Nenda kwa yaliyomo

Kujibiwa Dua

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Jina la ukurasa la kikomo)
Makala hii inahusiana na kujibiwa dua. Ili kujua kuhusiana na mafuhumu ya dua angalia makala ya dua.

Kujibiwa dua (Kiarabu: استجابة الدعاء) ni kutakabali na kukubali Mwenyezi Mungu maombi ya waja. Mwenyezi Mungu amewaahidi waja wake katika Qur’ani juu ya kujibu dua na maombi yao; ingawa wakati mwingine wakati wa kujibiwa dua huchelewa kutokana na hekima kama vile kutokuwa na maslahi jambo hilo na kadhalika. Katika barua ya Imamu Ali (a.s) kwa Imamu Hassan (a.s) kwenye Nahaj al-Balagha anataja hekima tatu za kuchelewa kujibiwa dua: Wakati mwingine tatizo liko katika nia na kusudio la mtu (muombaji), wakati mwingine Mwenyezi Mungu anakusudia kumpatia ujira mkubwa zaidi na wakati mwingine Mwenyezi Mungu atampatia mja huyo kitu bora zaidi katika wakati mwingine.

Mustajab al-Da’wah ni mtu ambaye dua zake ni zenye kutakabaliwa. Katika hadithi dua za wazazi kwa watoto wao, dua ya mdhulumiwa dhidi ya dhalimu, dua ya Imamu na kiongozi muadilifu kwa watu na raia wake na dua ya Muumini kwa ndugu yake muumini ni miongoni mwa dua zilizotambuliwa kwamba, hukubaliwa na si zenye kukataliwa.

Aya na hadithi zinaeleza kwamba, kukubaliwa dua kunafungamana na kuchunga masharti na baadhi ya mambo kama vile kuwa pamoja nia ya moyoni na utamkaji katika ulimi wa dua husika, kufumbia macho na kukata kabisa mategemeo na matarajio kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kumtambua Mwenyezi Mungu. Kadhalika baadhi ya mienendo kama dhambi, kula vya haramu na kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu ni mambo ambayo yametajwa kuwa kizuzizi na kizingiti cha kujibiwa dua.

Kujibiwa dua hakuishii katika wakati na sehemu maalumu; lakini katika hadithi imeelezwa kuwa, katika baadhi ya wakati kama Siku ya Arafa na Usiku wa Laylatul-Qadr na baadhi ya maeneo kama kando ya Kaaba, pembeni ya kaburi la Bwana Mtume (s.a.w.w) na vilevile katika makaburi ya Maimamu Maasumina (a.s) hususan kaburi la Imamu Hussein (a.s) kwamba, yanalifanya suala la kutakabaliwa dua na maombi kuwa karibu zaidi. Kwa maana kwamba, uwezekano wa kutakabiliwa dua katika maeneo hayo ni mkubwa mno.

Ahadi ya Mwenyezi Mungu

Kujibiwa dua ni kutakabaliwa na kukubaliwa na Mwenyezi Mungu maombi ya waja. [1] Mwenyezi Mungu amewaahidi waja wake katika Aya kadhaa za Qur’ani juu ya kujibu dua na maombi yao. [2] Mujib ina maana ya mwenye kujibu maombi ya waja ambapo hili ni katika majina ya Mwenyezi Mungu (Asmaaullah). [3]

Allama Muhammad Hussein Tabatabai anasema: kujibiwa dua ni jambo la siku zote (daima) katika maisha ya mwanadamu. [4] Lakini ahadi ya kujibiwa dua haipaswi kuchukua nafasi ya juhudi za mwanadamu kwa ajili ya kufikia malengo na hivyo kumfanya aweke kando na kuacha sababu za dhahiri na zinazotia dosari na kukwamisha njia yake ya kawaida ya maisha. [5]

Sababu na Masharti

Aya na hadithi zinaeleza kwamba, kukubaliwa dua kunafungamana na kuchunga masharti na baadhi ya mambo ambapo baadhi yao ni:

  • Kuwa pamoja ulimi na moyo katika dua: Katika Qur’ani suala la kujibiwa dua limetajwa kuwa jambo lisilo na shaka kwa sharti kwamba ameombe Mwenyezi Mungu kwa ukweli wa kumuomba. [6] Allama Tabatabai anasema kuwa, “kumuomba dua Mwenyezi Mungu kwa ukweli wa kumuomba” amefasiri kuwa ni kusoma dua kwa ulimi sambamba na kuhudhurisha moyo.[7] Kadhalika imenukuliwa kutoka kwa Imamu Ali (a.s) kwamba; Mwenyezi Mungu haitakabali dua ambayo inaombwa ilihali moyo umeghafilika. [8]
  • Kufumbia macho na kukata kabisa mategemeo na matarajio kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu: Kuachana na sababu za kidhahiri na kusoma dua kwa ikhlasi, kwani Mwenyezi Mungu amewataka waja wamuombe yeye, wamuitikie na kumuamini yeye tu. [9]
  • Dua inayoambatana na kumtambua Mwenyezi Mungu: Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) akitoa jibu kwa kundi lililouliza kuhusiana na kutojibiwa dua alisema: Kutokuwa na ufahamu na maarifa kuhusu muombwaji ni miongoni mwa sababu za kutokubaliwa dua. [10]
  • Khushui na unyenyekevu: Aya ya 55 ya Surat al-A'raf inawataka waumini wamuombe Mwenyezi Mungu kwa kuogopa na kwa kutumai. Imamu Sadiq (a.s) pia anaamini kuwa, moja ya nyakati za kutakabaliwa dua ni pale mtu anapomuomba Mwenyezi Mungu ilihali anabubujikwa machozi, mwili unatetemeka na moyo wenye huzuni. [11]
  • Dua pamoja na amali njema: Ili dua ijibiwe, kumekokotezwa na kutiliwa mkazo kuhusiana na kufanya amali njema hususan kutoa sadaka. [12] Katika Qur'ani Mwenyezi Mungu amewapa ahadi ya kujibu dua zao wale walioamini na wakatenda mema. [13]
  • Dua katika mkusanyiko wa waumini: Imekuja katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ya kwamba: Hakuna mkusanyiko wa waumini 40 ambao utaomba dua na kumuelekea Mwenyezi Mungu na dua yake isikubaliwe, na Mtume mwenyewe wakati wa matatizo alikuwa akikusanya familia na watoto wake na kuomba dua na kisha wao wakiitikia Amin. [14]
  • Kutanguliza dua: Kuomba dua kabla ya kukumbwa na matatizo na mambo magumu, yaani kuomba dua katika zama za utulivu, raha na mambo yakiwa yanakwenda vizuri kuna athari kama: Kujibiwa dua, kuzuia balaa na kukidhi mahitaji wakati wa shida. Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ni kwamba, kila ambaye ataomba dua kabla ya kukumbwa na balaa, wakati wa kukumbwa na matatizo na balaa dua yake hukubaliwa na malaika kwa kusikia sauti yake husema: Sauti yake si ngeni (ni mashuhuri) na dua yake haitokataliwa na kila ambaye hatatanguliza dua (anaomba dua wakati wa kukumbwa na balaa tu) dua yake haikubaliwi na wakati atakapoomba dua malaika wanasema: Sauti yake ni ngeni (hatujawahi kuisikia) na sisi hatumtambui. [15][Maelezo 1] Imekuja katika hadithi nyingine iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) ya kwamba, mtu ambaye wakati wa raha na mambo kumuendea vyema akawa si mtu wa kuomba sana dua bali akawa ni muombaji dua tu wakati wa matatizo na balaa ataambiwa, ulikuwa wapi kabla ya leo? (أَيْنَ كُنْتَ قَبْلَ الْيَوْمِ)[16]
  • Kuomba dua sana wakati wa raha na utulivu: Imam Swadiq (a.s) amesema katika hadithi moja: Mtu ambaye anataka dua yake ikubaliwe katika matatizo (wakati wa matatizo) aombe dua sana wakati wa raha. [17]

Kadhalika dua inayoambatana na istighfari (kuomba msahamaha na maghufira) [18] na dua inayoambatana na kufanya tawasuli (kuomba kupitia) kwa Ahlul-Bayt (a.s) [19] ni mazingira na sababu nyingine ambazo zimetajwa kuwa zinapelekea dua kukubaliwa.

  • Kutochoka kuomba dua: Imamu Ridha (a.s) amenukuu kutoka kwa Imamu Baqir (a.s) ya kwamba amesema: Inastahiki (ni jambo zuri) kwa mtu mwenye imani kuomba dua katika raha na utulivu kama anavyokuwa katika shida na matatizo. Kisha Imamu Ridha (a.s) akasema: Basi msichoke kuomba dua. [20]
  • Ukweli, kuomba vya halali na kuunga udugu: pia ni mambo ambayo katika hadithi yameusiwa kuyafanya yule anayeomba dua.[Maelezo 2] [21]
  • Kufanya ibada: Katika Dua Kumayl kufanya ibada waja kumetajwa kuwa moja ya masharti yayodhamini dua kutakabaliwa. Imamu Ali (a.s) anasema katika moja ya dondoo za mwishoni mwishoni mwa dua Kumayl kwamba: (فانک قضیت علی عبادک بعبادتک وامرتهم بدعائک وضمنت لهم الاجابة ; Hakika uliwaamulia waja Wako wakuabudu, na ukawaamrisha wakuombe, na umewadhamini majibu)). [22]

Wakati na Mahali

Kujibiwa dua hakuhusiani tu na wakati na mahali maalumu. Lakini baadhi ya nyakati na baadhi ya maeneo yamekokotezwa kwamba, dua inakubaliwa; inaelezwa katika hadithi kwamba, Laylatul-Qadr, 15 Shaaban (nusu ya Shaaban), 27 Rajab, Eidul-Fitr, Siku ya Arafa, Eidul-Adh'ha, siku ya kwanza ya Muharram, wakati wa usiku na wakati wa adhana, usiku wa kuamkia Ijumaa, wakati wa mvua kunyesha, baada ya Sala za wajibu, wakati wa kuiona Kaaba na miezi maalumu kama Rajab, Shaaban na Ramadhan ni miongoni mwa nyakati ambazo zimetambulishwa kuwa dua hukubaliwa. [23]

Kadhalika katika maandiko ya hadithi mji wa Makka, Masjidul-Haram, Kaaba, kando ya Hajar al-Aswad (Jiwe Jeusi), Rukn Yamani (Nguzo ya Yamani), Hijr Ismail, katika jangwa la Arafa, katika maeneo ya kando kando na kaburi la Mtume (s.a.w.w), Rawdhat al-Nabbi, Haram za Maimamu wa Kishia hususan chini ya kuba la Imamu Hussein (a.s), [24] Masjid al-Sahla na Kufa ni miongoni mwa maeneo ambayo yameelezwa kuwa dua inakubaliwa. [25]

Vizingiti

Katika Aya na hadithi kumetajwa mambo ambayo ni vizingiti na vizuizi vya dua kukubaliwa. Baadhi ya mambo hayo ni:

  • Dhambi: Inaelezwa katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Muhammad Baqir (a.s) kwamba, dhambi ni sababu muhimu zaidi ya dua za mtu kutojibiwa. [26] Imamu Sajjad (a.s) pia amesema, nia mbaya, uovu, ukhabithi, nifaki kwa ndugu wa kidini, kuchelewesha Sala za wajibu mpaka wakati mwingine (wakati wake kupita), lugha chafu (matusi) na kutotoa sadaka ni madhambi yaliyotambuliwa kwamba, yanazuia dua kujibiwa. [27] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, kudhulumu [28], kutomtii baba na mama, kukata udugu [29], kukiuka ahadi, [30] na usengenyaji [31] ni katika vizingiti na vikwazo vya dua kutokubaliwa. Katika Dua Kumayl Mwenyezi Mungu anaombwa atoe msamaha na maghufira kwa dhambi zinazo zuia dua. [32]
  • Tonge la haramu: Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali, chumo la haramu na kula vya haramu huwa kikwazo cha kujibiwa dua kwa muda wa siku 40. [33] Katika Hadith al-Qudus Mwenyezi Mungu ameahidi kujibu na kutakabali dua za waja wake wote isiokuwa walaji vya haramu. [34]
  • Dua wakati wa shida tu: Kwa mujibu wa hadithi mtu ambaye anataka dua yake ikubaliwe katika shida na matatizo, hapaswi kuacha na kughafilika kuomba dua wakati wa raha na neema. [35]
  • Kushuku Wilaya (Uongozi) ya Ahlul-Bayt (a.s): Imekuliwa katika hadithi kwamba, mtu ambaye katika moyo wake ana shaka na Wilayat Ahlul-Bayt (a.s), hata kama katika umri wake wote atakuwa katika hali ya dua na kumtaaradhia Mola, dua yake haitokubaliwa. [36]
  • Khiyana na usaliti: Imamu Ali (a.s) anasema katika jibu lake alipoulizwa kuhusu kutojibiwa dua kwamba, khiyana na usaliti kwa nyoyo za watu kunazuia kujibiwa dua katika sehemu nane. Kumtambua Mwenyezi Mungu na kutotekeleza haki yake, kumuamini Mtume (s.a.w.w) na kutotekeleza sira na mwenendo wake, kusoma Qur'ani na kutoifanyia kazi, hofu ya moto wa jahanamu katika maneno na kufanya harakati kuilekea katika vitendo, kuwa na raghba na matamanio na pepo katika maneno na kujitenga nayo mbali katika matendo, kula neema za Mwenyezi Mungu na kutomshukuru, kuona aibu na mapungufu ya watu na kutoona mapungufu yako na kumfanyia uadui shetani katika ulimi na kufanya naye urafiki katika matendo ni khiyana na usaliti wa nyoyo sifa na matendo ambayo Imamu Ali (a.s) ameyataja kuwa yanazuia kujibiwa dua. [37]

Kadhalika kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu, [38] na kuipuuza Sala [39] ni katika vikwazo na vizingiti vya kujibiwa dua.

  • Dua bila ya juhudi na kuzingatia jukumu: Licha ya kuwa dua ni kumuita Mwenyezi Mungu na kumuomba, lakini hii haina maana ya kupuuza jukumu na kuacha kustafidi na suhula na nyenzo za lazima kwa ajili ya kufikia matakwa na malengo, kimsingi dua inapaswa kuambatana na kufanya harakati, ghairi ya hivyo, kuomba dua na kuwa katika hali ya kutofanya harakati na kukwepa majukumu, hakuna wakati ambao kutakuwa na matarajio ya kujibiwa dua kama hiyo. Katika baadhi ya hadithi, wametajwa watu ambao wanaomba kutattuliwa matatizo yao bila ya kuzingatia suhula na nyenzo ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka. Mifano ya dua kama hizi imetajwa katika hadithi kama:
  1. Mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempatia mali na kisha yeye anaitumia mali hiyo kwa isirafu na ubadhirifu na kutumia mahali si pake anapelekea kupotea mali hiyo, lakini bado anamuomba Mwenyezi Mungu ampatie riziki.
  2. Mwanaume ambaye amechoka na tabia mbaya ya mkewe pamoja na maudhi yake yasiyokwisha anamuomba Mwenyezi Muungu amuepushe na mkewe huyo ili asalimike, hii ni katika hali ambayo Mwenyezi Mungu ameweka talaka mbele yake.
  3. Mtu ambaye anashtakia maudhi ya mara kwa mara ya jirani yake na anamlaani kwa hilo, katika hali ambayo, anaweza kuuza nyumba yake na kwenda kuishi sehemu nyingine mwafaka zaidi.
  4. Ambaye amekaa nyumbani na hafanyi kazi yoyote na kisha anamuomba riziki Mwenyezi Mungu katika hali ambayo, Mwenyezi Mungu ameweka mbele yake njia za kutafuta riziki.
  5. Mtu ambaye amemkopesha mali mtu mwingine na aliyekoposhwa anakana. Kisha ananyanyua mikono juu na kuomba dua akimuomba Allah amrejeshee mali yake, ilihali Mwenyezi Mungu ametoa amri ya kuweka mashahidi. [40] Kuna nukta zingine mbili ambazo zinapasa kuzingatiwa. Nukta ya kwanza ni kwamba, hii ni mifano tu ya watu ambao wanadhani dua maana yake ni kuacha kufanya kazi na kuacha kujituma na kuweka mipango na badala yake kukaa tu na kuomba dua kwa ajiili ya kufikia malengo yao. Nukta ya pili ni kuwa, kile ambacho kinazungumziwa katika hadithi, lengo ni kwa ajili ya kufanya nukta hii izingatiwe ya kwamba, kila tatizo lina utatuzi na sio kwamba, kila mwenye matatizo na mwenza wake katika ndoa anapaswa kufikiria chaguo la talaka tu au kila ambaye atakuwa na matatizo na jirani yake, basi anapaswa kuhama mali anapoishi.

Hekima za Kuchelewa Kujibiwa Dua

Allama Tabatabai anasema kuwa, kujibiwa dua ni katika sunna na mipango ya Mwenyezi Mungu isiyo na shaka kwa sharti la kuchunga taratibu zake na kuondoa vikwazo. [41] Lakini kuna wakati kutokana na maslahi na hekima, kujibiwa dua hucheleweshwa. [42] Baadhi ya hekima hizo ni:

  • Kutokuweko maslahi kwa waja: Kuna wakati mtu anaomba dua au anataka kitu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambapo si maslahi kwake kupatiwa hilo. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu anachelewesha kujibu dua na takwa lake hilo au hajibu kabisa. Katika Qur'ani Waislamu wanahutubiwa kwa kuambiwa kuwa, huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua kile ambacho kina maslahi na nyinyi, lakini nyinyi hamjui. [43] Imamu Ali (a.s) pia anamhutubu mwanawe Imamu Hassan kwa kumwambia: Kuna vitu vingi ambavyo unavitaka wewe lakini ndani yake kuna kuangamia dini na dunia. [44]
  • Katika barua ya Imamu Ali (a.s) kwa Imamu Hassan (a.s) katika Nahaj al-Balagha anataja hekima tatu za kuchelewa kujibiwa dua: Wakati mwingine tatizo liko katika nia na kusudio la mtu (muombaji), wakati mwingine Mwenyezi Mungu anakusudia kumpatia ujira mkubwa zaidi na wakati mwingine Mwenyezi Mungu atampatia mja huyo kitu bora zaidi katika wakati mwingine. [45] Aidha Imamu Sajjad (a.s) amenukuliwa akisema: Dua ya muumini ina moja kati ya faida tatu: Ima inakuwa akiba kwake, inajibiwa duniani au inaondoa balaa ambayo ilikuwa impate. [46]

Mustajab al-Da’wah

Makala Asili: Mustajab al-Da’wah

Mustajab al-Da’wah ni mtu ambaye dua zake zinatakabaliwa. [47] Katika hadithi, dua za wazazi kwa watoto wao, dua ya mdhulumiwa dhidi ya dhalimu, dua ya Imamu na kiongozi muadilifu kwa watu na raia wake na dua ya muumini kwa ndugu yake muumini ni miongoni mwa dua zilizotambuliwa kwamba, hukubaliwa na si zenye kukataliwa. [48]

Kadhalika imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Hassan (a.s) kwamba: Kama mtu anauchunga moyo wake ili mambo ambayo hayamridhishi Mwenyezi Mungu yasipenye na kuingia humo, mimi ninadhaminia kwamba atakuwa mtu ambaye dua zake zinatakabaliwa (Mustajab al-Da’awah). [49]

Maelezo

  1. (مَنْ تَقَدَّمَ فِي الدُّعَاءِ اسْتُجِيبَ لَهُ إِذَا نَزَلَ بِهِ الْبَلَاءُ وَ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ صَوْتٌ مَعْرُوفٌ وَ لَمْ يُحْجَبْ عَنِ السَّمَاءِ وَ مَنْ لَمْ يَتَقَدَّمْ فِي الدُّعَاءِ لَمْ يُسْتَجَبْ لَهُ إِذَا نَزَلَ بِهِ الْبَلَاءُ وَ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ إِنَّ ذَا الصَّوْتَ لَا نَعْرِفُهُ)
  2. (الامام الرضا(ع):...وعليك بالصدق وطلب الحلال ، وصلة الرحم)

Rejea

Vyanzo

  • Fakhr al-Din al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Mafātīḥ al-ghayb. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Ḥarrānī, Ḥasan b. ʿAlī al-. Tuḥaf al-ʿuqūl. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Daftar-i Nashr-i Islāmī, 1404 AH.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1409 AH.
  • Ibn Fahd al-Ḥillī, Aḥmad b. Muḥammad. ʿUddat al-dāʿī wa najāḥ al-sāʿī. Edited by Aḥmad Muwaḥḥidī Qumī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Ibn Manẓūr, Muḥammad b. Mukarram. Lisān al-ʿArab. Beirut: Dār al-Fikr-Dār al-Ṣādir, 1414 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Dar Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1371 Sh.
  • Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣāliḥ.
  • Qarāʾatī, Muḥsin. Tafsīr-i nūr. Tehran: Markaz-i Farhangī-yi Darshāyī az Qurʾān, 1388 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Maʿānī l-akhbār. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1403 AH.
  • Ṭabāṭabāyī, Muḥammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1390 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Miṣbāḥ al-mutahajjid. Beirut: Muʾassisat Fiqh al-Shīʿa, 1411 AH.