Imamu Musa Kadhim (a.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Abu Hassan Awali)
Imamu Musa Kadhim (a.s)
Imamu wa (7) wa Mashia
Muonekano wa Zamani wa Haram ya Kadhimein
Muonekano wa Zamani wa Haram ya Kadhimein
JinaMussa bin Ja'afar
KuniaAbu Hassan Awal. Abu Ibrahim. Abu Ali
Siku ya Kuzaliwa20 Dhulhijjah 127 Hijria au 7 Safar Mwaka 128 Hijria
Mahali AlipozaliwaAbua, Madina
Kipindi cha UimamuMiaka 25 (148 - 183 Hijria)
Kifo25 Rajab, 183 Hijria
AlipozikwaKadhimein
AlipoishiMadina
LakabuKadhim, Babu al-Hawaij, Abdus Salih
BabaImamu Swadiq (a.s)
MamaHamida Barbariyah
WakeNajmah mama yake Imamu Ridha (a.s)
WatotoImamu Ridha (a.s), Maasuma, Ibrahim, Qasim, Shahcheragh, Hamza, Abdullah, Is'haq, Hakimah
UmriMiaka 55
Maimamu wa Kishia
Imamu Ali • Imamu Hassan MujtabaImamu Hussein • Imamu Sajjad • Imamu Baqir • Imamu SwadiqImamu Kadhim • Imamu Ridha • Imamu JawadImamu Hadi • Imamu Mahdi


Mussa bin Ja’afar (Kiarabu: الإمام موسى الكاظم عليه السلام) (alizaliwa 127 au 128 na kufariki 183 Hijiria) anajulikana kwa jina la Imamu Musa Kadhim الإمام موسى الكاظم (ع)), ambapo lakabu zake ni "Kadhim" na Babu Al-Hawaaij. Yeye ni Imamu wa saba kwa mujibu wa itikadi ya madhehebu ya Shia wanaoamini Maimamu 12. Imamu Musa Kadhim (a.s), alizaliwa mnamo mwaka wa 128 Hijiria, tukio ambalo liliambatana na tukio la wa mwanzo wa uasi wa Abu Muslim Khorasani, wakili wa Bani Abbas dhidi ya Bani Umayya, nalo ni tukio lilitokea ndani ya mwaka wa 148 Hijiria, baada ya kuuawa kishahidi baba yake Imam Kadhim (a.s), ambaye ni Imam Swadiq (a.s). Baada ya kifo hicho cha Imam Swadiq (a.s), nafasi ya Uimamu ikashikwa na Imamu Kadhim (a.s), yeye alishika nafadi hiyo kwa muda wa miaka 35 mfululizo. Kipindi hicho cha miaka 35 ya Uimamu wake kiliambatana na ukhalifa wa Mansour, Hadi, Mahdi na Harun Abbasi. Mara kadhaa alitiwa kifungoni na Mahdi na Harun Abbasi, na hatimae aliuawa kishahidi katika jela ya Sindi Bin Shaahik mnamo mwaka 183 Hijiria. Baada ya kifo chake, Uimamu ulihamia kwa mwanawe Ali bin Musa (a.s).

Kipindi cha muhula wa Uimamu wa Imamu Kadhim (a.s) kiliambatana na kilele cha nguvu za Ukhalifa wa Bani Abbas, jambo ambalo lilimfanya afanye taqiyyah (afiche imani na itikadi yake) dhidi ya serikali ya wakati huo, na pia kuwaamuru Mashia kufanya hivyo. Kwa hiyo, Imamu wa saba wa Mashia hakuchukua msimamo wa wazi dhidi ya Makhalifa wa Abbasiyyina, na Imamu hakuonekana na msimamo wa wazi kabisa dhidi ya serikali ya wakati wake, kama walivyofanya waasi wa Kialawi, likiwemo vuguvugu na ghasia za kundi la waasi lililoongozwa na Shahidi Fakh. Pamoja na hayo, pale Imamu (a.s) alipokuwa akifanya mijadala na mazungumzo na Makhalifa wa Bani Abbas na wengineo, hakuacha kuonesha kuto kuwepo uhalali wa Ukhalifa huo wa Bani Abbas.

Mazungumzo mijadala na ya Mussa bin Ja’afar (a.s) na baadhi ya wanazuoni wa Kiyahudi na Kikristo yamesimuliwa katika vyanzo tofauti vya kihistoria na Hadith. Nafasi kubwa ya mazunguzo hayo, ilijikita katika kujibu maswali yao ya kidini. Kuna zaidi ya Hadithi elfu tatu kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s), zilizokusanywa katika Musnad Al-Imam Al-Kadhim, ambapo baadhi ya Hadithi hizo zimepokewa na kusimuliwa na baadhi ya As-habu Al-Ijma’a. As-habu Al-Ijma’a ni kundi la wanazuoni ambao wamewafikia katika nadharia fulani za kisheria, ambao muafaka wao hutumika kama ni hoja na dalili ya kukubalika kwa sheria hizo.

Ili kuwasiliana na Mashia, Imamu Kadhim (a.s) alipanua mtandao wa mawakala wake kwa kuwateua watu kadhaa wanaomuakilisha yeye katika mikoa mbalimbali. Kwa upande mwingine, maisha ya Imamu Kadhim (a.s) yalisadifiana na kutokea mifarakano miongoni mwa Shia na kuchipuka madhehebu tofauti, kama vile; Madhehebu ya Ismailia, Fatahiyyah, na Naausiyyah. Madhehebu hayo yaliundwa mwanzoni mwa Uimamu wake, na baada ya kifo chake cha kishahidi yakazuka madhehebu ya Waaqifiyyah.

Vyanzo vyote viwili vya Kishia na Kisunni vimemsifu yeye kwa ubora wa elimu, ibada, uvumilivu na ukarimu wake. Pia alisifika kwa lakabu za Kadhim na Abdu Saleh. Wakuu wa madhehebu ya Kisunni walimheshimu Imamu huyo wa 7 wa Kishia na kuhisabu kuwa ni miongoni mwa wanazuoni wa kidini, na kama wafanyavyo Mashia, Masunni nao walikuwa na kawaida ya kulitembelea na kulizuru kaburi lake pamoja na kaburi la mjukuu wake, ambaye ni Imamu Jawad (a.s). Makaburi ambayo yapo katika eneo la Kaskazini mwa Baghdad linayojulikana kwa jina la Kaadhimaini, na ni moja ya sehemu inayotembelewa na Waislamu wengi kwa ajili ya kufanya ziara kwenye makaburi hayo, hususan Mashia.

Wasifu Wake

Musa bin Ja’afar ima alizaliwa Dhul-Hijjah mwaka wa 127 Hijiria [1] au mwezi 7 Safar mwaka 128 Hijiria [2]. Tokeo hilo lilitokea wakati Imamu Swadiq (a.s) na mkewe Hamida walipokuwa wakirejea kutoka Hija, katika eneo la Abuwa'a [3]. Pia kuna ripoti isemayo kuwa; Yeye alizaliwa katika mji wa Madina mnamo mwaka 129 Hijiria. [4] Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuzaliwa kwa Imam wa saba kunasadifiana na tarehe 20 Dhu Al-Hijjah. [5] Baadhi ya vyanzo vimeripoti kuwa, Imam Swadiq (a.s) alikuwa na shauku na mapenzi makubwa juu ya Imamu Musa bin Ja'afar (a.s). [6] Kwa mujibu wa riwaya ya Ahmad Barqiy, Baada ya Imam Swadiq kuzaliwa mwanawe huyo, Imamu (a.s) alichukuwa hatua ya kuwalisha watu kwa muda wa siku tatu mfululizo. [7]

Makala Asili: Orodha ya lakabu na kuniya za Imamu Kadhim (a.s)

Ukoo wa Musa bin Ja’afar bin Muhammad bin Ali bin Husein bin Ali bin Abi Talib unaishia kwa Imam Ali (a.s) kupitia mababu wanne. Baba yake ni Imamu Swadiq (a.s), ambaye ni Imamu wa sita wa Mashia, na mama yake ni Hamida Barbariyyah. [8] Kuniya zake ni; Abu Ibrahim, Abul Hasan Al-Wwal, Abul Hasan Maadhiy, na Abu Ali. Alipewa lakabu ya Kadhim [9] kwa sababu ya udhibiti wa hasira zake dhidi ya tabia mbaya za wengine, pia ana lakabu ya Abdu Saleh. [10] Lakabu nyingine maarufu ya Imamu Musa (a.s), ni Baabu Al-Hawaaij. [11] Watu wa Madina walikuwa wakimwita; (زَیْنُ المُجتَهدین) "Pambo la wanajitihada". [12]

Musa bin Ja’afar (a.s) alizaliwa ndani ya zama za uhamisho wa madaraka kutoka kwa Bani Umayya kwenda kwa Bani Abbas. Khalifa wa kwanza wa Bani Abbas aliingia madarakani huku yeye akiwa na umri wa miaka minne, Hakuna ripoti nyingi kuhusiana na maisha ya Imamu Kadhim (a.s) ya kuanzia udogoni mwake mpaka kipindi cha kuanza kwa Uimamu wake, isipokuwa tu yale mazungumzo na mijadala ya kielimu ya zama za utotoni mwake, yakiwemo mazungumzo baina yake na Abu Hanifah [13] na wanazuoni wa dini nyingine, [14] yaliyofanyika ndani ya mji wa Madina.

Kwa mujibu wa riwaya ya kitabu cha Al-Manaqib, kuna siku aliingia katika kijiji kimojawapo cha Syria bila kujulikana jina lake, kisha akafanya mazungumzo na mtawa mmoja katika kijiji hicho, jambo ambalo lilipelekea mtawa huyo kusilimu yeye pamoja na wafuasi wake. Pia kuna ripoti za safari kadhaa alizozifanya kuelekea Makka kwa ajili ya Hija na Umrah. [16] Yeye alisafiri kwenda Baghdad mara kadhaa kupitia wito na matakwa ya Makhalifa wa Bani Abbas. Ukiachana na safari hizo, kipindi chote cha maisha yake kilichobakia, alikitumia katika mji wa Madina.

Mke na Watoto

Tazama pia: Orodha ya watoto wa Imamu Kadhim (a.s)

Hakuna ripoti na habari za wazi kuhusiana na idadi ya wake wa Imamu Kadhim (a.s). Mke wa kwanza miongoni mwa wake zake ni Najmah, ambaye ni mama wa Imamu Ridha (a.s). [29] Kuna idadi tofauti zilizotajwa katika vyanzo vya kihistoria kuhusiana na idadi ya watoto wake (a.s). Kwa mujibu wa maandiko ya Sheikh Mufid; Imamu Kadhim (a.s) alikuwa na watoto 37, (18 ni wa kiume na 19 ni wanawake). Watoto hao kwa upande wa kiume ni; Imam Ridha (a.s), Ibrahim, Shaahcheragh, Hamza, na Is'haq. Na kwa upande wa wanawake ni; Fatima Maasuma na Hakiimah. [30] Masharifu wa kizazi cha Imam Kadhim (a.s) wanajulikana kama ni Saadat Al-Muusawiy. [31]

Muhula wa Uimamu Wake

Musa bin Ja’afar (a.s) alikamata nafasi ya Uimamu tokea mwaka wa 148 Hijiria, baada ya kuuawa kishahidi Imam Swadiq (a.s). Alikamata nafasi hiyo ya Uimamu akiwa na umri wa miaka 20. [32] Kipindi cha Uimamu wake kiliambatana na Ukhalifa wa Makhalifa wanne wa serikali ya Abbasiyyiina. [33] Kwa kiasi cha muda wa mika 10, ukhalifa wake ulisadifiana na serikali ya Mansuri, iliodumu kuanzia (mwaka 136 hadi 158 Hijiria). Uimamu wake pia uliendelea hadi katika utawala wa Mahdi Abbasiy, uliodumu kwa muda wa miaka 11, yaani kuanzia mwaka (158 hadi 169 Hijiria). Pia Imamu Musa bin Ja'afar alidiriki kipinda cha utawala wa Hadi Abbaasiy, uliodumu kipindi cha mwaka mmoja tu, (ambapo alitawala kuanzia mwaka 169 hadi 170 Hijiria). alidiki tena miaka 13 ya utawala wa Harun (aliyetawala kuanzia mwaka 170 hadi 193 Hijiria). [34] Kwa hiyo Muda wa Uimamu wa Musa bin Ja’afar (a.s), ulidumu kwa muda wa miaka 35. Kupitia kifo chake cha kishahidi cha mwaka wa 183 Hijiria, jukumu la Uimamu lilichukuliwa na mwanawe, ambaye ni Imam Ridha (a.s). [35]


  • Maandiko Juu ya Ithibati za Uimamu

Tazama pia: Uimamu wa Maimamu Kumi na Wawili

Kwa mtazamo wa Kishia, Imamu huteuliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe bila ya kuingiliwa na mtu yeyote. Mojawapo ya njia za kumtambua Imamu ni ithibati za kimaandishi au kimatamshi, zilizo wazi kabisa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), au kutoka kwa Imamu aliyetangulia kabla ya Uimamu wa Imamu huyo anayefuatia). [36] Kuna ithibati tofauti zilizonukuliwa kutoka kwa Masahaba wa karibu wa Imamu Ja'afar Swadiq (a.s) kuhusiana na Uimamu wa Imamu Musa bin Ja'afar. Katika kila moja ya vitabu vya Al-Kafi, [37] Al-Irshaad, [38] A'alamu Al-Wara [39] na Bihar Al-Anwar, [40] kuna milango maalumu kuhusu maandiko yanayothibitisha Uimamu wa Musa bin Ja’afar (a.s). Milango ambayo tutaitaja hapa kulingana na utaratibu wa vitabu hivyo, nayo ni; 16, 46, 12 na 14. Hiyo ndiyo milango iliyonukuu maandiko [41] na riwaya tofauti kuhusiana na suala hilo. Miongoni mwa riwaya hizo ni kama ifuatavyo:

  • Katika moja kati ya riwaya, Faiz bin Mukhtar anasema: "Nilimuuliza Imam Swadiq (a.s), ni nani Imamu atakayefuatia baada yako? Swali langu hilo likawa limeambatana na ujio wa mwanawe ambaye ni Musa, Imamu Swadiq (a.s) akamtambulisha Musa bin Ja'afar kama ndiye Imamu aatakayefuatia baada yake (a.s)". [42]
  • Ali bin Ja’afar naye amesimulia akisema: "Imamu Swadiq (a.s) akimzungumzia kuhusu Imamu Musa bin Ja'afar (a.s) alisema; «فَإِنَّهُ أَفْضَلُ وُلْدِی وَ مَنْ أُخَلِّفُ مِنْ بَعْدِی وَ هُوَ الْقَائِمُ مَقَامِی وَ الْحُجَّةُ لِلَه تَعَالَی عَلَی كَافَّةِ خَلْقِهِ مِنْ بَعْدِی» ; “Yeye ni mbora wa watoto wangu wenye kunirithi mimi na ndiye atakayefuatia kushika nafasi ya Uimamu baada yangu, Naye ndiye Khalifa wa Mwenye Ezi Mungu juu ya viumbe wote baada yangu mimi." [43]

Pia katika 'Uyunu Al-Akhbari Al-Ridha imeelezwa kwamba; Harun Al-Rashid alizungumza na mwanawe Maamuun, akamtambulisha kwake Musa bin Ja’afar (a.s), kuwa ndiye Imamu mwadilifu na anayestahiki zaidi kumrithi Mtume (s.a.w.w), na akauelezea uongozi wake (Maamuun) kuwa ni uongozi wa kidhahiri tu na ni uongozi wa mabavu. [44]

Wosia wa Imam Swadiq (a.s) na Kutangatanga kwa Baadhi ya Mashia

Imeelezwa katika vyanzo kihistori ya kwamba Imam Swadiq (a.s) akizingatia ubeberu na ukakasi wa utawala wa Bani Abbas, pia akizingatia umuhimu wa kuokoa maisha ya Imamu Kadhim (a.s), aliwatambulisha watu watano, akiwemo Khalifa wa Kiabbasi, kuwa ni miongoni mwa warithi wake. [45] Ingawaje Imam Swadiq (a.s), Mara nyingi alikuwa akimtambulisha Imamu atakayefuata baada yake mbele ya Masahaba zake maalum, ila kitendo hicho cha kuashiria majina matano ya watu tofauti, kilisababisha kutokea hali ya utata hata kwa upande wa Mashia. Katika kipindi hicho, hata baadhi ya Masahaba mashuhuri wa Imamu Swadiq (a.s) kama vile Muumin Taaq na Hisham bin Salem pia waliingiwa na shaka. Kwanza kabisa walikwenda kwa Abdullah Aftah, aliyedai Uimamu, na wakamuuliza maswali kadhaa kuhusiana na zaka. Lakini majibu ya Abdullah hayakuwaridhisha. Kisha wawili hao wakakutana na Musa bin Ja’afar (a.s) na wakatosheka na majibu yake, wakamuamini na kuukubali Uimamu wake. [46]

Mgawanyiko wa Ndani ya Ushia

Kuna madhehebu kadhaa yaliozuka katika kipindi cha Uimamu wa Musa bin Ja'afar (a.s), nayo ni; Ismailia, Fatahiya na Nawuusiyyah. Ingawaje misingi ya mgawanyiko wa Shia ulikuwa imeshaanza kuota mizizi yake tokea uhai wa Imam Swadiq (a.s), ila mgawanyiko huo haukudhihiri miongoni mwao katika kipindi hicho cha uhai wake. Baada tu ya kifo cha kishahidi cha Imam Swadiq (a.s), na mwanzoni wa Uimamu wa Musa bin Ja'afar, Mashia waligawanyika katika madhehebu na makundi tofauti; Moja ya makundi hayo lilikanusha kifo cha Ismail, mtoto wa Imam Swadiq (a.s) na wakamchukulia kuwa yeye ndiye Imamu. Baadhi ya wafuasi wa kundi hili, ambao walikata tamaa kuhusiana na uhai wa Ismail, walimhisabu mwanawe Ismail ambaye ni Muhammad kama ni Imamu. Kundi hilo lilijulikana kwa jina la Ismailia. Wengine walimtabua Abdullah Aftah kuwa ndiye imamu wao, nao hao wakajulikana kwa jina la Fatahiyyah, lakini baada ya kifo chake, kilichotokea siku 70 takriban baada ya kifo cha kishahidi cha Imam Swadiq (a.s), walihamia kwa Imamu Musa bin Ja’afar na wakamtambua yeye kuwa ndiye Imamu wao. Baadhi yao waliachana na Musa bi Ja'afar, badala yake wakashikamana na mtu aliyejulikana kwa jina la Naauus na kumfanya ndiye Imamu wao, pia kuna baadhi waliouamini uimamu wa Muhammad Diibaaj na kushikamana naye. [47]

Harakati za Maghulati (Waliokiuka Mipaka)

Pia kulikuwa na harakati za Maghulati katika kipindi cha Imam Kadhim (a.s). Katika kipindi hicho hicho kulizuka kundi la madhehebu ya Bashiiriyyah, kundi ambalo lilijinasibisha kwa Muhammad bin Bashiir, mmoja wa masahaba wa Imamu Mussa bin Ja’afar (a.s). Yeye huyu katika uhai wake, alizua uongo dhidi ya Imamu Mussa bin Ja'afar (a.s). [48] Muhammad bin Bashir alidai kwamba; Mtu anayefahamika mbele ya watu kwa jina la, Mussa bin Ja’afar, yeye huyo hakuwa ni Mussa bin Ja’afar wa kweli kweli, ambaye ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake. [49] Yeye alidai ya kwamba; Mussa bin Jafa'afa wa kweli yuko pamoja naye, na iwapo watu watakuwa tayari kwenda kuonana naye, basi yeye atawapeleka akawaoneshe Imamu huyo kweli mahala alipo. [50] Bwana huyo kiukweli alikuwa ni mjuzi wa uchawi, kwa hiyo yeye kupitia njia ya mazingaombwe, aliweza kumtayarisha mtu mwenye uso kama uso wa Imamu Kadhim (a.s), kisha akawaonesha watu, na kudai kuwa yeye huyo ndiye Imamu Kadhim (a.s). [51] Hivyo basi kutokana na ujanja huo, aliweza kupata baadhi ya watu waliohadaika kupitia ujanja huo. Ni jambo lililo wazi kabisa ya kwamba, kabla ya kifo cha kishahidi cha Imamu Kadhim (a.s), Muhammad bin Bashir na wafuasi wake walikuwa tayari wamesha eneza uvumi ndani ya umma, ya kwamba Imamu Kadhim (a.s) hajaenda gerezani, na bado hajafa, bali yuko hai. [52] Imamu Kadhim katika uhai wake alikuwa akimlaani Muhammad bin Bashir na kumhisabu kuwa ni najisi, pia Imamu (a.s) aliihalalisha damu yake. [53]

Harakati za Kielimu

Kuna harakati mbali mbali za kielimu zimeripotiwa kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s); Nakala ya harakati hizo za kielimu zimehifadhiwa na kurikodiwa katika mfumo wa masimulizi, na mijadala ya kielimu katika vitabu vya Kishia vilivyonukuu Hadith za Maimamu wa Kishia. [54]

Kuna Hadith nyingi katika vyanzo vya Hadith vya Shia zilizosimuliwa kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s), Hadithi hizo zimezungumzia mada tofauti; zikiwemo mada za kitheolojia, kama vile tauhidi [55], badaa [56] na masuala ya kiimani [57] pamoja na masuala mbali mbali ya kimaadili. [58] Pia miongoni mwa yaliyorikodiwa kutoka kwake, ni ile dua maarufu ya Joushan Saghir.

Katika nyaraka na ripoti za riwaya mbali mbali, yeye ameonekana kusifiwa na kupewa majina tofauti. Miongoni mwa majina aliyosifiwa nayo ni; Al-Kadhim, Abi Al-Hassan, Abi Al-Haasan Al-Awwal, Abi Al-Hasan Al-Maadhi, Al-A'alim [59] na Al-Abdu Al-Saleh. Mpokezi maarufu wa Hadithi ajulikanaye kwa jina la Azizullah Ataaridiy, alikusanya na kurikodi kutoka kwake kiasi cha Hadith 3134 ndani ya kitabu chake kiitwacho Musnad Al-Imam Al-Kadhim. [60] Abu ‘Imran Marwazi Baghdadi (aliyefariki mnamo mwaka 299 Hijiria), ni mmoja wa wanachuoni wa Kisunni, aliyekusanya baadhi ya Hadithi za Imamu wa saba wa Mashia katika kitabu chake Al-Musnadu Al-Imam Musa bin Ja’afar. [61]

Pia kuna vitabu na maandiko mengine yaliyopokewa kutoka kwa Musa bin Ja’afar (a.s), nayo ni kama ifuatavyo:

  • Ali bin Ja’afar, ambaye ni kaka wa Imamu Kadhim (a.s) alikuwa na kitabu kilichokusanya maswali mbali mbali ndani yake, kitabu ambacho alirikodi ndani yake maswali tofauti aliyomuuliza Imamu Kadhim (a.s) na kupokea majibu yake kutoka kwake (a.s). [62] Mada hasa ya kitabu hichi inahusiana na masuala mabali mbali za kifiqhi. [63] Kitabu hicho kimepewa jina la Masuala ya Ali Ibn Ja'afar ambacho baadae kilikuja kukamilishwa na kuchapishwa na Taasisi ya Aal-Al-Bait, kwa jina la Masailu Ali bin Ja'afar wa Mustadrakaatihaa.
  • Pia kuna makala kuhusiana na masuala ya kiakili yalioandikwa kumuelekea Hishaam bin Hakam. [64]
  • Makala juu ya fani ya akida, ambayo ni jawabu ya maswali ya Fat-hu bin Abdullahi. [65]
  • Ali bin Yaqtin pia alikusanya masuala kadhaa aliyojifunza kutoka kwa Imamu Musa bin Ja’afar (a.s). Masuala hayo aliyakusanya katika kitabu kiitwacho Masaail 'An Abi Al-Hasan Musa bin Ja’afar. [66]

Mijadala na Mazungumzo

Makala Asili: Mijadala ya Imam Kadhim (a.s)

Kuna Mijadala na mazungumzo kadhaa yaliyofanyika baina ya Imamu Kadhim (a.s) na baadhi ya Makhalifa wa Bani Abbas, [67] Mayahudi [68] na wanazuoni wa Kikristo, [69] na Abu Hanifah. [70] Mwanahistoria Baqir Sharif Qureshiy amekusanya mazungumzo na majadiliano manane ya Imamu Kadhim (a.s) chini ya kichwa cha habari kilichojumuisha mijadala yake (a.s). [71] Imamu Kadhim (a.s) alijadiliana na Mahdi Abbaasiy kuhusiana na suala la ardhi na bustani ya Fadak, pamoja na uharamu wa mvinyo ndani ya Quran. [72] Vile vile Imamu Kadhim (a.s) aliwahi kuwa na majadiliano kadhaa baina yake na Haruna Abbasiy. Baadhi mijadala hiyo ilitokana na kule Harun kutaka kuonesha kwamba; Nasabu yake inakaribiana zaidi na nasabu ya Mtume (s.a.w.w) kuliko nasabu ya Musa bin Ja’afar, jambo ambalo lilimfanya Imamu Kadhim (a.s) afungue mjadala mbele ya Harun kuhusiana na nasabu yake. Alifanya hivyo ili kumuonesha ukaribu wa nasaba ulioko baina yeke na bwana Mtume (s.a.w.w). [73] Kwa kawaida mazungumzo na majadiliano ya Musa bin Ja’afar na wanazuoni wa dini nyinginezo yalikuwa ni kwa ajili ya kuwajibu maswali yao ya kidini, ambayo hatimaye yaliwapelekea kusilimu kwa wanazuoni hao. [74]

Nyenendo Zake (a.s)

Maisha na Nyenendo za Kiibadi

Kwa mujibu wa vyanzo vya Shia na Sunni, Imamu Kadhim (a.s) alikuwa amejikita kwenye dini kisawasawa; Hiyo ndiyo sababu hasa ya yeye kuitwa Abdu Saleh. [75] [76] Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, Imamu Kadhim (a.s) alikuwa ni mwenye kufanya ibada nyingi mno, kiasi ya kwamba walinzi wake wa jela pia waliathiriwa na tabia hiyo ya kuabudu. [77] Sheikh Mufid amemuhisabu Mussa bin Ja'afar (a.s), kuwa ndiye mcha Mungu zaidi katika watu walioishi katika zama zake. Yeye pia ameripoti ya kwamba; Mussa bin Ja'afar alikuwa akilia sana kutokana na khofu ya Mwenyezi Mungu, kiasi ya kwamba ndevu zake zilikuwa zikirowa kutokana na wingi wa machozi yake. Alikuwa akikariri sana dua isemayo: «عَظُمَ الذَّنْبُ مِنْ عَبْدِكَ فَلْيَحْسُنِ الْعَفْوُ مِنْ عِنْدِكَ» ; “Dhambi zimekithiri kutoka kwa mja wako, basi acha uzuri wa usamehevu wako uje kutoka kwako.” Pia alikuwa akikariri sana katika sijda zake dua isemayo: «اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الرَّاحَةَ عِنْدَ الْمَوْتِ وَ الْعَفْوَ عِنْدَ الْحِسَابِ» ; "Ewe Mola wangu, kwa hakika mimi ninakuomba rehema zako wakati wa mauti, na ninakuomba msamaha wako wakati wa hisabu”.) [78] Hata alipopelekwa jela kwa amri ya Harun, alimshukuru Mwenyezi Mungu. kwa kupata fursa ya kumuabudu Mola wake kwa kusema: “Ee Mwenye Ezi Mungu, siku zote nilikuwa nikikuomba fursa kwa ajili ya ibada, nawe tayari umeshanipa fursa hiyo. Hivyo basi ninakushukuru kwakunipatia fursa hii." [79]

Maandishi yaliokuwa yameandikwa kwenye pete ya Imamu Kadhim (a.s) yalikuwa ni (حَسْبِيَ اللهُ حَافِظِي ; Mungu anatosha kunilinda). [80] (وَالْمُلْكُ لِله وَحْدَهُ ; Na ufalme ni wake yeye peke yake). [81]

Maisha na Nyenendo za Kimaadili

Katika vyanzo vya pande zote mbili; Shia na Sunni, kuna ripoti mbalimbali zinazohusiana na uvumilivu [82] [83] pamoja na ukarimu wa Imamu Kadhim (a.s). [84] [85] Sheikh Mufid amemzingatia yeye kuwa ndiye mkarimu zaidi kuliko wakarimu wote walioishi ndani ya zama za wakati wake, ambapo katika nyakati za usiku, alikuwa akibeba chakula kuwapelekea masikini wa mji wa Madina. [86] Ibn Anba akizungumzia ukarimu wa Imamu Mussa bin Kadhim (a.s), anasema: “Yeye alikuwa akitoka nje ya nyumba yake usiku huku akiwa na mifuko ya dirham, na alikuwa akimpa kila aliyekutana naye njiani, au kila aliyetarajia hisani kutoka kwake. Alifanya hivyo mpaka mifuko yake ya pesa ikawa ni methali kwa watu”. [87] Pia inasemekana kuwa; Mussa bin Ja'afar aliwasamehe waliomdhulumu, na alipojulishwa kuwa kuna mtu anataka kumdhuru, basi yeye alikuwa akimpelekea zawadi. [88] Sheikh Mufid amemuhisabu Imamu Kadhim (a.s), kuwa ndiye mtu mwenye jitihada zaidi katika kuunga udugu baina yake na watu wa familia yake pamoja na jamaa zake. [89]

Sababu hasa ya Imamu wa 7 wa Kishia kupewa lakabu ya Kadhim, inatokana na uwezo wake wa kudhibiti hasira zake. [90] [91] Kuna ripoti mbalimbali kutoka vyanzo tofauti ya kwamba; Imamu Kadhim (a.s) alizikandamiza hasira zake dhidi ya maadui zake, pamoja na wale waliokuwa wakimuudhi. [92] [93] [94]

Kwa habari zaidi, angalia pia: Jina (Kadhim)

Hata Bishr Haafiy, ambaye baadaye alikuja kuwa ni Sheikh wa Kisufi, alitubia kutokana na makosa yake, chini ya ushawishi wa maneno na maadili ya Imamu Kadhim (a.s). [95] [96]

Nyenendo za Kisiasa

Baadhi ya duru zimenukuu zikisema kuwa, Imam Kadhim (a.s) alithibithisha uharamu wa UkhAlifa wa Makhalifa wa Banu Abbas kupitia njia mbalimbali, zikiwemo njia za mijadala na kutoshirikiana nao. Pia alijitahidi kudhoofisha imani za watu juu yao. [97]

  • Alifanya hivyo wakati ambapo, Makhalifa wa Bani Abbas walikuwa wakijaribu kuhalalisha utawala wao kwa kujinasibisha na Mtume (s.a.w.w). Baada ya kulijua jambo hilo, aliitangaza nasaba yake na kuwaonesha kwamba; Yeye yuko karibu zaidi na Mtume Muhammad (s.a.w.w) kinasaba kuliko Bani Abbas.

Miongoni mwa jitihada za kUwadhoofisha watawala hao, ni yale majadilano yaliyofanyika kati ya Harun Abbasi na Imam Kadhim (a.s), ambapo Imamu Kadhim (a.s) akitegea Aya za Qur’an mojawapo ikiwa ni ile Aya ya Mubahalah, aliweza kuwapiku watawala hao kwa kuwathibitishia ukaribu uliopo baina yake na Mtume wa Mwenyezi Mungu, kupitia nasabu ya bibi Fatima (a.s). [98] [99]

  • Wakati Mahdi Abbasi alipokuwa anatoa pesa, ikiwa ni kama fidia za baadhi ya haki za watu alizodhulumu, Imamu Kadhim (a.s) alimdai bustani ya Fadak kutoka kwake. [100] Mahdi Abbasi akamtaka abainishe mipaka ya bustani hiyo ya Fadak, na Imam aliweka mipaka ambayo ilienda sawa na eneo la mipaka ya utawala wa serikali ya Bani Abbas [101]. Alifanya hivyo ili kuwaonesha ya kwamba; si Bustani ya Fadak tu kuwa ndiyo mali ya Ahlu Al-Bait, bali utawala mzima wa serikali ya Makhalifa hao ulistahiki kuwa mikononi mwa Ahlu Al-Bait.
  • Imamu wa 7 wa Mashia (a.s) aliwaamuru Masahaba zake wasishirikiane na Utawala wa Bani Abbas, akiwemo Sahaba wake Safwan Jimaal, ambaye alimkataza kuwakodisha ngamia wake kwa Harun. [102] Wakati huo huo alimtaka Ali bin Yaqtin, ambaye ni Sahaba wake aliyekuwa ni mmoja wa mawaziri wa serikali hiyo, kubaki serikalini kuwasaidia na kuwatumikia Mashia. [103] Imamu Kazim (a.s) alimtaka amhakikishie ya kwamba atawaheshimu marafiki wa Ahlul-Bait (a.s), na Imamu naye akampa dhamana ya kuepukana na kifo cha kidhalimu na kutopata matatizo ya kuigia kifungoni. [104]

Hata hivyo, haijawahi kuripotiwa kwamba MuSsa bin Ja’afar (a.s) alikuwa akipingana na serikali ya wakati huo wazi wazi. Yeye alikuwa ni mtu mwenye kuficha itikadi yake (mwenye taqiyyah), pia akawaamrisha Mashia kufuata njia hiyo. Kwa mfano, katika barua ya taazia ya Khaizran, ambaye ni mama yake Hadi Abbasi, alimpa pole katika barua hiyo kutokana na kifo cha mama yake. [105] Kwa mujibu wa maandiko ya riwaya, Pale Harun alipomUita, yeye alisema: “Kwa kuwa ni wajibu kufanya taqiyaah mbele ya mtawala dhalimu, basi nitakwenda kwa Harun." Vile vile alipokea na kukubali zawadi za Harun kwa ajili ya ndoa ya familia ya Abi Talib. Alipokea zawadi na fedha kutoka kwa utawala huo, ili kusaidia kizazi cha Mashia wake kisije katika, kwani wengi alikuwa hawana uwezo wa kifedha wa kuwawezesha kufunga ndoa na kulea familia zao. [106] Hata katika barua fulani, Imamu Kadhim (a.s) alimtaka Ali bin Yaqtin kwa muda fulani awe anatawadha kama wanavyotawadha Ahlu-Sunnah, alimtaka kufanya hivyo ili aepukane shari. [107]

Imam Kadhim (a.s) na Uasi wa Ma'alawi

Wakati wa uhai wa Mussa bin Ja'afar ulikwenda sambamba na wakati wa Bani Abbas kuchukuwa madaraka, pamoja na uasi wa Ma'alawi dhidi yao. Bani Abbas waliingia madarakani kwa kauli mbiu ya kuwapendelea na kuwaunga mkono Ahlul-Bait, lakini haikuchukua muda mrefu, wao wakageuka kuwa ndio adui mkali wa Alawiyyiina (watu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w)) na wakawaua au kuwafunga wengi miongoni mwao. [108] Ukandamizaji wa serikali ya Abbaasiyyiina dhidi ya kizazi cha Mtume (s.a.w.w) ulipelekea idadi kadhaa ya Alawiyyiina kusimama dhidi ya serikali yao. Uasi wa Shahid Fakh na uasi wa Yahya bin Abdullah, pamoja na uundwaji wa serikali ya Idrisa, ulikuwa ni miongoni mwa na natija ya ukakasi na ukandamizaji wa serikali hiyo. Uasi wa Fakh ulitokea mnamo mwaka wa 169 Hijiria ndani ya zama za Uimamu wa Imamu Musa bin Ja’afar (a.s) katika zama za utawala wa Hadi Abbasi. [109] Imamu Mussa bin Ja’afar (a.s), hakushiriki katika uasi huo, na hakuna msimamo wowote ule wa wazi ulioripotiwa kutoka kwake, kuhusiana na kuunga au kutounga mkono kwake uasi huo. Hata Yahya bin Abdullah alimlalamikia Imamu katika barua yake kuhusiana na kutoungana nao mkono katika uasi wa Tabaristan. [110]

Kwa mujibu wa maoni ya wanahistoria wawili wa madhehebu ya Zaidiyyah, ambao ni Ahmad bin Ibrahim Husni na Ahmad bin Sahli, ni kwamba; Katika karne ya nne Hijiria, wakati wa tukio la Fakh lilipotoke, Imamu Kadhim (a.s) alikuwa Makka kwa ajili ya kuhiji. [111] Kwa mujibu wa ripoti za waandishi wawili hawa, Mussa bin Isa, Mmoja wa watendaji wa ndani wa serikali ya mfumo wa Ukhalifa wa Bani Abbas, alimuita Imamu wakati wa vita hivyo vilipotokea, na Imamu akaenda na kukaa naye hadi mwisho wa kampeni yake. [112] Kwa mujibu wa ripoti hii, baada ya kampeni hiyo kumalizika, wakati Imam alipoelekea Mina, aliletewa vichwa vya miongoni mwa waasi hao vilivyokatwa. [113] Kwa mujibu wa riwaya ya Abul Faraj Isfahani, Imam Kadhim (a.s) alipokiona kichwa cha Saahib Fakh, alisoma Aya ya 'Estirjaa' (Aya ya 156 ya Surat al-Baqarah), huku akitaja mazuri yake. Imamu (a.s) alimhisabu mwenye kichwa hicho kuwa ni mtu muadilifu. [114] Kwa mujibu wa ripoti ya Baihaqi katika kitabu chake Lubab Al-Ansab, baada ya kifo cha Saahib Fakh, Imamu Kadhim (a.s) aliusalia mwili wa mpambanaji huyo. [115]

Kwa mujibu wa kile alichokinukuu Sayyied Ibn Taawuus kutoka kwa wanazuoni wa Kishia wa karne ya 7 Hijiria, ni kwamba; Hadi Abbasi ameuhisabu uasi wa Sahib Fakh kuwa ulitendeka kupitia amri ya Imamu Kadhim (a.s). [116] Ila kulingana na riwaya fulani iliyonukuliwa na Kulaini katika kitabu cha Al-Kafi, pale Saahibu Fakh aliposimama dhidi ya serikali, alimuita Imamu Kadhim (a.s) kumuunga mkono kwa kumpa kiapo cha ahadi ya utiifu, ila Imamu aliikataa kutoa ahadi hiyo, na kumtaka asiendelee kumtaka ampe ahadi hiyo ya kiapo cha utiifu, naye akakubali kutosisitiza suala hilo. [117] Abdullahi Mamqani anaamini kwamba; kiapo cha utiifu alichotaka Sahib Fakh kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s), kilikuwa ni kiapo cha dhahiri tu, ambapo kwamba, iwapo yeye angelifaulu katika uasi wake huo, na kuitia mikononi serikali ya Bani Abbas, basi alikuwa na nia ya kumkabidhi Imamu Kadhim (a.s) hatamu za serikali hiyo. Kwa hiyo, kule Imam kumkataza asiasi, kulikuwa na maana ya taqiyyah tu, lakini kiundani, Imamu (a.s) alikuwa aameridhika na kitendo chake hicho. Na dalili wazi ya jambo hilo, kule yeye kumuombea dua ya rehema baada ya kufa kwake kishahidi. [118] Kwa upande mwingine kuna baadhi ya watafiti wanaoamini ya kwamba; Inagawaje kuna riwaya zinazomuunga Saahibu Fakh, ila riwaya hizo si dalili za kuungwa mkono na Maimamu wa Kishia. [119] Ingawaje Rasul Jafarian, mhakiki na mwanahistoria wa karne ya 15 Hijiria, ameuhisabu uasi wa Fakh kuwa ni miongoni mwa uasi salam na madhubuti zaidi dhidi ya utawala wa Bani Abbas, ila anaamini ya kwamba; hakuna uhakika kama uasi huo ulipata baraka na idhini kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s). Wala hakuna dalili inayoonesa kuwa uasi ulitekelezwa kwa amri ya Imamu Kadhim (a.s). Kinyume chake, inaweza kusemwa ya kwamba; Mashia wanaoamini Maimamu 12 hawakukubaliana na uasi huo, kwa sababu waasi hao walikuwa wakisuguana na Ma'alawiy katika suala hilo la uasi wao huo, jambo ambalo lilisababisha kukazuka khitilafui kati yao. [120]

Jela

Mara kadhaa Imam Kadhim (a.s) alipewa wito kutoka serikalini na kutiwa kiauizini, na hatimaye kufungwa na Makhalifa wa Banu Abbas. Kwa mara ya kwanza kabisa Imam Kadhim (a.s), akiwa katika zama za Ukhalifa wa Mahdi Abbasi, alihamishwa kutoka Madina na kupelekwa kifungoni Baghdad kwa amri ya Khalifa huyo. [121] Harun pia alimfunga Imamu (a.s) mara mbili tofauti. Haijulika kihistoria tarehe hasa ya kukamatwa kwa Imamu (a.s) katika mara yake hiyo ya kwanza na kuingizwa gerezani. Ila mara ya pili ya kukamatwa kwake, ilikuwa ni tarehe 20 Shawwal ya mwaka 179 Hijiria, akiwa huko Madinah. [122] Pia alikamatwa kwa mara nyingine tena, mnamo tarehe 7 Dhul Hijjah akiwa huko Basra katika nyumba ya Issa bin Ja'afar. [123] Kwa mujibu wa riwaya ya Sheikh Mufid, mnamo mwaka wa 180 Hijiria, Harun alimtumia barua Isa bin Ja’afar, akiimtaka amuue Imamu Kadhim (a.s), lakini yeye alikataa kutekeleza amri hiyo. [124] Baada ya muda, Imamu alihamishswa na kupelekwa kwenye jela ya Fadhlu bin Rabbi, iliyoko huko Baghdad. Maisha ya mwisho ya Imam Kadhim (a.s) yalimalizikia katika magereza ya Fadhlu bin Yahya na Sindi bin Shaahik. [125]

Katika kitabu cha ziara cha Imam Kadhim (a.s), kuna ibara isemayo: (الْمُعَذَّبِ فِي قَعْرِ السُّجُون) "Ewe Mola sala na salamu zako zimshukia walii wako Musa bin Ja'afar..... Mtu aliyeteswa ndani ya mashimo ya jela..." [126] Pia katika kitabu hicho kuna ibara iliyozisifu jela alizofungwa ndani yake kupitia ibara isemayo. (ظُلَم‌ المطامیر) Maana ya Dhulam Al-Matamiir; Ni Gereza lenye mfumo wa shimo kama kisima, kwa namna ambayo haiwezekani kunyoosha miguu yako na kulala ndani yake. Pia, kutokana na Baghdad kuwa iko karibu na Mto Tigris, hivyo basi magereza hayo ya chini ya ardhi yalikuwa na unyevunyevu wa kiasili. [127]

Kuna ripoti tofauti kuhusiana na sababu hasa ya kukamatwa Imam wa 7 wa Kishia kupitia amri za Makhalifa wa Bani Abbas na kupelekwa jela. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, sababu ya kukamatwa kwa Mussa bin Ja’afar kupitia amri ya Harun, ilitokana na hasadi ya Yahya Barmaki na chokochoko za Ali bin Ismail bin Jafar, ambaye ni mtoto wa kaka yake Harun. Harun alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na Imamu (a.s) kuwa anajenga uhusiano baina yake na Mashia, na hilo lilikuwa ni moja kati ya mambo yanayomtisha Harun, na kudhani ya kuwa; uhusiano huo unaweza kupelekea kudhoofika kwa serikali yake. [129] Pia, kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, sababu ya kufungwa kwa Imamu Kadhim (a.s), ilikuwa ni kule baadhi ya Mashia kutoficha imani zao mbele ya maadui zao. Kwa mfano; ingawa Imamu (a.s) alimuaru Hisham bin Hakam afanye taqiyyah (afiche imani yake), ila yeye hakushikamana na amri hiyo. [130] Pia ripoti hizo zimeeleza ya kwamba; Moja kati ya sababu zilizopelekea Imamu Kadhim (a.s) kutiawa ndani, ni ile mijadala ya Hisham Ibn Hakem. [131]

Kifo cha Kishahidi

Maombolezo ya kuuawa shahidi Imamu Kazim (a.s) katika haram ya kaadhimein

Siku zake za mwisho za maisha yake Imamu Kadhim (a.s) alimazia katika kutumikia jela ya Sindi Bin Shaahik. Sheikh Mufid alisema kwamba; Imamu (a.s) alipewa sumu na Sindi kupitia amri ya Harun Al-Rashid, sumu ambayo ilimpelekea Imamu kuuawa kishahidi siku tatu baada ya kupewa sumu hiyo. [132] Kauli maarufu zaidi kuhusiana na kifo chake [133] cha kishahidi, ni kwamba; kifo hicho kilitokea siku ya Ijumaa ya mwezi 25 Rajab, mwaka 183 Hijiria huko Baghdad. [134] Kulingana na nukuu za za Sheikh Mufid, kifo cha kishahidi cha Imamu Kadhim (a.s) kilitokea tarehe 24 Rajab. [135] Pia kuna maoni mengine tofauti na hayo kuhusian na wakati na mahali pa kifo chake cha kishahidi (a.s). Vile vile kuna kauli nyingine zisizokuwa hizo, kuhusiana na tokeo hilo la kifo chake (a.s). Miongoni mwa kauli hizo ni ile kauli iliyonukuu kifo hicho kutokea mnamo mwaka 181, na ile iliyoashiria mwaka wa 186 Hijiria. [136] [137] Mwandishi wa kitabu Al-Manaqibu akinukuu kutoka katika kitabu Akhbaru Al-Khulafa cha Suyuti, ameripoti kwamba; Sababu hasa iliyopelekea Imamu kukamatwa na kutiwa kizuizini na hatimaye kuuwawa, inatokana na lile tukio la Mahdi Abbas la kumtaka Imamu ainishe mipaka ya bustani ya Fadak, na badala yake, Imamu (a.s) akauashiria utawala wote wa Abani Abbas kuwa ndiyo mipaka halisi ya eneo la Ahlul-Bait. Jambo ambalo lilipelekea Haruna Rashid kukasirika, na akamwambia Imamu (a.s), "kila kitu umekitia ndani ya matakwa ya mipaka ya milki yako, na wala hujatuachia kitu". Hilo basi ndilo lililomfanya Haruna Al-Rashid kumuuwa Imam Kadhim (a.s). [138]

Baada ya Mussa bin Ja'afar (a.s) kuuawa kishahidi, Sindi bin Shaahik aliwaita baadhi ya wanachuoni maarufu wa Baghdad na kuwaonesha mwili wa Imamu Mussa bin Ja’afar (a.s) ili wauone, na washuhudie kuwa mwili huo hauna alama yoyote ile ya majaraha yanayoashiria kuteswa. Alifanya hivyo ili ionekane kuwa Imam (a.s) alikufa kifo cha kawaida. Pia, kwa amri yake yeye, mwili wa Imamu (a.s) uliwekwa kwenye daraja la Baghdad na wakatangaza ya kwamba, Mussa bin Ja'afar amekufa kifo cha kawaida. [139] Kuna ripoti tofauti kuhusu jinsi ya yeye alivyouawa kishahidi; Wanahistoria wengi wanaamini kwamba; Yahya bin Khalid na Sindi bin Shaahik walimpa sumu. [140] [141]

Kuna sababu mbili zilizotolewa kuhusiana na kuuweka mwili wa Imamu Kadhim (a.s) hadharani: Ya kwanza ni kuthibitisha kwamba Imamu (a.s) alikufa kifo cha kawaida, na nyingine ni kubatilisha imani ya wale walioamini Umahdi wake (yaani kubatilisha nadharia ya kuwa yeye ndiye Imam Mahdi, ambaye ni Imamu atakayesimama kutetea haki na kusimamisha serikali halali ya Kiislamu). [143]

Mwili wa Mussa bin Ja’afar (a.s) ulizikwa kwenye makaburi ya familia ya Mansuri Dawaaniiq, yaliyojulikana kama ni makaburi ya Waquraishi. Inasemekana ya kwamba, sababu ya Bani Abbas kuizika maiti ya Imamu Kadhim (a.s) katika mava hiyo, inatokana na khofu ya Bani Abbas kudhani ya kwamba, iwapo Imamu (a.s) atazikwa sehemu nyingine isiyokuwa hiyo, basi Mashia wataitumia sehemu hiyo kama ndiyo makao makuu yao ya kukutana ndani yake. [145]

Kaburi Lake

Nakala Asili: Makaburi ya Kadhimeini

Makaburi ya Imamu Kadhim na Imamu Jawad (a.s) yapo katika eneno la kitongoji cha Kadhimeini kilichoko karibu na mji wa Baghdad, nayo ni sehemu maarufu inayotembelewa na Waislamu tofauti -hususan Mashia- kwa nia ya kuzuru makaburi hayo. Tukizingatia riwaya iliyopokewa kutoka kwa Imamu Ridha (a.s), malipo ya kuzuru kaburi la Imamu huyu (a.s), ni sawa na malipo ya kuzuru makaburi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w), Imamu Ali (a.s), pamoja na kaburi la Imamu Hussein (a.s). [146]

Masahaba na Mawakala

Makala Asili: Orodha ya Masahaba wa Imamu Kadhim (a.s)

Kuna khitilafu baina ya wanazuoni kuhusu idadi halisi ya Masahaba wa Imamu Kadhim (a.s), na wala hakuna taarifa madhubuti kuhusu idadi yao. Sheikh Tusi ameorodhesha idadi watu 272 ambao ni Mashaba wa Imamu Kadhim (a.s). [147] Al-Bariqiy naye ametathmini idadi ya Masahaba hao, kuwa ni idadi ya watu 160. [148] Baaqir Sharif Quraishiy ameikanusha na kuipinga kauli ya Al-Barqiy iliyonukuu idadi ya Masahaba 160, huku yeye mwenyewe akinukuu idadi ya Watu 321 na kuwatajwa kuwa ndio Masahaba wa Imamu Kadhim (a.s). [149] Miongoni mwa Masahaba maarufu wa Imamu Kadhim (a.s), ni; Ali bin Yaqtin, Hishaam bin Hakam, Hishaam bin Salim, Muhammad bin Abi 'Umair, Hammad bin ‘Issa, Yunus bin Abdul Rahman, Safwan bin Yahya na Safwan Jamaal, ambapo Baadhi yao wamezingatiwa kuwa ni miongoni mwa As-habu Al-Ijmaa. [150] Yaani; (Ni wanazuoni ambao wanamakubaliano maalumu ya ndani ya baadhi ya tungo za fani ya sheria). Baada ya Imam Kadhim (a.s), akiwemo Ali ibn Abi Hamzah Batainiy, Ziyad bin Marwan, na Othman bin ‘Issa, hawakuukubali Uimamu wa Ali bin Musa Al-Ridha (a.s). Nao walikomea kwenye Uimamu wa Imamu Mussa bin Ja’afar bila ya kuendelea mbele. [151] Kundi lao hilo baadae lilikuja kujulikana kwa jina la Waqifiyyah. Baada ya kupita kipindi fulani, baadhi yao walirudi nyuma na kukubaliana na Uimamu huo wa Ali bin Musa Al-Ridha (a.s). [152]


Mtandao wa Mawakala

Makala Asili: Umoja wa Mawakala

Ili kuwasiliana na Mashia na kuimarisha uwezo wao wa kiuchumi, Imam Kadhim (a.s) alipanua ushirika na umoja wa mawakala uliloanzishwa wakati wa Imam Swadiq (a.s). Yeye aliwatuma baadhi ya Masahaba wake kama ni mawakala wake katika mikoa mbalimbali. Vyanzo vya kihistoria vimerikodi na kunukuu majina ya watu 13 waliokuwa ni mawakala wa Imamu Kadhim (a.s). [153] Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo hivyo vimewataja; Ali bin Yaqtin na Mufadhal bin Umar huko Kufa kuwa ndio mawakala wa mji huo wa Kufa. Abdul Rahman bin Hajjaj alitajwa kuwa ni wakala wa Baghdad, Ziyad bin Marwan alikuwa ni wakala wa Kandahar, Othman bin Issa ni wakala wa Misri, Ibrahim bin Salam ni wakala wa huko Neishabur, na Abdullah bin Jundab akiwa ni wakala katika mji wa Ahvaz. [154]

Kuna ripoti kadhaa katika vyanzo vilivyonukuu historia na maandiko mbali mbali ya kwamba; Mashia walikuwa wakitoa na wakipeleka khumsi zao ima kwa Imam Kadhim (a.s) au wakiwapa wawakilishi (mawakala) wake. Sheikh Tusi anaamini ya kuwa; Sababu iliyowafanya baadhi ya mawakala wa Imam Kadhim (a.s) kujiunga na kundi la Waaqifiyyah, inatokana na wao kudanganyika na mali walizokuwa wakizikusanya kwa niaba ya Imamu (a.s). [155] Katika ripoti iliyopelekea Imamu kutiwa kizuizini na kufungwa jela, ilitokana na Ali bin Ismail bin Ja’afar kumwandikia barua Harun, akisema; Kuna mali nyingi zilioje anazotumiwa Imamu Kadhim (a.s), kutoka mashariki na magharibi, na ana hazina na baitul-mali iliyojaa ndani yake aina mbalimbali za sarafu. [156]

Mawasiliano kupitia barua, ilikuwa ni moja kati ya njia kadhaa za Imamu Kadhim (a.s) katika kufanya mawasiliano na Mashia wake, barua ambazo zilibeba aina tofauti za ujumbe; kama vile masuala ya kisheria, imani, mawaidha, dua, pamoja na masuala mengine yanayohusiana na masuala ya mawakala wake. Imeripotiwa kuwa, hata alipokuwa gerezani, aliendelea kuwasiliana na wafuasi wake kupitia mfumo wa barua, [157] pia alikuwa akiwajibu maswali yao yanayowakwaza, kupitia njia hiyo hiyo ya barua. [158] [159]

Nafasi yake Mbele ya Sunni

Masunni wanamheshimu sana Imamu wa saba wa Shia na kumhisabu kama ni mwanachuoni wa kidini. Baadhi ya wakuu na viongozi wa madhehebu ya Sunni wameonekana kumsifu Imamu Kadhim (a.s) kwa sifa kadhaa za elimu na kimaadili. [160] Pia viongozi hao wamezungumzia sifa za uvumilivu wake, ukarimu wake, wingi wake wa ibada, pamoja na sifa nyinginezo za kimaadili. [162] Kuna ripoti zinazoonesha kwamba; Baadhi ya wanazuoni wa Kisunni kama vile Sam-'aani, ambaye ni mwanahistoria, mpokezi wa Hadithi na faqihi wa madhehebu ya Shafi'i wa karne ya 6 Hijiria, alikuwa akilizuru kaburi la Imam Kadhim na kutawassal kutoka kwake. [163] (Yaani kumuomba Mungu matilaba yake kupitia jina na utukufu wa Imamu huyo). Abu Ali Al-Khallaal, mmoja wa wanachuoni wa Kisunni wa karne ya tatu Hijiria, alisema ya kwamba; "Kila nilipokuwa na tatizo fulani, nilikuwa nikilizuru kaburi la Musa bin Ja’afar na kutawassal kwake, na baada ya hapo tatizo langu litatatuka. Imepokewa kutoka kwa Imamu Shafi'i aakisema; kaburi la Musa bin Ja'afar ni "dawa yenye kuponya". [165]

Orodha ya vitabu

Makala Asili: Orodha ya vitabu kuhusu Imam Kadhim (a.s)

Kuna kazi na maandiko mengi yalioandikwa kuhusu Imamu Kadhim (a.s), kazi zote hizo zimerikodiwa katika mfumo wa vitabu, nadharia, na makala katika lugha mbalimbali. Rikodi za kazi hizo ni imefikia idadi ya kazi 770. [166] Kazi zilizofanywa na kuandikwa kupitia maandiko mbali bamli, zimehifadhiwa katika mijalada maalu ya vitabu.

Vitabu vilivyosajili na kurikodi kazi zinazohusiana na Imam Kadhim (a.s), ni: Kitabnameh Imamu Kadhim (a.s), [167] Kitabshenasi Kadhimaini, [168] na makala za Kitabshenasi Imam Kadhim (a.s). [169] Mada ya nyingi zilizorikodi ndani ya mijalada hiyo, zimejikita zaidi kuhusiana na maisha pamoja na shakhsia ya Imam wa 7 wa Kishia. Pia, kuna kongamano lililopewa jina la "Maisha na Nyakati za Imamu Kadhim (a.s)" lilifanyika nchini Iran mwezi Februari 2013, ambapo makala za kongamano hilo zimechapishwa kwa jina la mkusanyiko wa makala za Kongamano la Maisha ya Imam Kadhim (a.s). [170]

Kitabu Musnad Al-Imam Al-Kadhim cha Azizullah Ataaridiy, Babu Al-Hawaij Imam Musa Al-Kadhim cha Hussein Haj Hassan, Hayatu Imam Musa bin Ja'afar cha Muhammad Baqir Sharifiy Quraishiy, Imam Al-Kadhim (a.s) 'Inda Ahlu-sunnah cha Faris Hassun, na kitabu Siratu Al-Imami Musa Al-Kadhim cha Abdullah Ahmad Yusuf, ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na Imamu Kadhim (a.s).

Rejea

Vyanzo

  • Abū l-Faraj al-Isfahānī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Maqātil al-ṭālibīyyīn. Beirut: Dār al-Maʿrifa, n.d.
  • Amīn, Sayyid Muḥsin al-. Aʿyān al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Taʿārīf, 1403 AH.
  • Amīn, Sayyid Muḥsin. Sīrah-yi Maʿṣūmān. Translated by ʿAlī Ḥujjatī Kirmānī. Tehran: Surūsh, 1376 Sh.
  • ʿAṭārudī, ʿAzīz Allāh. Musnad Imām al-Kāẓim. Mashhad: Āstān-i Quds-i Raḍawī, 1409 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Minḥāj al-kirāma fī maʿrifat al-imāma. Mashhad: Muʿassisi-yi ʿĀshūrā, 1379 Sh.
  • Ibn Abī l-Ḥadīd, ʿAbd al-Ḥamīd b. Hibat Allāh. Sharḥ nahj al-balāgha. Qom: Kitābkhānih-yi Āyat Allāh Marʿashī, n.d.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1385 AH.
  • Ibn al-Jawzī, Yusuf b. ʿAbd Allāh. Tadhkirat al-khawāṣṣ. Qom: Manshūrāt al-Sharīf al-Raḍī, 1418 AH.
  • Ibn ʿInaba, Aḥmad b. ʿAlī. ʿUmdat al-ṭālib fī ansāb Āl Abī Ṭālib. Qom: Anṣārīyan, 1417 AH.
  • Ibn Shahrāshūb, Muḥammad b. ʿAlī. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Qom: ʿAllāma, 1379 AH.
  • Irbilī, ʿAlī b. ʿIsā al-. Kashf al-ghumma. Qom: al-Raḍī, 1421 AH.
  • Jabbārī, Muḥammad Riḍā. Sāzmān-i wikālat. Qom: Muʾassisi-yi Imām Khomeini, 1382 Sh.
  • Jaʿfarīyān, Rasūl. Ḥayāt-i fikrī wa sīyāsī-yi Imāmān-i Shīʿa. Qom: Anṣārīyān, 1381 Sh.
  • Kashshī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Rijāl. Mashhad: Muʾassisi-yi Nashr-i Dānishgāh-i Mashhad, 1409 AH.
  • Khaṭīb al-Baghdādī, Aḥmad b. ʿAbd al-Maj¬¬īd al-. Tārīkh Baghdād. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1417 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Baqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Ithbāt al-waṣīyya. Translated by Muḥammad Jawād Najafī. Tehran: Islāmīyya, 1362 Sh.
  • Mufīd, Muḥammad b. Nuʿmān al-. Al-Irshād. Qom: Kungiri-yi Shaykh-i Mufīd, 1413 AH.
  • Nawbakhtī, al-Ḥasan b. Mūsā al-. Firaq al-Shīʿa. Beirut: Dār al-Awḍāʾ, 1404 AH.
  • Pīshwāyī, Mihdī. Sīra-yi pīshwāyān. Qom: Muʾassisi-yi Imām Ṣādiq, 1372 Sh.
  • Qarashī, Bāqir Sharīf al-. Ḥayāt al-Imām Mūsā b. Jaʿfar. Qom: Mihr-i Dildār, 1429 AH.
  • Qummī, Shaykh ʿAbbās. Al-Anwār al-bahīyya. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1417 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Tawḥīd. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1398 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Kamāl al-dīn wa tamām al-niʿma. Tehran: Islāmīyya, 1395 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿUyūn akhbār al-Riḍā. Tehran: Nashr-i Jahān, 1378 AH.
  • Samʿānī, ʿAbd al-Karīm b. Muḥammad al-. Al-Ansāb. Hyderabad: Majlis Dāʾirat al-Maʿārif al-ʿUthmānīyya, 1404 AH.
  • Shabrāwī, Jamāl al-Dīn al-. Al-Itḥāf bi-ḥubb al-ashrāf. Qom: Dār al-Kitāb, 1423 AH.
  • Shūshtarī, Muḥammad Taqī al-. Risāla fī tawārīkh al-Nabī wa l-Āl. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1423 AH.
  • Ṭabarī al-Shīʿī, Muḥammad b. Jarīr al-. Dalāʾil al-Imāma. Qom: Biʿthat, 1403 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan. Iʿlām al-warā bi-aʿlām al-hudā. Mashhad: Āl al-Bayt, 1417 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Fihrist. Qom: Maktibat al-Muḥaqiq al-Ṭabāṭabāʾī, 1420 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Ghayba. Qom: Dār al-Maʿārif al-Islāmīyya, 1411 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Rijāl. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1415 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Tahdhīb al-aḥkām. Qom: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.