Sanda
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Sanda (Kiarabu: الكفن) ni vazi au nguo maalumu avishwazo maiti wa Kiislamu kabla ya kuzika. Uchache wa vazi hili aveshwalo maiti huwa ni vitambaa vitatu: kitambaa cha chini (hufungwa chini kama seruni), shati (ammbayo huanzia shingoni hadi magotini) na cha tatu ni kitambaa kirefu, ambacho huzongoreshwa nacho maiti kuanzia kichwani hadi miguuni. Ni wajibu kifaya kwa waislamu kumkafini maiti wa Kiislamu. Na si halali, kutumia vitambaa vilivyoibiwa au vitambaa vyenye najisi katika kutekeleza amali hii. Ni mustahabu kujiandaa kwa sanda kabla ya mtu kufariki.
Ufafanuzi Vazi la Sanda na Majukumu ya Kumkafini Maiti
Sanda (kafani), ni kitambaa ambacho ni wajibu kwa Waislamu kumzonga nacho maiti wa Kiislamu kabla ya kuzikwa kwake. [1] Ni wajibu kifaya kwa Waislamu kumkafini maiti wa Kiislamu wa kike au wa kiume kabla ya kuzikwa kwake. [2] Ni wajibu kwa mume kumtayarishia sanda mkewe, [3] Hata hivyo, si wajibu kwa Waislamu kuwatayarishia wengine sanda, bali ni jukumu la kila mtu kujiandalia sanda yake mwenyewe, kwani lililo wajibu ni kumkaini maiti, na sio kumtayarishia sanda (Kafani). [4] Na si jukumu la mtu hata mmoja miongoni mwa Waislamu kuwanunulia wengine sanda, [5] na kulingana na fat'wa za wanazuoni ni kwamba; ikiwa maiti atakuwa hana mali ya kutosha kwa ajili ya kukunua sanda, katika hali kama hiyo yaweza kumnunulia sanda kutoka katika mapato ya mali za zaka. [6]
Sanda huwa na vitambaa vitatu ambavyo ni: [7]
- Kitambaa cha chini (izaar): ni kitambaa ambacho kinapaswa kufunika mwili kutoka kwenye kitovu hadi magoti. Ni vyema ikiwa kitambaa hicho kitafunika mwili wa maiti kutoka kifua kwake hadi miguni. [8]
- Shati (qamis): ni vazi ambalo linapaswa kufunika mwili wa maiti kutoka mabegani mwake hadi kwenye nusu ya miundi. [9] Ni vyema zaidi iwapo litafunika mwili wake hadi miguuni. [10]
- Kitambaa kirefu: ni vazi ambalo linapaswa kufunika mwili mzima wa maiti, kutoka kichwani hadi miguuni. [11] Na ni vyema ikiwa kitambaa hicho kitakuwa ni kirefu kiasi ya kutosha kufungwa fundo kichwani na mwishoni mwa miguu ya maiti. [12]
Wasifu wa sanda
- Ni marufuku kumvisha maiti sanda kwa kitambaa kilichoibiwa au chenye najisi.
- Pia ni marufuku kumvisha maiti sanda kupitia kitambaa cha hariri au kitambaa kilichotengenezwa kupita manyoya au ngozi ya wanyama ambao ni haramu kuliwa, bila ya kuwepo dhadhura maalumu inayo kubalika kisheria. [13]
- Kabla au wakatia wa kumvisha sanda maiti, inapaswa kupakwa kafur (karafuu maiti) kwenye sehemu saba za mwili wake, ambazo kwa kawaida huwa ni zenye kugusana na ardhi wakati wa kusujudu. [14] Amali hii kwa lugha ya Kiarabu huitwa tahniit na ni amali ya wajibu. [15]
- Mtu aliye kufa kifo cha kishahidi, huwa hahitaji kukafiniwa wala kuvikwa sanda, isipokuwa ikiwa alikuwa uchi. Katika kesi hii, ni wajibu kumvisha sanda. [16]
Mambo Yaliyo Mustahabu na Makruhu katika Masuala ya Sanda ( Kafani)
Ni mustahabu kujiandaa kwa sanda tokea wakati wa uhai. [17] Ni vyema kutumia vitambaa vya aina ya burd vya Yemeni kwa ajili ya sanda, (hii ni aina maalumu ya vitambaa vinavyo zalishwa nchini Yemeni, ambavyo thamani yake ni kubwa ukilinganisha na vitambaa vya kawaida). [18] [19] Kwa upande wa pili, imesemwa kwamba; ni makruhu (haipendekezwi) kufanya mambo yafuatayo: Kutumia kitambaa cha kitani, [20] Kukata sanda kupitia kifaa cha chuma, kama vile mkasi wa chuma na Sanda kitiwa vifungo na kuwa na mikono mirefu. Ila jambo hilo halitakuwa ni tatizo iwapo maiti huyo atakuwa amekafiniwa kupitia nguo yake aliyokuwa amevaa ambayo ilikuwa na vifungo na mikono mirefu. ila sharti ya kumvika sanda maiti kupitia nguo yake, ni lazima nguo hiyo iwe na uwezo wa kuyayaenea maeneo ya mwili ambayo ni wajibu kuyasitiri katika mwili wa maiti hiyo. Sanda kuwa ya rangi nyeusi au kuwa na maandishi ya rangi nyeusi, kumfunga kilemba maiti kisha kuzungusha mkia mmoja wa kilemba hicho shingoni mwake, kumvisha sanda chafu, kupatana (kuomba punguzo la bei) katika kununua sanda na la mwisho ni kuishona sanda. [21]