Kufutwa dhambi
- Makala hii inahusiana na takfir (kufutwa na kuondolewa madhambi). Kama unataka kujua matumizi mengine ya neno hili angalia takfir.
Kufutwa madhambi (Kiarabu: تكفير الذنوب) huelezwa kuwa ni kuondolewa na kufutiwa madhambi au kuondolewa adhabu yake siku ya Kiyama kutokana na athari ya thawabu za matendo mema. Katika Qur'an na hadithi mambo kama imani, amali njema, kufanya toba, jihadi, kutoa sadaka kwa siri na kufanya ibada yanatajwa kuwa sababu ya kufutiwa madhambi na mtu kuondolewa madhambi yake.
Kufutiwa madhambi ni maudhui ya kiitikadi na kiteolojia ambapo wanateolojia wa Kiislamu hulijadili hili kwa anuani mbalimbali kama ihbat (kuondoka na kufutiwa thawabu za ibada na matendo mema kutokana na athari ya dhambi), takfir (kufutiwa dhambi), adhabu na kadhalika.
Waislamu wa madhehebu ya Shia Imamiyyah na Ash'ariyah wanakubaliana na suala la kufutiwa dhambi zile ambazo tu zimetajwa katika Qur'an Tukufu na Hadithi. Ama Mu'tazila wao wanaamini kwamba, takfir inahusisha suala la kufuta dhambi zote. Wanazuoni wa teolojia wa Shia Imamiya wanauona mtazamo wa Mu'tazila kwamba, ni wenye kwenda kinyume kabisa na baadhi ya Aya za Qur'an ambapo Mwenyezi Mungu anahesabu kando kabisa ujira wa matendo mema na adhabu ya matendo mabaya.
Utambuzi wa maana
Takfir maana yake ni kufunika na kuficha; [1] kwa msingi huo, mtu ambaye anakana neema za Mwenyezi Mungu anahesabika kuwa ni kafiri. [2] Katika elimu ya teolojia kufutiwa dhambi maana yake ni kuondolewa adhabu ya madhambi kutokana na athari ya matendo mema. Kwa msingi huo, takfir ni mkabala wa Ihbat yenye maana ya kuondolewa thawabu za ibada na matendo mema kutokana na athari ya dhambi. [3]
Takfir inatumika pia kwa maana ya kunasibisha ukafiri kwa Waislamu ambayo inatambulika pia kama kukufurisha watu wa kibla. [4]
Sababu
Katika Qur'an na katika hadithi kumebainishwa mambo na sababu ambazo kupitia kwazo dhambi huondolewa. Baadhi ya mambo hayo ni imani, amali njema, [5] kufanya toba, [6] kujiweka mbali na madhambi makubwa, [7], kutoa sadaka kwa siri, jihadi [8] na kufanya ibada. [9] Aidha katika hadithi mambo mengine kama shufaa (uombezi), [10] kumzuru Imam Hussein (a.s), [11] kusoma Qur'an [12] na kusali Sala za usiku. [13]
Takfir katika elimu ya teolojia
Kufutwa dhambi (takfir) ni mjadala na maudhui ya kiteolojia ambayo kawaida huzungumziwa pamoja na ihbat (kuuondoka thawabu za ibada na matendo mema kutokana na athari ya dhambi), takfir (kufutiwa dhambi). [14] wanateolojia wa Kiislamu hujadili maudhui ya kufutwa madhambi chini ya anuani kama ihbat, [15] ihbat na takfir, [16] kubatilishwa amali [17] na ruhusa ya kuwa pamoja thawabu na adhabu. [18] Baadhi ya wanazuoni na Maulamaa wa Kishia na Ahlu-Sunna wamelizungumzia suala hili katika maudhi ya ufufuo [19] na Mu'tazila wamelijadili hili katika maudhui ya bishara na vitisho (al-Wa'd wal-Waid). [20]
Wanateolojia wa Kiislamu wana mtazamo mmoja kwamba, kama kafiri atasilimu na kuwa Mwislamu adhabu ya ukafiri na vilevile adhabu ya dhambi alizozifanya alipokuwa kafiri hufutiwa na kuondolewa; [21] lakini kuna hitilafu za kimitazamo baina yao kuhusiana na dhambi ambazo mtu anazifanya akiwa Mwislamu.
- Mu'tazilah wanakubaliana na suala la kufutwa na kuondolewa dhambi zote na wanaamini kwamba, amali njema inaweza kufuta dhambi yoyote ile. [22] Wanasema, sababu ya kuamini kwao nadharia hii ni kwamba, wanateolojia wa Kimu'tazila, baada ya kuzunguumzia ustahiki wa thawabuu na adhabu kwa ajili ya amali njema na madhambi, walikuumbana na mushkili (tatizo) na tatizo hilo ni kwamba, kama amali itakuwa imechanganyika na thawabu na adhabu kunajitokeza ulazima kwamba, mukallafu katika wakati mmoja anastahiki thawabu na wakati huo huo anastahiki adhabu na hivyo wakasema hili ni jambo lisilowezekana na ni muhali. [23] Kwa mtazamo huo, wakaja na nadharia ya ihbat (kufutika na kubatilika thawabu za amali njema kutokana na athari ya dhambi) na takfir (kufutwa dhambi). [24]
- Waislamu wa madhehebu ya Kishia na Ash'ari [25] hawakubaliani na suala la ihbat kwa sura jumla na wanasema: Amali njema zinafutwa na madhambi tu ambayo yameashiriwa katikak Qur'an na katika vitabu vya hadithi. [26] Kuhusiana na hili, Waislamu wa madhehebu ya Kishia wanaamini wakitegemea baadhi ya Aya za Qur'an kama zile za 7 na 8 katika Surat Zilzal zinazosema: (فَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْراً يَرَهُ * وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرّاً يَرَهُ ; Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona), wanaamini kwamba, Mwenyezi Mungu anahesabu kando juuu ya amali njema na mbaya. Kwa maana kwamba, amali njema ina hesabu yake na amali mbaya inahesabuu yake pia. [27]
Ni kufutwa dhambi au kuondolewa adhabu yake?
Kuna tofauti ya maoni juu ya iwapo takfir ina maana ya kufuta dhambi yenyewe au kuondoa adhabu yake; Abu Ali al-Jubba'i, mmoja wa shakhsia wakubwa wa Mu'tazila, anaamini kwamba takfir inafuta dhambi yenyewe, lakini mwanawe Abu Hashim al-Jubba'i anasema: Takfir inaondoa adhabu yake, yaani adhabuu ambayo ilipaswa kutolewa kwa dhambi husika. [28] Kadhalika imeandikwa kuwa, baadhi ya wanafalsafa wa Kiislamu wanaitambua takfir kwamba, maana yake ni kufuta dhambi yenyewe na wafafanua kwamba, dhambi inafutwa kupitia moja ya njia hizi zifuatazo:
- Kila dhambi kama ilivyo ni dhambi, ni jambo lisilo na uwepo na sio kitu kilichoumbwa.
- Kama ambavyo mtenda dhambi anabadilika kwa kufanya toba na kuwa kiumbe mpya, ni vivyo hivyo katika suala la mambo na amali mbaya ambazo hubadilika na kuwa amali njema. [29]
Rejea
Vyanzo