Nenda kwa yaliyomo

Ahlul-Bayt (a.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Ahlul-Bait)
Makala hii ni kuhusu Ahlul-Bayt (a.s). Kama unataka kuwafahamu Maimamu 12 na Maasumina 14 (a.s), angalia makala ya Maimamu wa Waislamu wa Kishia na Maasumina 14.
Hadith ya Thaqalein (Qur'an & Ahlul-bayt(a.s))

Ahlul-Bayt (a.s) (Kiarabu: أهل البيت (ع)) familia ya Mtume na watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w) ambao wanakusudiwa katika fasihi na vitabu vya Kishia ni Maasumina 14. Vielelzo na vigezo vingine vya Ahlul-Bayt ambavyo vimebainishwa ni kama Ahlul-Kisaa (watu wa shuka au Kishamia) na wake za Mtume.

Katika vitabu na vyanzo vya Kishia kumenukuliwa fadhila mbalimbali, sifa maalumu na haki za Ahlul-Bayt (a.s). Kwa mujibu wa itikadi ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia ni kwamba, Ahlul-Bayt (a.s) yaani watu wa nyumba ya Mtume wana daraja ya Umaasumu (hali ya kutotenda dhambi), wana daraja ya juu na ni watu bora kuliko masahaba wote wa Mtume (s.a.w.w) bali ni wabora kuliko viumbe wengine wote na kwamba, Wilaya (uongozi) na usimamizi wa jamii ya Kiislamu uko mikononi mwao na Waislamu wanapasa kuwatambua hawa kuwa ni marejeo yao katika mafundisho yote ya dini, kuwatanguliza na kuwafanya kuwa viongozi wao.

Kadhalika kwa mujibu wa vyanzo vya Kishia ni wajibu kwa Waislamu kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s) na hilo limetambulishwa katika hadithi kwamba ni msingi wa Uislamu. Aya ya Tat’hir (utakaso), Aya ya Mawaddah na Hadithi al-Thaqalayn (vizito viwili), Safina na Amani au hadithi ya Nujum (nyota) ni miongoni mwa Aya na hadithi mashuhuri katika mlango wa fadhila za Ahlul-Bayt (a.s).

Licha ya kuwa Ahlu-Sunna wanatofautiana kimtazamno na Mashia kuhusiana na mifano na vielezo vya Ahlul-Bayt, lakini akthari yao wamewataja Ahlul-Kisaa (watu wa Kishamia) kwamba, ni miongoni mwa mifano na vielelezo vya wazi vya Ahlul-Bayt na wamenukuu fadhila zao; miongoni mwa fadhila hizo ni wajibu wa kuwapenda, kuharamishwa kuwaudhi na kuwafanyia uadui, kuwa na fadhila bora na daraja ya juu watu wa Kishamia, kuwa marejeo ya elimu na kuwa kwao Maasumu (wasiotenda dhambi). Kumeandikwa vitabu mbalimbali na Waislamu kuhusiana na Ahlul-Bayt kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiarabu na Kiurdu.

Nafasi na Umuhimu Wao

The names of Ahl al-Bayt (a.s) written in thuluth, Islamic calligraphy.

Inaelezwa kuwa, Waislamu wote kuanzia mwanzoni mwa Uislamu ukiacha watu wachache kama manaswibi (wenye chuki na uadui na Imam Ali au mmoja wa Ahlul-Bayt) walikuwa na wamekuwa na mapenzi maalumu na Ahlul-Bayt wa Mtume na wanakubaliana juu ya nafasi na daraja yao ya juu ya elimu na matendo; hata hivyo baina ya makundi ya Kiislamu, Mashia wanatambulika kuwa wafuasi wa Ahlul-Bayt na wameondokea kuwa mashuhuri katika hili. [1] Mashia kutokana na kuwa na itikadi na Ahlul-Bayt na kuwa wafuasi wao, fikra na mitazamo yao inafahamika kwa jina la Maktaba ya Ahlul-Bayt (a.s). [2] Kadhalika maktaba ya Kifiq’h ya Kishia inatajwa na kufahamika kwa jina la Maktaba ya Kifiq’h ya Ahlul-Bayt (a.s). [3]

Hoja na itibari ya Sunna za Mtume (kauli, kitendo na taqrir –kufanywa jambo mbele yake na kulinyamazia-) ni mambo ambayo Mashia na Masuni wanaafikiana katika hilo na wanahesabu kuwa, Sunna za Mtume ni moja ya vyanzo vya kutolea (kunyambulia) hukumu za kisheria; hata hivyo Mashia kinyume na Masuni na kwa mujibu wa Aya na hadithi za Mtume, wao wanazihesabu Sunna za Ahlul-Bayt (Maimamu na Bibi Fatma) pia kwamba, nazo ni hoja na ni moja ya vyanzo na hoja za hukumu za kisheria. [4]

Mashia wanaamini kwamba, Uislamu ambao unatambulishwa katika Maktaba ya Ahlul-Bayt ni Uislamu halisi, kamili na jumuishi. [5] Katika vyanzo vya Kishia na Kisuni kuna hadithi nyingi zilizonukuliwa katika mlango wa fadhila, sifa maalumu na haki za Ahlul-Bayt (a.s). [6] Mtume (s.a.w.w) mara chungu nzima alimrisha kulindwa na kuheshimiwa Ahlul-Bayt. [7]

Kumeandikwa vitabu na makala chungu nzima na Waislamu iwe ni Masuni au Mashia na kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiarabu na Kiurdu zikizungumzia Ahlul-Bayt (a.s). [8] Waislamu hususan Mashia, daima wamekuwa wakionyesha huba na mapenzi yao yasiyo na kifani kwa Ahlul-Bayt (a.s) kupitia njia mbalimbali kama vile kufanya maombolezo katika masiku ya huzuni ya Ahlul-Bayt [9] na kuonyesha furaha na bashasha katika masiku yao ya furaha. [10] Kuna mashairi [11] na athari mbalimbali pia za kisanaa kama kaligrafia (sanaa ya kuandika vizuri na kurembesha maandishi) [12] kuhusiana na Ahlul-Bayt. Miongoni mwa mashairi mashuhuri kuhusiana na Ahlul-Bayt ni beti zilizotungwa na Ferdowsi, [13] Sa'adi [14] na mashairi ya Imam Shafi’i mmoja wa mafakihi wa wa madhehebu manne ya Kisuni ambapo anasema katika beti zake hizo: “Enyi Ahlul-Bayt kuwapenda nyinyi ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo ameishusha ndani ya Qur’an”. [15]

Waislamu na hususan Mashia wamekuwa wakizingatia sana suala la kuwapa watoto wao majina ya Ahlul-Bayt. [16] Zaidi ya hayo, Waislamu wamevipa vituo mbalimbali vya kielimu jina la Ahlul-Bayt. Kwa upande wa vyuo vikuu ni kama Chuo Kikuu cha Ahlul-Bayt cha Tehran, [17] Chuo Kikuu cha Aal Beyt katika nchi ya Jordan, [18] na taasisi kama Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), [19, na misikiti mbalimbali [20] imejengwa na kuitwa kwa jina la Ahlul-Bayt. Kadhalika jina la Ahlul-Bayt limetumika katika bendera na maandishi ya kidini. [21]

Utambuzi wa Maana (Conceptology)

Ali Rabbani Golpeygani anasema, makusudio ya Ahlul-Bayt katika vyanzo vya Kishia kama kutatajwa bila qarina (kiashirio cha uhusiano) ni kundi la familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w) ambao wana nafasi na daraja maalumu ambapo maneno na matendo yao ni kigezo cha haki na dira ya uongofu. [22]

Raghib Esfahani amesema, inapotajwa Ahlul-Bayt kwa sura mutlaki (bila ya sharti) makusudio huwa ni familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w) na wao wanatambulika kwa istilahi hii. [23] Kwa mtazamo wa Hassan Mustafawi, mfasiri na mhakiki wa Ulul al-Qur’an na Muhammad Muhammadi Reyshahri, mtafiti wa hadithi ni kwamba, maana halisi na jumuishi ya ahli ni mtu wa karibu na mwenye mfungamano na mtu ambaye huitwa kwa jina la ahli wake na inatofautina kwa mujibu wa uimara na udhaifu. Mwenza, watoto, wajukuu na mkwe wote wanahesabiwa kuwa ni ahli (aila). [24] Kadhalika umma wa kila Mtume ni ahli wa Mtume huyo yaani aila na watu wake, na wakazi wa nyumba au mji pia wanahesabiwa kuwa ni watu wa nyumba na mji huo. [25]

Ahlul-Bayt katika lugha imekuja kwa maana ya wakazi wa nyumba; [26], hata hivyo Hassan Mustafawi anasema kuwa, makusudio ya neno Ahlul-Bayt ni aina na familia na siyo nyumba. [27]

Vielelezo

Kuhusiana na kwamba, Ahlul-Bayt ni akina nani, Maulamaa wa Kishia na Kisuni wametaja mifano na vielezo mbalimbali:

Ahlul-Kisaa (Kishamia)

Kwa mujibu wa nukuu ya Fadhl bin Hassan Tabarsi ni kwamba, Waislamu wana ijma'a (kauli moja) kwamba, makusudio ya Ahlul-Bayt katika Aya ya Tat’hir (utakaso) ni watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SWT), na kwa mujibu wa hadithi za pande mbili na kwa mtazamo wa Mashia, Aya hiyo inawahusu Mtume (s.a.w.w), Ali (a.s), Fatma (a.s), Hassan (a.s) na Hussein (a.s). [28] Allama Tabatabai, mwandishi wa Tafsir al-Mizan amesema katika ufafanuzi wake chini ya Aya ya utakaso kwamba, neno Ahlul-Bayt katika ada ya Qur’an ni jina makhsusi na linaitwa watu watano; licha ya kuwa katika ada na mazoea jumla, linatumika pia kwa familia yote. [29]

Kwa mtazamo wa Hassan Mustafawi ni kwamba, Ahlul-Bayt katiika Aya ya utakaso (Tat’hir) anajumuishwa na Mtume mwenyewe; kwani kinyume na mtazamo wa baadhi ya wafasiri, neno Ahlul-Bayt halijaongezwa katika neno Rasulullah. [30]

Maasumina 14

Kwa mujibu wa Rabbani Golpeygani ni kwamba, katika vitabu vya Kishia, kila mara kunapotajwa jina la Ahlul-Bayt bila qarina (kiashirio cha ufuasiano) wakusudiwa huwa ni kundi maalumu na makhsusi la familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambao wana sifa maalumu ya Umaasumu (kutotenda dhambi) na mfano na kielelezo chao kwa mujibu wa Aya na hadithi mbalimbali ni Maasumina 14. [31] Katika baadhi ya hadithi pia Maimamu wote wa Kishia wametambulishwa kuwa ni kielelezo cha Ahlul-Bayt. [32] Miongoni mwa hadithi hizo ni pale Mtume (s.a.w.w) alipoulizwa: Ahlul-Bayt wako ni akina nani? Mtume akajibu kwa kusema: “Ni Ali, watoto wangu wawili Hassan na Hussein na Maimamu wengine tisa kutoka katika kizazi cha Hussein (as)”. [33]

Imeelezwa kuwa, kwa mujibu wa itikadi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Imamiyah na wanazuoni wengi wa Kisuni, Maimamu wote wa Kishia wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya Ahlul-Bayt wa Mtume. [34] Muhammad Muhammadi Reyshahri anaamini kwamba, kwa kuzingatia mlolongo na madhumuni ya Aya ya Tat’hir (utakaso) na hatua zilizochukuliwa na Mtume katika kuwatambulisha watu wa nyumbani kwake (Ahlul-Bayt) na kadhalika ishara zingine zilizopo, hakuna shaka kwamba, makusudio ya Ahlul-Bayt katika Aya hii ni kundi maalumu la familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambalo limekabidhiwa uongozi wa umma baada ya Mtume. [35]

Wake za Mtume (s.a.w.w)

Baadhi ya wafasiri wa Ahlu-Sunna, wamesema kuwa, misdaqi na kielelezo cha Ahlul-Bayt katika Aya ya Tat’hir ni wake za Mtume tu. [36] Baadhi ya wanazuoni wengine wa Kisuni wamewatambua watu watano (Ahlul-Kisaa) na wake wa Mtume (s.a.w.w.) kuwa wao ni kigezo na kielelezo cha Ahlul-Bayt katika Aya ya Utakaso. [37] Imenukuliwa kutoka kwa Zayd ibn Ali ya kwamba, kama makusudio ya Ahlul-Bayt katika Aya ya utakaso yangelikuwa ni wake za Mtume badala ya kutumika viwakilishi wa kiume katika Aya kungetumiwa viwakilishi vya kike. [38] Kadhalika imeelezwa kuwa, kutokana na kutumiwa vitu kama viwakilishi vya kiume, hadithi mbalimbali na tofauti ya matumizi ya Aya zinazohusiana na wake za Mtume na Aya ya utakaso, hilo linafanya Aya hii isijumuishe wake za Mtume. [39]

Jamaa wa Nasaba Ambao Kwao Sadaka ni Haramu

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi zilizopokelewa na Waislamu wa Kisuni ni kwamba, jamaa wote ambao wana uhusiano wa nasaba na Mtume, kwao ni haramu kupokea sadaka kama vile familia ya Ali, familia ya Aqil, familia ya Abbas na familia ya Ja’afar hawa wanahesabiwa kuwa mfano wa wazi wa Ahlul-Bayt. [40]

Waumini Wakweli

Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, Ahlul-Bayt wanajumuishwa pia Waislamu ambao hata hawana nasaba au udugu na Bwana Mtume (s.a.w.w) la msingi wawe ni watu ambao walikuwa imara na wakweli katika kumfuata Bwana Mtume (s.a.w.w); [41] kama ambavyo kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, watu kama Salman Farsi [42] na Abu Dharr al-Ghifari [43] walitajwa na Bwana Mtume (s.a.w.w) kuwa ni katika Ahlul-Bayt wake. Imenukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ya kwamba, kila ambaye atakuwa mchaji Mungu na mja mwema, basi ni katika Ahlu-Bayt wetu. [44]

Fadhila za Ahlul-Bayt

Katika Aya na hadithi mbalimbali kumebainishwa fadhila tofauti kuhusiana na Ahlul-Bayt. [45] Kwa mtazamo wa Muhammad Muhammad Reyshahri, katika ziyara ya Jamiat al-Kabirah katika mlango wa fadhila na sifa maalumu za Ahlul-Bayt, kumetajwa maneno na ibara jumuishi zaidi. [46] Baadhi ya fadhila za Ahlul-Bayt ni:

Umaasumu

Makala ya Asili: Umaasumu wa Maimamu na umaasumu wa Fatma Zahra (a.s)

Kwa mujibu wa Ja’afar Sobhani [47] ni kwamba, Maulamaa wa Kishia [48] wametumia Aya ya 33 ya Surat al-Ahzab ambayo ni mashuhuri kama Aya ya Tat’hir kama hoja ya kuthibitisha utoharifu na umaasumu wa Ahlul-Bayt (as). Kwa mujibu wa Aya hii, Mwenyezi Mungu amekusudia kuwaondolea kila aina ya dhambi na kitendo kichafu watu wa Nyumba ya Mtume na kuwatakasa kabisa kabisa. Kwa msingi huo, Aya hii ni ishara ya wazi ya kwamba, Ahlul-Bayt ni Masumina (hawatendi dhambi) na Aya hii inawahusu wao. [49]

Hadithi ya Thaqalayn (vizito viwili) [50] ambayo ni miongoni mwa hadithi ambazo ni mutawatir (kumekithiri mapokezi yake), [51] inahesabiwa kuwa moja ya hoja za kuthibitisha Umaasumu wa Ahlul-Bayt wa Mtume; kwani hadithi hii imebainisha wazi suala la kutotengana Qur’an na Ahlul Bayt. Kwa msingi huo, kufanya dhambi yoyote ile au kukosea, kutapelekea kutengana kwao na Qur’an. [52] Kadhalika imeelezwa kwamba, katika hadithi hii Mtume amebainisha wazi na bayana kwamba, kila ambaye atashikamana na Qur’an na Ahlul-Bayt hatapotea. Hivyo basi kama Ahlul-Bayt hawatakuwa na umaasumu (hali ya kutotenda dhambi), kuwafuata wao bila sharti, hilo lenyewe litapelekea mtu kupotea. [53] Hadithi ya Safina ni hadithi nyingine imetumiwa kuthibitisha umaasumu na hali ya kutotebda dhambi Ahl-Bayt (a.s).

Wabora Zaidi Kuliko Wengine

Makala Asili: Ubora wa Ahlul-Bayt (a.s)

Sheikh Swaduq amesema, itikadi ya Mashia ni hii kwamba, Mtume na Ahlul-Bayt wake ni wabora zaidi, wapendwa zaidi na waja wanaotukuzwa zaidi miongoni mwa viumbe wa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ameumba ardhi, mbingu, pepo, jahamu na viumbe wengine kwa sababu yao. [55] Kwa mtazamo wa Allama Majlisi ni kwamba, mtu ambaye atafanya uhakiki na utafiti katika hadithi, atafikia yakini kuhusiana na Mtume na Maimamu (a.s) kuwa wabora, na ni jahili na mjinga tu wa hadithi na riwaya ambaye atakana ubora wa watu hawa. [56].

Aya ya Mubahala (maapizano) ni hoja nyingine inayotumiwa kuthibitisha ubora wa Ahlul-Kisaa juu ya masahaba wengine na familia ya Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa wanazuoni kama Allama Hilli na Fadhl bin Hassan Tabarsi ni kwamba, wafasiri wamefikia ijma'a na kauli moja kwamba, Aya hii ilishuka kwa ajili ya watu wa Kishamia (Ahlul-Kisaa). [58] Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ya kwamba, kama katika mgongo wa ardhi kungeweko na watu watukufu zaidi ya Ali, Fatma, Hassan na Hussein, Mwenyezi Mungu angetoa amri kupitia kwao nifanye Mubahala (maapizano); lakini Mwenyezi Mungu alinitaka nifanye Mubahala (maapizano na Wakristo wa Najran) kwa msaada wao. [59]

Kwa mujibu wa Muhammad Hussein Mudhaffar, Aya ya Mawaddah nayo inaonyesha ubora na utukufu wa Ahlul-Bayt (Ahlul Kisaa) na kwamba, wao ni wateule wa Mwenyezi Mungu; kwani kinyume na hivyo hakukuwa na maana ya wajibu wa kuwapenda na hilo likawa ni ujira wa risala ya Mtume [60].

Kuna hadithi mbalimbali pia zinazoonyesha na kuthibitisha ubora na utukufu walionao Ahlul-Bayt; ambapo miongoni mwazo ni Hadithi ya Thaqalayn (Vizitio Viwili) ambapo kwa mujibu wake, Mtume (s.a.w.w) amewaweka Ahlul-Bayt (a.s) kando ya Qur'an na ameiita Qur'an kuwa ni kizito kikubwa na Ahlul-Bayt ni kizito kidogo. Kama ambavyo Qur'an ni kitu chenye hadhi, heshima na utukufu wa juu kabisa kwa Waislamu, Ahlul-Bayt pia wana daraja ya juu na utukufu kwa watu wengine. [61] Hadithi ya Aman (au hadithi ya nujum) nayo inathibitisha ubora na daraja ya juu waliyonayo Ahlul-Bayt (as). [62]

Ahlul-Bayt Marejeo ya Kielimu

Katika Hadithi ya Vizito Viwili imetambuliwa kuwa, Ahlul-Bayt ni marejeo ya kielimu; kwani hatua ya Mtume ya kuwataka watu washikamane na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt, inaweka wazi suala la kurejewa Ahlul-Bayt na kufanywa kuwa marejeo katika masuala ya elimu, na Waislamu wanapaswa kuwarejea wao katika mambo na matukio mbalimbali yanayohusiana na dini yao. [63] Inaelezwa kuwa, baada ya Mtume, hakuna mtu anayefahamu maarifa na uhakika wa Qur'an na Sunna za Bwana Mtume ghairi ya Ahlul-Bayt. Kwa msingi huo, baada ya Mtume wao ndio marejeo ya kielimu ya Waislamu katika kufahamu maarifa na hukumu za dini na ili kudiriki maarifa hayo ni lazima kuwarejea wao. [64]

Wilaya na Uongozi

Wilaya na uongozi wa kisiasa wa Ahlul-Bayt ni katika mambo mengine yanayohesabiwa kuwa ni katika fadhila za Ahlul-Bayt. Wito wa Mtume kwa watu kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt umebainishwa wazi katika hadithi ya vizito viwili na kwamba, uongozi wa kisiasa unapaswa kuhodhiwa na watu hawa. [65] Katika baadhi ya nukuu za hadithi ya vizito viwili badala ya neno thaqalayn yaani vizito viwili, kumebadilishwa na kumetumika neno Khalifatayn yaani makhalifa wawili. [66] Kwa mujibu wa hadithi hii, Ahlul-Bayt ni makhalifa na viongozi baada ya Mtume na ni warithi wake katika pande zote ambapo hilo linajumuisha masuala ya kisiasa na kiuongozi. [67] Kwa mujibu wa Ja'afar Sobhani, katika tukio la Ghadir Khom, Mtume alimtangaza Ali (a.s) na Ahlu-Bayt wake kuwa viongozi baada yake. [68] Baadhi ya wengine kwa kuzingatiia sifa maalumu ya umaasumu, wanasema kuwa, Uimamu na uongozi wa kisiasa baada ya Mtume (s.a.w.w) ni maalumu kwa Ahlul-Bayt (a.s). [69] Kadhalika kutokuweko sharti lolote katika suala la kutakiwa kuwafuata Ahlul-Bayt ni hoja na dalili ya uongozi wao wa kisiasa; kwani wajibu wa kufuata unajumuisha maamrisho na makatazo yote yanayohusiana na maisha ya Waislamu, yawe ni ya kiibada, kisiasa au kiutamaduni. Kwa msingi huo basi katika masuala ya kisiasa na na mambo yanayohusiana na jami na utawala pia ni wajibu kuwafuata Ahlul-Bayt (a.s). [70]

Haki za Ahlul-Bayt

Kwa mujibu wa Aya na hadithi, Ahlul-Bayt wana haki katika mabega ya Waislamu na kwa mujibu wa haki hizi, Waislamu wana majukumu ambayo wanapaswa kuyatekeleza mkabala wa Ahlul-Bayt. Baadhi ya haki hizo ni:

Wajibu wa Kuwafuata

Makala Asili: Kufaradhishwa Kuwatii

Kwa mujibu wa Aya ya Ulul-Amr (Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu) suala la kuwatii Ulul-Amr (wenye mamlaka) limewekwa pamoja na agizo la kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake bila ya sharti. [71] Kwa mujibu wa Fadhl bin Hassan Tabarsi ni kwamba, kwa mtazamo wa Maulamaa wa Shia Imamiya, makusudio ya Ulul-Amr ni Maimamu (a.s). [72]

Hadithi ya vizito viwili pia, imetumiwa kama hoja ya kuthibitisha wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt; kwani katika hadithi hii Ahlul-Bayt wamewekwa kando ya (pamoja na) Qur'an. Hii ina maana kwamba, kama ambavyo kuifuata Qur'an ni wajibu kwa Waislamu, basi vivyo hivyo kuwati Ahlul-Bayt ni jambo la wajibu. [73]

Hadithi ya Safina pia inatoa ashirio na ithbati juu ya wajibu wa kuwafuata Ahlul-Bayt na kuwatii; kwani kwa mujibu wa hadithi hii, kuokoka wafuasi wao kunafungamana na kuwafuuata, na kuangamia kwao kunatokana na wao kuwaasi na kutowafuata. [74] Katika hadithi hii Mtume (s.a.w.w) amewafananisha Ahlul-Bayt wake na safina ya Nabii Nuhu. Mtume (s.a.w.w) amesema: Hakika mfano wa Ahlul-Bayt wangu ni mithili ya Safina ya Nuhu (a.s). Anayepanda ndani ya Safina anaokoka na yule asiyepanda anaangamia.

Mfananisho na mshabaha huu maana yake ni kwamba, kila ambaye atarejea kwa Ahlul-Bayt ataongoka na ambaye hatowafuata atapotea. [75]

Kuwapenda Ahlul-Bayt

Makala Asili: Kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s)

Kwa mujibu wa itikadi ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia ni kwamba, Aya ya Mawaddah suala la kuwapenda Ahlul-Bayt ni wajibu kwa kila Muislamu. [76] Wajibu wa kuwapenda Ahlul-Bayt ni jambo ambalo Waislamuu wameafikiana ispokuwa watu wachache kama manaswibi (wenye chuki na uadui na Imam Ali au mmoja wa Ahlul-Bayt) na hili linahesabiwa kuwa dharura miongoni mwa dharura za dini ya Uislamu. [77]

Aya ya mawaddah inasema: "Sema na uwaambie: Mimi sitaki ujira wowote ule kutoka kwenu kuhusiana na ujumbe ninaokuleteeni kutoka kwa Mola wenu, ila nakutakeni muwapende watu wa karibu yangu)." [78]

Kwa mujibu wa mtazamo wa Mashia, Aya ya Mawaddah ni miongoni mwa Aya ziliteremshwa kuhusiana umuhimu na nafasi maalumu waliyonayo Ahlul-Bayt wa Mtume (s.a.w.w), na inaashiria ulazima wa kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s). Pia, wengine wanaihisabu Aya hii kama ni moja ya dalili za Uimamu na ubora wa Imamu Ali (a.s).

Kwa mujibu wa Maulamaa kama Muhanmmad Ridha Mudhaffar, kupitia hadithi ambazo ni Mutawatir zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kwamba, kuwapenda Ahlul-Bayt ni ishara za kuwa na imani na kuwaudhi ni dalili ya nifaki, na wanaowapenda ni marafiki wa Mwenyezi Mungu na Mtume (s.a.w.w) na maadui wao ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. [79]

Ahlul-Bayt kwa Mtazamo wa Ahlu-Sunna

Ahlu-Sunna wanashirikiana kimtazamo na Mashia kuhusiana na kwamba, Ahlul-Kisaa (Watu wa Kishamia) ni miongoni mwa Ahlul-Bayt. Kuna hadithi nyingi katika vyanzo mbalimbali vya Ahlu-Sunna ambamo ndani yake, Mtume (s.a.w.w) amenukuliwa mara chungu nzima akiwatambulisha na kuwaarifisha Ali, Fatma, Hassan na Hussein (a.s) kwamba ni Ahlul-Bayt wake. [80]

Kadhalika imekuja katika vyanzo vya Ahlu-Sunna kwamba, Mtume amenukuliwa akisema kuhusiana na Ali, Fatma, Hassan na Hussein kwamba: Kila mwenye kuwapenda hao, amenipenda mimi na kila mwenye kuwafanyia uadui amenifanyia uadui mimi. [81] Mtume amenukuliwa katika hadithi nyingine akisema kuwa, mwenye kuwapenda Ahlul-Bayt siku ya Kiyama atakuwa pamoja nami na katika daraja yangu. [82] Fakhrurazi, mmoja wa wafasiri wa Qur'an wa Kisuni amesema kuwa, ni wajibu kuwapenda Ahlul Bayt, kwani Mtume alikuwa akiwapenda Ali, Fatma, Hassan na Hussein, na kumfuata Mtume ni wajibu kwa Umma wote wa Kiislamu. [83]

Zamakhshari na mwandishi wa kitabu cha al-Kashshaf anasema, Aya ya Mubahala ni hoja kubwa na madhubuti zaidi ya kuonyesha ubora wa watu wa Kisaa (Kishamia). [84] Ja'afar Sobhani mwanazuoni wa Kishia anasema kuwa, wanazuoni na wasomii wengi wa Ahlu-Sunna wamekiri kuhusiana na kwamba, Ahlul-Bayt ni wajuzi zaidi kielimu na watu wenye kuijua zaidi dini. [85] Kwa mfano Abu Hanifa mwanzishi wa madhehebu ya Hanafi na mmoja wa mafakihi wa madhehebu nne za Kisuni amenukuliwa akisema, "Sijamuona mtu aliyebobea katika fiq'h kumshinda Ja'afar bin Muhammad (a.s), akimkusuudia Imam Swadiq. [86]

Bibliografia

Makala asili: Faharasa ya vitabu kuhusiana na Ahlul-Bayt (a.s)
Ensaiklopidia ya Ahlul-Bayt(a.s)

Kumeandikwa vitabu vingi kuhusiana na Ahlul-Bayt au kwa anuani ya Ahlul-Bayt ambapo hapa tutataja baadhii tu:

Rejea

Vyanzo

  • Fāḍil Miqdād. Al-Lawāmiʿ al-ilāhīyya. Qom: Maktabat al-Marʿashī, 1405 AH.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Tafsīr al-kabīr. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Fayyūmī, Aḥmad b. Muḥammad al-. Al-Miṣbāḥ al-munīr. Cairo, [n.d].
  • Ḥāfiẓ Muḥammad, ʿAbd al-ʿAzīz al-. Al-Nibrās. Maktabat al-Ḥaqqānīyya, [n.d].
  • Haythamī, ʿAlī b. Abī Bakr al-. Majmaʿ al-zawāʾid. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿArabī, [n.d].
  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Nahj al-ḥaqq wa kashf al-ṣidq. Qom: Dār al-Hijra, 1414 AH.
  • Ibn Fāris, Aḥmad. Muʿjam maqāyīs al-lugha. Beirut: Dār al-Fikr, 1418 AH.
  • Ibn Ḥajar, Aḥmad b. Muḥamamd. Al-Ṣawāʾiq al-muḥraqa. Beirut: al-Maktaba al-ʿAṣrīyya, 1425 AH.
  • Ibn Ḥanbal, Aḥmad. Al-Musnad. Cairo: Dār al-Ḥadīth, 1416 AH.
  • Ibn Ḥanbal, Aḥmad. Faḍāʾil al-ṣaḥāba. Edited by Waṣīyy Allāh b. Muḥammad. Mecca: Jāmiʿat Um al-Qurā, 1403 AH.
  • Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Āndulus, 1416 AH.
  • Ibn Manẓūr, Muḥammad b. Mukarram. Lisān al-ʿArab. Beirut: Dār al-Ṣādir, 2000.
  • Ibn Shahrāshūb, ʿAlī b. Muḥammad. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, [n.d].
  • Kāshif al-Ghitāʾ, Muḥammad Ḥusayn al-. Aṣl al-Shīʿa wa uṣūluhā. Cairo: al-Maṭbaʿa al-ʿArabīyya, 1377 AH.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: al-Maktaba al-Islāmīyya, 1388 AH.
  • Manāwī, Muḥammad ʿAbd al-Raʾūf al-. Fayḍ al-ghadīr fī sharḥ al-jāmiʿ al-ṣaghīr. Beirut: Dār al-Fikr, 1416 AH.
  • Muslim al-Niyshābūrī. Saḥīḥ Muslim. Edited by Muḥammad Fuʾād ʿAbd al-Bāqī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-Islāmī, [n.d].
  • Muzaffar, Muḥammad Ḥasan al-. Dalāʾil al-ṣidq. Tehran: Maktabat al-Dhujāj, [n.d].
  • Qāḍī Nuʿmān al-Maghribī, Daʿāʾim al-Islām. Cairo: Dar al-Maʿārif, [n.d].
  • Qundūzī, Sulaymān b. Ibrāhīm al-. Yanābīʿ al-mawadda li-dhawī l-qurbā. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī, 1418 AH.
  • Rāghib al-Iṣfahānī, Ḥusayn b. Muḥammad al-. Al-Mufradāt fī gharīb al-Qurʾān. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawīyya, [n.d].
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. al-Tafsīr al-kabīr. Edited by Maḥmūd Shākir. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1421 AH.
  • Ṭabāṭabāyī, Muḥamamd Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Muʾasisat al-Aʿlamī, 1393 AH.
  • Ṭabrisī, Ḥasan b. al-Faḍl al-. Makārim al-akhlāq. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī, 1392 AH.
  • Ṭaḥāwī, Aḥmad b. Muḥammad al-. Mushkil al-āthār. Beirut: Dar al-Ṣāsir, [n.d].