Nenda kwa yaliyomo

Sahw al-Nabi

Kutoka wikishia
Kitabu Risalat fi Sahw al-Nabi kilichoandikwa na Sheikh Mufid

Sahw al-Nabi (Kiarabu: سَهْوُ النَّبی (ص)) ni uwezekano wa kukosea na kusahau Mtume (s.a.w.w) katika masuala ya kila siku ya maisha. Akthari ya Maulamaa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaamini kwamba, ni jambo lisilowezekana kwa Mtume kukosea au kusahau (Sahw al-Nabi); hata hivyo baadhi yao kama Sheikh Saduq na mwalimu wake Ibn Walid wanaamini kwamba, hilo ni jambo ambalo linawezekana; yaani licha ya kuwa wanakubali kwamba, kuhusiana na suala la kutenda dhambi na majukumu ya Utume, Mtume (s.a.w.w) ni Maasumu (hatendi dhambi wala hakosei katika haya) lakini yumkini katika masuala mengine ya maisha akakosea au akasahau.

Wanaoafiki na kukubali suala la uwezekano wa Mtume kusahau au kukosea katika masuala ya maisha wakiwa na lengo la kuthibitisha nadharia na mtazamo wao huu wanategemea hadithi ambapo zinaeleza kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikosea katika Sala; hata hivyo wapinzani na wanaokataa mtazamo huo wanasema kuwa, kusahau au kukosea Mtume ni jambo ambalo haliwezi kuwa pamoja na Utume (haiwezekani kwa Mtume kusahau au kufanya kosa) na wanasema kuwa, hadithi hizo hazina itibari na wala si kutegemeka.

Utambuzi wa maana

Sahw al-Nabi ni kosa na kukosea Mtume (s.a.w.w) katika kufanyia kazi hukumu ya kidini na masuala ya kawaida. [1] Katika suala la Sahw al-Nabi, kuna swali hapa nalo ni kwamba, je, katika kufanyia kazi hukumu za kisheria au kufanya mambo ya kawaida ya kimaisha yumkini Mitume wakakosea au kusahau? Kwa mfano wasahau kitu katika Sala au wakakosea na kusahau na hivyo wakamrejeshea mtu dinari 100 mtu ambaye walimkopa dinari 1000. [2]

Sahw al-Nabi ni maudhui ya kiteolojia [3] na kumefanyika mazungumzo na mijadala mirefu na mipana kuhusiana nayo baina ya wanateolojia. [4] Kadhia ya Sahw al-Nabi huzungumziwa katika vitabu vya teolojia [5] na maudhui inayohusiana na Umaasumu wa Mitume na katika vitabu vya Fiqhi [6] jambo hili huzungumziwa katika maudhui ya kusahau katika Sala.

Mitazamo tofauti

Kuna mitazamo miwili baina ya Maulamaa wa Shia Imamiyyah kuhusiana na uwezekano wa Mtume kusahau au kukosea katika masuala ya kawaida ya maisha. Akthari yao wanasema kuwa, haiwezekani Mtume kusahau au kuikosea; [7] lakini baadhi yao wanaamini kwamba, yumkini Mtume akakosea au akasahau kufanyia kazi hukumu za kisheria. [8]

Wanaoafiki

Ibn Walid Qomi, Sheikh Saduq, Sayyid Murtadha, [9] Fadhl bin Hassan Tabarsi mwandishi wa tafsiri ya Maj’maa al-Bayan, [10] na Muhammad Taqi Shushtari, [11] ni miongoni mwa wafuasi wa nadharia na mtazamo wa uwezekano wa Mtume kusahau au kukosea (Sahw al-Nabi). [12] Katika kitabu chake cha Man La Yahdhuruh al-Faqih, Sheikh Saduq ametetea mtazamo wa Sahw al-Nabi na wanaopinga amewatambua kuwa ni maghulati na watu wa Tafwidh (Mwenyezi Mungu amempa mamlaka na uhuru kamili mwanadamu wa kufanya atakavyo). Anaamini kwamba, Mtume (s.a.w.w) ni Maasumu (hatendi dhambi wala hakosei) katika jambo la risala na kufikisha dini kwa watu, lakini katika masuala mengine kama kusali, yuko kama watu wengine tu wa kawaida na yumkini akakosea; [13] hata hivyo Shekhe Saduq hatambui Sahw al-Nabi kwamba, ni sawa na Sahw ya wanadamu wengine, bali anatambua kuwa, Sahw hii inatoka kwa Mwenyezi Mungu ili kusitokee mkanganyo na makosa baina ya daraja ya Utume na daraja ya Uola na Uungu. [14]

Katika kitabu hiki hiki Shekhe Saduq anatoa ahadi ya kuandika kitabu ambacho ndani yake atathibitisha kwamba, Mtume anasahu na kukosea katika mambo ya kawaida ya maisha na kukana mtazamo wa wanaopinga hili. [15] Ananukuu kutoka kwa Ibn Walid ambaye ni mwalimu wake kwamba, daraja ya kwanza ya ughulati ni kukana kwamba, Mtume anaweza kukosea au kusahau katika mambo ambayo hayahusiani na risala yake. [16]

Hoja za wanaoafiki

Wanaoamini uwezekano wa kusahau na kukosea Mtume (s.a.w.w) wanategemea hoja za Aya za Qur’ani na hadithi mbalimbali. Fadhl bin Tabarsi amesema katika tafsiri ya Aya ya 68 ya Surat al-An’am kwamba: Kwa mujibu wa itikadi ya Mashia, Mtume na Maimamu kile ambacho wanabainisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu hawakosei wala kusahau, lakini kuna uwezekano wakakosea na kusahau katika masuala mengine. Hata hivyo jambo hili ni mpaka pale ambapo hawajakumbwa na hali ya matatizo ya kiakili. [17]

Anasema: Kama ambavyo tunakubali kwamba, Mtume na Maimamu wanakumbwa na hali ya kulala na kupoteza fahamu, ni lazima tukubali kwamba, kukosea na kusahau ni jambo ambalo kwao linawezekana pia; kwani usingizi na kupoteza fahamu ni mithili ya kusahau. [18]

Sheikh Saduq pia ametumia hadithi ambazo ndani yake zinaonyesha kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikosea katika Sala. [19] Hadithi hizi zimenukuliwa katika vyanzo na vitabu vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Sunni na Shia. [20] Sheikh Ja’far Sobhani anasema kuwa, idadi ya hadithi hizi katika vitabu vya hadithi vya Kishia haizidi 12. [21] Miongoni mwa hadithi hizo ni ile ambayo imenukuliwa na Sheikh Kulayni katika al-Kafi akinukuu kutoka kwa Imamu Ja’far Sadiq (a.s). Kwa mujibu wa hadithi hii, Mtume (s.a.w.w) alifanya makosa katika Sala ya Adhuhuri ambapo akiwa katika rakaa ya pili alitoa kimakosa salamu ya Sala (ya kumaliza Sala) na baada ya kukumbushwa na Waislamu, alikamilisha Sala na kisha akaleta sijda mbili za kusahau. [22]

Wapinzani wa Sahwa al-Nabi

Sheikh Ja’far Sobhani anasema kuwa, akthari ya Maulamaa wa Kishia hawakubaliana na suala la Mtume kusahau au kukosea (Sahw al-Nabi). [23] ananukuu maneno ya Maulamaa waliotangulia wa Kishia kama Sheikh Mufid, Allama Hilli, Muhaqqiq Hilli na Shahid al-Awwal wakipinga Sahw al-Nabi [24] na wanasema kwamba, nadharia ya Sahw al-Nabi ni mtazamo ambao haukubaliki katika madhehebu ya Shia. [25] Allama Tabatabi, mfasiri mkubwa wa Qur’ani wa Kishia pia anasema kuwa, kusahau au kukosea Mtume (s.a.w.w) ni jambo ambalo haliendani wala kuoana na Umaasumu. [26]

Wapinzani wa nadharia hii wametilia ishkali mtazamo wa wanaounga mkono Sahw al-Nabii katika mijadala na maudhui mbalimbali kama za kifiq’h wakati wa kuzungumzia suala la kusahau katika Sala na katika teolojia wakati wa kujadili Umaasumu wa Mitume. Wameandika vitabu vya kujitegemea pia katika uwanja huu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni “Risalat fi adam sahw al-Nabi (s.a.w.w)”, kitabu ambacho kimenasibishwa na Sheikh Mufid na vilevile Sayyid Murtadha; Hata hivyo, Allama Majlisi katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar anaona kuwa, kunasibishwa kitabu hicho kwa Sheikh Mufid ni jambo mwafaka zaidi. [28] Kadhalika kuna kitabu kingine kinachoitwa al-Tanbih bil-ma’lum minal Burhan an tanzih al-ma’sum min al-Sahw wal-nisyan”, ambapo ndani yake Sheikh Hurr al-Amili amebainisha na kuzungumzia kwa mapana na marefu maudhui hii. [29]

Hoja za wapinzani

Sheikh Mufid anaamini kwamba, hadithi zinazotumiwa kuthibitisha Sahw al-Nabii ni hadithi za khabar wahed (hadithi ambayo kutokana na idadi ya wapokezi wake hakuna uhakika kama imetoka kwa Maasumu) na kwa msingi huo inatia shaka na dhana. Matokeo yake ni kutokuwa na itibari ya kisheria. [30] Kadhalika kutokana na matini na andiko la hadithi hizi ambapo kuna hitilafu kubwa, ametilia ishkali itibari yake. [31]

Allama Hilli ameandika katika Kashf al-Murad: Kama kusahau na kukosea Mtume ni jambo linalowezeikana, kuna uwezekano wa kosa hilo kuingia pia katika Utume wake. [32] Ameandika katika kitabu chake cha fiq’h cha Muntaha al-Matlab fi tahqiq al-Madh’hab ambacho kipo katika sura ya fiq’h istilad na Fiq’h Muqarana (fiq’h ya utoaji hoja na ulinganishaji) kwamba: Kwa hoja hii ni muhali kiakili kuweko Sahw al-Nabi na amezitambua hadithi zinazungumzia uwezekano wa Nabii kusahau au kukosea kuwa ni batili. [33] Shahid al-Awwal pia katika cha Dhikra, ametilia shaka hadithi zinazozungumzia Sahw al-Nabi kwa hoja hiyo hiyo. [34]

Allama Tabatabi katika tafsiri yake ya al-Mizan anautambua uhakika wa Umaasumu kwa Mitume kwamba, ni aina ya elimu na hisia ambayo haiwezekani kudirikiwa na wanadamu wa kawaida na ina tofauti na elimu nyingine na ni kupitia hilo kunapatikana kinga mutlaki kwa Mitume ya kufanya aina yoyote ile ya upotofu au kukosea. [35]

Bibliografia

Baadhi ya vitabu vilivyoandika kuhusiana na Sahw al-Nabi ni:

Muhammad Baqir Majlisi pia katika kitabu chake cha Bihar al-Anwar ametenga faslu ya 16 ya historia ya Mtume wa Uislamu na kuifanya maalumu kwa maudhui ya Sahw al-Nabi. [37]

Masuala yanayofungamana

Vyanzo

  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Kashf al-murād. Seventh edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Muntahā l-maṭlab fī taḥqīq al-madhhab. Mashhad: Majmaʿ al-Buḥūth al-Islāmīyya, 1412 AH.
  • Ibrāhīmī Rād, Muḥammad. 1388 Sh. "Taḥlīl wa barrasī-yi riwāyāt-i sahw al-Nabī." ʿUlūm Ḥadīth 52:55-70.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al- Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī. Fourth edition. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. ʿAdam sahw al-Nabī. Qom: al-Muʿtamar al-ʿĀlamī li-l-Shaykh al-Mufīd, 1413 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Second edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Sayyid Murtaḍā. Tanzīh al-anbīyāʾ wa l-aʾimma. Edited by Fāris Ḥasūn al-Karīm. Qom: Būstān-i Kitāb, 1422 AH.
  • Shahīḍ al-Awwal, Muḥammad b. al-ʿĀmilī al-. Dhikrā al-Shīʿa fī aḥkām al-sharīʿa. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt, 1419 AH.
  • Subḥānī, Jaʿfar. ʿIṣmat al-anbīyāʾ. Second edition. Qom: Muʾassisat Imām al-Sādiq, 1420 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān. Tehran: Nāṣir Khusru, 1372 Sh.