Nenda kwa yaliyomo

Uchawi

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na uchawi (urogaji). Ili kujua kuhusiana na Aya yenye jina kama hili angalia makala ya Ayat al-Sihr (Aya ya Uchawi).

Uchawi au urogaji au ndumba (Kiarabu: Kigezo:Arabicالسحر) ni kitendo kisicho cha kawaida ambacho hufanywa ili kumiliki watu au vitu au mambo. Mafakihi wa Shia wanakubaliana juu ya kuwa haramu kutumia uchawi, kujifunza, kufundisha na kulipwa kwa ajili yake. Wanachuoni wa maadili pia wameuchukulia uchawi kuwa ni moja ya madhambi makubwa. Imenukuliwa katika hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu (a.s) kwamba, uchawi ni sawa kukufuru na ni haramu kuufanya.

Kwa mujibu wa wafasiri, kwa mujibu wa Qur’ani kuna aina mbili za uchawi: Baadhi ya uchawi ni wa kufikirika na hauna ukweli na uhalisia wowote; lakini pia kuna uchawi ambao huacha athari halisi kama kuleta utengano kati ya mwanaume na mwanamke.

Wanazuoni wa Kiislamu wametofautisha kati ya uchawi na muujiza: Muujiza unaambatana na madai ya unabii, na kwa sababu unafanyika kwa nguvu na matakwa ya Mwenyezi Mungu, hauihitaji mazoezi ya kabla; kinyume na uchawi, ambao hauwezi kuwa na madai ya Utume na pia unahitaji mazoezi na kujifunza.

Baadhi ya mafaqihi wameona kuwa, inajuzu au hata kuwa ni wajibu kifai kujifunza uchawi ili kukabiliana na uchawi au kumuumbua mtu anayetoa madai ya uwongo ya utume. Pia, kuna tofauti ya rai kuhusu kubatilisha uchawi kwa njia ya dua na Qur'an tu, au kama uchawi unaweza kubatilisha uchawi.

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafaqihi, ikiwa mchawi ni kafiri, ataadhibiwa kwa adhabu itakayoainishwa na mtawala (taazir); lakini ikiwa yeye ni Mwislamu na anatambua uchawi kuwa ni halali, basi sheria za kuritadi zitatekelezwa dhidi yake. Pia iwapo mtu atauawa kwa uchawi, baadhi ya mafaqihi wanaona adhabu ya kisasi (kulipiziwa) na dia itatekelezwa kwa muuaji, na wengine hawakubaliani na hukumu hii.

Nafasi ya Uchawi

Katika utamaduni wa mazungumzo, neno uchawi au ndumba limeelezwa kama ifuatavyo: "kudhibiti nguvu za asili na zisizo za kawaida kwa kusoma na kukariri baadhi ya maneno na mambo ya siri na kumiliki watu, vitu na mambo". [1]

Katika Qur’an [2] na hadithi [3] suala la uchawi limezungumziwa. Wafasiri [4] na wataalamu wa elimu ya hadithi [5] pia wamejadili na kuzungumzia maudhui hii chini ya Aya na hadithi zinazohusiana na uchawi. Kadhalika uchawi ni moja ya masuala ya kielimu katika fikihi na mafakihi wanazungumzia maudhui mbalimbali kama vile kujuzu uchawi au kuwa kwake halali [6] adhabu ya mchawi [7] na mambo mengine yanayohusiana na jambo hili. [8]

Historia Yake

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Qur’an ya Nemooneh: Kuhusiana na kwamba, uchawi ulianza lini na kuenea, haiwezekani kutoa tamko la uhakika kuhusu jambo hili. Inaweza kusemwa tu kwamba, uchawi lilikuwa ni jambo la kawaida miongoni mwa watu tangu zama za kale. [9] Inaelezwa katika riwaya iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Hassan Askary (a.s) kwamba, uchawi na urogaji uliongezeka na kukithiri kuanzia zama za Nabii Nuhu (a.s). [10]

Tofauti ya Muujiza na Uchawi

Makala kuu: Muujiza

Moja ya sifa au majina ambayo walikuwa wakipewa na kunasibishwa nayo Mitume katika historia yote na hasa kwa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) ni uchawi; [11] lakini wanazuoni wa Kiislamu hawakubaliani na hili na wanaeleza tofauti kati ya uchawi na miujiza:

  • Uchawi na muujiza vyote vina athari; lakini miujiza ni haki na uchawi ni batili. Muujiza unafanyika katika fremu na mkondo wa mageuzi, marekebisho na elimu; lakini uchawi hauna lengo au una malengo ya juu juu tu na ya thamani ya chini. [12]
  • Uchawi unategemea mambo ya binadamu. Na ni kwa sababu hiyo, ndio maana wachawi hufanya mambo ya ajabu ambayo wamejifunza na kuyafanyia mazoezi; lakini muujiza ni jambo la Kimungu, na Manabii walikuwa wakifanya mambo ambayo watu waliwataka wayafanye. [13]
  • Muujiza unaambatana na madai ya Utume; lakini mchawi hawezi kudai unabii; kwa sababu hekima ya Mwenyezi Mungu humzuia mtu kudai Utume kwa uwongo, na akifanya hivi atafedheheka na kuumbuka. [14]

Sisitizo la Qur’an la Uwepo wa Uchawi

Waandishi wa Tafsiri ya Qur’an ya Nemooneh (al-Amthal), kwa kuchunguza takriban matumizi 51 ya neno “Sihr” (uchawi) katika Qur’ani, wameugawanya uchawi katika sehemu mbili kwa mtazamo wa Qur’ani:

  1. Uchawi ambao ni ulaghai, kiini macho na hila na mazingaombwe usio na ukweli; kama katika Aya ya 66 ya Surat Taha na Aya ya 116 ya Surat al-A’raf.
  2. Uchawi ambao una ukweli na unafanya kazi kweli; kama katika Aya ya 102 ya Surah Al-Baqarah, ambayo inaashiria athari ya uchawi juu ya kutengana kwa mume na mke. [15]
Makala Kuu: Ayat Sihr

Wafasiri pia, katika tafsiri ya Aya ya 102 ya Sura Baqarah, wanasimulia kisa cha Malaika wawili walioitwa Haaruta na Maaruat waliokuja katika umbo la wanadamu wawili katika zama za Nabii Suleiman (a.s) miongoni mwa banu-Israil na kutokana na kuenea kwa uchawi miongoni mwao na kuibuka kwa fitna mbalimbali, watu walifundishwa njia za kukabiliana na uchawi. Kwa mujibu wa Aya hii, waliwaambia watu wazitumie njia sahihi na katika njia ya kubatilisha uchawi tu na huu ulikuwa ni mtihani kwao; lakini walifanya mambo fulani mabaya kwa kutumia uchawi. [16]

Kuamiliana Maimamu (a.s) na Uchawi na Ndumba

Sheikh Kulayni amenukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), ambamo ndani yake anambainishia mbinu na mikakati kwa mtu aliyetumia maisha yake katika njia ya uchawi na kisha akajuta na akaomba suluhisho la kufidia kwamba, anapaswa kuitumia elimu hii kukabiliana na uchawi. [17] Allama Majlisi ametumia hadithi hii kama hoja ya kujuzisha na kuruhusu kujifunza uchawi kwa ajili ya kukabiliana nao. [18]

Hadithi nyingine imepokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s), ambamo ndani yake anatambulisha kuwa, kujifunza uchawi ni kukufuru na kusema kwamba ikiwa mtu anayejihusisha na uchawi hatatubu, adhabu yake ni kuuawa. [19] Ibn Idris Hilli pia ananukuu hadithi kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s.), ambayo kwa mujibu wake mtu anamwendea na kuomba amri ya kumrejelea mtu ambaye anajulisha kuhusu mahali vilipo vitu vilivyoibiwa. Imamu Sadiq, katika jibu lake, anasimulia riwaya kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kwamba yeyote anayekwenda kwa kuhani au mchawi na kuyathibitisha maneno yake, huyo ni kafiri kwa mujibu wa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu. [20]

Njia za Kukabiliana na Uchawi

Allamah Majlisi amekusanya riwaya chini ya jina la "Dua za kukabiliana na uchawi na kijicho" katika kitabu Bihar al-Anwar. [21] Katika kitabu cha Tibb al-Aimah pia kumekusanywa hadithi chini ya anuani ya "Hirizi (talasimu) za kubatilisha uchawi."[22] Kwa mfano, Imam Ali (a.s) katika kuitikia ombi la baadhi ya masahaba, aliwafundisha dua inawataka waandike juu ya ngozi ya mnyama Swala na wawe nayo daima popote. [23] Kadhalika katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ni kuwa, kila ambaye anaogopa uchawi au shetani, asome aya ya 54 ya Surah A'raf [24] inayosema: (إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ أَلاَ لَهُ الْخَلْقُ وَالأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ; Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote).

Utambulisho wa Uchawi na Maana Yake Kifikihi na Vielelezo Vyake

Mafakihi wana mitazamo tofauti kuhusu ufafanuzi, maana na utambulisho wa uchawi. Wengine wanaona kuwa una ukweli wa nje, wengine wanaamini kuwa uchawi hauna ukweli (ni kitu ambacho hakipo) na kundi jingine linasema kuwa, haiwezekani kutoa maoni ya uhakika ikiwa ni jambo la ukweli au la kufikirika:

Utambulisho wa Uchawi

Sheikh Tusi na Shahid Thani wanaona kuwa uchawi ni kitu ambacho kipo. [25] Ayatullah Khui anasema kwamba, uchawi hauna uwepo katika hisia na mawazo ya mtu ambaye amerogwa na ni jambo ambalo halina ukweli wa nje yaani halipo). [26] Kwa mujibu wa Shahid Awwal ni kuwa, wasomi wengi wamekubali maoni haya. [27] Muhaqqiq Karaki anaamini kwamba, haiwezekani kutoa maoni ya uhakika kuhusu uchawi kuwa ni jambo la kufikirika au ni kitu halisi ambacho kipo. [28]

Fasili na Maana ya Uchawi na Vielelezo Vyake

Kwa mujibu wa Mulla Ahmad Naraqi, haiwezekani kufikia maana moja ya uchawi unaojumuisha vipimo vyake vyote katika kauli ya mafaqihi. [29] Anazingatia ujuzi wa kawaida na uliozoeleka wa dhana ya uchawi na anasema kwamba katika mtazamo wa ada na mazoea, uchawi ni jambo la siri na halifanyika kwa sura ya kawaida na ilioenea. [30] Allama Hilli alifafanua uchawi kuwa ni maandishi, neno, au kitendo ambacho huathiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja mwili, moyo, au akili iliyorogwa. [31] Uchawi huu unaweza kuwa sababu ya mauaji, maradhi, kutengana kwa mume na mke, mapenzi au chuki kwa wanadamu. [32] Imam Khomeini pia ana tafsiri hiyo hiyo ya uchawi. [33] Shahid al-Awwal ameongezea mambo kama kuajiri majini, mashetani na malaika kwa ajili ya kitu ambacho hakiwezi kupatikana au kutibu ugonjwa, kuita roho na kuzungumza nayo, kufichua mambo yasiyojulikana za vitu mbalimbali na talasimu. [34]

Fakhr al-Muhaqiqin anachukulia uchawi kuwa ni kufanya mambo ya ajabu na yasiyo ya kawaida kwa nguvu za ndani na za kinafsi, au kwa msaada wa nyota (vitu vya mbinguni), au kwa kuchanganya nguvu za mbinguni na nguvu za dunia, au kwa msaada wa roho rahisi. [35] Ayatullah Golpayegani anaamini kwamba, uchawi na urogaji ni kitu chochote chenye athari zisizo za kawaida na kinafanana na mujiza na makarama; bila kujali kinaacha alama na athari kwenye mwili uliorogwa au la; iwe aliyerogwa ni mnyama au binadamu au kitu kisicho na uhai; kama vile kutikisa mti au kutikisa paa na ukuta au kusimamisha maji bila kutumia vitu vinavyoonekana au mambo ya kidini kama vile Aya na dua ambazo zimepokewa kutoka kwa Maasumina (a.s). [36] Kwa mtazamo wa Ayatullah Khui ni kuwa, kufanya mambo yasiyo ya kawaida kutokana na athari ya kusafishwa nafsi au kufanya mazoezi hakuhesabiwi kuwa ni uchawi. [37]

Inajuzu au ni Haramu Kutumia Uchawi?

Uharamu wa kuwaroga wengine, kujifunza na kufundisha uchawi, na kulipwa kwa ajili yake kumezingatiwa kuwa ni jambo ambalo mafaqihi wa Kishia wameafikiana. [38] Katika vitabu vya maadili, uchawi pia umezingatiwa kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa. [39] Abdul Hussein Dastghaib anaamini kuwa, sababu ya kuwa kwake ni katika madhambi makubwa ni kuwa wazi hadithi kuhusiana na hilo. Kuhusiana na hili, ananukuu hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ambaye aliuweka uchawi katika orodha ya madhambi makubwa na kuitumia hiyo kama hoja yake. [40]

Pamoja na hayo, kwa maoni ya baadhi ya mafaqihi, hukumu ya jambo hili ni tofauti. Kwa mfano, kundi la mafaqihi wameona kuwa inaruhusiwa kutumia uchawi ili kujikinga na uchawi wa wengine. [41] Sahib Jawahir amesema kuwa, kujifunza uchawi peke yake tu si tatizo kwa sababu inaweza kuwa muhimu katika hali za dharura. [42] Shahid al-Awwal na Thani wao wamesema kwamba, kujifunza uchawi ni wajibu kifai ikiwa ni kumfedhehesha mwongo au mdai Unabii wa uwongo. [43] Sahib Jawahir anasema kwamba, uchawi unaweza kubatilishwa kwa Qur'an, dua na dhikri. [44]

Adhabu ya Mchawi

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafaqihi wa Kishia, ikiwa mchawi ni kafiri ataadhibiwa kwa makosa ya ta’aziri (makosa ambayo mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye jukumu la kuainisha adhabu hizo), [45] lakini akiwa Mwislamu na kuuona uchawi kuwa ni halali, anahesabiwa kuwa ni kafiri na murtadi, na adhabu za kuritadi zitatekelezwa dhidi yake. [46] Iwapo haoni uchawi kuwa halali kulingana na baadhi, ataaadhibiwa kwa adhabu ya uchawi yaani kuuawa; [47] lakini kundi jingine la mafaqihi wanapinga hukumu ya mauaji. [48]

Kuua kwa Uchawi

Fat'wa ya mafakihi kuhusu kuua kwa kutumia uchawi ni tofauti: Kwa mujibu wa fat’wa ya Sheikh Tusi, mtu akiuawa kwa uchawi, hakuna kisasi wala dia. [49] Lakini Muhaqqiq Hili amesema kama suala la uchawi linawezekana kuwa ni jambo la uhalisia na la kweli yaani liko, basi natija yake ni kuweko kisasi na dia. [50] Allama Hilli [51] na Shahidi Thani [52] wanazingatia kwamba, adhabu ya kisasi inafuata na kutegemea kukiri kwa mchawi: Ikiwa mchawi atakiri kwamba alifanya uchawi kwa nia ya kuua, basi malipo na adhabu ya mchawi ni kufanyiwa kisasi yaani adhabu ya kisasi itatekelezwa dhidi yake. [53] Kwa mtazamo wa Imamu Khomeini ikiwa taathiira ya uchawi katika mauaji itathibitika na kusudio la mchawi lilikuwa ni kuua, hayo yatakuwa ni mauaji ya kukusudia; na kama hakukuweko na nia ya kuua, yatakuwa ni mauaji yasiyo ya kukusudia. Kadhalika kama uchawi utakuwa kwa namna fulani ni wa kuua (ni wenye kuua) pia hilo litakuwa ni mauaji ya kukusudia. [54]