Hadithi ya Man Mata

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Hadithi ya “Man Mata”)

Hadithi ya Man Mata (Kiarabu: حَدِيثُ مَنْ مَاتَ) ni hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo kwa mujibu wake ni kwamba Atakayekufa hali ya kuwa si mwenye kumfahamu Imamu wa zama zake, amekufa kifo cha kijahilia. Hadithi hii imenukuliwa kwa lafudhi mbalimbali katika vitabu na vyanzo vya Kishia na Kisunni na hadithi ambayo imeafikiwa na pande zote mbili (Mashia na Masuni).

Pamoja na hayo, kuna ufahamu na welewa tofauti baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni kuhusiana na hadithi hii:

Waislamu wa Kishia wanaitambua hadithi hii kwamba, inahusiana na kadhia ya Uimamu na wanachukua na kunyambua kutoka humo ulazima wa kumtambua Imamu na kumtii; hata hivyo Ahlu Sunna wanaamini kuwa, hadithi hii inahusiana na kadhia ya mahusiano baina ya watu na mtawala wa Kiislamu na ulazima wa baiya na kutoa kiapo cha utii.

Nafasi ya Hadithi ya Man Mata

Katika vyanzo mbalimbali vya Kiislamu kuna hadithi ambazo zimenukuliwa kwa ibara ya:[1] «من ماتَ»; hata hivyo makusudio ya ibara ya hadithi ya «من ماتَ» ni maneno mashuhuri ya Bwana Mtume (s.a.w.w): «مَنْ ماتَ وَ لَمْ یعْرِفْ إمامَ زَمانِهِ مَاتَ مِیتَةً جَاهِلِیة» Atakayekufa hali ya kuwa si mwenye kumfahamu Imamu wa zama zake, amekufa kifo cha kijahilia. Hadithi hii ni mashuhuri na imenukuliwa katika vyanzo na vitabu vya Waislamu wa madhehebu ya shia na Sunni.[2]

Hadithi hii imemukuliwa pia kwa ibara tofauti ambapo kuna tofauti ndogo. Kwa mfano katika kitabu cha Kafi, hadithi hii imenukuliwa hivi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s): «مَنْ مَاتَ وَ لَیسَ لَهُ إِمَامٌ فَمِیتَتُهُ مِیتَةٌ جَاهِلِیةٌ» Mwenye kufa hali ya kuwa hana Imamu, kifo chake ni kifo cha kijahilia.[3] Kadhalika katika baadhi ya vyanzo vya Ahlu Sunna imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ya kwamba amesema: «مَنْ مَاتَ بِغَیرِ إِمَامٍ مَاتَ مِیتَةً جَاهِلِیةً» Mwenye kufa bila ya Imamu, amekufa kifo cha kijahilia.[4]

Allama Majlisi ameitambua hadithi hii kuwa ni (yenye mapokezi mengi) kwa Waislamu wa Kishia na Kisuni.[5] Sheikh Bahai pia amesema, Mashia na Masuni wameafikiana katika hadithi hii.[6]

Makusudio ya Kifo cha Kijahilia

Katika nukuu ya Kulayni inaonekana Imamu Swadiq (a.s) amenukuliwa akibainisha maana ya: «من مات» kwamba, ni kifo cha kijahilia. Matini kamili ni kama ifuatavyo: Ibn Abi Ya’qub ananukuu: Imenukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) kuhusiana na maneno ya Bwana Mtume (s.a.w.w) kwamba: Kila ambaye atakufa katika hali ambayo hana Imamu, kifo chake ni kifo cha kijahilia. Nikauliza: Je, makusudio ni kufa katika hali ya ukafiri? Imamu Swadiq (a.s) akajibu kwa kusema: Kufa katika hali ya upotofu na kupotea. Nikasema: Kila ambaye atakufa katika katika zama hizi na akawa hana kiongozi, kifo chake kitakuwa kifo cha kijahilia? Akasema: Ndio.[7]

Vyanzo vya Hadithi

Baadhi ya vyanzo vya hadithi vya Shia na Ahlu Sunna ambavyo vimenukuu hadithi ya “man mata” ni kama ifuatavyo:

Vyanzo vya Kishia

Vyanzo vya Ahlu-Sunna

  • Musnad Ahmad bin Hanbal.[11]
  • Musnad Abu Dawud Sleiman bin Dawud Tayalisi.[12]
  • Musnad al-Shamiyyin, Abul Qassim Tabarani.[13]

Maana ya Hadithi Kwa Maulamaa wa Kishia na Kisunni

Maulamaa wa Kishia na Kisunni kila kundi moja miongoni limetoa maana na mafuhumu (yaliyokusudiwa) ya hadithi ya Mana Mata kulingana na itikadi yao ya kiteolojia:

Shia

Mashia wametumia hadithi ya Man Mata katika suala la Uimamu na kulitambua hilo kuwa hoja ya ulazima wa kuweko Imamu katika zama zote[14] na udharura wa kumtambua Imamu na kumtii.[15] Kwa msingi huo itikadi za Shia ni kwamba, makusudio ya Imamu katika hadithi hii ni Ahlul-Bayt na Maimamu Maasumu na katika zama hizi, ni lazima kuwa na imani juu ya Imamu Mahdi kwa anuani ya kuwa yeye ndiye Imamu wa zamani hizi.[16]

Ahlu-Sunna

Ahlu Sunna wametoa tafsiri na maana nyingine ya hadithi hii. Wao wanaona kuwa, makusudio ya Imamu katika hadithi hii ni mtawala wa jamii ya Kiislamu ambapo ili kulinda na kuhifadhi jamii ya Kiislamu, inapasa kumfuata yeye na kubakia katika baiya na utiifu kwake.[17] Ulazima wa kumfuata mtawala wa Kiislamu unajumuisha watawala wote wa Kiislamu na kuwa kwao madhalimu na kutenda kwao dhambi watawala hao hakutii dosari katika ulazima wa kuwafuata. Katika kufasiri hadithi iliyotangulia, Ibn Taymiyyah amesema kuwa, hadithi hiyo inaonyesha ulazima wa kufuata na kutoa kiapo cha utii maswahaba wa Mtume na tabiina kwa Yazid bin Muawiya.[18]

Hata hivyo baadhi ya vyanzo vya Ahlu-Sunna vimetoa maana ya hadithi iliyotangulia ya “Imamu” kuwa ni Mtume (s.a.w.w) na vinaamini kwamba, ni lazima kuwa na imani juu ya Mtume kwa sababu yeye ni Imamu wa watu wa ardhini katika dunia hii.[19]

Rejea

Vyanzo