Ismail mtoto wa Imam Swadiq (a.s)

Kutoka wikishia

Ismail bin Ja’afar (aliaga dunia 143 au 145), ni mtoto mkubwa wa Imam Swadiq (a.s) ambapo kundi la Ismailiya linamtambua yeye au mwanawe Muhammad kwamba, ni Imam baada ya Imam Swadiq (a.s). Hata hivyo kwa mtazamo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithna’asharia na vile vile kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w), Mussa bin Ja’afar(a.s) ndiye Imam baada ya Imam Swadiq (a.s). Kuamini kwamba, Ismail ndiye Imam baada ya Imam Swadiq (a.s) ulikuwa mwanzo wa kujitenga Ismailiya na Shia Ithnaasharia na kuibuka kundi la Ismailiya.

Kuna hitilafu za kimitazamo kuhusiana na wasifu wa Ismail. Baadhi ya watu wakitumia na kujengea hoja hadithi wanaamini kuwa, Ismail alikuwa na uhusiano na maghulati (waliochupa mipaka katika dini hususan kuwatukuza kupita kiasi Maimamu na hata kuamini kwamba, ni Mitume na wana daraja ya Uungu. Hata hivyo Ayatullah Khui sambamba na kulalalisha hadithi hizo akitumia hadithi nyingine anamtambua kuwa, ni mtu mwenye shakhsia kubwa na mlengwa wa mapenzi ya baba.

Ismail aliaga dunia katika zama za uhai wa Imam Swadiq (a.s) na amezikwa katika makaburi ya Baqi'i. Imam Swadiq alisindikiza maiti yake na kufanya mazishi yake kwa uwazi kabisa ili kuondoa utata na tetesi za watu ambao hawakuwa wakiamini kifo chake na hata kuamini kwamba, atarejea.


Maisha na familia

Ismail ni mtoto wa Imam Swadiq (a.s) na Fatma mjukuu wa Imam Sajjad. [1] Hakujatajwa katika vitabu vya historia kuhusiana na tarehe ya kuzaliwa kwake. Pamoja na hayo kwa kutegemea kuzaliwa Imam Kadhim (a.s) mwaka 127 [2] au 128 Hijria [3] na hitilafu ya miaka 25 baina ya Imam Kadhim na Ismail, [4], mwaka wa kuzaliwa kwake unakadiriwa kwamba, ni miaka ya awali ya karne ya pili. [5] Ali ibn Muhammad Alawi Umri, ameutaja mwaka wa kuaga dunia Ismail kuwa ni 138 Hijiria. [6] Hii ni katika hali ambayo, Tabari, mwandishi wa kitabu cha Tarikh Tabari amesema kuwa, mpaka mwaka 140 Hijiria Ismail alikuwa hai. [7]

Imekuja katika kitabu hicho kwamba, miaka ya 143 [8] na 145 Hijiria [9] kuwa ni miaka aliyoaga dunia Ismail. Kizazi cha Ismail kiliendelea kupitia kwa watoto wake Muhammad na Ali. [10]Muhammad alikuwa na watoto wawili waliojulikana kwa majina ya Ismail Thani na Jafar Akbar [11] na kizazi cha Ali ibn Ismail nacho kilibakia kupitia kwa mtoto aliyejulikana kwa jina la Muhammad. [12] Wajukuu wa Ismail walikuwa wakiishi katika ardhi kama Khorasan, Neyshabour, Samarra, [13] Damascus, [14] Misri, [15] Ahwaz, Kufa, Baghdad, [16] Yemen, [17] Sour, [18] Halab, [19] na Qom. [20]

Wasifu wa Ismail

Ayatullah Khui anasema: Katika vyanzo na vitabu vya hadithi na wapokezi wa hadithi kuna makundi mawili ya hadithi kuhusiana na wasifu wa Ismail. Baadhi ya hadithi zinamsifu na nyingine zinamlaumu na kumkosoa. [21] Hadithi zinazomkosoa na kumlaumu Ismail zinamtaja kuwa alikuwa na uhusiano na maghulati kama Mufadhal ibn Omar na Basham Sairafi na Imam Swadiq (a.s) alionyesha kuchukizwa na mahusiano hayo. [22] Kadhalika Ismail alikuwa akishiriki vikao na hafla ambazo zilipelekea kuweko shaka kuhusiana na usahili wake wa tabia njema na maadili yake mema. [23] Hata hivyo, Ayatullah Khui anaaamini kuwa, hadithi zinazomlaumu na kumkosoa Ismail zina udhaifu wa sanadi na mapokezi na hivyo amefadhilisha riwaya zinazomsifu na kwa muktadha huyo anamtaja kuwa, ni mtu mwenye wasifu mkubwa na mlengwa wa mapenzi ya baba. [24]

Baadhi wameashiria kuwa, Ismail alikuwa na uhusiano na Khattabiyya na nafasi yao katika kuundika kundi la Ismailiya. Wanasema kuwa, Abul-Khattab na Ismail wakisaidiana katika zama za uhai wa Imam Swadiq (a.s) walianzisha itikadi ambazo ziliondokea kuwa msingi wa kuasisiwa kundi la Ismailiya [25]. Hata hivyo inaelezwa kuwa, hakuna hoja ya kuthibitisha madai haya. [26] Louis Massignon, mtambuzi wa Uislamu wa nchini Ufaransa naye anamtambua Abul-Khattab kuwa, baba wa kimaanawi wa Ismail. [27] Hata hivyo Kadhi Numan fakihi wa Ismailiya (283-363 H) haamini kama Abul-Khattab alikuwa na nafasi na mchango wowote katika kujitokeza kundi la Ismailiya na anamtaja kama ni mletaji wa bidaa na mtu ambaye alilaaniwa na Imam Swadiq (a.s).


Uhusiano wake na Mansur

Muhammad ibn Jarir Tabari mwandishi wa historia wa karne ya tatu Hijiria amenukuu ya kwamba, katika mwaka 140 Hijria, Mansur mtawala wa Bani Abbas alielekea Makka kwa ajili ya ibada ya Hija. Idadi kadhaa ya watu wa kizazi cha Ali ibn Abi Twalib na Mashia wake kama Muhammad Nasf al-Zakiyyah na Ibrahim na watoto wa Abdallah Mahdh na kundi la watu wa Khorasani waliokuwa wafuasi wake walikuwa wamekusanyika pia katika mji wa Makka. Baadhi yao walikata shauri kumuua Mansur, lakini Muhammad akapinga. Ismail alimfikishia uamuzi huo Mansur, naye akamtia mbaroni Abdallah na kuwaita watoto wake. Abdallah alitiwa jela na milki zake zikauzwa. [29]

Kudai Uimamu

Mtazamo wa Mashia Ithna’asharia

Maulamaa wa Mashia wa Maimamu 12 wanapinga kuweko hoja na ushahidi wa Uimamu wa Ismail na wamepinga na kunukuu hadithi zinazopinga kuwa Ismail aliteuliwa kuwa Imam. [30] Miongoni mwa hadithi hizo ni hadithi ya Lawh [31] na hadithi ya Jabir [32] ambazo kwa mujibu wake, Mtume (s.a.w.w) amebainisha majina ya Maimamu 12 ambapo baada ya Jafar ibn Muhammad Swadiq limekuja jina la mwanawe Mussa Kadhim na sio Ismail. Kadhalika Imam Swadiq alimtambulisha mwanawe Mussa kwa masahaba zake wa karibu katika matukio mbalimbali. Katika vitabu vya al-Kafi, [33] Irsha,[34] I’lam al-Wara,[35] na Bihar al-Anwar,[36] kuna mlango kuhusiana na hadithi zinazoonyesha na kuthibitisha Uimamu wa Mussa ibn Jafar ambapo zimenukuliwa hadithi kwa utaratibu, 16,46,12 na 14.[37]

Kutangazwa wazi kifo cha Ismail

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Zurarah ibn A’yun ni kuwa, baada ya kifo cha Ismail na kabla ya kuzikwa kwake, Imam Swadiq (a.s) alichukua ushahidi wa kifo cha mwanawe huyo kutoka kwa takribani wafuasi na masahaba zake karibu 30.[38] Kadhalika alilifanya kwa uwazi na bila kificho suala la ghusl, kuvisha sanda na kusindikiza jeneza pamoja na maziko ya mwanawe huyo ili kila mtu afahamu kwamba, Ismail ameaga dunia na amezikwa.[39] Aidha alitoa agizo la kufanyiwa Hija kwa niaba.[40] Lengo la Imam Swadiq (a.s) kufanya yote haya lilikuwa ni kuondoa itikadi juu ya Uimamu wake kwani baadhi walikuwa wakiamini kwamba, yeye ndiye Imam baada ya Imam Swadiq (a.s).[41] Pamoja na hayo yote baadhi ya Ismailiya walikuwa wakiamini kwamba, Ismail hajaaga dunia na kwamba, kuonyesha na dhihirisha kuwa, amefariki dunia ni kuwahadaa watu na kulinda uhai na roho yake pamoja na watu wake wa karibu. [42]

Mtazamo wa Ismailiya

Makala asili: Ismailiya

Ismailiya ni jina la makundi yanayoamini kwamba, baada ya Imam Swadiq (a.s), Ismail mtoto wa Imam Jafar Swadiq ndiye Imam baada ya baba yake huyo au mjukuu wake yaani Muhammad ibn Ismail.[43] Mubarakiyya na Qaramitah ambayo ni makundi miongoni mwa makundi ya Ismailiya yanaamini kwamba, baada ya Jafar ibn Muhammad, ni Muhammad ibn Ismail kwani Ismail alikuwa mrithi na kiongozi baada ya Imam Swadiq (a.s) na kwa kuwa yeye aliaga dunia katika zama za uhai wa baba yake, Imam Swadiq alikabidhi jukumu la Uimamu kwa mwanawe Muhammad. Makundi hayo yanaamini kuwa, baada ya kuaga dunia Hassan na Hussein (a.s) haijuzu Uimamu kutoka kwa kaka kuhamia kwa kaka. [44] Saad ibn Abdallah Ash’ari ameinasibisha itikadi hii kwa Ismailiya halisi au kwa Khattabiya. [45] Baadhi ya Waismailiya wanaamini kwamba, Ismail ibn Jafar hakuaga dunia bali yeye ni Mahdi Muahidiwa. [46] Pamoja na hayo yote katika vitabu na vyanzo vya ismailiya na athari za Qadhi Numan hakujaja hadithi inayoeleza kwa uwazi na kuwa hoja madhubuti kuhusiana na Uimamu wa Ismail. [47] Hata hivyo, Jafar ibn Mansur al-Yaman mhubiri wa Kismailiya wa mwishoni mwa karne ya tatu na mwanzoni mwa karne ya nne Hijiria ametaja na kukusanya hadithi kuhusiana na Uimamu wa Ismailiya ingawa hakutaja mlolongo na sanadi ya hadithi hizo. [48] Kadhalika katika baadhi ya vitabu imekuja kuwa, Makhalifa wa Fatimiya wa mwanzoni badala ya Ismail walikuwa wakimtambulisha kaka yake Abdallah Aftah kuwa ndiye Imam. Hata hivyo baadaye walibadilisha mtazamo huo na kuzungumzia Uimamu wa Ismail. [49]

Al-Bada'a kuhusu Ismail

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi kuhusiana wakati wa kifo cha Ismail ni kwamba, hilo lilikuwa ni kubainika wazi jambo ili watu wafahamu kwamba, baada ya baba yake, yeye sio Imam.[50] Hii ni kutokana na kuwa, kundi miongoni mwa Mashia lilikuwa likiamini kwamba, Ismail atakuwa Imam baada ya baba yake na kwa kufa kwake katika zama za uhai wa baba yake ikadhihirika na kufahamika wazi kwamba, Ismail hakuwa Imam na Imam baada ya Imam Swadiq (a.s) ni Mussa ibn Jafar (a.s)[51] Hata hivyo, vitabu vya Ismailiya vimezihusisha hadithi za Al-bada'a na Uimamu wa Ismail.[52]

Mahali alipozikwa

kaburi la Ismail bin Ja'afar baada ya kuhamishiwa Baqi'i katika ramani ya makaburi ya Baqi'i

Ismail aliaga dunia katika eneo linalojulikana kwa jina la Uraydh karibu na mji wa Madina na kuzika katika eneo la Baqi'i. [53] Katika zama za utawala wa Fatimiyya (297-567 Hijiria) kaburi lake lilijengewa. [54] Kaburi lake lilikuwa nje ya makaburi ya Baqi'i umbali wa mita 15 kutoka katika ukuta wa Baqii upande wa magharibi mkabala na makaburi ya Maimamu. [55] Kaburi la Ismail lilikuwa likitembelewa na Mashia hususan Ismailiya. [56] Mahujaji wa Kiirani walipokuwa wakielekea Madina, aghalabu wakati walipokuwa wakifanya ziara Baqi'i walikuwa wakimzuru pia mtoto au mjukuu huyu wa Imam na wameandika wasifu wa kaburi lake katika vitabu vyao vya kumbukumbu za safari. [57]

Muhammad Swadiq Najmi (1315-1390 Hijria Shamsia) mwaka 1394 Hijiria wakati wa kujenga barabara ya magharibi mwa Baqi'i, eneo la kaburi la Ismail liliharibiwa na ikaenea tetesi kwamba, mwili wake ulikuwa salama na bila ya kuharibika licha ya kupita karne nyingi. Mwili wa Ismail ukahamishiwa ndani ya makaburi ya Baqi'i, na hii leo kaburi hilo linapatikana upande wa mashariki mwa makaburi ya mashahidi wa Harra umbali wa mita 10 kutoka katika kaburi la Halima Sa'diyah. [58]