Adliyyah
Adliyyah (Kiarabu: العَدليِّة) ni istilahi ya kielimu inayotumika katika uwanja wa fani ya theolojia ikirejelea madhehebu ya Shia na Mu'tazila. Istilahi hii inatokana na imani ya pamoja ya madhehebu haya isemayo kwamba; Kwa mujibu wa akili na mantiki salama, katika ulimwenguni kuna uzuri na ubaya wa kimantiki (dhati au asilia), ambao kwa mujibu wake Mwenye Ezi Mungu hupitisha hukumu zake ambazo ima ni thawabu au adhabu. Imani hii inaeleza kuwa; Mwenye Ezi Mungu hutenda kulingana na mantiki hiyo, na ndio Yeye akapewa sifa na jina la Mtenda haki (Adil) au Mwadilifu.Hivyo ni vyema kuelewa ya kwamba; imani ya uadilifu wa Mungu, ni moja ya misingi mikuu ya imani za madhehebu ya Shia pamoja na Mu'utazila.
Kinyume na itikadi ya Adliyyah, ni madhehebu ya Ash'ariyyah ambao wanaamini juu ya dhana ya uzuri na ubaya wa kisheria. Hii ina maana kwamba, kwa mujibu wa imani yao, hakuna uzuri au ubaya wa kimantiki na kiakili, unao husisha uwepu halisi wa dhana mbili hizo; bali chochote kile ambacho Mwenye Ezi Mungu ameamuru kutekelezwa au kushikana nacho kinachukuliwa kuwa kizuri, na chochote ambacho amekataza kinachukuliwa kuwa kibaya. Kwa mtazamo wa Ash'ariyyah, amri na makatazo ya Mwenye Ezi Mungu ndiyo yanayounda ubaya na uzuri na ambavyo ndio msingi wa maadili na sheria. Kwa mujibu wa kauli ya Murtadha Mutahhari, mwanafalsafa na msomi maarufu wa Kiislamu, madhehebu yote ya Kiislamu yanakubaliana kuwa Mwenye Ezi Mungu ni Mwadilifu. Hata hivyo, tofauti inatokea katika tafsiri na uelewa wa dhana ya uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu ulivyo. Wakati Adliyyah wanasisitiza kuwa uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu unalingana na mantiki na akili ya kibinadamu, Ash'ariyyah wanasisitiza kuwa uadilifu wa Mungu hauna uhusiano wa lazima na mantiki na akili, bali unategemea amri zake ya kisheria.
Matokeo ya imani ya Adliyyah katika dhana ya uzuri na ubaya wa kiakili ni kwamba wao, tofauti na baadhi ya madhehebu mengine, wanaikubali akili kama moja ya vyanzo vya msingi vya kisheria. Kwa mujibu wa itikadi ya Adliyyah, akili ina nafasi ya kipekee katika kuelewa na kutafsiri sheria za Mwenye Ezi Mungu, na hivyo inaweza kutumika sambamba na vyanzo vingine vya sheria kama Qur'ani, Sunna na Ijmaa katika utoaji wa sheria za kifiq-hi. Kwa maoni ya Adliyyah, akili inachukuliwa kuwa hoja kamili inayoweza kutoa mwanga katika masuala ambayo yanaweza kuwa na utata au yasiyoelezwa moja kwa moja katika maandiko ya kisheria. Hii inamaanisha kuwa, mbali na kufuata maandiko, wanazuoni wa Adliyyah hutumia mantiki na tafakuri za kiakili ili kutoa hukumu za kisheria ambazo zinazingatia muktadha wa kiakili na wa kimaadili. Katika mtazamo huu, akili si tu chombo cha kufafanua maandiko, bali pia ni mwongozo wa kufikia haki na maadili sahihi. Imani hii inawapa Adliyyah uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kimaadili kwa njia inayowiana na mantiki na haki, huku wakilinda misingi kamili ya sheria za Kiislamu.
Uadilifu wa Mwenyezi Mungu: Suala Muhimu katika Theolojia ya Kiislamu
- Makala Asili: Uadilifu wa Mwenyezi Mungu
Suala la uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu linachukuliwa kuwa ni mojawapo ya masuala muhimu na ya kimsingi katika theolojia ya Kiislamu. Umuhimu wa dhana hii ni mkubwa kiasi kwamba imepelekea wanatheolojia wa Kiislamu kugawika katika makundi mawili makuu, yanayojulikana kama Adliyyah na wasiokuwa Adliyyah. [1] Kwa madhehebu ya Shia, uadilifu ni mojawapo ya misingi ya nguzo tano zao za imani (itikadi), inayoashiria msimamo wa imani yao juu uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu. [2] Pia, uadilifu ni msingi wa pili wa misingi mitano ya madhehebu ya Mu'tazila, ambao ni miongoni makundi ya kitheolojia ya upande wa Ahlul-Sunna. [3]
Suala Kuu Katika Uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu
Kwa mujibu wa maoni ya Murtadha Mutahhari, suala linalojitokeza katika uadilifu wa Mwenyezi Mungu halihusu iwapo Mungu ni Mwadilifu au la, kwani wanazuoni wote wa Kiislamu wanakubaliana juu ya uadilifu wa Mungu, na hakuna madhehebu yoyote yanayopingana na dhana hiyo. Hata hivyo, tofauti kubwa ipo katika tafsiri na uelewa wa uadilifu wa Mungu. [4] Mjadala muhimu unajikita juu ya kuwepo kwa kipimo maalum cha uadilifu ambacho mbele ya Mwenye Ezi Mungu huwa ndiyo kigezo cha upangaji na uendeshaji wake, zikiwemo sheria za maamrisho na makatazo Yake kwa waja wake. Hili linahusisha swali la msingi la kwamba: Je, kuna viwango vya haki na uadilifu vinavyojulikana kupitia akili ya mwanadamu ambavyo Mungu huvifuata, au kwamba kila kitendo cha Mungu kichukuliwe kuwa ni kielelezo cha haki au uadilifu, bila kujali uelewa wa kiakili wa wanadamu? [5]
Kwa lugha nyengine ni kwamba, je, mema na mabaya, manufaa na madhara, haki na batili ni vitu vilivyokuwepo kabla ya maagizo na amri za Mwenyezi Mungu, kisha Mwenye Ezi Mungu akatoa maagizo yake kwa kuzingatia uwepo wa mambo hayo? Au maagizo ya Mwenye Ezi Mungu yalitangulia, na kisha mema na mabaya, haki na batili vikaorodheshwa kulingana na msingi wa maagizo hayo. [6]
Kwa hiyo swali ni kwamba, je, Mungu anahimiza uaminifu kwa sababu uaminifu ni jambo jema kiasili na lina manufaa kwa wanadamu, na anakataza usaliti kwa sababu usaliti ni jambo baya kiasili na lina madhara kwa wanadamu? Au kwamba kiasilia, hakuna uaminifu ulio na manufaa! Wala usaliti wenye madhara, bali kwa sababu Mungu ameamuru uaminifu, basi umekuwa jambo jema, na kwa sababu amekataza usaliti, basi umekuwa ni jambo baya? [7]
Kwa mujibu wa maoni ya madhehebu ya Adliyyah, bila shaka kuna viwango vya haki na uadilifu vinavyoweza kutambuliwa na akili, na Mwenye Ezi Mungu hutenda kwa mujibu wa viwango hivyo. Hii inamaanisha kwamba amri na makatazo ya Mungu lazima yalingane na mantiki ya haki na uadilifu. Kwa upande mwingine, madhehebu mengine kama Ash'ariyyah wanakataa dhana ya uwepo wa kipimo cha kiakili cha haki uadilifu, bali wanasisitiza kwamba; kila kitendo cha Mungu ni kielelezo cha haki, bila kujali kama kinaeleweka au hakieleweki wala hakiendani na akili na mantiki ya mwanadamu. Katika mtazamo huu, haki ya Mungu haitegemei vipimo vya nje au viwango vya kiakili, bali kitendo chochote kile cha Mungu kinachukuliwa kuwa ni kitendo cha haki adilifu.
Adliyyah ni Akina Nani?
Katika historia ya madhehebu ya theolojia ya Kiislamu kumezaliwa pande mbili zenye mitazamo tofauti. Jina la Adliyyah linarejelea vikundi vya theolojia kama vile Shia na Mu'tazilah. [8] Wanateolojia wa madhehebu haya wanashikilia imani juu ya uwepo wa dhana ya uzuri na ubaya wa kiakili. Kwa mujibu wa itikadi hii, akili ina uwezo wa kudiriki na kugawa matendo sehemu mbili; mema na mabaya, jambo ambalo linafanyika bila ya kuhitaji uamuzi wa Mungu juu ya uzuri au ubaya wa mambo hayo. Kwa maneno mengine, Adliyyah wanaamini kwamba akili ya mwanadamu inaweza kutambua wema na ubaya wa baadhi ya mambo fulani, bila ya kuhitajia amri na makatazo ya Mungu. [9]
Wapinzani wa Adliyyah
Ash'ariyyah, kundi la wanateolojia wa Kiislamu, lina maoni kinyume na yale ya Waislamu wa Kishia na Mu'tazilah kuhusiana na uwepo wa dhana ya uzuri na ubaya. Kundi hili linakataa uwepo dhana ya uzuri na ubaya wa kiakili na badala yake linaamini juu ya uwepo wa dhana ya uzuri na ubaya wa kisheria. Kwa mujibu wa Ash'ariyyah, akili hawezi kubaini uhalisia na uhakika wa mema na mabaya wa jambo fulani. Hii ina maana ya kwamba; kiuhalisi hakuna uzuri wala ubaya; badala yake, uzuri na ubaya hutegemea amri na sheria za Mungu. Kile ambacho sheria inakubaliana kuwa kizuri kinakuwa kizuri, na kile ambacho sheria inakataza kinakuwa kibaya. Kwa hivyo, ikiwa sheria isingekuwepo, dhana ya uzuri na ubaya ingekuwa ni dhana isiyo na msingi wala mashiko. [10]
Uhalali wa Akili kwa Wafuasi wa Adliyyah
Kulingana na Murtadha Mutahhari, wafuasi wa Adliyyah hawashikamani na dhana ya uzuri na ubaya wa kiakili akili kavu kavu, bali wanakubali na dhana hiyo kwa maana kwamba; akili ni nyenzo na sehemu muhimu ya ushahidi wa kisheria sambamba na Qur'ani, Sunna na Ijmaa (makubaliano ya wanazuoni). Nazo ni nyezo zinakubalika kwa Waislamu wote duniani. [11] Hili linamaanisha kwamba akili ni chanzo cha sheria na hutumika katika kutafuta na kubaini hukumu za kisheria. Hii inatofautiana na wale wenye mtazamo kinyume na wafuasi wa Adliyyah, ambao wanaamini kwamba akili haiwezi kutumika kama mwongozo katika kufikia hukumu za kisheria. [12]