Sala ya jamaa

Kutoka wikishia
Sala ya jamaa katika Masjid Al-haram

Sala ya jamaa (Kiarabu: صلاة الجماعة) ni Sala inayosaliwa kwa pamoja. Sala ya jamaa ni miongoni mwa ibada zenye fadhila nyingi mno. Yule mwenye kusimama mbele na kusalisha Sala ya jamaa huku wengine wakumfuata nyuma yake, huitwa imamu wa Sala ya jamaa, na wale wanaomfuata wanao mfuata nyuma yake huitwa maamuma.

Kwa mujibu wa baadhi ya mafaqihi (wanazuoni wa kifiqhi), mwanzoni mwa Sala kufaradhishwa, Sala ilikuwa ikisaliwa kwa mfumo wa jamaa, na Sala ya kwanza ya jamaa ilisaliwa na watu wawili ambao ni Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s). Katika Hadithi imeelezwa kuwa, ubora wa Sala moja ya jamaa ni kuliko Sala 25 za mtu anayesali peke yakle. Sala ya jamaa ni Sala iliotiliwa mkazo mno, hasa kwa wale majirani wanaoishi karibu na msikiti.

Kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wa Kishia, kushiriki katika Sala za jamaa ni jambo la mustahabu (liliotiliwa mkazo sana), na ni sunna iliyokokotezwa. Sala zinazopaswa kusaliwa kwa mfumo wa jamaa, ni zile Sala za faradhi peke yake. Nazo ni Sala za kila siku, Sala za Ayat, Sala mbili za Idi (Idul Fitri na Idul Adh-ha), Sala ya maiti na Sala ya Ijumaa. Kwa mujibu wa rai na maoni ya mafaqihi maarufu wa Kishia, haijuzu kusali jamaa Sala ya mustahabu (ya sunna) isipokuwa Sala ya kuomba mvua. Masunni wanasali Sala ya Tarawehe kwa jamaa, lakini Mashia wanaona jambo hilo kuwa ni bid'ah.

Dhana ya Sala

Sala ya jamaa ni Sala inayosaliwa kwa mfumo wa mjumuiko. Katika Sala hii, Imamu wa Sala (kiongozi) husimama mbele, na waongozwaji (maamuma) husimama nyuma yake. Sala ya jamaa inaundwa au husimamishwa kupitia watu wasiopungua wawili, yaani imamu na mamuma (mfuasi) mmoja. [1]

Umuhimu wa Sala ya jamaa

Sala ya jamaa ni ibada iliyosuniwa au ni ibada iliyotiliwa mkazo katika Uislamu. [2] Maelezo ya Hadith kuhusiana na Sala ya jamaa yanasema kwamba; Kuiacha Sala ya jamaa bila ya udhuru ni miongoni mwa sababu za kuto kubaliwa Sala. kuipuza Sala ya jamaa kunahesabiwa ni sawa na kumdharau na kumpuza Mwenyezi Mungu. [3]

Hekima ya kisheria ya Sala ya jamaa

Kwa mujibu wa Riwaya iliyosimuliwa na Imamu Ridha (a.s), sababu hasa ya kufaradhishwa Sala ya jamaa, ni kuitangaza na kuiweka bayana dini ya Kiislamu, kujenga tauhidi pamoja na roho ya ikhlasi miongoni mwa watu. [12] Imepokewa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) katika Kitabu cha 'Ilalu Al-Shara'i (Sababu za Tungo za Sheria), kwamba; Lengo la Mwenyezi Mungu la kufaradhisha Sala ya jamaa, ni kutaka watambuliwe wale wanaosali miongoni mwa wale wasiosali, na wajulikane wale wachungao nyakati za mwanzo za Sala na wale wapuzao nyakati hizo. Pia imeelezwa kwamba; Kama kusingekuwa na Sala ya jamaa, kusingekuwa na mtu atakayeweza kutoa bishara ya kheri ya kumbashiria mwengine.[13]

Umuhimu wa Sala ya jamaa haukufafanuliwa kwa uwazi katika Qur'an Tukufu. Ila mafaqihi wamelifafanua jambo hili chini Aya ya 43 ya Suratu Al-Baqarah. Nayo ni kama ifuatavyo: ((وَ أَقیمُوا الصَّلاةَ وَ آتُوا الزَّکاةَ وَ ارْکعُوا مَعَ الرَّاکعین ; Na simamisheni Sala na toeni zaka na murukuu pamoja na wanaorukuu)).[5] Maoni ya baadhi ya wanatafsiri ni kwamba: Aya hii ni kiashirio na na kidokezo dhahiri kinachodokeza suala la Sala ya jamaa. [6] Pia suala la Sla ya jamaa, limezungumzwa kibaga unaga ndani ya baadhi ya vitabu vilivyo kusanya hazina za Hadith za Kishia. Ambapo suala hilo linaonekana kuchambuliwa chini ya mlango maalumu unaohusiana na ubora wa Sala ya jamaa na kanuni zake [7].

Ayatullah Borujerdi, akitegemea baadhi ya Riwaya anaamini ya kwamba; Mwanzoni mwa dini ya Kiislamu, Sala iliamriwa kusaliwa kwa mfumo wa jamaa. [8] Mwanzoni mwa utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Sala ya jamaa ilisaliwa chini ya uongozi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na Imam Ali alikuwa ni maamuma pekee wa kiume aliye salishwa katika Sala hiyo, [9] huku bibi Khadija naye akiwa ndiye maamuma pekee wa kike katika Sala hiyo. [10] Na Baada ya kipindi fulani, Jafar Tayyar naye akaingia katika jopo lao (akajiunga nao). [11]

Fadhila za Sala ya jamaa

Kuna thawabu na fadhila nyingi zilizotajwa kuhusiana na Sala ya jamaa. Imepokewa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwamba; Kadiri idadi ya watu wanaohudhuria katika Sala ya jamaa inavyokuwa kubwa, ndivyo watu hao wanavyopendwa zaidi na Mola wao, [14] na kadri ya wao wanavyokuwa wengi katika Sala hiyo, ndivyo thawabu kubwa zaidi zinavyo wamiminika juu yao. Iwapo Sala ya jamaa itahudhuriwa na mtu mmoja, basi fadhila zake zitakuwa ni mara 150. Na iwapo Sala ya jamaa itahudhuriwa na watu wawili, basi ujira wake utakuwa ni sawa na mara 600. Iwapo Sala hiyo itakuwa na kiwango cha watu zaidi ya tisa, basi fadhila na ujira wa Sala hiyo aujuao ni Mungu peke yake. [15]

Vile vile imeelezwa katika Hadith ya kwamba; Sala moja ya jamaa ni bora zaidi kuliko Sala 25 zisiyokuwa za jamaa. [16] Na thawabu ya Sala moja ya jamaa inazingatiwa kuwa ni bora kuliko Sala za miaka arobaini zilizosaliwa nyumbani bila ya jamaa. [17] Ubora wa fadhila ya Sala ya jamaa iongozwayo na Imamu ambaye ni mwanachuoni, ni kama Sala iliyosalishwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w). [18]

Tija ya Sala ya jamaa

Kwa mujibu wa Riwaya zisemavyo, Sala ya jamaa huepusha unafiki, [19] hupelekea kusamehewa dhambi, [20] hupelekea mtu kujibiwa dua zake, [21] inasahilisha na kuepusha dhiki za Siku ya Kiyama, inarahisisha kuingia Peponi, [22] pia inamkaribisha mja na radhi za Mola wake pamoja na Malaika wake [23]. Kwa upande mwengine, mtu anayeshiriki Sala za jamaa hupewa fursa na Mola wake ya kuwaombea wengine shufaa siku ya Kiama.[24]

Imepokewa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwamba, kila hatua aipigayo mja kuelekea msikitini, huandikiwa wema elfu moja na kupandishwa daraja 70,000, na iwapo ataaga dunia akiwa katika hali hiyo, Mungu hutuma Malaika 70,000 kumzuru kwenye kaburi lake. Malaika hao watabakia ndani ya kaburi lake na kumliwaza kutokana na upweke wa kaburini humo. Mailka hao wataendelea kubakia kaburini mwake mpaka atakapofufuliwa na kutoka nje ya kaburi hilo.[25]

Pia baadhi ya malengo muhimu na ya msingi ya Sala ya jamaa, ni kuupa utambulisho Uislamu pamoja na kujenga sura maalumu kwa umma wa Kiislamu, kuwafanya Waislamu wafahamiane zaidi wao kwa wao, kujenga na kuimarisha fikra ya ushirikiano miongoni mwao, kupanda mbegu za mapenzi na mahaba yatakayo jenga mahusiano mazuri baina yao. Hayo ni miongozi mwa mambo ya msingi na manufaa ya Sala ya jamaa. [26]

Hukumu ya Sala ya jamaa

Kwa mtazamo wa kifikqhi wa mafaqihi wa Kishia ni kwamba; Kushiriki Sala ya jamaa ni jambo linalopendekezwa sana, au kwa lugha nyengine ni sunna iliokokotezwa. [27] Sala zilizo sisitizwa zaidi kusaliwa kwa mfumo wa jamaa, ni Sala ya asubuhi, magharibi pamoja na Sala ya ishaa. Pia usahihi na sharti la kusihi kwa Sala ya Ijumaa ni kusaliwa kwa jamaa. Yaani Sala ya Ijumaa haiwezi kusaliwa na mtu mmoja peke yake (haiwezi kusaliwa kwa mfumo wa furada). [30]

Mahambali na baadhi ya Mahanafi ambao ni miongoni mwa Masunni, wameichukulia Sala ya jamaa kuwa ni faradhi ya lazima kwa kila mmoja ndani ya jamii. [31] Kwa mujibu wa mtazamo kundi la Shaafi'iy; Sala ya jamaa ni faradhi kifaya kwa wanaume, isipokuwa wakiwa safarini. [32]

Kusaliwa jamaa Sala ya sunna

Kwa mujibu wa mafaqihi wa Kishia, haijuzu kusali Sala za sunna kwa jamaa isipokuwa Sala ya mvua. [33] Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya mafaqihi wa Kishia, ni sunna kusali Sala ya Idi katika zama asizokuwepo Khalifa (Imamu) wa Kiislamu ndani ya jamii ya Kiislamu. [34] Kwa nadharia za mafaqihi mashuhuri wa Kishia ni kwamba; Sala ya Eid-ul-Adha-ha ni lazima isaliwe kwa jamaa iwe ni katika zama za faradhi au zama za sunna za Sla hiyo. Yaani ni wajibu kusaliwa kwa jamaa katika zama zote mbili, iwe ni zama kuwepo Imamu (Imamu Mahdi) (a.s) -ambapo Sala ya Idi huwa ni wajibu- au ni zama ambazo Imamu Maasumu yupo katika ghaiba -ambapo Saya Idi huwa ni sunna-. [35] Sahib Al-Hadaiq amesema: 'Kuna wanazuoni waliojuzisha kusali Sala ya Ghadir kwa jamaa'. Mwanazuoni huyo ameihusisha kauli hiyo kwa baadhi ya mafaqihi wa Kishia wakiwemo Abu Salaah Halabiy na Shahidu Al-Awwal. Ila kwa mtazamo wa mwanazuoni Al-Bahrani, ambaye ni mwanazuoni mkongwe wa Kishia, ni kwamba; kusali Sala ya Ghadir kwa jamaa ni haramu. [36] Kwa upande mwingine, mafaqihi wote wa Kisunni wanaruhusu kusali Sala zote za sunna kwa jamaa. Miongoni mwa Sala hizo ni ile Sala maarufu ya Tarawehe.[39]

Sharti za Imamu wa Sala ya jamaa

Makala asili: Imam wa Sala ya Jamaa

Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, imamu wa Sala ya jamaa ni lazima awe na akili timamu, [40] mtu mzima (ayefikia umri wa kubaleghe), [41] muumini [42] na mwadilifu [43]. Pia, imamu wa wa Sala ya jamaa ni lazima awe mzaliwa wa halali (mwanahalali na si mtoto wa zinaa) [44], na awe na uwezo wa kusali Sala sahihi. Iwapo baadhi ya wafuasi (maamuma) wake au wote kwa jumla ni wanaume, ni lazima Sala hiyo isalishwe na mwanamme.

Kumfuata Imamu wa kisunni asiyekuwa shia

Moja ya masharti ya imamu wa Sala ya jamaa ni kuwa muumini, maana yake ni kuwa mfuasi wa madhehebu ya Kishia yanayo fuata Maimamu 12 wa Kshia. [47] Kwa muktadha wa matini ya Riwaya sahihi zilizopo ndani ya vitabu mbali mbali, mafaqihi wa Kishia hawajuzishi mfuasi wa madhehebu ya Shia kumfuata imamu wa Kisunni katika Sala yake. [48], [49] Ila wanazuoni wamekhitalifiana kuhusu Mshia kumfuata imamu wa kisunni iwapo akutakuwa na dharura maalumu itakayo mfanya yeye asali Sala ya jamaa inayosalishwa na imamu wa Kisunni. Kwa mfano, kuna khitilafu miongoni mwa maulama, kuhusiana na mtu kufanya taqiyyah na kusali jamaa huku akimfuata imamu wa Kisunni; Katika hali kama hiyo, Imamu Khomeini na baadhi ya wanazuoni wengine wameona kuwa; Hakuna tatizo Mshia kusalishwa na imamu wa Kisunni. [50] Wanazuoni wengine wameweka sharti katika suala hilo wakisema: Yaweza Mshia kusalishwa na imamu wa Kisunni, ila Mshia atakaposali nyuma ya imamu wa Kisunni, basi ni lazima asiache kusoma surat Al-Fatiha. Pia kuna waliosema kuwa: Mshia akisali nyuma ya imamu wa Kisunni, basi ni lazima arudia kusali Sala hiyo. [52].

Wanawake kushiriki katika Sala ya jamaaa

Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ni bora kwa wanawake kusali nyumbani kuliko kusali msikitini kwa jamaa. Katika Hadithi hizo, msikiti ulio bora zaidi kwa wanawake -kwa ajili ya kusali- ni nyumba zao (majumbani mwao). [53] Kwa mujibu wa Hadithi hizo, malipo ya Sala ya furada ya mwanamke nyumbani kwake, ni sawa na ya Sala ya jamaa iliyo saliwa msikitini. Kwa kuzingatia Hadithi hizo, maoni ya baadhi ya maulama ni kwaba; Ni sunna kwa mwanamke kusali nyumbani kwake, na ni bora zaidi kwa wanawake kusali nyumbani kuliko kusali msikitini. [55] Pia kuna baadhi ya mafaqihi wengine walioona kuwa; Hadithi hizi zinahusiana na hali maalum, na wanaamini kuwa ni bora kwa wanawake kusali msikitini iwapo watajistiri na kuvaa hijabu zao vizuri. [56] Kundi hili la wanazuoni wenye mtazamo huu, limethibitisha hayo kwa kunukuu baadhi ya Hadithi zilizoashiria kuwepo kwa wanawake walio hudhuria katika Sala za Mtume (s.a.w.w) na kusali nyuma yake bila ya kuwepo makatazo juu ya hilo [57].

Baadhi ya sheria nyengine

  • Ukiachana na Suratu Al-Fatiha na Sura isomwayo baada ya Suratu Al-Fatiha katika Sala, ambazo maamuma (anayesalishwa) hatakiwi kuzisoma katika rakaa ya kwanza na ya pili, maamuma anapaswa kusoma dhikri nyengine zoto za Sala peke yake kimya kimya. Kinacho kusudiwa hapo ni kwamba; Maamuma hatakiwi kusoma Suratu Al-Fatiha wala Sura inayofuata katika rakaa mbili za mwanzo. Ila anatakiwa kusoma nyiradi nyengine zisizokuwa Sura mbili hizo yeye mwenyewe kimya kimya.[58]
  • Mamuma anatakiwa kumfuata imamu katika vitendo vya Sala, Na si ruhusa kwa maamuma kumtangulia imamu wake katika matendo hayo. Kwa mfano: Maamuma haruhusiwi kurukuu au kusujudu kabla ya imamu wake kurukuu au kusujudu, na iwapo atafanya hivyo, basi Sala yake itakuwa na wasi wasi. [59]
  • Haitakiwi mahala aliposimama imamu kuwa pameinuka zadi (pako juu zaidi) kuliko mahala waliposimama maamuma. [60] Hivyo basi, siku zote eneo la kibla (mihrabu) kwa kawaida huwa lipo chini zaidi kuliko eneo la maamuma. [61]
  • Haitakiwi kuwepo aina yeyote ile ya kizuizi kati ya imamu na maamuma, kama vile pazia au ukuta. Pia haitakiwi kuwepo kizuizi kati ya safu moja ya maamuma na nyengine. Hata hivyo, uwekaji wa pazia kati ya safu za wanaume na wanawake ni jambo la dharura lilikubalika kisheria. [62]
  • Imam mteule ana haki na kipaumbele zaidi kuliko wengine katika suala la kusalisha Sala za jamaa. [63]
  • Mwanamke anaweza kuwa imamu wa Sala ya jamaa ikiwa washiriki wa Sala hiyo watakuwa ni wanawake watupu (peke yao). [64]

Adabu na mapambo ya Sala ya jamaa

Sala ya jamaa ina adabu na mapambo maalumu. Katika Sala ya jamaa kuna mambo ya sunna ambayo ni mazuri na inapendeza kuyafanya, na kuna mengine ni makruhu (hayapendezi au yaliyochukiwa na Mungu) na si mazuri wala haipendezi kuyafanya. Baadhi ya Baadhi ya yale ya sunna yanayopendeza kuyafanya ni:

  • Kusimama wachamungu na wanazuoni kwenye safu ya mwanzo. [65]
  • Maamuma kusimama upande wa kulia mwa imamu wao. [66]
  • Imamu kuto refusha Sala kwa kuzingatia na kujali hali za watu wazima, wagonjwa na wanyonge, ambao ni miongoni ni mwa watu unaowasalisha. [67]
  • Kusimama na kupanga safu kwa ajili ya Sala pale isomwapo iqama. [68]
  • Maamuma kusema "Alhamdulillah," baada ya imamu kumaliza kusoma Surat Al-Fatiha. [69]

Baadhi ya mambo ambayo ni makruhu (yanayo mchukiza Mungu) katika Sala ya jamaa ni: Maamuma kusimama peke yake kando mbali na safu ya maamuma, kusali Sala ya naafila (Sala ya sunna) wakati ambao Sala inakimiwa, Maamuma asiye msafiri kumfuata imamu msafiri au imamu msafiri kumsalisha maamuma ambaye si msfiri katika Sala za rakaa nne. [70] La mwisho ni maamuma kusoma nyiradi zake kwa sauti inayosika na imamu, jambo ambalo huweza kumshughulisha imamu pamoja na maamuma wengine.[71]

Mitazao na maandiko binafsi

Suala la Sala ya jamaa ni miongoni mwa masuala yaliofafanuliwa na mafakihi mbali mbali ndani ya vitabu vyao vya kifiqhi vinavyofafanua miongozo ya ibada. Pia kuna vitabu vingi vilivyo zungumzia Sala ya jamaa na hukumu zake [72] Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Risalatu Salati Al—Jama’ati, ni makala ilioandikwa na Muhammad Hossein Kompany kwa lugha ya Kiarabu (1296-1361 Hijiria). Muhammad Hossein Kompany ni mwanasheria wa fiqhi ya Kishia wa karne ya 14. Muhammad Hossein Kompany katika malaka yake hiyo, ametafiti na kuchunguza mambo yote nanayohusiana na Sala ya jamaa, yakiwemo mambo ya wajibu, ya sunna na yale yalio makruhu ambayo hayapendezi kutendwa kwenye Sala ya jamaa. Mnamo mwaka wa 1409 Hijiria, Taasisi ya Uchapishaji ya Kiislamu ya Qom (Nashre Islamiy Qom) ilichapisha makala hiyo katika kitabu kiitwacho "Buhuthu fi Salati Al-Jama'ati Walmusafiri

Wal-Ijaarati". [73]

  • Kitabu Nab-dhatu Haula Salati Al-Jama'ati ni kitabu kilichoandikwa kupitia nukuu na chopoo zilizochopolewa kutoka katika kitabu cha Ayatullah Borojerdi kiitwacho Salatu Al-Jamaati. Chopoo na nukuu hizo zilikusanywa na kuhaririwa na Seyyed Mohammad Taqi Shahrokhi Khorramabadi, na kuchapishwa na taasisi ya uchapishaji iitwayo Nasaaye-h. Katika kitabu hichi kuna mambo tofauti yaliofafanuliwa na kudadisiwa kuhusiana na Sala ya jamaa, yakiwemo masharti ya usahihi wa Sala ya jamaa, umuhimu wa Sala jamaa, kanuni za Sala ya jamaa, masharti ya imamu wa Sala ya jamaa, pamoja na masuala kuhusiana na kujuzu au kuto juzu kumfuata imamu wa Kisunni.[74]
  • Kitabu chengine kilicho tafiti Sala ya jamaa, ni kitabu kiitwacho Namaze Jama’at wa Barakate Aan (Sala ya Jamaa na Baraka Zake), kilichoandikwa na Mohammad bin Ismail Noori kwa lugha ya Kiajemi. Hichi ni kitabu kilicho kusanya ndani yake Aya zinazohusiana na habari ya Sala ya jamaa ndani ya Quran. Sala ya Jamaa na Baraka Zake, ni kitabu kilichotafiti mabo yanayohusiana na ya Sala ya jamaa na baraka zake, ubaya wa kutosali Sala ya jamaa, sharti za Sala ya jamaa pamoja na hukumu za Sala ya jamaa. Kitabu ambacho mwishowe kilichapiswa na taasisi ya uchapishaji iitwayo Intishaaraate Bustane Kiaab, ambpo toleo la nne ndio toleo la mwisho la kitabu hichi. [75]

Vyanzo

  • Burūjirdī, Ḥusayn. kitāb al-qibla sitr wa sātir wa makān al-muṣallī. Edited by ʿAlī Panāh Ishtihārdī. Qom: Muʾassisat al-Nashr al-Islāmī, 1416 AH.
  • Ḥurr al-ʿĀmilī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Wasāʾil al-Shīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth, 1409 AH.
  • Ibn Athīr al-Jazarī, Mubārak b. Muḥammmad. Jāmiʿ al-uṣūl fī aḥādīth al-Rasūl. Edited by ʿAbd al-Qādir Arnāʾūṭ. Beirut: Dār Ibn al-Athīr, 1403 AH.
  • Ibn Ḥanbal, Aḥmad b. Muḥammad. Musnad Aḥmad. Beirut: Dār Ṣādir, [n.d].
  • Imām Khomeini, Sayyid Rūḥ Allāh. Tawḍīḥ al-masāʾil. Tehran, Muʾassisa-yi Tanẓīm wa Nashr-i Āthār-i Imām Khomeini, 1387 Sh.
  • Jazīrī, ʿAbd al-Raḥmān al-. Kitāb al-fiqh ʿalā l-madhāhib al-arbaʿa. second edition. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1424 AH.
  • Khaṭīb al-Shirbīnī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Mughnī l-muḥtāj ilā maʿrifat maʿānī l-alfāẓ al-minhāj. Edited by Jūbilī b. Ibrahīm al-Shāfiʿī. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Khūʾī, Sayyid Abū l-Qāsim al-. Al-Mustanad fī sharḥ al-ʿurwa al-wuthqā. Edited by Murtiḍā Burūjirdī. Qom: [n.p], 1421 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Muʾassisat al-Ṭabʿ wa l-Nashr, 1410 AH.
  • Muḥaqqiq al-Ḥillī, Jaʿfar b. al-Ḥusayn al-. Al-Muʿtabar. Ed. Muḥammad ʿAlī Ḥaydarī, et al. Qom, Muʾassisa-yi Sayyid al-Shuhadaʿ, 1407 AH.
  • Mūṣilī, ʿAbd Allāh b. Maḥmūd al-. Al-Ikhtīyār li-taʿlīl al-mukhtār. Edited by Maḥmūd Abū Daqīqa. Istanbul: [n.p], 1984.
  • Najafī, Muḥammad Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāyiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Narāqī, Aḥmad b. Muḥammad al-. Mustanad al-Shīʿa fī aḥkām al-sharīʿa. Qom, Muʾassisa-yi Āl al-Bayt, 1415 AH.
  • Narāqī, Aḥmad b. Muḥammad al-. Mustanad al-Shīʿa fī aḥkām al-sharīʿa. Qom: Kitābkhāna-yi Āyatollāh Marʿashī al-Najafī, 1416 AH.
  • Nūrī, Mīrzā Ḥusayn al-. Mustadrak al-wasāʾil. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt li-Iḥyāʾ al-Turāth, 1408 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Muqniʿ fī l-fiqh. Qom, Muʾassisat al-Imām al-Hādī, 1415 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā-yaḍuruh al-faqīh. Ed. ʿAlī Akbar Ghaffārī. Qom, Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Muqniʿ fī l-fiqh. Qom: Muʾassisat al-Imām al-Hādī, 1415 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Thawāb al-aʿmāl. Qom: Dār al-Shrīf, 1406 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Kitab al-khilāf. Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1407 AH.
  • Yazdī al-Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Kāẓim al-. Al-ʿUrwa al-wuthqā. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlamī, 1409 AH.