sayyid Muḥammad Ḥasan. Tawḍīḥ al-masāʾil-i marajiʿ. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī affiliated to Jāmiʿa-yi Mudarrisīn-i Ḥawza-yi ʿIlmīyya-yi Qom, 1424 AH.
  • Ḥusaynī Shīrāzī, Sayyid Muḥammad. Al-Wūṣūl ilā kifāyat al-uṣūl. Qom: Dār al-Ḥikma, 1426 AH.
  • Ḥakīm, Muḥammad Taqī. Al-Uṣūl al-al-ʿĀmma fī al-fiqh al-muqārin. Qom: Majmaʿ Jahānī Ahl al-Bayt (a), 1418 AH.
  • Muḥaqqiq Dāmād, Musṭafā. Qawāʿid-i fiqhī. Twelfth edition. Tehran: Markaz-i Nashr-i ʿUlūm-i Islāmī, 1406 AH.
  • Mishkinī, ʿAlī. Iṣṭilāhāt al-uṣūl wa muʿẓam abḥāthihā. Sixth edition. Qom: Al-Hādī, 1374 Sh.
  • Muẓaffar, Muḥammad Riḍā al-. Uṣūl al-fiqh. Fifth Edition. Qom: Intishārāt-i Islāmī, 1430 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Dāʾirat al-maʿārif-i fiqh-i muqārin. First edition. Qom: Madrisat Imām ʿAlī b. Abī Ṭālib, 1427 AH.
  • Raḥmān Sitāyish, Muḥammad Kāẓim. Taqlīd 1 in Dānishnāmah-yi Jahān Islām. 1st ed. Tehran: Bunyād-i Dāʾirat al-Maʿārif al-Islāmī, 1382 Sh.
  • Sajjādī, Sayyid Jaʿfar. Farhang-i ʿulūm, shāmil-i iṣṭilāhāt-i adabī, fiqhī, uṣūlī, maʿānī bayān wa dastūrī. Tehran: Muʾassisa Maṭbūʿātī ʿIlmī, 1344 Sh.
  • Ṣadr, Muḥammad Bāqir. Al-Maʿālim al-jadīda li-l-uṣūl. Second edition. Qom: Kungira-yi Shahīd Ṣadr, 1379 Sh.
  • Ṣadr, Muḥammad Bāqir. Durūs fī ʿilm al-uṣūl. Fifth Edition. Qom: Intishārāt-i Islāmī, 1418 AH.
  • Wilāyī, ʿĪsā. Farhang-i tashrīhī-yi iṣṭilāhāt-i uṣūl. Sixth edition. Tehran: Nashr-i Ney, 1387 Sh.