Nenda kwa yaliyomo

Fat’wa

Kutoka wikishia

Fat’wa (Kiarabu: الفتوى) ni rai na mtazamo wa Mujtahidi au Marjaa Taqlidi kuhusu wadhifa na jukumu la kisheria la wakalafu (mukallifin) ambao unanyambuliwa na kuchukuliwa kutoka katika Adilat al-Ar’ba’ (Qur’an, Sunna, ijmaa na akili). Kwa mujibu wa mafakihi wa Kishia ni kwamba, uadilifu, kuwa Shia wa Maimamu 12, mjuzi zaidi, mwana wa halali na kuwa na ujuzi wa njia na elimu za lazima katika uga wa kunyambua hukumu za kisheria ni miongoni mwa masharti anayopaswa kutimiza yule anayefutu (kutoa fat’wa).

Kikawaida fat’wa hubainishwa kwa maneno ya wajibu, haramu, makuruhu, mustahabu na mubaha. Wakati mwingine ili kubainisha fat’wa hutumika pia maneno kama “lililo na nguvu”, “kwa kauli yenye nguvu” na “lililo dhahiri zaidi”. Kadhalika kusikia kauli kutoka kwa Mufti mwenyewe, kutoa habari watu wawili waadilifu, kutoa habari mtu mmoja muadilifu au mtu mmoja mwenye kuaminika ambapo kupitia maneno yake upatikane uhakika na vilevile kupata fat’wa katika vitabu vya Tawdhih al-Masail (Kufafanua Sheria za Kiislamu) ni miongoni mwa njia za kupata fat’wa ya mujtahidi.

Imeelezwa kuhusiana na tofauti baina ya fat’wa na hukumu ya kwamba, fat’wa ni ubainishaji wa hukumu kwa sura jumla kwa mukalidina (wafuasi) wa mujtahidi; lakini hukumu ni amri ya mtawala ya kufanya au kuacha kufanya kazi au jambo maalumu na hilo ni wajibu kwa watu wote wanaohutubiwa kutekeleza hukumu hii.

Baadhi ya fat’wa zilizotolewa na mafakihi wa Kishia ni: Fat’wa ya kuharamisha tumbaku (matumizi ya), fat’wa ya jihadi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na fat’wa ya kuharamisha kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu wa madhehebu ya Ahlu-Sunna.

Utambuzi wa maana

Fat’wa au kufutu maana yake ni mujtahidi kueleza rai na mtazamo kuhusiana na hukumu ya kisheria na kutangaza hilo kwa ajili ya kuwafahamisha wanaomfuata (muqalidina). [1] Kuombwa kutoa raia na mtazamo wa fakihi kuhusiana na suala la kisheria kunajulikana kwa jina la “istifita’”. [2] Anayefutu na kutoa fat’wa anajulikana kwa jina la “Mufti” na mtu ambaye anachukua fat’wa kutoka kwake anafahamika kwa jina la “Mustafti”. [3]

Katika vitabu vya fikihi katika mlango wa Ijtihadi na Mujtahidi kunajadiliwa kuhusiana na hukumu za fa’wa. [4]

Tofauti ya fatwa na hukumu

Mafakihi wamaetaja tofauti kadhaa baina ya fat’wa na hukumu. Miongoni mwazo ni:

  1. Fat’wa ni bainisho (ubainishaji) jumla. Kama vile, “matumizi ya madawa ya kulevya ni haramu kwa watu wote” lakini hukumu ya mtawala ni agizo la amri ya kufanya au kuacha kufanya kazi au jambo maalumu. Kama vile, hukumu ya kususia bidhaa maalumu. [5]
  2. Katika fat’wa kutabikisha na kuanisha maudhui ya jambo husika ni jukumu la mukallafu, lakini kutabikisha hukumu, ni kwa mujibu na aria ya mtawala na sio mukallafini kama vile hukumu ya mtawala wa kisheria kuhusiana na hilali (mwandamo) ya mwezi wa Ramadhani. [6]
  3. Fat’wa ya mujtahidi ni hoja ya kisheria kwa ajili ya wafuasi wake tu; lakini hukumu ya mtawala wa kisheria (mtawala wa kidini) sio maalumu kwa wafuasi tu balo ni hoja kwa watu wote. [7] Hata kwa mujtahidi ambaye ni msomi na mjuzi zaidi ya mtawala wa kisheria, naye pia anapaswa kufuata hukumu ya mtawala. [8]

Vyanzo vya kutoa fat’wa

Makala asili: Adilat al-Ar’ba’

Fa’twa huwa hoja pale inapokuwa na mashiko ya kisheria yenye itibari; kinyume na hivyo ni haramu kuifanyia kazi. [9] Hoja na mashiko ya kisheria yenye itibari yanatoka katika vyanzo vinne ambavyo ni:

  1. Qur’an: Takribani kuna Aya 500 kutoka katika Aya 6000 (takriban moja ya 13) ambazo ni maalumu kwa hukumu za kisheria. [10] Hata hivyo kwa mujibu wa nadharia na mtazamo wa Muhammad Hadi Maarefat, kunyambua na kutoa hukumu za kisheria hakuishii katika Aya hizi tu. [11]
  2. Sunna: Kauli, kitendo au taqriri ya Maasumu (kunyamazia kimya neno lililosemwa au kitendo kilichofanywa mbele yake na kutoonyesha upinzani); [12] Waislamu wa madhehebu ya Shia wanatambua Sunna za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu (a.s) kuwa ni hoja; lakini Waislamu wa madhehebu ya Sunni wao wanatambua Sunna za Mtume (s.a.w.w) tu kwamba, ndio hoja. [13]
  3. Ij’maa: Ijmaa ina maana ya itifaki, kauli moja na kukubaliana Maulamaa kuhusiana na jambo fulani. [14] Kwa mujibu wa mtazamo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Ij’maa huwa hoja pale inapokuwa na ishara za mtazamo wa Mtume (s.a.w.w) au Maimamu (a.s). [15]
  4. Akili: Hoja ya kiakili, ni hukumu ambayo kupitia kwayo inawezekana kufikia hukumu ya kisheria. [16] Hata hivyo kundi la Akhbariyun lenyewe halitambui akili kama dalili na hoja ya kunyambua hukumu za kisheria. [17]

Sifa maalumu za Mufti

Kumebainishwa sifa maalumu anazopaswa kuwa nazo Mufti. Kubaleghe, akili, uadilifu, kuwa Shia wa Maimamu 12, kuwa mjuzi zaidi na kuwa mwana wa halali ni miongoni mwa masharti ya anayefutu (kutoa fat’wa) ambayo anapaswa kuyatimiza. [18] Kadhalika Mufti anapaswa kuwa na ujuzi wa njia na elimu za lazima katika uga wa kunyambua hukumu za kisheria. Anapaswa kuwa msomi na alimu na aweze kubainisha hukumu kwa mujibu wa hoja na misingi yake. [19] Kwa muktadha huo, Mufti anapaswa kuwa mjuzi wa Qur’ani na Sunna (hadithi). Kadhalika awe anatambua kuhusu Nasikh na Mansukh, (zilizofuta na zilizofutwa), aam na Khaas (jumla na maalumu), mutlaki, qayyid (zilizo na sharti) na hakika na na majazi yake. [20]

Hukumu

Baadhi ya hukumu zinazohusiana na fat’wa ni:

  • Haijuzu kurejea kwa Mufti na kuwa muqalidi kwa mtu ambaye yeye mwenyewe ana uwezo na ujuzi wa kunyambua na kutoa hukumu za sheria kutoka katika vyanzo vyake. [21]
  • Ni haramu kutoa fat’wa kwa mtu ambaye hana uwezo wa kunyambua na kutoka hukumu kutoka katika vyanzo vya sheria (Adilat al-Ar’ba’). [22]
  • Njia za kupata fatu’wa ni: Kusikia kauli kutoka kwa Mufti mwenyewe, kutoa habari watu wawili waadilifu, kutoa habari mtu mmoja muadilifu au mtu mmoja mwenye kuaminika ambapo kupitia maneno yake upatikane uhakika na vilevile kupata fat’wa katika vitabu vya Tawdhih al-Masail (Kufafanua Sheria za Kiislamu). [23]
  • Kama fat’wa ya mujtahidi itabadilika kuna hitilafu kuhusiana na wajibu wa kuitangaza kwa ajili ya muqalidina. [24] Kwa mujibu wa baadhi ya mafakihi ni kuwa, kama fat’wa ya kabla inaafikiana na ihtiyah (tahadhari), sio wajibu kutangaza mabadiliko ya fat’wa kwa muqalidina. [25] Baadhi ya wengine wanasema, kutangaza fat’wa mpya kwa ajili ya muqalidina sio wajibu; kwani fat’wa ya kabla pia ilitolewa kwa mujibu wa mazingira na vigezo vya ijtihadi. [26]
  • Kama mujtahidi mjuzi zaidi (a’lam) atatoa fat’wa kuhusiana na maudhui fulani, mtu ambaye anamkalidi na kumfuata hawezi katika jambo hilo kufuata fat’wa ya mujtahidi mwingine. [27]
  • Mufti anaruhusiwa kufutu pale anapokuwa na uhakika kwamba, ana udhibiti na kila ambacho kinahusiana na unyambuaji wa hukumu. [28]

Maneno ambayo ni kiashirio cha fat’wa

Maneno ambayo ni kiashirio cha fat’wa yapo katika hali mbili:

  • Maneno ambayo yanaashiria moja kwa moja fat’wa: Kama vile wajibu, haramu, makuruhu, mustahabu na mubaha. [29] Wakati mwingine ili kubainisha fat’wa hutumika pia maneno kama “lililo lenye nguvu”, “kwa kauli yenye nguvu”, “lililo dhahiri zaidi” “si jambo lililo mbali” na tahadhari yenye nguvu zaidi”. [30
  • Maneno ambayo yamo katika ibara ya fat’wa: Kama “si jambo lililo mbali lakini jambo lina mushkili”, tahadhari licha ya kuwa halina nguvu” na mfano wa hayo, muqalidi hawezi katika mambo ambayo yametumika ibara kama hizi kurejea kwa mujtahidi mwengine. [31]

Ihtiyat Wajib na Ihtiyat Mustahab sio fat’wa

Ihtiyat wajib (tahadhari ya wajibu) na ihtiyat mustahab (tahadhari ya mustahabu) sio fat’wa. Katika tahadhari ya wajibu, mujtahidi hajafikia natija ya mia kwa mia kuhusiana na suala fulani la kisheria na hivyo hatoi fat’wa. Katika mazingira kama haya tangu awali anabainisha jukumu na wadhifa wa muqallid kwa sura na ihtiyat. Katika hali hii muqallid anaweza kuifanyia kazi hiyo hiyo tahadhari (ihtiyat) au arejee fat’wa ya Marjaa mwingine ambaye anamuona kuwa ni mjuzi zaidi baada ya Marjaa wake. [32]

Katika ihtiyat ya mustahabu (tahadhari ya mustahabu), Mujtahidi hajafikia natija na ametoa fat’wa; lakini ameonyesha pia njia ya kufanya ihtiyat. Katika hali hii, mukalidi anaweza kufanyia kazi fat’wa au ihtiyat. [33] Neno “ihtiyat” katika vitabu vya fat’wa, kama litakuja kabla au baada ya fat’wa, ni ishara kwamba, hiyo ni ihtiyat mustahabu, na kama halikuwa kabla au baada ya fat’wa, ni ishara kwamba, ni ihtiyat wajib. [34]

Fat’wa za kihistoria

Baadhi ya fat’wa za kihistoria na mafakihi wa Kishia ni:

  • Fa’twa inayonasibishwa na Sharih Qadhi kwa ajili ya kuidhinisha kuuawa Imamu Hussein (a.s). [35]
  • Fat’wa ya kuharamisha tumbaku: Fat’wa ya Mirza Shirazi ambayo aliitoa mwaka 1891 akitoa jibu kwa hatua ya Nassir al-Din Shah ya kuipatia mkataba wa kuhodhi tumbaku kampuni ya Uingereza Regie katika miji minne ya Iran na kwa mujibu wake mkataba huo ukafutwa. [36]
  • Fat’wa ya Mirza Taqi Shirazi juu ya ulazima wa jihadi na mapambano dhidi ya Uingereza: Fatwa hii ilitolewa 1919-20 na ikapelekea kuanza harakati na mapambano ya wananchi wa Iraq dhidi ya wavamizi wa Kiingereza [37] na kupelekea kukombolewa Iraq kutoka katika udhibiti na makucha ya mkoloni Muingereza. [38]
  • Fat’wa ya Muhsin Hakim ya kuharamisha kujiunga na chama cha Kikomunisti: Fat’wa hii ilitolewa 1960-1 baada ya kuingia madarakani Abdul-Karim Qassim huko Iraq na kuanza kuenea fikra zisizo za kidini. Sayyid Muhsin Hakim kupitia fat’wa mbili, alitangaza kuwa kisheria haijuzu kujiunga na chama cha kikomonisti na akalitambua hilo kuwa hukumu yake ni sawa na ukafiri na ulahidi au kueneza haya. [39]
  • Fat’wa (hukumu) ya kuuawa murtadi Salman Rushdie: Fat'wa hii ilitolewa na Imamu Khomeini mwaka 1989. [40] Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa fatwa ya kuuawa murtadi huyo kutokana na kuutukana Uislamu kwa kuandika kitabu cha Satanic Verses (Aya za Shetani).
  • Fat’wa ya jihadi dhidi ya Daesh (ISIS): Fat’wa ya Sayyid Ali Sistani, Marjaa Taqlid anayeishi Iraq ambayo aliitoa mwaka 2014. Katika fat’wa hiyo, Ayatullah Sistan alisema, ni wajibu kifai kuihami na kuitetea Iraq na matukufu yake na akayataka makundi ya wananchi kujitokeza na kukabiliana na matakfiri wa Daesh. Baada ya kutolewa fat’wa hiyo, kukaundwa kundi la wananchi la Hashd al-Sha’abi na hivyo kupelekea kufukuzwa kundi la kigaidi la Daesh kutoka katika ardhi ya Iraq. [41]
  • Fat’wa ya kuharamisha kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu wa Kisunni: Fat’wa hii ilitolewa na Ayatullah Khamenei baada ya Yassir al-Habib kumvunjia heshima Aisha mke wa Mtume (s.a.w.w) na Istifta’ ya Maulamaa wa Shia wa eneo la al-Ahsa Saudi Arabia. [42]
  • Fat’wa ya Sheikh Shaltut ya kujuzisha kufanyia kazi madhehebu ya Shia: Sheikh Mahmoud Shaltut ni katika mafakihi wa Ahlul Sunna na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar, mwaka 1958 alitoa fat’wa ya kiitikadi na akasema kwamba, inajuzu kufuata madhehebu ya Jaafariya (Shia) kama ilivyo kwa madhehebu zingine za Kisunni. [43]

Fat’wa ambazo ni “Shadhdh”

Fat’wa ambayo inapingana na fat’wa mashuhuri inatambulika kwa jina la fat’wa shadhdh au “tafarrud fat’wa (fat’wa kujitenga). [44] Baadhi ya fat’wa hizo ni:

  • Kuwa tohara viungo visivyo na uhai vya mbwa na nguruwe: Sayyid Murtadha mmoja wa mafakihi wa Kishia anaamini kwamba, nywele za mbwa na nguruwe sio najisi kutokana na kuwa ni katika viungo visivyo na uhai. [45] Kwa mujibu wa Muhammad Hassan Najafi, fat’wa hiyo ya Sayyid Murtadha inapingana na nadharia na raia mashuhuri ya mafakihi wa Kishia. [46]
  • Kuwa tohara pombe: Kwa mujibu wa Sahib al-Jawahir, baadhi ya mafakihi kama Sheikh Saduq, Ibn Abi Aqil al-Ummani [47] na Muhaqqiq Ardabili [48] wametoa fat’wa kinyume na rai na mtazamo mashuhuri wa mafakihi wa Kishia na kusema kuwa pombe na vileo ni tohara. Allama Hilli anasema katika kitabu cha Mukhtalaf al-Shi'a, kuwa najisi pombe na vileo ni mtazamo mashuhuri wa mafakihi wa Kishia. [49]
  • Kuwa sawa dia ya mwanamke na mwanaume: Kwa mujibu wa fat’wa ya Ayatullah Yousef Saanei mtazamo wake ni kuwa dia ya mwanamke na mwanaume ni sawa. [50] Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa mtazamo mashuhuri wa mafakihi wa Kishia dia ya mwanamke Mwislamu ni nusu ya dia ya mwanaume. [51]

Baraza la Fat’wa

Baraza la Fat’wa ni kundi la watu ambalo badala ya kumkalidi mtu fulani, linafuata mtazamo wa kundi fulani la mafakihi. Katika hili mpango kama kuwa na mtazamo mmoja katika masuala yote baina ya mafakihi ni jambo ambalo haliwezekani hivyo, kigezo kinakuwa ni mtazamo wa walio wengi. [52]

Kwa mujibu wa wafuasi wa nadharia hii ni kwamba, kufanyia tathmini na uchunguzi hoja za fat’wa na ulazima wa kumkalidi Mujtahidi zinaonyesha kuwa, kuna kigezo cha hoja katika fat’wa ya mtu na katika fat’wa ya kikundi (baraza). [53] Hata hivyo, mtazamo huu umekosolewa na baadhi ya wahakiki. [54]

Baraza la Istifta’

Baraza la Istifta’ ni kundi la mujitahidina ambalo linafanya uhakiki kuhusiana na suala fulani la kisheria na linampatia Marjaa Taqlidi mtazamo wa kiushauri kuhusiana na jambo hilo. [55] Marjaa Taqlidi akiwa katika daraja na nafasi ya kutoa majibu kwa wakalidi wake, anawapatia mtazamo wake wajumbe wa baraza hilo na wao kama kuna kitu cha kukamilishia fat’wa hiyo basi hutoa mtazamo wao na hatimaye hatua ya mwisho ni Marjaa mwenyewe kukusanya mitazamo hiyo na hivyo kutoa fat’wa kuhusiana na jambo husika. Kwa maana kwamba, jukumu la kutoa fat’wa ni la Marjaa Taqlidi mwenyewe. [56]

Masuala yanayo fungamana

Rejea

Vyanzo