Nenda kwa yaliyomo

Jeshi la Omar bin Sa’d

Kutoka wikishia
Kambi ya Imamu Hussein (a.s) na kambi ya Omar bin Saad

Jeshi la Omar bin Sa’d (Kiarabu: جيش عمر بن سعد) lilikuwa jeshi lililokuwa limekusanywa na Omar bin Sa’d kwa amri ya Ubaidullah ibn Ziyad na katika siku ya Ashura lilipigana na Imamu Hussein (a.s) na maswahaba zake katika jangwa la Karbala, Iraq na kuwaua shahidi; kisha likawachukua mateka watu wa nyumba ya Imamu Hussein (a.s).

Akthari ya vyanzo vimeitaja idadi ya wanajeshi wa jeshi la Omar bin Sa’d kuwa ni zaidi ya 20,000. Jeshi la Omar bin Sa’d liliundwa kutoka katika kaumu na makabila mbalimbali ya Kufa na liliingia katika jangwa la Karbala huku wapiganaji wake wakiwa na misukumo na malengo tofauti. Akthari yao kwa upande wa kiitikadi walikuwa wafuasi wa madhehebu ya Othmaniya (watu waliokuwa wakiamini kwamba, Othman alidhulumiwa). Kulikuweko na makhawariji pia miongoni mwao na kundi miongoni mwa jeshi la Omar bin Sa’d liliingia katika medani ya vita huko Karbal likiwa na uadui na Ahlul-Bayt huku baadhi yao wakiwa wamejiunga na jeshi hilo kutokana na vitisho na tamaa waliyopatiwa na Ibn Ziyad.

Jina na Idadi

Uongozi wa jeshi lililokabiliana na Imamu Hussein (a.s) siku ya Ashura ulikuwa chini ya jukumu la Omar bin Sa’d bin Abi Waqqas, na kwa sababu hii pia linajulikana kama jeshi la Omar bin Sa'd. Kulingana na vyanzo vingi, idadi ya watu wa jeshi hili mwanzoni ilikuwa karibu 4,000, [1] na kwa kujiunga wapiganaji wengine, idadi hiyo ikafikia 20,000; [2] hata hivyo idadi ya wapiganaji wa jeshi la Omar bin Sa’d imetajwa kuwa ni baina 6,000 hadi 35,000. Aidha kuna idadi zingine zilizotajwa kama 6,000, [3] 14,000 [4], 17,000, [5] 22,000, 28,000, [6], 30,000, [7] na 32,000 [8]. Imamu Hussein (as) katika siku ya Ashura, alitoa wasifu katika mashairi yake kuhusu jeshi la adui kuwa ni mithili ya matone makubwa ya mvua. [9] Mwandishi wa kitabu Lamaat al-Husayn alitumia tafsiri hii kwamba Ibn Sa'd alikuweko Karbala akiwa na jeshi kubwa kama matone makubwa ya mvua. [10].

Kuundwa Kwake

Kabla ya tukio la Karbala, Omar bin Sa'd alikuwa amepiga kambi nje ya mji wa Kufa katika kitongoji kilichojulikana kwa jina la Hammam A'yan akiwa na lengo la kuelekea Rey na kupigana vita na Daylami. Kabla ya kuelekea Rey, msafara wa Imamu Hussein (a.s) ukawa umesimama Karbala. Ubaidullah bin Ziyad, mtawala wa Basra na Kufa, alimuomba Omar bin Sa'd aende Karbala kupigana na Imamu Hussein (a.s) kabla ya kwenda Rey. Omar bin Sa'd awali hakukubali ombi hilo, lakini Ubaidullah aliliweka suala la kumpatia ugavana wa Rey kuwa sharti ni kuwepo kwake huko Karbala. Matokeo yake, Omar bin Sa'd alikwenda Karbala na jeshi lake. [11] Katika baadhi ya vyanzo, imeelezwa kwamba Ibn Sa'd, kabla ya kuamua kupigana na Imamu Hussein (a.s) aliwaza hili usiku kucha mpaka asubuhi kwamba, afanye hivyo au la. Akiwa na wazo kwamba atatubu kabla ya kifo chake, alitangaza kuwa tayari kupigana na Imamu Hussein (a.s). [12]

Kuimarishwa Jeshi na Ibn Ziyad

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, baada ya Omar Sa'd kuelekea Karbala, idadi kadhaa ya watu kutoka Kufa walijiunga na jeshi lake kutokana na tamaa au vitisho vya Ibn Ziyad. Ibn Ziyad aliwakusanya watu katika msikiti wa Kufa na akawatuliza wazee wao kwa kuwapa zawadi na kuwatia tamaa, kisha akawaita wafuatane na Omar bin Sa'd katika vita na Imamu Hussein (a.s). [13]

Ibn Ziyad alimteua Amru bin Hurayth badala yake huko Kufa, na kwa kuunda kambi Nukhayla, akawalazimisha wakazi wa mji wa Kufa kwenda huko [14]. Akawajibisha watu wote wa mji wa Kufa kujiunga na jeshi la Ibn Sa'd. Akamtuma Suwayd bin Abd al-Rahman Man'qari kwenda Kufa na akamuamuru afanye msako huko Kufa na amletee kwake yeyote aliyekataa kwenda kwenye vita dhidi ya Imamu Hussein (a.s). [15]

Ubaidullah bin Ziyad alimuita Huswain bin Tamim na askari 4,000 waliokuwa chini ya ukamnada wake kutoka Qadisiyah na kuja Nukhayla. [16] Kadhalika kwa amri yake Shimr bin Dhil Jaushan akiwa na wapiganaji 4000, Yazid bin Rakab al-Kalbi akiwa na wapiganaji 2,000 Huswain bin Numair akiwa na wapiganaji 4,000, Mudhayir bin Rahina Mazini akiwa na wapiganaji 3,000 na Nasr bin Harbah aliyekuwa na wapiganaji 2,000 walijunga na jeshi la Omar bin Sa'd Karbala. [17] Vilevile Shabath bin Rab'i, Hajjar bin Abjar [18], Muhammad bin al-Ash'ath [19] na Yazid bin al-Harith ambaye kila mmoja alikuwa na askari 1,000 nao kwa amri ya Ubaidullah bin Ziyad walijiunga na jeshi la Omar bin Sa'd huko Karbala. [20]

Kadhalikka Ibn Ziyad kila siku alikuwa akiwatuma watu 20 hadi 100 wa Kufa kuelekea Karbala. [21] Hatimaye tarehe 6 Mfunguo Nne Muharram, idadi ya askari wa jeshi la Omar bin Sa'd ilikuwa imefikia takriban 22,200. [22]

Makundi na Misukumo

Akthari ya watu waliokuwa wakiunda jeshi la Omar bin Sa'd walitoka katika jamii na makundi tofauti ya mji wa Kufa [23] na liliundwa kutokana na shauku, malengo na misukumo tofauti. [24] Vyanzo vya historia vimeyatambua makundi haya kwa upande wa kiitikadi kwamba, yalikuwa wafuasi wa madhehebu ya Othmaniyya [25] na wametajwa watu kama: Abu Barda bin Awf al-Azdi, [26] Shayban bin Makhzum, [27] Kathir bin Shihab, [28] Ka'b bin Jabir, Omar bin Sa'd, Bishr bin Sawt na Imarah bin Uqbah Abi Muit kwamba, walikuwa na itikadi hii. [29]

Idadi miongoni mwa askari wa Omar bin Sa'd walikuwa wafuasi wa Bani Umayyah na wapinzani wa Imam Ali (a.s) na maadui wa Mashia wake; Shayban bin Makhzum, [30] Shabath bin Rab'i, [31] Kathir bin Abdullah Shaabi, [32] Shimr bin Dhil al-Jushan, Omar bin Sa'd, Zahar bin Qays, Uzra bin Qays na Amr bin Hajjaj Zubaydi ni miongoni mwa watu hao. [33]

Idadi kadhaa ya waliokuwa wakiunda jeshi hilo walikuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa wa Kufa ambao walikuwa wamemwandikia barua Imamu Hussein (a.s) na kumwalika kwenye mji wao, lakini waliungana na Ibn Ziyad baada ya kutishiwa au kushawishiwa kwa ahadi. Urwa bin Qays, Shabath bin Rab'i, Hajar bin Abjar, Qays bin Ash'ath, Yazid bin Harith, Amr bin Hajjaj na Muhammad bin Umair Tamimi walikuwa katika kundi hili. [34]

Baadhi ya watu wa Kufa na Sham, walijunga na jeshi la Omar bin Sa'd kutokana na vitisho vya Ibn Ziyad, [35] baadhi ya watu pia walikuwa ni sehemu ya jeshi la Imam Ali (a.s) katika vita vya Jamal, Siffin, au Nahrwan, lakini katika tukio la Karbala, walikuwa kwenye jeshi la Omar bin Sa'd. Shimr bin Dhil al-Jushan, [36] Muhammad bin Umair Tamimi [37] na Zahar bin Qays Ju'fi [38] ni miongoni mwa hawa. [39]

Makamanda

Makamanda wa jeshi la Omar bin Sa'd walikuwa:

Bendera ya jeshi nayo ilikuwa mikononi mwa Zayd, mtumwa na ghulamuu wa Omar bin Sa'd. [40] Omar bin Sa'd, alimteua Hurr bin Yazid Riyahi kuwa kamanda wa Bani Tamimi na Bani Hamdan. Hata hivyo Hurr alijitenga na jeshi lake na kujiunga na Imamu Hussein (a.s) na masahaba zake. [41]

Waliojitenga

Katika siku ya Ashura kuna watu waliojitenga na jeshi la Omar bin Sa'd na kujiunga na jeshi la Imam Hussein. Katika baadhi ya vyanzo idadi ya watu hawa (waliojitenga) imetajwa kuwa ni 30. [42] Hurr ibn Yazid al-Riyahi, [43] Abu al-Hutuf na Sa'd bin Harth al-Ansari, [44] Nu'man, Halas bin Amru Azdi Rasibi, [45] Bakr bin Hayy Taymi, [46] Qassim bin Habib, [47] Juwayn bin Malik, [48] Abu al-Sha'atha al-Kindi [49 na Amru bin Dhabiah [50] ni miongoni mwa watu hao. Hata hivyo, baadhi ya waandishi wanaamini kuwa, baadhi ya watu hawa hawakuja katika jeshi la Omar bin Sa'd kwa ajili ya kupigana vita na Imamu Hussein (a.s); bali kutokana na Ibn Ziyad kufunga njia zote za kutoka katika mji wa Kufa, walimfikia Imamu Hussein kupitia jeshi la Ibn Ziyad.

Yaliyofanywa na Jeshi la Omar bin Sa'd

Wapiganaji wa jeshi la Omar bin Sa'd katika jangwa la Karbala walichukua hatua kadhaa na baadhi ya hatua hizo ni:

Kumzuia Maji Imamu Hussein na Masahaba Zake

Baada ya kuwasili kwa barua ya Ibn Ziyad kwa Omar bin Sa'd iliyomtaka amtenganishe Imamu Hussein (a.s) na maji, kwa amri ya Ibn Sa'd tarehe 7 Muharram Amru bin Hajjaj akiwa na jeshi la wapanda farasi 500 alielekea katika ukingo wa Mto Furati ili kumzuia Imamu Hussein na masahaba zake kuyafikia maji. [51]

Kuuawa Shahidi Imamu Hussein na Masahaba Zake

Wapiganaji wa jeshi la Omar bin Sa'd ndio walioanzisha vita siku ya Ashura (tarehe 10 Muharram). Mshale wa kwanza ulirushwa na Omar bin Sa'd mwenyewe. [52] Walimuua shahidi Imam Hussein na masahaba zake. Kisha wakapora na kuchukua kile alichokuwa amekivaa Imam Hussein (a.s). Qays bin Ash'ath na Bahr bin Ka'b walichukuua nguo, [53] Aswad bin Khalid Awdi alichukua viatu, Jumay bin Khalq Awdi alichukua upanga, Akhnas bin Marthad Amamah, Bajdal bin Sulaym alichukua pete na Omar bin Sa'd alichukua na kupora deraya (vazi la vita). [54]

Kuchoma Moto Mahema na Kufanya Uporaji

Baada ya kuuawa shahidi Imamu Hussein (a.s) na masahaba zake, wapiganaji wa jeshi la Omar bin Sa'd walivamia katika mahema na kupora mali zilizokuwa ndani yake [55[ na kisha wakachoma moto mahema hayo. [56]

Kukanyaga Mwili wa Imamu Hussein kwa Farasi

Kwa amri ya Omar bin Sa'd na katika kutekeleza amri ya Ibn Ziyad, watu kumi kutoka katika jeshi lake wakiwa wamepanda farasi walipita juu ya mwili wa Imamu Hussein na kuukanyagakanyaga. [57] Is'haq bin Hawya, Akhnas bin Marthad, [58] Hakim bin Tufayl, Amru bin Subayh, Rajaa bin Munqidh Abdi, Salim bin Kkhaythama Ju'fi, Wahidh bin Naim, Salih bin Wahab Ju'fi, Hani bin Shabath Khadhrami na Usayd bin Malik [59] ni watu ambao wametajwa katika historia kwamba, wakiwa wamepanda farasi walipita juu ya mwili wa Imam Hussein (a.s) na kuukanyagakanyaga.

Vichwa vya Mashahidi Vyapelekwa katika Mji wa Kufa

Wapiganaji wa jeshi la Omar bin Sa'd walikata vichwa vya mashahidi wa Karbala, wakaviweka kwenye mikuki na kuvipeleka Kufa. Khawli bin Yazid Asbahi na Hamid bin Muslim Azdi, walichukua kichwa cha Hussein bin Ali (a.s) na Shimr bin Dhil al-Jushan, Qays bin Ash'ath, Amr bin Hajjaj na Uzra bin Qays walichukua vichwa vya mashahidi wengine na kuvipelekka kwa Ubaidullah bin Ziyad huko Kufa [60].

Kuchukuliwa Mateka Watu wa Nyumba ya Imam Hussein (a.s)

Kwa amri ya Omar bin Saad, askari wake walizika maiti za wanajeshi wao waliouawa [61] kisha wakawakamata mateka manusura wa msafara wa Imam Hussein na kuwapeleka Kufa kwa Ibn Ziyad na kisha Sham na katika utawala wa Yazid. [62]

Waliouawa

Hakuna takwimu kamili kuhusu idadi ya waliouawa upande jeshi la Omar bin Sa'd. Baadhi ya vyanzo vya Kishia vimeripoti kwamba watu 225 au 226 waliuawa na masahaba wa Imamu Hussein (a.s), [63] na baadhi wamekadiria idadi hiyo kuwa karibu watu 900. [64] Kwa mujibu wa riwaya katika kitabu cha Manaqib cha Ibn Shahrashub, Imamu Hussein (a.s) aliua watu 1950 kutoka katika jeshi la Omar bin Sa'd siku ya Ashura na kujeruhi baadhi yao. Kadhalika katika kitabu cha Ithbat al-Wasiyah imeelezwa kuwa, Imam Hussain (a.s) aliua watu 1,800 wa jeshi la adui la Omar bin Sa'd. [66]

Rejea

Vyanzo

  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Edited by Iḥsān ʿAbbās. Beirut: Dār al-Taʿāruf li-l-Maṭbūʿāt, 1397 AH.
  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Futūḥ al-buldān. Beirut: Dār wa Maktabat al-Hilāl, 1988.
  • Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. Al-Akhbār al-ṭiwāl. Edited by ʿAbd al-Munʿim ʿĀmir, Qom: Manshūrāt al-Raḍī, 1368 Sh.
  • Hidāyatpanāh, Muḥammad Riḍā. Bāztāb-i tafakkur-i ʿuthmānī dar wāqiʿa-yi Karbalā. Qom: Pazhūhishgāh-i Ḥawza wa Dānishgāh, 1389 Sh.
  • Ibn al-Jawzī, Sabṭ. Tadhkirat al-khawāṣ. Qom: Manshūrāt al-Raḍī, 1418 AH.
  • Ibn ʿAsākir, ʿAlī b. al-Ḥasan. Tārīkh madīnat Damascus. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Ibn Aʿtham al-Kūfī, Aḥmad. al-Futūḥ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1411 AH.
  • Ibn Athīr, ʿAlī b. Muḥammad. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1965.
  • Ibn Shahrāshūb, ʿAlī b. Muḥammad. Manāqib Āl Abī Ṭālib. Qom: Nashr al-ʿAllāma, 1379 Sh.
  • Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Luhūf. Tehran: Jahān, 1348 Sh.
  • Kāshifī, Mullā Ḥusayn. Rawḍat al-shuhadāʾ. Qom: Nawīd-i Islām, 1382 Sh.
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Ithbāt al-waṣīyya. Qom: Anṣārīyān, 1426 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Irshād. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1399 AH.
  • Naṣr b. Muzāhim al-Minqarī. Waqʿat siffīn. Edited by ʿAbd al-Salām Muḥammad Hārūn. Qom: Maktabat Āyatollāh Marʿashī, 1404 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. ʿIlal al-sharāʾiʿ. Qom: Kitābfurūshī-yi Dāwarī, 1385 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Amālī. Tehran: Kitābchī, 1376 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al. Dalāʾil al-imāma. Qom: Biʿthat, 1413 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm, Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.