Nenda kwa yaliyomo

Kuzika

Kutoka wikishia
Picha: namna ya kuiweka maiti kaburini

Kuzika (Kiarabu: الدفن) maana yake ni kufukia maiti ya chini ya ardhi. Kuzika maiti ni katika Wajib Kifai ambapo mkusudiwa sio mtu maalumu; kwa maana kwamba, kwa mujibu sheria, kila ambaye atatekeleza hilo basi itatosheleza. Kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kabla ya maiti kuzikwa kuna mambo ambayo ni lazima kumfanyia maiti kama kumuosha, kumkafini (kumvisha sanda) na kumsalia. Kwa mujibu wa hadithi ni kwamba, falsafa ya kuzika maiti ni kuchunga na kuheshimu maiti ya Mwislamu na kuzuia adha kwa watu na kuzuia pia kudhihirika kuharibika mwili huo.

Kuzika maiti kuna ada, adabu na hukumu zake ambapo baadhi yake ni wajibu na zingine ni mustahabu ambapo baadhi ya mambo ya mustajabu ya kumfanyia maiti ni kumsomea talqini na kumswalia Salat Laylat al-Dafn au Salat al-Wahshah (Sala ya usiku wa kwanza kaburini).

Utambuzi wa maana na nafasi yake

Kuzika maiti ni kuutia na kuufukia kaburini mwili wa mtu aliyeaga dunia kwa namna ambayo, wanyama wakali wasiweze kuutoa mwili huu kama ambavyo maiti inapaswa kufukiwa kwa namna ambayo harufu yake isiudhi watu wengine wanaoishi au kupita karibu na eneo husika. [1] Kuzika maiti ni katika Wajib Kifai [2] ambapo mkusudiwa sio mtu maalumu; kwa maana kwamba, kwa mujibu sheria, kila ambaye atatekeleza hilo basi itatosheleza. Sheria na hukumu za maiti zimebainishwa katika vitabu vya ufafanuzi wa hukumu na sheria za Kiislamu (Tawdhih al-Masail) [3] au vitabu milango na faslu za hukumu za jeneza kwenye vitabu vya fikihi na hadithi. [4]

Falsafa

Kwa mujibu wa hadithi kumebainisha hekima na falsafa ya kuzika maiti kwamba, ni kuchunga na kuheshimu maiti ya Mwislamu, kuzuia adha kwa watu kwa kuenea harufu, kuzuia pia kudhihirika kuharibika mwili huo na kuepusha lawama za maadui na huzuni za marafiki. [5] Wakati Qabil alipomuua Habil hakujua afanye nini. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu kunguru wawili wakapigana na mmoja akamuua mwingine na kisha aliyebakia hai akitumia mdomo wake akachimba shimo na kumzika kunguru mwenziwe. [6]

Hukumu za wajibu kwa maiti

Baadhi ya hukumu ambazo ni wajibu kwa ajili ya kuzika ni:

  • Kwa mujibu wa fat’wa za mafakihi maiti anapaswa kuzikwa baada ya kuosha, tahnit (Kupakwa maiti kafuri mahali maalum ni faradhi kwa Waislamu baada ya kumwosha na kupanguswa (afutwe vizuri kwa nguo kavu) maiti kabla ya kusaliwa na kuzikwa apakwe Kafuri laini sehemu saba (viongo vya kusujudia) navyo ni kipaji, viganja viwili, magoti mawili, ncha za vidole gumba viwili), kukafiniwa (kuvishwa sanda) na kumswalia. [7]
  • Ni wajibu maiti kulazwa kaburini kwa ubavu wa kulia akiwa ameelekea kibla. [8]
  • Ili kuzika maiti ni lazima kuomba idhini ya walii wake. [9]
  • Haijuzu kuwazika Waislamu katika makaburi ya makafiri na kinyume chake pia. [10]
  • Kuzika maiti hakuhitajii kutia nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. [11]

Adabu na mambo ya mustahabu

Katika vyanzo vya fikihi kumetajwa na kubainishwa adabu ambazo zinapaswa kufanywa kabla na baada ya kuzika. Miongoni mwazo ni:

  • Kumsomea talqini maiti (kutikisa mabega ya maiti sambamba na kutaja jina la maiti na kusoma dhikri maalumu).
  • Kuweka chini jeneza karibu na kaburi na kulinyanyua na kuliweka chini mara kadhaa.
  • Kusoma dua maalumu wakati wa kuingiza maiti kaburini.
  • Maiti ya mwanamnke iingizwe kaburini kwa kutangulia ubavu na ya mwanaume iingizwe kwa kutanguliza kichwa.
  • Kuzika maiti katika makaburi ya karibu zaidi isipokuwa kama kupelekwa maiti katika makaburi ya mbali kuna kitu na sifa maalumu kwa mfano makaburi hayo ni sehemu ya kuzikwa makaburi ya Maulamaa, waja wema au kujitokeza watu hapo kwa ajili ya kwenda kusoma fatiha kwa ajili ya maiti.
  • Kuianisha sehemu aliyozikwa maiti na kuandika jina juu yake.
  • Kuwapelekea chakula wafiwa kwa muda wa siku tatu na ni makuruhu kula chakula chao.
  • Kusali Salat al-Wahsha katika usiku wa kwanza kaburini.
  • Kuwaliwaza na kuwapa pole wafiwa. [12]
  • Kupeleka maiti katika maeneo matakatifu kabla ya kumzika. [13]
  • Kuchimba lahad (mwanadani) katika kaburi ili kuzuia udongo kumfikia maiti. [14]

Hukumu ya mtu ambaye amefia baharini

Kama mtu atafia baharini na mpaka kufika ufukweni mwili wake ukawa umeharibika kwa kukauka, baada ya kuoshwa, kukafiniwa na kusaliwa utatupwa baharini kwa adabu na taratibu maalumu. Kadhalika endapo kutakuwa na hatari ya kaburi lake kufukuliwa na adui. [15]

Ni haramu kufukua kaburi

Mafakihi wa Kishia wanasema kuwa, ni haramu kufukua kaburi. Isipokuwa kama maiti amezkwa katika sehemu ya ghasb (sehemu ambayo imepatikana kwa njia ya unyang’anyi), sanda yake ni ya ghasb, amezikwa bila kuoshwa au hakuvishwa sanda kwa njia sahihi, hakuoshwa kwa njia sahihi, [16] kuzikwa maiti katika maeneo ambayo itakuwa sababu ya kuvunjiwa heshima, (kama vile kuzika Waislamu katika makaburi ya makafiri). Hivyo katika hali hizi inajuzu kufukua kaburi. [17]

Rejea

Vyanzo